Mkopo:Al-Raj'a
| Kifo | |
|---|---|
| Sakratul-Mauti • Malaika Izraili • Kuosha maiti • Kafani • Sala ya maiti • Mazishi • Shahada | |
| Barzakh | |
| Usiku wa kwanza kaburini • Maswali ya kaburini • Munkar na Nakir • Maisha ya Barzakh • Mwili wa Kibarzakh | |
| Siku ya Kiyama | |
| Israfil • Ufufuo wa mwili • Kupulizwa kwa Baragumu • Kitabu cha matendo • Sirat • Uwanja wa Mahshar • Watu wa kuliani • Watu wa kushotoni | |
| Peponi | |
| Milango ya Pepo • Huri al-Ayn • Ghilman • Ridhwan • Neema za Peponi | |
| Jahannamu | |
| Milango ya Jahannam • Ngazi za Jahannamu • Zaqqum • Asfala Safilina • Hawiya • Jahim • Ghassaq | |
| Dhana Zinazohusiana | |
| Uombezi • Kudhihirika kwa matendo • Raqib na Atid • Kuzaliwa upya • Raj'a • Roho • Mema yenye kubaki | |
Al-Raj'a (Arabic: الرَّجعَة); ni dhana maalumu maana ya kurejea tena duniani kabla ya kufika Siku ya Kiama. Jambo lililolihusu kundi la watu maalumu waliokufa ambao wanatarajiwa kurudi tena ulimwenguni humu. Suala hili linahesabiwa kuwa ni miongoni mwa itikadi pekee zilizohusishwa na madhehebu ya Shia Imamiyyah. Wanazuoni wa madhehebu haya, hutegemea baadhi ya Aya za Qur’ani pamoja na Hadithi maalumu katika kuthibitisha ukweli wa itikadi hii. Aidha wanazuoni hawa, wanalichukulia suala hili kuwa ni miongoni mwa misingi ya lazima na isiyopingika katika madhehebu ya Kishia, huku wakisisitiza kuwa kuna ijmai na muwafaka wa kauli moja kuhussiana na usahihi wake. Idadi kubwa ya wanazuoni wa Shia Imamiyyah wanaona kuwa tukio hili la kurejea tena duniani, litaendana sambamba na kusimama na kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.f).
Licha ya kuwepo kwa ijmai na makubaliano ya jumla kati ya wanachuoni wa Imamiyyah kuhusu msingi mkuu wa Al-Raj'a, yaliosimama juu ya msingi wa Hadithi yaliyothibitika kupitia mfululizo wa mapokezi mengi na tofauti (mutawatir), ila bado kuna mitazamo tofauti na mbalimbali juu ya maelezo ya kina juu ya namna tukio hilo litakavyofanyika. Katika muktadha huu, baadhi yao wanaona kuwa, wale watakaorejea watahudhuria huku wakiwa na miili ileile ya kimaumbile waliyokuwa nayo hapa duniani. Wakati huo huo, kundi jengine la wanazuoni linasema kuwa watu hao watarejea wakiwa na miili ya mfano wa kiroho (ajsad mithaliyyah). Aidha, kuna upande mwengine unaoamini kuwa, ingawa msingi wa Al-Raj'a ni jambo lililokubaliwa na wanazuoni wote, ila undaniwake na namna halisi ya kutokea kwake linabaki kuwa ni jambo lisiyojulikana na mwengingene yeyote yule isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na mawalii Wake tu.
Kwa mujibu wa mapokezi kadhaa ya Hadithi, mtu wa kwanza kabisa atakayerejea duniani ni Imamu Husayn (a.s). Maandiko hayo yanaashiria kundi maalumu la watu watakaorejea tena duniani huumu. Nao ni Mtume Muhammad (s.a.w.w), Imam Ali (a.s), na Maimamu wengine wote watokano na kizazi cha Ahlul Bait (a.s). Aidha, wengine wanaohusishw na tukio hili ni pamoja na; waumini wa dhati, mashahidi, na watu mashuhuri wa kihistoria kama vile Watu wa Pangoni (As'habul-Kahf), Yusha bin Nun, na yule Muumini wa ukoo wa Firauni. Kadhalika, kuna baadhi ya wanawake wema waliotajwa kurejea ulimwenguni humu, akiwemo Ummu Ayman, Hubabah al-Walibiyyah, Sumayyah, na Siyanah al-Mashitah. Katika upande mwingine, mapokezi yanaeleza kuwa hata maadui wa Ahlul Bait na Manabii, pamoja na wanafiki, watarudishwa tena ulimwenguni humu, ili kulipizwa kisasi cha matendo yao.
Kuna vitabu vingi vilivyotungwa na wanachuoni mbalimbali kuhusiana na mada hii ya kurejea uzimani. Miongoni mwa maandiko mashuhuri juu ya mada hii ni, kitabu kiitwacho Al-Iiqaadhu min al-Haj’ah bi al-Burhan ‘ala al-Raj’ah kilichoandikwa na Al-Hurru al-Amili, pamoja na kitabu kiitwacho Al-Shiah wa al-Raj’ah kilichotungwa na Muhammad Rida al-Tabasi al-Najafi.
Maana na Nafasi ya Kiitikadi ya Al-Raj'a
Kimsingi, Al-Raj'a ina maana ya kurejea uzimani (ulimwenguni) kwa kundi la watu fulani baada ya kufa na kabla ya kufika Siku ya Kiama. [1] Kwa mujibu wa maoni ya Sheikh Mufid, itikadi hii kwa upande wa Kishia inamaanisha kuamini kuwa Imamu Ali pamoja na Maimamu wengine (a.s) watarejea tena duniani humu. Kwa mujibu wa maelezo yake, tukio hili litajiri baada ya kuuawa kwao kishahadi kwa Imam Mahdi, ambapo warudi na wakisimamisha na kueneza utawala wao kote ulimwenguni, bila kukabiliwa na upinzani au vizuizi vyovyote. [2] Kilugha, neno Al-Raj'a linamaanisha "marudio" au "marejeo", [3] na katika baadhi ya mapokezi ya Hadithi pia limekuja likitumia istilahi ya "Al-Karrah" (Mzunguko wa Kurejea). [4]
Dhana ya Al-Raj'a ni miongoni mwa masuala ya kiitikadi inayofungamana moja kwa moja na dhana ya Uimamu na Imamu Mahdi (Al-mahdawiyya), hii ni kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine inahisbiwa kuwa ni msingi imara wa kuamini Siku ya Mwisho (Ma'ad), malipo, na adhabu. Hii ndiyo iliyopelekea suala hili lijadiliwe kwa kina katika elimu ya theolojia ya Kiislamu (Ilm al-Kalam) ili kuthibiti usahihi na ukweli wake. [5] Hali kadhalika, maudhui hii inasimama kama moja ya pointi kuu za hitilafu za kimitazamo kati ya Shia na Ahlu Sunna. [6]
Aidha kuna mifumo kadhaa ya kiimani inayofanana na Al-Raj'a inanasibishwa na dini za Kiyahudi na Kikristo. Kwa mfano, vitabu vya Taurati vinaashiria kufufuliwa kwa Wana wa Israili (Banu Israil), kurejea kwa utawala wa Nabii Daudi (a.s), na kurejea kwa idadi kubwa ya wafu katika zama za mwisho. Katika upande wa Injili pia, kumetajwa kurejea kwa wafuasi wa Nabii Isa (a.s) na kuenea kwa utawala wake katika "Ufufuo wa Kwanza" ambao utatangulia kabla ya ule Ufufuo wa Pili ambao ni ufufuo wa mwisho kabisa. [7]
Imani ya Al-Raj'a Kama Alama ya Ushia
Kwa mujibu wa maelezo ya Al-Hurr al-Amili, ni kwamba; kuamini Al-Raj'a ni miongoni mwa sifa maalum na alama kuu zinazoutambulisha Ushia. [8] Sheikh al-Saduq naye akielezea itikadi hii katika kitabu chake cha "Al-I’tiqadat" anasema: Haki na ukweli wa dhana hii ni kwamba; itikadi hili ni sehemu ya misingi ya imani ya Kishia. [9] Aidha, wanazuoni mashuhuri kama vile Sheikh Mufid [10] na Sharif al-Murtada [11] wamedai kuwepo kwa ijmai na makubaliano ya kauli moja kuhusiana na usahihi wa kiitikadi wa suala hili.
Baadhi ya watafiti wanalichukulia suala hili kuwa ni jambo lililokubaliwa kikamilifu miongoni mwa Washia na hata kulihisabu kuwa ni miongoni mwa mambo ya lazima (misingi ya wazi) ya madhehebu ya Shia. Wakati huo huo, wapo wengine ambao, ingawa hawalichukulii kuwa ni jambo la lazima, ila hawakutaja ushuhuda wowote ule wa kulikataa jambo hili. [12] Kwa mfano, Allamah al-Majlisi katika kitabu cha Haqq al-Yaqin, anasema: Al-Raj'a inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa masuala ya ijmai na hata misingi ya lazima ya madhehebu ya Kishia, [13] na kwamba kulikana suala hili ni sawa na kujiondoa katika madhehebu hayo. [14] Kadhalika, Sayyid Abdullah Shubbar naye ameona kuwa kuamini suala hili ni sehemu ya misingi na ya lazima ya madhehebu ya Shia, huku akimhesabu yeyote anayelikataa jambo hili kuwa ametoka nje ya mduara wa Ushia. [15] Al-Hurr al-Amili anaongeza akisema kuwa; Imani ya Al-Raj'a ni miongoni mwa mambo ya lazima mbele ya idadi kubwa ya wanazuoni wa madhehebu ya Shia Imamiyyah, na hakuna mwanazuoni yeyote yule maarufu aliyepata kulikataa suala hili kwa kauli au kwa maandishi. [16] Kulingana na maelezo ya Marja wa kidini Ayatullah Lutfullah al-Safi al-Gulpaygani, ni kwamba; Mashia wote wanaamini itikadi ya kurejea duniani, na kulikana jambo hili kunapelekea kuikataa Qur'ani na mapokezi ya Hadithi yaliyothibitika kwa njia ya mfululizo (mutawatir) yaliyomo katika vyanzo vya Hadithi. [17]
Kinyume chake, kuna baadhi ya wanazuoni wa Kishia kama vile; Sayyid Muhsin al-Amin, Muhammad Jawad Mughniyyah, na Muhammad Ridha al-Mudhaffar wanaona kuwa, kuamini Al-Raj'a si miongoni mwa misingi ya lazima ya madhehebu ya Kishia. Mtazamo wao unasisitiza kuwa, itikadi hii inathibitika kupitia mapokezi yaliyopokewa kutoka kwa Maimamu wa Kishia, na kwamba kuamini suala hili ni wajibu tu kwa mtu yeyote anayesadiki usahihi wa mapokezi hayo. [18] Ama kuhusu Ayatullah Ruhullah Khomeini, yeye anaamini kuwa, msingi mkuu wa Al-Raj'a ni jambo la lazima, lakini maelezo ya kina na namna ya tukio hilo litakavyofanyika si miongoni mwa mambo ya lazima na hakuna ushahidi thabiti unaoyafafanua suala hilo. [19]
Mitazamo Tofauti Kuhusu Ufafanuzi wa Al-Raj'a
Kwa mujibu wa maelezo ya Sheikh al-Mufid, wanachuoni wa Imamiyyah wanakubaliana kwa kauli moja kuhusiana na msingi mkuu wa Al-Raj'a, lakini wana mitazamo tofauti juu ya maana na namna ya tukio hilo litakavyofanyika. [20] Sayyid Abdullah Shubbar anaona kuwa; ni wajibu kwa kila Mshia kuamini msingi mkuu wa Al-Raj'a, ila hakuna uwajibu wa undani wake, kwani elimu hiyo iko kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na mawalii Wake tu. [21] Baadhi ya wanazuoni wa Hadithi na theolojia wanaamini kuwa; Al-Raj'a ni sawa kabisa na Siku ya Kiama, kwa maana ya kwamba Mwenyezi Mungu atafufua miili ya wafu kutoka makaburini na kuwakusanya pamoja. [22] Katika kufafanua mtazamo wa Al-Faidh al-Kashani kuhusu namna ya kurejea huku, Murtadha Mutahhari anasema kuwa; Al-Raj'a haina maana ya kurejea kwa wafu duniani wakiwa na miili yao ya kimaumbile waliyokuwa nayo hapa duniani; bali inamaanisha kurejea kwa roho zao zikiwa katika miili ya kiroho, mfano wa ile miili inayodaiwa kuonwa na watu wenye uwezo wa kushuhudia masuala ya kiroho (kashf). [23]
Kwa upande mwingine, Ayatullahi Khomeini anaamini kuwa; nafsi za watu watakaorejea zitaumba miili ya kidunia (na si miili ya kiroho), na hivyo watarejea duniani wakiwa na miili hiyo ya kimaumbile (kimaada). [24] Muhammad Ali Shah-Abadi yeye anaamini kuwa; kurejea huku duniani kutafanyika kwa kutumia miili ya kiroho au ya kibarzakhi. [25] Mtafiti wa Kishia, Muhammad Baqir al-Behbudi, anashikilia msimamo uemao kuwa; Al-Raj'a haitashuhudiwa na kila mtu, na kwamba kuielezea kama ufufuo wa kutoka makaburini ni mtazamo wa kijuujuu tu wa kijamii, ambao hauendani na mantiki ya Qur'ani wala akili. Yeye anaamini kuwa kurejea kwa mwanadamu kunategemea mfumo wa sasa wa kimaumbile, ambapo mbegu za kiume huingia katika matumbo ya wanawake kutoka katika migongo ya wanaume, na baada ya kuzaliwa, mwanadamu husahau kumbukumbu zote za maisha ya nyuma. [26]
Aidha, baadhi ya wanazuoni wameenda mbali zaidi kwa kufanya taawili (ufafanuzi pembuzi) wa mapokezi ya Hadithi ziliyopo katika mlango wa Al-Raj'a. Wanazuoni hawa wanasema kuwa; makusudio ya kurejea huku si kurudi kwa Maimamu wa Kishia (a.s) kwa miili yao wenyewe katika maisha ya dunia; bali makusudio yake ni kwamba, katika zama za kudhihiri kwa Imamu Mahdi, dola zao, sheria zao, maamrisho yao, na makatazo yao ndivyo vitakavyorejea na kutawala. [27] Sharif al-Murtada amenasibisha mtazamo huu na idadi ndogo sana ya wanazuoni wa Imamiyyah huku akapinga vikali hoja zao. [28]
Zama za Al-Raj'a
Kwa mujibu wa wanazuoni wengi wa madhehebu ya Shia Imamiyyah, ni kwamba; tukio la Al-Raj'a limefungamana moja kwa moja na kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.f), ingawa kuna mitazamo tofauti kuhusu wakati kamili wa kutokea kwake. [29] Hivyo Idadi kubwa ya wanazuoni wanaona kuwa tukio hili litaendana sambamba na tukio la kudhihiri kwa Imamu Mahdi (a.f). [30]
Sheikh al-Mufid anabainisha katika kitabu chake cha Al-Irshad akisema kuwa; Al-Raj'a ni miongoni mwa alama za kudhihiri kwa Imamu Mahdi (a.s). [31] Hata hivyo, baadhi ya watafiti wakitokana na mapokezi ya Hadithi zinayotaja kurejea mara kadhaa kwa Imam Ali (a.s), [32] wamefikia hatua ya kusema kuwa; Al-Raj'a itatokea baada ya kudhihiri kwa Imam Mahdi. (a.f) [33] Wakati huo huo, kuna Hadithi inayoashiria kurejea kwa Imam Hussein (a.s) kabla ya kudhihiri kwa Imamu Mahdi, [34] ilhali mapokezi mengine yanaeleza kuwa kurejea kwa Imamu Hussein (a.s) kutatokea baada ya kufariki kwa Imamu Mahdi (a.f). [35]
Katika Tafsir al-Qummi, kumepokewa Hadithi kutoka kwa Imam Ali (a.s) inayoeleza kuwa; pale Mtume Muhammad (s.a.w.w) alipowafahamisha watu kuhusiana na tukio la Al-Raj'a, walimuuliza kuhusu wakati wa kutokea kwake, nayo ikawa ndiyo sababu ya Mwenyezi Mungu kumshushia Aya ya 25 ya Surat al-Jinn isemayo: (قُلْ إِنْ أَدْرِي أَقَرِيبٌ ما تُوعَدُونَ أَمْ يَجْعَلُ لَهُ رَبِّي أَمَداً). "Sema: Sijui kama hayo mloahidiwa yapo karibu, au Mola wangu Mlezi atayawekea muda mrefu." [36] Kutokana na mapokezi haya, baadhi ya wanazuoni wanasema kwamba; hakuna mtu anayejua wakati halisi wa Al-Raj'a na elimu yake iko kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake.
Watakaorejea Duniani (Ashaab Al-Raj'a)
Kuna watu wengi waliotajwa katika mapokezi ya Hadithi wakiorodheswa kwenye orodha ya watu maalumu watakaorejea tena duniani. Miongoni mwao ni:[37]
- Maimamu wa Kishia (a.s): Kwa mujibu wa Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam al-Sadiq (a.s), mtu wa kwanza kabisa atakayerejea tena duniani humu, ni Imam Hussein (a.s), ambaye atatawala kwa muda wa miaka arobaini.[38] Kadhalika, kuna mapokezi yanayoeleza kurejea kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Imam Ali (a.s),[39] pamoja na Maimamu wengine wote waliosalia.[40]
- Masahaba wa Maimamu: Kulingana na baadhi ya Hadithi, kundi la masahaba na wafuasi watiifu wa Maimamu maasumu (a.s) watarejea pia nao waterejea ulimwenguni.[41]Katika baadhi ya masimulizi ya Hadithi hizi, miongoni mwa watu watakaorudi tena ulimwenguni, ni Salman al-Farsi, Al-Miqdad, Abu Dujana al-Ansari, na Malik al-Ashtar.[42]Aidha, imeelezwa kuwa, masahaba sabini wa Imam Husein (a.s) pia nao watarejea pamoja naye katka kurudi kwake ulimwenguni.[43]
- Masahaba wa bwana Mitume (a.s): Kwa mujibu wa Hadithi kadhaa, miongoni mwa watakaorejea tena duniani, ni kundi la waumini kutoka katika kaumu ya Nabii Musa (a.s), Watu wa Pangoni (As'haabul-Kahf), Yusha bin Nun, na Hizqil aliye kuwa Muumini wa ukoo wa Firauni (Muumin Aali Fir'aun).[44]
- Mashahidi na Waumini: Baadhi ya mapokezi ya Hadithi yanasema kwamba, mashahidi na waumini wa dhati ni sehemu ya wale watakaorejea ulimwenguni.[45]
- Wanawake Waumini: Moja ya Hadithi imetaja majina ya wanawake kumi na tatu watakaorejea duniani, miongoni mwao akiwemo; Ummu Ayman, Hubabah al-Walibiyyah, Sumayyah (mama yake Ammar bin Yasir), Zubaydah, Umm Said al-Hanafiyyah, na Siyanah al-Mashitah.[46]
- Maadui na Wanafiki: Katika upande mwingine, mapokezi ya Hadithi yanasisitiza kuwa, maadui wa Ahlul Bait (a.s), maadui wa bwana Mitume (s.a.w.w), pamoja na wanafiki, pia nao watarudishwa dunianai kwa ajili ya kulipizwa kisasi na kuadhibiwa kwa matendo yao maovu.[47]
Dalili
Zifuatazo ni dalili zinazotumiwa kuthibitisha usahihi wa itikadi ya Al-Raj'a:
Ushahidi wa Qur'ani Tukufu
Zifuatazo ni baadhi ya Aya zinazotumiwa na madhehebu ya Shia Imamiyyah kama hoja thabiti za kuthibitishea ukweli wa Al-Raj'a:
- Aya ya 83, Suratu an-Naml: ﴾وَيَوْمَ نَحْشُرُ مِنْ كُلِّ أُمَّةٍ فَوْجًا مِمَّنْ يُكَذِّبُ بِآيَاتِنَا﴿ "Na siku tutakapokusanya kutoka katika kila umma kundi la wale wanaokanusha Aya zetu."[48]Aya hii inaashiria kusanyiko la kundi fulani tu, tofauti na ufufuo wa jumla wa Siku ya Kiama ambapo viumbe wote watakusanywa, kama ilivyoelezwa katika Suratu al-Kahf, Aya ya 47: (وَحَشَرْنَاهُمْ فَلَمْ نُغَادِرْ مِنْهُمْ أَحَدًا) "Na tutawakusanya wala hatutamwacha yeyote miongoni mwao." [49]Aya hizi zinaonesha tukio la Al-Raj'a litakalotokea duniani, tukio linaungwa mkono na tafsiri ya Imam al-Sadiq (a.s) inayopatikana katika Tafsir al-Qummi. [50] [51]
- Aya zinazoashiria mifano ya kufufuliwa kwa wafu hapo awali (kabla ya Siku ya Kiama) katika umma zilizopita, kama vile Aya ya 73, 243, na 259 za Suratu al-Baqarah:
- Aya ya 73: (فَقُلْنَا اضْرِبُوهُ بِبَعْضِهَا كَذَلِكَ يُحْيِي اللَّهُ الْمَوْتَى وَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ) "Tukosema: Mpigeni kwa baadhi ya vipande vyake (huyo ng'ombe). Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyofufua wafu, na anakuonesheni ishara zake ili mpate kufahamu."
- Aya ya 243: (أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ خَرَجُوا مِنْ دِيَارِهِمْ وَهُمْ أُلُوفٌ حَذَرَ الْمَوْتِ فَقَالَ لَهُمُ اللَّهُ مُوتُوا ثُمَّ أَحْيَاهُمْ) "Je, huwajawaona (huwajui) wale waliotoka katika miji yao, kwa kuogopa kifo nao wakiwa ni maelfu kwa maelfu? Mwenyezi Mungu akawaambia: Kufeni! Kisha akawafufua."
- Aya ya 259: (أَوْ كَالَّذِي مَرَّ عَلَى قَرْيَةٍ وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَى عُرُوشِهَا قَالَ أَنَّى يُحْيِي هَذِهِ اللَّهُ بَعْدَ مَوْتِهَا فَأَمَاتَهُ اللَّهُ مِائَةَ عَامٍ ثُمَّ بَعَثَهُ) "Au kama yule aliyepita karibu na mji uliokwisha poromoka (ulioteketea) na kulaliwa na paa zake, akasema: Ataufufuaje Mwenyezi Mungu mji huu baada ya kufa kwake? Mwenyezi Mungu akamfisha kwa muda wa miaka mia moja, kisha akamfufua."[52]
Pia katika Taurati kumetajwa matukio ya kurejea uzimani kwa baadhi ya watu, mfano kuhuishwa kwa mtoto kupitia Nabii Al-Yasa, [53] na kuhuishwa kwa kijana kupitia Nabii Iliya (ambaye ni miongoni mwa Manabii wa Bani Israil). [54]
- Aya Nyinginezo zinazotumika kuthibitisha Al-Raj'a pale zinapounganishwa na mapokezi ya Hadithi kuhusiana na tafsiri ya Aya hizo. Nazo ni: Suratu an-Naml, Aya ya 82: (وَإِذَا وَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِمْ أَخْرَجْنَا لَهُمْ دَابَّةً مِنَ الْأَرْضِ تُكَلِّمُهُمْ) ; Suratu al-Qasas, Aya ya 85: (إِنَّ الَّذِي فَرَضَ عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لَرَادُّكَ إِلَى مَعَادٍ) ; Suratu Ali 'Imran, Aya ya 157: (وَلَئِنْ قُتِلْتُمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ أَوْ مُتُّمْ لَمَغْفِرَةٌ مِنَ اللَّهِ وَرَحْمَةٌ خَيْرٌ مِمَّا يَجْمَعُونَ) ; Suratu as-Sajdah, Aya ya 21: (وَلَنُذِيقَنَّهُمْ مِنَ الْعَذَابِ الْأَدْنَى دُونَ الْعَذَابِ الْأَكْبَرِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ) ; Suratu Ghafir, Aya ya 11: (قَالُوا رَبَّنَا أَمَتَّنَا اثْنَتَيْنِ وَأَحْيَيْتَنَا اثْنَتَيْنِ فَاعْتَرَفْنَا بِذُنُوبِنَا) ; Suratu al-Ma'idah, Aya ya 20: (وَإِذْ قَالَ مُوسَى لِقَوْمِهِ يَا قَوْمِ اذْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ إِذْ جَعَلَ فِيكُمْ أَنْبِيَاءَ وَجَعَلَكُمْ مُلُوكًا) ; Suratu an-Nisa, Aya ya 159: (وَإِنْ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ) ; na Suratu al-Anbiya, Aya ya 95: (وَحَرَامٌ عَلَى قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَاهَا أَنَّهُمْ لَا يَرْجِعُونَ) . [55]
Hadithi Mutawatir Kuhusu Al-Raj'a
Inasemekana kuwa, kuna Hadithi Mutawatir kuhusiana na Al-Raj'a. [56] Allamah al-Majlisi amebainisha katika kitabu chake cha Haqq al-Yaqin kuwa amefanikiwa kukusanya zaidi ya hadithi 200 zilizorekodiwa na waandishi zaidi ya 40 wa madhehebu ya Shia Imamiyyah. [57] Hadithi hizi zinasemekana kuwa zimenukuliwa katika vyanzo 50 vya hadithi vinavyoaminika, ambapo mwanazuoni huyu alizikusanya kwa pamoja chini ya mada maalum aliyoipa jina la Babu al-Raj'ah (Mlango wa Urejeo) ndani kitabu chake maarufu kiitwacho Bihar al-Anwar. [58] Mwanazuoni huyu anasisitiza kwamba, kama mapokezi yanayohusiana na Al-Raj'a hayatachukuliwa kuwa ni mutawatir, basi haitakuwa ni halali kwa mtu yeyote yule kudai kuwepo kwa jambo lolote lile katika dini, lililothibitika kupitia mfululizo wa Hadithi (Mutawatir). [59]
Sayyid Abdullah Shubbar naye anaona kuwa Hadithi zinazozungumzia kurejea kwa Imam Ali (a.s) na Imam Hussein (a.s) zimefikia kiwango cha thibitisho lililosimama kwa njia ya mutawatir, na anaeleza kuwa, Hadithi zinazofafanua kurejea kwa Maimamu wengine wote waliotakasika (a.s) ziko karibu sana na kiwango hicho cha uthabiti (yaani ni Mutawatir). [60] Aidha, kuna ishara za wazi zinazothibitisha ukweli wa Al-Raj'a ndani ya baadhi ya dua na ziara maarufu zilizopokewa kutoka kwa Ahlul Bait (a.s), miongoni mwa dua hizo ni: Du'a al-Ahd, Du'a Dahwu al-Ardh, Al-Ziaratu al-Jamiah al-Kabirah, Al-Ziaratu al-Mutlaqah ya Imamu Hussein (a.s), Ziaratu Aal Yasin, na Ziaratu al-Imamu al-Mahdi (a.s). [61]
Uwezekano wa Kiakili
Mbele ya mtazamo wa Kiimamiyyah, Al-Raj'a huhesabiwa kuwa ni mojawapo ya mambo yanayowezekana kutokea kiakili, bali ni tukio litakalotokea bila ya pingamizi yoyote. [62] Wanazuoni wa Shia wanalichukulia suala hili kuwa si jambo lisilowezekana mbele ya uwezo wa Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ana uwezo kamili wa kuwahuisha baadhi ya waja Wake baada ya kufa na kabla ya kufika Siku ya Kiama, na kuwarejesha tena duniani humu. Aidha tayari kumeshawahi kutokea tukio la namna hii katika baadhi ya nyumma zilizopita,[63] hii ni kwa mujibu wa ushahidi uliothibitishwa na maandiko ya Qur'ani Tukufu.[64] Pamoja na kuwepo kwa ushahidi huo, kuna baadhi ya watu ambao hawajakubali kabisa uwezekano wa kutokea na kuhakikika kwa Al-Raj'a, [65]huku wengine wakiwa na shaka juu ya kutokea kwake. [66]
Falsafa na Hekima ya Al-Raj'a
Ufuatayo ni muhtasari wa mambo makuu yaliyobainishwa kama ndiyo kiini cha hekima ya kurejea ulimwenguni kabla ya Kiama katika mapokezi ya Hadithi na maneno ya wanazuoni:
- Kulipiza kisasi dhidi ya madhalimu na kuzipoza nyoyo za waumini: Inaelezwa kuwa, tukio la Al-Raj'a linajumuisha makundi mawili makuu ya wanadamu. Kundi la kwanza ni lile la watu wenye imani ya daraja la juu kabisa, ambao Mwenyezi Mungu atawarejesha duniani ili wajionee wenyewe namna mamlaka ya haki yanavyopata heshima. Kundi la pili linajumuisha wale madhalimu wakuu, ambao kuadhibiwa na kulipizwa kisasi kwao, hupelekea kufarajika kwa nyoyo za waliodhulumiwa. [67]
- Kuwalipa malipo mema watenda mema na kuwaadhibu wakosaji: Inaelezwa katika baadhi ya Hadithi kuwa, kuna kundi maalumu la wanafiki na madhalimu ambao—pamoja na adhabu zao maalum zinazowasubiri Siku ya Kiama— ni lazima wapate sehemu ya adhabu yao hapa duniani. Adhabu hii ni sawa na ile iliyowasibu watu walioasi hapo kale kama vile kina Firauni, kina Aad, Thamud, na kaumu ya Nabii Luti, ambapo njia pekee ya kutekelezeka kwa adhabu hiyo ya kidunia ni kupitia Al-Raj'a. [68]
- Ushindi wa Kiungu: Raj’ah ni mchakato wa utekelezaji wa ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ya kuwapa ushindi Mitume, Maimamu, na waumini kabla ya kufika Siku ya Kiama, pale tu atakapodhihiri Imamu Mahdi (a.f) duniani humu. Hekima hii imejengeka juu ya msingi wa mapokezi ya Hadithi yaliyokuja chini ya Aya ya 51 ya Suratu Ghafir isemayo: (إِنَّا لَنَنْصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ) "Hakika sisi tutawanusuru Mitume wetu na wale walioamini katika maisha ya dunia na siku wataposimama mashahidi." [69]Kulingana na ahadi hii, bila shaka Mwenyezi Mungu atawanusuru Mitume, Maimamu na waumini wa kweli kabla kufika Siku ya Kiama, nao ni ule wakati wa kudhihiri Imamu Mahdi (a.f). [70]
- Kukamilika kwa nafsi za wanadamu: Kitabu cha Tafsir al-Amthal kimetaja kundi maalumu la waumini wa dhati ambao walikumbana na vikwazo mbalimbali maishani mwao wakati wa mapambano yao ya kuelekea kwenye ukamilifu wa kiroho, na hivyo wakafariki kabla ya kuikamilisha safari ya ukamilifu wao. Na hekima ya Kimungu inabidi kudhamini mwendelezo wa harakati za mapambano ya waumini hawa ili kufikia ukamilifu wao, jambo ambalo litabidi kutimizwa kwa kuwarejesha tena ulimwenguni, ili wakamilishe harakati hizo, wawe mashuhuda wa serikali ya haki na uadilifu wa ulimwengu mzima, na wapate kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa dola hiyo adilifu. [71]
- Kujenga matumaini na kujiandaa kwa wanaongojea ukombozi: Al-Raj'a huwapa matumaini makubwa wanadamu, kwa kuwapa ahadi ya kwamba, hata kama watakufa kabla ya kufikia ukombozi huo, watafufuliwa tena ili waishi chini ya utawala wa Imamu Mahdi na kushuhudia zama za kudhihiri kwake. Matumaini haya yanawachochea na kuwatia shime ya kufanya juhudi ili waweze kuwa miongoni mwa waumini wa dhati kabisa. [72]
Vitabu Kuhusu Al-Raj'a

Wanazuoni wa madhehebu ya Shia Imamiyyah wamefanya tafiti mkubwa na kutunga athari nyingi mno kuhusiana na mada hii ya kurejea tena duniani. Katika moja ya makala ya kitaaluma iitwayo "Manba’ Shinaasi Mawdhuu’i Raj’at" (Uchambuzi wa Kimaada wa Vyanzo vya Urejeo), kuna orodha ya athari 127 zilizotungwa kwa ajili ya mada hii. [73] Miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa kwa ajili ya mada hii kama ifuatavyo:
- Kitabu cha Al-Iiqadhu min al-Haj’ah bi al-Burhan ‘ala al-Raj’ah: Kilicho andikwa na Al-Hurr al-'Amili. Mwandishi huyu ametegemea Aya za Qur'ani na mapokezi ya Hadithi ili kuthibitisha haki na usahihi wa imani ya Al-Raj'a kwa mujibu wa mtazamo wa Kiiyamiyyah. Ameeleza kwamba, lengo lake kuu la kuandika kitabu hichi ni kuyajibu makundi matatu ya Washia: wale waliokuwa na kusitasita na kuwa na mashaka katika kuamini suala hili, wale wanaolikataa kabisa, na wale waliojaribu kufanya taawili (upotoshaji wa maana) za hadithi zilizopokewa kuhusu mada hii. [74]
- Kitabu cha Raj'at (Urejeo): Kilicho andikwa na Allamah al-Majlisi. Kitabu hichi kimeandikwa kwa lugha ya Kiajemi (Kifarsi), ambapo ndani Allamah al-Majlisi amechambua kwa kina kabisa Hadithi kumi na nne zinazohusu kudhihiri kwa Imamu Mahdi (a.f) pamoja na maudhui ya Al-Raj'a. [75]
- Kitabu cha Al-Shiah wa al-Raj’ah (Washia na Urejeo): Kilicho andikwa na Muhammad Ridha al-Tabasi al-Najafi. Mtunzi anafafanua katika maandiko haya nafasi ya Al-Raj'a ndani ya Qur'ani Tukufu, katika dua na ziara, pamoja na makubaliano ya kauli moja (ijmai) ya mafakihi na maoni ya wanazuoni wa theolojia kuhusu suala hili. [76]
- Kitabu cha Al-Raj'a aw al-'Awdah ila al-Hayati al-Dunia Ba'ada al-Maut (Kurejea au Kurudi Kwenye Maisha ya Dunia Baada ya Kifo): Kilicho andikwa na Ali Musa al-Ka'abi. Mtunzi anafafanua katika kitabu hiki dalili za Hadithi na za Qur'ani zinazohusu Al-Raj'a na uwezekano wa kutokea kwake.[77]
- Kitabu cha Bazgasht be Dunia dar Payane Tarikh (Tahlil wa Barrasi Mas'aleye Raj'at) (Kurudi Duniani Mwishoni mwa Historia - Uchambuzi na Tathmini ya Suala la Raj'ah): Kilicho andikwa na Khodamurad Suleimiyan. Kitabu hiki kinajumuisha sura kumi zinazozungumzia mada zifuatazo: Mijadala ya maneno (Kilugha), Al-Raj'a kwa mtazamo wa madhehebu ya Kiislamu, Zama za Al-Raj'a, Uwezekano wa kutokea Al-Raj'a, Al-Raj'a katika zama za mwisho, Utata na ukosoaji na mapitio yake, Watu watakaorejea, Majukumu (Taklifu) katika zama za Al-Raj'a, na Malipo na adhabu katika Al-Raj'a.[78]
Rejea
- ↑ Al-Hurr al-'Amili, Al-Iqadhi min al-Haj'ah, uk. 423.
- ↑ Sheikh al-Mufid, Awa'il al-Maqalat, uk. 324.
- ↑ Ibn Manzur, Lisan al-'Arab, chini ya neno "Raja'a".
- ↑ Tazama: At-Tabari, Dala'il al-Imamah, uk. 542.
- ↑ Ridhwani, Maw'ud Shinasi wa Pasokh be Shubuhat, uk. 661.
- ↑ Al-Muzaffar, Bidayat al-Ma'arif al-Ilahiyyah, Juz. 2, uk. 169.
- ↑ Kiyani Farid, "Raj'at", uk. 593.
- ↑ Al-Hurr al-'Amili, Al-Iqaz min al-Haj'ah, uk. 101.
- ↑ Sheikh as-Saduq, Al-I'tiqadat, uk. 60.
- ↑ Shaykh al-Mufid, Awa'il al-Maqalat, uk. 48.
- ↑ Sayyid al-Murtadha, Rasa'il ash-Sharif al-Murtadha, Juz. 1, uk. 125.
- ↑ Salimiyan, Bazgasht be Donya dar Payan-e Tarikh, uk. 39.
- ↑ Al-'Allamah al-Majlisi, Haqq al-Yaqin, Juz. 2, uk. 335.
- ↑ Al-'Allamah al-Majlisi, Haqq al-Yaqin, Juz. 2, uk. 354.
- ↑ Shubbar, Haqq al-Yaqin, Juz. 2, uk. 337.
- ↑ Al-Hurr al-'Amili, Al-Iqaz min al-Haj'ah, uk. 96.
- ↑ As-Safi al-Gulpaygani, Majmu'at ar-Rasa'il, Juz. 2, uk. 406.
- ↑ Al-Amin, Naqd al-Washi'ah, uk. 376; Mughniyyah, Al-Jawami' wa al-Fawariq, uk. 300–302; Al-Muzaffar, Aqa'id ash-Shi'ah, uk. 84.
- ↑ Al-Musawi al-Ardabili, Taqrirat-e Falsafah (Taqrirat Dars-e Falsafah Imam Khomeini), Juz. 3, uk. 197.
- ↑ Sheikh al-Mufid, Awa'il al-Maqalat, uk. 46.
- ↑ Shubbar, Haqq al-Yaqin, Juz. 2, uk. 337.
- ↑ Tazama: Al-Hurr al-'Amili, Al-Iqaz min al-Haj'ah, uk. 95; Mutahhari, Majmu'ah Athar, Juz. 4, uk. 562.
- ↑ Mutahhari, Majmu'ah Athar, Juz. 4, uk. 562.
- ↑ Al-Musawi al-Ardebili, Taqrirat-e Falsafah (Taqrirat Dars-e Falsafah Imam Khomeini), Juz. 3, uk. 197.
- ↑ Muhammadi, "Falsafah-ye Raj'at az Manzar-e Ayatullah Shah Abadi", uk. 85.
- ↑ "Raj'at dar Qur'an wa Andishe-ye Shi'iyan", tovuti ya Athar-e Ustadh Muhammad Baqir Behbudi.
- ↑ Sayyid al-Murtadha, Rasa'il ash-Sharif al-Murtadha, Juz. 1, uk. 125; Al-Hurr al-'Amili, Al-Iqaz min al-Haj'ah, uk. 94.
- ↑ Sayyid al-Murtadha, Rasa'il ash-Sharif al-Murtadha, Juz. 1, uk. 125.
- ↑ Muhammadi ar-Rayshahri, Daneshnameh-ye Imam Mahdi (a.s.) bar Asas-e Qur'an, Hadith wa Tarikh, Juz. 8, uk. 77.
- ↑ Tazama: Shaykh al-Mufid, Awa'il al-Maqalat, uk. 77; Sayyid al-Murtadha, Rasa'il ash-Sharif al-Murtadha, Juz. 1, uk. 125; At-Tabrisi, Majma' al-Bayan, Juz. 7, uk. 367; Al-Hurr al-'Amili, Al-Iqaz min al-Haj'ah, uk. 38.
- ↑ Shaykh al-Mufid, Al-Irshad, uk. 369–370.
- ↑ Tazama: Al-Hilli, Mukhtasar al-Basa'ir, uk. 120–122.
- ↑ Tazama: Al-Ka'bi, Al-Raj'a wa al-'Awdah, uk. 55.
- ↑ Al-'Ayyashi, Tafsir al-'Ayyashi, Juz. 2, uk. 281.
- ↑ Sheikh al-Mufid, Al-Ikhtisas, uk. 257–258; Al-'Ayyashi, Tafsir al-'Ayyashi, Juz. 2, uk. 326.
- ↑ Al-Qummi, Tafsir al-Qummi, Juz. 2, uk. 391.
- ↑ Al-Ka'bi, Al-Raj'a aw al-'Awdah, uk. 53–54.
- ↑ Al-Hilli al-'Amili, Mukhtasar al-Basa'ir, uk. 91; Al-'Allamah al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Juz. 53, uk. 64.
- ↑ Tazama: Al-Qummi, Muhammad, Tafsir al-Qummi, 1404 H, Juz. 2, uk. 147.
- ↑ Tazama: Al-Qummi, Muhammad, Tafsir al-Qummi, 1404 H, Juz. 2, uk. 147. Al-Qummi, Tafsir al-Qummi, Juz. 1, uk. 25; Al-Hurr al-'Amili, Al-Iqaz min al-Haj'ah, uk. 345; Al-'Allamah al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Juz. 53, uk. 108–109.
- ↑ Tazama: Al-Kulayni, Al-Kafi, Juz. 8, uk. 50–51.
- ↑ Tazama: Al-'Ayyashi, Tafsir al-'Ayyashi, Juz. 2, uk. 32; Al-'Allamah al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Juz. 53, uk. 68.
- ↑ Al-'Allamah al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Juz. 51, uk. 56.
- ↑ Al-'Ayyashi, Tafsir al-'Ayyashi, Juz. 2, uk. 32.
- ↑ Al-'Ayyashi, Tafsir al-'Ayyashi, Juz. 2, uk. 112–113; Al-Hilli al-'Amili, Mukhtasar al-Basa'ir, uk. 93.
- ↑ At-Tabari, Dala'il al-Imamah, uk. 484.
- ↑ Al-Qummi, Tafsir al-Qummi, Juz. 1, uk. 385; Al-'Allamah al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Juz. 53, uk. 24.
- ↑ Suratu An-Naml, Aya ya 83.
- ↑ Sura Al-Kahf, Aya ya 47.
- ↑ Tazama: Shaykh al-Mufid, Awa'il al-Maqalat, uk. 325; At-Tabrisi, Majma' al-Bayan, Juz. 7, uk. 405–406; Shabbar, Haqq al-Yaqin, Juz. 2, uk. 298–299; Mughniyyah, Al-Jawami' wa al-Fawariq, uk. 300–301.
- ↑ Al-Qummi, Tafsir al-Qummi, Juz. 1, uk. 24.
- ↑ Sheikh al-Mufid, Awa'il al-Maqalat, uk. 324–325.
- ↑ 'Agano la Kale, Kitabu cha Wafalme wa Pili, kifungu cha 32–38.
- ↑ Agano la Kale, Kitabu cha Wafalme wa Kwanza, kifungu cha 17–24.
- ↑ Tazama: Shabbar, Haqq al-Yaqin, Juz. 2, uk. 299–304.
- ↑ Al-Hurr al-'Amili, Al-Iqaz min al-Haj'ah, uk. 73–74; Shabbar, Haqq al-Yaqin, Juz. 2, uk. 305.
- ↑ Al-'Allamah al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Juz. 53, uk. 39.
- ↑ Al-'Allamah al-Majlisi, Haqq al-Yaqin, Juz. 2, uk. 336.
- ↑ Al-'Allamah al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Juz. 53, uk. 123.
- ↑ Shubbar, Haqq al-Yaqin, Juz. 2, uk. 337.
- ↑ Tazama: At-Tabrisi, Al-Ihtijaj, Juz. 2, uk. 494; Al-Qummi, Mafatih al-Jinan, uk. 249, 325, 524, 540 na 548.
- ↑ Tazama: At-Tabrisi, Majma' al-Bayan, Juz. 7, uk. 405.
- ↑ At-Tabrisi, Majma' al-Bayan, Juz. 7, uk. 405.
- ↑ Tazama: Sura Al-Baqarah, Aya za 56, 73 na 259.
- ↑ Salimiyan, Bazgasht be Donya dar Payan-e Tarikh, uk. 59.
- ↑ Tazama: Al-Alusi, Tafsir Ruh al-Ma'ani, Juz. 10, uk. 237.
- ↑ Shaykh al-Mufid, Awa'il al-Maqalat, uk. 78; Shaykh al-Mufid, Al-Fusul al-Mukhtarah, uk. 153; Al-'Allamah al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Juz. 53, uk. 39 na 126.
- ↑ Shaykh al-Mufid, Al-Fusul al-Mukhtarah, uk. 155; Al-'Allamah al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Juz. 53, uk. 126–127; Makarim ash-Shirazi, Tafsir al-Amthal, Juz. 12, uk. 145.
- ↑ Suratu Ghafir, Aya ya 51.
- ↑ Al-Hurr al-'Amili, Al-Iqaz min al-Haj'ah, uk. 345–346.
- ↑ Makarim ash-Shirazi, Tafsir al-Amthal, Juz. 12, uk. 146. Muhammadi ar-Rayshahri, Daneshnameh-ye Imam Mahdi, Juz. 8, uk. 50.
- ↑ Muhammadi ar-Reishahri, Daneshnamehye Imam Mahdi, Juz. 8, uk. 50.
- ↑ Zuhush, "Manba-Shinasi Mawdhui Raj'at", uk. 72–80.
- ↑ Al-Hurr al-'Amili, Al-Iqadhi min al-Haj'ah, uk. 44–45.
- ↑ Al-'Allamah al-Majlisi, Raj'at, uk. 50.
- ↑ Al-Ka'bi, Al-Raj'a awi al-'Awdah ila al-Hayati ad-Dunia Ba'ada al-Maut, uk. 105.
- ↑ Al-Ka'bi, Al-Raj'a aw al-'Awdah ila al-Hayati al-Dunia Ba'ada al-Maut, uk. 105.
- ↑ Suleimiyan, Bazgasht be Dunia dar Payane Tarikh, uk. 7–12.
Vyanzo
- Qur'ani Tukufu.
- Taurati.
- Raj'at dar Qur'an wa Andishe Shieyan, tovuti ya Athar Ustadh Muhammad Baqir Bihbudi.
- Al-Alusi, Mahmud bin Abdullah, Tafsir Ruh al-Ma'ani, Beirut, Dar al-Kutub al-Ilmiyyah, 1415 H.
- Al-Amin, Sayyid Muhsin, Naqd al-Washi'ah, Beirut, Muassasat al-A'lami li al-Matbuu'at, 1403 H.
- Al-Hurr al-'Amili, Muhammad bin Hassan, Al-Iiqadh min al-Haj'ah bi al-Burhan 'ala al-Raj'ah, Qum, Kitengo cha Uchapishaji cha Dalile Maa, 1386 Sh (2007 M).
- Al-Hilli al-'Amili, Hassan bin Suleiman bin Muhammad, Mukhtasar al-Basa'ir, Qum, Muassasat al-Nashr al-Islami, Chapa ya kwanza, 1421 H.
- Sayyid al-Murtadha, Ali bin Hussein, Rasa'il al-Sharif al-Murtadha, Qum, Dar al-Qur'an al-Karim, 1405 H.
- Sheikh al-Saduq, Muhammad bin Ali, Al-I'tiqadat, Qum, Kongamano la Sheikh al-Mufid, 1414 H.
- Sheikh al-Mufid, Muhammad bin Muhammad, Awa'il al-Maqalat fi al-Madhahib wa al-Mukhtarat, Beirut, Dar al-Mufid, 1414 H.
- Sheikh al-Mufid, Muhammad bin Muhammad, Al-Irshad, Qum, Kongamano la Sheikh al-Mufid, Chapa ya kwanza, 1413 H.
- Sheikh al-Mufid, Muhammad bin Muhammad, Al-Ikhtisas, Qum, Kongamano la Sheikh al-Mufid, Chapa ya kwanza, 1413 H.
- Sheikh al-Mufid, Muhammad bin Muhammad, Al-Fusul al-Mukhtarah, Qum, Kungarah Sheikh al-Mufid, Chapa ya kwanza, 1413 H.
- Safi Gulpaygani, Lutfullah, Majmu'atu al-Rasa'il, Qum, Muassasat Imam al-Sadiq (a.s), 1404 H.
- Al-Tabrisi, Ahmad bin Ali, Al-Ihtijaj, imehaririwa na Muhammad Baqir Khurasan, Mashhad, chapa ya Murtadha, 1403 H.
- Al-Tabrisi, Fadl bin Hassan, Majma' al-Bayan, Beirut, chapa ya al-A'lami li al-Matbu'at, 1414 H.
- Al-Tabari, Muhammad bin Jarir, Dala'il al-Imamah, Qum, Taasisi ya al-Bi'ithah, Chapa ya kwanza, 1413 H.
- Al-'Allamah al-Majlisi, Muhammad Baqir, Bihar al-Anwar, Beirut, Taasisi ya al-Wafa', 1403 H.
- Al-'Allamah al-Majlisi, Muhammad Baqir, Haqq al-Yaqin, Qum, chapa ya Islamiyyah, bila tarehe.
- Al-'Allamah al-Majlisi, Muhammad Baqir, Raj'ah, Qum, chapa ya Dalile Maa, 1386 Sh. (2007 M).
- Al-'Ayyashi, Muhammad bin Mas'ud, Tafsir al-'Ayyashi, imehaririwa na Sayyid Hashim Rasuli Mahallati, Tehran, Chapa ya kwanza, 1380 H.
- Al-Qummi, Sheikh Abbas, Kulliyyat Mafatih al-Jinan, Qum, chapa ya Uswah, bila tarehe.
- Al-Qummi, Ali bin Ibrahim, Tafsir al-Qummi, imehaririwa na Tayyib Musawi Jazairi, Qum, Dar al-Kitab, chapa ya tatu, 1404 H.
- Al-Mudhaffar, Muhammad Ridha, Bidayat al-Ma'arif al-Ilahiyyah fi Sharhi 'Aqa'id al-Imamiyyah, maelezo ya Sayyid Muhsin Kharazi, Qum, Muassasat al-Nashre al-Islami, 1417 H.
- Al-Mudhaffar, Muhammad Ridha, Aqa'id al-Shi'ah, Qum, Ansariyan, 1429 H.
- Al-Ka'abi, Ali Musa, Al-Raj'ah aw al-'Awdah ila al-Hayati al-Dunia Ba'ada al-Maut, Qum, Taasisi ya Markaz al-Risalah, 1426 H.
- Al-Kulaini, Muhammad bin Ya'qub, Al-Kafi, imehaririwa na Muhammad Akhundi na Ali Akbar Akhundi, Tehran, Dar al-Kutub al-Islamiyyah, 1407 H.
- Ridhwani, Ali Asghar, Maw'ud Shenasi wa Pasokh be Shubuhat, Qum, Masjid Muqaddas Jamkaran, 1388 Sh. (2009 M).
- Zadehush, Muhammad Ridha, Manbashenasi Maudhue Raj'at, Jarida la kila mwezi la Din, Toleo Na. 62, Azar 1381 Sh. (2002 M).
- Suleimiyan, Khodamurad, Bazgasht be Dunia dar Payane Tarikh (Uchambuzi na Tathmini ya Suala la Raj'a), Qum, Bustan Kitab, 1387 Sh. (2008 M).
- Shubbar, Abdullah, Haqqu al-Yaqin fi Ma'rifat Usul al-Din, Beirut, Taasisi ya al-A'lami li al-Matbu'at, 1418 H.
- Muhammadi Raishahri, Muhammad, Daneshname Imam Mahdi (a.f) bar Asase Qur'an, Hadith wa Tarikh, Qum, Intisharat Dar al-Hadith, 1393 Sh. (2014 M).
- Muhammadi, Behzad, Falsafahye Raj'at az Manzare Ayatullah Shah Abadi, Andishahe Novin, Toleo Na. 41, Kiangazi 1394 Sh. (2015 M).
- Mutahhari, Murtadha, Majmu'ah Athar, Qum, Intisharat Sadra, 1390 Sh. (2011 M).
- Mughniyyah, Muhammad Jawad, Al-Jawami' wa al-Fawariq, Beirut, Muassasat 'Izz al-Din, 1414 H.
- Musawi Ardebili, Abd al-Ghani, Taqrirate Falsafe (Taqrirat Darse Falsafe Imam Khomeini), Tehran, Muassasah Tanzim wa Nashr Athar Imam Khomeini, 1381 Sh. (2002 M).
- Makarim Shirazi, Nasir, Tafsir Nemuneh, Tehran, Dar al-Kutub al-Islamiyyah, 1374 Sh. (1995 M).
- Kiani-Farid, Maryam, Raj'at, ndani ya Danishnamah Jahan-i Islam, Juz. 19, Tehran, Bunyad Da'irat al-Ma'arif al-Islamiyyah, 1393 Sh. (2014 M).
- Ibn Mandhur, Muhammad bin Mukarram, Lisan al-'Arab, Beirut, Dar al-Sadir, 1414 H.