Nenda kwa yaliyomo

Kuosha maiti

Kutoka wikishia
Qur'an: 2: 156; Sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea

Kuosha maiti (Kiarabu: غسل الميت) ni moja ya majosho ya faradhi (wajibu), ambayo inahusu kuosha maiti ya Muislamu kwa mfumo maalum. Katika josho hili, maiti yapaswa kuoshwa mara tatu kwa maji yaliyochanganywa na majani ya mkunazi (cedar), maji yaliyochanganywa na karafuu maiti na kwa maji safi. Ikiwa majani ya mkunazi na karafuu maiti haikupatikani, maiti huogeshwa kwa maji safi tu, na ikiwa haiwezekani kumwogesha kwa maji, hufanyiwa tayammum (hutayamamishwa).

Ni wajibu kumwosha maiti aliyefariki akiwa na umri wa miezi minne au zaidi. Bila shaka kuna hukumu tofauti kuhusiana na mtu aliyekufa kishahidi, tofauti hii ni kwamba, aliyekufa kishahidi huwa huzikwa bila ya kuoshwa.

Tendo la kumwosha maiti, ni tendo lenye hukumu ya wajibu kifaya, na ni haramu kwa muoshaji maiti kupokea ujira kutokana na kazi hiyo.

Umuhimu na nafasi yake

Josho la maiti ni moja wapo ya matendo ya wajibu kifaya, ambapo kama Muislamu atafariki dunia, basi itakuwa ni wajibu kwa Waislamu waliohai kuiosha maiti ya Muislamu huyo. Haifai wala haijuzu kumzika Muislamu bila ya kumuosha. [1] Mara nyingi kila sehemu ya kuzikia maiti (mava), karibu yake huwa na sehemu maalumu ya kukoshea maiti (tamaduni hii ipo Iran na baadhi ya nchi). [5]

Katika kitabu cha Wasal al-Shia, kuna idadi ya hadithi 175 zimepokewa kuhusu kuosha maiti. [6] Katika Hadithi iemeelezwa ya kwamba; kuosha maiti ni moja ya sababu za kumuepusha mtu (mkoshaji) kutokana na moto wa Jahannam, na Mwenyezi Mungu siku ya Kiama atampa muoshaji maiti nuru itakayomuongoza hadi Peponi [7] Pia, kwa mujibu wa Hadithi kutoka kwa Imam Baqir (a.s), kuosha maiti ya muumini hupelekea kupata msamaha wa dhambi ndondogo za muda wa mwaka mmoja. [8]

Maiti kabla ya kukoshwa huwa ni najisi, hivyo basi ni wajibu kwa mtu atakayeugusa mwili wa maiti ambao tayari umeshakuwa baridi kuoga josho la kuugusa mwili wa maiti. Mwili wa maiti ambaye tayari amesha koshwa huwa ni safi, na si tatizo kuugusa mwili wake, wala haitopelekea mtu kuwajibika kukoga josho la kumgusa maiti. [9]

Namna ya kukosha maiti

Kijusi hakihitaji kuoshwa kabla ya kufikia umri wa miezi minne, lakini ikiwa kijusi kimeshatimia umri wa miezi minne, basi ni lazima kioshwe kabla ya kuzikwa kwake. [10]

Kwa mujibu wa fat'wa za mafaqihi wenye mamlaka ya kutoa fat'wa, maiti yapaswa kuoshwa mara tatu kwa utaratibu ufuatao: kwa maji yaliyochanganywa na majani ya mkunazi (cedar), kwa maji yaliyochanganywa na karafuu maiti, na kwa maji safi. Katika kukosha maiti, ni sawa na majosho mengine ya wajibu, ni lazima kutiwe nia ya kukosha josho la maiti kabla ya kuanza kazi hiyo, baada ya nia, kwanza kikoshwe kichwa na shingo, kisha upande wa kulia na kisha upande wa kushoto wa maiti. [11]

Ikiwa majani ya karafuu maiti au mkunazi yameadimika, maiti hiyo itabidi kuikosha kwa maji ya kawaida, ila kuna tofauti ya maoni katika hali ya kukosekana kwa karafuu maiti na majani ya mkunazi, kwamba je, katika hali hiyo, maiti atatakiwa kukoshwa kwa maji safi mara moja tu au akoshwe mara tatu. [12] Pia, ikiwa haiwezekani kuisho maiti hiyo kutokana na hali maalumu, basi itabidi atayamamishwe, pia kuna maoni tofauti kuhusu kumtayamamisha maiti, kwamba je, atayamamishwe mara moja tu au mara tatu. [13]

Maiti ya shahidi aliyeuliwa vitani haioshwi

Kwa mujibu wa fat'wa za mafaqihi wa Kishia, maiti ya shahidi aliyekufa vitani huwa haioshwi, [14] ila kama mtu atajeruhiwa vitani, kisha akafariki baada ya kumalizika vita, huyo yeye atabidi aoshwe. [15] Kwa mujibu wa maoni ya Sayyid Muhammad Kadhim Tabatabai, ni kwamba; Shahidi wa vitani ni yule ambaye aliyeingia vitani kwa idhini ya Imamu Maasumu, au kwa idhini ya naibu makhususi wa Imamu Maasumu kisha akauwawa vitani humo, au mtu aliyekwenda kuutetea Uislamu katika zama ambazo jamii haina Imamu dhahiri (zama za Ghaiba), huyo pia huhisabiwa ni shahidi. [16]

Kanuni nyingine za kukosha maiti

  • Muoshaji lazima awe Muislamu, Shia anayeamini Maimamu Kumi na Wawili, mtu mzima na mwenye akili timamu. [17] Pia, maiti ya mwanamume lazima ioshwe na mwanamume, na maiti ya mwanamke lazima ioshwe na mwanamke. [18] Ila hakuna tatizo mumu kuosha maiti ya mkewe na mke kuosh maiti ya mumewe, ila imesisitisha zaidi mwanamke kukoshwa na mwanamke mwenziwe na mwanamme kukoshwa na mwanamme mwenziwe. [19]
  • Kwa mujibu wa fat'wa za mafaqihi wenye mamlaka ya kutoa fat'wa, ni haramu kuchukua ujira kwa ajili ya kukosha maiti, na kwa mujibu wa fat'wa za baadhi yao, kama kazi hii haitakuwa na nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, basi josho hilo litabatilika. Bila shaka, inaruhusiwa kupokea ujira kwa ajili ya matayarisho ya kumtayarisha maiti au kutayarisha mazingira ya usafishaji. [20]
  • Iwapo mtu aliyehukumiwa kifo atakoga josho la maiti kabla ya kunyogwa kwake, basi mtu hahitaji kuoshwa tena baada ya kuuawa. [21]
  • Sio sahihi kumuosha maiti kwa kumzamisha katika maji (ghuslu irtimasi). [22]
  • Ni lazima maiti awe tohara (hana najisi) kwabla ya kumuosha.[23]
  • Muosha maiti ni lazima aombe ruhusa kwa walii (mmiliki wa kisheria) wa maiti. [24]
  • Haijuzu kuiosha maita ya kafiri. [25]
  • Inapendekezwa kwamba kichwa na kifua cha maiti kiwe juu zaidi kuliko miguu yake, kiasi ya kwamba mwili wake uelekee Qiblah kama vile anavyowekwa wakati wa kutoka roho (wakati wa kufa). [26]
  • Kukausha maiti baada ya kuoga kwa kitambaa safi.
  • Mwenye kuosha mwili wa maiti ajishughulishe na dhikri ya kumdhukuru Allah na kuomba msamaha na akariri sana ibara isemayo "Rabbi Afwaka Afwaka". [27]
  • Muosha maiti hatakiwi kutoa aibu za maiti ambazo pengine amekutana nazo akiwa katika hali ya kumwosha maiti huyo. [28]

Josho la maiti za Maimamu (a.s)

Kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, kila Imamu huogeshwa tu na Imamu anayefuata baada yake. [29] Katika vitabu vya Hadith kuna mlango maalumu usemao ((أَنَّ الْإِمَامَ لَا يُغَسِّلُهُ إِلَّا إِلامَام ; Maiti ya Imamu Haioshwi Ila na Imamu)). [30] Baada kuuawa shahidi kwa Imam Mahdi (a.t.f.s), Imamu Husein (a.s) atarejea duniani kisha ataukosha mwili wa Imam Mahdi (a.t.f.s), atausalia na kuuzika. [31]

Rejea

Masuala yanayofungamana

Vyanzo