Nenda kwa yaliyomo

Ali bin Muhammad al-Samuri

Kutoka wikishia
Kaburi la Ali bin Muhammad al-Samarri lililopo magharibi mwa Baghdad, Iraq

Ali bin Muhammad al-Samarri au al-Samuri (Kiarabu: علي بن محمد السمري) (aliaga dunia 329 Hijiria) ni naibu wa nne na wa mwisho miongoni mwa Manaibu wanne wa Imamu Mahdi (a.t.f.s) ambaye alichukua jukumu na Unaibu baada ya kufariki dunia Hussein ibnu Ruh al-Nawbakhti na alishikilia wadhifa huo kwa muda wa miaka mitatu (326-329 Hijiria). Katika zama za Unaibu wake alikuwa kiunganishi baina ya Imamu Mahdi na Mashia, na watu walikuwa wakimpatia na kumkabidhi yeye fedha zao za malipo ya kisheria (Wujuhat Shari’). Yeye amehesabiwa pia kuwa mmoja wa masahaba wa Imamu Hassan al-Askary (a.s) ambaye alikuwa akiandikiana na Imamu. Kipindi cha Unaibu wa al-Samuri kilikuwa kifupi ikilinganishwa na Manaibu wengine watatu maalumu wa Imamu Mahdi (a.t.f.s), na hakujatolewa maelezo zaidi kuhusiana na hilo. Sababu ya al-Smarri kuwa na harakati chache imetambuliwa kuwa ilitokana na hatua kali za utawala wa wakati huo ambazo zilimzuia kutokuwa na harakati pana na kubwa katika kanali na mtandao wa mawasiliano wa uwakala. Barua (tawqi’) ya Imamu Mahdi kwa Ali bin Muhammad al-Samuri kuhusiana na habari ya kifo chake na kufikia tamati kipindi chake na Unaibu ni miongoni mwa matukio muhimu ya kipindi hiki. Kuaga kwake dunia kulipelekea kufikia tamati mawasiliano ya moja kwa moja ya Manaibu na Imamu Mahdi na kuanza kipindi cha Ghaiba Kubwa.

Historia ya Maisha Yake

Katika vyanzo vya histioria hakujatajwa mwaka aliozaliwa Ali bin Muhammad al-Samuri. Kuniya yake ni Abul-Hassan [1] na lakabu yake imetajwa kuwa ni Samarri, Saimuri, Saimari au Swaimari. Hata hivyo mashuhuri ni al-Samarri. [2] Pamoja na hayo, baadhi ya vyanzo vya Kishia vimesajili lakabu yake kuwa ni al-Samuri. Sammar au Sumarr [3] au Swaymarri ni moja ya vijiji vya mji wa Basra, Iraq ambapo ndugu na jamaa zake walikuwa wakiishi huko. [4]

Ukoo

Ali bin Muhammad alitoka katika familia ya Kishia iliyokuwa imeshikamana na dini ambayo ilikuwa maarufu kwa kuwatumikia Maimamu wa Shia, na asili ya familia yake ilimfanya asikabiliwe na upinzani mkubwa kama Naibu wa Imamu [5]. Yaqoubi anaamini kwamba watu wengi wa familia hii walikuwa na mali nyingi huko Basra na nusu ya mapato ya mali hizi yalitolewa wakfu kwa Imamu wa 11. Imamu alipokea mapato hayo kila mwaka na alikuwa akiandikiana naye barua. [6] Miongoni mwa jamaa wengine wa Samari ni Ali bin Muhammad bin Ziyad ambaye alikuwa mmoja wa wawakilishi wa Maimamu wawili yaani Imamu Hadi na Askary (a.s) na aliandika kitabu kiitwacho "Al-Awsiya" katika kuthibitisha Uimamu wa Imamu wa kumi na mbili (a.s) [7]

Uhusiano wake na Imamu Askary (a.s)

Sheikh Tusi amemwita kuwa ni “Ali bin Muhammad Swaymari” na akamhesabu kuwa ni miongoni mwa masahaba wa Imamu Hassan Askari (a.s) [8] ambaye pia alikuwa akiandikiana na Imamu. Ali bin Muhammad Samari anasema: Abu Muhammad (Imam Askari) aliniandikia: “Kutatokea fitna itakayokupoteza na kukuchanganya. Kuwa makini na jiepushe nayo. Baada ya siku tatu, tukio lilitokea kwa Bani Hashim ambalo liliwasababishia maafa na matatizo mengi. Niliandika barua kwa Imamu: Je! Ndiyo lile tukio ulilosema? Alijibu: "Hapana, ni tofauti na lile. Jilinde." Siku chache baadaye, kukatokea tukio la kuuawa Mu’taz. [9]

Kuaga dunia

Kwa mujibu wa riwaya ya Sheikh Tusi, Samari alifariki mwaka 329 Hijiria na mwili wake ukazikwa Baghdad kwenye mtaa wa Khalanji. [10] Kaburi lake liko jirani na kaburi la Sheikh Kulayni. [11] Mwandishi wa kitabu cha A’yan al-Shia ameitaja tarehe ya kufariki dunia Samuri kuwa ni 15 Shaaban. [12] Sheikh Saduq na Tabarsi waliandika mwaka wa kifo chake kuwa ni 328 Hijiria. [13] [14].

Unaibu kwa Imamu Mahdi (a.t.f.s)

Naibu wa tatu wa Imamu wa Zama (a.t.f.s) aliusia kwamba, Ali bin Muhammad Samari ndiye atakayechukua jukumu lake la Unaibu wa Imamu Mahdi. [15] Chaguo hili lilifanywa kwa amri na maelezo ya Imamu Mahdi (a.t.f.s) mwenyewe. Hakuna riwaya juu ya hili, lakini Tabarsi anaandika katika kitabu cha Ihtjaj: Hakuna hata mmoja katika hawa Manaibu aliyefikia cheo hiki kikubwa, isipokuwa amri ya kuteuliwa kwao ilitolewa na Imamu Mahdi na hivyo mtu wa kabla yake alikuwa akimtangaza mrithi wake. [16]

Kipindi chake cha Unaibu

Hakuna maneno yaliyokuja kuhusiana na harakati za al-Samuri katika kipindi cha Unaibu wa Manaibu watatu wa kabla na hakuna taarifa na maelezo yaliyonukuliwa ya kubainisha kwa mapana na marefu kuhusu harakati zake katika kipindi chake cha Unaibu wa Imamu Mahdi, [17] hata hivyo imeelezwa kwamba, itikadi ya Mashia kwa adhama na uaminifu wake, ilikuwa kama kwa Manaibu wengine, na alikubaliwa na Mashia wote. [18] Kwa mujibu wa riwaya ya Sheikh Saduq, mawakala wake walitambuliwa kuwa ni mabalozi wa kweli wa Imamu na watu walikuwa wakimpatia na kumkabidhi yeye fedha zao za malipo ya kisheria (Wujuhat Shari’). [19]

Kipindi cha Unaibu wa al-Samuri ulikuwa wakati wa ukatili na umwagaji damu, na hii ilisababisha shughuli na harakati zake kuwa za siri zaidi kuliko Manaibu wengine. [20] Baadhi ya watafiti wanaamini kwamba, sababu kuu ya kuwa kifupi kipindi cha Unaibu wake na hata kukatizwa na kufikia tamati zama za Ghaiba ndogo ni mbinyo na ukandamizaji kupita kiasi wa vyombo vya utawala wa Bani Abbas katika zama hizo. [21][22]

Barua (tawqi’) ya Imamu Mahdi

Siku sita kabla ya kuaga dunia al-Samuri, Imamu Mahdi alitoa barua (tawqi’). Katika barua hiyo, Imamu Mahdi alitoa habari ya kifo cha Samuri na kuanza zama za Ghaiba kubwa na akamtaka akamilishe kazi zake zilizobakia na asimtangaze mtu kuwa mrithi wake. [23] [24] Siku sita baada ya barua na andiko hilo la Imamu, mawakala wakuu walikusanyika katika lahadha za mwisho za uhai wa balozi na Naibu wa Nne wa Imamu na wakamuuliza ni nani atakayechukua jukumu lake? Samuri alijibu: Jambo, ni jambo la Mwenyezi Mungu na yeye mwenyewe ndiye atakayeshughulikia mambo. Haya ndiyo yaliyokuwa maneno yake ya mwisho kabla ya kuaga dunia. [25] Baada ya kifo cha Samuri, mawasiliano ya moja kwa moja baina ya Manaibu na Imamu wa Kumi na Mbili yakafikia tamati na huo ndio uliokuwa mwisho wa zama za Ghaiba ndogo (Ghaibat al-Sughra). [26]

Karama

Katika vyanzo vya hadithi kumenukuliwa karama za Ali bin Muhammad al-Samuri ambazo zilikuwa ni kwa ajili ya kuondoa shaka kwa Mashia. Kuwapa habari watu kutoka Qom kuhusiana na kifo cha Ibn Babawayh (baba wa Sheikh Saduq na mkazi wa Qom) ni miongoni mwa karama hizo. [27] Salih bin Shuaib Taliqani ananukuu kutoka kwa Ahmad bin Ibrahim Mukhallad kwamba, mimi nilifika Baghdad kwa Masheikh na katika kikao hicho alikuweko pia Ali bin Muhammad al-Samuri. Yeye alianza kuzungumza na kusema: Mwenyezi Mungu amrehemu Ali bin Babawayh Qummi (baba wa Sheikh Saduq). Mashekhe waliokuweko katika kikao hicho wakaandika tarehe. Hatimaye ikaja habari ya kifo cha Alib bin Babawayh ambayo ilikuwa ni siku ileile. [28]

Rejea

Vyanzo

  • Ghaffārzāda, ʿAlī. Zindigānī-yi nuwwāb-i khāṣ-i Imām Zamān. Qom: Intishārāt-i Nubūgh, 1379 Sh.
  • Jabbārī, Muḥammad Riḍā. Sāzmān-i wikālat wa naqsh-i ān dar ʿaṣr-i aʾimma. Qom: Muʾassisa-yi Āmūzishī Pazhūhishī-yi Imām Khomeini, 1382 Sh.
  • Jaʿfarīyān, Rasūl. Ḥayāt-i Fikrī wa sīyāsī-yi imāmān-i Shīʿa. Qom: Anṣārīyān, 1381 Sh.
  • Jāsim Ḥusayn. Tārīkh-i sīyāsī-yi Imām dawāzdahum. Translated to Farsi by Muḥammad Taqī Āyatollāhī. Tehran: Amīr Kabīr, 1385 Sh.
  • Ṣadr, Sayyid Muḥammad al-. Tārīkh al-ghayba. Beirut: Dār al-Taʿāruf, 1412 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Kamāl al-dīn wa tamām al-niʿma. Tehran: Islāmīyya, 1395 AH.
  • Ṭabrisī, Aḥmad b. ʿAlī al-. Al-Iḥtijāj. Edited by Ibrāhīm Bahādurī. Qom: Uswa, 1383 Sh.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Iʿlām al-warā bi-aʿlām al-hudā. Qom: Āl al-Bayt, 1417 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Ghayba. Qom: Muʾassisat al-Maʿārif al-Islāmīyya, 1411 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Rijāl al-Ṭūsī. Edited by Jawād Qayyūmī Iṣfahānī. Qom: al-Nashr al-Islāmī, 1373 Sh.