Uimamu katika hali ya utotoni
Uimamu katika hali ya utotoni (Kiarabu:الإمامة في الصغر) humaanisha uongozi wa mtu fulani ambaye bado hajafikia ukomavu wa kisheria. Kwa imani ya Shia, Imamu Jawaad (a.s), Hadi (a.s) na Mahdi (a.s), ni miongoni mwa Maimamu 12 wa Shia ambao walifikia cheo cha uongozi (Uimamu) hali wakiwa na umri kati ya miaka 5 hadi 8. Mashia Imamiyyah wanaamini kuwa; Uimamu ni nafasi takatifu ambayo ukomavu sio sharti ya kufikia cheo nafasi hiyo.
Wafuasi wa Shia hujibu wapinzani wa imani yao hiyo kwa kutumia Aya za Qur'an zinazo zungumzia utume wa Nabii Suleiman, Nabii Yahya (a.s) na Nabii Isa (a.s) wakiwa utotoni. Hoja nyengine zitumiwazo kama ni vielelezo vya kuthibitisha imani ni; Uwezo wa kielimu wa Maimamu wakiwa bado wamo katika maisha ya utotoni pamoja na uteuzi wa Imam Ali (a.s) kama ni mrithi wa bwana Mtume (s.a.w.w) katika tukio la Yaumu al-Dar hali akiwa na umri mdogo.
Pia, kuna maandiko yaliyo andikwa kwa ajili ya kufafanua imani ya Shia kuhusiana na iamani ya uongozi wa utotoni na kujibu pingamizi za wapinzani wa imani hiyo.
Umuhimu wa Suala Hili katika Imani ya Imamiyyah
Uongozi wa utotoni bila kufikia ukomavu wa kimwili na kisheria, ni mojawapo ya masuala muhimu yanayo husiana na Uimamu, yanayo jadiliwa katika vitabu vya theolojia. [1] Tafit za mjadala huu zinahusiana zaidi na kujibu pingamizi za wapinzani wa Shia juu ya imamani ya uongozi wa baadhi ya Maimamu wa Shia (Imamu Jawad (a), Imamu Hadi (a), na Imam Mahdi (a)) ambao walipata uongozi kati ya umri wa miaka 5 hadi 8. [2] Suala hili lilisababisha shaka na wasi wasi kwa baadhi ya wafuasi wa Shia katika kuukubali uongozi wa Imamu Jawad (a.s), kwani hadi wakati huo, watu walikuwa waiamini kwamba; moja ya masharti ya mtu kushika na nafasi hiyo, ni kuwa na ukomavu wa kisheria (kubaleghe). [3]
Kwa mtazamo wa wanazuoni wa Ahlu-Sunna, ukomavu ni mojawapo ya masharti muhimu ya uongozi. [4] Hata hivyo, wanazuoni wa Shia wanaamini kwamba; Uimamu ni nafasi ya Kiungu ambayo Mwenye Ezi Mungu humpa nafasi hiyo mtu maalumu mwenye sifa zinazostahili kushia cheo hicho. [5] Mashia Wanaamini kuwa; isma (kutokosea), kuwa na sifa ubora, na kuwepo kwa maandiko ya wazi, ndio masharti muhimu kwa ajili ya cheo cha Uimamu. [6] Imani ya Shia Imamiyyah isemayo kwamba; ukomavu sio sharti kwa Imamu, imezua pingamizi kadhaa kutoka kwa wapinzani wao, jambo amabalo lililazimisha wanateolojia wa Kishia kusimama na kutoa majibu dhidi ya wapinzai hao. [7]
Ibnu Taymiyyah (aliye fariki dunia mnamo mwaka 728 Hijria), Ibn Hajar al-Haytami (aliye fariki mnamo mwaka 974 Hijria), na Ahmad al-Katib, ni miongoni mwa waliotoa pingamizi kuhusiana na imani ya uongozi wa utotoni. [8] Baadhi ya sababu walizotoa kuhusiana na maoni yao ya kwa nini uongozi wa mtoto si wa kimantiki, wamesema kwamba; Mtoto yatima huwa chini ya uangalizi wa watu maalumu, [9] hali ya mtoto ya kutokuwa na uwezo au haki ya kufanya maamuzi, [10] kutokuwa na mamlaka, kutokuwa na wajibu wa kidini, [11] na kutokuwepo kipindi na nafasi ya kujifunza. [12]
Maimamu Waliofikia Uongozi Wakiwa Watoto
- Imamu Jawad (a.s): Alipata uongozi akiwa na umri wa takriban miaka minane. [13] Kwa mujibu wa Hassan bin Musa Nawbakhti (aliyeaga dunia mano mwaka 310 Hijria), ni kwamba; Wakati wa kifo cha Imamu Ridha (a.s) umri mdogo wa Imamu Jawad (a.s) ulisababisha kutoelewana miongoni mwa wafuasi wa Shia, [14] na baadhi yao hawakukubaliana katu na wa mtoto huyo. [15]
- Imamu Hadi (a.s): Alipata nafasi ya uongozi akiwa na umri wa miaka minane. [16] Kwa mujibu wa mtafiti wa kihistoria wa Kiiraqi, Jassim Hussein, kwa sababu suala la Uimamu wa utotoni lilikuwa lilikuwa tayari limesha eleweka wakati wa Imamu Jawad (a.s), hilo lilipelekea uongozi wa Imamu Hadi (a.s) kukubalika bila pingamizi. [17]
- Imamu Mahdi (a.s): Alifikia uongozi akiwa na umri wa miaka mitano. [18] Inasemekana kuwa kufikia uongozi kwa Imamu Jawad (a.s) na Imamu Hadi (a.s) wakiwa watoto kulisahilisha na kuwaandaa wafuasi wa Shia kukubaliana na uongozi wa Imamu Mahdi (a.s) hali akiwa na umri mdogo. [19]
Hoja za Wafuasi wa Shia Katika Kuutetea Uongozi wa Utotoni
Wanateolojia wa madhehebu ya Imamiyyah wakisimamisha hoja zao wamesme kwamba; ukamilifu wa akili hauhusiani kabisa na ukomavu wa kimwili, na kama uongozi wa mtu utakuwa umetibitishwa kwa ushahidi wa yakinifu kabisa, basi kiotomatiki sifa ya isma (kutokosea) na elimu ya Kiungu itathibiti kwa mtu huyo, na umri wa Imamu hauna athari wala uhusiano wowote ule katika suala hilo. Pia, vizuizi ambavyo sharia imeweka kwa ajili ya umri wa utotoni vinahusiana na wanadamu wa kawaida ambao hukua kiakili na kielimu kwa kadri wanavyo endelea kukua, na sio kwa Imamu maasumu ambaye ana elimu asilia kutoka kwa Mungu (elimu laduni). [20]
Uwezo wa Kielimu wa Maimamu Wakiwa Watoto
Kama ilivyosimuliwa na Sheikh Mufid kutoka katika moja ya Riwaya ya kwamba; Imamu Jawad akiwa bado ni kijan mdogo, alishiriki katika mjadala na Yahya bin Aktham na kujibu swali la Yahya kwa namna iliyowashangaza waliokuwepo katika mjadala huo. [21] Kafuatia tukio hili la kushangaza, Mamun alisema kuwaambia waliomzunguka ya kwamba; utoto wa Imamu Jawad (a.s) si kigezo cha upungufu wa elimu na akili yake. [22]
Kwa mujibu wa maelezo ya Sheikh Mufid (aliye fariki dunia mnamo mwaka 413 Hijria), ni kwamba; tukio la kushiriki kwa Hassan na Hussein (a.s) katika tukio la Mubahala kati Mtume (s.a.w.w) na Wakristo wa Najran linaonyesha kwamba, hata mtu akiwa ni mtoto, pia naye anaweza kuwa na majukumu makubwa ya Kiungu katika jamii. [23] Hata, imani ya Imamu Ali (a.s) ya kumuamini bwana Mtume (s.a.w.w) alikiwa bado ni kijana mdogo, inaonyesha uwezekano wa mtoto kuwa na uelewa na akili ya juu kuliko wengine. [25]
Rejeleo la Utume wa Suleimani, Yahya na Isa (a.s) Hali Wakiwa ni Watoto
Mashia wametaja baadhi ya aya za Qur'an zinazozungumzia utume wa manabii fulani waliopata utume hali wakiwa ni watoto. Wao wametumia Aya hizo kama ni vielelezo katika kuthibitisha mamlaka ya uongozi wa utotoni. [26] Kwa mujibu wa maelezo ya Fakhru al-Din al-Razi, ni kwamba; Hukmu iliyo tajwa katika Aya ya 12 ya Suratu Mariam, ambayo Mwenye Ezi Mungu alimpa Nabi Isa na Yahya (a.s) wakiwa bado ni wadogo, ni “hukmu” ya Utume. Vile vile, Ja'far Subhani, mwanatheolojia wa Shia, anasema kwamba; Aya ya 30 ya Suratu Mariam, inayozungumzia matamshi na maneno ya utotoni ya Nabi Isa (a.s), yaonesha kwamba, kama Mwenye Ezi Mungu atapenda, bila shaka anaweza kumpa mtu elimu, akili, na hekima maalumu zinazohitajika kwa ajili ya uongozi hali akiwa bado ni mtoto mdogo. [28]
Imesimuliwa na kuelezwa ya kwamba; Imamu Ridha (a.s) alimtambulisha mwanawe (Jawad) kama ni Imamu hali akiwa na umri wa miaka mitatu, alifanya hivyo huku akitolea mfano wa Nabii Isa (a.s), ili kuonesha kwamba, uongozi wa utotoni si jambo la muhali bali ni kitu kinacho wezekana. [29] Pia, Imamu Jawad (a.s) katika Hadithi nyingine alitaja kisa cha Nabi Suleimani (a.s) kuwa mrithi wa Nabii Daud (a.s) hali akiwa bado ni mtoto mdogo, alifanya hivyo ili kuonesha kuwa jambo hilo linawezekana. [30]
Rejeleo la Kitendo cha Mtume (s.a.w.w) cha Hadithi ya Yaumu al-Dar
Kwa mujibu wa maelezo ya Sheikh Mufid, mwanatheolojia wa Shia, ni kwamba; Kitendo cha bwana Mtume (s.a.w.w) katika Hadithi ya Yaumu al-Dar kinaonesha ya kwamba, iwapo Mungu akitaka, basi yuwaweza kumfanya mtoto kuwa hoja yake (mjumbe wake) kwa ajili ya waja wake. [31] Kwa mujibu wa makubaliano kati ya Shia na Sunni, ni kwamba; Katika Yaumu al-Dar, bwana Mtume (s.a.w.w) alimteua Imamu Ali (a.s), ambaye bado hakuwa amefikia ukomavu wa kimwili, kama ni mrithi na khalifa wake anaye stahiki kushika nafasi yake baada yake. [32]
Bibliografia (Vitabu Vilivyoandikwa Kuhusu Uongozi katika Umri wa Utotoni)
Kuna vitabu kadhaa vilivyoandikwa juu ya suala la uongozi katika umri wa utotoni, miongoni mwavyo ni:
- Kitabu "Imamaamat Dar Sinne Kuudakiy / Uimamu katika Umri wa Utotoni" kilichoandikwa na Ali-Asghar Ridhwani, kikiwa na kurasa 48, kitabu hichi kilichapishwa mwaka 1385 Hijria Shamsia (2006) na Shirika la Uchapishaji la Msikiti Mtakatifu wa Jamkaran. [33]
- Kitabu "Setaaregane Hidaayat: Imaamat Dar Kuudakiy / Nyota za Uongozi: Uongozi wa Utotoni", kilichoandikwa na Mohammad Baamiri, kikiwa na kurasa 176, hichi ni kitabu kilicho chapishwa mwaka 1391 Hijria Shamsia (2012) na Shirika la Uchapishaji la A-imma. [34]
- Kitabu "Imaamat Dar Kuudakiy / Uimamu katika zama za Utotoni: Mwelekeo wa Kichambuzi juu ya Uongozi katika Utotoni," kilichoandikwa na Hadi Turkmani, kikiwa na kurasa 166, ambacho kilichapishwa mwaka 1402 Hijria Shamsi (2023) na Shirika la Uchapishaji la Daa'iyah. [35]