Nenda kwa yaliyomo

Shia Imamiyyah

Kutoka wikishia

Shia Imamiyyah au Shia Ja'afariyyah au Shia Ithnaashariyyah (Kiarabu: الاثنا عشرية أو الشيعة الجعفرية أو الإمامية), ndio tawi moja kubwa zaidi miongoni mwa matawi ya wafuasi wa madhehebu ya Shia. Kulingana na imani na itikadi ya madhehebu ya Shia Imamiyyah ni kwamba; Imamu ndiye mwenye jukumu la kuiongoza jamii baada ya Mtume (s.a.w.w). Pia wao wanaitakidi ya kwamba; Imamu huteuliwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Wafuasi wa madhehebu ya Shia, kwa kuzingatia Hadithi kadhaa, kama vile Hadith ya Ghadir, wao wanamuhisabu Ali bin Abi Talib (a.s), kuwa ndiye mrithi wa Mtume wa (s.a.w.w), na ni Imamu wa kwanza baada ya Mtume (s.a.w.w). Mashia Ithnaashariyyah wanaamini Maimamu 12 na wanamini kuwa; Imamu Mahdi ameshazaliwa na yupo hai hadi sasa, ila haonekani kwa sababu yeye yupo mafichoni. Naye ndiye Imamu wa mwisho, ambaye atadhihiri kabla ya zama za mwishoni mwa dunia. Zaidiyyah na Ismailiyyah, ni matawi mingine mawili ya madhehebu ya Shia, ambao wao hawaamini maimamu wote kumi na wawili. Wao pia hawazingatii idadi ya Maimamu kuwa ni Maimamu 12 tu.

Shia Ithnaashariyyah wanaamini misingi mikuu mitano ya Imani; Sawa na Waislamu wengine. Wao wanaihisabu misingi ya Tauhidi, Utume na Ufufuo, kuwa ni miongoni mwa misingi mikuu ya dini yao. Isitoshe, wao wanaamini mingine miwili inayowatofautisha na madhehebu ya Ahlu-Sunnah, nayo ni; Uimamu na Uadilifu wa Mwenyezi Mungu. Imani juu ya Raja'ah ni moja ya imani maalum za Shia Ithnaashariyyah. Maana ya itikadi ya Raa'ah, ni kuamini ya kwamba; baadhi ya wafu wanarudi tena ulimwenguni katika zama za kudhuhiri kwa Imam wa Mahdi.

Mambo mengi nadani ya mfumo wa maisha ya Shia Ithnaashariyyah kama vile; ibada, zaka, pamoja miamala mbali mbali, hutekelezwa kupitia misingi maalumu ya sheria za dini ya Kiislamu. Qur'an, Hadith za Mtume (s.a.w.w) na Maimamu 12, pamoja na hoja za kiakili na makubaliano ya wanazuoni, ndiyo tegemeo lao asili katika nadharia zao za; kitheolojia, kifiqhi, kimaadili n.k. Sheikh Tusi, Allamh Hilli na Sheikh Murtadha Ansari, ni miongoni mwa mafaqihi mashuhuri wanaotegemewa na madhehebu hayo. Kwa upande wa pili; Sheikh Mufid, Khawaja Nasir Al-Din Tusi pia Allamah Hilli, ndio wanatheolojia maarufu wa madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah.

Mnamo mwaka wa 907 Hijiria, Shah Ismail Safawiy alianzisha serikali ya Safawiyyah na kuyafanya madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah, kuwa ndiyo madhehebu rasmi nchini Iran. Serikali hii ilikuwa na nafasi kubwa katika uenezaji wa hayo nchini Iran. Mfumo wa sasa wa kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ndio serikali pekee inayojitambulisha kufuata misingi ya madhehebu na fiqhi ya Maimamu 12 wa Kishia.

Eid Al-Ghadir, siku ya kuzaliwa Ali bin Abi Talib, siku ya kuzaliwa Fatimah binti ya Mtume, na nusu ya Sha'ban, ndizo sikukuu muhimu na adhimu zaidi za katika madhehebu ya Shia, hasa kwa wafuasi wa Shia Ithnaashariyyah. Miongoni kwa ibada muhimu kwa wafuasi wa madhehebu haya, ni kuomboleza na kuwalilia Maasumina (watu waliotoharishwa), hasa hasa kuomboleza maombolezo ya kifo cha Hussein bin Ali (a.s) na masahaba zake. Maombolezo hayo hufanyika ndani ya mwezi wa Muharram, hasa katika siku 10 za mwanzo za mwezi huo.

Hakuna takwimu madhubuti juu ya idadi ya Shia wanaofuata maimamu 12 duniani. Baadhi ya takwimu zilizopo hivi sasa, zimewaingiza Shia Ismailia na Shia Zaidiyyah na kuwaweka kundi moja bila ya kuwabagua kiitikadi. Kwa mujibu wa nukuu ya baadhi ya takwimu, idadi ya Mashia duniani ni kati ya watu milioni 154 na 200, nayo ni sawa na asilimia 10 hadi 13 ya Waislamu wote duniani. Ila kwa mujibu wa takwimu nyingine ni zaidi ya milioni 300, nayo ni asilimia 19 ya Waislamu wote duniani. Mashia wengi duniani, ambao ni kati ya asilimia 68 na 80, wanaishi katika nchi nne, nazo ni: Iran, Iraq, Pakistan na India.


Historia ya kujitokeza kwa madhehebu ya Shia

Kuna mitazamo tofauti kuhusiana na asili na historia ya mashehebu ya Shia. Miongozi mitazamo hiyo ni; ule mtazamo usemao kwamba, madhehebu hayo yalianza tokea enzi za Mtume (s.a.w.w), baada ya vuguvugu la Saqifah. Mtazamo mwingine unasema kuwa; madhehebu hayo yamezuka ndani ya zama za kifo cha Othmani, baada ya tukio la Haakimiyaah. Hiyo ndiyo mitazamo muhimu iliyotajwa kuhusiana na tarehe ya kuzaliwa au kuzuka kwa madhehebu ya Shia. [1] Kwa itikadi ya mwanafalsafa maarufu na mfasiri wa Qur'an wa karne ya 15, Sayyied Hussein Tabatabaai, ni kwamba; Madhehebu ya Shia yalianza mwanzoni mwa maisha ya bwana Mtume (s.a.w.w), ambapo mwanzoni walikuwa wakiliitwa "Shia wa Ali". [2]

Hadi karne chache baada ya kuja kwa Uislamu, neno Shia halikutumiwa tu kwa wale walioamini katika uongozi wa Kiungu wa Maimamu; Bali, wapenzi wote wa Ahlul-Bayt (a.s) au pia wale waliomhisabu Ali (a.s) kuwa ni mbora kuliko Othman pia nao waliitwa Shia Ali. [3] Wengi wa masahaba wa Ahlul-Bait (a.s) walikuwa miongoni mwa makundi mawili hayo ya mwisho. [4] Imesemekana kwamba tangu zama za Ali (a.s), kulikuwa na Shia kwa maana ya kiitikadi na kisiasa; Ikimaanisha ya kwamba, tokea hapo mwanzo kulikuwa na baadhi ya wafuasi wake walioamini kwamba; yeye ni mteule wa Mwenyezi Mungu. [5] Bila shaka, idadi ya kundi hii ilikuwa ni ndogo sana. [6]

Ingawaje idadi ya Mashia iliongezeka katika kipindi cha Imamu Hassan na Imamu Husein (a.s), ila bado hawakufikia kiasi cha kuwahisabu kuwa ni kundi na kuwapa jina la madhehebu fulani. [7] Wafuasi na wapenzi wa Ahlul-Bait walikuwa na wengi katika kipindi hicho. Lakini idadi ya walioamini kuwa; Imamu Ali (a.s) amechaguliwa na Mwenyezi Mungu kushika na nafasi ya Uimamu, ilikuwa ni ndogo, ambayo kwa makisio, labda walikuwa ni kiasi cha watu 50 tu ndiyo waliokuwa na imani kama hiyo. [8]

Kuanzia mwisho wa karne ya tatu ya mwandamo, Shia Ithnaashariyyah walitofautiana na madhehebu mengine ya Shia. Baada ya kuuawa shahidi Imamu Hassan Askari (a.s), kundi la Mashia walioamini kwamba; Kamwe ardhi ya Mwenyezi Mungu haitabaki bila Imamu, waliamini kuwepo kwa Imamu wa kumi na mbili ambaye yupo mafichoni. Kundi hilo lilijulikana kwa jina la Shia Imamiyyah au Shia wanaoamini Maimamu 12. [9] Kuanzia wakati huo, idadi ya wafuasi wa madhehebu ya Shia Imaamiyyah iliongezeka polepole. Kwa mujibu wa nukuu za Sheikh Mufid, katika zama zake yaani mnamo mwaka 373 Hijiria, madhehebu ya Shia wanaoamini maimamu Kumi na Mbili, walikuwa na wafuasi wengi zaidi ukilinganisha na madhehebu mengine ya Kishia. [10]

Misingi ya Imani

Sawa na Waislamu wengine, wafuasi wa madhehebu ya Shia Imaamiyyah wana misingi mitano ya Imani. Misingi yao mikuu ya Imani ni; Tauhidi, Utume na Ufufuo, ukiongezea na misingi mingine miwili inayowatofautisha na kuwatenganisha na wafuasi wa madhehebu ya Sunni, nayo ni; Uimamu na Uadilifu. [11] Kwa mujibu wa itikadi ya Kishia, baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w), ni lazima nafsi yake ishikwe na Imamu na kuendeleza nyadhifa zake. Kwa mtazamo wa Kishia, uteuzi wa Imamu hautofautiani na uteuzi wa Mitume, yaani Mwenyezi Mungu ndiye mteuzi halisi wa Mitume pamoja na Maimamu. Na baada ya uteuzi huo, wadhifa wa Mtume huwa ni kumtambulisha Imamu huyo katika umma wake. [12]

Wafuasi wa madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah, kwa mujibu wa Hadith walizozinukuu kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w), wanaamini kwamba; Mtume (s.a.w.w) alimtambulisha Imamu Ali (a.s) kama ni mrithi wake na ni Imamu wa kwanza baada yake, kwa amri ya Mwenyezi Mungu. [13] Misingi ya imani hiyo kuamini Maimamu 12 imeegemea kwenye Hadithi kadhaa, kama vile Hadith ya Louh n.k. [14] Majina ya Maimamu 12 wa Kishia ni kama ifuatavyo:

  1. Ali ibn Abi Talib
  2. Hassan bin Ali (Imamu Hassan Mujtaba)
  3. Hussein bin Ali
  4. Ali bin Hussein (Imamu Sajjad)
  5. Muhammad bin Ali (Imamu Baqir)
  6. Ja'afar bin Muhammad (Imamu Sadiq)
  7. Mussa bin Ja'afar (Imamu Kadhim)
  8. Ali bin Mussa (Imamu Reza)
  9. Muhammad bin Ali (Imamu Jawad)
  10. Ali bin Muhammad (Imamu Hadi)
  11. Hassan bin Ali (Imamu 'Askari)
  12. Hujjatu bin Al-Hasan (Imamu Mahdi) [15]


Kwa mujibu wa itikadi ya madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah ni kwamba; Imam wa kumi na mbili, Mahdi (a.s), bado yu hai na anaishi mafichoni (yupo katika Ghaibatu Al-Kubra), ila kuna siku atadhihiri na kusimamisha uadilifu duniani. [16]

Itikadi juu ya Uadilifu, kama itikadi juu ya Uimamu, ni moja ya misingi mikuu ya madhehebu ya Shia. Mashia wamepewa jina la Adliyyah kama walivyo walivyopewa wafuasi wa Muutazilah, wameitwa hivyo kwa sababu ya imani yao juu yake Uadilifu wa Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa itikadi ya Uadilifu, Mwenyezi Mungu humpa mtu neema na rehema au balaa fulani kulingani na sifa na mazingira yaliomo nafsini mwake. [17] Itikadi ya Raja'ah na Badaa ni miongoni mwa itikadi za msingi za Shia Ithnaashariyyah. Raja'ah ni itikadi ya kuamini ya kwamba; Kuna watu watakaorudi tena duniani baada kufa kwao, nao miongoni mwa waumini, Mashia pamoja na baadhi ya maaadui wa Ahlu-Bait, watakaofufuliwa katika zama atakapodhihiri Imamu Mahdi (a.s). Kwa mujibu wa itikadi hii, maadui wa Ahlul-Bait watafufuliwa ili wahukumiwe hapa duniani kabla ya Akhera, na waonje jazaa(malipo) yao kuanzia hapa duniani kabla ya kesho Kiama. [19] Imani ya Badaa nayo, ni; Imani juu ya kuwepo kwa hukumu zenye za kipindi cha mpito, hukumu ambazo hubadilika kulingana na mazingira na nyakati zilivyo. Kwa lugha nyingine ni kwamba; Mwenyezi humdhihirishia Mtume au Imamu (a.s) fulani kulingana na maslahi ya nyakati na mazingira yalivyo, kisha Mwenyezi Mungu huibadilisha hukumu hiyo kulingana mabadiliko ya zama na mazingira yalivyobadilika. [20] Vitabu kama vile; Awaa-ili Al-Maqaalaat, Tashiihu Al-I’itiqaad, Tajriidu Al-I’itiqaad na Kashfu Al-Muraad, ndiyo miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vya Shia Ithnaashariyyah katika ‘ilmu al-kalaam (fani ya akida). [21] Wanazuoni madhubuti na makini zaidi wa fani ya akida katika madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah ni; Sheikh Mufid, (aliyezaliwa mwaka 336 au 338 na kufariki mwaka 413 Hijiria), Sheikh Tusi (aliyezaliwa mwala 385 na kufariki mwaka 460 Hijiria), Khawajah Nasir Al-Diin Al-tusi (aliyezaliwa mwaka 597 na kufariki mwaka 672 Hijiria) na Allamah Hilli (aliyezaliwa mwaka 648 na kufariki mwaka 726 Hijiria). [22]

Tofauti baina ya Mashia Ithnaashariyya na Mashia wengine

Pia angalia: Zaidiyyah na Ismailiyyah

Miongoni mwa matawi ya madhehemu ya Shia, ni; Shia Ismailiyyah na Shia Zaidiyyah, amabo wao hawawaamini Maimamu wote 12 wanaoaminiwa na Mashia Ithnaashariyyah. Pia wao hawasimami juu ya idadi ya Maimamu 12 tu. Shia Zaidiyyah wanaamini ya kwamba; Mtume (s.a.w.w) alitoa kauli ya wazi kuhusiana na Maimamu watatu tu, nao ni Imamu Ali (a.s), Imamu Hassan (a.s) na Imamu Hussein (a.s). [23] Na baada yao, katika zama zozote zile, iwapo atatokea mchamungu, asiyependa makuu, shujaa na mkarimu kutoka katika kizazi cha bwana Mtume (s.a.w.w), ambaye atasimama kwa jili ya kusimamisha haki, basi huyo atahisabika kuwa ni Imamu miongoni mwa Maimamu. [24] Miongoni mwa Maimamu wa madhehebu ya Shia Zaidiyyah, ni; Zaid bin ali, Muhammad bin Abdullah bin Hassan (Nafsu Zakiyyah), Ibrahim bin Abullah na Shahid Fathu. [25] Wafuasi wa madhehebu ya Shia Ismailiyyah hawakubalianai na Imamu wa pili wa Shia Ithanaashariyyah, yaani Imamu Hassan Mujtaba (a.s). [26] Baada ya kumuweka kando Imamu Hassan (a.s), wameendelea kukubaliana na Maimamu wailiofuata baada yake hadi kufikia kwa Imamu Swadiq (a.s). [27] Baada ya kifo cha Imamu Swadiq (a.s), walishikamana na Ismail, ambaye mwana wa Imamu Swadiq (a.s), kisha wakamuamini Muhammad mwana wa Ismail kuwa ndiye Imamu wa haki. [28]

Sheria za Fiqhi

Madhehebu ya Shia Imamiyyah, kama yalivyo madhehebu mbali mbali ya Kiislamu, mfumo wake wa maisha ya kijamii na kidini, kama vile ibada, miamala, malipo ya kafara, khumsi na zakat, ndoa na mgawanyo wa mirathi, yote hayo ni lazima yatekelezwe kwa mujibu wa kanuni na sheria za kidini. [30] Qur'an na Hadithi za Maimamu kumi na mbili, ndiyo vyanzo viwili vikuu vya hukumu za kidini ndani ya madhehebu ya Shia Imamiyyah. [31] Hukumu na sheria za kidini hutongolewa na kuvuliwa kupia nyenzo na msaada wa elimu kadhaa, kama vile elimu za; dirayah, rijal, fiqhi na usuli al-fiqhi. [32]

Vitabu maarufu vya kifiqhi ya Shia Ithnaashariyyah ni; Sharai'u Al-Islam, Al-Lum-'ah Al-Damashqiyyah, Sharhu Lum-'ah, Jawaharu Al-Kalaam, Makasib na Al-'Urwatu Al-Wuthqa. [33] Wanazuoni maarufu zaidi wa Madhebu hayo ni; Sheikh Tusi, Muhaqqiq Al-hilli, Allaamah Al-Hilli, Shahidu Al-Awwal, Shahidu Al-Thani, Kaashifu Al-ghitaa, Mirza Qummiy na Sheikh Murtadha Ansariy . [34]

Mafaqihi warejewao na jamii (Marji'u Al-Taqliid)

Makala asili: Mafaqihi warejewao na jamii (Marji'u Al-Taqliid)

Katika zama zetu za leo, hukumu za kisheria zimeorodheshwa katika vitabu viitwavyo Taudhihu Al-Masail, ambavyo vimeandikwa na Mafaqihi waliofikia daraja za kuwa ni rejeo la jamii katika masuala mbali mbali ya kidini. [35] Wao ni wanazuoni waliofikia daraja ya ijitihad, ambao huwa ndio tegemeo linalofuatwa na watu wasiofikia daraja kama zao kielimu; Yaani, watu wanatekeleza matendo yao ya kidini kwa kuzingatia rai zao za kifiqhi (fat'wa). Pia wanajamii huwapelekea wao zaka zao, pamoja matozo mbalimbali yanayofungamana na sheria za Kiislamu. [36]

Mila na desturi za kidini

Kuachana na Eid al-Fitr, Eid al-Adha, Eid al-Mubaath, na Maulidi ya Mtume (s.a.w.w), ambazo huhisabiwa kuwa ni sikukuu za kidini za Waislamu wote duniani, Mashia Ithnaashariyyah husherehekea Eid Al-Ghadir, Maulidi ya Imam Ali (a.s) , Maulidi ya Fatima (a.s), na nusu ya mwezi wa Sha'ban. Hizo kwa upande wa madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah, ndiyo sikukuu muhimu zaidi za kuliko nyingine zeto. Ukiachana na sikukuu hizo, pia Mashia Ithnaashariyyah husherehekea siku za kuzaliwa kwa Maimamu wao wengine. [37]

Katika madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah kila siku kuu miongoni mwa siku kuu hizo, huwa kuna matendo (amali) maalum za kidini yanapendekezwa kwa ajili yake; Kwa mfano, katika siku ya Eid Al-Adha, vitendo kama vile kuoga josho, kusali swala ya Eid Al-Adha, kuchinja, kusoma ziara ya Imamu Husein (a.s) na kusoma dua ya Nudba, vitendo vinavyopendekezwa kutenda ndani ya siku hiyo.[38]

Maombolezo muhimu na makubwa zaidi yanayofanywa na wafuasi wa madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah katika siku za mwaka mzima kwa ajili ya Maimamu wao, ni yale maombolezo yanayoomboleza kifo cha Imamu Hussein na Masahaba zake, yanayofanyika ndani ya kumi la mwanzo la mwezi wa Muharram na kumi la mwisho la mwezi wa Safar.Maombolezo ya kumi la mwisho la mwezi wa Safar hujulikana kwa jina la Ayyaamu Faatimiyyha na arubaini ya Imamu Hussein (a.s).


Kuzuru kaburi la bwana Mtume pamoja makaburi ya Ahlul-Bait (a.s), ni miongoni mwa mila na ibada muhimu za madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah. [40] Pia wao hutilia mkazo mno suala la kutembelea na kuzuru makaburi ya Masharifu pamoja na makaburi ya wanazuoni wa kidini. [42] Baadhi ya ziyara na dua maarufu za madhehebu ya Shia ni: Dua ya Kumayl [43], Dua ya Arafa [44], Dua ya Nudbah [45], Dua ya Shabaniyah (Munaajati Shaabaniyyah, [46] Dua ya Tawassal, [47] Ziyaratu Ashura, [48] Ziyaratu Al-Jaami'ah [49] na Ziaratu Aminullah. [50]

Vyanzo vya fikra za madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah

Kuna vyanzo vinne vikuu ambavyo ndiyo tegemeo na marejeo asili ya madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah vilivyojenga fikra zao za; kitheolojia, kifiqhi, kimaadili, n.k. Vyanzo hivyo ni: Qur'an, Hadith za Mtume na maimamu, pamoja na hoja za kiakili na makubaliano ya wanazuoni. [51]

Qur'an

Makala asili: Qur'an

Mashia Ithnaashariyyah, wanaizingatia Qur'an kuwa ni chanzo cha kwanza na muhimu zaidi cha elimu na mafundisho ya kidini. Umuhimu wa Qur’an miongoni mwao ni kwamba; Ikiwa Hadithi fulani itapingana na misingi mikuu ya Qu'an, basi kitaalamu Hadithi hiyo haitakubalika. [52] Kwa mujibu wa maandiko ya Mohammad Hadi Maarifatiy; Mashia wote wanaihisabu Qur’an iliyo mkononi mwa Waislamu hivi leo, kuwa sahihi na kamili isiokuwa na dosari ya mapungufu au ziada yoyote ile. [53]

Hadithi za Mtume na Maimamu

Makala Asili: Hadithi

Mashia Imamiyyah, kama yalivyo madhehebu mengine ya Kiislamu, huzichukulia Sunnah za Mtume (s.a.w.w), yaani; Maneno, tabia, na taqriri zake, kuwa ndio rejeo na tegemeo la Waislamu wote katika hoja za nyenendo zao za kidini za kila siku. [54] Mashia Ithnaashariyyah wanawahisabu Ahlul-Bait kuwa ni moja kati marejeo imara na tegemezi ya dini na madhehebu yao. Wamefanya hivyo kwa kutegemea Hadithi kadhaa, ikiwemo Hadithi maarufu ijilikanayo kwa jina la Hadithu Al-Thaqalaini, pamoja na Hadithu Al-Safina, ziliyoamrisha kuwarejelea Ahlul-Bait (a.s), kuwafuata na kushikamana nao katika nyenendo za maisha yao ya kijamii, kidini na kisiasa, kiuchumi n.k. [55] Mashia Ithnaashariyyah wanaziangalia kwa jicho maalumu Hadithi za Mtume na Maimamu 12 (a.s). [56]

Vitabu muhimu zaidi vya Hadithi katika madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah ni; Al-Kafi, Tahdheeb Al-Ahkaam, Al-Istbasar na Man Laa Yahdhuruhu Al-Faqiih, ambavyo umaarufu wake ni; Al-Kutubu Al-Arba'ah au Usul Arba'ah. [57] Vitabu vyengine maarufu vya hazina za Hadithi za Shia Ithnaashariyyah ni: Al-Wafi, Bihar Al-Anwar, Wasaailu Al-Shi'a [58], Al-Mostadrak, Mizanu Al-Hikma, Jaami'u Ahaadiithi Al-Shi'ah na Al-Hayatu wa Aatharu Al-Saadiqaini. [59]

Mashia hawaichukulii kila Hadith kuwa ni sahihi. Kwa maoni yao; Ili hadithi ikubalike, ni lazima iwe na vigezo maalumu, kama vile: kutokinzana na Qur'an, kukubalika kwa wapokezi wake, pamoja na Tawaatur (yaani kupokelewa hadithi na idadi kubwa ya watu/maswahaba). Ili sharti na vigezo hivyo vikamilike, wao hutumia nyenzo mbali mbali, kama vile; Elmu Al-Diraayah na Elmu Al-Rijaal. [60]

Akili

Makala asili: Akili

Akili ina nafasi maalumu katika madhehebu ya Shia Imaamiyyah. Mashia wa madhehebu ya Imaamiyyah hutegemea akili katika kuthibitisha misingi ya itikadi zao. [61] Pia wanaichukulia akili kuwa ni mojawapo ya vyanzo vya hukumu za sheria. Wao pia hutegemea akili hata katika kuthibitisha baadhi ya misingi ya sheria za kifiqhi, usuli al-fiqhi, na fiqhi. [62]

Ij-ma'a (Makubaliano ya wanazuoni)

Makala kuu: Ijma'a (Makubaliano ya Wanazuoni)

Makubaliano ya wanazuoni, ni miongoni mwa vyanzo vinne vya kutohoa hukumu za kisheria (hukumu za fiqhi). hili nalo ni miongoni mambo yaliojadiliwa vya kutosha katika fani ya usulu al-fiqhi. [63] mafakihi wa madhehebu ya Imaamiyyah, ni tofauti na mafakihi wa Kisunni, wao hawayazingatii makubaliano ya mafakihi kuwa ni ushahidi unaojitegemea kando na Qur'an Tukufu, Sunnah, na hoja za kiakili; Badala yake, wanayahisabu makubaliano hayo sababu tu inayoweza kuashiria kuwepo kwa dalili na hoja maalumu kutoka kwa Maasuumina (watu waliotoharishwa). [64]

Serikali

Kuna serikali nyingi za Kishia zimeundwa ndani ulimwengu wa Kiislamu, zikiwemo; Serikali za Alawiina za Tabaristan, Aal Buweihi (Aali (Buyeh), Fatimiiyyina, Ismailia na serikali ya Safawiyyah. Serikali ya Alawiina ilianzishwa na wafuasi wa madhehebu ya Zaidiyyah. [65] serikali za Fatimiyyah na Ismailiyyah aa Alamut lilisimamishwa kwa misingi ya Kiismailiyyah, [66] Ila kuna maoni tofauti kuhusiana na serikali za Aali Buweihi (Aali Buyeh). Wengine wanaamini kuwa; Aali Buweihi walikuwa ni wafuasi wa madhehebu ya Zaidiyyah, wengine wanadhani kuwa wao wlikuw ni Mashia Imaamiyyah, huku wengine wanasema kuwa hapo walikuwa Zaidiyyah kisha wakabadili madhehebu, na kuwa ni Mashia Imaamiyyah. [67]

Sultan Mohammad Khodabande anayejulikana kwa jina la Ulijaito (aliyetawala kuanzia mwaka 716 hadi 703 Hijiria), anahisabiwa kuwa yeye ndiye mtawala wa kwanza aliyetangaza kuwa madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah ndiyo madhehebu rasmi katika utawala wake. Yeye alijitahidi kueneza madhehebu hayo kadri ya uwezo wake. [68] Kutokana na matatizo ya mfumo wa serikali ya wakati huo, ambapo wengi waliokuwemo serikalini walikuwa ni wafuasi wa madhehebu ya Kisunni, ilipelekea jitihada zake kugonga ukuta. [69]

Serikali ya Sarbedaaraan ya huko Sabzewaar, pia ni moja ya serikali iliyotajikana kuwa ni serikali ya Kishia. [70] Ila madhehebu halisi ya viongozi na watawala wa serikali ya Sarbedaaraan hayajulikani. Lilofahamika kutoka kwao ni kwamba; Viongozi hao walikuwa ni Masufi ambao pia walikuwa na mielekeo ya Kishia. [71] Hata hivyo, Khawaja Ali Mu-ayyed, ambaye ni mtawala wa mwisho wa Sarbedaran, [72] aliyatangaza madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah kuwa ndiyo madhehebu rasmi ya serikali yake. [73]

Utawala wa Safawi

Makala Asili: Safawi

Shah Ismail alianzisha serikali ya Safawi mnamo mwaka wa 907 Hijiria na kutangaza madhehebu ya Shia Ithnaasharia kuwa ndio madhehebu rasmi ya Iran. [75], Yeye pamoja na wafalme wenzake walieneza madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah miongoni mwa Wairani na kuigeuza Iran kuwa ni nchi ya Shia kabisa kabisa. [76]

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Makala kuu: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianzishwa nchini Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran tarehe ya 22 Bahman mwaka 1357 Shamsia chini ya uongozi wa Imam Khomeini. [77] Mfumo wa serika hii ya Iran umesimama juu ya misingi ya madhehebu ya kifiqh ya Shia Ithnaashariyyah. [78] Msingi wa Wilayatu Al-Faqiih (Uongozi wa serikali kipitia nadharia na mamlaka ya mwanafiqhi), ndiyo msingi na nguzo muhimu zaidi ya Serikali ya Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran. Mwanafiqhi huwa ndiye kiongozi mkuu ndani serikali hiyo, huwa ndiye mwenye mamlaka kamili ya kiuongozi serikalini humo. [79] Kulingana na Katiba ya Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni kwamba; Ikiwa kutatokea kipengele cha sheria kiendacho kinyume na misingi ya dini ya kiislamu, basi kipengele hicho hakitakuwa na nafasi ndani ya katiba ya nchi hiyo. [80]

Jiografia

Hakuna takwimu kamili za idadi ya Mashia wanaoamini Uimamu wa Maimamu 12 duniani, na takwimu zilizopo ni takwimu zilizowajumuisha ndani yake Shia Zaidiyyah na Shia Ismailiyyah. Kulingana na ripoti ya cha uchunguzi ya Pew Religion and Public Life Association, ni kwamba; Idadi ya Mashia duniani inakadiriwa kuwa ni kati ya watu milioni 154 na 200, ambayo ni sawa na asilimia 10 hadi 13 ya Waislamu wote duniani.[81] lakini mfasiri wa ripoti hii, hakukubaliana na takwimu hiyo, naye ametoa makadiro yasemayo kuwa; Idadi halisi ya Mashia duniani ni zaidi ya milioni mia tatu, ambayo ni 19% ya idadi ya Waislamu wote duniani.[82] Mashia wengi, kati ya asilimia 68 na 80, wanaishi katika nchi nne, nanzo ni: Iran, Iraq, Pakistan na India. Mashia milioni 66 hadi 70 wanaishi Iran, ambayo ni sawa na asilimia 37 hadi 40 ya Mashia wote duniani. Kila nchi miongoni mwa Pakistan, India na Iraq ina zaidi ya Mashia milioni 16. [83]

Katika nchi nne za Iran, Azabajani, Bahrain, na Iraq, ndio wenye idadi kubwa ya wakazi wa nchi hizi. [84] Pia kuna Mashia wengine wanaoishi katika maeneo kama vile Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini, eneo la Uturuki, Yemen, Syria, Saudi Arabia, America, Canada na Asia-Pacific. Nchi za Asia-Pacific ni; Afghanistan, Australia, Bangladesh, Bhutan, Burma, Brunei, Cambodia. [85]