Nenda kwa yaliyomo

Muhammad bin Ali al-Shalmaghani

Kutoka wikishia

Muhammad bin Ali al-Shalmaghani (Kiarabu: محمد بن علی الشلمغاني) (aliuawa: 323 H) mashuhuri kama al-Azaqiri, ni mmoja wa watu waliokuwa wakidai Unaibu wa Imamu Mahdi (a.t.f.s) na ni kutokana na sababu hiyo kukatolewa tawqi' (barua) kutoka kwa Imamu Mahdi (a.t.f.s) ya kumpinga. Shalmaghani alikuwa mmoja wa masahaba wa Imamu Hassan Askary (a.s) na mafakihi wa Kishia katika zama za Ghaiba Ndogo (Ghaibat al-Sughra). Kwa mujibu wa taarifa za waandishi wa wasifu wa wataalamu wa elimu ya hadithi ni kwamba, baadaye Shalmaghani aliondokea kuwa na mielekeo ya Ghulu (mtu aliyechupa mipaka katika itikadi kuhusiana na Mitume na Maimamu) na hivyo akawa na upotovu wa kiitikadi. Akiwa katika hali hiyo alipata wafuasi ambao waliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Shalmaghaniyah. Shalmaghani alifukuzwa na Hussein bin Ruh na alikataliwa kupitia barua (tawqi’) iliyotolewa na Imam Mahdi (a.t.f.s) ambapo aliwataka Mashia wamchukie.

Kitabu cha al-Takalif ni miongoni mwa athari za Shalmaghani ambapo ukitoa mas’ala mawili matatu inaelezwa kuwa, kilithibitishwa na kuungwa mkono na Hussein bin Ruh. Kwa mujibu wa Sheikh Tusi na baadhi ya wengine, athari ya Shalmaghani kabla ya kuchupa kwake kiitikadi ilikuwa na itibari na ilikuwa ikifanyiwa kazi na Mashia. Alitiwa mbaroni kwa amri ya Radhiu Billlah mmoja wa makhalifa wa Bani Abbas na akauawa mwaka 323 Hijiria.

Utambulisho

Shalmaghani ni miongoni mwa masahaba wa Imam Hassan Askary (a.s) na alikuwa mmoja wa mafakihi na wapokezi wa hadithi wa Shia Imamiyyah katika zama za Ghaiba Ndogo. [1] Sheikh Tusi (aliaga dunia: 460 H) katika kitabu cha Kitab al-Ghaibah amenukuu nadharia mbili kuhusiana na Shalmaghani kwa Hussein ibnu Ruh al-Nawbakhti, Naibu wa Tatu miongoni mwa Manaibu Wanne wa Imamu Mahdi (atfs). [2] Kwa mujibu wa nukuu moja, yeye alikuwa na nafasi maalumu kwa Hussein bin Ruh na alikuwa kiunganishi baina yake na watu na alikuwa akifikisha kwake mahitaji ya Mashia. [3] Kwa mujibu wa nukuu nyingine, Hussein bin Ruh hakumpa daraja hiyo bali yeye alikuwa mmoja tu wa mafakihi wa Kishia aliyekuwa akiaminika. [4]

Shalmaghani alikuwa mashuhuri kwa jina la al-Azaqiri alizaliwa katika kijiji cha Shalmaghani jirani na moja ya miji ya Iraq. [5] Kuniya yake ni Abu Ja’afar. [6] Alitiwa mbaroni kwa amri ya Radhiu Billah Abasi, mtawala wa 20 wa ukoo wa Bani Abbas na akauawa kwa amri yake mwaka 323 Hijiria. [7]

Muelekeo wa Kuchupa Mipaka na Madai ya Naibu wa Imamu Mahdi (a.t.f.s)

Inaelezwa kuwa, Shalmaghani alikuwa na matarajio ya kukabidhiwa unaibu wa Imamu Mahdi (a.s) [9] na kutokana na hilo ndio maana baada ya jukumu hilo kukabidhiwa kwa Hussein bin Ruh alijitokeza na kumpinga na kumnasibishia mambo ya uongo. [10].

Kwa mujibu wa ripoti ya Ibn Athir (aliaga dunia: 630 H) mwanandishi wa historia wa Ahlul-Sunna ni kwamba, kulitokea upotovu katika itikadi ya Shalmaghani na akawa amekuwa na mielekeo ya kighulati. [11] Aliamini kwamba roho ya Mungu iko ndani ya Adam (a.s) na baada yake ilikuwa kwa Mitume na mawasii wengine mpaka ikamfikia Imam Hassan Askari (a.s) na baada yake ikayeyuka katika mwili wake [12] Shalmaghani pia alidai kuwa Yeye ni Naibu wa Imamu Mahdi (a.s) na alijiona kuwa anawajibika kwa nafasi hii [13] na akapata wafuasi waliojulikana kwa jina la Shalmghaniyyah [14].

Barua ya Imamu Mahdi ya Kumkataa Shalmaghani

Baada ya kuwa, Hussein bin Ruh kufahamu kuhusiana na itikadi zake, alimchukia na kumlaani na akatoa agizo kwa Mashia kujitenga na kujiweka mbali naye. [15] Kadhalika, kulitolewa tawqi’ (barua) kutoka kwa Imam Mahdi (a.s) ya kumpinga Shalmaghani na kumfikia Hussein bin Ruh ambapo ndani yake alimchukia Shalmaghani na kumtambulisha kama mtu muongo, aliyekengeuka katika Uislamu na murtadi na akawapa amri Mashia kujiweka mbali naye. [16]

Nafasi ya Shalmaghani katika kupokea hadithi

Uaminifu na itibari

Kwa mujibu wa Abbas Iqbal Ashtiani (aliyefariki: 1334 Hijiria Shamsia) katika kitabu “Khandan Nobakhti”, (familia ya Nowbakhti) kazi za Shalmaghani zilikuwa na itibari miongoni mwa Mashia kutokana na msimamo wake wa kielimu na ukaribu wake kwa Hussein bin Ruh kabla ya kuasi kwake na kuwa ghulati. Baada ya kupotoka kwake, Hussein bin Ruh aliulizwa kuhusu vitabu vyake, na Hussein bin Ruh akajibu kwamba chukueni aliyoyanukuu kutoka kwa Maimamu (a.s.) na acheni yale aliyoyaleta kwa mujibu wa rai yake mwenyewe;[17] kwa hiyo baadhi wamesema kwamba, kabla ya yeye kukengeuka na kuwa ghulati alikuwa thiqah (muaminifu). [18] Sheikh Tusi katika kitabu chake cha al-Fehrest ni kwamba, Mashia walikuwa wakifanyia kazi vitabu vya Shalmaghani kabla ya kukengeuka na kupotoka kwake. [19]

Athari za Shalmaghani

Najjashi mmoja wa waandishi wa wasifu wa wapokezi wa hadithi wa Kishia katika karne ya 5 Hijiria ametaja athari 17 za Shalmaghani katika kitabu chake cha Feherest Asmaa Musannafi al-Shia. [20] Kitabu cha “al-Taklif” ni moja ya athari hizo [21] ambacho kina hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Maimamu wa Shia na zilikusanywa kabla ya kupotoka kiitikadi na kuwa ghulati na kilikuwa kikifanyiwa kazi na Mashia. [22] Kwa mujibu wa Sheikh Tusi (aliaga dunia: 460 Hijiria) katika kitabu chake cha al-Ghaibah ni kuwa, kundi miongoni mwa Mashia lilichukua kitabu hicho na kukipeleka kwa Hussein bin Ruh na akakisoma chote na kukiidhinisha isipokuwa mambo mawili au matatu, lakini mambo mengine ya kitabu hicho aliyanukuu kutoka kwa Maimamu (a.s) na maudhui zake hazikuwa zikikinzana na sheria za Mwenyezi Mungu. [23] Muhammad Taqi Shushtari (aliaga dunia: 1415 Hijiria) katika Qamus al-Rijal amejaalia uwezekano huu kwamba, kitabu cha Fiq’h al-Ridha ambacho nakala yake ilipatikana katika zama za Allama Majlisi, ndio kile kile kitabu cha «al-Taklif» cha Shalmaghani. [24]