Aya ya Ulul-Amr

Kutoka wikishia
Makala hii inazungumzia Aya ya Ulul-Amr. Kama unataka kufahamu mafuhumu na maana ya Ulul-Amr angalia makala ya Ulul-Amr.
Aya ya 59 ya Surat al-Nisaa

Aya ya Ulul Amr au Aya ya utii (Kiarabu: آية أولي الأمر أو آية الطاعة) Ni Aya ya Surat al-Nisaa 59 ambayo imewapa amri waumini ya kumtii Mwenyezi Mungu, Mtume (s.a.w.w) na wenye mamlaka juu yao. Kwa mujibu wa Mashia na baadhi ya Ahlu-Sunna, makusudio ya Ulul-Amr (wenye mamlaka) ni Maimamu wa Kishia na wanaamini kwamba, Aya hii ni hoja ya kuwa kwao Maasumu na wajibu wa kuwatii; hata hivyo Waislamu wa madhehebu ya Kisuni wana mitazamo na rai tofauti kuhusiana na hili. Khulafaa Rashidun (kwa mujibu wa Masuni ni viongozi wa awali waliotawala baada ya Mtume), kila mtawala muadilifu, kiongozi wa dini na majimui ya umma wa Kiislamu ni miongoni mwa mifano ya wazi ambayo Maulamaa wa Kisuni wameibainisha kwa ajili ya Ulul-Amr.

Andiko la Aya na tarjuma yake

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَطِيعُواْ اللَّهَ وَأَطِيعُواْ الرَّسُولَ وَأُولِي الأَمْرِ مِنكُمْ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ ذَلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلاً


Enyi mlio amini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.



(Quran: 4: 59)


Ithbati ya Umaasumu na Wajibu wa Kuwatii Ulul-Amr

Kwa mujibu wa wafasiri wa Qur'an wa Kishia, Aya ya Ulul-Amr ni ithbati ya kwamba, Ulul-Amr (wenye mamlaka) wana hali ya umaasumu (hawatendi dhambi). [1] Allama Tababai anasema, kuunganishwa Ulul-Amr na Mtuume (s.a.w.w) katika Aya hii bila ya kukaririwa neno "atwiu" yenye maana ya mtiini ni ishara ya wazi kwamba, kama ambavyo kumtii Mtume ni wajibu mutlaki, vivyo hivyo ni wajibu kuwatii Ulul-Amr bila ya sharti [2] Mwenyezi Mungu akitoa amri ya kutiiwa mtu bila ya kuweka sharti, basi mtu huyo atakuwa ni Maasumu na mtu asiyetenda dhambi; kwani kama siyo Maasumu na akatoa amri ya kufanya dhambi, kutajitokeza hali ya kukutana pamoja mambo mawili yenye kukinzana; yaani ni lazima kumtii (kwa mujibu wa amri ya Mwenyezi Mungu) na wakati huo huo kutomtii (kwani mtu hapaswii kutenda dhambi). [3] Fakhrurazi, mmoja wa wafasiri watajika wa Ahul-Sunna yeye anaaminii kwamba, Aya hii ni ashirio na ithibati kwamba, Ulul-Amr (wenye mamlaka waliokusudiwa katikaa Aya hii) hawatendi dhambi yaani ni Maasumina. Hata hivyo anakataa kuwa, waliokusudiwa hapo ni Maimamu wa Kishia. [4]

Ibn Taymiyyah [5] kiongozi wa pote la Usalafi na Nassir al-Qifari [6] mmoja wa Mawahabi wanasema kuwa, kinachofahamika katika Aya isemayo: {فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّهِ وَالرَّسُولِ ; “Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume”}, ni ishara ya wazi kwamba, ghairi ya Mtume hatuna Maasumuu mwingine; kwani katika Aya hii, Waumini wametakiwa pindi wanapozozana katika jambo warejee kwa Mwenyezi Mungu na Mtume. Kwa mtazamo wao ni kwamba, kama kungekuweko na Maasumu mwingine asiyekuwa Mtume, Mwenyezi Mungu angeliamrisha kumrejea yeye pia. Katika kuwajibu wenye mtazamo huu imeelezwa kwamba, hitilafu na tofauti zipo katika hukumu na sheria jumla za Uislamu ambazo watungaji wake ni Mwenyezi Mungu na Mtume, na Maimamu (as) daima ni watekelezaji wa sheria za Mwenyezi Mungu na Mtume (s.a.w.w). [7] Kwa mujibu wa Aya ya 83 ya Surat al-Nisaa, kuwarejea Maimamu ni sawa na kumrejea Mwenyezi Mungu na Mtume Wake; kwani Maimamu kama alivyo Mtume ni walinzi na wenye kuhifadhi sheria. [8]

Ulul-Amr ni Akina Nani?

Kuna hitilafu za kimitazamo baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni huhusiana mfano na kielelezo cha Ulul-Amr (wenye mamlaka). Waislamu wa madhehebu ya Kishia wanaamini kwamba, makusudio ya Ulul-Amr ni Maimamu 12; hata hivyo, Masuni wao wanasema kuwa, Khulafaa Rashidun, watawala waadilifu au Maulamaa ndio vigezo na wakusudiwa wa Ulul-Amr (wenye mamlaka) katika Aya hiyo.

Maimamu wa Kishia

Kuna hadithi mbalimbali katika vitabu na vyanzo wa Kishia [9] na Ahlu-Sunna [10] ambazo zinaeleza kuwa, makusudio ya Ulul-Amr ni Maimamu (a.s). [11] Kwa mujibu wa hadithi hizi, Maulamaa wa Kishia wanawatambua Maimamu 12 kuwa wao ndio Ulul-Amr (wenye mamlaka). [12] Baadhi ya hadithi hizi ni kama ifuatavyo:

  1. Jabir bin Abdillah al-Ansari katika hadithi ambayo ni mashuhuri kwa jina la hadithi ya Jabir, alimuuliza Bwana Mtume (s.a.w.w) kuhusiana na neno "Ulul Amr". Mtume katika kumjibu Jabir alisema: Wao ni warithi wangu na Maimamu wa Waislamu baada yangu ambapo wa kwanza wao ni Ali ibn Abi Talib na baada yake akataja majina ya Maimamu 12 kwa utaratibu. [13]
  2. Katika kufasiri Aya ya Ulul-Amr, imenukuliwa kutoka kwa Imam Baqir (a.s) kwamba, Ulul-Amr ni Maimamu kutoka katika kizazi cha watoto wa Ali na Fatma (a.s) mpaka Siku ya Kiyama itakapowadia. Katika hadithi nyingine, iimenukuliwa kutoka kwa Imam Baqir (a.s) kwamba, Mwenyezi Mungu ametukusudia sisi tu kuhusu Ulul-Amr na akawaamrisha wauumini kutufuata sisi mpaka Siku ya Kiyama. [14]
  3. Imam Swadiq (a.s) amesema: Wao (Ulul-Amr) ni Ali bin Abi Talib, Hassan, Hussein, Muhammad bin Ali na Ja'afar yaani mimi. Kisha mshukuruni Mwenyezi Mungu kwa kuwatambua Maimamu na viongozi wenu katika kipindi ambacho watu wanawakana. [15]

Khulafaa Rashidun na Kila Mtawala Muadilifu

Maulamaa wa Kisuni wana mtazamo na rai tofauti kuhusiana na mifano na vielelezo vya Ulul-Amr. Baadhi yao wanasema kuwa, makusudio ya Ulul-Amr ni Khulafaa Rashidun. Kundi jingine la Maulamaa wa Kisuni linaamini kwamba, makusudio ya Ulul-Amr ni Maulamaa na wasomi wa dini. Aidha kuna wengine wanaoamini kuwa, makamanda wa vita ambavyo vilipiganwa bila ya Mtume kuwa na mahudhurio ya moja kwa moja ni kielelezo cha wazi cha Ulul-Amr (wenye mamlaka). [16] Kwa mujibu wa mtazamo wa Zamakhshari, mmoja wa wafasiri watajika na mashuhuri wa Kisuni anasema, makusudio ya Ulul-Amr katika Aya hiyo ni kila mtawala muadilifu ambaye anatawala na kuongoza kwa mujibu wa mafundisho ya dini; na vilevile Khulafaa Rashidun na watawala wanaofanya mambo kama wao. [17] Fakhrurazi anasema, mfano na kielelezo cha Ulul-Amr ni kundi na watu wenye taathira na wenye ujuzi wa masuala wa sheria. [18]

Mtazamo wa Allama Tabatabai

Allama Tabatabai amesema katika Tafsir al-Mizan kwamba: Makusudio ya Ulul-Amr ni watu ambao kila mmoja wao ana Umaasumu (hali ya kutotenda dhambi) na kuna wajibu wa kutekeleza maagizo yake na hili halipingani na mafuhumu na maana ya Ulul-Amr kuwa yenye wigo mpana; lakini kielelezo chake kinaeleweka na kina mpaka; kama ambavyo katika Aya hii hii neno Rasul (Mtume) mafuhumu na maana yake ni pana; katika hali ambayo bila shaka makusudio hapo ni Mtume (s.a.w.w). [19]

Vyanzo

  • Ayyāshī, Muḥammad b. Masʿūd al-. Tafsīr al-ʿAyyāshī. KImehaririwa na: Hāshim Rasūlī Maḥallatī. Tehran: Maktabat al-ʿIlmīyya al-Islāmīyya, 1363 Sh.
  • Baḥrānī, Sayyied Hāshim al-. Al-Burhān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Ismāʾīlīyān, n.d.
  • Fakhr al-Rāzī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Mafātīḥ al-Ghayb (al-Tafsīr al-Kabīr). Chapa ya tatu. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1420 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Āyāt-i wilāyat dar Qurʾān. Qom: Intishārāt-i Nasl-i Jawān, 1386 Sh.
  • Muẓaffar, Muḥammad Ḥasan al-. Dalāʾil al-ṣidq. Tehran: Maktabat al-Dhujāj, n.d.
  • Qundūzī, Ḥāfiẓ Sulaymān al-. Yanābīʿ al-Mawadda. Edited by ʿAlī Jamāl Ashraf. Qom: Dār al-Uswa li-l-Ṭabāʿa wa l-Nashr, 1416 AH.
  • Rabbānī Gulpāyigānī, ʿAlī. Imāmat dar bīnish-i Islāmī. Qom: Būstān-i Kitāb, 1386 Sh.
  • Ṭabrasī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Kimehaririwa na: Hāshim Rasūlī Maḥallatī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1379 AH.