Othman bin Said al-Amri
Othman bin Said al-Amri (Kiarabu: أبو عمرو عثمان بن سعيد العمري) (alifariki dunia 267 Hijria) mashuhuri kwa jina la Abu Amru ni Naibu wa Kwanza kati ya Manaibu Wanne wa Imamu wa 12 wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika kipindi cha Ghaiba Ndogo. Othman bin said Amri ametambuliwa kuwa mmoja wa masahaba wa Imamu Hadi (a.s), Imamu Hassan Askary (a.s) na Imamu Mahdi (a.s). Hata hivyo kuna shaka na utata kuhusiana na suala la kwamba, alikuwa mmoja wa masahaba wa Imamu Jawad (a.s). Othman bin Said alikuwa Naibu wa Imamu Mahdi, baada ya kuanza Uimamu wa Imamu Mahdi (a.t.f.s) (mwaka 260 Hiijria), mpaka mwishoni mwa umri wake. Alikuwa Naibu na mwakilishi maalumu wa Imamu Mahdi (a.t.f.s) kwa muda wa takribani miaka 6 hadi 7. Baada yake, aliyechukua jukumu la Naibu wa Imamu ni mwanawe Muhammad bin Othman. Katika zama za Unaibu wake, Othman alikwenda Baghdad na kupitisha kipindi cha uwakala na Unaibu wake akiwa katika mji huo. Alikuwa na mawakala na wawakilishi katika mji wa Baghdad na miji mingine ya Iraq ambao walikuwa wakikusanya fedha za malipo ya kisheria (Wujuhaat) kama Zaka, Khumsi na kadhalika na kumpelekea. Wakati wa Othman alipofariki dunia, Imamu Mahdi alimtumia mwanawe barua ya rambirambi na mkono wa pole. Katika hadithi Othman bin Said ametajwa kwa lakabu mbalimbali kama Zayyat na Amri.
Maisha yake
Hakuna taarifa za uhakika na makini kuhusiana na tarehe aliyozaliwa Othman na inaelezwa kwamba, alikuwa hadimu na mfanyakazi wa Imamu Jawad (a.s) kuanzia umri wa miaka 11. [1] Lakini kwa mujibu wa nukuu ya Sheikh Tusi ni kwamba, yeye alikuwa hadimu wa Imamu Hadi (a.s) kuanzia alipokuwa na umri wa miaka 11. [2] Alikuwa wakili wa Imamu Hadi (a.s) Imamu Hassan Askary (a.s) na Imamu wa zama (Imamu Mahdi) na daima alikuwa akiaminiwa nao. Awali Othman bin Said alikuwa akiishi Samarra na baada ya kufa shahidi Imamu wa 11 yaani Imamu Askary (a.s) alihamia Baghdad. Katika zama hizo Samarra yalikuwa makao makuu ya askari wa utawala wa ukoo wa Bani Abbas ambao tangu mwanzo haukuwa na uhusiano mzuri na Maimamu wa Shia. Baadhi wamesema kuwa, kuna uwezekano ni kutokkana na sababu hiyo ndio maana Othman bin Said akahamia Baghgad na akakifanya kitongoji cha Karkh kilichokuwa makazi ya Mashia kuwa kituo na kitovu cha uongozi wa Imamiyyah. [3]
Majina na Lakabu
Jina la Othman limekuja katika vitabu vya wasifu wa wapokezi wa hadithi kwa anuani ya «Othman bin Said». Lakini katika Rijaal Kashi ametajwa pia kwa jina la Hafsa bin Amru ambapo inawezekana hilo lilikuwa ni jina lake la utani katika mikutano yake ya siri na mawakala wengine. [4] Kuniya yake imetajwa katika vitabu vyote vyenye itibari kwamba, ni Abu Amru, lakini katika kitabu cha Bihar al-Anwar na Safinat al-Bihar imetajwa kuwa ni Abu Muhammad kwani alikuwa na mtoto aliyejulikana kwa jina la Muhammad. [5]
Hata hivyo umashuhuri wake zaidi ni Amri na imeelezwa kwamba, anaitwa kwa jina hilo kwa sababu mbili; kwanza ni kwamba, Imamu Hassan Askary (as) hakuruhusu jina la Khalifa wa Tatu (Othman) na lakabu yake (Abu Amru) yakusanyike katika Othman bin Said na kuanzia hapo akawa akiitwa Amri. Sababu nyingine ni kuwa, alikuwa akinasibishwa na Amru baba yake wa upande wa baba na hivyo akaitwa Amri. [6] Mpokezi wa hadithi Qummi pia anasema kuwa, sababu ya kuitwa kwake Amri ni nasaba yake kwa upande wa mama na Omar bin Atraf A'la. [7]
Lakabu za Othman zimeelezwa kuwa ni «Samman» na «Zayyat». [8] Kadhalika kutokana na kunasibishwa na kabila la Bani Asad, aliitwa pia kwa jina la Asadi kama ambavyo aliitwa kwa lakabu ya Askary kutokana na kuwa alikuwa akiishi katika kitongoji cha Askar huko Samarra. [9]
Watoto
Othman bin Said alikuwa na watoto wawili wa kiume:
- Muhammad bin Othman, ambaye baada ya kuaga dunia baba yake alichukua jukumu la Naibu wa Imamu Mahdi na anatambuulika kuwa Naibu wa pili wa Imamu Mahdi kati ya Manaibu wake wanne katika zama za Ghaiba Ngodo.
- Ahmad bin Othman ambaye jina lake halijaja katika vitabu na vyanzo. Lakini katika orodha ya waliodai kwa uwongo kwamba, ni Manaibu wa Imamu Mahdi kuna jina la mtu anayefamika kama "Abu Bakr Muhammad bin Ahmad bin Othman" ambapo imeelezwa bayana kwamba, ni mtoto wa kaka yake Muhammad bin Othman. [10]
Kifo
Kama ilivyo kuhusiana na kutofahamika tarehe yake ya kuzaliwa, vivyo hivyo, tarehe hasa ya kuaga dunia Othman bin Said haifahamiki. Hata hivyo kuna kauli mbili zilizonukuliwa kuhusiana na hili:
- Kabla ya mwaka 267 Hijria: Hili limekubaliwa na kuafikiwa na akthari ya waandishi wa historia na wanazuoni wa Ilm Rijaa (elimu ya wasifu wa wapokezi wa hadithi).
- Baada ya mwaka 280 Hijria: Kauli hii hoja yake ni tawqi' (barua ya Imamu) ambayo imenukuliwa mwaka 280 Hijria. Sheikh Tabarsi amesema wazi kwanmba, mpokezi wa hadithi hii alisikia hadithi hii mwaka 280 Hijria na hii haiwezi kuweka wazi tarehe ya kuaga dunia Othman. [11]
Baada ya kuaga dunia Othman bin Said, mwanawe Muhammad alimuosha na kumzikka magharibi mwa Madinat al-Salaam, katika kitongoji mashuhuri kwa jina la al-Darb mjini Baghdad. Sheikh Tusi amesema, kuanzia zama alizoingia Baghdad mwaka 408 Hijria mpaka 430 Hijria alikuwa akifanya ziara katika kaburi la Othman bin Said eneo hilo tajwa. [12] Hii leo kaburi la Othman linapatikana katika kitongoji cha Rassafa mashariki mwa Baghdad na katika eneo linalofahamika kwa jina la Bazaar Shurjah. [13]
Uwakala wa Maimamu
- Makala Asili: Mtandao wa Uwakala
Kwa mujibu wa kile kilichokuja katika vitabu na vyanzo vya wasifu wa wapokezi wa hadithi ni kwamba, Othman bin Said alikuwa wakala wa maimamu watatu Maasumu (Imamu Hadi (a.s), Askary (a.s) na Mahdi (a.t.f.s)). Pamoja na hayo katika baadhi ya vitabu vingine ametambuliwa kuwa alikuwa hadimu wa Imamu Hadi (a.s) tangu alipokuwa na umri wa miaka 11 na alikuwa akiaminiwa na wakati mwingine akikabidhiwa baadhi ya majukumu muhimu. [14] Ibn Sharashub pia amemtambua kuwa mlango wa Imamu Jawad. [15] Baadhi ya Maulamaa wa Kishia, wameikataa kauli hii na kuona kuwa haikubaliki kwamba, awe ni katika masahaba wa Imamu Jawad hasa kwa kuzingatia umri wake mdogo na kwamba, mtazamo huu umetajwa kimakosa. [16]
Wakala wa Imamu Hadi
Othman bin Said alikuwa katika orodha ya masahaba wa Imamu Hadi na uwakala wake kwa Imamu umebainishwa wazi na Imamu huyo. [17] Katika hadithi iliyonukuliwa na Ahmad bin Is'haq Qummi kutoka kwa Imamu Hadi, Othman bin Said anatambuliwa kuwa mtu muaminifu na mtunza amana na kwamba, kila ambacho anakinasibisha kwa Imamu na kukifikisha kwa watu yote hayo ni kutoka kwa Imamu Hadi (a.s). [18]
Wakala wa Imamu Askary
Othman mbali na kuaminiwa na Imamu Hadi (a.s) alikuwa akiaminiwa na Imamu Hassan Askary (a.s). [19] Katika orodha yake ya wasifu wa wapokezi wa hadithi, Sheikh Tusi amemtambulisha Othman bin Said kuwa ni wakala na mwakilishi wa Imamu Hassan Askary (a.s). [20] Katika hadithi mbalimbali imenukuliwa kwamba, Imamu Hassan Askary (a.s) alimhutubu Othman bin Saidi na kumtambua kuwa mwakilishi na wakili wake na katika sehemu nyingine watu wa karibu wanashuhudia kuwa, Othman bin Said ni wakili wangu. Imamu alimtambulisha Othman bin Said kuwa kiongozi wa mawakala; kwa maana kwamba, fedha za malipo ya kisheria (Wujuhaat) zilizokuwa zikitolewa na Mashia na kutumwa na mawakala, alikuwa akitiwa Othman na kisha yeye kuzifikisha kwa Imamu. [21]
Baada ya kufa shahidi Imamu Hassan Askary (a.s), Othman bin Said alichukua jukumu la kusimamia shughuli ya kumkafini na kumzika Imamu. Shia Imamiyyah wanaamini kuwa, hii ni ishara na ithbati kwamba, Othman alikuwa mwakilishi wa Imamu Mahdi (a.t.f.s). [22]
Naibu wa Imamu Mahdi
Imamu Hassan Askary (a.s) amesema bayana kuhusiana na unaibu wa Othman bin Said. Alimuonyesha mwanawe kwa watu arubaini miongoni mwa masahaba zake na akawaambia wamtii Othman katika kipindi chote cha ghaiba na kutokuwepo kwa Imamu wa kumi na mbili. [23] Kwa mujibu wa riwaya nyingine, Imamu Mahdi alipokutana na watu wa Qom, aliashiria Unaibu wa Othman bin Said na kuwataka wamrejee yeye. [24] Othman bin Said, kutokana na kuweko hatua kali za maafisa wa serikali huko Samarra na kuwepo kwa maadui wengi, alikwenda Baghdad kwa amri ya mtukufu Imamu Mahdi. Kwa mujibu wa Jassim Hossein katika kitabu cha Tarikh Siyasi Ghaibat Imam Davazidahom (Hitoria ya Kisiasa na Ghaiba ya Imamu wa 12), ingawa Samarra ulikuwa mji mkuu, lakini kutokana na uwepo wa jeshi la ukoo wa Bani Abbas ambao siku zote walikuwa wakiwapinga Maimamu na yeye alikuwa akitaka kuuongoza mtandao wa uwakala mbali na macho ya maadui, aliamua kuelekea Baghdad na kulifanya eneo la makazi ya Mashia la Karkh kuwa kituo na kitovu cha uratibu na uongozi wa Imamiyyah.[25]
Katika kipindi cha kuwa kwake Naibu wa Imamu Mahdi, Othman alikuwa kiongozi wa mawakala wa maeneo mbalimbali na alikuwa akipokea amana, fedha za malipo ya kisheria na zawadi kutoka kwa watu na kuzipeleka kwa Imam. Vile vile alikuwa akiwasilisha barua za Shia kwa Imamu na kuchukua barua zilizoandikwa na Imamu Mahdi kama jibu kwa Shia na kuziwasilisha pia kwa wenyewe. [26] Wakati Jafar, kaka yake Imam Askari (a.s) alipodai kuwa ni Naibu, Ahmad bin Is’haq, mmoja wa masahaba wa Imam Hassan Askari, aliandika barua ili kujua kama dai la Jafar lilikuwa sahihi au la, na akaituma kwa Imamu Mahdi kupitia kwa Othman bin Said. Katika jibu lake, Imam aliukataa Uimamu wa Jafar na akamwita mharibifu (fisadi) na mtu asiyetekeleza ibada ya Sala. [27]
Barua ya Tanzia
Wakati wa Othman alipofariki dunia, Imamu Mahdi alimtumia mwanawe barua ya rambirambi na mkono wa pole. Katika barua hiyo, Imamu Mahdi alionyesha na kutangaza ridhaa yake kamili kwa Othman bin Said na akamuombea maghufira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Kadhalika Imamu Mahdi, alizungumzia upweke wake kwa kutokuweko Othman na akamteua mwanawe Muhammad kuchukua nafasi yake. [28]
Sehemu ya Barua ya Tanzia ya Imamu Mahdi
Baba yako aliishi kwa saada, ufanisi na wema na alikufa katika hali ya kusifiwa na ya kupendeza. Mwenyezi Mungu amrehemu na amuunganishe na Mawalii, masayyid na wafuasi wake. Mungu auburudishe uso wake na amsamehe makosa yake na akuzidishie malipo na akupe subira njema katika msiba wake, wewe umepatwa na msiba na sisi tumepatwa na msiuba pia na kutengana na baba yako umekupa wewe na sisi hofu na wasiwasi. Basi Mwenyezi Mungu amfurahishe kwa rehema zake katika kaburi lake ambalo ni makazi yake. Kutoka katika makavazi ya kumbukumbu za historia
Mbinu ya Harakati
Alikuwa akinunua na kuuza mafuta na zeituni, na biashara hii ilikuwa fubazo na pazia la kazi yake kuu; kwa sababu alikuwa akificha jukumu lake ambalo ni wakala na Naibu wa Imamu ili asalimike na shari ya utawala. Othman alikuwa akiweka mali na barua za Shia kwenye vyombo vya mafuta na kuzipeleka kwa Imam ili mtu yeyote asijue kuhusu uwepo wake na maudhui yake. Kwa hivyo, jina lake la utani ni «Samman» na «Zayyat» pia. [29]
Wasaidizi
Katika kipindi cha kuwa kwake Naibu wa Imamu Mahdi, Othaman bin Said kulikuweko na mawakili mashuhuri waliojulikana kwa majina ya Ahmad bin Is’haq, Muhammad Qattan na Hajiz bin Yazid Wash-shaa waliohesabiwa kuwa wasaidizi wake na walikuwa na jukumu la kuunganisha na kusimamia mawakala wengine katika maeneo tofauti wakiwemo mawakala wa Kufa. [30]
Andiko la Ziyara
Allama Majlisi katika kitabu chake cha Bihar al-Anwar amenukuu matini na andiko la ziyara kwa ajili ya Othman bin Said na kubainisha kwamba, aliona andiko hilo katika nakala ya kale ya alimu na msomi mmoja wa Kishia. Hata hivyo, Majlisi hajaashiria kabisa jina la kitabu na mwandishi wake. [31]