Aya ya Ibtilaa
Jina la Aya | Aya ya Ibtilaa Ibrahim |
---|---|
Sura Husika | Baqara |
Namba ya Aya | 124 |
Juzuu | 1 |
Sababu ya Kushuka | Kutahiniwa kwa Nabii Ibrahimu (a.s) |
Mahali pa Kushuka | Madina |
Maudhui | Itikadi |
Mengineyo | Umaasumu na Uteuzi wa Cheo cha Uimamu |
Aya ya Ibtilaa (Kiarabu: آية الابتلاء) yaani majaribu au kutahiniwa ni Aya ya 124 katika Surat al-Baqarah ambayo inaashiria kuteuliwa Nabii Ibrahim na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya cheo cha Uimamu baada ya kutiwa majaribuni na kutahiniwa mara kadhaa. Wanazuoni na wasomi wa madhehebu ya Shia wanaitambua Aya hii kwamba, ni hoja ya Qur’ani ya kuonyesha kwamba, Imamu anateuliwa na Mwenyezi Mungu na ni lazima awe Maasumu (asiyetenda dhambi).
Wanateolojia na wafasiri wa Qur’ani wa madhebu za Shia na Sunni wamezungumzia mambo mengi na kuwa na mijadala mingi kuhusiana na kadhia hii. Baadhi yao wamesema, makusudio ya «کلمات» yaani matamko au maneno ambayo kwa mujibu wa Aya, Nabii Ibrahim (a.s) aliyakamilisha na kuyatimiza ni ndoto ya Ibrahim kuhusu kumchinja mwanawe Ismail. Wengine wanasema, huko ni kutahiniwa Nabii Ibrahim kwa taklifu za kiakili na kisheria. Allama Muhammad Hussein Tabatabai anaamini kuwa, makusudio ya «کلمات» yaani matamko (maneno) katika Aya hii ni ahadi za Ibrahim na Mwenyezi Mungu na mitihani na majaribu ya Allah kwake.
Tafsiri za wafasiri zinasema kuwa, neno Imamah katika Aya hii lina maana: Uongozi wa kisiasa, Wilayah (uongozi) wa kibatini, Uimamu wa ulimwengu na Utume.
Andiko la Aya na Tarjumi yake
وَإِذِ ابْتَلَى إِبْرَاهِيمَ رَبُّهُ بِكَلِمَاتٍ فَأَتَمَّهُنَّ قَالَ إِنِّي جَاعِلُكَ لِلنَّاسِ إِمَامًا قَالَ وَمِن ذُرِّيَّتِي قَالَ لاَ يَنَالُ عَهْدِي الظَّالِمِينَ
Na Mola wake Mlezi alipo mjaribu Ibrahim kwa matamko, naye akayatimiza. Alimwambia: Hakika Mimi nimekufanya Imam wa watu. Akasema: Na katika kizazi change (pia)? Akasema: Ahadi yangu haitawafikia madhalimu.
(Qur'ani: 2: 124)
Maana tofauti za Kalimat
Kwa mujibu wa Aya ya Ibtilaa Ibrahim (majiribu), Mwenyezi Mungu alimtahini Nabii Ibrahim kwa Kalimat (maneno). Wafasiri wana mitazamo kadhaa kuhusiana na neno «کلمات» yaani matamko (maneno): [1]
- Ndoto ya Ibrahim (a.s) ya kumchinja mwanawe Ismail (a.s).
- Amri na maagizo kuhusiana na usafi au amri kumi za usafi na tohara ya mwili.
- Sifa 30 za kimaadili zilizokuja katika Aya ya 112 ya Surat al-Tawbah, Aya ya 35 ya Surat al-Ahzab na Aya ya 1 hadi ya 9 katika Surat al-Muuminun.
- Mjadala na ujengeaji hoja wa Ibrahim (a.s) na waabudu nyota, mwezi na jua, kutupwa yeye ndani ya moto, kuhajiri kutoka eneo alilozaliwa na kumchinja mwanawe Ismail;
- Kutahiniwa Ibrahim (a.s) na taklifu zote za kiakili na kisheria.
- Kutekeleza amali za Hija. [2]
Tabarsi anasema katika tafsiri yake ya Majmaal Bayan, sambamba na kuamini kwamba neno «کلمات» yaani matamko (maneno) lililokuja katika Aya linajumuisha uwezekano wote unaozungumziwa, ameashiria pia riwaya na hadithi ya Imam Swadiq (a.s) kwamba maneno katika Aya hiyo yanawahusu watu watano wa Kishamia (Ahlul-Kisaa); watu wale wale ambao kupitia kwao toba ya Nabii Adam ilikubaliwa. [3]
Allama Tabatabai anaamini kuwa, licha ya kuwa katika Qur’ani hakujabainisha makusudio ya neno kalimat, lakini kupitia siyaq na mtiririko wa Aya inaweza kufahamika kuwa: Kalimat inajumuisha ahadi za Ibrahim na Mwenyezi Mungu na vitu vyote alivyotahiniwa navyo; kama vile, kisa cha nyota, masanamu, kuhajiri na kumchinja mwanawe Ismail. [4] Kwa mtazamo wake ni kuwa, kama mtendaji katika kitendo cha (فَاتَمّهنّ) yaani akayatimiza” ni Ibrahim, basi maana ya kutimiza kalimat ni kwamba, Ibrahim alitekeleza kile alichotakiwa na Mwenyezi Mungu, lakini kama mtendaji katika kitendo cha (فَاتَمّهنّ) yaani akayatimiza atakuwa ni Mwenyezi Mungu ambapo dhahiri ya Aya ni hivyo, katika hali hii, maana ya kutimiza ni kuwa, Mwenyezi Mungu alimpa tawfik Ibrahim (a.s) na akamsaidia ili aweze kufaulu mitihani. [5]
Makusudio ya Uimamu wa Ibrahim ni nini?
Neno Imamu ni katika maneno mengine ambayo yana tafsiri tofauti:
- Sheikh Tusi amesema katika tafsiri ya Tibyan kwamba, Uimamu katika Aya hii maana yake ni Wilaya (uongozi) na mamlaka (uongozi) wa kisiasa. Yeye hatambui kama Wilaya na uongozi wa kisiasa kuwa ni mambo ya Utume na risala; kwa msingi huo anaamini kwamba, Mitume wote mbali na kuwa na cheo cha Utume, hawakuwa na Wilayat, bali baadhi yao walikuwa na ustahiki wa cheo hicho. [6]
- Kwa mtazamo wa Allama Tabatabai, Imam ni mtu ambaye watu wanamfuata yeye katika maneno na matendo yake na makusudio ya cheo cha Uimamu katika Aya hii ni uongofu wa kibatini; cheo ambacho ili kukifikia kuna ulazima wa kuwa na ukamilifu wa uwepo na cheo cha umaanawi makhsusi ambapo hilo linapatikana baada ya kufanya hima na jihadi kubwa, na hii ni tofauti na Utume na ni kutokana na ukweli huo ndio maana Imamu ana Wilaya kwa watu. [7]
- Tabari mmoja wa wafasiri wa Kisunni wa karne ya 3 Hijria amefasiri Uimamu kwa maana ya Uimamu wa ulimwengu wa Ibrahim. Anaamini kwamba, kwa mujibu wa Aya hii, Ibrahim alikuwa Imamu wa zama zake na zama zingine na hata kwa Mitume wengine na ada zote za Kitawhidi zinapaswa kumfuata yeye. [8]
- Fakhr al-Razi, mfasiri mwingine wa Kisunni amefasiri Uimamu kwa maana ya Utume. [9]
- Jafar Sobhani naye anaamini kwamba, makusudio ya cheo cha Uimamu katika Aya hii, ni Ibrahim kuwa kigezo katika pande zote. Kwa mtazamo wake ni kuwa, daraja na cheo hiki wanapatiwa watu ambao hawa hawana Tark Awla (kuacha kufanya lililobora). Anasema, cheo hiki ni daraja ya juu kabisa ya Umaasumu na ni baadhi ya Mitume tu ambao walikuwa na daraja hii. [10]
Dalili ya Aya kwa Umaasumu wa Imamu
- Makala asili: Umaasumu wa Maimamu
Wanazuoni na Maulamaa wa Kishia wakitumia ibara iliyokuja katika Aya hii:
(لاینالُ عَهدی الظّالِمینَ ;
Ahadi yangu haitawafikia madhalimu). Wamefikia natija juu ya ulazima wa Imamu kuwa Maasumu. [11] Wanaamini kwamba, kwa mujibu wa Aya hii Imamu lazima awe Maasumu na asiwe ni mwenye kutenda aina yoyote ile ya dhambi na dhulma na kwa kuwa watoto wa Ibrahim hawakuwa hivyo, Mwenyezi Mungu akakataa ombi la Ibrahim la Uimamu kwa watoto wake. [12]
Ishkali Iliyotiwa kwa Mtazamo wa Maulamaa wa Kishia
Baadhi wametilia ishkali na kukosoa mtazamo na tafsiri hii kwa kusema, dhalimu ni mtu ambaye kwanza, awe ametenda dhambi kubwa na pili, asitubie dhambi yake. Anuani ya dhalimu, haijumuishi watenda dhambi ambao wametubia dhambi zao. Kwa msingi huo Aya hii haina ishara na dalili za Umaasumu wa Imamu. [13]
Majibu ya Wanazuoni wa Kishia
Sheikh Tusi na Fadhl bin Hassan Tabarsi katika kujibu ishkali na walakini huo wamesema, kukana na kukataa kumekuja katika sura mutlaki katika Aya ya:
(لاَ يَنَالُ عَهْدِي الظَّالِمِينَ ;
Ahadi yangu haitawafikia madhalimu}}. Kwa msingi huo Aya inajumuisha kila dhalimu katika kila zama. Kwa muktadha huo, haiwezekani kusema kuwa, hukumu ya Aya haijumuishi mtu ambaye amefanya dhulma lakini akatubia. Kwa mtazamo wake ni kuwa, kwa kuzingatia jambo hili, ili kumuondoa mtu kama huyu tunahitajia dalili na hoja nyingine, sasa dalili kama hii haijazungumziwa. [14]
Allama Tabatabai pia katika kujibu ishkali hii amesema, Ibrahim hakuwaombea Uimamu kwa Mwenyezi Mungu watu ambao hawakutubia dhambi zao. Kwa msingi huo, ombi lake ima lilikuwa kwa ajili ya watu ambao kimsingi hawakutenda dhulma au kwa watu ambao walitubia dhulma zao; [15] lakini kutokana na watoto wa Ibrahim kufanya dhulma Mwenyezi Mungu alikataa ombi hilo na kwa msingi huo natija inakuwa kwamba, hukumu ya Aya hii (kukataa Uimamu) inajumuisha watu ambao walifanya dhulma na kisha hawakutubia. [16]
Masuala Yanayo Husiana
Rejea
Vyanzo
- Qurʾān.
- Baḥrānī, Sayyid Hāshim al-. Al-Burhān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1393 AH.
- Fāḍil al-Miqdād, jamāl al-Dīn b. ʿAbd Allāh al-. Al-Lawāmiʿ al-ilāhīyya. Qom: Maktabat al-Marʿashī, 1405 AH.
- Fakhr al-Rāzī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Mafātiḥ al-ghayb(al-Tafsīr al-kabīr). Second edition. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1420 AH.
- Ibn Athīr, Mubārak b. Muḥammad. Al-Nihāya fī gharīb wa l-athar. Qom: Ismāʾīlīyān, 1361 Sh.
- Ibn kathīr al-Dimashqī, Ismāʿīl b. ʿAmr. Tafsīr al-qurʾān al-ʿaẓīm. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1419 AH.
- Jurjānī, Mīr Sayyid Sharīf al-. Sharḥ al-mawāqif. Qom: Manshūrāt al-Sharīf al-Raḍī, 1412 AH.
- Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr nimūna. Forty first edition. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1380 Sh.
- Qurṭubī, Muḥammad b. Aḥmad al-. Al-Jāmiʿ ali-aḥkām al-Qurʾān. Edited by ʿAbd al-Razzāq al-Mahdī. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿArabī, 1423 AH.
- Sayyid Murtaḍā, ʿAlī b. al-Ḥusayn. Al-Shāfī fī al-imāma. Tehran: Muʾassisat al-Ṣādiq, 1407 AH.
- Subhānī, Jaʿfar. Manshūr-i Jāwīd. Qom: Muʾassisa-yi Imām Ṣādiq (a), 1383 Sh.
- Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Jamiʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān (Tafsīr al-Ṭabarī). Beirut: Dār al-Maʿrifa, 1412 AH.
- Ṭabāṭabāyī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurān. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī, 1393 AH.
- Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1379 Sh.
- Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Rasāʾil al-ʿashr. Qom: Muʾassisat al-Nashr al-Islāmī, 1363 Sh.
- Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Tibyān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Maktab al-Aʿlām al-Islāmī, 1409
AH.
{{End]]