Ja'far mtoto wa Imam Hadi (a.s)

Kutoka wikishia
Makala hii ni kuhusiana na Ja'far bin Ali maarufu kwa jina la Ja'far Kadhab. Kwa ajili ya matumizi mengine angalia Ja'far ibn Ali

Ja'far ibn Ali (Kiarabu: جعفر بن‌ علي‌ الهادي) (aliaga dunia 271 H) maarufu kwa jina la Ja'far Kadhab (Kiarabu: جعفر الكذّاب) ni mtoto wa Imam Hadi (a.s) na alikuwa akidai kwamba, yeye ni Imam baada ya kufa shahidi kaka yake Imam Hassan al-Askary (a.s); na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Mashia Ithna'asharia wakampatia lakabu ya Kadhab (muongo).

Ja'far akiwa na lengo la kuthibitisha Uimamu wake, alikana uzawa wa Imam Mahdi (a.t.f.s) na kudai kwamba, yeye ndiye mrithi wa Imam Askary (a.s). Kadhalika alitaka kuswalia jeneza la Imam wa kumi na moja yaani Imam Hassan Askary (a.s), lakini Imam Mahdi akamzuia.

Wafuasi wa Ja'far Kadhab nao walifahamika kwa jina la Ja'fariyya. Hata hivyo wafuasi wake wametofautiana kuhusiana na suala la kwamba, J'afar amekuwa Imam baada ya Imam yupi. Baadhi walimtaja kama mrithi wa Imam Hadi huku wengine wakisema ni mrithi Sayyid Muhammad huku wengine walikuwa wakimtambua kwamba, ni mrithi wa Imam Hassan Askary (a.s).

Nasaba na Lakabu

Ja'far ni mtoto wa Imam Hadi (a.s) Imam wa kumi na ndugu wa Imam Hassan al-Askary (a.s) ambaye ni Imam wa kumi na moja. [1] Katika vyanzo na vitabu vya historia hakujatajwa tarehe ya kuzaliwa kwake; hata hivyo kwa kuzingatia hoja hii kwamba, Imam Hassan Askary (a.s) ni mkubwa kwake, imeelezwa kuwa, atakuwa amezaliwa baada ya mwaka 232 Hijria. [2] Aliaga dunia 271 Hijiria katika mji wa Samarra na kuzikwa katika nyumba ya baba yake. [3] Ja'far amezikwa katika Haram za Maimamu wawili Hadi na Askary (a.s). [4]

Kutokana na kudai kwake Uimamu, Mashia wamempa lakabu ya kadhāb (mwenye kusema sana uongo). [5] Kwa mujibu wa hadithi, Mtume (s.a.w.w) alimpa lakabu ya al-Kadhāb kutokana na madai yake ya uwongo kwamba, ni Imam na akapasha habari ya kuzaliwa kwake na mambo atakayoyafanya na akampatia Imam wa sita lakabu ya Swadiq ili kumtofautisha na Ja'far Kadhāb. [6]

Imeelezwa pia ya kwamba, kupewa kwake lakabu ya al-Kadhāb kunatokana na kudai kwake kuwa ni mrithi wa Imam wa Kumi na Moja na kukana kwake kuweko mtoto wa Imam Hassan al-Askary. [7] Pamoja na hayo yote, wafuasi wake walikuwa wakimuita kwa lakabu ya Zakiyyu (mtakasifu). [8]

Kuniya ya J'afar ilikuwa Abu Abdillah; [9] lakini kutokana na kuwa kupitia kizazi chake walizaliwa watoto 120, alikuwa akifahamika kwa lakabu ya Abu Karrayn (baba wa watoto wengi). [10]

Alifahamika pia kwa lakabu Zuqq al-Khamr (mfuko wa divai uliotengezwa kwa ngozi); hilo nalo lilitokana na kuwa, alikuwa akituhumiwa kwamba, anakunywa pombe. [11] Baadhi wanasema kuwa, kuna uwezekano lakabu hiyo chimbuko lake ni uadui baina ya Mashia Ithna'asharia na wafuasi wa Ja'far; [12] hii ni kutokana na kuwa, wafuasi wa Ja'far nao pia walikuwa wakimnasibisha na mambo mabaya na yasiyofaa Imam Askary (a.s) pamoja na wafuasi wake. [13]

Madai ya Uimamu

Baada ya kuuawa shahidi Imam Hassan al-Askary (a.s), Ja'far alijitokeza na kudai Uimamu. [14] Ama kuhusiana na kwamba, alikuwa mrithi wa Imamu yupi, kulikuwa na hitilafu baina ya wafuasi wake. [15] Baadhi walimtambua J'afar kuwa ni mrithi wa Uimamu baada ya Imam Hadi [16] huku wengine wakimtaja kama mrithi wa kaka yake yaani Sayyid Muhammad ambaye aliaga dunia katika kipindi cha uhai wa baba yake. Walikuwa wakiamini kuwa, Sayyid Muhammad alikuwa Imam baada ya Imam Hadi. [17] Kundi jingine la wafuasi wake lilikuwa likimtambua kuwa ni Imam baada ya Imam Hassan Askary (a.s) [18].

Ja'far akiwa na lengo la kuthibitisha madai yake alifanya baadhi ya mambo; hata hivyo kwa mujibu wa Sheikh Mufid hakuna kati ya harakati zake ambazo zilikuwa na natija. [19] Baadhi ya hatu zake ni:

  1. Alitaka kuswalia jeneza la Imam Hassan Askary (a.s), ingawa alikabiliwa na upinzani ambapo Imam Mahdi ambaye wakati huyo alikuwa kijana mdogo alimuondoa na kisha yeye akaswalia jeneza la baba yake. [20] Baadhi ya waandishi wanaamini kwamba, hatua hiyo ya Ja'far ililenga kuthibitisha madai yake ya Uimamu. [21
  2. Alimchochea Mu'tamid Abbasi afanye upekuzi katika nyumba ya Imam Askary (a.s) ambapo ni kwa ushirikiano naye ambapo mmoja wa vijakazi wa Imam Askary alitiwa gerezani. [22] Hatua hii ya Ja'far, aliichukua baada ya kundi la watu waliotoka Qom kwenda Samarra kwa ajili ya kwenda kuonana na Imam Askary (a.s) ambapo walikumbana na habari ya kufa kwake shahidi, [23] na wakamtanguliza Ja'far kama Imam baada yake. Shekhe Swaduq anasema: Walipomuuliza maswali wakamtambua kwamba, hana ustahiki wa kuwa Imam na wakapata majibu ya maswali yao kutoka kwa Imam Mahdi. [24]
  3. Baada ya Imam Hassan Askary (a.s) kuzikwa na licha ya kuwa mama wa Imam alikuwa hai, Ja'far alidai mirathi ya Imam wa kumi na moja; [25]. Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa fikihi ya Kishia, ikiwa mmoja kati ya watu wa tabakala la kwanza katika urithi yuko hai kama wazazi wawili, urithi haumfikii mtu wa tabaka la pili. [26]
  4. Alikuwa tayari kutoa kiwango fulani cha fedha kila mwaka kwa uatwala wa wakati huo ili uidhinishe na kuunga mkono Uimamu wake. [27]

Msimamo wa Mashia

Kwa mujibu wa Sheikh Swaduq ni kwamba, Mashia walimtahini Ja'far kwa njia na mbinu mbalimbali. [28] Mashia wamepinga na kukataa Uimamu wa Ja'far na hawakumuona kama mtu anayestahiki kuchukua cheo na wadhifa huo muhimu na nyeti. [29] Aidha katika kupinga na kukataa madai ya Ja’far, walikuwa wakitumia hadithi zilizokuwa zikipinga kundi la Fatahiyya. [30] Kwa mujibu wa hadithi hizo, ukiacha Imam Hassan na Hussein, haijuzu Uimamu kuweko kwa makaka wawili. [31]

Sifa Zake Maalumu

Katika vyanzo na vitabu vya hadithi, Ja’far anatambuliwa kuwa, mtu mtenda makossa (mhalifu), fasiki na muovu. [32] Sheikh Tusi anasema katika kitabu chake cha al-Ghaiba ya kwamba; wakati wa kuzaliwa Ja'far, Imam Hadi alitoa habari ya kupotea watu kupitia kwa mwanaye huyu. [33]

Katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam wa Zama, Imam Mahdi (a.t.f.s) akijibu barua ya mmoja ya Mashia, Ja’far anatambuliwa kama mtu ambaye hakuwa na ufahamu wa hukumu za dini na asiyeweza kuainisha na kutofautisha baina ya halali na haramu. Kwa mujibu wa hadithi hii, Ja'far aliacha kuswali kwa muda wa siku 40 kwa lengo la kujifunza uchawi. [34]

Imeelezwa pia ya kwamba, Ja’far alikuwa akimfuata na kuwa upande wa Faris bin Hatim (fasiki na mtu aliyekuwa na itikadi ya ughulati); hii ni katika hali ambayo, Imam Hadi (a.s) alimlaani Faris na alikuwa ametoa amri ya kuuawa kwake. [35]

Kutubia

Inaelezwa kuwa, Ja'far alifanya toba kabla ya kifo chake. [36] Waliotoa madai haya walitumia tawqi’ (barua au maandiko) kutoka kwa Imam Mahdi (a.t.f.s) ambapo ndani yake kulishabihishwa kitendo cha Ja’far na kitendo cha ndugu za Yusufu. [37] [38]. Hata hivyo baadhi wakitumia maneno ya Sheikh Mufid kuhusiana na madai ya Uimamu ya Ja’far [39], wametambua makusudio ya Imam wa zama (a.t.f.s) katika tawqi’ hii kwamba, suala pekee hapo ni kuweko historia ya watoto wa Mitume waliopotea. [40]

Kundi la Ja’fariya

Wafuasi wa Ja’far ni mashuhuri katika historia kwa jina la Ja’fariya. [41]. Hata hivyo kabla ya hapo anuani na jina hili lilikuwa likitumiwa zaidi kwa wafuasi wa Imam Ja’far Swadiq (a.s). [42] Watoto wa Ja’far Tayyar, wafuasi wa Ja’far ibn Harb Hamedani (mmoja wa viongozi wa kundi la Mu’tazilah aliyeaga dunia 236 H) na Ja’far ibn Mubashir Thaqafi (mmoja wa viongozi wa Mu’tazilah mjini Baghdad aliyefariki dunia 234 H) nao walikuwa wakiitwa kwa jina la Ja’fariyya. [43]

Wafuasi wa kundi la Fatahiyya ambao walikuwa wakijuzisha na kukubali Uimamu kwa makaka wawili, walirejea kwa Ja’far. [44] Ni kwa muktadha huo, ndio maana Sheikh Swaduq amempatia Ja’far lakabu ya Imam wa pili wa Fatahiyya. [45]

Baada ya J’afar kuaga dunia, baadhi ya wafuasi wake walimrejea mwanawe yaani Abul Hassan Ali aliyekuwa kiongozi mkuu wa masayidi (masharifu) Baghdad. [46] [47] Baadhi ya watu wengine wanaamini kuwa, Uimamu uligawanywa baina ya Abul-Hassan na dada yake Fatma na baada ya wawili hao Uimamu ukawafikia waliobakia katika ukoo wa Ja’far. [48] Sa’d ibn Abdallah Ash’ari ameandika kitabu akijibu nadharia za kundi la Ja’fariya, kitabu ambacho amekipa jina la Dhiya fir radd alaa al-Muhammadiyah wa al-Ja’fariyah. [49] Ali Tahin ametambulika kama mmoja wa viongozi wa kundi la Ja’fariya. [50]

Watoto wa Ja’far kutokana na kunasibnishwa kwao na Imamu Ridha (a.s), walikuwa wakiitwa Banu al-Ridhwa [51] au Ridhawiyun. [52] Sheikh Mufidu amesema, katika zama za kuandika kitabu chake, hakufanikiwa kumpata mtoto yeyote miongoni mwa watoto wa Ja’far ambaye hakujiunga na madhehebu ya Shia Ithna'asharia.