Hadithi

Kutoka wikishia
Al-Kafi, athari ya Sheikh Kuleyni, kutoka katika vitabu vinne vya hadith vya Shia

Hadithi (Kiarabu: الحديث) ni maneno yanayoashiria matamshi, kitendo au taqrir (kufanywa jambo mbele yake na kutokea au kunyamazia kimya) ya Mtume (s.a.w.w) au maasumina wengine. Baada ya Qur'an, Hadithi inatambuliwa kuwa chanzo cha pili cha kujua mafundisho ya dini na imekuwa na nafasi muhimu katika ufahamu wa Waislamu kuhusu dini na kupatikana elimu za Kiislamu, kama vile fiq'h, usul, theolojia na tafsiri.

Hapo mwanzo, mchakato wa kurekodi na kusajili Hadith ulikuwa ukifanyika kwa mdomo. Kisha ikaja hatua ya kusajili hadithi kwa maandishi. Uandishi wa Hadith unachukuliwa kuwa jambo muhimu zaidi katika kuhifadhi, kusambaza na kueneza Hadith za maasumina. Uandishi wa hadithi ulikatazwa na kupigwa marufuku kipindi fulani kutokana na hali ya kisiasa. Hiyo ilikuwa ni katika zama za makhalifa wawili wa kwanza; lakini miaka mia moja baadaye, kwa amri ya Omar bin Abdul Aziz, khalifa wa nane wa Bani Umayyah, sheria hii iliondolewa rasmi na kuandika hadithi likawa jambo la kawaida na lililoenea.

Hata hivyo, watafiti wa hadithi wa Kishia, tangu awali wao walikuwa wakisajili na kuandika hadithi wakitekeleza maagizo ya Maimamu. Inaelezwa kitabu cha kwanza cha Hadith kilichoandikwa katika Uislamu ni kitabu cha Ali au Al Jamia. Hatua za uandikaji wa Hadith za Shia zilijumuisha kusajili Hadithi, kuainisha na kupanga Hadithi, na kisha kuzikusanya katika vitabu vya Hadithi. Vyanzo muhimu vya hadithi au vitabu vya riwaya na hadithi vya Shia Imamiya ni: Al-Kafi kilichoandikwa na Kulayni (aliyefariki: 329 Hijria,), Man La Yahdhuruh al-Faqih kilichoandikwa na Sheikh Swaduq (305-381 Hijria), na Tahdhib al-Ahkam na Istibsar viliyoandikwa na Sheikh Tusi (385-460 Hijria). Vitabu hivi vinajulikana kama Kutub al-Arba'h (Vitabu Vinne). Al-Wafi, kilichoandikwa na Faiz Kashani (1007-1091 Hijiria), Bihar al-Anwar kilichoandikwa na Allama Majlisi (1037-1110 Hijiria) na Wasail al-Shi'a kilichoandikwa na Hurr al-Amili (1033-1104) Hijiria) ni vitabu vingine vya hadithi vya Kishia vilivyoandikwa katika karne za baadaye.

Ahlu-Sunna walianza zoezi la kukusanya hadithi za Mtume (s.a.w.w) katika nusu ya karne ya pili Hijiria. Katika karne ya tatu Hijiria, waliandika vitabu mashuhuri vya Sihah Sittah (Sahihi sita) vitabu ambavyo vinahesabiwa kuwa vyanzo mashuhuri zaidi vya hadithi miongoni mwa Ahlu-Sunna. Vitabu hivyo ni: Sahih Bukhari (194-256 Hijiria), Sahihi Muslim (204-261 Hijiria), Jamiu Tirmidhi, Sunan al-Nasai, Sunan Abi Dawud na Sunan ibn Majah.

Hadithi ina migawanyiko tofauti ambayo miongoni mwayo ni: Al-Khabar al-Wahid na Hadith mutawatir. Khabar Wahid kwa upande wake ina migawanyiko tofauti kama sahih (sahihi), hasan (nzuri), muwathaq (ya kuamianika) na dhaif (dhaifu). Wanazuoni wa Kiislamu hawakubali kila hadithi. Wanaitambua hadithi mutawatir na khabar wahid yenye ishara za uletaji elimu kuwa ni hoja ya kusihi mapokezi na sanadi yake. Wamehitalifiana kuhusiana na Khabar Wahid ambayo haileti elimu. Akthari ya wanazuoni wa fiq'h wa Kishia na Kisuni wanaikubali habari kama hiyo ikiwa itakuwa imepokewa na mtu muaminifu. Ili kufanya uchunguzi, tathmini na kuzigawa hadithi katika makundi kuna mbinu na njia ya kufikia hilo ambapo kuna elimu maalumu kuhusiana na jambo hilo ambazo ni: Ilm Rijaal, Dirayat al-Hadith na Fiq' al-Hadith.


Maana ya hadithi

Hadithi ni kauli, kitendo au taqriri ya Maasumu (kunyamazia kimya neno lililosemwa au kitendo kilichofanywa mbele yake na kutoonyesha upinzani) ; [1] kama hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) na vilevile itikadi ya Mashi ni kuwa, hadithi zilizopokewa kutoka kwa Maimamu. [2] Kwa mujibu wa maandiko ya Maulamaa wa Kiislamu ni kwamba, hadithi huitwa pia kwa jina la “khabar” [3], “riwaya”[4] na “athari”. [5]

Umuhimu wa hadithi kwa Waislamu

Abdul-Hadi Fadhli (1314-1392 Hijiria Shamsia) ameandika: Baada ya Qur’an, hadithi ndio chanzo cha pili cha Waislamu kwa ajili ya kupokea sheria. Juu ya hayo, kwa upande wa wingi, ni pana zaidi kuliko Qur'an na ina mafundisho mengi zaidi ya kidini. Kwahiyo, kupata elimu ya Hadith ni utangulizi na msingi wa ijtihadi na utoaji (unyambuaji) wa hukumu za Shariah. [6]

Kadhim Mudir Shanechi (aliyefariki: 1381 Hijiria Shamsia), mwanazuoni wa hadithi, aliandika katika utangulizi wa kitabu "Ilm al-Hadith" kwamba, elimu zote zilizojitokeza katika Uislamu msingi wake ulikuwa hadithi, na bila ya hadithi zisingefikia ukamilifu: Elimu ya tafsiri, mwanzoni ilikuwa ikijumuisha hadithi tu. Fiq’h na usul daima zimekuwa pamoja na Hadith, na katika elimu ya theolojia na mijadala baina ya madhehebu za Kiislamu, Hadith za Mtume (s.a.w.w) zilikuwa zenye kuianisha maamuzi na kubanisha usahihi na upotovu wa wazo na fikra fulani. Historia na sira navyo havikuwa isipokuwa masimulizi ya hadithi ambayo yalisimuliwa kwa mlolongo. Katika fasihi, maneno ya Mtume yalichukuliwa kama ushahidi pia. [7]

Uandishi wa hadithi

Makala kuu: Uandishi wa hadithi

Kwa mujibu wa watafiti, mchakato wa kurekodi na kusajili Hadithi awali ulikuwa ukifanyika kwa mdomo. Kisha baadaye ukawa katika sura ya maandishi. [8] Wao wanaamini kwamba, uandishi wa hadithi ulikuwa sababu muhimu sana ya kuhifadhiwa riwaya na hadithi za Kiislamu. [9] Nuruddin, mtafiti wa elimu ya hadithi wa Ahlu-Sunna ameandika: Uandishi wa hadithi ulihesabiwa kuwa wenzo muhimu zaidi wa kuhifadhi na kuhamisha hadithi kwa ajili ya vizazi vya baadaye. [10]

Kwa mujibu wa hadithi, Maimamu walitilia mkazo suala la kuandika hadithi. [11] Kwa mujibu wa Sayyid Muhsin Amin, mwandishi wa kitabu cha A’yan al-Shiah, kuanzia zama za Imam Ali (a.s) mpaka katika duru ya Imam Hassan Askary (a.s), Mashia waliandika vitabu 6,600 vya hadithi. [12] Shahidi Thani, kutokana na ukweli kwamba hapakuwa na vitabu vya kutosha vya kidini katika kipindi chake, aliona suala la kuandika hadithi kuwa ni wajibu wa kila mtu (Wajib Aini) [13]


Marukufu ya kuandika hadithi

Makala kuu: Marukufu ya kuandika hadithi

Al-Istbasar, athari ya Sheikh Tusi, kutoka katika vitabu vinne vya Hadith vya Shia

Marukufu ya kuandika hadithi huelezwa kitendo cha kuzuia kuandika na kunukuu hadithi za Mtume (s.a.w.w). Jambo hili lilianza kufanyika baada ya kuaga dunia Bwana Mtume (s.a.w.w) na ilikuwa ni katika kipindi cha ukhalifa wa Abu Bakr na Omar [14]. Mwenendo huu uliendelea kwa muda wa miaka 100, mpaka Omar bin Abdul-Azizi khalifa wa nane wa Bani Umayyah ambaye alikuja na kumuandikia barua Abu Bakr bin Hazm, mtawala wa wakati huo wa Madina na kumtaka aandike hadithi za Mtume; kwani kuna hofu na wasiwasi elimu hiyo na watu wake vikapotea. [15]

Wanachuoni wa Kisunni wanasema kwamba Khalifa wa kwanza na wa pili walipiga marufuku kunukuu na uandishi wa Hadith kwa sababu hizi: Uwezekano wa kuchanganya Hadith na Qur'an, [16] kuzuia kutokea tofauti baina ya Waislamu [17] na khofu ya watu kushughulishwa na jambo jingine lisilokuwa Qur’an. [18]

Lakini kwa mujibu wa Sayyid Ali Shahristani, wengi wa wanazuoni wa Kishia wanaamini kwamba sababu ya kupigwa marufuku uandishi wa Hadithi ilikuwa ni kuzuia kuenea kwa maneno ya Mtume kuhusu fadhila za Imam Ali (a.s.) na watoto wake na Uimamu wao. [19] Kwa mujibu wa Mashia, kuzuiwa kuandika hadithi kulipelekea kujitokeza upachikaji wa hadithi bandia [20], kuangamia matini na maandiko ya awali ya hadithi, [21] kuibuka madhehebu mbalimbali [22] na kubadilishwa Sunna za Mtume (s.a.w.w). [23]

Historia ya uandishi wa hadithi

Majid Maarif ameandika katika kitabu cha "Tarikh umumi hadith" kwamba: Hadithi za Shia zilipitia milima na mabonde mengi. Amegawanya matukio haya katika duru mbili za waliotangulia na waliokuja baadaye: Kipindi cha waliotangulia kinajumuisha karne tano za awali za Hijria. Katika kipindi hiki, Maimamu wa Mashia walitoa hadithi na masahaba zao wakaandika na wasomi waliokuja baadaye waliziweka na kuzipanga hadithi hizo katika makundi mpaka ilipofika zama za wapokezi watatu wa hadithi yaani Kulayni (aliyeaga dunia 329 Hijria), Sheikh Swaduq (305-381 Hijiria) na Sheikh Tusi (385-460) ambapo wao walikuja kuandika na kukusanya hadithi hizo katika vitabu vinne (Kutub al-Ar’baa). [24]

Kipindi cha waliokuja baadaye (mutaakhirin) kilianza mwanzoni mwa karne ya 6 mpaka katika zama hizi na ndani yake kulikamilika vitabu vya hadithi. Kipindi cha waliokuja baadaye, kimsingi zilikuwa zama za upangaji, ukamilishaji na uchambuzi wa athari za waliotangulia. [25]


Tahzeeb al-Ahkam, athari ya Sheikh Tusi, kutoka katika vitabu vinne vya Hadith vya Shia

Kipindi cha waliotangulia

Kipindi cha waliotangulia kinagawanywa katika vipindi vinne:

1. Kipindi cha Imam Ali mpaka katika zama za Imam Sajjad as (karne ya kwanza)

Katika kipindi hiki, kutokana na kuwa, kulikuwepo kwa sera ya marufuku ya kuandika Hadithi na mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Mashia na sera ya taqiya ya Maimamu, hadithi hazikustawi sana. [26] Pamoja na hayo kuna vitabu vilivyoandikwa katika kipindi hiki na miongoni mwavyo ni Kitab Ali. [27] Kitabu hiki kinatambuliwa kuwa kitabu cha kwanza cha hadithi cha Kishia. [28] Kitabu cha Nahaj al-Balagha ambacho katika zama hizo kilikuwa katika sura ya vitabu vyenye anuani ya “Khutab Amiril-Muuminina” au “Khutab Ali” kilikuwa mikononi mwa Mashia [29] na Sahifat al-Sajjadiyah ni miongoni mwa vitabu vingine vya hadithi vilivyokuweko katika kipindi hicho. [30

2. Zama za Imam Baqir na Imam Swadiq (karne ya pili)

Kipindi hiki kilikuwa na nafasi muhimu katika kuundika hadithi za Shia na kuliandikwa athari za hadithi zenye thamani kubwa katika zama hizo. [31] Kipindi hiki zilikuwa zama za kuandikwa elimu na kuondoa marufuku ya kuandika hadithi. Imam Baqir (a.s) na Imam Swadiq (a.s) wakitumia nafasi na fursa hii, waliandaa vikao vya umma, kufundisha majumbani, kuwa na mikutano na watu, kufanya midahalo na kuwa na vikao maalumu vya kufundisha fiq’h na hadithi na hivyo kuwa na nafasi muhimu na isiyo na kifani katika kuundika fiq’h na hadithi kwa upande wa Mashia. [32] Moja ya matunda muhimu zaidi ya duru hii ni kuandikwa misingi minne ya hadithi ambayo ni maarufu kwa jina la Usul al-Ar’baa. [33] Asl (msingi) huitwa kitabu cha hadithi ambacho mwandishi wake amekiandika kwa kusikia hadithi moja kwa moja kutoka kwa Maasumu au kupitia mtu mmoja tu baada ya Maasumu. [34]

3. Zama za Imam Kadhim mpaka mwisho wa Ghaibat Sughra

Katika kipindi hiki, makhalifa walikuwa wakiwadhibiti na kuwawekea mbinyo Maimamu sambamba na kuwashinikiza Mashia. [35] Kwa msingi huo, kulipokewa na kunukuliwa hadithi chache kutoka kwa Maimamu ikilinganishwa na kipindi cha kabla yake. [36] Katika zama hizi kulizingatiwa suala la kukusanya na kupangailia vitabu vya hadithi vya kabla na wapokezi wa hadithi, waliandika vitabu vipana na vilivyokuwa na ubainishaji zaidi kuhusu misingi na riwaya zilizokuwa zimebakia kutoka katika kipindi cha kabla na kuziweka katika mpangilio na milango kulingana na maudhui za kifiq’h. [37]

4. Zama za kudhiri vitabu vya hadithi

Katika zama hizi kutokana na kuwweko harakati amilifu za ufundishaji wa hadithi katika vituo vya elimu, kulibuka haja ya kuandikwa vitabu jumuishi zaidi vya hadithi. Jambo hili lilipelekea kujitokeza vitabu vya hadithi ambavyo baadhi yavyo vilikuwa na maudhui zote za kidini kama fiq’h na theolojia kama vile al-Kafi kilichoandikwa na Sheikh Kulayni na baadhi ya vitabu vilivyokuwa na sura ya maadhui maalumu na za kitaaluma zaidi vilivyojumuisha fiq’h au aqaid (theolojia); kama vile vitabu vya Tauhidi, Uyun Akhbar al-Ridha na Kamal al-Din vilivyoandikwa na Sheikh Swaduq, na al Ghaibah na Amali vya Sheikh Tusi. [38] Kutub al-Arbaa vya Mashia viliandikwa katika zama hizi. [39] Kutub al-Ar’baa (Vitabu Vinne) au Usul al-Ar’baa ni Vitabu Vinne vya hadithi vya Waislamu wa Madhehebu ya Kishia. Mashia wanavitambua vitabu hivyo kuwa ndio vitabu vyao muhimu na vyanzo vyenye itibari katika hadithi. Vitabu hivyo ni al-Kafi, kilichoandikwa na Kulayni (aliaga dunia: 329 Hijria), Man laa yahdhuruh al-Faqih, kilichoandikwa na Sheikh Swaduq (305-381 Hijiria), Tahdhib al-Ahkam na Istibsar vilivyoandikwa na Sheikh Tusi (385-460 Hijria). [40]


Kipindi cha waliokuja baadaye

Mwanzoni mwa kipindi hiki, yaani karne ya 6 mpaka ya 11 Hijiria, mchakato wa uandishi wa vitabu vya hadithi ulikumbwa na hali ya kudorora na kuzorota; hata hivyo kuanzia karne ya 11 Hijiria iliyosadifiana na kuchomoza Feyz Kashani (1007-1091 Hijria), Allama Majlisi (1037-1110 Hijiria) na al-Hurr al-Amili (1033-1104 Hijria), uandishi wa vitabu vya hadithi ulistawi na kushika kasi. Vitabu muhimu kabisa vya hadithi katika kipindi hiki ni: Al-Wafi, kilichoandikwa na Feyz Kashani, Bihar al-Anwar kilichoandikwa na Allama Majlisi na Wasail al-Shiah kilichoandikwa na al-Hurr al-Amili. [41] katika zama za leo yaani miaka 100 ya hivi karibuni pia kuna wanazuoni ambao walikuja na kukusanya, kupanga na kuchagua hadithi sahihi. Vitabu muhimu zaidi vya duru hii ni: Mustadrak al-Wasail, Safinat al-Bihar, Jamiu Ahadith al-Shia, Athar al-Swadiqin, Mizan al-Hikmah na al-Hayat. [42]


Historia ya uandishi wa hadithi kwa Ahlu-Sunna

Abdul-Hadi Fadhli ameigawa historia ya hadithi ya Ahlu-Sunna katika hatua na duru tatu:

 • Hatua na duru ya kwanza: Ukusanyaji wa hadithi, hatua ambayo ilianza katika nusu ya karne ya pili. Katika kipindi hiki, shakhsia na wanazuoni wakubwa wa Ahlu-Sunna, walijuhusisha na kazi ya kukusanya hadithi na kuziweka katika vitabu pamoja na fat’wa za masahaba na tabiina. Kitabu cha Al-Muwatta cha Malik ibn Anas kiliandikwa katika kipindi hiki. [43]
 • Duru ya vitabu vya Musnad: Vitabu vya Musnad ni vitabu vya hadithi ambavyo ndani yake kumeandikwa na kunukuliwa hadithi za Mtume tu. [44] Kuanzia mwishoni mwa karne ya pili, baadhi ya viongozi wa Ahlu-Sunna walijihusisha na kuandika vitabu vya Musnad. Musnad Ahmad bin Hanbal ni moja ya vitabu vilivyoandikwa katika duru hii. [45]
 • Duru ya vitabu vya sahih: Sahih ni kitabu cha hadithi ambacho mwandishi wake ameleta humu kama anavyoamini hadithi sahihi tu ambazo amezinasibishwa kwa Mtume (s.a.w.w). [46] Mtu wa kwanza ambaye aliandika kitabu cha hadithi cha sahih ni Muhammad bin Ismail Bukhari (194-296 Hijria). Sahih Bukhari na Sahih Muslim ni vitabu vya hadithi vilivyoandika katika duru na kipindi hiki. [47]

Mgawanyo wa Hadithi na hoja zake

Vilevile tazama: Khabar Wahid na hadithi mutawatir

Ili kujadili na kuchunguza hoja ya hadithi na ithbati yake au itibari yake, wanazuoni wamegawanya hadithi katika vigawanyo tofauti. Katika mgawanyo wao kuna aina mbili za hadithi. Hadithi inayojulikana kama Khabar Wahd na Hadith Mutawatir.

Khabar Wahid ni hadithi ambayo idadi ya wapokeaji wake haijafikia kiwango ambacho kinaleta yakini kwamba, imetoka kwa Maasumu, [48]. Khabar Wahid ni mkaba wa hadithi mutawatir. Hadith mutawatir ni hadithi ambayo idadi ya wapokezi wake imefikia kiwango ambacho kinaleta yakini kwamba, hadithi hiyo imenukuliwa kutoka kwa Maasumu. [49]

Khabar Wahid nayo ina migawanyo mbalimbali. [50] Migawanyo hiyo ni kwa kuzingatria sifa maalumu za wapokezi na ina migawanyo minne mikuu ambayo ni sahih (sahihi) hasan (nzuri), muwathaq (ya kuaminika) na dhaif (dhaifu). [51]


Hadithi gani zenye hadhi?

Mjadala na maudhui ya mapokezi sahihi na hadhi ya hadithi ni jambo linalohusiana na uga wa elimu ya Usul al-Fiq’h [52]. Abdul-Hadi Fadhli anasema, wanazuoni wa elimu ya usul wana ijma'a na kauli moja kuhusiana na sanadi na mapokezi sahihi ya hadithi ambayo ni mutawatir, kutokana na kuwa inaleta yakini. [53] Kwa maana kwamba, wanakubali na kuzifanya hoja hadithi zote ambazo zimetimiza sifa ya kuwa ni mutawatir (zilizokithiri mapokezi yake). Aidha wanaikubali hadithi ambayo ni khabar wahid ambayo imeambatana na ishara na ithibati za elimu na hawana shaka katika hilo. [54] Hata hivyo, wamehitalifiana kuhusiana na Khabar Wahid ambayo haijaambatana na ishara za kuleta elimu. [55]


Mtazamo wa Ahlu Sunna

Kwa mujibu wa Shawkani ambaye ni mwanazuoni wa fiq’h wa Kisuni (aliaga dunia: 1250 Hijiria) ni kwamba, wanazuoni wa Ahlu-Sunna pia wanaikubali na hawana neno kuhusiana na usahihi wa mapokezi wa hadithi mutawatir. [56] Hata hivyo wana mitazamo tofauti kuhusiana na kuwa sahihi hadithi ya khabar wahid. [57] Wengi wao akiwemo Ahmad bin Hambal [58] wanaamini kwamba, ina itibari. [59]. Wengine wanasema haina itibari isipokuwa kama kutakuwa na ishara nje ya hadithi yenyewe ambazo zitapelekea tupate yakini. [60]

Sanadi (mlolongo wa upokezi wa hadithi)

Makala kuu: Sanadi

Makusudio ya Sanadi ni kutajwa mlolongo na silsila ya wapokezi wote wa hadithi mpaka kufika kwa Maasumu; kwa maneno mengine ni kuwa, kubainishwe mlolongo na majina ya wapokezi wa hadithi. [61] Mapokezi au kutaja mlolongo wa mapokezi ya hadithi ni jambo lenye umuhimu kutokana na kuwa, ni moja ya njia na mbinu za kutambua hadhi na usahihi wa hadithi. [62] Inaelezwa kuwa, ni kutokana na sababu hii ndio maana Mamimamu wa Shia na vilevile Maulamaa wa Ahlu-Sunna daima walikuwa wakitilia mkazo suala la kuandikwa hadithi. [63]

Kughushi Hadithi

Makala kuu: Kughushi Hadithi

Kughushi hadithi au kupachika hadithi bandia, maana yake ni kutunga hadithi na kisha kuinasibisha na Mtume (s.a.w.w) au Imam Maasumu, yaani kudai kwamba, amesema yeye ilhali ni hadithi ya kubuni na kutunga. [64] Hadithi ya namna hii inajulikana pia kwa jina la “hadithi bandia” au ya kughushi. [65] Inaelezwa kuwa kughushi hadithi kulikuwa kukifanyika zaidi katika maudhui za kiitikadi, kimaadili, kihistoria, kitiba, kifadhila na katika dua. [66]

Kughushi hadithi kulifanyika kwa mbinu na mitindo tofauti: Kuna wakati kulikuwa kukitungwa hadithi kamili (ambayo haikuweko kikamilifu), wakati mwingine baadhi ya lafudhi na maneno yalikuwa yakiongezwa au kubadilishwa katika hadithi ambayo imenukuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) au Imam. [67]

Mfano wa wazi wa kughushi hadithi ni hatua ya Masur Dawaniqi, khalifa wa Kiabbasi ambaye alitia mkono katika hadithi hii ya Mtume isemayo: “Mwenyezi Mungu atamleta mtu kutoka katika Ahlu-Bayt wangu ambaye, jina lake ni jina langu” [68]. Mansur akaongezea ibara isemayo: “Na jina la baba yake, ni jina la baba yangu” katika hadithi hiyo ili mwanawe aliyekuwa akiitwa Muhammad awe ni mfano na kielelezo cha hadithi hii, kwani jina la Mansur lilikuwa Abdallah sawa na jina la baba yake Mtume. [69]

Baadhi wanaamini kuwa, kughushi hadithi kulianza katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w). [70] Hata hivyo kundi jingine linasema, utungaji wa hadhi na kughusshi hadithi ulianza baada ya kumalizika kipindi cha Khulafaar-Rashidin, yaani baada ya kuuawa shahidi Imam Ali (a.s).

Inaelezwa kuwa, katika zama za Muawiyyah suala la kughushi hadithi na hadithi bandia lilichukua wigo mpana sana. [71] Ibn Abil-Hadid aliyetoa sherh na ufafanuzi wa Nahaj al-Balagha katika karne ya saba Hijiria ameandika, Muawiyyah alikuwa akiwaunga mkono wapokezi wa hadithi waliokuwa wakitunga hadithi za kueleza fadhila za Othman na masahaba wengine na waliokuwa wakija na hadithi bandia zinazoeleza aibu na mapungufu ya Imam Ali (as). [72]

Vitabu muhimu vya Hadithi

Makala kuu: Vitabu vya Hadithi


Man la yahduruh al-faqih, moja ya vile vitabu vinne

Vitabu muhimu vya hadithi kwa upande wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ni:

Al-Kafi, Tahdhib al-Ahkam, Istibsar na man la yahdhuruh al-Faqih ambavyo vinatambulika kwa jina na Kutub al-Ar’baa (vitabu vinne). [73] Vitabu vingine vya hadithi ambavyo ni mashuhuri kwa Mashia ni: Al-Wafi, Bihar al-Anwar, Wasail al-Shiah, [74] Mustadrak al-Wasail, Mizan al-Hikmah, Jamiu Ahaadith al-Shia, al-Hayata na Athar al-Swadiqin. [75]

Kwa upande wa Waislamu wa Kisuni, vitabu mashuhuri zaidi vya hadithi kwao ni: Muwatta Malik, Musnad Ahmad bin Hanbal, Sahih Bukhari, Sahih Muslim, Jamiu Tirmidhi, Sunan Abi Daud, Sunan Nasai na Sunan ibn Majah. [76] Aidha vitabu sita vya mwisho katika orodha hii ni mashuhuri kwa jina la Sihah Sittah (Sahihi Sita). [77]

Elimu ya hadithi

Katika karne za mwanzoni mwa Uislamu kulijitokeza elimu mbalimbali kuhusiana na hadithi ambamo ndani yake hadithi zilikuwa zikichunguzwa na kujadiliwa pande zake mbalimbali kama vile matini (andiko) ya hadithi na sanadi (mlolongo wa mapokezi) yake n.k. [78]

Baadhi ya elimu hizo ni:

 • Rijaal: Elimu hii inatambulisha wapokezi wa hadithi na kuchunguza sifa zao kama uadilifu na imani yao, na hilo kuwa na nafasi muhimu katika kuzikubali au kuzikataa hadithi kutoka kwao. [79]
 • Dirayat al-Hadith au Mustalahul-Hadith: Elimu hii inachunguza migawanyo ya hadithi, istilahi za hadithi kuhusiana na sanadi, na matini ya hadithi, njia na masharti ya tahammul hadith (kusikiliza na kupokea hadithi) na adabu za kunukuu. [80]
 • Mukhtalif al-Hadith: Katika elimu hii kunajadiliwa hadithi ambazo zina mgongano na njia za kuondoa mgongano huo. [81]
 • Nasikh wa Mansukh: Katika elimu hii kunajadiliwa hadithi zenye mgongano ambazo hakujapatikana njia ya kuondoa mgongano wake. [82]
 • Fiq’h al-Hadith: Katika elimu hii hujadiliwa misingi, mipaka na mbinu za kufahamu matini (maandiko) ya hadithi.


Vyanzo

 • Abū al-Sheikh Iṣfahānī. Al-Amthāl fī l-ḥadīth al-nabawī. Edited by ʿAbd al-ʿAlī ʿAbd al-Ḥamīd. Mumbai: Dār al-Salafīyya, 1982.
 • Anṣārī, Zakarīyya b. Muḥammad al-. Al-Ḥudūd al-anīqa. Edited by Māzin Mubārak. Beirut: [n.p], 1411 AH.
 • Dihkhudā, ʿAlī Akbar. Amthāl wa ḥikam. Tehran: [n.p], 1352 Sh.
 • Ibn Ḥibbān, Muḥammad. Ṣaḥīḥ. Edited by Ṣaḥīḥ Irnāʾūṭ. Beirut: Muʾassisat al-Risāla, 1414 AH.
 • Mālik b. Anas. Al-Muwaṭṭaʾ. Edited by Muḥammad Fuʾād ʿAbd al-Bāqī. Cairo: Maṭbʿat Dār Iḥyāʾ al-Kutub al-ʿArabīyya, 1370 AH.
 • Muslim b. Ḥajjāj. Ṣaḥīḥ Muslim. Edited by Muḥammad Fuʾād ʿAbd al-Bāqī. Cairo: [n.p], 1955.
 • Tirmidhī, Muḥammad b. ʿĪsā al-. Sunan al-Tirmidhī. Aḥmad Muḥammad al-Shākir et.al. Cairo: Jamʿīyyat al-Makniz al-Islāmī, 1421 AH.
 • Qāsimī, Muḥammad. Qawāʾid al-taḥdīth. Edited by Muḥammad Bahjat. Cairo: [n.p], 1380 AH.
 • Saʿdī, Muṣliḥ b. ʿAbd Allāh. Būstān-i kitāb. Tehran: Andīsha-yi Kuhan, 1384 Sh.
 • Sanāʾī Ghaznawī, Majdūd b. Ādam. Dīwān. Tehran: Ibn Sīnā, 1341 Sh.
 • Shahīd al-Thānī, Zayn al-Dīn b. ʿAlī al-. Al-Riʿāya fī ʿilm al-dirāya. Edited by Muḥammad ʿAlī Baqqāl. Qom: Maktabat Āyatollāh Marʿashī, 1408 AH.
 • Shaybānī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Āthār. Edited by Abū l-wafāʾ al-afghānī. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1993 AH.
 • Shūshtarī, Muḥammad Taqī. Al-Akhbār al-dakhīla. Tehran: [n.p], 1401 AH.
 • Ṣubḥī Ṣāliḥ. ʿUlūm al-ḥadīth wa muṣṭaliḥuḥ. Qom: Maktaba al-Ḥaydarīyya, 1417 AH.
 • Suyūṭī, ʿAbd al-Raḥmān b. Abī Bakr al-. Tadrīb al-rāwī. Edited by ʿAbd al-Wahhāb ʿAbd al-Laṭīf. Cairo: [n.p], 1966.