Kitabu cha Jafr
Jafr (Kiarabu: الجفر والجامعة) ni jina la kitabu cha hadithi kilichoandikwa kwa mkono wa Imam Ali (as) akisomewa imla na Mtume (s.a.w.w). Kwa maana kwamba, Mtume alikuwa akisoma imla na Imam Ali akiandika juu ya ngozi ya mwanambuzi. Kitabu cha Jafr ni katika vitu vilivyoachwa na Mtume (s.a.w.w), Imam Ali (as) na Fatma Zahra (as) kwa ajili ya Maimamu na kinahesabiwa kuwa moja ya vyanzo vya elimu ya Imam, ambapo kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, ni Mtume tu na mawasii wake ndio wanaoweza kukiangalia kitabu hiki. Baadhi ya wahakiki wanaamini kwamba, kitabu cha Jafr kimeandikwa kwa mafumbo na imesajiliwa humo elimu ya wakati wa kifo, misiba na mabalaa. Baadhi ya wahakiki wakitegemea baadhi ya hadithi wanaamini kwamba, kwa sasa kitabu hicho kipo mikononi mwa Imam Mahdi (atfs).
Utambulisho na nafasi yake
Kwa mujibu wa hadithi zilizopokewa na Waislamu wa Kishia, Jafr ni kitabu ambacho kiliandikwa kwa mkono na hati ya Imam Ali (as) kwa kusomewa na Mtume (s.a.w.w). [1] Kilugha Jafr ina maana ya mwanakondoo au mbuzi. [2] Kwa msingi huo, katika istilahi ya hadithi, Jafr ni kitabu maalumu ambacho kimeandikwa na Imam Ali juu ya ngozi ya mwanambuzi akisomewa na Mtume (s.a.w.w). [3] Kwa mujibuu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Kadhim (as), katika kipindi cha mwishoni mwa umri wa Mtume, Mwenyezi Muungu alimuamrisha aendele katika Mlima Uhud akiwa pamoja na Imam Ali (as) na wamchinje mtoto wa mbuzi watakayemkuta huko. Baada ya wawili hao kutekeleza amri hiyo, walichuna ngozi ya mnyama huyo. Malaika Jibril alishuka akiwa na kundi la Malaika akiwa amekuja na kalamu na wino wa rangi ya kijani na Imam Ali (as) alitumia wino na kalamu hiyo kuandikia juu ya ngozi ya mnyama yule na aliandika kila alichosomewa na Mtume. [4] Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, kitabu cha Jafr ni katika vitu waliavyaochiwa Maimamu ambacho kinathibitisha Uimamu wa mhusika aliye nacho. [5] Agha Bozorg Tehran, mwandishi wa kitabu cha al-Dhariah anasema: Kitabu cha Jafr kama vilivyo vitu vingine waliavyoachiwa Maimamu (kutoka kwa Mtume, Imam Ali na Bibi Fatma Zahra), walipokezana Maimamu wa Kishia mkono kwa mkono na hivi sasa kipo mikononi mwa Imam Mahdi (atfs). [6] Baadhi ya waandishi wameinasibisha elimu ya Jafr kwa Imam Ali (as), [7] mkabala na wao, kuna wahakiki wamesema kuwa, unasibishaji huo hauna hoja na mashiko. [8]
Jafr zingine
Katika baadhi ya hadithi kumezungumziwa na kuashiria Jafr zingine kama Jafr nyeupe na Jafr nyekundu. [9] Akram Barakat mwandishi wa Kilebanon (aliyezaliwa 1968 Miladia) anaamini kwambva, Jafr zingine ghairi ya kitabu cha Jafr ni mifuko ya ngozi ya kuhifadhia vitu vya kimaanawi. [10] Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, vitabu kama Kitabu cha Ibrahim (as) [11], Torati, Injili, Zaburi na msahafu wa Fatma (as) viko katika Jafr nyeupe [12], na upanga wa Mtume unahifadhiwa katika Jafr nyekundu. [13]
Maudhui na sifa maalumu
Kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kuutoka kwa Imam Sadiq (as) elimu ya wakati wa kifo, wakati wa kutokea mabalaa na masaibu, habari za matukio yote kuanzia mwanzo mpaka siku ya Kiyama yamesajiliwa katika kitabu cha Jafr. [14] Kwa mujibu wa hadithi iliyoinukuliwa kutoka kwa Imam Sadiq (as) ni kwamba, alama na ishara za kudhihiri Imam Mahdi, habari za marafiki na maadui wa Imam Ali (as) ambao watazaliwa mpaka siku ya Kiyama na tafsiri ya kile ambacho anakijua Mwenyezi Mungu tu na wale walio na msingi madhubuti katika elimu kuanzia mambo madogogo madogo yameandikwa na kutajwa katika kitabu cha Jafr. [15] Baadhi wanaamini kwamba, kitabu hiki kimeandikwa kwa njia ya mafumbo. [16] Udogo wa kitabu hiki (ngozi ya mwanambuzi) na mambo mengi yaliyotajwa humo (kusajiliwa matukio yote ya ulimwengu) ni jambo ambalo liliwafanya wahakiki wafanye utafiti wa kutatua hali hii ya kutokuweko mlingano. (matukio mengi katika ngozi ndogo) [17] Sayyid Mir Sharif Jarjani (740-816 Hijria), ni mmoja wa Maulamaa wa Kihanafi wa karne ya 8 Hijria ambaye katika kutatua tatizo hilo anasema kuwa, kitabu cha Jafr kimeandikwa kwa mbinu ya elimu ya herufi. [18] Hata hivyo, Akram Barakat, mwandishi wa Kilebanon sambamba na kukubaliana na kauli ya kwamba, kitabu hiki kimeandikwa kimafumbo, anasema kuwa, maneno ya Jarjan ni madai ambayo hayana hoja na anaamini kwamba, katika hadithi hakuna maelezo na ufafanuzi wowote uliotolewa kuhusiana na jambo hili. [19]. Kutochakaa ngozi ya mwanambuzi na kutosambaratika muundo wake, ni miongoni mwa sifa maalumu zilozotajwa katika hadithi kuhusiana na kitabu hiki. [20] Imam Kadhim (as) amenukuliwa akisema kuwa, kutazama Jafr ni katika sifa maalumu na upendeleo kwa Mtume (s.a.w.w) na warithi wake na kwamba, ni hawa tu ndio wanaoweza kuangalia kitabu cha Jafr. [21]
Mifano ya nyaraka za Maimamu (as) kwa kitabu cha Jafr
Katika baadhi ya hadithi, kumeelezewa suala la Maimamu (as) kukirejea kitabu hicho na kutoa kwao habari kuhusiana na masuala ya ghaiba; miongoni mwa hadithi hizo ni kutoa habari Imam Sadiq (as) kuhusiana na wakati na kuzaliwa Imam Mahdi, umri wake na matukio ya ghaiba [22].
Mtazamo wa Ahlu-Sunna
Akthari ya Waislamu wa Ahlu-Sunna wamekinasibisha kitabu cha Jafr na Imam Sadiq (as) [23] Ibn Khaldun, mwandishi wa historia wa karne ya 8 Hijria anaamini kwamba, kitabu cha Jafr kiliandikwa na Harun bin Said Ajli mmoja wa shakhsia wakubwa wa Zaydiyah ambapo alinukuu hadithi mbalimbali kutoka kwa Imam Sadiq (as) zinazoelezea na kusimulia matukio ya baadaye. [24] Ibn Taymiyyah, kiongozi wa Usalafi, amepinga kuweko kitabu cha Jafr au kitabu kingine chochote kutoka kwa Maimamu (as) kinachozungumzia na kusimulia habari za matukio ya baadaye. [25] Kwa mujibu wa baadhi yya waandishi wa Ahlu-Sunna, elimu ya ghaibu kuwa maalumu kwa Mwenyezi Mungu na kwa baadhi ya Mitume ndio sababu ya Ibn Taymiyyah kukana kitabu cha Jafr.
Monografia
Kuhusiana na maudhui ya kitabu cha Jafr, kumeandikwa vitabu mbalimbali na baadhi yavyo ni:
- Haqiqat Jafr inda al-Shiah, mwandishi Akram Barakat al-Amili. [26]
- Negahe nu be Jafr Ali (as), mwandishi Sayyid Hussein Musawi Zanjani. [27]
- Bahth Hawla Jafr wa Ilm al-Maasumu (as) Min Khilal al-Athaar, mwandishi Sayyid Ammar Sadr al-Din Musawi Amili, [28]
Rejea
Vyanzo