Kufariki kishahidi kwa bibi Fatima (s.a)

Kutoka wikishia
Assalam aleik ya Fatima Zahraa (a.s)

Shahadat Sayyidah Fatima (a.s) (Kiarabu: شهادة السيدة فاطمة (ع)), Imani juu ya kufariki kishahidi kwa bibi Fatima (s.a), ni imani ya zamani na iliyo sambaa zaidi miongoni mwa Mashia, ambapo kulingana na imani hiyo, bibi Fatima (a.s) binti wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliuawa shahidi, na hakufa kwa kifo cha kawaida, bali ni kutokana na madhara yaliyosababishwa na baadhi ya masahaba wa Mtume (s.a.w.w). Ahlu Sunnah wanaamini kifo chake kilisababishwa na huzuni ya kuondokewa na baba yake (Mtume Muhammad (s.a.w.w)). Lakini Mashia wanamchukulia Omar bin Khattab kuwa ndiye sababu kuu ya kifo chake, nao huomboleza kifo chake katika masiku maalumu yajulikanayo kwa jina la Ayyamu Fatimiyya.

Mashia wameelezea sababu za kifo cha Fatima al-Zahra (a.s) kupitia vielelezo mbali mbali; ikiwa ni pamoja na Hadithi kutoka kwa Imamu Kadhim (a.s), ambapo ndani ya Hadithi hiyo yeye amepewa wasifu wa Siddiqah al-Shahida kwa maana ya mkweli aliye kufa kishahidi. Pia, Muhammad bin Jarir al-Tabari, mwanathiolojia wa madhehemu ya Shia wa karne ya tatu Hijiria, katika kitabu chake Dalail al-Imamah, amenukuu Hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (a.s), ambapo kwa mujibu wake; sababu ya kifo cha bibi Fatima (a.s) inahusishwa na tukio la kuharibika kwa mimba yake kutokana na kipigo.

Vyanzo vya Shia na Sunni vimeelezea maelezo ya kina juu ya matukio yaliyo pelekea kifo cha Bibi Fatima (a.s); ikiwa ni pamoja na uvamizi wa nyumba ya bibi Fatima na Imam Ali (a.s) kupitia masahaba fulani, kuharibika kwa uja uzito wa mtoto wake aliye julikana kwa jina la Mohsin, pamoja na kupigwa na kufinywa kibao pamoja na mijeledi. Chanzo cha zamani zaidi kinacho tegemewa na Mashia kama ni kielelezo juu ya tukio hilo, ni kitabu cha Sulaym bin Qais al-Hilali, kilicho andikwa katika karne ya kwanza Hijiria. Mashia pia wanaamini ya kwamba; suala la kufariki kishahidi kwa bibi Fatima (a.s), ni suala lenye vielelezo kamili katika Hadithi mbali mbali. Hadithi zinazoelezea tukio hili pia zimeripotiwa kutoka katika vyanzo vya Sunni. Kitabu al-Hujum ‘Alaa Baiti Fatima ni kitabu kilicho nukuu tukio hili kupitia Hadithi 84 kutoka vyanzo vya Sunni.

Imani juu ya kifo cha kishahidi cha bibi Fatima al-Zahra (a.s) imekabiliwa na dadisi kadhaa, huku upande wa pili ukijaribu kujibu hoja dhidi ya dadisi hizo; miongoni mwa ukosoaji juu ya suala hili, ni kwamba madai haya ya upande wa Mashia au pia baadhi ya waandishi wengine, yanayo husiana na bibi Fatima kutiliwa moto au pia kusukumizwa kwenye mlango, hayaendani na hali ya zama hizo, kwa sabau nyumba za Madina wakati huo hazikuwa na milango. Sayyid Ja'far Murtadha Amili (aliye fariki mwaka 1441 Hijiria) ambaye ni mwanahistoria wa Shia, amejibu kwa kutoa ushahidi kutoka katika Hadithi ambazo zinaonyesha kuwa nyumba za Madina zilikuwa na milango. Vilevile kuhusiana na suala la kuvamiwa kwa bibi Fatima (a.s), wapinzani wamejaribu kupinga tukio hili kwa kusema; kwa nini Imam Ali (a.s) pamoja na wengine walio kuwepo walikaa kimya bila ya kumlinda? Katika kujibu hoja hii, Mashia pamoja na kutoa maelezo ya kwamba; Ali (a.s) alikuwa amepewa amri na bwana Mtume (s.a.w.w) kuwa mvumilivu na subira kwa ajili ya maslahi ya umma wa Kiislamu. Pia imesemwa kuwa; kulingana na Hadithi kutoka katika kitabu cha Sulaim ni kwamba, baada ya kitendo cha Omar bin Khattab cha uvamizi huo, Ali (a.s) alimvamia na kumweka chini, jambo ambalo lilimfanya Omar aombe msaada kutoka kwa wafwasi wake, ambao walimshika na kumfunga. Waandishi wa upande wa Kisunni wanaamini kuwa; kuna ushahidi wa kuwepo kwa uhusiano chanya kati ya Imam Ali (a.s), bibi Fatima al-Zahra (a.s) na Makhalifa watatu, jambo ambalo linatosha kuwa ni uthibitisho wa kukanusha kifo cha bibi Fatima kupitia mateso au shinikizo kutoka kwa Makhalifa hao. Walakini, kwa maoni ya waandishi wa upande wa madhehebu ya Shia, ushauriano wa Makhalifa na Ali (a.s) haukuwa ni sababu ya ushirikiano na mshikamano wake pamoja nao, kwa sababu yeye (Ali) aliwajibika kutoa mwongozo kwa ajili ya manufaa ya umma, kwani mwongozo juu ya hukumu za kidini ni jambo la wajibu linalo hitajika kutoka kwa kila mwanachuoni. Pia, Makhalifa hao hawakuonekana kumfanya yeye kama ndiye mshauri wao, bali walionekana kumtenga moja kwa moja, na walishauriana naye katika hali za wao kuto kuwa na budi tu katika jambo hilo. Pia Mashia wakijibu ukaribu wa nasaba baina ya Omar kupitia ndoa yake na Ummu Kulthum, wanasema kwamba ndoa ya Ummu Kulthum, binti wa Imam Ali, na Omar Bin Khattab ilifanyika kwa nguvu na haikuwa ndoa ya hiari, jambo ambalo haliwezi kuwa ni ishara ya uhusiano wa karibu kati ya Imam Ali (a.s) na Makhalifa hao.

Umuhimu wa maudhui

Maana halisi ya dhana ya kifo cha kishahidi cha bibi Fatima al-Zahra (s.a) ni kwamba; kifo cha Fatima binti wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) hakikuwa ni kifo cha kawaida, bali ni kwa sababu ya madhara yaliyosababishwa na baadhi ya masahaba wa Mtume (s.a.w.w). Suala la kwamba je, yeye alikufa kishahidi au kupitia kifo cha kawaida? Ni miongoni mwa masuala yenye khitilafu kati ya Shia na Sunni. [1] Mashia, licha ya tofauti zao katika kunukuu Hadithi zenye kuelezea matukio yaliyo tokea baada ya kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w.w), aghalabu yao wanaamini kuwa bibi Fatima al-Zahra (s.a) aliuawa shahidi, na tukio hilo lilitokana na kupigwa kwenye ubavu wake lililo pelekea kuharibika kwa mimba yake tomboni. Kwa upande mwingine, Ahlu-Sunnah wanaamini ya kwamba; bibi Fatima (a.s) alikufa kifo cha kawaida kutokana na ugonjwa na huzuni ya kuondoka kwa Mtume wa Allah (s.a.w.w). [2]

Mashia kila mwaka huadhimisha maombolezo ya kifo bibi Fatima al-Zahra (s.a), maombolezo hayo kwa kawaida hufanyika katika siku zinazojulikana kwa jina la Ayyamu Fatimiyyah. [3] Mashia huadhimisha maombolezo hayo kuanzia siku ya tatu ya mwezi wa Jumada al-Thani, ambayo kwa mujibu wa riwaya maarufu ndio siku ya kifo cha bibi Fatima (a.s), [4] siku hii ni siku ya likizo rasmi nchini Iran, [5] ambapo maandamano ya maombolezo hayo hufanyika mitaani nchini humo. [6] Kwa kuwa Mashia wanamchukulia Omar bin Khattab kuwa ndio sababu kuu ya kifo cha bibi Fatima (a.s), katika hadhara za mikutano mingi ya maombolezo hayo, huonekana maneno makali kutolewa na kuelekezwa kwa Omar bin al-Khattab huku wengine wakimlaani kutokana na ukatili wake huo. [7] Hii ndio moja ya sababu ya kupatikana kwa khitilafu na mizozo kati ya Mashia na Masuni. Suala la kifo cha kishahidi cha bibi Fatima (s.a) limefanya baadhi ya Mashia kuita tarehe 9 ya mwezi wa Rabiu al-Awwal, ambayo kwa mujibu wa riwaya fulani ndiyo siku ya kuuawa kwa Omar bin Khatab, kuwa ni Eid al-Zahra (a.s) na kusherehekea siku hiyo kutokana na kuuawa kwa adui yao. [9]

Utafiti wa kihistoria

Mgogoro kuhusu je, bibi Fatima Zahra (a.s) alifariki kwa kifo cha kishahidi au kwa kifo cha kawaida, ni mgogoro wa muda mrefu miongoni mwa wanazuoni wa madhehebu mbali mbali. Kulingana na baadhi ya watafiti, kupitia kitabu kiitwacho al-Tahrish kilichoandikwa na Dharaaru bin Amru, aliyeishi katika karne ya pili Hijiria, imeelezwa ndani yake ya kuwa; Mashia wanaamini kwamba bibi Fatima (a.s) alifariki kutokana na kipigo alichopata kutoka kwa Omar bin Khatab. [10] Pia Abdullah bin Yazid Fazari, mwanathiolojia wa karne ya pili Hijiria, katika kitabu chake al-Rudud, ameashiria imani ya Mashia juu ya Fatima kupata madhara kutoka kwa baadhi ya Masahaba na kupoteza mimba yake. [11] Kulingana na Muhammad Hussein Kashif al-Ghitaa (aliyefariki mnamo mwaka 1373 Hijiria), washairi wa Kishia wa karne ya pili na ya tatu, kama Kumayt Asadiy, Sayyid Himyariy, na Da’abil Khuzai wameandika mashairi yaliyoelezea kwa kina namna ya mateso yaliyompata bibi Fatima (a.s). [12]

Kulingana na maandishi ya Abdul Karim Shahrestani (aliyefariki mwaka 548 Hijiria), ambaye ni mtafiti maarufu wa madhehebu ya Ahlul Sunnah, ni kwamba Ibrahim bin Sayyar anayejulikana kama Nadhaam Muu’tazili (aliyefariki mwaka 221 Hijiria), alikuwa akiamini kuwa Fatima (a.s) alikuwa na mimba tumboni mwake, mimba ambayo iliharibika kutokana na kugongwa na Omar. [13] Kulingana na maelezo ya Shahrestani, imani hii na imani nyingine za Nadhaam Mu’utazili zilisababisha yeye kuwa mbali na wanazuoni wenzake. [14] Qadhi Abdul Jabbar Mu’utazili (aliyefariki mwaka 415 Hjiria) katika kitabu chake Tathbitu Dalailu al-Nubuwwah ametaja ndani ya kitabu chake hicho habari za Imani ya baadhi ya wanazuoni wa Shia wa walioisha katika zama zake huko Misri, Baghdad na maeneo mengine ya Sham ambao walikuwa na kawaida ya kuomboleza siku ya msiba wakilia na kusikitika kutokana na maafa yaliyo mkuta bibi Fatima na mtoto wake Mohsin aliye fariki akiwa tumboni. [15] Katika vitabu vya Ahlul Sunnah, wale ambao wanaamini kwamba Fatima binti wa Mtume (s.a.w.w) amefariki kupitia kipigo cha Omar bin al-Khattab, wamepewa jia la Rafidhi (wapingao ukhalifa wa makhalifa watatu, ambao ni Abu bakar, Omar na Othman). [16]

Kiini cha khitilafu

Mizizi ya khitilafu katika suala la kifo cha kishahidi cha bibi Fatimah (a.s) inatokana na kule kifo chake kutokea mapema mno na muda mfupi tu baada ya kifo cha bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w), kifo ambacho kilitokea wakati wa mvutano juu ya mzozo wa haki ya ukhalifa na urithi wa Ali bin Abi Talib katika kushika nafsi hiyo ya ukhalifa baada ya Mtume (s.a.w.w). Baada ya kundi la Muhajirin na Ansar kumwapisha Abu Bakar wakiwa katika mkusanyiko uliofanyika kwenye banda Saqifah la Bani Sa’aidah, kundi la masahaba wengine walikataa kumwapisha Abu Bakr na kumtambua kama ni khalifa, hii ni kwa kuzingatia maagizo ya bwana Mtume (s.a.w.w) juu ya haki ya Ali bin Abi Talib (a.s), ya kushika nafasi ya ukhalifa na urithi wa bwana Mtume (s.a.w.w). Hiyo ndiyo sababu khasa iliyo mfanya Abu Bakr na Omar bin Khattab wakiambatana na masahaba wengine, kwenda nyumbani kwa Ali (a.s) kwa ajili ya kumlazimisha awape kiapo cha utiifu na kumtatambua Abu Bakar kama ni khalifa halali. Katika purukushani hizo Omar alimtishia Ali na kumwambia kwamba; ikiwa hatafanya atakataa kutoa kiapo hicho, yeye (Omar) atachukua hatua ya kuchoma moto nyumba ya bibi Fatimah (a.s) pamoja na wakaazi waliomo ndani yake. [17] Katika kipindi na muhula huu huu wa fazaa, bibi Fatimah (a.s) alikwenda kukutana na Abu Bakar na kutoa malalamiko yake dhidi ya tendo la khalifa huyo la kumyang’anya bibi Fatima (a.s) bustani ya Fadak, na kumtaka airudishe bustani hiyo kwa wahusika wake. [18] Baada ya serikali ya ukhalifa huo kukataa kuirudisha bustani hiyo kwa bibi Fatima (a.s), [19] yeye (bibi Fatimah (a.s)) alikwenda kwenye Msikiti wa Madina akatoa hotuba kali ya malalamiko msikitini humo.

Vyanzo vya Shia vinaonesha ya kwamba; kwa kiasi kikubwa mno Mashia wanakubaliana kuwa mimba ya mtoto wa bibi Fatimah (a.s) (Mohsin), iliharibika kutokana na shambulio lililo fanyika kwenye nyumba yake, katika harakati za shindikizo la Omar na wafuasi wake la kumtaka Ali (a.s) kumtambau Abu Bakar kama ni khalifa. [20] Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo vya Sunni, mtoto huyo alizaliwa hai na kufariki akiwa utotoni. [21] Hata hivyo, Ibn Abi al-Hadid al-Mu’utazili (aliyefariki mwaka 656 Hijiria), mfasiri wa Nahjul Balagha, katika majadiliano yaliopita baina yake na mwalimu wake (Abu Jafar Naqibu), amekihusisha kifo cha mtoto huyo na vuguvugu la kuchukua kiapo kutoka kwa Ali (a.s). [22] Pia Ibrahima bin Sayyaar, maarufu kwa jina la Nadhim Mu’utazili (aliyefariki mwaka 221 Hijiria), anasadikiwa kuwa na imani hii. [23]

Kulingana na ripoti nyingi ni kwamba; Fatima alizikwa usiku, [24] na kwa mujibu wa maoni ya Yusuf Gharawi, mwanahistoria wa karne ya 15, mazishi haya yalifanyika kulingana na wasia wa Fatima Zahra (a.s), [25] hii ni kwa sababu -kama ilivyoelezwa katika hadithi kadhaa- bibi Fatima hakupenda wale waliomdhulumu washiriki kwenye mazishi yake. [26]

Vyanzo na vielelezo vya Mashia katika kuthibitisha jinai dhidi ya bibi Fatima (a.s)

Waislamu wa Shia wanaamini ya kwamba bibi Fatima (a.s) amekufa shahidi, imani imeegemea kwenye Hadhithi itokayo kwa Imamu Kadhim (a.s), ambamo ndani yake Fatima Zahra (a.s) amepewa wasifu wa Siddiqatu al-Shahidah (mkweli aliye uawa shahidi).[27] Tabari naye pia amenukuu Hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) katika kitabu chake Dalail al-Imama isemayo kwamba; sababu ya kifo cha bibi Fatima Zahra (a.s) ilitokana na kuharibika kwa mimba yake kutokana na kupigwa. [28] Kulingana na hadithi hii, pigo hilo lilitekelezwa na Kunfudh (mtumwa wa Omar), kupitia amri yake. [29] Kulingana na hadithi nyingine iliyonukuliwa katika kitabu kijulikanacho kwa jina la Nahjul Balagha, Imamu Ali (a.s) amezungumzia suala la kundi la Waislamu (baadhi ya masahaba) walio shikamana katika kumdhulumu bibi Fatima Zahra (a.s). [30]

Mirza Jawad Tabrizi, mmoja wa wanazuoni wa Kishia wa karne ya kumi na tano Hijiria, ameorodhesha vielelezo mbali mbali katika jitihada zake za kuthibitisha tukio hili. Miomngoni mwa yaliomo katika orodha hiyo ni; maneno ya Imam Ali (a.s) wakati wa mazishi ya Fatima (a.s), Hadithi ya Imam Kadhim (a.s), hadithi ya Imam Swadiq (a.s) iliyoko katika kitabu Dalail al-Imama, kufichika kwa kaburi la bibi Fatima (a.s) pamoja na wasia wake wa mazishi ya usiku. Ametoa vielelezo hizi kama ni sehemu ya hoja za kuthibitisha tukio la kudhulumiwa na kufa kishahidi kwa bibi Fatima (a.s). [31]

Vyanzo vya kishia

Katika kitabu kinacho tambulikana kwa jina la al-Hujumu, kilichoandikwa na Abdulzahra Mahdi, ambaye ni mwandishi wa karne ya 15, kuna idadi ya Hadithi na rikodi za kihistoria zipatazo 260 kutoka kwa zaidi ya waandishi na wapokezi wa Hadithi 150 wa Shia, kila moja kati ya rikodi hizo ikinukuu sababu maalumu ya kifo cha bibi Fatima Zahra (a.s); kama vile shambulio dhidi ya nyumba ya Fatima (a.s), kukuharibiwa kwa mimba ya mtoto wake tumboni, kumpiga na kumchapa kwake kibao. [32] Chanzo kikongwe zaidi kinachotumiwa na waandishi wa Shia ni kitabu cha Salim bin Qais, aliye fariki mnamo mwaka wa 90 Hijiria. [33] Kulingana na maelezo ya Sheikh Tusi (aliyofariki mwaka 460 Hijiria) katika kitabu chake Talkhisu al-Shaafi, Shia hawana tofauti ya kwamba Omar ndiye aliye mpiga bibi Fatima (a.s) kwenye sehemu ya tumbo lake, na kusababisha mimba yake kuharibika, [34] na hadithi za Shia kuhusu hii ni nyingi mno. [35]

Shia wanavyorejelea na kunukuu katika vyanzo vya Sunni

Ili kuthibitisha baadhi ya matukio yaliyopelekea kifo cha kishahidi kwa bibi Fatima Zahra (s.a.w.w), Mashia wametaja na kunukuu vyanzo vingi vya Hadithi na vitabu vya kihistoria na hata kifiqhi kutoka katika madhehebu ya Sunni. Kwa mfano, kitabu Shambulio la Nyumba ya Ali ya Fatima (الهجوم علی بیت فاطمه) mwandisi wa kitabu hichi amejaribu kukusanya vyanzo vya Kisunni katika mkusanyo mmoja kisha kuuweka mkusanyo wake huo wa vyanzo vya vitabu vya Kisunni juu ya shambulio la nyumba ya Fatimah katika kitabu kimoja. Yeye aliweza kuorodhesha wasimulizi na waandishi wapatao 84 kitabuni mwake humo. [36] Chanzo kikongwe zaidi katika orodha hii ni a kitabu kiitwacho Al-Maghazi kilichoandikwa na Mussa bin Uqbah (aliye fariki mwaka wa 141 Hijiria). [37]

Hussein Ghaib Ghulami (aliyezaliwa mwaka 1338 Shamsia) pia amekusanya zaidi ya riwaya 20 kutoka katika vitabu na wasimulizi wa Kisunni katika kitabu chake kiitwacho Ihraqu Bayti Fatima fi al-Kutubu al-Mutabara ‘Inda Ahli al-Sunnah (إحراقُ بیت فاطمة فی الکتب المعتبرة عند أهل السنة) [38]. Riwaya ya mwanzo kitabuni humo ni kutoka katika kitabu kiitwacho al-Musannif cha Ibnu Abi Shaiba (aliye fariki mwaka 235 Hijiria), [39] na nukuu ya mwisho kitabuni humo, ni nukuu itokayo katika kitabu kiitwacho Kanzu al-Umal kilichoandikwa na Mutaghi Hindi (aliyefariki mwaka 977 Hijiria) [40] Pia, katika kitabu kiitwacho Ushahidi wa mama yangu Zahra sio hadithi za Paukwa Pakawa (شهادت مادرم زهرا افسانه نیست), ndani yake mmenukuliwa kisa cha kushambuliwa kwa nyumba ya Fatimah ni kutoka katika vyanzo 18 vya Kisunni. [41] Vyanzo hivi kutoka upande wa Kisunni, kwa namna mmoja au nyengine vimesimulia kisa cha kujaribu kuchukua kiapo cha utiifu kutoka kwa Imam Ali (a.s) kwa nguvu na kutishia kuichoma moto nyumba ya bibi Fatima katika siku hiyo. [42]

Baadhi ya maswali kuhusu tukio

Je, nyumba za Madina kweli zilikuwa hazina milango?

Kuna baadhi walio sema kwamba huko Madina wakati huo, nyumba zao hazikuwa na milango, [44] na kupitia dhana hiyo wao wamehitimisha kwa kusema kwamba;  Hadithi ya kuchomwa moto mlango wa nyumba ya bibi Fatimah haiwezi kuwa ni sahihi, kwa sababu yeye alikuwa akiishi katika nyumba isiyo na mlango. Kwa upande mwingine, Jafar Murtadha alitaja vyanzo kadhaa katika kitabu chake Maasatu al-Zahra (مأساة الزهراء), ambapo kulingana na vyanzo hivyo ni kwamba; ilikuwa ni jambo la kawaida kwa nyumba za wakati huo kuwa na milango. Kwa hiyo hata nyumba ya bibi Fatima pia ilikuwa na mlango. [45]

Ni kwa nini Ali na wengine hawakutetea na kuepusha fitna?

Moja ya maswali kuhusu tukio la kushambuliwa kwa nyumba ya bibi Fatima (a.s) na kuuawa kwake kishahidi, ni madai yasemayo kwamba; ni kwa nini Ali (a.s), ambaye anajulikana kwa ushujaa wake, pamoja na masahaba wengine walinyamaza kimya katika tukio hili na hawakuitetea wala kuingilia kati na kumwokoa bibi Fatimah? [46] Mbali na Masunni, hata Muhammad Hussein Kashif al-Ghita, ambaye ni mmoja wa wakuu wa wanazuoni wenye mamlaka na uwezo wa kutoa fat'wa kutoka upande wa madhehebu ya Kishia aliyeishi karne ya 14, pia naye amezusha swali kama hilo. [47] Jibu kuu la Mashia kwa nukta hii ni kwamba; Ali (a.s) aliamrishwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w) kudumisha subira na Kukawa kimya kwa manufaa ya umma wa Kiislamu. [48] [Maelezo 1]. Katika baadhi ya mashairi ya washairi mbali mbali, pia kuna beti zinazoashiria wasia wa Mtume (s.a.w.w) wa kumtaka Ali (a.s) kuwa na subira katika matukio ya baadae. Miongoni mwa washairi hao ni Sayyid Redha Hindi, aliye sema katika beti za shairi lake maarufu liitwalo (Qasiidatu Ra'iyyah) kama ifuatavyo:

لو لم تُؤمَر بالصبر و کظم          الغیظ ولَیْتَک لم تؤمر

ما نال الامرَ اخوتیم                 و لا تناوله منه حبتر



Lau usinge amrishwa kuwa na subira na kuzuia hasira yako, kama ingeamrishwa kufanya hivyo, basi Ukhalifa usingemfikia Akhu Tayyimu (Abu Bakar) wala Abu Habtari (Omar). [26]

Zaidi ya hayo, pia kuna riwaya kutoka kwa Salman Farsi iliyoko katika kitabu cha Sulaim (ambapo kaungana na maoni ya Yusuf Gharawi; hii ndiyo riwaya imara zaidi kuhusiana na tukuio la kuvamiwa kwa nyumba ya Ali). Kulingana na riwaya hii; baada ya Omar kumshambuia bibi Fatima, Imamu Ali alimwingia mwilini na kumlaza chini, kiasi ya kwamba ilionekana kama vile anataka kummaliza. Katika pirika hizo Imamu Ali (a.s) alimwambia Omar; Wewe mwenyewe unajua ya kwamba, laiti kama nisingekuwa na ahadi baina yangu na Mtume (s.a.w.w), basi usingeweza kuingia ndani ya nyumba yangu. Katika hali hiyo Omar aliamua kuomba msaada kutoka kwa wafuasi wake, ambapo walimvamia Ali (a.s) na kumpapatua Omar kutoka mikononi mwa Ali (a.s). [50]

Tuhuma katika kuharibika kwa mimba kwa Mohsen

Hata hivyo kuna kundi la waandishi wa upande wa Masunni ambao wana shaka na tukio la kuharibika kwa mimba changa ya Mohsin bin Ali (a.s) katika tukio la siku ya kuchukua kiapo cha utiifu kutoka kwa Ali (a.s). Wao wanaamini kwamba; mtoto huyu alizaliwa kabla ya siku hii na kufariki akiwa bado ni mchanga. [51] Ila wengi wa Shia wanaamini kwamba; mimba ya mtoto huyo iliharibika katika tukio la shambulio dhidi ya nyumba ya Ali (a.s) kupitia pigo alilopata bibi Fatima katika heka heka hizo. [52] Ni idadi chache tu ya vyanzo vya Masunni vilivyo elezea waziwazi kuharibika kwa mimba au kuharibiwa kwa mimba ya Mohsin. [53] Mwandishi wa kitabu (المحسن السبط مولود أم سقط) Je, Muhsin ni Mjukuu aliyezaliwa au ni Mimba Iliyo Haribika katika sura ya tatu kitabuni mwake, baada ya kuchunguza na kulinganisha maandishi ya kihistoria kupitia vyanzo mbali mbali, amehitimisha kwa natija isemayo kwamba; tukio la kuharibika kwa mimba ya Mohsin bin Ali lilitokea siku ya shambulio dhidi ya nyumba ya Ali kupitia pigo na shinikizo la wavamizi wa nyumba hiyo dhidi ya bibi Fatima (a.s). [54]                                  

Kuto kutajwa kwa suala la kuchoma moto kwa nyumba katika vyanzo vya kihistoria

Moja ya maswali yenye ukungu katika Hadithi na riwaya zinazo zungumzia tukio la kufa shahidi kwa bibi Fatima (a.s) ni kule kunukuliwa kwa tukio hilo katika vitabu vingi vya kihistoria na hadithi za Masunni vilivyo nukuu vitisho tu vya kuchoma moto nyumba ya bibi Fatima bila ya kubainishwa kutokea kwa vitendo hicho. [55] Hata hivyo, watafiti wamekusanya vyanzo kadhaa vinavyothibitisha asili ya tukio la shambulio hilo; ikiwa ni pamoja na kitabu kiitwacho Al-Hujumu ‘Alaa Bayti Fatima, [56] na kitabu Ihraqu Bayti Fatima. [57] Katika baadhi ya vyanzo hivi, imeelezwa waziwazi kuhusu kupigwa kwa bibi Fatima (a.s), kuingia kwa wavamizi hao ndani ya nyumba yake pamoja na kuharibika kwa mimba yake kupitia uvamizi huo. [58]

Kundi la waandishi wa upande wa madhehebu ya Kisunni limetia shaka kuhusu uhalali wa hati za maandishi haya ya kihistoria. [59] Lakini katika baadhi ya pingamizi zao hazina hati madhubuti za kuweza kutetea pingamizi hizo; kwa mfano, al-Muda'ihish, mwandishi wa Kisunni (Muwahabi) wa kitabu Fatima bint al-Nabi, amepuuza kabisa Hadithi ilioko katika kitabu Tarikh Ya'aqubi kwa visingizio kwamba; mwandishi wake ni mrafidhi (Mshia) na kwamba kitabu chake hakithaminiwi kielimu. [60] Pia Hadithi ya Ibnu 'Abdi al-Rabbi ilioko katika kitabu al-'Iqdu al-Farid ameikataa bila ya kuwa hoja wala hati madhubuti katika kusimamisha pingamizi zake. Yeye ameisifu Hadithi kuwa ni Hadithi inayo kataliwa. Pia amemtilia shaka mwandhishi wake kwa kudai kuwa; yeye pia yawezekana kuwa ni Shia, na kusema kuwa jambo hili linapaswa kuchunguzwa. [61] Mwandishi huyu pia anapuuuza nukuu za Hadithi za kitabu al-Imamatu wa al-Siyasah kwa madai ya kwamba mwandishi wake si Ibn Qutaybah Dinawari. [62] Mudaihish amekanusha na kukataa nukuu za wale walio nukuu kutoka kitabu Nahju al-Balagha kisa cha uvamizi wa nyumba ya bibi Fatima (a.s), amekanusha nukuu hizo kwa madai ya kitabu Nahjul Balagha hakihusiani na Imamu Ali (a.s). [63] Hata hivyo, waandishiwengi wa Kisunni hawakuweza kukanusha tukio hili moja kwa moja, angalau wao wanakubaliana tukio la kukusanyika kwa baadhi ya Masahaba mbele ya numba ya bibi Fatima (a.s) na kutoa vitisho dhidi ya wakaazi wliomo nyumbani humo. Hii ni kwa sababu ya wingi wa Hadithi zilizosimuliwa kuhusiana na vitisho hivyo. [64]

Kuabiriwa tukio la kifo cha bibi Fatima (a.s) kwa kutumia neno kifo

Moja ya hoja za wapinzani wa imani juu ya mauaji ya bibi Fatima Zahra (a.s) ni kwamba; katika vyanzo vya kale vya Shia, neno kifo ndilo lililo kuwa likitumika katika kuelezea kifo chake, na sio neno shahidi ambalo lina maana ya kuuawa. Kundi la waandishi wa Shia wamejibu kwamba neno kifo katika lugha ya Kiarabu lina maana pana ambayo inajumuisha kifo cha kawaida na kifo kinachosababishwa na sababu nyingine, kama vile kufa kwa sumu kupitia kwa mtu wengine. Kwa mfano, katika makala inayo zungumzia Mauaji au Kifo cha Bi Fatima (a.s), mifano ya matumizi haya imeonyeshwa kwa wazi kabisa. Pia katika baadhi ya vyanzo vya kihistoria vya Sunni katika kuzungumzia tukio la kifo cha Omar na Othman, walitumia neno kifo, ingawa wote wawili waliuawa. [65] Hata Tabari, mahali fulani alitumia neno kifo alipo kuwa akiashiria tukio la mauaji ya Imam Hussein (a.s). [66]

Mahusiano Mazuri Baina ya Imam Ali (a.s.) na Makhalifa

Sababu nyengine ya Waislamu wa Sunni ya kukanusha mauaji ya bibi Fatima Zahra (s.a) zimetegemea kwenye uhusiano wa karibu kati ya Makhalifa na Imam Ali (a.s) pamoja na familia yake. Katika kitabu chenye maelezo marefu juu ya maisha ya bibi Fatima kiitwacho Fatiha Binti Nabii, mwandishi amejaribu kuonyesha kwamba Khalifa wa kwanza na wa pili walikuwa na mapenzi makubwa kwa bibi Fatima Zahra (a.s), [67] lakini hata hivyo, mwandishi katika muhtasari anabainisha kwamba Fatima baada ya tukio la Fadak alikatiza mawasiliano yake na Abubakar na hakumpa kiapo cha utiifu cha kumtambua kama yeye ni khalifa. [68] Muhammad Naafi mmoja wa waandishi wa Sunni aliye andika kitabu alicho kiita Wenye Rehema baina yao (رحماء بینهم), ndani yake amejaribu kuonyesha kwamba; Makhalifa Watatu walikuwa na uhusiano mzuri na Ali. [69] Pia katika makala ya jarida la Nidaul-Islam, mwandishi kwa kunukuu matukio juu ya uhusiano kati ya Makhalifa na Imam Ali (a.s) na pia uhusiano uliopo kati ya wake zao na mabinti zao na Fatima (a.s), amejaribu kuonyesha kwamba; uhusiano huu haulingani na hasira za bibi Fatima na upinzani wake dhidi yao. [70] Kulingana na Sayyid Murtadha (aliye fariki mwaka 436 Hijiria) ambaye ni mwanathiolojia wa Shia, ni kwamba; haiwezekani kuutegemea ushirikiano wake na wao na kuutumia kama ni hoja ya kuwepo kwa uhusiano mwema baina yao, kwa kuwa Imam Ali (a.s) alitoa ushauri huo kwa ajili ya kuweka wazi sheria za kiungu na kwa manufaa ya Waislamu, jambo ambalo ni wajibu wa kila mwanazuoni. [71] Pia mwandishi wa kitabu Encyclopedia of Political Relations of Ali (a.s.) with the Caliphs (دانشنامه روابط سیاسی حضرت علی(ع) با خلفاء), baada ya kuchunguza matukio 107 ya ushauri wa Imam Ali (a.s) na Makhalifa Watatu, alifikia kwenye hitimisho lisemalo kwamba; ushauri ulio kuwa ukifanyika kati ya Makhalifa na Imam Ali (a.s), si ishara ya uelewano na kukubaliana kwake na Makhalifa hao. Hii ni kwa sababu ya kwamba ushauri kama huo ulikuwa ukitendeka kama ni ushauri wa shirikisho la umma katika kusaidia mawazo ya kusogeza mbele gurudumu la maendeleo ya umma wa Kiislamu, na sio kwamba Makhalifa walimfanya Ali (a.s) kuwa ni waziri au mshauri wao maalumu, bali Ali (a.s) katika hali ya kutengwa kwake kisiasa, alikuwa akijishughulisha na kilimo na kuchimba visima. Kwa hiyo kama kuna baadhi ya masuala ambayo Makhalifa waliyapeleka kwa Ali (a.s) ili kupata ufumbuzi wake, hilo lililotokana na wao kulazimika kufanya hivyo, kwa ajili ya kutatua tata zilizo kuwa zikiwakabili katika kujibu mahitaji ya jamii ya Kiislamu. [72]

Ndoa ya binti ya Imam Ali Umm Kulthum na Khalifa wa pili ni mfano mwingine unaotumika katika kuthibitisha urafiki na mapenzi ya Omar kwa Ahlul Bayt, ambapo jambo hili linapingana na uhusikanaji wake na mauaji ya bibi Fatima (a.s). [73] Baadhi ya waandishi wanakanusha kuthibi kwa ndoa hii. [74] Sayyid Murtadha anaiona ya kwamba, ndoa hii ilifanyika chini ya shinikizo na vitisho [75], jambo ambalo haliwezi kuwa ni dalili ya kuwepo kwa uhusiano wa karibu kati ya watu wawili hawa. [76] Pia kuna Hadithi kutoka kwa Imamu Ja'far as-Sadiq (a.s) ambayo hutumika katika kuthibitisha kuwepo kwa shinikizo katika ndoa hii, hii ni kwa kuwa imeisifu ndoa hii kutumia neno kuchukuwa kwa mabavu. [77] [Maelezo 2].

Watoto wa Ahlul Bayt kupewa majina ya Makhalifa

Kundi la Waislamu wa Sunni wanasisitiza kwamba kwa kuwa Imam Ali (a.s) aliwapa watoto wake majina ya Makhalifa, basi hiyo ni dalili ya kuwa yeye alikuwa ana mapenzi na Makhalifa hao. [78] Hii hutumiwa kama ndio hoja ya kukanusha madai ya kuuawa kwa Bibi Fatima (a.s) kupitia sindikizo la Makhalifa. Mada hii pia imeelezwa katika kitabu kidogo kinachoitwa Maswali ambayo yanawaongoza vijana wa Shia kwenye ukweli (اسئلة قادت شباب الشیعة الی الحق). [79]

Sayyid Ali al-Shahristani (aliyezaliwa mwaka 1938 Shamsia) mwandishi wa kitabu kiitwacho Ufafanuzi  kati ya uvumilivu wa Maalawi (Ahlulbait) na utumiaji wa Fursa Maamawi (التسميات بین التسامح العلوی و التوظیف الاموی), ametoa uchambuzi wa kina juu ya upewaji wa majina kwa watoto walioishi katika karne ya kwanza ya Uislamu hadi karne zilizofuata baadae, ambapo ametaja nukta 29 kuu kitabuni humo, kisha akahitimisha kwa hitimisho lisemalo kwamba; aina hii ya upewaji majina hayawezi kuonyesha uhusiano mzuri kati ya watu, kama vile kuto tumia majina hayo pia hakuwezi kuwa ni ishara ya uadui baina yao. [80] Kwa sababu majina kama haya yalitumika kabla na baada ya maisha ya Makhalifa hao. [81] Kwa upande mwingine, kulingana na Hadithi kutoka kwa Khalifa wa pili, ni kwamba; Imam Ali (a.s) alimchukulia kuwa mwongo na msaliti, [82] hata hivyo jina Abu Bakr kimsingi si jina la mtu maalum bali ni jina la umashuhuri (kunia), na kimsingi mtu hawezi kuchagua jina la umaarufu na kumpa mtoto wake. [83]

Ibn Taymiyyah al-Harrani (aliyezaliwa mwaka 728 Hijria), mwanazuoni mashuhuri wa Kiwahabi, pia anaamini kwamba kumwita mwanawe kwa jina la mtu fulani, si ushahidi wa kumpenda mtu huyo, kwani Mtume (s.a.w.w) na Masahaba zake, walitumia majina ya makafiri. [84] Kulingana na maelezo ya Sayyid Ali al-Shahristani ni kwamba; pia kuna vitabu vyengine viwili kuhusiana kupewa watoto majina ya Makhalifa, moja ya vitabu hivyo kimeandikwa na Wahid al-Bahbahani (aliyezaliwa mwaka 1125 Hijiria) na cha pili kimeandikwa na Tunkabuni (aliyezaliwa mwaka 1202 Hijria), ambaye ni mwandishi wa kitabu maarufu kiitwacho Qisas al-Ulama. [85]

Vitabu vilivyo andikwa kuhusiana na mada hii

Kuna vitabu makhusi vilivyo andikwa juu ya kuuawa kwa Bibi Fatima (a.s), miongoni mwavyo ni pamoja na:

  • Baitu al-Ahzan fii Masaaibi Sayyidatu al-Niswani (بیت الاحزان فی مصائب سیدة النسوان), kilicho meandikwa na Sheikh Abbas Qummi kwa lugha ya Kiarabu mnamo mwaka 1330 Hijiria. Katika moja ya sehemu za kitabu, kumeripotiwa matukio yaliyohusiana na maisha ya Fatima (a.s) baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w), pamoja na matukio ya kuuawa kwake. [86] Kitabu hichi kimetafsiriwa kwa Kiajemi kwa jina Ranjhaa wa Faryadhaaye Fatimeh (a.s).
  • Ma’asaatu al-Zahraa (a.s) (مَأساةُ الزّهراء(س)، شُبَهات و رُدود), kilicho andikwa na Sayyid Ja'far al-Musawi al-Madani kwa lugha ya Kiarabu mnamo mwaka 1441 Hijiri. Mwandishi katika kitabu hichi amejaribu kujibu shaka na tata zilizoko juu ya matukio ya mwisho wa maisha ya bibi Fatima Zahra (a.s) na kuuawa kwake. Kitabu hichi kimefasiriwa kwa Kiajemi kwa jina Ranjhaye Hadhrate Fatimeh Salamu Llahi Alaiha.
  • Alhujuum (الهجوم), kilichoandikwa na Abdulzahra Mahdi, mwandishi wa karne ya 15, kitabu ambacho kimekusanya ndani yake Hadithi na Riwaya za kihistoria kutoka kwa zaidi ya wasimulizi na waandishi 150 wa Shia, ambapo kila moja kati yazo inataja baadhi ya sababu za kuuawa kwa bibi Fatima Zahra (a.s). [87]

Pia, waandishi wa Sunni nao wameandika vitabu kwa lengo la kuonyesha uhusiano mzuri kati ya Makhalifa na Ahlul Bayt (a.s) na kukanusha kuuawa kwa bibi Fatima (a.s). Baadhi ya vitabu hivi ni pamoja na:

  • Fatimatu al-Zahraa Bintu Rasulillahi wa Ummu al-Hasanaini (فاطمه الزهراء بنت رسول الله و ام الحسنین) kilichoandikwa na Abdul-Sattar al-Sheikh. Kitabu hichi ni sehemu ya seti kubwa ya vitabu vinavyoelezea juu ya maisha ya watu muhimu kutoka katika jamii za Kiislamu. Kitabu hichi kinahusiana na maisha ya Bibi Fatima (a.s). Ila mwandishi wa kitabu hichi hakuzungumzia matukio yaliyotokea siku ya vugu vugu la kutaka kuchukua kiapo cha kumtambua Abu Bakar kama ni Khalifa, na kutiwa moto kwa nyumba ya bibi Fatima (a.s). Badala yake, mwandishi ameashiria tu khitilafu juu ya bustani ya Fadak, chini ya kichwa cha habari kisemacho; Urithi wa Mtume (میراث النبی). Hatima yake mwandishi huyu alifikia natija ya kudai kwamba; hakukuwa na khitilafu yoyote ile kati ya bibi Fatima (a.s) na Abu Bakr kuhusiana na ardhi ya Fadak, [88] na kwamba bibi Fatima (a.s) hakuwahi kumkasirikia wa Khalifa wa kwanza wala Khalifa wa pili. Mwandishi pia amedai kwamba; Hadithi kuhusu bibi Fatima (a.s) kutozungumza na Makhalifa wa kwanza na wa pili ni nadharia iliyo buniwa na mnukuu wa Hadithi. Bali kwa madai yake, ni uvumi uliotengenezwa na wanachuoni wa Kishia. [90]
  • Baina al-Zahraa wa al-Siddiqi Haqiiqatun wa Tahqiiqun (بین الزهراء و الصدیق حقیقة و تحقیق) (Kati ya Bibi Fatima na Abu Bakr Ukweli na Utafiti) kilichoandikwa na Badru al-Omari. Kitabu hichi kilichapishwa mwaka wa 2014, na ni juu ya uhusiano kati ya Abu Bakr, Khalifa wa kwanza, na bibi ]]Fatima (a.s)]]. [91]
  • Difa’an ani al-Aali wa al-As’habu (دفاعاً عن الآل و الاصحاب) (Utetezi Juu ya Ahlul Bayt na Masahaba) kilichoandikwa na mwandishi asiyejulikana. Kitabu hichi, kilichochapishwa na Jam’iyyatu Ahlul Bayt wa al-Ashabi mnamo mwaka wa 1431 Hijiria nchini Bahrain. [92] Maudhui ya kitabu hichi yamejikita kwenye jumla ya majibu dhidi ya tata na ukosoaji unao elekezwa juu ya imani za Kisunni. Sehemu za kitabu hichi pia zinahusiana maudhui ya kuuawa kwa Bibi Fatima (a.s). [93]

Maelezo

  1. Kwa mujibu wa Hadithi iliyotajwa katika kitabu cha al-Kafi, ni kwamba; Ali (a.s) aliahidi mbele ya Mtume (s.a.w.w) kwamba atakuwa ni mvumilivu mbele ya udhalimu utakao fuatia baada ya kifo cha bwana Mtume (s.a.w.w), na kuvumilia dhidi uvunjwaji wa heshima yake na kutuliza hasira yake (Kulayni, Kafi, vol. 1, ukurasa wa 281 hadi 282)
  2. Kwa hakika yeye alikuwa ni mke aliye chukuliwa kwa mabavu kutoka kwetu (إِنَّ ذَلِكَ فَرْجٌ غُصِبْنَاهُ‌)