Kurejea kwa Nabii Isa (a.s)
Kurejea kwa Nabii Isa (a.s): ni miongoni mwa matukio ya yakini na yasiyopingika, ambalo litatokea katika kipindi cha kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.s). Waislamu pamoja na Wakristo duniani wanaamini katika kurejea kwa Nabii Isa katika kipindi cha mwisho wa dunia. Hili limetajwa mara kadhaa ndani ya Injili, huku baadhi ya wafasiri wa Qur’ani wakiamini kuwa; Aya fulani za Qur’ani zinabashiria kurejea kwa Nabii Isa (a.s) katika zama za hizo za mwisho. Kuna Riwaya katika vyanzo vya Kishia kuhusiana na lengo hasa la kurudi kwa Nabii Isa (a.s). Kwa mujibu wa Riwaya hizo ni kwamba; Sababu kuu ya kurejea kwa Nabii Isa (a.s) ni kutoa msaada kwa Imamu Mahdi (a.f). Kwa upande wa madhehebu ya Kisunni, Riwaya zinasema kwamba; Pale Nabii Isa (a.s) atakaporejea tena duniani humu, atajitambulisha kama msaidizi mkuu wa Imamu Mahdi (a.f). Vyanzo vya Kishia pamoja na Kisunni vimetaja maeneo mbalimbali yanayotarajiwa kuwa, moja wapo ndio eneo atakalolitumia katika kurejea kwake, yakiwemo Makka, Damaskasi na Baytul Maqdis. Kwa mujibu wa hadithi nyingi (mustafidhu) zilizopokelewa kutoka kwa Mashia na Masunni, ni kwamba; Plae Nabii Isa (a.s) atakaporejea duniani humu, yeye atakuwa ni mfwasi atakayesali sala zake nyuma ya Imamu wa Kumi na Mbili wa Waislamu wa Kishia. Baadhi ya mapokezi (Hadithi), yameonekana kuyahusisha tukio baadhi ya matukio ya zama za mwisho wa dunia na Nabii Isa (a.s), miongoni mwayo ni pamoja na; kuuawa kwa Dajjal pamoja na kuangamizwa kwa Yajuj na Majuj. Hata hivyo, Najmuddin Tabasi, mmoja wa watafiti wa Hawza (chuo cha kidini), anaamini kuwa; Bani Umayyah, ambao ni watu wenye chuki dhidi ya Ahlul-Bayt (a.s), ndiwo waliojaribu kupandikiza fikra tofauti ili kumshusha hadi Imamu Mahdi (a.f). Kwa imani yake yeye, miongoni yale yalipandokizwa na Bani Umayyah, ni hili suala la kumhusisha Nabii Isa (a.s) na matukio mawili haya, ambapo walifanya hivyo ili kumwonesha kuwa Nabii Isa (a.s) ndiye Mahdi mtarajiwa. Kuna vitabu na makala mbalimbali vimeandikwa juu ya kurejea kwa Isa (a.s), ikiwa ni pamoja na "Kushuka kwa Masihi na Kuonekana kwa Aliyeahidiwa" (miratibu: Mirtaqi Hosseini Gorgani), na "Nafasi ya Nabii Isa (a.s) katika Serikali ya Mahdi" kilichoandikwa na Majid Yaqubzadeh. Umuhimu na Hadhi ya Kurejea kwa Nabii Isa (a.s) Kurudi kwa Nabii Isa (a.s) kunachukuliwa kuwa moja ya matukio thabiti na yasiyo na shaka katika zama za kudhihiri kwa Imamu Mahdi (a.f). [1] Ingawa bado kuna mjadala kati ya wanazuoni wa Kiislamu kwamba je Isa (a.s) alifariki au anaendelea kuishi hadi sasa? Mitazamo mingi inaelekea kuunga mkono dhana ya kwamba yeye yuko hai na naendelea kushi hadi sasa. [2] Katika Asr al-Zuhur, Ali Korani ambaye ni mmoja wa wanazuoni wa Kishia, anajaribu kusisitiza kuwa kurejea kwa Isa (a.s) kutakakotokea wakati wa kudhihiri kwa Mahdi, ni moja ya dhana yenye maridhiano ya pamoja kati ya Waislamu wote ulimwenguni. [3] Watafiti wengine wanaongeza kusema kwamba; mitazamo kama hiyo haipo tu kwa Waislamu, bali hata Wakristo pia nao wanashirikiana na Waislamu katika nadharia hii, [4] huku watofauti yao ikiwa ni kwamba; Ukristo unamuona Nabii Isa (a.s) kuwa yeye mwenyewe ndiye mkombozi aliyeahidiwa, hali ambayo ni tofauti kabisa na mtazamo wa Kiislamu unaomtaja Mahdi (a.s) kama mkombozi, na Isa akiwa ni msaidizi wake. [5] Tukirejea katika vyanzo vya Riwaya, tutakuta vyanzo vya Kisunni vinanukuu takriban Riwaya 28 kuhusiana na kushuka kwa Nabii Isa (a.s), [6] huku vyanzo vya Kishia vikitaja karibu Riwaya 30 kuhusiana na jambo hilo. [7] Kwa mujibu wa maelezo ya mfasiri mkubwa wa Qur’ani ajulikanaye kwa jina la Sayyid Muhammad Hussein Tabatabai yaliopo katika kitabu chake al-Mizan, ni kwamba; Riwaya hizi zilizonukuliwa kuhusiana na kuja kwa Nabii Isa (a.s), ni Riwaye zilizotiririka hadi kufikia kiwango cha mustafidh, yaani ni Riwara zenye idadi kubwa mno katika muktadha huo. [8]
Kurejea kwa Nabii Isa (a.s) Kulingana na Maandiko ya Vitabu vya Mbinguni Baadhi ya wafasiri wa Qur'ani Tukufu wakiifasiri Aya ya 46 ya Surat Aal-Imran na Aya ya 159 ya Surat An-Nisaa wamejaribu kuzihusisha Aya mbili hizo na tukio la kurejea kwa Nabii Isa (a.s) linalotarajiwi kujiri wakati wa kudhihiri kwa Imamu Mahdi (a.f). Pia Katika maandiko yaliomo ndani ya Injili, kuna sehemu nyingi zinazosisitiza na kuleza wazi kabisa juu ya tukio hili la kurejea kwa Isa (a.s), likitajwa kuwa ni tukio la mwisho kabla ya kusimama kwa hukumu ya Mwenye Ezi Mungu.
Aya ya 46 ya Surah Aal-Imran na Utabiri wa Kurejea kwa Nabii Isa (a.s) Kulingana na maelezo ya Nasir Makarim Shirazi, mwandishi wa tafsiri ya Qur’ani ijulikanayo kwa jina la Tafsir-Namuneh, ni kwamba; kuna uwezekano wa kuwa ile Aya inayosema “وَ یُکَلِّمُ النَّاسَ فِی الْمَهْدِ وَ کَهْلًا وَ مِنَ الصَّالِحِینَ” (Na atazungumza na watu akiwa bado ni mtoto wa kubebwa (mbwelekono) na pia akifikia umri wa makamo, naye ni miongoni mwa watu wema” ni moja ya Aya zinazotoa utabiri juu ya kurejea kwa Isa (a.s) kabla ya Siku ya Kiama. [9] Hii ni kwa sababu kwamba; kwa mujibu wa lugha ya Kiarabu, neno "kahlan" humaanisha mtu mwenye umri wa kati na kati au wa makamo. [10] Na suala jengine linalosisitiza jambo hili, ni uwepo wa kauli isemeyo kwamba; Nabii Isa (a.s) alipaa mbinguni huku akiwa na umri wa miaka 32 [11] au 33. [12] Pia moja ya Hadithi kutoka kwa Imamu Ja’far al-Sadiq (a.s), inasema kwamba; Nabii Isa (a.s) hakufikia umri wa makamo kabla ya kupaa kwake. [13] Hivyo basi, kuzungumza kwake akiwa ni mtu mwenye umri wa makamo, kunahusiana na kurejea kwake duniani katika kipindi kijacho cha kudhihiri kwa Imamu Mahdi (a.f). [14] Watafiti wengine wanasema kwamba; kuna umuhimu mkubwa katika vipindi viwili vya kauli ya Nabii Isa (a.s): 1- Kauli ya utotoni mwake: Pale mazungumzo yake yaalipoidhamini heshima ya mama yake (bibi Mariam), ili kumtakasa dhidi ya tuhuma za ufisadfi wa kimaadili. 2- Na wakati wa kudhihiri kwa Imamu Mahdi (a.f), wakati ambao Nabii Isa (a.s) atasimama na kuwahubiria Watu wa Kitabu (Ahlul-Kitab) na kuwalingania kumfuata Imamu Mahdi (a.f). [15]
Aya ya 159 ya Surah An-Nisaa na Muktadha wa Kurejea kwa Nabii Isa (a.s) Kwa mtazamo wa Muhammad Husayn Tabatabai na Muhammad Sadiqi Tehrani, ambao ni miongoni mwa wafasiri mashuhuri wa Kishia, ni kwamba ile Aya isemayo: (وَ إِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ ۖ وَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا؛) “Na hapatopatikana hata mmoja miongoni mwa Watu wa Kitabu (Ahlul-Kitab), ila bila shaka atamwamini (Nabii Isa) kabla ya kufa kwake; na Siku ya Kiyama atakuwa ni shahidi juu yao” [16], inakusudia kutuelewesha kuwa; kabla ya kufariki kwa Nabii Isa (a.s), Watu wote wa Kitabu watamwamini kuwa yeye ni mtume wa haki. Hii ina maana ya kwamba; Wayahudi wataukubali utume wake (ambao waliupinga), na Wakristo nao wataacha imani ya uungu wake ulioko kwenye nadharia ya utatu (Trinity). Uchambuzi huu unatokana na imani isemayo kwamba; Isa (a.s) atashuka kutoka mbinguni wakati wa kudhihiri kwa Imamu Mahdi (a.f), na atamuunga mkono kwa kusali nyuma yake, jambo ambalo litawashtua na kuwaongoza Watu wa Kitabu na kuwafanya wautambue ukweli. [17] Kadhalika, katika moja Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imamu al-Baqir (a.s), imeelezwa kwamba; Aya hii inahusishwa moja kwa moja na suala la kushuka kwa Nabii Isa (a.s), tukio linalotarajiwa kutokea wakati wa kudhihiri kwa Mahdi (a.s). [18]
Dhana ya Urejeo wa Masihi (Nabii Isa) Katika Injili Katika mafundisho ya Kikristo, dhana ya urejeo wa Yesu Masihi (Nabii Isa), ni moja ya dhana za kitheolojia zilizomo katika Injili, inayojulikana kwa jina la "Parousia" au "Ujio wa Pili" (second coming). [19] Ushahidi wa kimaandishi ulioko katika maandiko ya Injili utoa ishara na bayana za wazi kabisa juu ya urejeo huu, katika vifungu mbalimbali vya kitabu hichi. [20] Baadhi ya wasomi wa fani ya theolojia wanadokeza kuwa, hoja hii ya kitheolojia imedokezwa na kujirudia kwa zaidi ya mara mia tatu ndani ya Injili, huku baadhi ya wakati ikionekana kujadiliwa katika sura kamili ya kitabu hicho, kama inavyoonekana katika Mathayo 24-25 na Marko 13. [21] Kwa mujibu wa tafakuri za ki-Injili, Wakristo wanashikilia fundisho lisemalo kwamba; Kristo atarejea katika upeo wa wakati (akhirizaman), ili kuhitimisha mpango wa ukombozi. Katika kipindi hicho, amani timilifu itatala ulimwenguni, na vitendo vya vita na mauaji vitakoma kabisa. [22] Miongoni mwa ishara zinazotangulia manzo katika kipindi cha karibu na urejeo wake, kama ilivyoelezwa katika Injili, ni; kuenea kwa uonevu, kutokea kwa majanga ya njaa na mitetemeko ya ardhi, mabadiliko ya ki-kosmolojia (Cosmology), kama vile kutiwa giza kwa jua na mwezi, na la mwisho ni kuja kwa Mpinga-Masihi anayejulikana kwa jina la Dajali. [23]
Nyakati na Maeneo Yanayotajwa Kuhusiana na Kurejea kwa Nabii Isa (a.s.) Kulingana na Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s), ni kwamba; Damaskasi ndilo eneo litakalotumiwa na Nabii Isa (a.s) katika ujio wake wa pili hapa duniani. [24] Hata hivyo, kuna mtazamo tofauti uliotolewa na mwanazuoni Muhammad Taqi Majlisi, alioubainisha katika kitabu chake kiitwacho Lawami'u Sahibqirani. Kulingana na maoni ya Muhammad Taqi Majlisi yalioko katika kitabu hicho, Nabii Isa (a.s) atarudi duniani kupitia ardhi ya Makka. [25] Vyanzo vya Kisunni navyo vinataja maeneo mbalimbali kuhusiana na kuja kwake (a.s). Miongoni mwa maeneo yaliyotajwa ndani ya vyanzo vya Kisunni, ni Baytul Maqdis, [26] ikielezwa kwama yeye atashuka kwenye eneo maalum la daraja jeupe lililoko kwenye lango la mashariki ya jiji la Damaskasi. [27] Ingawa hakuna Hadithi wala maandiko fulani ya kidini yaliyotaja muda kamili wa kurejea kwa Nabii Isa (a.s), ila baadhi ya watafiti wanadhania kwamba tukio hili litajiri katika nyakati za mwanzoni mwa kudhihiri kwa Imamu Mahdi (a.f). [28] Baadhi ya wanazuoni wa kale kama vile Abul-Futuh Razi na Tabarsi, ambao ni wafasiri wa Qur’ani wa karne ya 6 Hijiria, waliona Aya ya 61 ya Surat Az-Zukhruf {Maelezo 1: وَإِنَّهُ لَعِلْمٌ لِّلسَّاعَةِ فَلَا تَمْتَرُنَّ بِهَا وَاتَّبِعُونِ ۚ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ Na kwa hakika, yeye (Issa mwana wa Maryam) ni alama ya wazi ya Saa (Tukio la Kiyama). Basi msiifanyie shaka, la hasha! Na nifuateni mimi (katika njia ya Mwenye Ezi Mungu), hii ndiyo njia Iliyonyooka (Siraat-ul-Mustaqiim)} kuwa ni miongoni mwa Aya zinazohusiana na ujio wa Nabii Isa (a.s). Wanazuoni wawili hawa wanaamini kwamba; kurejea kwa Nabii Isa (a.s), ni sharti la kimetafizikia linaloashiria kukaribia kwa Siku ya Kiyama. [29] Ufafanuzi huu, ambao pia unashuhudiwa katika baadhi ya Riwaya za Kisunni, [30] unaanishwa kama ni hoja juu ya urejeo wa Nabii Isa (a.s) katika kipindi cha kudhihiri kwa Imamu Mahdi (a.f). [31] Sababu ya msingi katika uanishaji huu unatokana na kwamba; tukio la kudhihiri kwa Imamu Mahdi (a.f) pia nalo kunatabiriwa kutokia katika nyakati za mwishoni mwa dunia. [32]
Jukumu la Nabii Isa (a.s.) Katika Ujio Wake wa Pili Kulingana na vyanzo vya Hadithi vya Kiislamu, ni kwamba; kurejea kwa Nabii Isa (Yesu) (a.s) duniani hakutakuwa ni kwa ajili ya kuanzisha uongozi wake mwenyewe, bali jukumu lake kuu litakuwa ni kumsaidia na kumuunga mkono Imam Mahdi (a.f) katika kusimamisha haki na uadilifu ulimwenguni. Ujio wake ni sehemu ya mpango mkuu wa Mungu wa kuleta enzi ya amani na ustawi kamili duniani. [33] Majukumu atakayoshika Nabii Isa (a.s) kama yalivyotajwa na vyanzo mbali mbali vya kiislamu ni kama ifuatavyo: 1. Msaidizi Mkuu na Waziri wa Imam Mahdi. Lengo kuu la kurejea kwa Nabii Isa (a.s) ni kuwa msaidizi mkuu wa Imamu Mahdi. Mapokezi ya Hadithi ya upande wa Kishia yanamtaja kama ni "mweka hazina" wa serikali ya Imamu Mahdi (a.f), [34] wakati mapokezi ya Kisunni yanamtaja kama ni "waziri" [35] atakayekuwa na jukumu la kusimamia mahakama na utoaji wa haki. [36] 2. Kusahihisha Imani na Kuvunja Mila Potofu. Kulingana na Riwaya fulani iliopo katika Sahihi Bukhari ni kwama; Moja ya hatua zake za kwanza kabisa katika ujio wake, itakuwa ni kurekebisha baadhi ya itikadi na desturi potofu. Atafanya mambo yafuatayo ya ki-ishara za kuonesha upofu wa desturi hizo: A- Atavunja msalaba: Akitoa ishara ya kukanusha heshima inayopewa msalaba hiyo. B- Atamuua nguruwe: Akionesha ishara ya kukataza kabisa ulaji wa nyama ya nguruwe, jambo ambalo limeharamishwa katika dini ya Mwenye Ezi Mungu. [37]
C- Ataweka Jizya: Ataweka kodi maalumu kwa Wakristo, ikiwa ni ishara ya kuwepo kwa sheria moja ya uadilifu chini ya utawala wa Kiislamu.
3. Kuleta Enzi ya Fanaka na Utoshelezi. Ujio wa Nabii Isa na Imamu Mahdi (a.f) utaleta kipindi cha ustawi na utajiri usio na kifani. Mapokeo yanaeleza kuwa dunia itajaa neema kiasi kwamba watu watakuwa na mali nyingi mno, na hakuna mtu atakayekubali kupokea sadaka au zawadi kwa sababu kila mtu atakuwa amejitosheleza na hatakuwa na uhitaji wa kuhitajia mali. [38] Kulingana na Riwaya zilizopo katika vyanzo vya Kiislamu vya Shia pamoja na Sunni ni kwamba; Katika ujio wake, Nabii Isa afanya mambo muhimu yafuatayo:
Kusali kwa Nabii Isa Nyuma ya Imam Mahdi (a.s) Kwa mujibu wa riwaya kadhaa kutoka madhehebu ya Shia pamoja na Sunni, imeelezwa kuwa; Nabii Isa (a.f) atatekeleza ibada zake za sala nyuma ya Imamu Mahdi (akiongozwa na Imamu Mahdi) (a.f). [39] Baadhi ya watafiti wamebainisha kuwa; Kuna idadi ya Riwaya kumi na nne katika vyanzo vya Riwaya za upande wa madhehebu ya Kishia, zinazotaja suala la Nabii Isa kusali nyuma ya Imamu Mahdi (a.f). [40] Ijapokuwa Riwaya hizi hazikufafanua jukumu jingine lililobeba ujumbe maalumu ndani yake, [41] ila wachambuzi wamejaribu kutoa tafsiri nyengine kadhaa kuhusiana ujumbe uliomo ndani yake, kulingana na muktadha pamoja na malengo ya Riwaya hizo zilivyo. Jumla ya aina za ujumbe zilizotajwa na wachambuzi hao ni kama ifuatavyo: • Tendo la kusali nyuma ya Imamu Mahdi (a.f), ni uthibitisho usio na shaka wa mamlaka (marja'iyyah) ya kisiasa na kidini ya Imamu Mahdi (a.s.). [42] • Ni kichocheo cha kusalimu amri kwa Wakristo mbele ya Imamu Mahdi (a.f) na hatimaye wao kuikubali dini ya Kiislamu. [43] • Kwa mujibu wa mtazamo wa Ali Korani, tendo hili la kusali nyuma ya Imamu (a.f), litatokia kimkakati pale Warumi watakapokiuka mkataba wao na Imamu ((a.f), hivyo basi Nabii Isa (a.s) atatumia kitendo hicho ili kuweka bayana msimamo wake dhidi yao. [44]
Kumuangamizaji Masihi Dajjal
Makala Asili: Dajjal
Kwa mujibu wa moja ya Riwaya inayonukuliwa kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s), imeelezwa kwamba; Hatimae Dajjal atakuja kuaangamizwa na Nabii Isa (a.s). [45] Kulingana na Riwaya iliyonukuliwa katika Ilzaamu al-Nasib, ni kwamba; Imamu Mahdi (a.f) atamkabidhi Nabii Isa (a.s.) ukamanda wa jeshi lake, na yeye ndiye atakayetekeleza mauaji ya Dajjal, tukio litakalotoke katika ardhi ya Hijaz. [46] Dhana hii ya kuuawa kwa Dajjal kupitia mkono wa Nabii Isa pia imeripotiwa ndani ya vyanzo vya Riwaya za upande wa madhehebu ya Ahl al-Sunnah. [47] Aidha, kuna baadhi ya vyanzo vya Kishia vinavyohusisha utekelezaji wa mauaji ya Dajjal na Imamu Mahdi (a.f). Wachambuzi wanatoa ufafanuzi wao wakisema kuwa; hakuna ukinzani wowote kati kati ya dhana mbili hizi; kwani iwapo Nabii Isa (a.s) atatekeleza kitendo hicho, basi atakitekeleza kwa mujibu wa mamlaka amri ya Imamu Mahdi (a.f). [48] Kwa mantiki hiyo, kitendo cha mauaji kinaweza kuhusishwa na wahusika wote wawili bila ya kupatikana utata wowote ule ndani yake kati ya mtoaji amri na mtekelezaji. [49] Kulingana na moja ya Riwaya ya upande wa Kisunni ni kwamba; Nabii Isa atashirikiana na Imam Mahdi (a.f) katika kumuangamiza Dajjal huko Palestina. [50]
Kuuawa kwa Ya'ajuj na Ma'ajuj Kupitia Mkono wa Nabii Isa (a.s)
Makala Asili: Ya'ajuj na Ma'ajuj
Kwa mujibu wa maelezo ya Ali bin Ibrahim al-Qummi na Tabarsi, ambao ni wafasiri wa Qur’ani wa upande wa madhehebu ya Kishia, ni kwamba; Moja kati ya matukio yatakayotokea mwishoni mwa dunia, ni tukio la kuzuka kwa Yajuuj na Majuuj. Tukio ambalo limetajwa na Mwenye Ezi Mungu katika Aya ya 96 ya Surah Al-Anbiya. Habari zinaeleza kwamba; viumbe hawa watakuja na uharibifu mkubwa mno, katika siku za mwishoni mwa kumalizika dunia. [51] Habari hizi pia zinaonekana kuripotia na Agano la Kale pamoja na Agano Jipya pia. [52] Hadithi za Kisunni zikiripoti tukio hili, zinaeleza kuwa; Yajuuj na Majuuj watauawa kupitia mikono ya Nabii Isa (53).
Propaganda za Bani-Umayya za Kumuarifishawa Isa (a.s) kama Ndiye Mahdi Mtarajiwa
Mmoja kati ya Watafiti wa Kishia ajulikanaye kwa jina la Najmuddin Tabasi, anaamini kwamba; licha ya kuwepo kwa itikadi thabiti katika Uislamu, kuhusiana na kurudi kwa Nabii Isa (a.s) katika zama za kudhuhiri kwa Imamu Mahdi (a.f), ila dhana hii imeonekana kutumiwa vibaya na Bani Umayya. Kwa sababu ya uhasama wao wa kihistoria dhidi ya Ahlul-Bayt (a.s). Bani Umayya ndiyo waliohusika katika kughushi wa hadithi zilizojaribu kuficha ukweli wa tukio hili. Miongoni mwa Hadithi bandia zilizoasisiwa nao, ni ile Hadithi isemayo: "La Mahdi illa Isa ibn Maryam" (Hakuna Mahdi isipokuwa Isa mwana wa Maryam), [54] Hadithi hii pamoja na Hadithi nyengine zinazofanana nayo [55] zilitumiwa kama chombo cha propaganda kwa ajili ya kumkanusha Imamu Mahdi (a.s. Kimsingi, mkakati wa Bani Umayya ulikuwa na malengo mawili: kwanza, kupinga nasaba ya Mahdi aliyeahidiwa kutoka kwa Ahlul-Bayt, na pili, kumtawaza Isa (a.s) kama ndiye Mahdi mtarajiwa. [56]
Tabasi akielezea maoni yake haya, anaendelea kufafanua akisema; Ili kutekeleza upotoshaji wao huu, dhima na majukumu ya msingi ya Imam Mahdi (a.f) yalipokonywa na kuhawilishwa kwa Nabii Isa (a.s). Hii inajumuisha matukio makuu ya nyakati za kudhihiri kwa Mahdi mtarajiwa, kama vile mauaji ya Dajjal na vita dhidi ya Ya'ajuj na Ma'ajuj. Aidha, eneo na mahala pa kudhihiri kwake pia palibadilishwa, ambapo Baitul Maqdis (Yerusalemu) ndilo enelo lililohusisha naye badala ya Makka. Walijaribu kutaja eneo hilo kuwa ndiyo aneo la kudhihiri kwa Nabii Isa (a.s) ambaye walidai kuwa ndiye Mahdi Mtarajiwa. [57]
Tasnifu Mahususi (Monografia) Kuna idadi kadhaa ya kazi andishi zilizotungwa makhususi kuhusiana na maudhui ya urejeo wa Nabii Isa (a.s). Miongoni mwa kazi hizo ni kama ifuatavyo: • Nuzulu Masihi wa Dhuhuri Mau’uud; kazi ya Mirtaqi Husseini Gurgani, kitabu hichi kilichapishwa na shirika la uchapishaji la Bustan Kitab, Qom Iran, mnamo mwaka 1390 Shamsia, (swa na mwaka 2011 Miladia). • Naqshe Hadhrat Masih (a.s) Dar Dolate Mahdi (a.f); Majid Yagub-Zadeh aliandaa kazi hii kwa kuiunda katika sura nne, na hatimae kazi yake hii ikachapishwa na shirika la Mau’ud Asr, mnamo mwaka 1398 Shamsia (sawa na 2019 Miladia). • Nuzulu Isa bin Maryam Aakahre Zaman; hii ni kazi ya Jalaluddin al-Suyuti, mwanazuoni wa madhehebu ya Kisunni wa karne ya kumi Hijria. Kazi hii ilichapishwa na Dar al-Kutub al-Ilmiyya, Beirut, mnamo mwaka 1405 Hijiria.