Hussein ibnu Ruh al-Nawbakhti

Kutoka wikishia
Kwa ajili ya matumizi mengine angalia Nawbakhti
Kaburi la Hussein ibn Ruh Nawbakhti

Hussein ibn Ruh Nawbakhti (Kiarabu: الحسين بن روح النوبختي) (aliaga dunia 326 Hijiria) ni Naibu wa tatu miongoni mwa Manaibu wanne wa Imamu Mahdi (a.t.f.s). Nawbakhti alishikilia jukumu la Naibu Maalumu wa Imamu Mahdi kwa muda wa miaka 21 (305-326). Alikuwa mmoja wa masahaba wa Imamu Hassan al-Askary (a.s) na mmoja wa masahaba wa karibu wa Naibu wa pili mjini Baghdad. Katika lahadha za mwisho za umri wake, Muhammad bin Othman (Naibu wa pili) alimtangaza Hussein ibn Ruh kwa amri ya Imamu Mahdi kuwa mrithi wake na kushikilia wadhifa wa Naibu wa Tatu wa Imamu Mahdi (a.t.f.s). Baada ya muda, 6 Mfunguo Mosi Shawwal 305 Hijria, kulitolewa barua na andiko la kwanza kutoka kwa Imamu Mahdi (a.s) likithibitisha unaibu wa Hussein ibn Ruh Nawbakhti.

Mwanzoni mwa unaibu wake Hussein ibn Ruh alikuwa na wadhifa na heshima maalumu katika vyombo vya utawala wa Bani Abbas, lakini baadaye alikumbwa na matatizo na kipindi fulani alilazimika kuishi maisha ya kujificha, kisha akafungwa jela miaka mitano. Moja ya matukio muhimu sana ya zama za Hussein ibn Ruh ni suala la Shalmaghani, ambaye alikuwa balozi na wakili wake wa kutegemewa, lakini alipatwa na upotovu wa kiitikadi, na Imamu Mahdi (a.t.f.s) akatoa andiko la kumlaani. Nafasi ya kielimu ya Hussein ibn Ruh Nawbakhti imechukuliwa kuwa bora na nzuri kutokana na uandishi wa vitabu vya fiqhi na umahiri wa kutosha katika midahalo na mijadala ya kielimu. Katika vyanzo vya hadithi kumenukuliwa baadhi ya karama zake.

Maisha yake

Mwaka aliozaliwa Hussein ibn Ruh Nawbakhti haufahamiki. Kuniya yake ni Abul-Qassim na katika vyanzo ametajwa kwa lakabu za Nawbakhti, Ruh [1] na Qummi. [2] Kuwa kwake mtu wa Qom kumeelezwa kuwa huenda kumetokana na kuzungumza lahaja ya Kiajemi ya watu wa Abeh (karibu na Saveh) na uhusiano wake wa karibu na watu wa huko, [3][4][5] hata hivyo katika vyanzo vingi, anajulikana kama Nawbakhti. Inasemekana kwamba alinasibishwa na ukoo wa Nawbakhti kwa upande wa mama yake. [6] Wengine pia wamesema kwamba alitoka tawi la Banu Nawbakht la Qom na alihamia Baghdad katika zama za Naibu wa kwanza. [7]

Uhusiano na Imamu Askary (a.s)

Kuna hitilafu kuhusiana na kwamba, Hussein ibn Ruh alikuwa mmoja wa masahaba wa Imamu Hassan Askary (a.s). Ibn Shahrashub katika kitabu chake cha al-Manaqib anamchukulia kuwa ni mmoja wa masahaba na pia msaidizi maalumu wa Imamu Askary (a.s), [8] lakini wanachuoni wengine wa Elimu ya Rijal hawajasema lolote kuhusu hili. Baadhi wanaamini kwamba ni vigumu kuzikubali habari hizi, kwa sababu Imam Askary (a.s) aliaga dunia mwaka 260 Hijiria na Nawbakhti alifariki dunia mwaka 326 Hijiria. [9]

Sifa maalumu

Sheikh Tusi amesema katika kitabu Al-Ghaibah kwamba, Hussein ibn Ruh alikuwa mtu wenye hekima na akili zaidi katika zama zake na alikuwa akifanya taqiyyah katika kushirikiana na kuingiliana na wapinzani; [10] kiasi kwamba, alimfukuza kazi mmoja wa wafanyakazi wake kutokana na kumtukana Muawiya. [11]

Kwa mujibu wa Jassim Hussein katika kitabu cha Tarikh Siyasat Ghaibat ni kwamba, kile kilichomfikisha Hussein ibn Ruh kwenye nafasi hii ni sifa zake, ustahiki na kazi zake ambazo zilimfanya awe mtu anayefaa kwa ajili ya jukumu la unaibu. [12] Ummu Kulthum binti ya Muhammad ibn Othman anazungumzia uhusiano wa baba yake na Hussein kwamba, Hussein Nawbakhti alikuwa mmoja wa watu wake wa karibu na maalumu na baba yake alikuwa akimueleza mambo ya ndani na binafsi ya maisha yake. [13]

Abu Sahl Nawbakhti amesema kuhusu utunzaji siri wa Hussein bin Ruh kwamba: Ikiwa atamficha Imamu chini ya kanzu yake na mwili wake ukakatwa vipande vipande kwa mkasi ili kumdhihirisha na kumfichua, kamwe hatafanya hivyo. [14]

Kifo

Hussein ibn Ruh Nawbakhti alifariki dunia 18 Sha'ban 326 Hijiria. Kaburi lake liko katika kitongoji cha Nawbakhtiyah katika soko la Attaran au Shorjah katika mji wa Baghdad, Iraq ambayo sasa inajulikana kama maqam na mahali pa Hussein ibn Ruh na ni mahali pa Mashia kufanya ziara. [15]

Unaibu

Makala Kuu: Unaibu maalumu

Baada ya kifo cha Naibu wa pili wa Imamu Mahdi mwaka 305 Hijiria, Hussein ibn Ruh aliteuliwa kuchukua jukumu la unaibu wa Imam Mahdi (a.s). Kabla ya hapo, alikuwa mmoja wa wafanyakazi wa masuala ya kifedha wanaotegemewa na wa karibu sana wa Muhammad ibn Othman, [16] [17] na Muhammad bin Othman alimfanya kuwa kiunganishi wake na mabalozi na mawakili wengine huko Baghdad. [18]

Ingawa kulikuwa na wawakilishi na mawakili wapatao kumi wa Naibu wa pili huko Baghdad, lakini Muhammad ibn Othman wakati wa kuugua kwake alimwita na kumtaja Ibn Ruh kama naibu wake na balozi wa Imamu Mahdi na akawataka Shakhsia wa Kishia kumrejea yeye baada ya kifo chake.[19] Allama Majlisi ameandika, siku ambayo Naibu wa Pili alifariki dunia, Husein bin Ruh alikaa nyumbani kwake na mtumishi wa Muhammad bin Uthman akakabidhi sanduku lililokuwa na amana ya Uimamu kwa Hussein bin Ruh.[20] Baada ya muda fulani, tarehe 6 Shawwal 305 Hijiria, kulitolewa barua na andiko la kwanza kutoka kwa Imamu Mahdi (a.t.f.s) lilikithibitisha Unaibu wa Hussein ibn Ruh Nawbakhti. [21]

Katika baadhi ya nukuu inafahamika kwamba nafasi ya Ibn Ruh, tofauti na balozi wa kwanza na wa pili, ulikuwa wazi miongoni mwa Shia Imamiyyah, na kwa ajili hiyo, ndio maana baadhi ya Mashia waliamua kuwapuuza mawakala wa maeneo yao na kuwasiliana moja kwa moja na Naibu wa tatu. [22]

Mabalozi na mawakili

Hussein ibn Ruhh alianza shughuli zake katika nafasi ya Unaibu kwa ushirikiano na mawakili kumi huko Baghdad na mawakili wengine katika nchi nyingine za Kiislamu. Majina ya baadhi ya mawakili na mawakala wake ni kama ifuatavyo:

Ushawishi ndani ya utawala

Wakati wa uhai wa Muhammad bin Othman (Naibu wa pili wa Imamu Mahdi), Hussein bin Ruh alikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya utawala wa Bani Abbas, na alikuwa akipokea misaada ya kifedha kutoka kwa maafisa wa serikali. [24] Baada ya kuchukua nafasi na jukumu la unaibu, wakati wa mtawala wa Muqtadir, alikuwa na ushawishi katika utawala wa Bani Abbas na alikuwa akiheshimiwa nao. Sababu ya nafasi yake hii ilikuwa, kwa upande mmoja, athari na ushawishi wa familia ya Nawbakhti, na kwa upande mwingine, uwaziri wa Abul-Hassan Ali bin Muhammad kutoka Aali-Furat, ambaye alikuwa miongoni mwa wafuasi wa Mashia. [25] [26] Kwa mujibu wa Ummu Kulthum binti ya Muhammad bin Othman (Naibu wa pili) katika kipindi hiki fedha na mali za watu wa Furat zilikuwa zikimfikia Hussein bin Ruh. [27] Sababu nyingine za nafasi na ushawishi wa Hussein bin Ruh katika utawala ni misimamo yake ya tahadhari, ambapo alijaribu kujiepusha na uasi wa wakati huo, kama vile Qaramitah. [28] Hata hivyo, wakati Hamid bin Abbas alipochukua madaraka kama waziri, mtu ambaye alikuwa akiwaunga mkono wapinzani wa Mashia, matatizo yakajitokeza kwa Hussein bin Ruh. [29]

Kwenda mafichoni

Baadhi ya vyanzo vimefahamisha kuhusu kujificha kwa Hussein bin Ruh muda fulani baada ya kuteuliwa kuwa Naibu wa Imamu Mahdi (a.t.f.s). Muda wa kipindi hiki haujulikani na pengine ilikuwa kati ya mwaka wa 306 na 311 Hijiria, wakati wa Hamid bin Abbas kuhudumu kama waziri katika utawala wa Bani Abbas.[30] Kwa mujibu wa kile alichokiandika Sheikh Tusi ni kwamba, katika kipindi hiki Muhammad bin Ali Shalmaghani alikuwa balozi na kiunganishi cha Ruh na watu. [31] Hakuna taarifa zaidi kuhusiana nna kipindi hiki.

Kufungwa jela

Hussein bin Ruh Nawbakhti alifungwa kwenye jela ya Muqtadir ya Khalifa wa Kiabbasi kuanzia mwaka 312 hadi 317 Hijria. Hakuna sababu zilizoelezwa za kufungwa kwake katika vyanzo vya Kishia, lakini baadhi ya watafiti wamesema mambo mawili kulingana na riwaya za Sunni:

Kukataa kwake kutoa fedha kwa utawala

Kuwa na uhusiano na Qaramitah waliokuwa wakidhibiti na kutawala Bahrain katika zama hizo.

Baadhi ya watafiti wamezingatia sababu ya kufungwa kwake kuwa ni umashuhuri wake katika jukumu la unaibu wa Imamu Mahdi, uhusiano wake na Mashia, na kukubalika kwake katika kupanga hali zao na kukusanya barua na fedha zao za malipo ya kisheria (Wujuhat Shar’i) na kuziwasilisha kwa Imamu Mahdi (a.t.f.s). [33] Hata hivyo, baadhi wanaamini kwamba kukamatwa kwake kulitokana na uadui wa Shalmaghani ulifanywa na Muhsen bin Ali bin Furat (mtoto wa Ali bin Furat waziri na mmoja wa wafuasi wa Shalmaghani) wakati wa uwaziri wa Ali bin Furat mwaka 311-312 AH. [34]

Baada ya kuachiliwa kutoka gerezani, kwa sababu ya kuwepo kwa watu mashuhuri kutoka kwa familia ya Nawbakht katika serikali ambao walikuwa na nyadhifa muhimu, hakukuwa na mtu ambaye angeweza kumsumbua tena. [35]

Mkasa wa Shalmaghani

Makala asili: Shalmaghani

Shalmaghani alikuwa mmoja wa wanazuoni wa Kishia huko Baghdad na mtu wa karibu wa Hussein bin Ruh al-Nawbakhti. Baada ya Hussein bin Ruh kuteuliwa kushika wadhifa wa Naibu wa Imamu Mahdi (a.t.f.s), alimtambulisha Shalmaghani kama wakili wake na akamkabidhi usimamizi wa masuala ya Shia, hadi kufikia hatua ya kwamba wakati wa maisha ya siri na ya kifichoni ya Hussein bin Ruh, maandiko na barua za Imam Zaman kwa Ibn Ruh zilikuwa kuwa zikisambazwa na Shalmaghani. [36] Lakini yeye, wakati wa kufungwa kwa Hussein bin Ruh na kwa kutumia vibaya nafasi yake, kwanza alijitambulisha yeye kuchukua nafasi ya Hussein bin Ruh na baadaye akawa na upotofu wa kiitikadi na akaritadi. Upotofu wake ulipodhihirika, Hussein bin Ruh, ambaye alikuwa gerezani, aliwafahamisha Mashia kuhusu hili na akawakataza kushirikiana naye ambapo mwaka 312 Hijiria na kulitolewa amri na barua ya Imamu Mahdi (a.t.f.s) ya kumlaani. [37]

Daraja yake ya kielimu na karama

Hussein bin Ruh aliandika kitabu kuhusu fiqhi kiitwacho al-Taadib na akakipeleka Qom kwa ajili ya kutoa maoni na nadharia katika uga wa hadithi na akawataka wanachuoni wa huko kutaja nukta ambazo ni kinyume na maoni yao. Baada ya kutathmini yaliyomo ndani ya kitabu hicho, wanazuoni wa Qom waliidhinisha isipokuwa katika sehemu moja tu na wakairejesha kwake. [38]

Pia alikuwa na mijadala katika wakati wake kama naibu, ambayo imenukuliwa kwa mapana na marefu katika vyanzo vya hadithi. [39] [40] [41] Majibu yaliyotolewa na Hussein bin Ruh kwa maswali yaliyoulizwa katika mazungumzo haya yanaonyesha umahiri na ubobezi wake katika masuala ya kidini na pia daraja yake ya kielimu. [42]

Pia amenukuu baadhi ya hadithi. [43] Sheikh Tusi amenukuu Ziyara ya Rajabiyah kutoka kwa Hussein bin Ruh Nawbakhti. [44]

Karama

Katika baadhi ya vyanzo, kumenukuliwa karama kutoka kwa Hussein bin Ruh. Wakati fulani alikuwa akifichua baadhi ya siri na kufichua baadhi ya ishara ili kuondoa mashaka ya upande mwingine na wakati mwingine kujithibitisha. Barua ya Ali Ibn Babawayh (baba yake Sheikh Swaduq) kwa naibu wa tatu kwa ajili ya kupata mtoto na kuomba dua kutoka kwa Imam Mahdi (a.t.f.s), [45] au barua nyingine kutoka kwa Ibn Babawayh (baba yake Sheikh Sadouq) kwenda kuamua taklifu na jukumu lake kwa ajili ya safari ya Hija, [46] kutoa habari ya kifo cha Ahmad bin Is’haq Qummi, [47] kutoa habari kwa Muhammad bin Hassan al-Sayrafi kuhusu mkuo wa dhahabu uliopotea [48] na hadithi nyingine, ni mifano ya wazi ya karama zake.

Rejea

Vyanzo

  • Amīn, Sayyid Muḥsin al-. Aʿyān al-Shīʿa. Beirut: Dār al-Taʿāruf, 1421 AH.
  • Dhahabī, Muḥammad b. Aḥmad al-. Siyar aʿlām al-nubalāʾ. Edited by Shuʿayb al-Arnāʾūṭ. Beirut: Muʾassisat al-Risāla, 1413 AH.
  • Ghaffārzāda, ʿAlī. Zindigānī-yi nuwwāb-i khāṣ-i Imām Zamān. Qom: Intishārāt-i Nubūgh, 1379 Sh.
  • Ibn Shahrāshūb, Muḥammad b. ʿAlī. Manāqib Āl Abī Ṭālib. Qom: ʿAllāma, 1379 AH.
  • Iqbāl Āshtīyānī, ʿAbbās. Khāndān-i Nawbakhtī. Tehran: [n.p], 1345 Sh.
  • Jaʿfarīyān, Rasūl. Ḥayāt-i Fikrī wa sīyāsī-yi imāmān-i Shīʿa. Qom: Anṣārīyān, 1381 Sh.
  • Jāsim Ḥusayn. Tārīkh-i sīyāsī-yi Imām dawāzdahum. Translated to Farsi by Muḥammad Taqī Āyatollāhī. Tehran: Amīr Kabīr, 1385 Sh.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Rijāl al-Kashshī. Mashhad: Dānishgāh-i Mashhad, 1348 Sh.
  • Khoei, Sayyid Abū l-Qāsim. Muʿjam rijāl al-ḥadīth. Beirut: Dār al-Zahrāʾ, 1403 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Muʾassisat al-Wafā, 1403 AH.
  • Mūsawī, Sayyid Ḥasan & Kasāʾī, Nūr Allāh. 1378 Sh. "Pazhūhishī pīrāmūn-i zindigī-yi sīyāsī wa farhang-i nuwwāb-i arbaʿa." Dānishkada-yi Adabīyāt wa ʿUlūm-i Insānī-yi Dānishgāh-i Tehran 150:276-292.
  • Najāshī, Aḥmad b. ʿAlī al-. Rijāl al-Najāshī. Edited by Shubayrī Zanjānī. Qom: [n.p], 1407 AH.
  • Ṣadr, Sayyid Muḥammad al-. Tārīkh al-ghayba. Beirut: Dār al-Taʿāruf, 1412 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Kamāl al-dīn wa tamām al-niʿma. Tehran: Islāmīyya, 1395 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Ghayba. Qom: Muʾassisat al-Maʿārif al-Islāmīyya, 1411 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Miṣbāḥ al-mutahajjid. Beirut: Muʾassisat Fiqh al-Shīʿa, 1411 AH.