Nenda kwa yaliyomo

Umaasumu wa Maimamu

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na Umaasumu wa Maimamu. Ili kujua kuhusiana na maana ya Umaasumu (isma) na Umaasumu wa Manabii angalia makala ya Umaasumu na Umaasumu wa Mitume.
Aya ya Tat'hir, imechorwa na Abdul Rasool Yaqouti.

Umaasumu wa Maimamu (Kiarabu: عصمة الأئمة) ni utakasifu wa Maimamu wa Kishia wa kutotenda madhambi makubwa wala madogo kama ambavyo hawafanyi kosa kwa makusudi au kwa kusahau. Umaasumu wa Maimamu ni miongoni mwa masharti ya Uimamu katika mtazamo wa Mashia Ithaashariya na Shia Ismailiya na ni katika sifa za Maimamu. Mashia Imamiyah wameafikiana kwamba, Maimamu (a.s) wana kinga na Umaasumu wa kutofanya madhambi yote makubwa kwa madogo, iwe ni kwa makusudi au kwa kusahau na kamwe si wenye kufanya kosa. Kwa mujibu wa Abdullah Jawad Amoli, Maimamu (as) kama ambavyo ni Maasumu katika mienendo, elimu yao pia ni ya haki na imekingwa kunako makosa.

Maulamaa wa Kishia wakiwa na lengo la kuthibitisha Umaasumu wa Maimamu wametumia Aya mbali zikiwemo Aya ya Ibtilaa (majaribu) Ibrahim, Aya ya Ulul-Amr, Aya ya Tat'hir, na Aya ya Swadiqin, Aya ya Mawaddah na Aya ya Swalawat (kumswalia Mtume). Katika vyanzo na vitabu vya hadithi kumenukuliwa hadithi nyingi kuhusiana na maudhui hii. Hadith Thaqalayn (hadithi ya Vizito Viwili) na Hadithi ya Safina ni miongoni mwa hadithi hizo ambazo zinatumiwa kuthibitisha kwamba, Maimamu ni Maasumu na hawatendi dhambi wala kukosea. Licha ya kuweko hoja na dalili mbalimbali za kuthibitisha Umaasumu wa Maimamu, lakini kundi la Mawahabi na Ibn Taymiyyah, kiongozi wa kundi la Salafi wamekana hilo na kutilia ishkali. Hata hivyo Maulamaa wa Kishia wamejibu ishkali na nukta zote zilizoelezwa kama ni utata. Kuhusiana na Umaasumu wa Imamu na Maimamu kumeandikwa vitabu vingi.

Nafasi na Umuhimu

Umaasumu wa Imamu na hoja zake inahesabiwa kuwa miongoni mwa maudhui muhimu za Kiqur'an na kitheolojia. [1]Umaasumu wa Maimamu ni miongoni mwa masharti sifa za Uimamu katika mtazamo wa Mashia Ithaashariyah na ni katika itikadi zao za kimsingi. [2] Kwa mujibu wa nukuu ya Allama Majlisi ni kuwa, Mashia Imamiyyah wameafikiana kwamba, Maimamu (a.s) wana kinga na Umaasumu wa kutofanya madhambi makubwa kwa madogo, iwe ni kwa makusudi au kwa kusahau na kamwe si wenye kufanya kosa. [3] Inaelezwa kuwa, Shia Ismailiyah nao wanatambua Umaasumu kama sharti la Uimamu. [4] Mkabala na wao kuna Waislamu wa Ahlu-Sunna ambao hawalitambui suala la Umaasumu na kinga ya kutotenda dhambi kama ni sharti la Uimamu [5], kwani wao wana ijma'a na kauli moja kwamba, makhalifa watatu (Abu Bakr, Omar na Othman) walikuwa Maimamu; lakini hawakuwa Maasumu. [6] Wao badala ya Umaasumu, wameutambua uadilifu kama sharti la Uimamu. [7] Pamoja na hayo, Sibt bin Jawzi, mmoja wa Maulamaa wa Ahlu-Sunna wa karne ya Saba, ameukubali Umaasumu wa Imam. [8] Mawahabi nao hawakubaliani na suala la Umaasumu wa Imam na Maimamu wa Mashia na wanaamini kwamba, hiyo ni sifa makhsusi kwa Mitume tu. [9] Ibn Abil-Hadid mfuasi wa kundi la Mu’tazilah anunukuu na kusema kuwa, Abu Muhammad Hassan bin Ahmad bin Mattawayh, mwanateolojia wa kundi la Mu’tazilah wa karne ya 5 Hijiria, licha ya kuwa hakuwa akitambua Umaasumu kama sharti la Uimamu, lakini amebainisha wazi kuhusiana na Umaasumu wa Ali (a.s) na kulitambua hilo kama mtazamo wa fikra za Mu’tazilah. [10]

Kwa mujibu wa Ayatullah Ja'far Subhani, tofauti hii ya maoni chimbuko lake ni imani ya makundi mawili ya Shia na Sunni kuhusu Uimamu na ukhalifa wa Mtume. Kwa mtazamo wa Mashia, Uimamu, kama ulivyo Utume, ni nafasi na wadhifa unaotoka kwa Mwenyezi Mungu, na Mungu lazima ateue mtu wa kuchukua jukumu hilo. [11] Lakini kwa mtazamo wa Sunni, Uimamu ni nafasi na cheo cha kiada [12] na kwamba, Imamu anachaguliwa na watu na elimu yake na uadilifu upo katika kiwango sawa na cha watu wengine katika jamii na kwamba, hateuliwi na Mwenyezi Mungu. [13]

Umaasumu wa Maimamu unatambuliwa kuwa moja ya misingi ya kiitikadi na kiteolojia ya elimu ya Usul-al-Fiq'h ya Shia; kwani Umaasumu wa Maimamu, Sunna ya Imam (neno kauli, kitendo chake na taqriri) katika elimu ya Usul al-Fiq'h inatambuliwa rasmi kama moja ya vyanzo vya kuchukulia sheria (kunyambulia); lakini kama Umaasumuu wa Maimamu hautathibitishwa, haiwezekani kutumia Sunna zao katika kunyambua hukumu za sheria. [14] Kadhalika inaelezwa kuwa, kwa mujibu wa mtazamo wa Maulamaa wa Kiishia ni kwamba, kigezo cha kuwa hoja na kusihi ijma'a ni Umaasumu wa Imam; kwani kwa uoni wao ni kwamba, Imam ni mrithi na kiongozi baada ya Mtume na kama alivyo Mtume na yeye ni Maasumu.

Utambuzi wa Maana (Conceptology)

Umaasumu wa Maimamu maana yake kulindwa kwao na kutenda aina yoyote ya dhambi au kosa. [15] Umaasumu katika istilahi ya wanatheolojia na wanafalsafa wa Kiislamu kilugha ina maana ya kulindwa na kukingwa; [16] hata hivyo kwa mujibu wa misingi yao, kumetolewa fasili na maana tofauti kuhusiana na Umaasumu. Baadhi ya fasili na maana hizo ni:

  • Fasili na maana iliyotolewa na wanateolojia: Wanatheolojia wa Adliyah (Imamiyyah na Mu'tazilah) [17] wameitambulisha isma kuwa ni ukarimu na wema wa Mwenyezi Mungu na wanafalsafa wa Kiislamu wao wanasema ni uwezo na nguvu ya kinafsi ambayo inamfanya Maasumu aepukane na dhambi na kufanya makosa. [18] Kwa msingi huo, isma au Umaasumu maana yake ni ukarimu wa Mwenyezi Mungu ambao amempatia mja wake na kupitia kwake hafanyi mambo mabaya au dhambi. [19]
  • Fasili na maana iliyotolewa na wanafalsafa: Wanafalsafa wa Kiislamu wametoa maana ya Umaasumu kwamba, ni nguvu na uwezo wa kinafsi ambayo kwa uwepo wake, mwenye Umaasumu hafanyi dhambi. [20]

Wigo Mpana

Wanachuoni wa Imamiyya wanaamini kwamba Maimamu wa Shia, kama walivyo Mitume, ni Maasumu na wameepushwa na aina yoyote ile ya madhambi makubwa au madogo, yawe ya kukusudia au kutokana na kughafilika na kusahau, na wamekingwa kutokana na kukosea na kufanya makosa yoyote. [21] Kwa mujibu wa mtazamo wao ni kwamba, Maimamu (a.s) ni Maasumu katika maisha yao yote, kabla na baada ya Uimamu [22] Fayaz Lahiji, pamoja na Umaasumu na kutofanya dhambi na makosa, wana Umaasumu (kinga) ya kasoro za kimwili, kiakili, kisaikolojia na kifamilia (kinasaba) na kwamba, hilo sharti kwa Imamu. Kwa mujibu wake ni kwamba Imamu hatakiwi kuugua magonjwa ya muda mrefu au ya kuchukiza kimwili, kama vile ukoma na kuwa bubu, au kasoro za kihisia na kinafsi kama vile ubakhili, na utumiaji mabavu (ukatili), au kasoro za kiakili kama vile wazimu, ujinga, usahaulifu na kasoro za kinasaba. Sababu yake ni kwamba kasoro hizi huwafanya watu kuwachukia Maimamu (a.s) na kutokuwa na raghba nao na haya ni mambo ambayo hayaendani na wajibu wa kuwatii. [23]

Sheikh Mufid ameona kuwa inajuzu kiakili kwa Imam kuacha jambo la mustahabu kwa kusahau hata hivyo anaamini kuwa, katika maisha yao yote hakuna wakati ambao Maimamu waliacha jambo la mustahabu. [24]

Abdullah Javad Amoli, ameugawa Umaasumu katika sehemu mbili za kivitendo na kielimu na kueleza kwamba, Maimamu (a.s) wamekusanya aina zote hizi mbili. Anasema kuwa, kama ambavyo miamala na mienendo ya Maimamu inaendana na haki, elimu yao pia ni ya haki na iko kwa namna ambayo, hakuna uwezekano wa kufanya kosa lolote au kusahau katika njia hiyo. [25] Kwa mtazanmo wake ni kwamba, kila ambaye amefikia daraja ya Umaasumu wa kivitendo, amehifadhika na ushawishi wa shetani na kwamba, shetani hawezi kupenya na kuuingia katika fikra zake na kufanya atakacho. [26]

Ali Rabani, mtafiti wa elimu ya theolojia anasema: Umaasumu wa kivitendo ndio ule Maasumu wa kutotenda dhambi na Umaasumu wa kielimu una madaraja yafuatuayo:

  1. Umaasumu katika kutambua hukumu za Mwenyezi Mungu.
  2. Umaasumu katika kufahamu maudhui za hukumuu za Mwenyezi Mungu.
  3. Umaasumu katika kuainisha maslahi na ufisadi wa mambo yanayohusiana na uongozi wa jamii.
  4. Umaasumu katika mambo yanayohusiana na maisha ya kawaida mbali na masuala ya mtu binafsi na ya kijami. [27]

Kwa mtazamo wake ni kuwa, Maimamu wa Kishia wanayo madaraja yote haya. [28]

Hoja za Wajibu wa Kumtii Imam

Kwa mujibu wa hoja mbalimbali kama Aya ya Ulul-Amr, ni wajibu kumtii Imam; [29] kwa namna ambayo baadhi wamelitambua suala la wajibu wa kumtii Imam kwamba, ni jambo walilokubaliana Waislamu (ijma'a). [30] Sasa kama Imam hatokuwa Maasumu na akawa ni mwenye kufanya dhambi au akateleza, kumtii ni haramu na kwa mujibu wa mafundisho ya kuamrishana mema na kukatazana maovu, itakuwa wajibu kumkataza asitende dhambi; katika hali hii kwa upande mmoja ni lazima kumpinga Imam na kwa upande mwingine ni lazima kumtii, jambo ambalo haliwezekani; kwa muktadha huo Imam ni lazima awe Maasumu. [31]

Hoja ya Qur'an

Ili kuthibitisha Umaasumu wa Maimamu kumetumika Aya kadhaa ikiwemo Aya ya Ibtilaa (majaribu) Ibrahim, Aya ya Ulul-Amr, Aya ya Tat'hir, Aya ya Swadiqin, [32] Aya ya Mawaddah, [33] na Aya ya Swalawat (kumswalia Mtume). [34]

Aya ya Ibtilaa (majaribu)

Makala kuu: Aya ya Ibtilaa Ibrahim
وَ إِذِ ابْتَلی إِبراهیمَ رَبُّه بِکلماتٍ فَأتَمَّهُنَّ قالَ إِنّی جاعِلُک لِلنّاسِ إِماماً قالَ وَمِنْ ذُرّیتی قالَ لاینالُ عَهدی الظّالِمینَ


...Na Mola wake Mlezi alipo mjaribu Ibrahim kwa kumpa amri fulani, naye akazitimiza, akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya uwe kiongozi wa watu (Imam). Akasema: Je, na katika vizazi vyangu pia? Akasema: Ahadi yangu haitawafikia wenye kudhulumu.



(Quran: 2: 123)


Katika kutumia Aya hii kama hoja, imeelezwa kwamba, kuelezwa kiujumla kwamba: " Ahadi yangu haitawafikia wenye kudhulumu", ni ishara kwamba, mtu ambaye kwa namna yoyote atakapokuwa dhalimu, Uimamu hamjumishi yeye. Kwa msingi huo, Aya hii inaonyesha na kuthibitisha Umaasumu wa Imam wakati wa Uimamu na kabla ya hapo. [36] Fadhil Miqdad anaitumia Aya hii kama hoja kwa kubainisha kwamba: Asiyekuwa Maasumu ni dhalimu; dhalimu hana ustahiki wa kuwa Imam; asiyekuwa Maasuumu hana sifa za Uimamu. Kwa minajili hiyo, Imam ni lazima awe Maasumu. [37] Maulamaa wa Kishia wanasema kuwa, makusudio ya "ahadi" katika Aya hiyo ni Uimamu. [38]

Aya ya Ulul-Amr

Makala kuu: Aya ya Uluul-Amr
...يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَطِيعُواْ اللّهَ وَأَطِيعُواْ الرَّسُولَ وَأُوْلِي الأَمْرِ مِنكُمْ


...Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi (wenye mamlaka juu yenu).



(Quran: 4: 59)


Maulamaa wa Kishia wakitumia Aya hii kama hoja wamesema: Katika Aya hii watu wametakiwa kuwatii Ulul-Amri bila sharti. Kutokana na dalili na uthibitisho wa Aya ya Ulul-Amr wa kutilia mkazo na msisitizo juu ya wajibu wa kuwatii Ulul-amr bila sharti lolote, kwa hakika Aya hii inathibitisha suala la kuhifadhika na Ismah hawa Ulul-amr. Kwani kama Ulul-Amr wasingekuwa Maasumu na wakawa ni watu wenye kufanya dhambi na kukosea, basi hekima ya Mwenyezi Muungu ingekuwa inalazimu asiamrishe watiiwe kwa sura mutlaki na bila ya sharti. [40] Kwa mujibu wa hadithi mbalimbali [41] Mashia wanaamini kwamba, makusudio ya Ulul-Amr ni Maimamu wa Kishia. [42]

Aya ya Tat'hir (utakaso)

Makala kuu: Aya ya Tat'hir


إِنَّمَا یُرِیدُ اللهُ لِیُذْهِبَ عَنْکُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَیتِ وَ یُطَهِّرَکُمْ تَطْهِیراً


...Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukusafisheni baarabara.



(Quran: 33: 33)


Aya hii pia imetumiwa kama hoja ya kuthibitisha Umaasumu wa Maimamu (a.s). [44] Baadhi hoja za Aya hii zilizobainishwa ni:

  • Mosi: Makusudio ya Ahlul-Bayt (a.s) katika Aya ya Tat'hir ni Watu watano wa Kisaa (watu wa Kishamia).
  • Pili: Aya hii inatoa habari kuhusiana na takwa na irada ya Mwenyezi Mungu kwamba, anataka kutakasa na kuondoa uchafu kwa Ahlul-Bayt (a.s).
  • Tatu: Mbali na kuweko irada ya kuondoa uchafu, ilikuwa ikimpitikia katika fikra zake kutimia kwa kitendo hiki; kwani Aya ipo katika nafasi ya kubainisha daraja na sifa za Ahlul-Bayt (a.s). [45]
  • Nne: Kuondolewa uchafu Ahlul-Bayt (a.s) maana yake ni wao kuwa na Umaasumu. [46] Kwa mujibu wa hadithi mbalimbali zilizonukuliwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia [47] na Ahlu-Sunna [48], Aya ya Tat'hir ilishuka kwa Ahlul-Kisaa (watu wa Kishamia). Kwa msingi huo, makusudio ya Ahlul-Bayt katika Aya hii ni watu waliokuwa katika Kishamia (Mtume, Ali, Fatma, Hassan na Hussein). [49]

Hoja ya Hadithi

Kuna hadithi nyingi kama Hadithi ya vizito viwili (Hadith Thaqalayn) na Hadithi ya Safina za kuthibitisha Umaasumu wa Maimamu ambazo zimenukuliwa kupitia masahaba na Maimamu (a.s). [50] Baadhi ya hadithi hizo zinazotumiwa na Mashia kuthibitisha madai yao haya ni:

Hadithi ya Vizito Viwili (Hadith al-Thaqalayn)

Makala kuu: Hadith al-Thaqalayn

Hadithi hii imebainisha wazi juu ya kutotengana Qur'an na Ahlul-Bayt (a.s) katika ibara isemayo: «لَنْ يَفْتَرِقَا حَتَّي يَرِدَا عَلَيَّ الْحَوْض» ; Havitatengana kamwe mpaka vitakaponijia huko kwenye hodhi (ya kauthar).

Hii ni ithbati juu ya Umaasumu wa Ahlul-Bayt; kwani kufanya dhambi yoyote au kukosea, kutawafanya watengane na Qur'an. [51] Kadhalika katika hadithi hii, Mtume wa M.mungu amebainisha bayana kwamba, kila ambaye atashikamana na Qur'an na Ahlul-Bayt (a.s) kamwe hatapotea. Ibara hii nayo inaonyesha Umaasumu wa Ahlul-Bayt; kwani kama wasingekuwa Maasumu kushikamana nao na kuwafuata kwa sura ya mutlaki (bila sharti) kungepelekea kupotea. [52] Kwa maneno mengine ni kuwa, hadithi hii inathibitisha wajibu wa kuwatii Ahlul-Bayt (a.s) na wajibu wa kuwatii ni dalili na hoja ya kuuwa kwao Maasumu. [53]

Katika hadithi zilizopokewa na Waislamu wa Kishia, Ahlul-Bayt katika hadithi ya Thaqalayn imefasiriwa kuwa ni Maimamu wa Shia [54], baadhi ya Ahlu-Sunna, [55] wanasema, makusudio ya Ahlu-Bayt ni Ahlu-Kisaa huku baadhi [56] wakisema kielelezo cha wazi cha hilo ni Imam Ali (a.s).

Baadhi ya wanatheolojia wa Kishia wameihesabu Hadithi ya Vizito Viwili kuwa ni katika hadithi mutawatir na wanaamini kwamba, hakuna shaka katika usahihi wa hadithi hii. [57] Baadhi yao wameihesabu kuwa ni mutawatir maanawi. [58]

Hadithi ya Amani

Makala kuu: Hadithi ya amani

Hadithi ya amani ni hadithi mashuhuri iliyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) na Mashia [59] na Ahlu-Sunna [60]. Hadithi hiyo ni kama ifuatavyo ikiwa na tofauti kidogo: «النُّجُومُ أَمَانٌ لِأَهْلِ السَّمَاءِ وَ أَهْلُ بَيْتِی أَمَانٌ لِأُمَّتِی ; Nyota ni amani kwa watu wa mbinguni na Ahlul-Bayt wangu ni amani kwa umati wangu.

Katika kuelezea kuwa hadithi hii ni hoja imeelezwa kuwa, Mtume wa Mwenyezi Mungu amewafananisha Ahlul-Bayt wake na nyota na kuwatambulisha kwamba, wao ni sababu ya amani kwa umma au kwa watu wa ardhini. Maneno haya ya Mtume ambayo hayana sharti yanaonyesha kuwa, wao ni sababu ya kupatikana amani na yanathibitisha Umaasumu wa Ahlul-Bayt; kwani bila ya Umaasumu hiki ni kitu ambacho hakiwezekani. [61]

Katika hadithi iliyonukuliwa katika kitabu cha Kifayat al-Athar, Ahlul-Bayt imefasiriwa kwa maana ya Maimamu (a.s) na suala la kuwa kwao Maasumu limebainishwa na kuwekwa wazi. [62] Hakim Neyshabouri, mmoja wa wapokezi wa hadithi wa Ahlu-Sunna katika karne ya 4 Hijria ameitambua hadithi ya amani kuwa ni sahihi kimapokezi (kisanadi). [63]

Hadithi ya Safina

Makala Asili: Hadithi ya Safina

Hadithi mashuhuri ya Safina inatoa ashirio na ithbati juu ya wajibu wa kuwafuata Ahlul-Bayt na kuwatii; kwani kwa mujibu wa hadithi hii, kuokoka wafuasi wao kunafungamana na kuwafuata wao, na kuangamia kwao kunatokana na wao kuwaasi na kutowafuata. Katika hadithi hii Mtume (s.a.w.w) amewafananisha Ahlul-Bayt wake na safina ya Nabii Nuhu (a.s).

Hadithi mashuhuri ya Safina imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume katika vyanzo mbalimbali vya Kishia [64] na Kisuni [65] ikiwa na tofauti kidogo: «إِنَّمَا مَثَلُ أَهْلِ بَیتِی فِیکُمْ کَمَثَلِ سَفِینَةِ نُوحٍ مَنْ رَکِبَهَا نَجَی وَ مَنْ تَخَلَّفَ عَنْهَا غَرِقَ؛ ; Hakika mfano wa Ahlul-Bayt wangu ni mithili ya Safina ya Nuhu (a.s). Anayepanda ndani ya Safina anaokoka na yule asiyepanda anaangamia

Mfananisho na mshabaha huu maana yake ni kwamba, kila ambaye atarejea kwa Ahlul-Bayt ataongoka na ambaye hatowafuata atapotea. Baadhi wameitambua hadithi hii kwamba, ni mutawatir. [66] Hakim Neyshabouri pia ameitambua hadithi hii kwamba, ni sahihi. [67]

Chimbuko la Imani ya Umaasumu

Kuhusiana na chimbuko na chanzo cha Umaasumu na sababu ya kinga ya kutotenda dhambi au kutofanya makosa, kuna mitazamo tofauti ambayo imebainishwa kuhusiana na hilo ambayo ni kama vile ni ukarimu wa kiungu aliyopatiwa Maasumu, elimu maalumu ya Maasumu kuhusiana na matokeo ya dhambi na irada na chaguo la Maasumu. Baadhi ya wapinzani wa Umaasumu wa Maimamu wanaamini kwamba, mwanzoni mwa Uislamu itikadi hii haikuweko, bali ilikuja baadaye. Kwa mfano Ibn Taymiyyah anasema, itikadi ya Umaasumu wa Imam chimbuko lake ni Abdalla bin Saba na ilikuwa ni bidaa yake. [68] Kwa mtazamo wa Nasir al-Qaffari ni kwamba, kwa mara ya kwanza itikadi hii ililetwa na Hisham bin al-Hakam. [69] Sayyid Hussein Modarresi Tabatabai, mtafiti wa Kishia na Kiirani wa elimu za Kiislamu ameandika katika kitabu chake cha Maktab dar Farayand takamol kwamba, fikra ya Umaasumu chimbuko lake ni Hisham bin al-Hakam. [70]

Al-Qaffari anaamini kwamba, Mawahabi kutokana na chuki na upinzani walionao dhidi ya Shia, wameinasibisha fikra ya Umaasumu na Abdallah bin Saba ambapo kwa upande wa kihistoria hilo sio sahihi. Aidha amesema: Mimi nimefuatilia na kufanya uchunguzi lakini sijapata maneno kama haya kutoka kwake. [71] Umaasumu wa Maimamu na asili ya neno Umaasumu si katika mambo yaliyoletwa na Hisham bin al-Hakam pia; kwani suala la Umaasumu limebainishwa na kuelezwa katika hadithi mbalimbali zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) na Maimamu kuhusiana na Umaasumu wa Maimamu (a.s). [72] Kwa mfano, Imam Ali (a.s) amebainisha katika hadithi moja kwamba, Umaasumu ni katika alama za Imam. [73] Imam Sajjad (a.s) katika hadithi aliyonukuu kutoka kwa baba yake Imam Hussein (a.s) anaseema: Mtume anawatambulisha Maimamu (a.s) kuwa ni Maasumu. [74] Katika vyanzo na vitabu vya Ahlu-Sunna pia, Abdallah bin Abbas amenukuu kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwamba, mimi, Ali, Hassan na Hussein ni wasafi, watoharifu na Maasumu. [75]

Umaasumu wa Maimamu na Ughulati

Nasir al-Qaffari mmoja wa wahakiki wa Kiwahabi wa Saudi Arabia na baadhi ya wengine [76] wanasema, kuwa kuwatambua Ahlul-Bayt kwamba, ni Maasumu ni ughulati. [77] Mashia wanaamini kwamba, maghulati ni watu ambao wametoka nje ya uwiano na wamechupa mipaka kuhusiana na fadhila za Ahlul-Bayt (a.s) na kuwahesabu kuwa na daraja ya uungu na kuwapa sifa maalumu za Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, Mashia hawana itikadi kama hii kuhusiana na Ahlul-Bayt. [78] Mashia wanaamini kwamba, Umaasumu ni kama sifa nyingine za ukamilifu za Mwenyezi Mungu; hata hivyo Mwenyezi Mungu amewapa baadhi ya waja wake ambao ni waongozaji msaada wa Umaasumu.

Bibliografia

Kumeandikwa vitabu na makala mbalimbali kuhusiana na Umaasumu wa Imam na Umaasumu wa Maimamu na baadhi ya vitabu hivyo:

  • Pezhuheshi dar shenakht va esmat Imam, Sheikh Ja’far Subhani.
  • Esmat Imam dar tafakkor Imamiyeh, mwandishi Muhammad Hussein Qaryab.
  • Esmat Imaman az didgah Aqal va wahy.
  • Emamat va Esmat Emaman dar Qur’an, Reza Kardar.
  • Qur’an va Esmat Ahlul-Bayt, Ali Reza Azimfar.