Muftaradh al-Ta'a

Kutoka wikishia

Muftaradh al-Ta'a (Kiarabu: مُفْتَرَضُ الطَّاعَة) ni daraja na cheo maalumu kwa ajili ya Maimamu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia na ina maana ya mtu ambaye ni wajibu kumtii na kumfuata kwa sura mutlaki, yaani bila ya sharti lolote. Wanazuoni wa Kishia wakitegemea Aya za Qur'ani na hadithi kama vile Aya ya Ulul-Amr, Hadithi ya Thaqalaini (hadithi ya Vizito Viwili), Hadithi ya Safina na Hadithi ya Manzila, wanawatambua Maimamu kwamba, ni watu ambao ni wajibu kuwatii. Baadhi yao kama Sheikh Tusi sambamba na kuthibitisha wajibu wa kutiiwa Imamu Ali (a.s) wanalitumia hilo kama hoja ya kuthibitisha Uimamu wake.

Katika vyanzo vya hadithi vya Waislamu wa madhehebu ya Shia, mbali na hadithi zilizotangulia, kuna hadithi zingine ambazo zinabainisha wazi na bayana kwamba, ni wajibu kuwatii Maimamu. Katika kitabu cha al-Kafi sehemu ya kitabu hiki imezungumzia hili na kuhusiana na hilo kumenukuliwa hadithi 17.

Hata hivyo katika hadithi kadhaa inaelezwa kuwa, Maimamu wenyewe hawakuwa wakiamini kwamba, ni wajibu wao kutiiwa; hata hivyo Maulamaa wa Kishia hawajazikubali hadithi hizi. Baadhi ya wahakiki wanasema kuwa, hadithi hizi zilitolewa kutokana na taqiya.

Utambuzi wa maana

Muftaradh al-Ta'a ina maana ya mtu ambaye ni wajibu kumtii na kumfuata kwa sura mutlaki yaani bila ya sharti lolote. [1] Maulamaa wa Kishia wanakitambua cheo na daraja hii kwamba, ni maalumu kwa ajili ya Maimamu. [2] Allama Majlisi anaona kuwa, "kuwa wajibu kutiiwa" ni katika mambo ya lazima ya Uimamu na amesema kuwa, hadithi ya Manzila inaashiria hili. [3] Kuna baadhi pia ambao wamesema, kimsingi maana ya Uimamu na Ukhalifa wa Mwenyezi Mungu ni hii hii daraja ya kuwa wajibu kutiiwa. [4]

Hoja za kuwa wajibu kutiiwa Maimamu

Wanazuoni wa Kishia wakitegemea Aya tofauti na hadithi mbalimbali wanaona kuwa, Maimamu ni watu ambao kuwatii ni jambo la wajibu. Aya ya Ulul-Amr, Hadithi ya Thaqalaini (Hadithi ya Vizito Viwili), Hadithi ya Safina na Hadithi ya Manzila ni miongoni mwa Aya na hadithi ambazo wamechukua natija kwazo kwamba, Maimamu ni watu ambao kuwatii ni wajibu (Muftaradh al-Ta’a).

Aya ya Ulul-Amr

Kwa mujibu wa Aya hii: ((أَطیعُوا اللَه وَ أَطیعُوا الرَّسُولَ وَ أُولِی الْأَمْرِ مِنْكُمْ ; Enyi mlio amini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi)). [5] Kando ya kumtii mwenyezi Mungu na Mtume wake, kutiiwa Ulul-Amr kumetambuliwa kuwa ni wajibu bila sharti lolote. [6] Allama Tabatabai anasema, kuunganishwa Ulul-Amr na Mtume katika Aya bila ya kukaririwa kitendo "mtiini" ni ishara kwamba, kama ambavyo kumtii Mtume ni wajibu mutlaki, basi kuwatii Ulul-Amr, pia ni wajibu mutlaki, yaani bila sharti lolote. [7] Maulamaa wa Kishia kwa mujibu wa hadithi, wanaamini kwamba, Ulul-Amr ni Maimamu kumi na mbili. [8]

Hadithi ambazo zinaashiria Muftaradh al-Ta’a

Katika Hadithi ya Thaqalaini (Vizito Viwili, Ahlul-Bayt (a.s) wamewekwa kando (pamoja) ya Qur’an. Kama ambavyo kuifuata Qur’an ni wajibu kwa Waislamu, basi vivyo hivyo, kuwatii Ahlul-Bayt (a.s) pia ni wajibu. [9] Abu al-Salah Halabi anasema, fakihi na mwanateolojia wa Kishia wa karne ya 4 na 5 Hijiria anasema kuwa: kutokana na maneno ya Mtume kuwa mutlaki katika hadithi ya Thaqaleyn, wajibu wa kuwatii Ahlul-Bayt pia hauna sharti lolote. Kwa muktadha huo, Waislamu wanapaswa kuwafuata Ahlul-Bayt (a.s) katika maneno, amali na matendo yao yote bila ya masharti yoyote. [10]

Hadithi ya Safina pia ina ishara na hoja ya wajibu wa kuwafuata na kuwatii Ahlul-Bayt (a.s); kwani kwa mujibu wa hadithi hii kuokoka kuko katika kuwatii na kuangamia na kupotea kuko katika kutowafuata. [11] Mir Hamid Hussein anasema kuwa, kwa mujibu wa hadithi hii, wajibu wa kuwatii Ahlul-Bayt (a.s) ni mutlaki na bila masharti. [12]

Baadhi ya Maulamaa kama Sheikh Tusi na Abu al-Salah Halabi, kupitia hadithi ya Manzila na kuthibitika wajibu wa kutiiwa Imamu Ali (a.s) wanalitumia hilo kama hoja ya kuthibitisha Uimamu wake. [13] Sheikh Tusi ameandika, Mtume (s.a.w.w) katika hadithi ya Manzila aliitambulisha nafasi ya Imamu Ali kwake kama ya Haruna kwa Mussa. Kwa kuzingatia kwamba, Harun alikuwa mrithi wa Mussa, alikuwa "Muftaradh al-Ta’a" (mtu ambaye ni wajibu kutiiwa), Imamu Ali (a.s) pia ni wajibu kumtii na hivyo hilo linathibitisha ni Imamu. [14]

Hadithi ambazo zinabainisha wazi "Muftaradh al-Ta’a"

Katika vitabu vya hadithi, kuna hadithi ambazo zinaeleza na kubainisha wazi kwamba, Maimamu ni Muftaradh al-Ta’a, yaani wanapaswa kutiiwa. Muhammad bin Ya’qub Kulayni, katika kitabu chake cha al-Kafi katika mlango wa "Bab Faradh taati al-Aimah" (Mlango wa wajibu kutiiwa Maimamu) amenukuu hadithi 17 kuhusiana na maudhui hii. [15] Katika moja ya hadithi hizi, Imam Swadiq (a.s) anatoa ushahidi wa kuwa wajibu kutiiwa Maimamu wa kabla yake na kuwatambulisha kuwa ni Maimamu ambao Mwenyezi Mungu amefanya wajibu na faradhi kuwatii. [16] Katika hadithi hiyo Imam Swadiq anaeleza pia kwamba, kwa kipindi kirefu Nabii Ibrahim alikuwa akishushiwa Wahyi na Mwenyezi Mungu, lakini haikuwa ni wajibu kumtii (hakuwa Muftaradh al-Ta’a), mpaka pale Mwenyezi Mungu alipotaka kumtukuza na kunyanyua daraja aliposema: ((إِنِّي جٰاعِلُكَ‌ لِلنّٰاسِ‌ إِمٰاماً ; Hakika Mimi nimekufanya Imamu wa wa watu)). Nabii Ibrahim akasema: ((وَ مِنْ‌ ذُرِّيَّتِي ; Je, na katika vizazi vyangu pia?)) Mwenyezi Mungu akamwambia: ((لاٰ يَنٰالُ‌ عَهْدِي اَلظّٰالِمِينَ‌ ; Ahadi yangu haitawafikia wenye kudhulumu)). [17]

Katika kitabu cha Bihar al-Anwar, Allama Majlisi pia amenukuu hadithi kutoka kwa Imam Ridha (a.s) akisema kuwa, daraja na cheo hiki kilifikishiwa Umma katika zama za uhai wa Mtume (s.a.w.w) na siku ya Ghadir ikachukuliwa ahadi na kiapo cha utii kutoka kwao. [18]

Kuna ripoti pia katika vitabu vya hadithi ambamo ndani yake zinaonyesha kuwa, kuna watu wanatoa ushahidi wa Maimamu kuwa ni wajibu kuwatii na Maimamu wanalikubali hilo. [19]

Hadithi zinazopinga

Katika vyanzo vya hadithi vya Kishia, kuna hadithi pia ambazo zinaonyesha kuwa, Maimamu wa Kishia walipinga suala la kwamba, wao ni Muftaradh al-Ta’a (ni wajibu kuwatii). Miongoni mwazo ni hadithi iliyonukuliwa na Sheikh Tusi. Katika hadithi hii, watu wawili walimuendea Imam Swadiq (a.s) na mmoja wao akamuuliza: Je, Imamu ambaye ni wajibu kumtii ni kutoka katika nyinyi? Imamu akajibu kwa kusema: Simfahamu mtu kama huyu miongoni mwetu. Kisha, mtu huyu anasema: Kuna kundi la watu huko Kufa ambalo linatambua kwamba; Imamu ambaye ni Muftaradh al-Ta’a anatoka katika nyinyi. Imam Swadiq akasema: "Sisi hatujawaamrisha jambo hilo". [20]

Kadhalika Sheikh Mufid ameandika katika kitabu cha al-Ikhtisas: Imam Kadhim (a.s) ameitambua itikadi ya kwamba, "Maimamu ni watu ambao ni wajibu kuwatii" kwamba, ni katika itikadi za maghulati na amelipinga na kulikataa hilo. [21]


Mtazamo wa Maulamaa wa Kishia kuhusu hadithi zinazopinga

Maulamaa na wanazuoni wa Kishia hawazikubali hadithi ambazo zinapinga suala la kwamba, Maimamu ni Muftaradh al-Ta’a na wanaamini kwamba, Maimamu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ni Muftaradh al-Ta’aa (wajibu kuwatii). [22] Sheikh Saduq, Sheikh Mufid na Sheikh Tusi wakitegemea hadithi ya Manzila, wamewatambua Maimamu kwamba, ni Muftaradh al-Ta’a. [23]

Baadhi ya wahakiki wamesema, hadithi ambazo hazikubaliani na suala la Maimamu kuwa ni Muftaradh al-Ta’a zinatokana na suala la taqiya. Wanasema kuwa, itikadi ya Maimamu kuwa ni Muftaradh al-Ta’a ilienea katika zama za Imamu Swadiq na Kadhim (a.s) na ni kwa sababu hiyo ndio maana hilo likawafanya makhalifa na watawala wa Kiabbasi kuwa na unyeti na jambo hilo; kwani itikadi hiyo haikuwa ikiendana na siasa zao. [24]