Tukio la Saqifa

Kutoka wikishia

Tukio la Saqifa ya Bani Saa'idah (Kiarabu: واقعة سقيفة بني ساعدة) lilikuwa ni tukio la kwanza baada ya kifo cha Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) lililotokea katika mwaka wa 11 Hijiria, ambapo Abu Bakar bin Abi Quhafa alichaguliwa kuwa khalifa wa Waislamu. Baada ya kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w.w), Imam Ali (a.s) na baadhi ya Masahaba walikuwa wakiiandaa mwili wa bwana Mtume (s.a.w.w) kwa ajili ya maziko yake, wakati huo huo, baadhi ya Ansari, wakiongozwa na Sa'ad bin Ubadah -mkuu wa kabila kubwa la Khazraj-, walikusanyika katika Saqifa ya Bani Saa'idah ili kufanya maamuzi ya kumchagua kiongozi atakayeongoza baada ya Mtume (s.a.w.w).

Kwa mujibu wa ufafanuzi wa baadhi ya wanahistoria; Mkusanyiko huu wa Maansari ulikuwa na nia ya kumchagua mtawala wa mji wa Madina tu. Lakini baadhi ya Muhajirina (wahajiri waliotoka Makka na kuhamia Madina), walipoingia kwenye mkutano huo, mijadala iliyopita baina yao ilibadilisha mwelekeo. Kwa hiyo muelekeo wa mkutano huo ukabadilika na kuaelekea kwenye suala la kumteuwa mrithi wa bwana Mtume (s.a.w.w), ambaye atawaongoza Waislamu wote bila ya kuzingatia miji wanaoishi Waislamu hao. Hatimaye, Abu Bakar akaungwa mkono na watu wakampa kiapo cha kumtii yeye kama ndiye kiongozi na Khalifa wa Waislamu. Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria, ukiachana na Abu Bakar ambaye alizungumza kwa niaba ya wahajiri, Omar Ibn Khattab na Abu Ubaidah Jarraah (‘Aamir bin Abdullah bin Jarraah) pia walikuwepo katika mkutano wa Saqifah.

Masunni ili kuhalalisha uongozi na Ukhalifa wa Abu Bakar, wametegemea msingi wa hoja ya makubaliano au mawafikiano ya Waislamu (Ijma'u Al-Muslimina). Hii ni pamoja na ukweli wa kwamba, kwa mujibu wa wanahistoria, mchakato wa kumteuwa Abu Bakar haukupita na kuungwa mkono na Waislamu wote. Baada ya tukio la uteuzi wa Abu Bakar, kulitokea watu wengi waliopingana na jambo hilo, miongoni mwao ni: Ali bin Abi Talib, (a.s), Fatima Zahraa (a.s), Fadhlu bin Abbas na Abdullah ambao ni watoto wa Abbas (ami yake Mtume). Pia kuna Masahaba kadhaa mashuhuri wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), walilalamikia na kupingana na uteuzi huo uliofanyika katika mukutano wa Saqifah, miongoni mwa ni: Salman Farsi, Abu Dharr al-Ghifari, Miqdad bin Amru, Zubeir bin Awam na Hudhaifa bin Yaman. Mashia wanalichukulia tukio la mkutano wa Saqifah pamoja matokeo ndani yake, kuwa ni kinyume na maneno ya Mtume (s.a.w.w) kuhusu nafasi ya urithi wa Ukhalifa wa Imam Ali (a.s), hususan ukizingatia tukio la Ghadir Khum.

Tukio la Saqifah halikupotea kutoka katika jicho la vyanzo vya kihistoria. Pia kuna maandishi chungu nzima yalioandikwa katika kulichunguza na kulitafiti tukio hilo. Wataalamu na watafiti wanaotafiti masuala na tamaduni za Kimashariki kama vile Henry Lamans, Caitani na Wilferd Madelung, nao pia wamenukuu na kulichambua tukio hilo la Saqifah. Kitabu The Succession to Muhammad cha Madelong ni miongoni mwa vitabu maarufu zaidi vya Wamagharibi wilotafiti suala ya Saqifah.

Mahali pa tukio

Mahali pa Saqifa Bani Sa'idah katika karne ya 15 AD.
Makala Asili: Saqifa Bani Saa'idah

Saqiyfah ilikuwa ni sehemu zenye umbo la jukwaa au paa (kama banda), sehemu ambazo zilikuwa zikitumiwa na koo au makabila ya Waarabu. Waarabu walikuwa na kawaida ya kukusanyika katika mabanda hayo kwa ajili ya kushauriana na kutoa maamuzi fulani kuhusiana na jamii. [1] Saqifah au banda walilikutania baadhi ya Maansari na Wahajiri baada ya kufariki Mtume (s.a.w.w), lilikuwa ni banda la ukoo wa Bani Saa'idah, ukoo ambao unatokana na shina la kabila la Wakhazraj wanaoishi Madina, ambapo tokea mwanza na hata kabla ya kuhama kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kutoka Makka kwenda Madina, watu wa ukoo huu, walikuwa wakifanyia mikutano yao katika banda hilo la Bani Saa'idah. Baada ya Mtume (s.a.w.w) kuhamia Madina, sehemu hii ilibaki bila matumizi kwa muda wa miaka kumi (mpaka kifo cha Mtume), ambapo Wahajiri (Muhajirina) na Maansari walipokusanyika ili kuamua mrithi wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), kwama nyengine tena watu wakakusanyika kwenye banda hilo. [2]

Ufafanuzi wa tukio

Kulingana na maelezo ya Wilfred Madelong (aliyezaliwa mwaka 1930), mtafiti wa mambo ya Kiislamu wa Ujerumani ni kwamb; Nukuu asili ya riwaya kuhusu mkusanyiko uliofanyika katika Saqifa ya Bani Saa'idah inarudi kwa Abdullah bin Abbas kutoka kwa Omar bin Khattab. Hivyo basi riwaya zote nyingine kuhusiana na tukio hilo zinatokana na chanzo hicho kimoja. Riwaya zote zilizosimulia tukio hili, zikiwemo riwaya za; Ibn Hisham, Muhammad Jarir al-Tabari, Abdul Razzaq bin Hammam, Muhammad bin Ismail Bukhari na Ibn Hambal, zimefanana sana katika masimulizi yake, ispokuwa unaweza ukakuta mabadiliko kidogo katika safu za wapokezi tofauti wa riwaya hii. [3]

Baada ya habari za kifo cha bwana Mtume (s.a.w.w) kuzagaa miongoni mwa Waislamu wa Madina, kundi la baadhi ya Maansari lilikusanyika katika kituo Saqifah cha Bani Saa'idah, ili kuamua juu ya hali zao na pia kutafuta suluhu kuhusiana na suala la mrithi wa wa nafasi ya uongozi baada ya Mtume (s.a.w.w). Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria, mwanzoni mwa mkutano huu, Saad bin Ubada, mkuu wa kabila la Khazraj, alizungumza na umati wa watu waliokusanyika mahali hapo kupitia mwanawe. Sa'ad bin Ubada alilazimika kumtumia mwanawe katika kuwahutubia watu hao, kutokana na hali mbaya ya ugonjwa aliokuwa nao. [Maelezo 1] Akitoa maoni yake juu ya mshika nafsi baada ya Mutume (s.a.w.w), yeye alitaja ithibati na hoja kadhaa zinazoashiria juu ya haki ya Maansari kurithi na kukamata nafasi hiyo. Waliohudhuria walithibitisha maneno yake na wakatangaza kwamba wamemchagua Sa'ad kuwa mtawala wao na wakasisitiza kwamba hawatafanya lolote kinyume na rai yake. [4] Lakini baadhi ya waliohudhuria waliibua fikra za kuwepo uwezekano wa wahajiri (Muhajirina) kupinga uamuzi huu na uwezekano wa kutosalimu amri juu ya maamuzi hayo. Jambo hilo likapelekea kuzaliwa nadharia nyengine mpya, iliopelekea pendekezo la kuchagua amir (kiongozi) mmoja kutoka kwa Maansari na amir mmoja kutoka kwa Muhajirina. [5]

Hatimae taarifa ya mkutano huu na sababu ya kuanzishwa kwake akamfikia Abu Bakar bin Abi Qahafa na Omar bin Khattab, wawili hawa wakashikamana pamoja na Abu Ubaydah Jarrah waelekea kwenye mkutano wa Saqifa. Walipoingia kwenye mkutano huo, Abu Bakar alichukua hatua ya kuzuia hotuba ya Umar, kisha akashika hatamu za mazongumzo na kuzungumzia ubora wa wahajiri (Muhajina) na kipaumbele cha Maquraish katika suala la kumrithi Mtume (s.a.w.w). [6] Hutuba ya Abu Bakar ilikabiliwa na makundi matatu tofauti, kundi moja liliunga mkono hutuba yake, huku kundi la pili likapingana na maoni ya hutuba hiyo, ila kundi la tatu lilisisitiza ubora wa Ali bin Abi Talib (a.s) katika katika kushika nafasi hiyo. hatimae Abu Bakar alimtangaza Omar na Abu Ubaidah kuwa ndio watu wanaostahiki kushika nafasi hiyo. Ila baada ya kupita mazungumzo kadhaa, wawili hao hawakukubaliana na pendekezo hilo la Abu Bakar. [8]

Kwa mujibu wa nukuu za kutoka katika kitabu Tarikh al-Tabari (kilichoandikwa mwaka wa 303 Hijiria), Omar Ibn Khattab akizungumzia mazingira ya wakati huo alisema hizi: Wakati ule wa tukio la Saqifah, kelele na ghasia zilizuka kutoka kila upande na maneno yasiyoeleweka yalisikika kutoka kila kona, kiasi ya kwamba niliogopa jambo hilo lisije leta mfarakano, na kusababisha kusambaratika kwa dhamira yetu tuliokuwa tumeshaipanga, hilo ndilo lililonifanya kwambia Abu Bakar; nyosha mkono wako ili nikupe kiapo cha kukutii kama ni khalifa wangu, ila kabla ya mkono wa Omar kuwa juu ya mkono wa Abu Bakar (kwa ajili ya kuunga mkono), mkono wa Bashir bin Saad Khazrajji, mmoja wa wapinzani wa Sa'ad bin Ubadah, ukawa umetangulia mbele kumpa mkono Abu Bakar na kuweka kiapo cha utiifu juu yake. [9]

Baada ya tukio hili, umati wa waliokuwepo katika ukumbi wa Saqifah ulianza kutoa kiapo cha utiifu kwa Abu Bakar hadi ikikakaria Sa’ad bin Ubadah ambaye alikuwa ni, kukanyagwa na kubaki chini ya mikono na miguu watu katika harakati hizo. Hali ambayo ilisababisha mzozo mkali kati ya Omar, Sa’ad na Qays bin Sa'ad, mzozo ambao ulimalizika kwa kuingiliwa Abu Bakar. [10] [Maelezo 2]

Mijadala ya Saqifa

Katika eneo la Saqifah, kulitokea mazungumzo mengi kati ya Maansari waliohudhuria hapo na wahajiri (Muhajirina) waliofika kwa kuchelewa kuchelewa katika eneo hilo, kila mmoja wao alikuwa na ushawishi tofauti katika mazungumzo yake. Lakini taathira kubwa zaidi ilitokana na maneno ya Abu Bakar na wanaoungana naye mkono. Baadhi ya mazungumzo yaliojiri katika tukio hilo ni kutoka kwa watu wafuatao:

  • Sa'ad bin Ubadah: Yeye hasa alishika hatamu za mazungumzo mwanzoni mwa mkutano na kabla ya kuwasili kwa Abu Bakar na wafuasi wake, ila kutokana na kutoweza kwake kuzungumza na kuufikisha ujumbe wake kwa watu walikuwapo mahali hapo kutokana na ugonwa aliokuwa nao, mwanawe alichukuwa jukumu la kuyafikisha maneno yake kwa umati. Ujumbe muhimu katika maneno yake ni: Kutaja sifa na historia ya Maansari, ubora wao juu ya makundi mengine ya Kiislamu, huduma za Maansari juu ya Uislamu pamoja na Mtume (s.a.w.w), na kule Mtume (s.a.w.w) kuridhika na Maansari kwabla ya kufariki kwake. Kwa hoja hizo, yeye aliwatangaza Maansari kuwa ndio wanaostahiki zaidi katika kumrithi Mtume (s.a.w.w) kwenye suala la uongozi na akawataka kushika hatamu za uongozi, na alilichukulia pendekezo la kumchagua amir (kiongozi) mmoja kutoka kwa Maansari na amir (kiongozi) mmoja kutoka kwa Muhajirina kuwa ni kushindwa na kurudi nyuma. [11]
  • Abu Bakar: Maneno yake ndio yaliozalisha matokeo na natija ya mkutano huo. Abu Bakar alitoa hutuba mara kadhaa na katika vipindi tofauti, mukhtasari wake ni kama ifuatavyo: ubora wa wahajiri (Muhajirina) juu ya Maansari, ikiwa ni pamoja na kuwatanguli wao katika kuukubali ujumbe wa Mtume (s.a.w.w), ubora wao katika imani na kumwabudu Mwenye Ezi Mungu, ukoo na urafiki uliopo baina wahajiri na Mtume (s.a.w.w), kipaumbele cha wahajiri kumrithi Mtume (s.a.w.w) kwa sababu hizo alizozitilia mkazo, sifa na historia ya Maansari, sifa na kipaumbele chao katika kushika nafasi ya uwaziri na sio serikali, makanyo dhidi ya Maansari waopinga suala la urithi wa wahajiri wa kushika nafasi ya uongozi. [12]
  • Habbab bin Mundhir: Alizungumza mara mbili au tatu ndani ya vuguvugu la Saqifah, na kila mara maneno yake yalibeba dhana ya uchochezi au vitisho dhidi ya wahajiri, hasa dhidi Abu Bakar na Omar. [13] Katika zamu nyengine za mazungumzo yake; alipendekeza kila kabila litoe amir (kiongozi) mmoja. [14]
  • Omar bin Khattab: Omar alitilia mkazo na kuunga mkono maneno mengi ya Abu Bakar na akayasisitiza kwa kuyajengea hoja kadhaa. Baadhi ya hoja hizo ni: uhakika wa Waarabu kutopinga urithi wa familia ya Mtume (s.a.w.w) katika kushika madaraka baada ya kifo chake, kutowepo uwezekano wa kuchagua maamiri wawili kutoka kundi la Ansari na Muhajirina, kwa sababu panga mbili haziwezi kuingia kwenye ala moja. [15]
  • Abu Ubaidah Jarrah: Katika hotuba aliyowahutubia Ansari, aliwakataza kubadili dini yao ua kuvunja msingi wa umoja wa Waislamu. [16]
  • Bashir bin Sa'ad: Anatokana na kabila la Khazraj na Ansari. Alizithibitisha na kuziunga mkono mara kadhaa hoja za Abu Bakar na wafuasi wake na akawakataza Ansari kupingana na Muhajirina, yeye akitilia mkazo suala hilo, alijaribu kutumia maneno ya kuwataka watu wamwogope Mungu na kutopingana haki halisi (ya Abu Bakar kuwa khalifa) isio na kiwingu ndani yake. [17]
  • Abd al-Rahman bin Auf: Alikumbusha hadhi na ubora wa watu kadhaa, kama vile; Ali bin Abi Talib (a.s), Abu Bakar na Omar na akaonesha kuwa Maansari wamepungukiwa na watu wakubwa kama hao. [18]
  • Mundhir bin Abi Arqam: Ni miongoni mwa Ansari, yeye katika Saqifah alikwenda kinyume kabisa na hoja za Abu Bak na Abd al-Rahman bin Aufr, Mundhir bin Abi Arqam alimtambulisha na kumuelezea Ali (a.s) kuwa ni mtu mwenye sifa zote zilizojadiliwa katika mkutano wa Saqifah za kushika nafasi ya ukhalifa, na kama angelichukua hatua ya kuwataka watu wampe kiapo cha utiifu, basi kusingelitokea mtu wa kupingana naye. [19] Maneno ya Mundhir yaliungwa mkono na baadhi ya Maansari na wakaanza walipiga kelele na kusema; hawatampa kiapo cha utiifu yeyote yule isipokuwa Ali (a.s). [20]

Vikundi vilivyokuwepo katika hadhara

Vyanzo vingi vya vya Kisunni vilivyonukuu tukio la Saqifah ya Bani Saa'idah vimeripoti vikisema kwamba; Tukio la Saqifah lilikuwa na hadhara kubwa ya kisiasa lililohudhuriwa na idadi kubwa ya wahajiri pamoja na Ansari walio wengi. [21] Hata hivyo vyanzo vingi vimetaja hatua mbili tofauti za Waislamu kutoa kiapo chao cha utiifu kwa Abu Bakar; kiapo cha utiifu cha siku ya Saqifah, na kiapo chengine ni kile cha waliokuwepo katika mji wa Madina, ambao hawakuwepo katika tukio hilo, kilichofanyika baada ya tukio hilo la Saqifa. Kiapo hicho cha mara ya pili kilifanyika siku ya pili baada ya Saqifa, ambacho kilijulikana kwa jina la kiapo cha wanajamii kwa jumla. [22]

Kwa mujibu ripoti za Wilfred Madelong; Abu Bakar, Omar, na Abu Ubaidah ndio watu pekee miongoni mwa Muhajirina waliokuwepo kwenye mkutano wa Saqifah, ambao yawezekana wao walindamana na baadhi ya wasaidizi wao binafsi, wanafamilia pamoja na watumwa zao. Na Si hasha wao kufanya hivyo, hasa ukizingatia ya kwamba; baadhi ya watafiti wameashiria uwepo Salim, ambaye ni mtumishi aliyeachwa huru wa Abu Hudhayfah, ambaye alikuwa ndiye mtu wa kwanza kutoa kiapo cha utiifu kwa Abu Bakar katika tukio hilo la Saqifah. Ila hakuna hata chanzo kimoja miongoni mwa vyanzo vya kwanza vya kihistoria vinavyoaminika, kilichotaja uwepo wake ndani ya tukio la Saqifah. Vyanzo vya kihistoria pia havijanukuu uwepo wahajiri wengine, hata wale Masahaba wa daraja la kati au la chini zaidi pia hawakutajwa ndani ya vyanzo hivyo. [23] Baadhi ya watafiti wakitoa baadhi ya ithibati juu ya suala hilo, wamebainisha wazi ya kwamba; Kulikuwa na idadi ndogo mno ya Muhajirina waliohudhuria katika tukio Saqifah. [24]

Kwa mujibu wa vyanzo kuhusiana na tukio la Saqifa, Ansari maarufu walioshiriki tukio la Saqifah ni: Sa'ad bin 'Ubada na mwanawe (Qays), Bashir bin Sa'ad ambaye ni binamu na mpinzani wa Sa'ad, Usaid bin Hudhair, Thabit bin Qays, Mundhir bin Arqam, Barra-u bin 'Aazib na Habbaab bin Mundhir. [25]

Ibn Qutaiba ametumia lugha ya kejeli akiashiria kukosekana kwa mawafikiano baina ya Ansari kulitokana na idadi ndogo ya watu awliohudhuria tukio la Saqifah, katika lugha hiyo Ibn Qutaiba amesema: “Lau Saa’d angelipata wapizizani wa kupigana nao, bila haka asingeacha kupigana nao". [27]

Shauku ya Maansari ya kukusanyika kwenye Saqifah

Baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa; kukusanyika kwa Ansari kwenye Saqifah, ni matokeo ya kuhofia mustakabali wao na hatima yao baada ya kifo cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w). Hasa ukizingatia matukio yaliofuatia baada ya Waislamu kuuteka mji Makka, ambapo Maquraishi walijenga mshikamano dhidi ya wasiokuwa Maqureishi, jambo ambalo lilikuwa likihatarisha mustakbali wao, na kuwatia wasiwasi juu ya kubadilika uzito wa mizani ya kisiasa dhidi yao katika siku zijazo. Watetezi na waunga mkono wa nadharia hii, hawakuacha kutia wasiwasi ya kwamba; yawezekano Maansari waligundua mpango uliobuniwa na kundi la Muhajirina la kufosi urithi wa nafasi ya uongozi baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w), ni moja ya sababu zilizopelekea Maansari kukukutana kwenye banda la Saqifah ili kujadili mustakbali wao. [28]

Baadhi ya waandishi wengine wamehisabu mkutano wa Saqifah kuwa ni tunda la masuala yafuatayo:

  • Ansari waliichukulia dini hii kuwa ni mtoto wao kutokana na mihanga ya roho zao pamoja na mali na watoto wao kwa ajili ya Uislamu na hawakumwona mwengine yeyote anayestahiki zaidi na mwenye huruma kuliko wao kuilinda na kuihifadhi dini ya Kiislamu.
  • Hofu ya Maansari juu ya Maquraishi ikulipiza kisasi dhidi yao, kutokana na ukweli kwamba; wengi wa viongozi wa kabila hilo la Maquraishi, waliuawa kwa upanga wa Maansari katika vita vya Mtume vilivyopiganwa katika zama za Mtume (s.a.w.w). Aidha, Mtume (s.a.w.w) aliwaahidi kutokea dhulma, ukandamizaji na utawala wa kimabavu au kidikteta kupitia watawala watakaokuja baada yake, na akawataka Maansari kuwa na subira katika hali hiyo.
  • Hisia za Maansari kwamba Maquraishi hawatashikamana na maneno ya Mtume (s.a.w.w) kuhusu nafasi ya Ali (a.s) baada yake. [29]

Kwa mujibu wa maoni ya baadhi ya waandishi wengine, Abu Bakar alitangaza rasmi kifo cha Mtume (s.a.w.w) msikitini, na jamii ya watu wa kawaida wa Madina ilikusanyika na kumzunguka na kumpa kiapo cha utiif juu yake na kumtambua yeye kuwa ni khalifa wao. Suala hilo lilizua utata na kujenga dhana kwenye akili za kundi la Maansari lililokuwepo Madinah kuhusiana na wao pia kuwa na haki ya kuteua khalifa kutoka upande wao wa Maansari, na kufuatia fikira hiyo, tukio la mkutano wa Saqifah likatokea. [30]

Radiamali ya Masahaba na wakuu wa Kiquraish

Ali (a.s), familia ya Mtume, pamoja na baadhi ya wahajiri na Ansari, walipinga kiapo cha utiifu kwa Abu Bakar, kwa mujibu wa nukuu za kihistoria, baadhi ya waliopingana na jakambo hilo ni: Abbas bin Abdil Muttalib, Fadhlu bin Abbas, Zubeir bin Awam, Khalid bin Said, Miqdad bin Amru, Salman Farsi, Abu Dhar Al-Ghafari, Ammar Yasir, Bara-a bin 'Aazib na Ubayya bin Ka'ab. [31]

Baadhi ya masahaba hawa au pia wakuu wa Maquraishi pia wamebainisha suala la Abu Bakr kutokuwa na vigezo vya kumrithi Mtume katika nafasi ya uongozi. Baadhi ya bayana zao kuhusiana na hilo ni:

  • Fadhlu bin Abbas; Yeye katika maelezo yake aliwashutumu Maquraish kwa kughafilika na kuficha siri au kunyamaza kimya katika tukio la kutawazwa Abu Bakar, pia katika maelezo aliwatangaza Ahlul-Bait wa Mtume (s.a.w.w), hususan Ali, kuwa ndio wenye kustahiki zaidi kwenye suala la urithi wa nafasi ya uongozi baada ya Mtume (s.a.w.w). [32]

Katika mazungumzo yake na Waislamu, Salman Farsi alilichukulia suala la kutawazwa Abu Bakar kwenye banda la Saqifah, kuwa ni kosa na akasema kuwa haki hiyo ya uongozi ni ya Ahlul-Bait wa Mtume Muhammad (s.a.w.w). [33]

  • Abu Dhar Al-Ghafari hakuwepo Madina katika siku ya tukio la Saqifah, na baada ya kuingia mjini, akapata habari kuhusu ukhalifa wa Abu Bakr. Kulingana na nukuu kutoka katika vyanzo vya kihistoria, baada tu ya kupata habari hizo, bila kusita alianza kufanya kazi mahususi ya kuuelezea uhalali wa Ahlul-Bait wa kumrithi Mtume katika uongozi [34] pia aliendelea kuuelezea ukweli huo hadi katika zama za utawala wa Othman bin Affan. [35]
  • Miqdad bin Amru aliusifu mwenendo wa Waislamu katika kufuata maamuzi ya Saqifah kuwa ni mwenendo wa kushangaza, naye hakuacha kuthibitisha ukweli wa haki ya Imam Ali (a.s) katika kushika nafasi ya uongozi baada ya Mtume (s.a.w.w). [36]
  • Omar Ibn Khattab katika mwaka wa mwisho wa maisha yake, khutba katika ya hadhara aliwahutubia watu akisema: “Kutawazwa kwa Abu Bakar kulikuwa ni mtetelezo na kosa lilifanywa na kupitishwa na watu na kumalizika, na Mungu aliwalinda watu kutokana na mtelezo uliopelekea kosa hilo kutokea, ila mtu yeyote atakaye rudia njia kama ile katika kumteuwa na kumchagua khalifa, muueni.” [37]
  • Abu Sufyan, ambaye alitumwa na Mtume aende kufanya kazi fulani nje ya Madina, baada ya yeye kurudi katika safari yake na kuingia Madina, alipata habari kuhusu kifo cha Mtume na kuteliwa kwa Abu Bakar, baada kupata habari hizo aliuliza kuhusu msimamo na radiamali ya Ali (a.s) na Abbas bin Abdul Muttab. Baada ya kuelewa kuwa watu wawili hao wamelazimika kujikalia kitako, alisema: "Naapa kwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nitaendelea kuwa hai kwa ajili yao, nitaikweza miguu yake (Ali) hadi ikanyage kwenye kilele cha uongozi." Akaongeza: “Mimi naona kiwingu cha vumbi ambacho hakituliziki ila baa ya kunyesha mvua ya damu.” [39] Kwa mujibu wa nukuu za zilizonukuu tukio hili; Baada ya Abu Sufiani kungia Madina, asisoma mashairi ya kumsifu Ali bin Abi Talib na kuwapondo Abu Bakar na Omar. [Maelezo 3]
  • Mu’awia bin Abi Sufiani katika barua aliyomtumia Muhammad bin Abi Bakar (miaka baada ya tukio la Saqiyfah), alisema: “... baba yako na Farooq wake ambaye ni Omar, walikuwa wa kwanza kupora haki ya Ali na kumpingana naye juu ya haki yake. Wawili hawa walishikana mikono (waliwafikiana); Kisha wakamwita Ali (a.s) ili wape kiapo cha utiifu juu wao. Wakati Ali (a.s) alipokataa na kupinga, walifanya maamuzi yasiyo ya haki na kumdhamiria mabaya, sababu hiyo ndiyo ilimfanya Ali awape wao kiapo cha utiifu. [41]

Pia, wakati wa tukio la kiapo cha utiifu kwa Abu Bakr lililofanyika msikitini, Bani Umayya walikuwa wamekusanyika na kumzunguka Othman kwa dhamira ya kumpa yeye kiapo cha ufiifu, na Banu Zuhra miongoni mwa koo za Kiquraishi wao walikubaliana kumchagua Abdu al-Rahman bin 'Auf au Sa'ad, ila baada ya juhudi za Omar, wote wakakubaliana kumchagua Abu bakar. [42]


Ibn Qutaiba katika al-Imamah na al-Siasah anasema:
Banu Umayyah walikuwa karibu na Othman, Banu Zuhra walikuwa karibu na Sa'ad na Abdu al-Rahman bin 'Auf. Wote walikuwa wamekusanyika katika msikiti mkuu, pale Abu Bakar na Abu Ubaidah walipowajia na watu msikitini humo, ambapo tayari Abu Bakar alikuwa ameshapewa kiapo cha utiifu na baadhi ya watu, Omar akawaambia wale watu waliokusanyika msikitini: Nini kimetokea ambacho kimepelekea mkusanyike kwenye makundi yalioparaganyika? Simameni mumpe kiapo cha utiifu kwa Abu Bakar, mimi tayari nimeshampa kiapo changu cha utiifu juu yake. Baada ya maneno ya Omar, Othman bin Affan na watu wa kabila la Bani Umayya wakampa kiapo cha utiifu Abu Bakar. Pia, Sa'ad na Abdul Rahman pamoja na waliokuwa wakiunga mkono maoni ya wawili hao, nao pia wakampa Abu Bakar kiapo cha utiifu. [38]

Radiamali ya Ali (a.s)

Katika siku ya tukio la Saqifah, Ali (a.s) hakutoa kiapo cha utiifu kwa Abu Bakr, ila kuna tofauti ya rai miongoni mwa wanahistoria kuhusu kilichoendelea baada ya hapo, kuhusiana na yeye kutoa kiapo cha kukumkubali Abu Bakar pamoja na wakati wa kutoa kiapo hicho. Kwa mujibu wa mwanachuoni wa Kishia Sheikh Mufid (aliyefariki mwaka wa 413 Hijiria); Wanazuoni wa Kishia wanaamini kwamba, Ali bin Abi Talib kamwe hakutoa kiapo cha utiif kwa Abu Bakar. [43]

Katika siku za mwanzo kabisa pale waandalizi wa tukio la Saqifah walipojaribu kumlazimisha kuweka kiapo cha utiif kwa Abu Bakar, Ali (a.s) alizungumza nao na kuwahutubia akisema:

“Mimi ninastahiki zaidi ukhalifa kuliko nyinyi, sitoweka kiapo cha utiifu juu yenu, kiuhakika nyinyi mnastahiki zaidi kuweka kiapo cha utiifu kwangu mimi, nyinyi mliuchukua ukhalifa kutoka kwa Maansari, na mkawapinga kwa sababu ya ukaribu uliopo baina yenu na Mtume wa Mwenye Ezi Mungu na mkawaambia: Kwa sababu sisi tuko karibu zaidi na Mtume na sisi ni miongoni mwa jamaa zake, sisi tunastahiki zaidi ukhalifa kuliko nyinyi, nao kwa msingi huo wakakupeni uongozi na uimamu. Nami basi vile vile ninapingana nanyi kwa msingi huo huo wa ubora mlioutegemea nyinyi katika madai yenu, na kupitia sifa na vigezo vile vile mlivyovitumia katika kuwapinga Maansari, basi ikiwa nyinyi mnamkhofu Mwenyezi Mungu, njoni pamoja nasi kupitia mlango wa uadilifu, na kwa kupitia kile kile walichokuridhieni Maansari na kukubali kukuachini nyinyi haki ya uongozi, nanyi basi kubalianeni nami, la sivyo basi eleweni kuwa nyinyi mumefanya dhulma kwa makusudi.” [44]

Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo; Ali (a.s) alikuwa na mjadala wa upole baina yake na na Abu Bakar lakini wa bayana usio na kificho, ambapo alilaani vitendo vya Abu Bakar katika tukio la Saqifah kutokana kupuuza kwake haki za Ahlul-Bait wa Mtume (s.a.w.w). Abu Bakar baada ya kusikia hoja na bayana za Amirul Muminina alilainika na akakaribia kumpa Ali (a.s) kiapo cha utiifu na kumtambua kuwa ndiye mrithi wa Mtume (s.a.w.w), lakini baada ya kushauriana na baadhi ya wafuasi wake, alishawishika na kuachana na jambo hilo. [45]

Ali (a.s) amepinga mambo yaliojiri kwenye mkutano wa Saqifah, yeye katika matukio mbalimbali na katika hotuba zake tofauti, alikuwa akiwakumbusha watu haki yake ya kurithi nafasi ya ukhalifa baada ya Mtume (s.a.w.w) Khutba ya Shaqshaqiyyah ni moja ya khutba alizotaja na kufafanua tukio hili la Saqifah. Mwanzoni mwa hotuba hii, alisema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu, mtoto wa Abu Quhafa aliuvaa ukhalifa kama shati, ingawa ana wazi ya kwamba, nafasi yangu katika ukhalifa ni kama nafasi ya mchi kwenye kiwe, ambapo elimu na sifa zangu zatiririka kutoka kangu kama vile mafuriko yanvyotiririka, na hakuna ndege anayeweza kupaa na kukifikia kilele cha hadhi yangu." [46]

Kwa mujibu wa nukuu ya baadhi ya vyanzo vya kihistoria; baada ya tukio la Saqifah na wakati wa uhai wa Fatima Zahraa (a.s), Ali (a.s), alikuwa akimchukua binti ya Mtume (s.a.w.w) usiku na kumpandisha kwenye kipando na kumpeleka kwenye nyumba na kwenye vikao vya Maansari na akiwataka msaada, ila wao walimjibu kwa kumwambia: "Ewe binti ya Mtume! Sidi tulishaweka kiapo cha utiifu kwa Abu Bakar. Lau Ali (a.s) angejitokeza mwanzo kabla ya Abu Bakar, basi tusingemkingiuka. Ali (a.s) naye alikuwa akiwajiju kwa kusema: "Je nilitakiwa nimuache Mtume bila ya kuzikwa, kisha niende kwenye mabishano ya ukhalifa? [47]


Sehemu ya khutba ya Shaqshaqiyyah
Enyi watu! Wallahi Abu Bakar mwana wa Abu Quhafa alivaa joho la ukhalifa huku akijua kuwa; nafasi yangu katika ukhalifa ni kama nafasi ya mchi wa kiwe ulioko kwenye kiwe, mafuriko ya elimu hutiririka kutoka kwangu kama mafuriko ya maji, na hakuna ndege yeyote yule wa fikra anaweza kupaa na kufikia kilele cha hadhi ya fikra zangu. Lakini niliachana na ukhalifa, na nikauepuka nao, na nilifikiri kwa kina kwamba vipi nitapigana kwa mkono uliokatwa na bila msaidizi, au kuvumilia giza ambalo wakati mwingine ni upofu, nikaa mahali ambapo wazee ndani yake wamechakazwa, vijana ndani yake wamezeeshwa na waamini watabaki mashakani hadi wakati wa kukutana na Mola wao![1]

Majibu na radiamali ya Fatima (a.s)

‍‍‍Baada ya tukio la Saqifah, Fatima Zahra (a.s) alilipinga matokeo na matunda ya Saqifah na akatangaza kuwa; maamuzi hayo ni ukiukaji wa amri za Mtume (s.a.w.w). Miongoni mwa misimamo yake pinzani inaakisika kwenye maneno na bayana zake alizozitoa wakati wa tukio linalohusiana na kuchukua kiapo cha utiifu kutoka kwa Ali bin Abi Talib (a.s) na kuzingirwa kwa nyumba yake. [49] Pia misimamo yake dhidi ya Saqifah inadhihirika katika khutba ijulikanayo kwa jina la khutba ya Fadakiyyah, aliyoitoa katika msikiti wa Mtume (s.a.w.w) uliopo Madina. [50]

Kwa mujibu wa ripoti za kihistoria, wakati Fatima Zahra (a.s) alipokua katika siku za mwisho za maisha yake akiwa mgonjwa kitandani, ambapo alizungumza na wanawake wa wahajiri na Ansari waliokuja kumtembelea, aliichukulia Saqifah kuwa ni muondoko hatari wa kutoka katika maagizo ya Mtume (s.a.w.w) na akatahadharisha matunda hatari ya tukio hilo yatakayojitokeza katika maisha ya baadae. [51]

Saqifah kwa mtazamo wa watafiti wa Kimagharibi

  • Henry Lammens na nadharia ya "The Triangle of Power: Henry Lammens mwananadharia wa Ubelgiji, (aliyezaliwa mwaka1862 na kufariki 1937), katika makala yake "The Triangle of Power" yenye maana ya "Pembetatu za nguvu"; akimaanisha "Abu Bakr, Umar na Abu Ubaydah” alidai kwamba lengo la ushirikiano wa karibu na wa pamoja wa watu hawa watatu lilianza tokea wakati wa uhai wa Mtume (s.a.w.w). Ushirikianao huo ndio uliowapa wao uwezo wa kusimamisha ukhalifa wa Abu Bakr na Umar, na kama Abu Ubaidah asingekufa, basi Omar anagelimteuwa yeye kuwa ndiye khalifa atakayefuata baada yake. Kufuatia madai hayo, Henry Lammens anaamini kwamba; Aisha na Hafsa, mabinti wa Abu Bakr na Umar, ambao walikuwa ni wake za Mtume (s.a.w.w), waliwafahamisha baba zao juu ya kila hatua na ajenda za siri za mume wao, na wawili hawa walifaulu kuwa na ushawishi mkubwa katika kazi za Mtume (s.a.w.w), njia hiyo waliyokuwa wakiitumia katika kuingiza madaraka na mamlaka mikononi mwao. [52]
  • Nadharia ya Leone Caetani: Mtafiti wa mambo ya Mashariki ya Kati wa Kiitaliano Leone Caetani katika utangulizi wa kitabu chake "Annali dell' Islam" kinachozungumzia mtiririko wa historia ya Uislamu, ameelezea ndani yake kiini cha mgogoro kati ya Abu Bakr na Bani Hashim. Leone Caetani anaeleza namna alivyoshangazwa na madai ya Abu Bakar ya ukhalifa aliyodai miongoni mwa Ansari katika Saqifah ya Bani Saa'idah, saa chache tu baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w). Leone Caetani anathibitisha kwa uwazi kabisa uzito

wa madai ya Ali katika haki ya ukhalifa kwa kuzikataa na kuzipindua hoja na bayana maarufu ambazo Abu Bakr alizitumia miongoni mwa Ansari ili kuonesha kipaumbele cha haki za Maquraishi -kama kabila la Mtume (s.a.w.w)- katika madai yake ya urithi wa nafasi ya uongozi. Kwa sababu hoja hii inazidi kutia nguvu madai ya Ali (a.s), kwa sababu; kama Abu Bakar alistahiki kushika nafasi hiyo kutokana na ujamaa wawe na ukaribu wake na Mtume (s.a.w.w), basi Ali ni jamaa aliye karibu zaidi na Mtume (s.a.w.w). Ila kwa maoni yake Leone Caetani ni kwamba; kama Muhammad (s.a.w.w) -mwenyewe yeye- angeliweza kumchagua mrithi wa ukhalifa baada yake, pengine angempendelea Abu Bakr kuliko mtu mwingine yeyote. Ametoa mtazamo kwa sababu katika mojawapo ya juzuu za kitabu chake historia cha Uislamu "Annali dell' Islam", Leone Caetani ametoa nadharia ya "nguvu ya pembetatu, ambayo ni Abu Bakr, Omar na Abu Ubaydah" ambyo kwa mtazamo wake, hii ndiyo nadharia inayohusiana zaidi na chimbuko la ukhalifa. [53]

  • Wilfred Madelong: Amezungumzia na kulichambua vya kutosha suala la ukhalifa pamoja na matukio ya Saqifah katika kitabu chake Succession of the Prophet of Islam. Anaamini kinyume na imani ya wanahistoria wengi, yeye anaamini ya kwamba Baraza la Saqifah mwanzoni mwake halikuanzishwa kwa ajili ya kuteuwa khalifa wa Waislamu, na kutokana na kwamba; nadharia ya ukhalifa ya kumrithi wa Mtume katika nafasi ya uongozi, haikuwapo hapo mwanzo katika jamii ya Kiislamu. Kwa hiyo ni duni isioingia akilili, kwamba Maansari walikutana pamoja kwenye mkutano wa Saqifah kwa ajili ya kuteuwa khalifa. [54] Madelong anaamini ya kwamba: Maansari walijaribu kuchagua kiongozi kutoka katika kundi la Ansari kwa wazo la kwamba; hakuna haja wala ulazima wa kumtii Mtume Muhammad (s.a.w.w) baada ya kifo chake. Hivyo basi wao walikuwa na dhana ya kwamba, jamii ya kisiasa aliyoianzisha Mtume (s.a.w.w) inaweza kuporomoka baada ya kifo chake. Hivyo basi mkusanyiko wao katika Saqifah ulikuwa na nia ya kuchagua kiongozi kutoka kwa Maansari atakayeweza kusimamia na kuendesha mambo ya mji wa Madina, ndiyo maana hawakuona hawakuona umuhimu wa kuwashirikisha Wahajiri katika maamuzi hayo. [55] Ansari walidhani ya kwamba wahajiri hawakuwa na sababu ya kubaki Madina baada ya kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w.w) na walidhani ya kwamba wahajiri hao wataamua kurudi Makka, na wale watakaotaka kubaki huenda wakaikubali serikali ya Ansari. [56]

Yeye ameitilia mkazo dhana yake isemayo kwamba; Abu Bakar na Omar ndio watu pekee walioamini kwamba mrithi wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni mtawala wa Waarabu wote na ukhalifa kama huo unawastahikia Waquraishi peke yao. [57]

Madelong anaamini kwamba hata kabla ya kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w.w), Abu Bakar alikuwa tayari amesha amua kushika cheo cha ukhalifa. Na ili kufikia ndoto hii, alikusudia kuwaondoa wapinzani wake wenye nguvu waliopewa katika Qur'ani daraja za juu kuliko Waislamu wengine. [59] Mpango wa Ansari katika kufanya mkutano wa Saqifah ulimpa Abu Bakar fursa nzuri ya kufikia lengo lake hilo. Mwanzo Abu Bakar alicheza mchezo wa guigiza kwa kuwapendekeza Omar na Abu 'Ubaida ambao hakukuwa na matumaini yoyote yale ya wao kuweza kufaulu katika mchakato wa uteuzi wa ukhalifa. Ila ilikuwa ni wazi kwamba; wazo lake halikuwa ni wazo la kweli, bali lilikuwa ni wazo la kuigonganisha jamii, ili hatimae mashiko na hatamu za uongozi ziishie mikononi mwake. [60]

Kwa mujibu wa maoni ya Madelong, hoja na madai ya Sunni na wanachuoni wa Magharibi ya kwamba; Ali (a.s) kutokana na ujana wake na kutokuwa na uzoefu, hakuwa ni mpizazi hatari katika sakata la kushika nafasi ya ukhalifa ikilinganisha na masahaba wengine, kama vile Abu Bakar na Umar, ni ya uongo yasio na mashiko. Bali kuna sababu nyingine kutoka upande wa Abu Bakar zilizosababisha Ali (a.s) asitajwe katika uteuzi wa ukhali katika tukio la Saqifah. [61]

Tukio la Saqifah kwa mtazamo wa Shia

Kulingana na mtazamo Washia, mkutano Wa Saqifah na matokeo yake ni ukiukaji wa maagizo ya wazi ya Mtume (s.a.w.w) kuhusu urithi wa Imam Ali (a.s) wa nafasi ya ukhalifa baada yake. Ili kupinga na kukataa uhalali wa Saqeefah na kuthibitisha uhalali wa Ali (a.s) katika kushika nafasi ya ukhalifa baada ya Mtume (s.a.w.w), Mashia wametegemea tafsiri ya baadhi ya aya za Qur'an, matukio ya kihistoria pamoja na Hadithi zinapatikana katika vyanzo vya madhehebu ya Sunni, muhimu zaidi kati yake ni tukio la Ghadir pamoja na Hadith zinazohusiana na tukio hilo. Kwa mujibu wa imani ya Mashia, katika tukio la Ghadir Khum, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alitangaza urithi wa Ali (a.s) kama ni ukamilisho wa ujumbe wake kwa Waislamu. [62]

Muhammad Rdha Mudhaffar amesimulia Hadithi 17 ambazo ni mutawaatir (zilizopokewa kupitia milolongo ya matabaka ya wapokezi tofauti walioshi zama tofauti) au mashuhuri, kuhusiana na matukio mbalimbali ya kihistoria, ambazo zinaelezea suala la Mtume (s.a.w.w) kumtaja Ali (a.s) kuwa ndiye mrithi wa wa ukhalifa baada ima kwa lugha ya mafumbo au kwa lugha bayana. Tukio la kuwaonya watu wa karibu yake aliloamrishwa na Mola wake kupitia Aya isemayo «وَأَنْذِرْ عَشِیرَتَکَ الاَْقْرَبِینَ», Hadith ya Ghadiyr, fungamano la udugu, vita vya Khandaq na Khaybar, Kisa cha Khasaf al-Na'alain "خاصف النعلین", kufungwa kwa milango ya nyumba za Masahaba zilizouzunguka Msikiti wa Mtume isipokuwa nyumba ya Ali (a.s) pamoja na baadhi ya Hadithi kama vile: ((إن علیا منی و أنا من علی، و هو ولی کل مؤمن بعدی ; Kwa hakika Ali yuwatokana nami nami ninatokana na Ali naye ni kiongozi wa kila muumini baada yangu)), ((لکل نبی وصی و وارث و إن وصیی و وارثی علی بن ابی طالب ; Kila Nabii ana mrithi na wasii wake, na kwa hakika wasii na mrithi wangu mimi ni Ali)) na ((أنا مدینة العلم و علی بابها ; Mimi ni mji wa elimu na mlango wake ni Ali)),hizi ni miongoni mwa Hadithi kuhusiana na suala hilo. [63] Aya ya 55 ya Surat al-Maaidah [Maelezo 4] ambayo ni maarufu kwa jina la Aya ya Wilaya, Aya ya 33 ya Surat al-Ahzab [ maelezo ya 5] inayojulikana kama Aya ya Utakaso, Aya ya 61 ya Surat al-Imran [Maelezo 6] ambayo ni maarufu kwa jina la Aya ya Mubahala, ni miongozi mwa Aya za Qur'an ambazo wanazuoni wa fani ya tauhidi na elmul al-Kalam wa madhehebu ya Shia, huzitegemea kama ni ithibati za kuthibitisha suala la haki ya Ali bin Abi Talib ya kushika nafasi ya ukhalifa baada ya Mtume (s.a.w.w) [64]


Natija

Baadhi ya watafiti wanaamini kwamba matukio mengi ya kihistoria baada ya kifo cha Mtume wa Mwenyezi Mungu ni natija ya tukio la Saqifah. Baadhi ya matukio hayo ni:

  • Shambulio dhidi ya nyumba ya Fatimah (a.s): Kwa mujibu wa ripoti na nukuu za kihistoria; wafuasi wa ukhalifa wa Abu Bakar, baada ya tukio la Saqifah na kukataa kwa baadhi ya masahaba, akiwemo Imam Ali (a.s), kumpa Abu Bakar kiapo cha utiifu, Abu Bakar na wafuasi wake walivamia nyumba ya Fatima kwa nia ya kuchukua kiapo cha utiifu kutoka kwa Ali (a.s) kwa mabavu. [65] Kwa mujibu wa mtazamo wa Mashia, sababu ya kifo cha bibi Fatima inatokana na majeraha aliyopata katika tukio la uvamizi huo. [66]
  • Kunyang'anywa kwa Fadak: Baadhi ya wachambuzi wa kihistoria wanaamini ya kwamba; upokonyaji wa bustani ya Fadak kutoka kwa bibi Fatima (a.s) baada ya tukio la Saqifah ulikuwa na lengo la mapambano ya kiuchumi dhidi ya Ahlul-Bait. Kitendo hichi kiliimarisha misingi ya utawala wa khalifa wa kwanza na kiliizuia familia ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kupigana na kupingana na utawala huo. [67]
  • Tukio la Karbala: Kwa mujibu mawazo na dhana za baadhi ya watafiti; mabadiliko katika njia ya urithi wa nafasi ya ukhalifa baada ya Mtume (s.a.w.w) huko Saqifah, yalisababisha mfumo wa kuchugua kuwa ni mfumo usiofuata misingi yeyote ile ya kisheria. Kwa hiyo, Khalifa wa Kiislamu wakati fulani alipewa kiapo cha utiifu kupitia mzozo kati ya Ansari na watu wachache kutoka katika kabila la Maquraish, katika kipindi chengine alichaguliwa kupitia wasia wa khalifa wa kwanza, aliyefuata baadae akachaguliwa kupitia baraza la watu sita, katika kipindi fulani akaja Mu'awiyah na kumteuwa mwanawe (Yazid), na Yazid naye akawa mhusika mkuu wa tukio la Karbala. [68] Sayyid Mohammad Hussein Tehrani (aliyezaliwa mwaka 1345 na kufariki 1416 Hijiria), ambaye ni mwanazuoni wa Shia, baada ya kunukuu mashairi ya Qadhi Abu Bakar bin Abi Qarii'ah kuhusu Ali (a.s) alipokuwa akitoa ufafanuzi wa ubeti usemao; "وَ أَرَیْتُکُمْ أَنَّ الْحُسَیْنَ أُصِیبَ فِی یَوْمِ السَّقِیفَهِ", Alisema: ubeti huu unatueleza ya kwamba; Ingelikuwa hawakuupora ukhalifa wa Ali (a.s), basi mshale wa Harmalah usingefika kwenye koo la Ali Asghar. [69] Pia, Muhammad Hussein Gharawi Esfahaniy (aliyezaliwa mwaka1296na kufariki 1361 Hijiria), mmoja wa wanavyuoni wa Kishia, ameeleza mada hii katika shairi lake kama ifuatavyo:

فما رَماه اِذْ رَماهُ حَرمَله *** و انَما رَماهُ مَن مَهَّدَ له سَهمٌ اَتی مِن جانب السقیفه و قَوسُه عَلی یدِ الخلیفه *** و ما أصاب سَهْمُهُ نَحرَ الصّبی بَل کَبدَ الدینِ و مُهجة النَب ***



[Basi hakupopoa Harmalah pale alipopoa * bali aliyepopoa ni yule aliye muandalia msingi wa kupopoa.

Mshale umekuja tokea upande wa Saqifah * Na upinde wake ukiwa mkonono mwa khalifa.

Wala mshale wake haukuingia kwenya koo ya yule mtoto * Bali kwenye moyo wa dini na Nabii yake roho.]

Saqifah na msingi wa makubaliano (Ijma'u al-Muslimina)

Nakala asilia: Ijma'a

Moja kati ya vyanzo msingi vya Ahlu-sunna vinavyo tumika katika kutoa fat'wa na kupata hukumu za kidini, ni msingi wa makubaliano ujulikanao kwa jina la Ijma'a. Hata katika tukio la Saqifah, msingi huo huo ndio unaotumika kama ndio hoja ya kuhalalisha maamuzi ya Saqifah ya kumchagua Abu Bakar. [72]

Kwa mujibu wa imani ya baadhi ya watafiti wa Kishia; Ahlu Sunna wameshikamana na hoja ya msingi wa "makubaliano ya umma" (ijma'u al-ummah) ili kuhalalisha ukhalifa wa Abu Bakar. [73] Masunni katika masuala yanayohusiana na sifa za jumla juu ya watu waofaa kuwa maimamu na pia katika masuala yanayohusina na maimamu kumi na mbili, yote kwa jumla wameyahusisha na "makubaliano ya umma". Wao wamevumbua nadharia hiyo ili iwe ni kama ngao ya kukabiliana na itikadi ya Mashia, ili ionekane kuwa, jamii ya Kiislamu haihitajii imamu maasumu. [74] Kwa mujibu wa maoni ya watafiti hawa; ubunifu wa kuingiza nadharia ya "ijma'u al-ummah" kulikuwa na nia ya kulikinda na kutetea kisa cha Saqifa na ukhalifa wa Abu Bakar, ambapo hatimae nadharia hiyo ikaenezwa katika pembe zote za dini; kama vile fiqhi, sifa kuu za uimamu na nyanja nyengine mbali mbali katika matawi na misingi ya Uislamu. [75]

Monografia (Vitabu kuhusiana na Maudhui)

Tukio la Saqifah limetajwa katika vyanzo mbali mbali vya historia vya Kiislamu; Taarikhu al-Tabari na Taarikhu Yaqubi ni miongoni mwa vitabu vilivyozungumzia tukio hili katika nyanja zake tofauti. Kwa upande wa pili, pia kuna makala na vitabu maalum vilivyojikita katika mada ya mchakato wa Saqifah peke yake, mfano wake ni kama vifuatavyo:

  • Al-Saqifah "السقیفة": Kilichoandikwa na Abi Saleh Al-Saliil bin Ahmed bin Issa (aliyeishi katika karne ya tatu Hijiria)
  • Saqifah wa Bai'atu Abi Bakar "السقیفة و بیعة ابیبکر": Kilichoandikwa na Muhammad bin Omar Waaqdi (aliyezaliwa mwaka 130 na kufariki 207 Hijiria).
  • Al-Saqifah "السقیفة": Kilichoandikwa na Abu Makhnaf Lut bin Yahya bin Said (aliyefariki mwaka 157 Hijiria).
  • Saqifah wa Ikhtilafe Dar Ta'ayiine khalifeh "سقیفه و اختلاف در تعیین خلیفه": Kilichoandikwa na Sahaabu bin Muhammad Zaman Tafrishi. Chapa ya Tehran ya mwaka 1334 Shamsia .
  • Saqifah "السقیفة": Kilichoandikwa na Abu Issa al-Warraaq Muhammad bin Harun. [76]
  • Saqifah "السقیفة": Cha Muhammad Ridha Mudhaffar.
  • Succession of Muhammad: Cha Wilfred Madelung.
  • Saqifah "سقیفه": Tafiti juu ya hakika na jinsi ya muundo wa serikali ulivyotimia baada ya kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w.w), kilichoandikwa na Murtadha Askari.
  • Al-Saqifah wa Al-khilafah "السقیفة و الخلافة": Cha Abdul-Fattah Abdul-Maqsoud.
  • Al-Saqifah wa Al-Fadak "السقیفة و فدک": Cha Ahmad bin Abdul-Aziz Jawhari Basri.
  • Muutamaru AlSaqifah "مؤتمر السقیفة": Utafiti wa Kimadhui Juu ya Tukio Hatari Zaidi Katika Historia ya Kisiasa ya Uislamu: Cha Baqir Sharif Qureishi.
  • Muutamaru Al-Saqifah: Utafiti mpya juu ya historia ya Kiislamu. Cha Sayyied Muhammad Tijani Samawi.
  • Wakoonesh-haye Saqifahe "ناگفتههایی از سقیفه" (Mbinu, matokeo na athari): Cha Najm al-Din Tabasi.

Saqifa katika kioo cha mashairi

Suala la kupinga kuchaguliwa kwa Abu Bakar kama mrithi wa bwana Mtume (s.a.w.w) na kupuuza haki ya Ahlul-Bayt (a.s) katika suala la uongozi baada yake, limekuwa ni mada ya mashairi ya washairi wa Kiarabu na Kiajemi. [77] Katika baadhi ya mashairi hayo tukio la Saqiyfah limetajwa moja kwa moja, kama vile beti hizi chache kutoka katika shairi lililoandikwa na Qazi Abu Bakar bin Abi Qurai'a:


يا من يسائل دائبا عن كل معضلة سخيفة * لا تكشفنَّ مُغطأ فلربما كشفت جيفة ولَرُبَّ مخبوء بدا كالطبل من تحت القطيفة* ان الجواب لحاضر لكنني اخفيه خيفة لولا اعتداء رعية القى سياستها الخليفة * وسيوف اعداءٍ بها هاماتِنا اَبدا نقيّة لَنشرتُ من اسرار آل * محمّدٍ جُمَلاً طریفة تُغنیکم عمّا رواه * مالکٌ و ابوحنیفة وأریتُکم أن الحسین * أُصیب فی یوم السقیفة ولأیِّ حالٍ لُحِّدت * باللیل فاطمة الشریفة.[78]


Ewe mwenye tabia ya kuuliza maswali kuhusu kila balaa * Usifunue yaliofunikwa utakuja funua mzoga kisha upigwe na butwaa

Huenda lifichwalo likadhihiri kama ngoma chini ya kitambaa * Hakika Hakika jabu ipo tayari ila mimi ninaificha kwa ukuogopa balaa.

Lau nisingeogopa raia kuhujumiwa na walioshika mpini wa siasa * Na panga mkononi mwa adui zenye nia vichwa vyetu kuviondoa.

Ningelitangaza siri kutoka Aali za wa Mtume * Nadra ya habari asilia.

Yakutosheni enyi waja yaliyopokewa * kutoka kwa Maliki na Abu Hanifa.

Na mmeona ya kwamba Husseini * Amesibiwa toka chanzo cha Saqifah.

Na vipi binti ya Mtume alivyozikwa * Usiku wa manane Fatima mtakasika.

Rejea

  1. Rejea Nahj al-Balagheh iliyotafsiriwa na Hussein Ansarian

Vyanzo

  • Āgā Buzurg al-Tihrānī, Muḥammad Muḥsin. Al-Dharīʿa ilā taṣānīf al-shīʿa. ٍEdited by Aḥmad b. Muḥammad Ḥusaynī. Beirut: Dār al-Aḍwāʾ, 1403 AH.
  • ʿAbd al-Maqṣūd, ʿAbd al-Fattāḥ. Al-Saqīfa wa l-khilāfa. Beirut: Dār al-Maḥajjat al-Bayḍāʾ, 1427 AH.
  • ʿAskarī, Murtaḍā. Saqīfa; barrasī-yi nahwa-yi shiklgīrī-yi ḥukūmat pas az riḥlat-i Payāmbar. Edited by Mahdī Dashtī. Qom: Dānishkada ʿUṣūl al-Dīn, 1387 Sh.
  • Balādhurī, Aḥmad b. Yaḥyā al-. Ansāb al-ashrāf. Edited by Muḥammad Bāqir Maḥmūdī, Iḥsān ʿAbbās, ʿAbd al-ʿAzīz al-Dawrī, Muḥammad Ḥamīd Allāh. Beirut: Muʾassisa al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, [n.d].
  • Bayḍūn, Ibrāhīm. Rafārshināsi Imām Alī (a). Translated by ʿAlī Aṣghar Muḥammadī Sījānī. Tehran: Daftar-i Nashr-i Farhang-i Islāmī, 1379 Sh.
  • Dhahabī, Muḥammad b. al-Aḥmad al-. Tārīkh al-Islām wa wafayāt al-mashāhīr wa l-aʿlām. Edited by ʿUmar ʿAbd al-Salām al-Tadmurī. Second edition. Beirut: Dār al-Kitāb al-ʿArabī, [n.d].
  • Dāwudī and Rustam Nizhād. Āshūrā; rīshahā, angīzahā, rūydādhā, payāmadhā. [n.p]. 1388 Sh.
  • Ḥamawī, Yāqūt b. ʿAbd Allāh al-. Muʿjam al-buldān. Beirut: Dār al-Ṣādir, 1995.
  • Henri Lammens. Muthallath-i qudrat, Abū Bakr, ʿUmar, Abū ʿUbayda. Quoting from Wilferd Madelung, Jānishīnī-yi Muḥammad. [n.p]. 1377 Sh.
  • Jawharī Baṣrī, Aḥmad b. ʿAbd al-ʿAzīz. Al-Saqīfa wa Fadak. Edited by Amīnī Muḥammad Hādī. Tehran: Maktabat Nineveh al-Ḥadītha, [n.d].
  • Ibn Abī l-Ḥadīd, ʿAbd al-Ḥamīd b. Hibat Allāh. Sharḥ Nahj al-balagha. Edited by Muḥammad Abu l-faḍl Ibrāhīm. Qom: Maktabat Ayatullāh Marʿashī Najafī, [n.d].
  • Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Abī l-Karam. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Beirut: Dār Ṣādir, [n.d].
  • Ibn Shahrāshūb, Muḥammad b. ʿAlī. Manāqib Āl Abī Ṭālib. Edited by Rasūl Ḥāshimī, Muḥammad Ḥusayn Āshtīyānī. Qom: Nashr-i ʿAllāma, [n.d].
  • Ibn Hishām, ʿAbd al-Malik. Al-Sīra al-nabawīyya. Edited by Muṣṭafā al-Saqā. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].
  • Ibn Qutayba al-Dīnawarī, ʿAbd Allāh b. Muslim . Al-Imāma wa l-sīyāsaʾ. Edited by ʿAlī Shīrī. Beirut: Dār al-Awḍāʾ. 1410 AH.
  • Ibn Kathīr, Ismāʿīl b. ʿUmar. Al-Bidāya wa l-nihāya. Edited by ʿAlī Shīrī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1408 AH.
  • Irbilī, ʿAlī b. ʿĪsā al-. Kashf al-ghumma fī maʿrifat al-aʾimma. Edited by Sayyid Hashim Rasūlī Maḥallātī. Tabriz: Maktabat Banī Hāshimī, 1381 AH.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Al-Fuṣūl al-mukhtarat min al-ʿuyūn wa al-maḥāsin. [n.p]. [n.d].
  • Muzaffar, Muḥammad Riḍā. Al-Saqīfa. Edited by Maḥmūd Muzaffar. Qom: Muʾassisa-yi Intishārāt-i Anṣārīyān, 1415 AH.
  • Maqdisī, Muṭahhar b. Ṭāhir. Al-Bidaʾ wa tārīkh. Thiqāfat al-Dīniyya, [n.p]. [n.d].
  • Muʿayyir, Zībā, Muftakharī Ḥusayn, Ṣādiq Āʾīenawand, ʿAlī Rajablū. Barrasī taʾthīr-i iʿzam lashkar-i Usāma bar chigūnigī-yi musharikāt-i siyāsi-yi nukhbigān-i muhājir wa anṣār dar Saqīfa wa tathbīt-i khilāfat. Muṭāliʿāt-i Tārīkh-i Islām. No 17, Summer 1392 Sh.
  • Nayyir Tabrīzī. Dīwān-i ātashkada. Tabriz: Kitābfurūshī-yi Hātif, 1319 Sh.
  • Naṣr b. Muzāhim Minqarī. Waqʿat Ṣiffīn. Qom: Maktabat Āyatullāh Marʿashī al-Najafī, 1404 AH.
  • Tījānī, Muḥammad. Muʾtamir al-saqīfa. London: Muʾassisa al-Fajr, 1424 AH.
  • Ṭabrisī, Aḥmad b. ʿAlī al-. Al-Iḥtijāj ʿalā ahl al-lijāj. Edited by Muḥammad Bāqir Khursān. Mashhad: Nashr-i Murtaḍā, [n.d].
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārīkh al-Ṭabarī. Edited by Muḥammad Abu l-faḍl Ibrāhīm. Beirut: Dar al-Turāth, 1387 AH.
  • Wilferd Madelung. Jānishīnī-yi Muḥammad. Translated to Farsi by Aḥmad Nimāʾī and others. Mashhad: Bunyād-i Pazhūhishhā-yi Islāmī, 1377 Sh.
  • Yaʿqūbī, Aḥmad b. Abī Yaʿqūb al-. Tārīkh al-Yaʿqūbī. Beirut: Dār Ṣādir, [n.p].
  • Zamakhsharī, Maḥmūd b. ʿUmar al-. Al-Fāʾiq fī gharīb al-ḥadīth. Manshūrāt Muḥammad ʿAlī Bayḍūn. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, [n.d].