Kutoka Sufyani
Kutoka au kuibuka harakati ya Sufyani (Kiarabu: السفياني) ni moja kati ya matukio matano yasiyo na shaka ambayo yatatokea wakati wa kukaribia kudhihiri Imam Mahdi (a.t.f.s). Matukio haya yatatokea kabla ya kudhihiri Imam wa zama. Tukio la Sufyani litatokea katika eneo la Sham (Syria). Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Ali bin Mussa al-Ridha (a.s) ni kuwa, kudhihiri Imam Mahdi hakutatokea pasi na kutokea harakati ya Sufiyani. Katika hadithi nyingine inaelezwa kuwa, baada ya Sufyani kutawala katika eneo la Sham (Syria) kwa muda wa miezi 9, atakusanya jeshi la kulipeleka upande wa Madina na kumezwa na ardhi katika eneo la Bayda'.
Sufyani ametajwa katika hadithi za Mashia na Masuni kwamba, ni katika wajukuu wa Abu Sufyan na kwamba, ana uso wa umwagaji damu na katili na watu wataingiwa na hofu na wahaka kwa kumuona yeye. Kumetajwa majina tofauti kumhusu kama vile Anbasah bin Marra.
Historia na sifa zake maalumu
Katika vyanzo na vitabu vya Mashia na Masuni, kumetajwa majina mbalimbali ya Sufyani: Miongoni mwa mwao ni yale yaliyotajwa katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Ali (a.s) ambayo ni Anbasah bin Marra [1], Harb bin Anbasa, [2] na Othman bin Anbasa, [3] na imeelezwa kuwa ni katika wajukuu wa Abu Sufyan. [4] Kadhalika jina lake katika vitabu na vyanzo vya Kisuni limetajwa kuwa ni: Harb bin Anbasa [5] na Muawiyah bin Utba. [6]
Wasifu wa Sufyani kwa mujibu wa hadithi ni mtu mmwagaji damu, muuaji na katili. [7] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi zilizopokewa kutoka kwa Imam Ali (a.s): Sufyani ni mwanamume mwenye mabega manne, ndui na jicho macho ambapo watu baada ya kumuona wataingiwa na woga na hofu [8]. Kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Sadiq (a.s) iliyonukuliwa katika kitabu cha Bihar al-Anwar ni kwamba, Sufyani ni adui wa Shia na mpiga mbiu wake atatangaza huko Kufa ya kwamba, kila atakayekata shingo ya Shia na kuitenganisha na mwili atampatia dirihamu 1000. [9]
Kutokea kwake kusikokuwa na shaka
Kutoka na kuja Sufyani ni jambo ambalo limetambuliwa katika hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) ya kwamba, lisilo na shaka. Kwa maana kwake kutokea kwake ni jambo la lazima, [10] ambapo imeelezwa kuwa, tukio hilo pamoja na matukio mengine kama kujitokeza na kuanzisha harakati Yamani, ngurumo au sauti kali kutoka mbinguni na kuuawa nafsi takasifu (Nafs Zakiya) na Khasf al-Bayda (kumezwa eneo la Bayda'), imetajwa kuwa ni moja kati ya alama tano zitakazoonekana kabla ya kudhihiri Imam Mahdi (a.t.f.s). [11]
Kadhalika kwa mujibu wa nukuu kutoka kwa Imam Ridha (a.s) ni kwamba, kudhihiri Imam Mahdi kwa amri ya Mwenyezi Mungu ni jambo lisilo na shaka, na kutokeza Sufiyani pia hilo halina shaka, na kwamba, Imam Mahdi hatodhihiri kabla ya kutokeza Sufyani. [12] Hadithi nyingine iliyonukuliwa kwa Imam Swadiq (a.s) inaeleza kuwa, suala la kutoka Sufyani na kuanzisha harakati ni jambo lisilo na shaka na kwamba, litatokea katika mwezi wa Rajab. [13] Hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Muhammad Baqir (a.s) inaeleza kwamba, kuja Sufyani, Sayyid Yamani na Sayyid Khorasani kutatokea katika mwaka mmoja, mwezi mmoja na katika siku moja. [14]
Khasf al-Bayda': Kuangamia Sufyani
- Makala asili: Khasf al-Bayda'
Katika hadithi zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) inaelezwa kuwa, moja ya alama za kudhihiri Imam Mahdi (a.t.f.s), ni kutoka jeshi huko Sham na kufunga safari kuelekea Makka kwa ajili ya kupigana vita na Imam Mahdi ambapo litakapofika katika eneo la Bayda' kutatokea muujiza ambapo litamezwa na ardhi ya eneo hilo. Tukio hili ni mashuhuri katika vyanzo vya hadithi kwa jina la Khasf al-Bayda' (kumezwa Bayda'). [15] Ardhi ya Bayda' ipo baina ya miji mitakatifu ya Makka na Madina. Hadithi nyingine iliyopokewa kutoka kwa Imam Ali bin Abi Talib (a.s) inaeleza kwamba, sehemu ya Aya ya 51 ya Surat Sabaa inayosema: "Na lau ungeli ona watapo babaika, basi hapana pa kukimbilia! Na watakamatwa mahala pa karibu", inaashiria tukio la jeshi la Sufyani na imebainisha kwamba, Bwana huyu atahukumu Sham kwa muda wa miezi 9 na kisha baada ya hapo atakusanya jeshi na kufunga safari kuelekea Madina na jeshi hilo likifika katika eneo la Bayda' litamezwa na ardhi. [16].
Rejea
Vyanzo
- Ḥimyarī, ʿAbd Allāh b. Jaʿfar al-. Qurb al-isnād. Qom: 1413 AH.
- Ibn Ṭāwūs, ʿAlī b. Mūsā. Al-Tashrīf bi l-minan fī al-taʿrīf bi l-fitan known as Malāḥim wa al-fitan. 1st edition. Qom: Muʾassisat Ṣāḥib al-ʾAmr, 1416 AH.
- Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Muʾassisat al-Wafāʾ, 1403 AH.
- Muḥammadī Reyshahrī, Muḥammad. Dānishnāma-yi Imām Mahdī. Qom: Dār al-Ḥadīth, 1393 Sh.
- Muqaddasī, Yūsuf b. Yaḥyā. ʿAqd al-durar fī akhbār al-muntaẓar. Qom: Intishārāt-i Masjid Jamkarān, 1428 AH.
- Nuʿmanī, Muḥammad b. Ibāḥīm al-. Kitāb al-ghayba. Tehran, Maktaba al-Saduq, [n.d].
- Shūshtarī, Nūr Allāh al-Ḥusaynī al-. Iḥqāq al-ḥaqq wa izhāq al-bāṭil. Edited by Marʿashī al-Najafī. Qom: Kitābkhāna-yi Āyatollāh Marʿashī al-Najafī, 1409 AH.
- Ṣadr, Sayyid Muḥammad. Tārīkh al-ghayba. Beirut: Dār al-Taʿāruf, 1412 AH.
- Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Kamāl al-dīn wa itmām al-niʿma. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī. Tehran: Islāmiyya, 1395 AH.
- Tāj al-Dīn, Mahdī. Al-Majālis al-mahdawīyya. Qom: al-Maktaba al-Ḥaydariyya, 1437 AH.