Shu’ayb bin Salih

Kutoka wikishia

Shu’ayb bin Salih(Kiarabu: شُعَیب بن صالح) ni mtu kutoka katika kabila la Bani Tamim ambaye kwa mujibu wa baadhi ya hadithi ataanzisha harakati na mapinduzi kabla ya kudhihiri Imamu Mahdi na harakati yake imetambuliwa kuwa ni katika dalili na ishara zisizo za uhakika (zisizo na uhakika wa mia kwa mia) za kudhihiri Imam Mahdi (a.t.f.s). Akiwa na jeshi la askari 4,000, bendera nyeusi na mavazi meupe atapigana na Sufyani na atamshinda. Katika baadhi ya hadithi imeelezwa kuwa, pengo la harakati yake mpaka kudhihiri Imamu Mahdi ni miezi 72.

Kwa mujibu wa Najmuddin Tabasi, mhakiki wa madhehebu za Kiislamu, Shu’ayb bin Salih na harakati yake vimenukuliwa katika hadithi kwa kiwango ambacho kinaweza kutambuliwa kuwa ni mutawatir maanawi au kwa akali mustafidh (hadithi ambayo ina mpokezi zaidi ya mmoja lakini haijafikia idadi ya wapokezi wa hadithi ya mutawatir); lakini hadithi ambazo zinazungumzia sifa maalumu ya harakati yake na jinsi atakavyoanzisha na kufanya harakati yake hazina itibari na ni hadithi moja tu iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Ridha (a.s) kuhusiana na hili ambayo ni sahihi, ambapo kwa mujibu wake, kutoka Shu’ayb bin Salih ni moja ya alama na ishara za uhakika na zisizo na shaka za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s).

Katika kipindi cha baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran shakhsia mbalimbali kama Hashemi Rafsanjani, baadhi ya wapiganaji katika vita vya Iran na Iraq na Rais wa zamani wa Iran Mahmoud Ahmadinejad, kuna wakati walitambuliwa kama Shu’ayb bin Salih au watu waliofanana naye. Ayatullah Ali Sistani anasema, utabikishaji na ufananishaji kama huu unapelekea kudhoofika itikadi ya jamii.

Sifa maalumu na jinsi harakati yake itakavyokuwa

Katika hadithi zinazohusiana na kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s), kumetajwa jina la Shu’ayb bin Salih na katika baadhi ya hadithi tajwa, kutoka kwake na harakati yake vimetambuliwa kuwa miongoni mwa ishara na alama za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s). [1] Hadithi ambazo zimenukuliwa kuhusiana na Shu’ayb bin Salih, wakati mwingine zinaeleza sifa zake binafsi, harakati yake itakavyokuwa, kutoka na kuanzisha harakati na mapinduzi yake kabla ya kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s) na kubeba bendera wakati wa kudhihiri Imamu Mahdi. Baadhi ya mambo hayo ni:

  • Sifa binafsi

Shu’ayb bin Salih katika hadithi ameelezwa kuwa ni kijana [2], mwenye rangi ya manjano [3], mwenye rangi ya ngano [4], kimo cha wastani [5] na mwenye ndevu chache [6]. Ametambuliwa kuwa mtu anayetokana na ukoo wa Bani Tamim [7] au kijakazi kutoka Bani Tamim. [8]

  • Harakati yake itakavyokuwa

Katika hadithi Shu’ayb bin Salih anatambulishwa kuwa ni kamanda wa harakati ya mtu kutoka Khorasani anayetokana na Bani Hashim [9] ambapo kwa ukamanda wake, harakati itaanzia Khorasani. [10] Inaelezwa kuwa atatokea Samarqand [11] na wakati mwingine inaelezwa kuwa atatotea Rey [12] na Taliqan. [13]

Katika hadithi idadi ya askari wa jeshi lake imeelezwa kuwa ni 4,000 [14] ambao watakuwa wamebeba bendera nyeusi [15] na mikanda myeusi [16] na mavazi meupe. [17] Jeshi hilo litapigana na Sufyani katika Istakhr [18] [19] na kulishinda jeshi la Sufyani na kwenda Baytul-Muqaddas (Jerusalem). [20] na litaibuka na ushindi mbele ya kila litakaopambana nao. [21]

Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi kutoka Shu’ayb bin Salih kutakuwa baada ya kutoka Awf bin al-Silmi na kabla ya kutoka Sufyani. [22] Katika baadhi ya hadithi imeelezwa kuwa, pengo la harakati yake mpaka kudhihiri Imamu Mahdi ni miezi 72. [23]

  • Mchango wake wakati wa kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s)

Imekuja katika hadithi kwamba, baada ya kuwa jeshi la Shu’ayb bin Salih limewashinda wanajeshi wa Sufyani, watu 300 kutoka Sham wanataungana nao na kwenda Baytul-Muqaddas na hivyo kuandaa mazingira ya kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s). [24] Miezi 72 kabla ya kutoka kwake atadhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s) na Shu’ayb bin Salih atatoa baia na kiapo cha utii kwa Imamu Mahdi (a.t.f.s). Katika hadithi kadhaa Shu’ayb anatambulishwa kuwa ni mbeba bendera ya jeshi la Imamu wa 12 wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Uchunguzi wa hadithi

Kwa mujibu wa Najmuddin Tabasi, mhakiki wa madhehebu za Kiislamu, sambamba na kufanya uchunguzi wa hadithi zinazohusiana na Shu’ayb bin Salih anaamini kuwa, Shu’ayb bin Salih na harakati yake vimenukuliwa katika hadithi kwa kiwango ambacho kinaweza kutambuliwa kuwa ni mutawatir maanawi au kwa akali mustafidh (hadithi ambayo ina mpokezi zaidi ya mmoja lakini haijafikia idadi ya wapokezi wa hadithi ya mutawatir); lakini sifa maalumu na jinsi harakati yake itakavyotokea hadithi hizo hazijafikia kiwango cha mustafidh. [26] Anaamini kwamba, baina ya hadithi zinazohusiana na sifa maalumu za Shu’ayb bin Salih hadithi sahihi ni ile tu iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Ridha (a.s). [27] Kitu ambacho mtu anaweza kustafidi kutoka katika hadithi hiyo ya Imamu Ridha (a.s) ni ishara tu ya kwamba, kutoka na kuibuka Shu’ayb bin Salih ni moja ya alama na ishara zisizo na shaka za kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s). Najmuddin Tabasi, mapokezi ya hadithi zingine kuhusiana na Shu’ayb bin Salih anayaona yana mushkili. [28] Kwa mujibu wake kuna hadithi takribani 300 katika Kutub al-Ar’baa (Vitabu Vinne) kuhusiana na itikadi ya Mahdi (a.t.f.s), lakini hakujanukuliwa kitu kuhusiana na Shu’ayb bin Salih. [29]

Nasaba yake na Nabii Shu’ayb

Katika Kitabu cha al-Nubwah, Sheikh Saduq ametaja hadithi ambayo kwa mujibu wake mtu mmoja aitwaye Shu’ayb bin Salih ni mmoja wa wajumbe wa Nabii Shu’ayb, ambaye watu wake watamuua shahidi. [30] Kwa msingi huo, Qutb Rawandi anaamini kwamba Shu’ayb bin Salih ambaye ataanzisha harakati wakati wa kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s) ndio yule yule Shu’ayb bin Salih, ambaye watu wake walimuua shahidi, kisha amerejea tena. [31] Pamoja na hayo Sheikh Muhammad Sanad, mmoja wa wahakiki wa zama hizi, anapingana na nadharia ya Ravandi na kusema kuwa, Shu’ayb bin Salih aliyetajwa katika hadithi ya Sheikh Saduq kuna uwezekano akawa ni Nabii Shu’ayb mwenyewe ambaye atarejea akiwa pamoja na Khidhr na Ilyas na sio Shu’ay bin Salih kamanda wa jeshi la Khorasani.

Mifano ya madai ya Shu’ayb bin Salih

Imedaiwa katika "Zohur bisiyar nazdik" kwamba, Mahmoud Ahmadinejad Rais wa zamani wa Iran ameshabihiana sana na Shu’ayb bib Salih. [33] Ayatullah Ali Sistani mmoja wa Marajii Taqlidi ameonyesha radiamali ya utabikishaji na ufananishaji kama huu na kusema kuwa, unapelekea kudhoofika itikadi ya jamii. [34] Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti kabla ya hapo pia, watu kama Akbar Hashemi Rafsanjani na baadhi ya makamanda wa Kiirani katika vita vya Iran na Iraq waliitwa na kushabihishwa na Shu’ayb bin Salih. [35].

Vyanzo

  • Ibn Ḥammād, Naʿīm al-Mirwazī. Al-Fitan. Edited by Suhayl Zakār. Beirut: Dār al-Fikr, [n.d].
  • Ibn Ṭāwūs, ʿAlī b. Mūsā. Al-Malāḥim wa l-fitan fī ẓuhūr al-ghāʾib al-muntaẓar. Qom: Manshūrāt al-Raḍī, [n.d].
  • Kūrānī, ʿAlī. Muʿjam aḥādīth al-imām al-Mahdī. Qom: Muʾassisat al-Maʿārif al-Islāmīyya, 1411 AH.
  • Nuʿmānī, Muḥammad b. Ibrāhīm al-. Al-Ghayba. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī. Tehran: Maktabat al-Ṣadūq, [n.d].
  • Rāwandī, Quṭb al-Dīn ibn Hibat Allāh. Al-Kharāʾij wa l-jarāʾiḥ. Qom: Muʾassisat al-Imām al-Mahdī, 1409.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al. Al-Nubuwwa. Tehran: Intishārāt-i Wizārat-i Farhang wa Irshād-i Islāmī, 1381 Sh.
  • Sanad, Muḥammad al-. Fiqh ʿalāʾim al-ẓuhūr. Najaf: Markaz al-Dirāsāt al-Takhaṣṣuṣīyya fī al-Imām al-Mahdī, 1425 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Ghayba. Edited by ʿAbd Allāh Tīhrānī & Aḥmad Nāṣiḥ. Qom: Muʾassisat al-Maʿārif al-Islāmīyya, 1411 AH.