Nenda kwa yaliyomo

Hadithi ya Khasifu an-Na'al

Kutoka wikishia

Hadithi ya Khasifu an-Na'al (Kiarabu: حديث خَاصِفُ النَّعْل) (kwa maana ya Mkarabati Viatu): Ni Hadithi yenye maana pevu kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), inayozungumzia nafasi na fadhila pekee za Imamu Ali (a.s). Kauli hii ilitamkwa na bwana Mtume (s.a.w.w) katika mazingira ambayo Imamu Ali (a.s) alikuwa katika hali ya kutiatia viraka au kukarabati viatu vya bwana Mtume (s.a.w.w). Hiyo ndiyo ikawa sababu hasa ya yeye kupewa jina la Khasifu an-Na'al, lenye maana ya “Mkarabati Viatu”. Kuna mifano mbalimbali ya Hadithi zilizokuja na ibara hii, ambazo zote zinafanana katika kutumia jina la Khassafu an-Na'al kwa Imamu Ali (a.s).

Kuna Mazingira na sifa zinayotajwa ndani ya Hadithi zilizobeba ibara hii, miongoni mwazo ni; mapambano ya Imamu (a.s) dhidi ya madhalimu na kupambana kwake kwa ajili ya kufikisha tafsiri (sahihi) ya Qur'ani. Pia miongoni mwa Hadithi hizi, kuna Hadithi zilizokuja kuthibitisha na kusisitiza nafasi na sifa nyengine kadhaa za Imamu Ali (a.s), kama vile; nafasi ya khalifa wake baada ya bwana Mtume (s.a.w.w), ujuzi wake kamili wa tafsiri ya Qurani, na haki yake katika vita vilivyotokea wakati wa zama za ukhalifa wake. Katika mifano mingine ya Hadithi zenye ibara ya “Khasifu Al-Na'al”, bwana Mtume (s.a.w.w) amemtaja Imamu Ali (a.s) kuwa ni kiongozi aongozae kwenye njia ya haki na ndiye mrithi wake katika uongozi baada yake.

Hadithi hizi zimeenea mno katika vyanzo vya pande zote mbili za madhehebu ya Kiislamu (madhebu ya Kishia na Kisunni), miongoni mwa vyanzo muhimu vilivorikodi Hadithi hizi, ni vitabu vinne muhimu vya Shia Ithnaashariya pamoja na vitabu sita vya Sunni (Sihahu Sitta). Baadhi ya wataalamu wamezitambulisha Hadithi hizi wakizipa sifa ya Hadithi Mustafidhu, (yaani ni Hadithi zilizosambaa kwa wingi mno ila ni chini ya kiwango cha Mutawatir). Pia kuna wengine waliozipa Hadithi hizi sifa ya mutawatir (zilizothibitishwa kwa mapokezi mengi yasiyo na shaka ndani yake), huku wengine wakisema kuwa ni Hadithi sahihi (zenye uhalisi wa juu kabisa).

Moja kati matukio muhimu kuhusiana na Hadithi hizi, ukumbusho wa Ummu Salama kwa bibi Aisha, ambapo alijarbu kumpa ukumbusho kupitia moja ya Hadithi hizi, na kumtaka aepukane na uasi dhidi ya Imam Ali (a.s). Katika baadhi ya ibara ya hotuba za Imam Ali (a.s), katika kuthibitisha haki yake, alionekana kutumia Hadithi za "Khasifu'n-Na'l" (zilizohusiana na ishara juu ya haki ya uongozi wake), ili kuthibitisha haki yake hiyo ya uongozi, aliyokuwa akistahiki kuipata baada ya kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w.w). Pia Hadithi hizi zimetajwa na kuakisiwa ndani ya mashairi ya watunzi mashuhuri, kama vile Sayyid Al-Himyari.

Nafasi na Umuhimu Wake

Hadithi ya Khasifu an-Na‘al au hadithi za Khasifu an-Na'al, ni mkusanyiko wa Riwaya zilizopokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), zinazobainisha daraja na sifa au fadhila za Imamu Ali (a.s), ikiwa ni pamoja na; Uimamu wake, ukhalifa wake, na juhudi zake katika kupambana na washirikina na madhalimu mbali mbali. Katika Hadithi hizi, Imamu Ali (a.s) anatajwa kwa jina la Khasifu an-Na‘al jina alilopewa pale alipokuwa akikarabati (akitia viraka) viatu vya bwana Mtume.[1] Jina Khasifu an-Na‘al ndani ya Riwaya hizi, limekuwa ni sifa maalumu kwa Imamu Ali (a.s). Jina hili ndio kiungo muhimu zinazoziunganisha na kuziweka pamoja Riwaya zote zile zilizotaja lakabu hii ndani yake.

Neno "Khasif" linamaanisha kukusanya na kuunganisha pamoja vitu vilivyoachana au vilivyochanika,[2] na mwenye kukarabati na kuvirejesha viatu katika hali yake ya awali huitwa "Khasifu an-Na‘al".[3] Ukarabati wa viatu vya Mtume Muhammad (s.a.w.w) uliofanya na Imam Ali (a.s) kunaakisi mambo yafuatayo: Unyenyekevu wa hali ya juu,[4] kutosheka na kutojali maisha ya kidunia na kuwa mfano bora wa kuridhika na maisha rahisi na ya kawaida.[5] Baada ya matumizi ya ibara hii kulikofanwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w),[6] neno "Khasifu an-Na‘al" limekuwa ni moja kati ya majina maalum yanayotumika kwa ajili ya Imam Ali (a.s).[7]

Imesemekana kuwa Riwaya hizi ni miongoni mwa maandiko muhimu (nusus) yanayothibitisha uimamu wa Maimamu (a.s),[8] na zinajumuisha baadhi ya fadhila maalum za Imamu Ali (a.s).[9] Riwaya hizi ni Hadithi zinaonesha ubora wa Imamu Ali (a.s) kuliko Masahaba wengine.[10] Ingawa Riwaya za "Khasifu an-Na‘al" humtaja Imamu kwa njia ya kutumia sifa zake makhususi, ila Riwaya hizi ni miongoni mwa Hadithi zilizo wazi kabisa kuhusiana na fadhila za Imamu Ali (a.s),[11] na ni miongoni mwa maandiko wazi yaliyo dhahiri kuhusiana na Uimamu na ukhalifa wake (a.s).[12] Baadhi ya wanazuoni wa Kishia na Kisunni wameonekana kuthibitisha umuhimu wa hadithi hizi, kwa kuzipa uzito sawa na Hadithi nyenge zinazozungumzia suala la ukhalifa wa Imamu Ali (a.s), kama vile; Hadithi ya Manzila na Hadithi ya Ghadir, ambazo zinahusiana na sifa za Imamu Ali (a.s).[13]

Tathmini Juu ya Uhalali wa Hadithi

Hashim bin Sulaiman al-Bahrani, mwanachuoni wa Shia wa karne ya 11 Hijria, anaamini kwamba Hadithi za "Khasifu an-Na‘al" zimeripotiwa kupitia Njia (isnad) tisa za kutoka katika vyanzo vya Kisunni,[14] Njia (isnad) mbili kutoka vyanzo vya Kishia.[15] Baadhi ya watafiti wanaamini kwamba; Hadithi hizi zimeenea kwa wingi mno[16] katika vyanzo vya Kishia pamoja na Kisunni.[17] Hadithi za "Khasifu an-Na‘al" Zimetajwa katika vyanzo muhimu vya madhehebu mawili haya. Miongoni mwa vyanzo muhimu vilivyonukuu Riwaya hizi ni pamoja na; Kutubu Al-Arba’a (Vitabu vinne muhimu vya Shia),[18] Vyanzo vya awali vya Kishia,[19] na hata vyanzo vilivyofuata baadaye vya Shia, vimeonekana kukariri mara kwa mara Riwaya hizi.[20] Miongoni mwa vyanzo vya kwanza vya Kisunni vilivyonuku Riwaha hizi kama vile: Sunan al-Tirmidhi,[21] Sunan al-Nasa'i,[22] Musnad Ahmad.[23] Pia, kuna vyanzo vyengine vya Sunni[24] vilivyoriko na kuakisi Haditi za "Khasifu an-Na‘al" ndani yake.[25]

Sheikh Mufidu kwa upande wake, amethibitisha kuwa baadhi ya hadithi za "Khasifu an-Na‘al" ni sahihi kwa mujibu wa pande zote mbili, yaani Shia pamoja na Sunni.[26] Al-Muqaddas Ardabili naye amezitaja Hadithi hizi kuwa ni Hadithi mashuhuri na yenye hadhi ya juu kabisa, akisisitiza suala hili ameandika akisema kuwa; hakuna yeyote yule alikuja na pingamizi fulani dhidi ya usahihi wa Hadithi hizi.[27] Baadhi ya wanazuoni wakionesha umuhimi wa Hadithi hizi, wameeleza wakisema kuwa kuna ijmaa (makubaliano ya wanazuoni) juu ya usahihi na uaminifu wa isnadi (mnyororo wa wapokezi) wa Riwaya hizi.[28] Wanazuoni wengine wa Shia wametoa mitazamo mbalimbali juu ya Riwaya hizi; baadhi wamezitambua kwa kusema kuwa ni Hadithi zenye sifa ya mustafiidh (zilizosimuliwa na idadi kubwa ya wapokezi),[29] huku wengine wakizichukulia kuwa mutawatir (zilizopokelewa kwa urudufu mkubwa kutoka kwa wapokezi wengi wa kuaminika kupitia matabaka mbali mbali).[30]

Imamu Tirmidhi, ambaye ni mwanahadithi mashuhuri kutoka upande wa madhehebu ya Kisunni, na mmoja mojawapo wa waandishi wa vitabu sita sahihi (Sihahu Sitta), ni miongoni mwa walionukuu Hadithi ya "Khasifu an-Na‘al" kutoka kwa wanahadithi wa zamani, ambaye ameithibitisha usahihi wa Hadithi hii katika kitabu chake hicho.[31] Vilevile, Ganji Al-Shafi‘i, mwanahadithi mwingine wa Kisunni, ameisifu Hadithi hii kwa kusema kuwa; Hadithi hii ni miongoni mwa Hadithi zenye hadhi ya juu, na miongoni mwa Hadithi safi na sahihi.[32]

Baadhi ya wanazuoni wa Shia wametenga sura maalum vitabuni mwao, kwa ajili ya Hadithi za "Khasifu an-Na‘al", ambazo wamezikusanya kutoka vyanzo mbalimbali, yakiwemo vyanzo vya Kishia pamoja na Kisunni.[33]

Aina za Hadithi, Tofauti Zake na Ufafanuzi Wake

Hadithi ya «Khasifu an-Na‘al» imeripotiwa kwa maneno, maudhui, na ibara mbalimbali, kulingana na nyakati na mazingira tofauti. Wataalamu wa hadithi wanasema kuwa urudufu wa matumizi ya ibara hii unaoonekana katika Hadithi mbali mbali, unaashiria msisitizo wa sifa hii maalum ya Imam Ali (a.s) kwa malengo ya kuthibitisha hadhi yake ya kipekee aliyokuwanayo Imamu huyu (a.s).[34] Baadhi ya matoleo ya Hadithi hii ni kama ifuatavyo:

Riwaya Kuhusu Kupigania Ufafanuzi sahihi au tafsiri sahihi ya Qur’ani

Katika moja ya matoleo, Hadithi yenye ibara hii inahusishwa na kauli ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliposema mbele ya Masahaba wake akisema:

إِنَّ مِنْكُمْ مَنْ يُقَاتِلُ عَلَى تَأْوِيلِ الْقُرْآنِ كَمَا قَاتَلْتُ عَلَى تَنْزِيلِهِ فَاسْتَشْرَفَ لَهَا الْقَوْمُ، وَفِيهِمْ أَبُوبَكْرٍ وَعُمَرُ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا، قَالَ أَبُوبَكْرٍ: أَنَا هُوَ، قَالَ: لَا قَالَ عُمَرُ: أَنَا هُوَ، قَالَ: لَا، وَلَكِنْ خَاصِفُ النَّعْلِ» - يَعْنِي عَلِيًّا

"Hakika, miongoni mwenu kuna mtu atakayepigania ufafanuzi wa Qur’ani kama nilivyopigania kwa ajili ya (kuufikisha) ufunuo wake". Masahaba waliokuwepo walitamani kujua ni nani anayehusika na kauli hiyo. Miongoni mwa waliouliza wakitamani kuwa na sifa ni Abu Bakr na Omar. Kila mmoja miongoni mwao alijaribu kumuuliza bwana Mtume (s.a.w.w), wakisema; "Je, mtu huyo ni mimi?" Mtume (s.a.w.w) akajibu akisema: "Hapana, bali ni mtu huyo ni yule anayerekebisha au anayekarabati viatu (Khasifu an-Na‘al) —akimrejelea Imam Ali (a.s).[35] Wakati huo, Imamu Ali (a.s) alikuwa akishughulika na kukarabati viatu vya bwana Mtume (s.a.w.w).[36] Baadhi ya watafiti wa hadithi na wafasiri wa Qur’ani wanaamini kuwa; Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliitamka Hadithi hii baada ya kushuka kwa Aya ya Qur’ani inayosisitiza umuhimu wa kurekebisha mahusiano na kudumisha amani.[37]

Watafiti wamewasilisha tafsiri mbalimbali kuhusiana na hadithi hii, maoni na mitazamo yao kuhusiana na ujumbe uliomo ndani ya Hadithi hizi ni kama ifuatavyo:

  • Uthibitisho wa Uimamu (Uongozi)

Al-Muqaddas Ardabili, mwanazuoni mashuhuri wa Kishia (aliyefariki mnamo mwaka 993 Hijria), aliichukulia Hadithi hii kuwa ni ushahidi thabiti juu ya Uimamu wa Imam Ali (a.s).[38] Kwa mujibu wa imani yake pamoja na baadhi ya wanazuoni wengine wa Kishia ni kwamba; ule ulinganisho wa mapambano ya Imamu Ali (a.s) na mapambano ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) unaonesha wazi nafasi ya Uimamu wa Imamu Ali (a.s),[39] na kuthibitisha kuwa hakuna mwingine anayestahili uongozi huo.[40] Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni wa madhehebu ya Kisunni, kama vile Imamu Shafi'i na Ibnu Taymiyya, licha ya kukubali usahihi wa Hadithi hii, ila hawakuikubali kama ni ithibati na ushahidi wa Uimamu wa Imamu Ali (a.s).[41] Imamu Shafi'i alieleza akisema kuwa; Hadithi hii inasisitiza tu namna ya kupambana na madhalimu, bila kuwa na maana ya kiutawala au kiumamu.[42]

  • Ufahamu Kamili wa Elimu ya Tafsiri ya Qur’ani

Baadhi ya wanazuoni wa Kishia wanaamini kuwa Riwaya kuhusu mapambano ya mtu aitwaye Khasifu an-Na‘al (Mtiaji Viraka au Mkarabati Viatu) kwa ajili ya ufasiri sahihi wa Qur’ani, ina nia ya kutoa uthibitisho wa kwamba; Imamu Ali (a.s) ndiye mwenye elimu kamilifu ya Qur'ani,[43] na ndiye mwenye ujuzi wa kina zaidi wa tafsiri yake kuliko wengine.[44][45] Aidha kwa mtazamo wao, Hadithi hii ni dalili tosha ya kwamba; Qur’ani Tukufu haiwezi kueleweka kikamilifu bila kuwepo kwa Imamu aliyeteuliwa na Mwenye Ezi Mungu mwenyewe. Wao pia wanaamini kwamba; Riwaya hii ni silaha kamili, dhidi ya kauli za wale wanaodai kuwa Qur’ani peke yake inatosha, na kwamba hakuna haja ya kuwepo na uongozi wa Maasumina (Viongozi wasio na dosari) katika kufafanua Aya zake na kutoa sura kamili ya ujumbe wa Qur’ani tukufu.[46]

  • Haki ya Imam Ali (a.s) Katika Vita Vilivyojiri Ndani ya Utawala Wake

Baadhi ya wanazuoni wanasema kwamba maneno ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika Hadithi hizi ni utabiri wa haki ya Imam Ali (a.s) katika vita alivyovipigana wakati wa ukhalifa wake dhidi ya makundi matatu:

  1. Nakithin – Wale waliovunja ahadi zao (vita vya Jamal).
  2. Qasithin – Watu waovu na madhalimu (vita vya Siffin).
  3. Mariqin – Wale waliotoka kwenye taa na kupotoka (vita vya Nahrawan).[47]

Wengine wamezifasiri hadithi hizi kuwa ni ishara ya uasi (uritadi) wa wale waliompinga Imam Ali (a.s) na kupigana naye.[48]

Simulizi Kuhusu Kupambana na Washirikina

Kulingana na ripoti ya Hakim al-Nayshaburi (mwanachuoni wa madhehebu ya Kishafi'i wa karne ya 4 Hijria), ni kwamba; Wakati wa mazungumzo ya Hudaibia, Suhail bin Amru, akiwa pamoja na viongozi wengine wa washirikina, walifikia mbele ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na kuweka moja ya masharti ya mkataba wa amani usemao kwamba: "Iwapo mmoja yeyote kati yetu sisi (Makuraishi) ataingia upande wenu, basi ni lazima mumrudishe kwetu sisi". Sharti hili lilimkasirisha mno bwana Mtume (s.a.w.w), na katika kujibu sharti alisema:

لَتَنْتَهُنَّ‌ يَا مَعْشَرَ قُرَيْشٍ‌ أَوْ لَيَبْعَثَنَّ اَللَّهُ إِلَيْكُمْ رَجُلاً اِمْتَحَنَ اَللَّهُ قَلْبَهُ‌ لِلْإِيمَانِ يَضْرِبُ رِقَابَكُمْ عَلَى اَلدِّينِ‌ فَقَالَ بَعْضُ مَنْ حَضَرَ يَا رَسُولَ اَللَّهِ أَبُو بَكْرٍ ذَلِكَ اَلرَّجُلُ قَالَ‌ لاَ قِيلَ فَعُمَرُ قَالَ لاَ وَ لَكِنَّهُ خَاصِفُ اَلنَّعْلِ فِي اَلْحُجْرَةِ فَتَبَادَرَ اَلنَّاسُ إِلَى اَلْحُجْرَةِ يَنْظُرُونَ مَنِ اَلرَّجُلُ فَإِذَا هُوَ أَمِيرُ اَلْمُؤْمِنِينَ عَلِيُّ بْنُ‌ أَبِي طَالِبٍ عَلَيْهِ السَّلاَمُ‌؛

«Enyi kundi la Makuraishi! Ima mtaachana na ukorofi wenu huu, la si hivyo, Mwenyezi Mungu atamtuma mtu ambaye amejaribiwa moyo wake kwa mtihani wa imani, ambaye atakakuja kuzikata shingo zenu kwa ajili ya (kuhuisha) dini ya Mwenye Ezi Mungu». Baada ya bwana Mtume (s.a.w.w) kutoa kauli hiyo, baadhi ya masahaba walimuuliza wakisema: «Je, mtu huyo ni Abu Bakr au Omar?" Mtume (s.a.w.w) akawajibu akisema: "Hapana! Bali Yeye ni yule anayetia viraka (anayekarabati) viatu vyangu». Baada ya masahaba kusikia kauli hiyo walikimbilia ndani ya chumba na kumkuta Amir al-Mu'minin Ali bin Abi Talib (a.s) akiwa ameshika viatu vya bwana Mtume (s.a.w.w), huku akiwa ameshughulika na kuvikarabati viatu hivyo.[49]

Sayyid Hashim Bahrani alipokuwa akiielezea Riwaya hii, alisema kwamba; Riwaya hii ilikuwa ni onyo maalumu kwa kabila la Thaqif,[50] huku Al-Nasa'i akisema kwamba; Riwaya hiyo ilikuwa ni onyo kwa kabila la Banu Wali'ah (kutoka eneo la Kinda au Hadramaut).[51]

  • Uthibitisho wa Uimamu wa Imam Ali (a.s)

Baadhi ya wanazuoni wameitazama na kuichukulia Hadithi hii kama dalili wazi katika kuthibitisha nafasi ya Uimamu wa Imam Ali (a.s). Wao wamesisitiza maoni yao hayo wakisema kwamba: Kupambana na washirikina na kukata shingo zao kulikuwa ni amri ya moja kwa moja kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu. "Yule anayetia viraka vya viatu" (kwa mujibu wa Riwaya hii), yule ambaye "moyo wake umejaribiwa kupitia mtihani wa imani," ndiye mtu pekee aliyestahili nafasi ya Uimamu na uongozi wa kiroho baada ya bwana Mtume (s.a.w.w), kwa hiyo yeye ndiye mrithi wa bwana Mtume (s.a.w.w) katika kuilinda na kuieneza dini ya Mwenye Ezi Mungu.[52]

Hadithi Inayobainisha Warithi wa Nafasi ya Bwana Mtume (s.a.w.w)

Al-Hurr al-‘Amili, mwanazuoni mashuhuri wa hadithi na fiqhi wa pande wa madhehebu ya Kishia, amenukuu Riwaya kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w), ambayo ndani yake ametajwa Imamu Ali (a.s), kwa lakabu ya Khasifu an-Na'al (Mkarabati Viatu). Katika Hadithi hii, imeelezwa wazi kwamba; Imamu Ali (a.s) ndiye khalifa wa bwana Mtume (s.a.w.w), na kwamba uongozi wa umma unapaswa kushikwa na kizazi cha Imamu Ali (a.s) kupitia kwa Imamu Hussein (a.s).[53] Katika Hadithi nyingine, Al-Hurr al-‘Amili anasimulia akisema kwamba; pale bwana Mtume (s.a.w.w), alipoulizwa na Abu Bakr na Omar kwamba, ni nani atakayekuwa khalifa baada yake, alimtaja Khasifu an-Na'al kuwa ndiye mrithi wake, tokeo ambalo lilijiri pale Imamu Ali (a.s) alipokuwa ameshughulika na kushona na kukarabati viatu vya bwana Mtume (s.a.w.w).[54] Pia kuna Hadithi nyengine yenye maudhui kama haya kutoka kwa Aisha.[55]

Abu al-Salah Halabi (aliyefariki mnamo mwaka 447 Hijria) katika kitabu chake Taqribu al-Ma‘arif, anasimulia akiema kwamba; Pale bwan Mtume (s.a.w.w), alipokuwa katika moja ya safari zake, aliwaambia Abu Bakar na Omar wampe wamsalamu Khasifu an-Na'al kwa kwa kutumia jina la Amiru al-Mu’minin (Kiongozi wa Waumini), tukio lililotokea pale Imamu Ali (a.s) alipokuwa ameshughulika na kurekebisha viatu vya bwana Mtume (s.a.w.w).[56]

Riwaya ya Mwongozi wa Umma

Moja ya Riwaya alizozinukuu Al-Khazzaz, mwandishi wa kitabu Kifayat al-Athar, ni ile Riwaya isemayo kwamba; Pale Mtume Muhammad (s.a.w.w), alipokuwa akifafanua maana ya neno mwongozi «هَادٍ» katika Aya ya saba ya Surat Ar-Ra'ad, alimtaja Imamu Ali (a.s) kwa jina la Khasifu an-Na'al, jambo lililotendeka wakati ambao Imamu Ali (a.s) alikuwa ameketi kando, akishughulika na kurekebisha viatu vya bwana Mtume (s.a.w.w). Baada ya bwana Mtume (s.a.w.w) aliendelea kueleza fadhila na sifa za Imamu Ali (a.s), kisha akawataja Maimamu watakaofuata baada yake. Akitambulisha idadi ya Maimamu hao, alisema kwamba; Idadi yao, ni Maimamu kumi na mbili, sawa na idadi ya viongozi wa Bani Isra’il, na akamtaja Imamu Mahdi (a.f), kisha akasema kwamba, Imamu Mahdi (a.f) ndiye Imamu wa kumi na mbili, amabye ni hitimisho la Maimamu hao. [57]

Matumizi Hadithi ya Mshona Viatu Kama Ithibati Maalumu

Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti za kihistoria ni kwamba; pale Aisha alipoamua kumuasi Imamu Ali (a.s), alimwomba Ummu Salama afungamane naye.[58] Hata hivyo, Ummu Salama alimkatalia suala hilo, na badala yake akampa ushauri wa kutotimiza dhamira hiyo. Baada ya Ummu Salam kumpa nasaha hiyo, alijaribu kumkumbusha (Aisha) fadhila za Imamu Ali (a.s), ambapo katika ukumbusho wake huo, alirejelea Riwaya ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), iliyomtaja mrithi wake kwa laqabu ya Mkarabati Viatu.[59] Aisha naye hakupingana na ukweli wa maneno ya Ummu Salama[60], ila hakukubali kuachana na msimamo wake wa kupingana na Ali (Ali), na akaendelea kumkosoa na kumshutumu Imam Ali (a.s).[61] Kwa mujibu wa baadhi ya simulizi, baada ya Aisha kusikia maneno ya Ummu Salama, aligutuka na kuelewa kwamba ilikuwa vyema kuachana na uasi dhidi ya Imamu Ali (a.s), ila Abdullah bin Zubair alimshawishi asibadili uamuzi wake.[62]

Hata Imamu Ali (a.s) mwenyewe pia, alirejelea Hadithi za Khasifu an-Na'al katika baadhi ya hotuba zake,[63] na kujivunia heshima hiyo aliyopewa na bwana Mtume (s.a.w.w).[64] Kwa mfano, Ahmad bin Ali Tabarsi, mwahadithi na mwanatheolojia mashuhuri wa Kishia wa karne ya sita Hijria, katika kitabu chake Al-Ihtijaj, amenukuu moja ya Riwaya inayosimulia jinsi Imamu Ali (a.s) alivyotumia Hadithi hizo wakati wa Vita vya Jamal, kama ni hoja thabiti ya kuthibitisha haki yake ya kushika hatamu za uongozi.[65]

Sababu ya Kutumia Lakabu Hii

Imeelezwa kuwa; Bwana Mtume (s.a.w.w) alitumia laqabu ya Khasifu an-Na'al kwa Imamu Ali (a.s), ili kudhihirisha upeo wa unyenyekevu wake, licha ya cheo chake maalum na uhusiano wake wa karibu na Mtume (s.a.w.w). Matumizi ya jina hili, yanaonesha upeo wa hekima za bwana Mtume (s.a.w.w) aliokuwa nao, kiasi ya kwamba, kwa kutumia jina hilo lenye lugha ya mafumbo ilioko nyuma ya pazia, aliwaelekeza watu wa umma wake, kwenye welewa wa kumtambua kiongozi maalumu atakayefuata baada ya bwana Mtume (s.a.w.w).[66] Baadhi ya wanazuoni wanaamini kuwa matumizi ya laqabu au jina jipya kwa mtu fulani badala ya jina lake maarufu, husaidia kudumu kwa dhana inayokusudiwa kufikishwa katika fikra za watu. Kwa hivyo, bwana Mtume (s.a.w.w), kwa kutumia vielezi au sifa mbalimbali katika kumtambulisha Imamu Ali (a.s), alimfanya mtambulishwa wake (Imamu Ali), (a.s) kudumu zaidi katika kumbukumbu za watu mbali mbali. Mfano wa mtindo huu ni yale matumizi ya jina la Abu Turaab kwa Imamu Ali (a.s), jambo ambalo lilifuata mwelekeo huo huo wa kuthibitisha nafasi yake adhimu.[67]

Hadithi ya Khasifu an-Na'al Katika Mashairi na Nudhumi Mbali Mbali

Kitabu Khasifu an-Na'al al-Nabii (s.a.w.w)

Riwaya zinazohusiana na lakabu ya "Khasifu an-Na'al", ni miongoni mwa Riwaya zilizopata nafasi maalumu ndani ya mashairi ya washairi mbalimbali katika historia.[68] Miongoni mwa washairi alitumia lakabu hiyo ndani ya mashairi yao, ni pamoja na; Sayyid Himyari,[69] Abu ʿAlawiyyah al-Isfahani na Sayyid Mahdi Bahru al-Uluum. Hawa ni baadhi ya washairi walioashiria au kuitaja Hadithi ya "Khasifu an-Na'al" ndani ya mashairi yao, amabo wameitaja lakabu ya[70] "Khasifu an-Na'al" kama ni lakabu maalumu kwa Imamu Ali (a.s).[71] Kuna vitabu kadhaa vilivyorikodi na kunukuu mashairi haya.[72]

Kazi Andhishi Kuhusiana na Mada Husika (Monografia)

  • Kitabu "Ali (a.s) Khasifu an-Na'al Al-Nabi (s.a.w.w) wa Qiraʾatun fi Rumuzi al-Ḥaditi wa Maʿaniihi", ni kitabu kilichoandikwa kwa lugha ya Kiarabu na Majid ʿAtiyyah. Mwandishi, katika kunukuu Hadithi hii ya bwana Mtume (s.a.w.w) yenye lakabu ya "Khasifu an-Na'al", analenga kuthibitisha Uimamu na ukhalifa wa Imamu Ali (a.s), upaswao kumfikia yeye, mara tu baada ya kufariki bwana Mtume (s.a.w.w).[73]
  • Tasnifu ya uzamili yenye kichwa kisemacho: Ithbate Imamat Bila Fasli Amiiri Al-Muuminina Dar Muqaatile "Khasifu an-Na'al", Baa Taakiid Bar Rawesh Allame Miir Hamid Hussein. Kiswahili ni (Thibitisho la Uimamu wa Moja kwa Moja wa Amir al-Muuminina (a.s) katika Hadithi ya Mapigano (Haditi ya "Khasifu an-Na'al", inayohusiana na mapambano ya Ali kwa ajili ya tafasiri sahihi ya Qur’ani), kwa Kuzingatia Mtazamo wa Allama Mir Ḥamid Hussein". Tasnifu hii imeandikwa kwa lengo la kuangaza uhakiki na uchambuzi wa maana ya Hadithi hii.[74]
  • Makala yenye kichwa kisemacho; Maanakavi Riwayathaye Jange Taawiil, Kiswahili; «Uchambuzi wa Maana wa Riwaya za Vita kwa ajili Tafsiri (Taʾwil)». Makala hii ni Makala inayochunguza maana sahihi ya neno «tafsiri» au (taʾwil) katika Riwaya ya "Khasifu an-Na'al», inayozungumzia mapambano kwa ajili ya muktadha wa tafsiri ya Qur’ani Tukufu.[75]

Makala Zinazo Fungamana

Rejea

  1. Bahrani, Ghayat al-Maram, 1422 AH, juz. 6, uk. 285; Irbali, Kashf al-Ghamma, 1381 AH, juz. 1, uk. 335; Allama Hilli, Nahj al-Haqq, 1982, uk. 220, Ibn Shahr-Ashub Mazandarani, Manaqib Aal Ali Abi Talib (a.s), 1379 AH, juz. 3, uk. 44.
  2. Ibn Mandhur, Lisan al-Arab, Beirut, juz. 9, uk. 71.
  3. Tabataba'i, Al-Mizan, 1417 AH, juz. 8, uk. 35.
  4. Atiyah, Ali (a.s), Khasifu an-Na‘al al-Nabii (a.s), 1436 AH, uk. 13.
  5. Makarim Shirazi, Payam Imamu Amir al-Mu'minin (a.s), 1385 S, juz. 2, uk. 303.
  6. Fadhil Lankarani, Ayat at-Tat-hir Ruuyat Mub-takirah, 1424 AH, uk. 138.
  7. Sibti Ibn al-Jawzi, Tadhkirat al-Khawas, 1418 AH, uk. 16; Muqaddas Ardabili, Hadiqa al-Shi'a, 1383 S, juz. 1, uk. 16; Shi'i Sabzawari, Rahat al-Arwah, 1378 S, uk.86.
  8. Halabi, Taqriib al-Maarif, 1404 AH, uk. 202.
  9. Sheikh Mufid, Al-Ifsah Fi al-Imamah, 1413 AH, uk. 136.
  10. Kundi la Waandishi, Fi Rihab Ahlul-Bayt (a.s), 1426 AH, juz. 22, uk. 52.
  11. Mudhaffar, Dalai al-Sidq, 1422 AH, juz. 5, uk. 85.
  12. Muqaddas Ardabili, Hadiqa al-Shi'a, 1383 S, juz. 1, uk. 16; Shi'i Sabzawari, Rahat al-Arwah, 1378 S, uk.86; Tabari, Kamil al-Baha'i Fi al-Saqifa, 1426 AH, juz.2, uk. 220; Atiyah, Ali (a.s), Khasifu an-Na‘al al-Nabii (s.a.w.w), 1436 AH, uk. 123.
  13. Kashf al-Ghitah, Kashf al-Ghitah, 1422 AH, juz. 1, uk.37; Ibn Abi al-Hadid, Sherh Nahjul al-Balagha Li Ibn Abi al-Hadid, 1383 S, juz. 9, 28; Bahrani, Ghayat al-Maram, 1422 AH, juz. 2, uk. 69.
  14. Bahrani, Ghayat al-Maram, 1422 AH, juz. 6, uk. 285.
  15. Bahrani, Ghayat al-Maram, 1422 AH, juz. 6, uk. 169.
  16. Kashif al-Ghita, Al-Aqaid al-Jaafariyyah, 1425 AH, uk. 74; Kashf al-Ghita, 1422 AH, juz. 1, uk. 37.
  17. Ibn Shadhan Neyshaburi, Al-Idhahu, 1363 S, uk. 451.
  18. Kulayni, Al-Kafi, 1407 AH, juz. 5, uk. 11; Sheikh Tusi, Tahdhib al-Ahkam, 1407 AH, juz. 4, uk. 116.
  19. Qomi, Tafsir al-Qomi, 1404 AH, juz. 2, uk. 321; Sheikh Mufid, Al-Irshad, 1413 AH, juz. 1, uk. 122; Sheikh Mufid, Al-Ikhtasas, 1413 AH, uk. 119; Ibn Hayyun, Sherh al-Akhbar, 1409 AH, juz. 1, uk. 203; Sheikh Saduq, Al-Khisal, 1362, juz. 1, uk. 275; Sheikh Tusi, Amali, 1414 AH, uk. 254.
  20. Tazama: Allamah Hilli, Kashf al-Yaqin, 1411 AH, uk. 137; Allamah Hilli, Nahj al-Haq, 1982, uk. 220; Tabrasi, Al-Ilam Al-Waraa, 1390 AH, uk. 189; Ibn Shahr-Ashub Mazandaran, Manaqib Aal Abi Talib (a.s), 1379 AH, juz. 3, uk. 44.
  21. Tirmidhi, Sunan Tirmidhi, 1419 AH, juz. 5, uk. 452.
  22. Nasa'i, Sunan al-Nasa'i, 1411 AH, juz. 5, uk. 127-128.
  23. Ibn Hanbal, Musnad al-Imam Ahmad bin Hanbal, 1416 AH, juz. 17, uk. 391.
  24. Tazama: Ibn al-Maghazili Shafi'i, 1424 AH, uk. 99; Hakim Neishaburi, al-Mustadrak Ala al-Sahihein, 1411 AH, juz. 2, uk. 149; Muttaqi Hindi, Kanz al-Ummal, 1989, juz. 13, uk. 99, 147; Ibn Abi al-Hadid, Sherh Nahj al-Balagha Li Ibn Abi al-Hadid, 1383, juz. 6, 217.
  25. Tazama: Sharaf al-Din, Al-Muraj'aat, 1426 AH, uk. 346; Firouz-Abadi, Fadhail al-Khamsa, 1392 AH, juz. 2, uk. 349-350.
  26. Sheikh Mufid, Al-Jamal, 1413 AH, uk. 80.
  27. Muqaddas Ardabili, Hadiqat al-Shi'a, 1383 S, juz. 1, uk. 232.
  28. Atiyah, Ali (a.s), Khasifu an-Na‘al al-Nabii (s.a.w.w), 1436 AH, uk. 19.
  29. Sheikh Mufid, Al-Jamal, 1413 AH, uk. 80; Sheikh al-Sharia Isfahani, Al-Qaul al-Sarah Fi Naqd al-Sihah, Qom, uk. 217; Atiyah, Ali (a.s), Khasifu an-Na‘al al-Nabii (s.a.w.w), 1436 AH, uk. 12.
  30. Sharaf al-Din, al-Mura'ajat, 1426 AH, uk. 319; Kashf al-Ghitah, Kashf al-Ghitah, 1422 AH, juz. 1, uk. 37.
  31. Tirmidhi, Sunan Tirmidhi, 1419 AH, juz. 5, uk. 452.
  32. Ganji Shafi'i, Kifayat al-Talib, 1404 AH, uk. 98.
  33. Bahrani, Ghayat al-Maram, 1422 AH, juz. 6, uk. 285; Irbali, Kashf al-Ghamma, 1381 AH, juz. 1, uk. 335; Allamah Hilli, Nahj al-Haq, 1982, uk. 220. Mar-ashi, Ihqaq al-Haq, 1409 AH, juz. 5, uk. 613-606; Mudhaffar, Dalail al-Sidq, 1422 AH, juz. 5, uk. 85-92; Naqwi, Abqat al-Anwar, 1366 S, juz. 15, uk. 100; Ibn Shahr-Ashub Mazandaran, Manaqib Aal Abi Talib (a.s), 1379 AH, juz. 3, uk. 44.
  34. Atiyah, Ali (a.s), Khasifu an-Na‘al al-Nabii (s.a.w.w), 1436 AH, uk. 19.
  35. Hakim Neishaburi, Al-Mustadrak Ala al-Sahihein, 1411 AH, juz. 3, uk. 132.
  36. Ibn Hanbal, Musnad al-Imam Ahmad bin Hanbal, 1416 AH, juz. 17, uk. 391, juz. 18, uk. 296. Kwa tofauti kidogo katika: Ibn Atiyah, Abhi al-Midad, 1423 AH, juz. 1, uk. 37; Sheikh Mufid, Al-Ifsah Fi al-Imamah, 1413 AH, uk. 135; Milani, Tashiid al-Murajaat, 1427 AH, juz. 3, uk. 282; Tabari, al-Mustarshid Fi Imamat Ali bin Abi Talib (a.s), 1415 AH, uk. 357; Sayyid Ibn Tawus, al-Taraif, 1400 AH, juz. 1, uk. 70; Mar-ashi, Ihqaq al-Haq, 1409 AH, juz. 31, uk. 149.
  37. Qomi, Tafsir al-Qomi, 1404 AH, juz. 2, uk. 321; Kulayni, Al-Kafi, 1407 AH, juz. 5, uk. 11; Ibn Shuubah Harani, Tuhf al-'Uqul, 1404 AH, uk. 289; Sheikh Tusi, Tahdhib al-Ahkam, 1407 AH, juz. 4, uk. 116.
  38. Muqaddas Ardabili, Hadiqat al-Shi’a, 1383 S, juz. 1, uk. 232.
  39. Muqaddas Ardabili, Hadiqat al-Shi’a, 1383 S, juz. 1, uk. 233; Bayadhi, Al-Sirat al-Mustaqiim, 1384 S, juz. 2, uk. 63.
  40. Mudhaffar, Dalail al-Sidq, 1422 AH, juz. 6, uk. 154.
  41. Milani, Tashiid al-Muraja’at, 1427 AH, juz. 1, uk. 469, Imenukuliwa na Ibn Taymiyyah; Muqaddas Ardabili, Hadiqat al-Shi’a, 1383 S, juz. 1, uk. 232, Iliyonukuliwa na Shafi’i.
  42. Mudhaffar, Dalail al-Sidq, 1422 AH, juz. 6, uk. 154; Muqaddas Ardabili, Hadiqat al-Shi’a, 1383, juz. 1, uk. 232, Iliyonukuliwa na Shafi’i
  43. Husseini Tehrani, Imam-shenasi, 1426 AH, juz. 2, uk. 148.
  44. Ibn Atiyah, Abhi al-Madad, 1423 AH, juz. 1, uk. 38.
  45. Husseini Tehrani, Imam-shenasi, 1426 AH, juz. 2, uk. 148.
  46. Husseini Tehrani, Imam-shenasi, 1426 AH, juz. 2, uk. 148.
  47. Naqwi, Abaqat al-Anwar, 1366 AH, juz. 11, uk. 166; Sheikh Mufid, al-Jamal, 1413 AH, uk. 79; Sultan al-Wa’izin Shirazi, Shabhaye Peshawar, 1379 AH, uk. 901.
  48. Sultan al-Wa’izin Shirazi, Shabhaye Peshawar, 1379 AH, uk. 901.
  49. Tirmidhi, Sunan Tirmidhi, 1419, juz. 5, uk. 451; Sheikh Mufid, Al-Irshad, 1413 AH, juz. 1, uk. 122; Tabrasi, Ilam al-Wari, 1390 AH, uk. 189; Mar-ashi, Ihqaq al-Haq, 1409 AH, juz. 5, uk. 606.
  50. Bahrani, Ghayat al-Maram, 1422 AH, juz. 6, uk. 286.
  51. Nasa'i, Sunan al-Nasa'i, 1411 AH, juz. 5, uk. 127-128.
  52. Arbali, Kashf al-Ghamah, 1381 AH, juz. 1, uk. 336-337; Bayadhi, Al-Sirat al-Mustaqeem, 1384 AH, juz. 2, uk. 63; Muqaddas Ardebili, Hadiqa al-Shi'a, 2004, juz. 1, uk. 232.
  53. Sheikh Hurr Amili, Ithbat al-Hudaat, 1422 AH, juz. 2, uk. 257.
  54. Sheikh Hurr Amili, Ithbat al-Hudaat, 1422 AH, juz. 3, uk. 123.
  55. Tabari, Al-Mustarshid Fi Imamat Ali ibn Abi Talib (a.s), 1415 AH, uk. 622; Sheikh Hurr Amili, Ithbat al-Hudaat, 1422 AH, juz. 3, uk. 275; Bahrani, Ghayat al-Maram, 1422 AH, juz. 1, uk. 242.
  56. Halabi, Taqrib al-Ma’rif, 1404 AH, uk. 203.
  57. Khazzaz, Kifāyat al-Aṣhar, 1401 AH, uk. 88.
  58. Tabari, Kamil al-Baha'i fi al-Saqifa, 1426 AH, juz. 2, uk. 218-220.
  59. Ibn Abi al-Hadid, Sherh Nahj al-Balaghah Li Ibn Abi al-Hadid, 1383, juz. 6, uk. 217; Tabrasi, al-Ihtjaj, 1403 AH, juz. 1, uk.166; Sheikh Hurr Amili, Ithbat al-Hudaat, 1422 AH, juz. 3, uk.123, 156; Bahrani, Ghayat al-Maram, 1422 AH, juz. 1, uk. 242; Sultan al-Wa'idhin Shirazi, Shabhaye Peshawar, 1379 S, uk. 740.
  60. Tabari, Kamil al-Baha'i fi al-Saqifa, 1426 AH, juz. 2, uk. 218-220.
  61. Sultan al-Wa'idhin Shirazi, Shabhaye Peshawar, 1379 S, uk. 741.
  62. Tabari, Kamil al-Baha'i fi al-Saqifa, 1426 AH, juz. 2, uk. 218-220.
  63. Ibn Shadhan Neyshaburi, Al-Idhahu, 1363 S, uk. 451; Bahrani, Ghayat al-Maram, 1422 AH, juz. 6, uk. 286; Majlisi, Bihar al-Anwar, 1403 AH, juz. 26, uk. 4.
  64. Mughniyeh, Al-Jawamiu wa Al-Fawarq, 1414 AH, uk. 179.
  65. Tabrasi, Al-Ihtjaj, 1403 AH, Juz. 1, uk. 170.
  66. «Name-Burdan Az Amir al-Muuminiin (a.s) Ba Onuan Khasifu an-Na'al Ya «Kafshiduz», Tovuti ya Thaqlain.
  67. «Name-Burdan Az Amir al-Muuminiin (a.s) Ba Onuan Khasifu an-Na'al Ya «Kafshiduz», Tovuti ya Thaqlain.
  68. Ibn Shahr-Ashub Mazandaran, Manaqib Aal Abi Talib (a.s), 1379 AH, juz. 3, uk. 45.
  69. Sheikh Hurr Amili, Ithbat al-Hudaat, 1422 AH, juz. 3, uk. 341; Al-Ghadir, juz. 2, 450; Ibn Shahr-Ashub Mazandaran, Manaqib Aal Abi Talib (a.s), 1379 AH, juz. 3, uk. 45.
  70. Atiyah, Ali (a.s), Khasifu an-Na'al al-Nabii (s.a.w.w), 1436 AH, uk. 131.
  71. Sibt Ibn al-Jawzi, Tadhkirat al-Khawas, 1418 AH, uk. 45; Muhaddis Urmuwa, Taaliqat Naqdhi, 1409 AH, juz. 2, uk. 976.
  72. Sheikh Hurr Amili, Ithbat al-Hudaat, 1422 AH, juz. 3, uk. 341; Al-Ghadir, juz. 2, 450; Ibn Shahr-Ashub Mazandaran, Manaqib Aal Abi Talib (a.s), 1379 AH, juz. 3, uk. 45.
  73. Atiyah, Majd bin Ahmad, Ali (a.s), Khasif Naal al-Nabii (s.a.w.w), Karbala, al-Utbah al-Husainiyyah al-Muqadassa, 1436 AH.
  74. [https://emamat.org/andishe-1335/ «Ithbat Imamat Bila Fasile Amir al-Muuminiin (a.s) Dar Hadith Muqatilihi Barresi Shud» Paygha Jamie Itilaat Risani Imamat.
  75. Muradi, Muhammad, «Maana-Kavi Riwayatihaye Jange Taawil», Nashiriye Ulum Hadith, juz. 19, Toleo la 74, Na. 74, 1394 S.

Vyanzo

  • Ibn Abi al-Hadid, Sherh Nahj al-Balaghah Li Ibn Abi Al-Hadid, Qom, Maktabat Ayatullah al-Marashi, 1383 S.
  • Ibn Hanbal, Ahmad bin Muhammad, Musnad al-Imam Ahmad bin Hanbal, Beirut, Muasasat al-Risala, 1416 AH.
  • Ibn Hayyun, Nu'man Ibn Muhammad, Sherh al-Akhbar Fi Fadha'il al-Imam al-At-har (a.s), Qom, Jamia Madrasein, 1409 AH.
  • Ibn Shadhan Neishabouri, Fadhl, Al-Idhah, Tehran, Intisharat Daneshghah Tehran, 1363 S.
  • Ibn Shuu'ba Harani, Hassan bin Ali, Tuhaf al-Aqoul An Aal al-Rasul (s.a.w.w), Qom, Jamia Madrasein, Chapa ya Pili, 1404 AH.
  • Ibn Shahr-Ashub Mazandarani, Muhammad Bin Ali, Manaqib Aal Abi Talib (a.s), Qom, Allamah, 1379 AH.
  • Ibn Atiyah, Jamil Hamoud, Abha Al-Maddad Fi Sherh Muutamar Ulamai Baghdad, Beirut, Muasasat Al-Alamy, 1423 AH.
  • Ibn Al-Maghazili Shafi'i, Manaqib Ibn Al-Maghazili al-Shafi'i, Beirut, Dar al-Adhwaa, Chapa ya Tatu, 1424 AH.
  • Ibn Mandhur, Muhammad Ibn Makram, Lisan al-Arab, Beirut, Dar Sadr, Chapa ya Tatu, Beta.
  • Arbali, Ali ibn Isa, Kashf al-Ghamma Fi Ma’rifat al-Aimah, Tabriz, Bani Hashimi, 1381 AH.
  • Bahrani, Sayyid Hashim Ghayat al-Maram wa Hujjat al-Khisam Fi Taayiin al-Imam Min Tariq al-Khisam, Beirut, Tarikh al-Tarikh al-Arabiya, 142 AH.
  • Bayadhi, Ali bin Yunus, Al-Sirat al-Mustaqiim Ila Mustahaqa al-Taqdir, Qom, Al-Maktab al-Murtadhawiyyah, 1384 AH.
  • Tirmidhi, Muhammad bin Isa, Al-Jamiu al-Sahih wahuwa Sunan al-Tirmidhi, Cairo, Dar al-Hadith, 1419 AH.
  • Halabi, Abu al-Salah, Taqrib al-Ma'arif, Qom, Intisharat al-Hadi, 1404 AH.
  • Khazaz Qummi, Ali ibn Muhammad, Kifayat al-Athar, Qom, Intisharat Bidor, 1401 AH.
  • Sibt Ibn Jawzi, Yusuf bin Qazawughli, Tadhkirat al-Khawas Min Ummah Fi Dhikir Khasais al-Aimah, Qom, Manshurat al-Sharif al-Ridha, 1418 AH.
  • Sultan al-Wa'idhin Shirazi, Shabhaye Peshawar Dar DifainA Harim Tashayui, Tehran, Dar al-Kutb al-Islamiyya, Chapa ya 39, 1379 AH.
  • Sayyid bin Tawus Hassani, Ali bin Musa, Al-Tara'if Fi Maa'rifat Madhahib al-Ta'if, Qom, Khayyam, 1400 AH.
  • Sharaf al-Din, Sayyid Abdul-Hussein, Al-Mujahid, Qom, Al-Majmau Ahlul-Bayt, Chapa ya Pili, 1426 AH.
  • Sheikh Saduq, Muhammad bin Ali, Al-Khisal, Qom, Jamia al-Mudrasein, 1362 AH.
  • Sheikh Tusi, Muhammad bin al-Hassan, Al-Amali, Qom, Dar al-Thaqafa, 1414 AH.
  • Sheikh Tusi, Muhammad bin al-Hassan, Tahdhib al-Ahkam, Tahqiq Khurasan, Tehran, Dar al-Kutb al-Islamiyyah, Chapa ya Nne, 1407 AH.
  • Sheikh Shara’i Isfahani, Al-Qawl al-Sirah Fi Naqd al-Sihah, Qom, Muasasat Imam Sadiq (a.s), Beta.
  • Sheikh Hurr Amili, Muhammad bin Hassan, Ithbat al-Hudat, Beirut, Muasasat Al-Alami, 1422 AH.
  • Sheikh Mufid, Muhammad bin Muhammad bin Nu’man, Al-Ikhtasas, Qom, Sheikh Mufid Congress, 1413 AH.
  • Sheikh Mufid, Muhammad bin Muhammad bin Nu'man, Al-Irshad Fi Ma'rifat Hujjaj-llah Ala al-Ibad, Qom, Sheikh Mufid Congress, 1413 AH.