Nenda kwa yaliyomo

Hadithi ya Jabir

Kutoka wikishia
Hadithi ya Jabir katika madhabahu ya Al-Jayto Msikiti wa Isfahan-Iran.

Hadithi ya Jabir (Kiarabu: حديث جابر), ni hadithi ambayo imenukuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ambayo ndani yake kumebainishwa majina yote ya Maimamu kumi na mbili. Hadithi hii aliisema Mtume (s.a.w.w) akijibu swali la Jabir bin Abdallah al-Ansari kuhusiana na mfano na kielelezo cha Ulul al-Amr katika Aya ya Ulul Amr. Katika hadithi hii kadhalika kuliashiriwa jina la Baqir ambalo ni lakabu ya Imam wa tano wa Mashia. Mashia wakiwa na lengo la kuthibitisha Uimamu na kuainisha Maimamu wao wamekuwa wakitumia hadithi hii iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w).

Hadithi ya Jabir imenukuliwa pia katika vyanzo vya Kishia kama Kifayat al-Athar, Kamal al-Din na Bihar al-Anwar. Aidha hadithi hii imenukuliwa katika vyanzo vya Kisuni kama Yanabiul Mawaddah. Kadhalika katika baadhi ya tafsiri za Kishia hadithi hii imetajwa wakati wa kufasiri Aya ya Ulul Amr.

Andiko la hadithi

Baada ya kushuka Aya ya kutii, Jabir bin Abdillah al-Ansari alimuuliza Bwana Mtume (s.a.w.w): Ewe Mtume wa Allah! sisi tumemtambua Mwenyezi Mungu na Mtume, sasa hawa Ulul Amr ni akina nani ambao Mwenyezi Mungu amewaweka bega kwa bega na pamoja na Yeye na wewe ili na wao watiiwe? Katika kujibu swali hili la Jabir, Bwana Mtume (s.a.w.w) alisema: “Wao ni warithi wangu na Maimamu wa Waislamu baada yangu ambapo wa kwanza wao ni Ali bin Abi Twalib na baada yake kwa utaratibu anafuata Hassan, Hussein, Ali bin Hussein na Muhammad bin Ali ambaye katika Torati ni mashuhuri kwa jina la Baqir na wewe utakutana naye uzeeni, na utakapomuona basi mfikishie salamu zangu. Baada yake ni Muhammad bin Ali kwa utaratibu, kisha Jafar bin Muhammad, Mussa bin Jafar, Ali bin Mussa, Muhammad bin Ali, Ali bin Muhammad, Hassan bin Ali na baada yake ni mwanawe ambaye jina na kuniya yake ni kama yangu. Yeye ndiye atakayeghibu na kutoweka katika upeo wa macho ya watu na ghaiba yake itakuwa ndefu kiasi kwamba, watakaobakia katika itikadi kuhusu yeye ni wale tu ambao wana imani ya kweli. [1]

Mpokezi na yaliyomo

Hadithi hii imenukuliwa na Jabir bin Abdillah al-Ansari kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) na ni kwa msingi huo ndio maana imeondokea kuwa mashuhuri kama hadithi ya Jabir. Katika hadithi ya Jabir kumetajwa Uimamu wa Maimamu 12 wa Mashia na hilo limebainishwa wazi na kwa majina yao. Mtume (s.a.w.w) wakati alipokuwa akitaja jina la Imam wa tano, aliashiria lakabu yake (Baqir) na akamtaka Jabir atakapokutana na Imam Baqir amfikishie salamu zake. [2] Katika hadithi hii pia kumeashiriwa ghaiba (kutoweka) ya Imam wa kumi na mbili wa Mashia na kuwa ndefu ghaiba yake na Imam wa zama amefananishwa na jua lililopo nyuma ya mawingu. [3]

Vyanzo vya hadithi

Hadithi hii imenukuliwa katika vyanzo vya Kishia kama Kifayat al-Athar, [4] Kamal al-Din, [5] na Bihar al-Anwar. [6] Aidha hadithi hii imenukuliwa katika vyanzo vya Kisuni kama Yanabiul Mawaddah, [7] na katika baadhi ya tafsiri za Kishia hadithi hii imetajwa na wafasiri wakati wa kufasiri Aya ya Ulul Amr au Aya ya Itwaa (kutii). [8]


Rejea

Vyanzo