Imamu Ridha (a.s) na urithi wa kiti cha uongozi
Urithi wa uongozi wa Imamu Ridha (as) (Kiarabu: ولاية العهد للإمام الرضا (ع)) unaashiria kuteuliwa Imamu Ridha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi wa Khalifa Maamun Abbasi, ambalo ni tukio muhimu sana katika maisha ya Imamu Ridha kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Kukubali Imamu Ridha cheo cha kuwa mrithi wa uongozi wa Maamum mbali na kuwa ni suala la changamoto katika historia ya Uislamu, lina umuhimu kwa upande wa teolojia. Kwa mujibu wa Seyyed Jafar Murtaza Amili, mwanahistoria wa Kishia, hadithi mutawatir zinaonyesha juu ya kutoridhia na kukubali Imamu Ridha cheo hicho kwa kulazimishwa. Kwa maana kwamba, hakuwa ameridhia lakini alilazimishwa kufanya hivyo.
Maamun alipendekeza ukhalifa kwa Imam kabla ya urithi wa ukhalifa, na wakasema kwamba lengo lake lilikuwa ni kuimarisha ukhalifa wake. Lakini pamoja na kukataa pendekezo la Maamun, Imam Ridha alihoji uhalali wa ukhalifa wa Maamun. Kwa kutoukubali ukhalifa, Maamun alimlazimisha kuukubali ukhalifa kwa kutishia kumuua Imamu Ridha (as). Kwa hiyo, ilimbidi Imamu alikubali pendekezo la Maamun; lakini aliweka sharti la kutoingilia masuala ya serikali. Hali hiyo ya kulazimishwa na kutenzwa nguvu iliendelea katika hatua zote nyingine alizofanya na mara zote alikuwa akisema, mimi nimetishiwa kuuawa ndio maana nimekubali kuwa mrithi wa kiti cha uongozi.
Aidha wakati alipopendekezewa jambo hilo alitoa masharti kwamba hayuko tayari kutoa amri kwa mtu yeyote yule, wala kuzuia kutendeka jambo lolote lile, wala asitoe fatwa na hukumu za kisheria kwa mtu yeyote yule na wala asimuuzulu wala kumteua mtu yeyote yule. Hivyo ni jambo lililo wazi kuwa, ukitoa anwani ya kulazimishwa kukubali jina la mrithi wa kiti cha uongozi, Imamu Ridha (as) hakushiriki kwa namna yoyote ile katika matendo yote ya utawala wa Khalifa Maamun.
Yote hayo yalionesha kuwa alitenzwa nguvu kukubali pendekezo hilo, kwani mtu asiye na nafasi katika jambo lolote lile, hawezi kuwa mfuasi wa utawala husika. Khalifa Maamun naye alitambua vyema jambo hilo na alifanya kila ujanja kuhakikisha kuwa Imam Ridha (as) anajihusisha na masuala ya utawala, lakini Imam alikataa. Baadhi ya malengo ya Maamun kwa kitendo hiki yametajwa kama ifuatavyo:
- Kusalimika na hatari ya Imamu.
- Kumuweka chini ya uangalizi wake.
- kunyamazisha mapinduzi ya Maalawi.
- Kumtumia Imamu kuhalalisha ukhalifa wake.
- Kuwaridhisha watu wa Khorasan.
Kwa upande mwingine, baadhi wanaamini kwamba Fadhl bin Sahl alitengeneza mpango wa urithi wa uongozi wa Imamu Ridha kwa ajili ya kufikia ufalme wa Iran. Hata hivyo, wanasema kwamba Imam (as) aliweza kuwazuia kufikia malengo yao kwa sera na shughuli zake.
Kwa amri ya Maamun, Imamu Ridha alihamishwa kutoka Madina hadi Khorasan mwishoni mwa mwaka wa 200 Hijiria. Maamun alichagua njia ya safari hiyo kwa namna ambayo asingepitia miji ya wakazi ambao ni Mashia. Imamu Ridha alisimulia na kubainisha hadithi ya Silsilat al-Dhahb akiwa njiani kuelekea Neishabur. Katika Ramadhani ya mwaka 201 Hijria, Ma'mun alifanya hafla ya kuteuliwa Imamu Ridha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi. Kwa muktadha huo, watu na maafisa wa serikali walitoa kiapo cha utii kwa Imam. Baada ya hapo, kwa mujibu wa amri ya Maamun, khutba zilisomwa kwa jina la Imamu na sarafu zilichongwa zikiwa na jina lake.
Kwa kutangazwa urithi wa kiti cha uongozi wa Imamu Ridha (as), watu kama Ali bin Abi Imran, Abu Yunus na mtawala wa Basra walipinga vikali jambo hilo. Watu wa Baghdad, ambao waliogopa kwamba ushawishi wao katika serikali ungepungua, waliasi na kula kiapo cha utii kwa Ibrahim bin Mahdi. Kwa mujibu wa vyanzo vya Shia, Imam Ridha (as) aliweza kutumia hali hiyo kwa maslahi ya Shia. Alieleza na kubainisha mafundisho mengi ya Ahlul-Bayt (as) kwa umma, na kufanaya mijadala na midahalo na viongozi wa madhehebu tofauti. Kulingana na baadhi ya watafiti, urithi wa kiti cha uongozi wa Imam Ridha (as) uliandaa uwanja na mazingira ya Wairan kuwa Mashia.
Umuhimu wa urithi wa kiti cha uongozi wa Imamu Ridha katika Uislamu
Suala la Imamu Ridha (as) kuwa Mrithi wa Kiti cha Uongozi ni mojawapo ya masuala yenye mjadala mkubwa katika historia ya Uislamu, [1] ambayo ni muhimu kisiasa na kiteolojia (kupingana kukubali urithi wa kiti cha uongozi na suala la Imamu kuwa Maasumu) [2] [3]. Kipindi cha Imamu Ridha cha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi wa Maamun kinahesabiwa kuwa kipindi muhimu zaidi cha maisha yake ya kisiasa. [4]
Kwa mujibu wa baadhi ya watafiti, katika kipindi nyeti cha cha ukhalifa wa Maamum, hatua ya Imam Ridha (as) ya kukubali cheo cha mrithi wa kiti cha utawala na wakati huo huo kufanya harakati katika kipindi hicho aliweza kuiongoza jamii kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kwani katika wakati huo, utawala wa ukoo wa Bani Abbas ulikuwa ukikabiliwa na hali isiyo thabiti na kulikuwa na uasi mwingi wa Maalawi sambamba na kuweko baadhi ya makundi potofu ambayo yalikuwa yameandaa mazingira na anga ya jamii kusambaratika. [5]
Pendekezo la cheo cha urithi wa kiti cha uongozi
Kwa mujibu wa Abul Faraj Esfahani katika Maqatil al-Talibiyyin na Sheikh Sadouq katika kitabu Uyun Akhbar al-Ridha (a.s.), urithi wa kiti cha uongozi wa Imamu Ridha ulifanyika na kutimia kwa takwa la Maamun; kwani yeye alikuwa amekula kiapo kwamba, endapo atamshinda nduguye yaani Amin ataukabidhi ukhalifa kwa Imamu Ridha. [6] Baada ya Amin kuuawa na utawala ukawa mikononi mwa Maamun, Sahl bin Fadhl waziri wa Maamun alimkumbusha ahadi aliyofunga na Mwenyezi Mungu na hivyo Maamun akachukua hatua za lazima, kwa ajili ya jambo hilo. [7]
Kwa upande mwingine, baadhi ya watu wanaamini kwamba pendekezo la urithi wa kiti cha uongozi kwa Imam Ridha lilitolewa na Fadhl bin Sahl. [8] Inasemekana kwamba, kwa hatua hii Fadhl alitaka kufikia ufalme wa Iran baada ya Imamu Ridha (as). [9] Kuteuliwa kwa Raja bin Abi al-Dhahhak ambaye ni katika jamaa wa Fadhl bin Sahl na kupewa jukumu la kumhamisha Imam Ridha kutoka Madina hadi Merv, onyo la baadhi ya wanasiasa kwa Maamun kuhusu mpango wa Sahl na ripoti nyingine za kihistoria zinazingatiwa kama uthibitisho wa dai hili. [10]
Malengo
Baadhi ya wataalamu wa mambo ya mashariki na baadhi ya waandishi wa Kishia kama vile Hassan Amin, mwandishi na mwanahistoria wa Lebanon, wanaamini kwamba Maamun alikuwa mwaminifu na alikuwa na nia njema katika kumtawaza Imamu na alifanya hivyo kwa imani na ikhlasi. [11] Hata hivyo kuna wahakiki wengi ambao wanaamini kwamba, hatua ya Maamun ya kumpatia Imamu Ridha (as) cheo cha mrithi wa kiti cha uongozi ilikuwa na malengo kadhaa na miongoni mwayo ni:
- Kusalimika na hatari ya Imamu na kumuweka chini ya uangalizi wake: Ma’amun ambaye alikuwa na wasiwasi na harakati za Imamu Ridha (as) mjini Madina, hatua yake ya kumleta Imamu Merv na kumpatia cheo cha mrithi wa kiti cha uongozi alitaka kwa kufanya hivyo asalimike na hatari ya Imamu kwa ajili ya utawala wake. [12]
- Kuzima na kunyamazisha mapinduzi ya Maalawi: Kupitia hatua ya kumfanya Imamu Ridha (as) kuwa mrithi wa kiti chake cha uongozi, Maamun alifanikiwa kunyamazisha mapinduzi ya Alawiyun; kwa namna ambayo baada ya Imamu kuchukua cheo cha mrithi wa kiti cha uongozi hakuna mapinduzi yoyote (isipokuwa harakati iliyoibuka huko Yemen na kuzimwa haraka) yaliyotokea ya Alawiyun yaliyotokea. [13]
- Kumuonyesha Imamu kuwa ni mtu mbaya mbele ya Mashia: Kwa mujibu wa riwaya iliyosimuliwa na Aba Salt (mmoja wa masahaba wa Imam Ridha as), Maamun kwa kumpatia Imamu cheo cha mrithi wa kiti cha uongozi alitaka kumdhihirisha Imam kama mtu anayependa dunia ili kwa njia hiyo apunguze hadhi na daraja yake miongoni mwa Mashia.[14]
- Kutumiwa Imamu Ridha kwa ajili ya kuhalalisha ukhalifa wa Maamun: Maamun, ambaye alijua kwamba akiwa mjini Madina Imam Ridha alikuwa akiwalingania watu kwake, kwa kumfanya Imamu kuwa mrithi wa kiti cha uongozi, alikuwa akitaka kutumia miito ya Imamu Ridha kama njia ya kuhalalisha ukhalifa wake, ili kwamba pamoja na uhalali wa Imam, ukhalifa wake mwenyewe pia upate uhalali. [15]
- Kuwaridhisha watu wa Khorasan: Watu wa Khorasani, ambao walikuwa wamekatishwa tamaa na ukandamizaji baada ya kuthibitishwa ukhalifa wa Bani Abbas, walikuwa wamemgeukia Imamu Ridha. [16] Kwa sababu hii, Maamun alijaribu kuwaridhisha kwa kumteua Imam Ridha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi. [17]
- Kuwatambua Mashia wakuu: Mashia ambao siku zote waliishi kwa siri, waliacha kuishi kwa siri wakati Imamu alipokuwa mrithi wa kiti cha uongozi na kwa sababu hiyo, walikuwa wakitambuliwa na serikali ya Bani Abbas. [18]
- Kuongezeka kwa nguvu za Maamun: Bani Abbas daima walikuwa wakimdunisha Maamun kwa sababu mama yake alikuwa kijakazi wa ikulu na alikabidhi kazi zote kwa Muirani (Fadhl bin Sahl). Kwa hiyo, aliamua kuimarisha nafasi yake kwa kumfanya mtu mkubwa kama Ali bin Musa Ridha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi. [19]
Baadhi ya waandishi pia wametaja malengo mengine ya hatua ya Maamun ya kumfanya Imamu Ridha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi. [20] Seyyed Ja'far Murtadha al-Amili mtafiti wa masuala ya historia wa Kishia, anaamini kwamba, kwa kuzingatia matatizo ambayo Maamun alikumbana nayo serikalini, kumchagua Imamu Ridha na kumfanya kuwa mrithi wa kiti cha uongozi ni jambo linaloonyesha uhodari na kukomaa kwake kisiasa na kufahamu kwake matatizo ya Serikali. [21] Hata hivyo, wanasema kwamba, utendaji wa Imamu Ridha (as) pamoja na misimamo yake vilimkwamisha Maamun na kumfanya ashindwe kufikia malengo yake. [22]
Kwa mujibu wa baadhi ya wataalamu wa historia ya Kiislamu ni kuwa, malengo ya utawala wa Maamun ya kumfanya Imamu Ridha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi yalikuwa ni:
- Kubadilisha uwanja wa mapambano makali ya mapinduzi ya Shia kuwa medani ya harakati tulivu za kisiasa na zisizokuwa na hatari.
- Kubatilisha madai ya Mashia kwamba, Makhalifa wa Bani Umayya na Bani Abbas walipora uongozi na ukhalifa na hivyo kuzihalalisha tawala za koo hizo.
- Kumdhibiti Imamu Ridha (as) (ambaye daima alikuwa kitovu cha upinzani na mapambano) na kuwadhibiti pia viongozi na wapiganaji wote wa Maalawi.
- Kumuweka Imamu (ambaye alikuwa ni kiini na mtu anayetokana na watu na elekeo na kimbilio la matumaini na marejeo ya maswali na malalamiko) katika mzingiro wa makachero wa serikali na kufifiza taratibu rangi yake ya kuwa kwake mtu wa watu na kuleta pengo baina yake na watu na kisha baina yake na huba na mapenzi ya watu.
- Kuchuma haiba na hadhi ya kimaanawii kwa uhalalishaji huu kwamba, katika ulimwengu wa zama zile, kila mtu anapaswa kumsifu Maamun kwa kuchagua mtoto wa kizazi cha Nabii na shakhsia takatifu na ya kiroho na kumfanya kuwa mrithi wa utawala wake na kuwanyima ndugu na watoto wake upendeleo huu.
- Kufanya juhudi za kumbadilisha Imamu na kumfanya kuwa mhalalishaji wa vyombo vya ukhalifa na hapana shaka kuwa, kama Imamu na nafasi yake isiyo na mithili angehalalisha vitendo na matukio katika utawala ule, hakuna sauti ya upinzani ambayo ingeweza kudhuru na kutia dosari hadhi na heshima ya mfumo huo. [23]
Utendaji wa Imamu Ridha (as)
Kwa mujibu wa Seyyed Jafar Murtadha al-Amili mwanahistoria wa Kishia, hadithi mutawatir zinaonyesha juu ya kukubali Imamu Ridha cheo hicho kwa kulazimishwa. [24] Kwa maana kwamba, hakuwa ameridhia lakini alilazimishwa kufanya hivyo. Kwa mujibu wa kile kilichokuja katika kitabu cha Manaqib ni kuwa, Imamu Ridha alitoa habari juu ya kutokuwa na natija cheo chake cha mrithi wa kiti cha uongozi.[25]
Kwa mujibu wa ripoti hizi, baada ya kukubalii kuchukua cheo cha mrithi wa kiti cha uongozi, akiwa mbele ya Maamun na Fadhl bin Sahl aliandika waraka wa urithi wa kiti cha uongozi na miongoni mwa mambo aliiyoyabainisha katika waraka huo ni kwamba, vitabu vya Jafr na Jam'i vina ashirio lililo kinyume na urithi wa kiti chake cha uongozi. [26] Maamun alipendekeza ukhalifa kwa Imam kabla ya urithi wa kiti cha uongozi; lakini Imamu Ridha alikataa na kusema: Kama Mwenyezi Munjgu amekupatia Ukhalifa basi sio sahihi na haifai umpatie mtu mwingine; na kama hujapatiwa ukhalifa, basi vipi unatoa kitu ambacho sio chako na kumpatia mtu mwingine?" [27]
Wahakiki wanaamini kwamba, jibu la Imamu kimsingi lilitilia alama ya swali uhalali wa ukhalifa wa Maamun. [28] Sayyid Ja'far Murtadha anaamini kwamba, Maamun hakuwa na nia ya dhati katika kupendekeza ukhalifa kwa Imam Ridha (a.s.) na kwamba pendekezo lake lilikuwa ni jaribio la kuimarisha ukhalifa wake [29] Fadhl bin Sahl pia alionyesha kushangazwa pia na hatua ya Maamun ya kujitwalia ukhalifa na Imamu kutoukubali kwamba, ni gani jinsi ukhalifa ulikuwa umeharibika.[30]
Pendekezo la Maamun kwa Imamu Ridha la kuchukua cheo cha urithi wa kiti cha uongozi lilipingwa vikali na Imamu Ridha. [31] Alipoona msimamo huo wa Imamu, Maamun aliwakumbushia tishio la Omar bin al-Khattab kwa wajumbe sita wa baraza lililoteuliwa kumchagua khalifa baada yake ambapo alisema, atamuua mpingaji. Hivyo akamtishia Imamu na kumlazimisha kukubali cheo cha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi. [32] Kwa sababu hii, Imamu Ridha hakuwa na budi isipokuwa kukubali cheo hicho; lakini alitoa sharti la kutoingilia mambo ya serikali. [33] M aamun pia alikubali sharti hili.[34]
Kwa mujibu wa riwaya kutoka kwa Rayyan bin Salt aliyoipokea kutoka kwa Imamu Ridha ni kwamba, kama Imamu asingekubali kuwa mrithi wa kiti cha uongozi angeliuawa na Ma'mun. [35] Imamu Ridha (as) alikabiliana na Maamun katika hali mbalimbali ili kukwamisha mpango wa Maamun wa urithi wa kiti cha uongozi wake. [36] Miongoni mwa hatua za Imamu tunaweza kutaja zifuatazo: Amri ya Imamu kwa familia yake ya kulia wakati alipoaga Madina, [37] kuaga kaburi la Mtume, [38] kutoingilia kazi yoyote ya serikali, kugeuza kituo cha serikali kuwa kituo cha kueneza na kufanya tablighi ya Ushia, na kujadiliana na viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali. [39]
Safari ya Imamu kutoka Madina kwenda Merv
Kwa mujibu wa ripoti ya historia ya Ya’qubi, Raja bin Abi Dhahhak (jamaa wa Fadhl bin Sahl) alipewa amri na Maamun ya kumleta Imam Ridha (a.s.) kutoka Madina hadi Khorasan. [40] Hata hivyo, kwa mujibu wa Sheikh Mufid, mjumbe wa Maamun alikuwa Isa Jaloudi. [41] Maamun alichagua njia maalumu za kupita kwa ajili ya safari ya Imamu Ridha kwenda Merv ili asipite katika vituo vya Mashia; kwa sababu aliogopa mkusanyiko wa Mashia kwa ajili ya Imamu. [42] Alitoa amri maalumu ya kutompitishia Imamu Ridha njia ya Kufa; bali Imamu aletwe Khorasan kupitia njia ya Basra, Khuzestan na Fars. [43] Imekuja katika kitabu cha Shia Atlas: Njia ilikuwa kama ifuatavyo: Madina, Naqra, Hawsijah, Nabaj, Hufr Abu Musa, Basra, Ahvaz, Behbahan, Istakhr, Abarkuh, Dehshir (Farashah), Yazd, Kharanaq, Rubat Pusht-i Bam, Nayshabur, Qadamgah, Deh Sorkh, Tous, Sarakhs na Merv. Inasemekana kwamba tukio muhimu na lililothibitishwa vyema njiani lilitokea Neishabur, ambapo Imam Ridha (a.s.) alitoa hadithi inayojulikana kwa jina la Silsilat Dhahab. [46]
Hafla ya urithi wa kiti cha uongozi
Siku ya Jumatatu, mwezi saba Ramadhani [47] au tano [48] au ya Ramadhani ya pili [49] ya mwaka wa 201 A.H, Maamun aliwataka watu badala ya kuvaa nguo nyeusi ambayo ni ishara ya Bani Abbas [50] aliwavisha nguo za rangi ya kijani (rangi ya kijani ni nembo ya masharifu wa Kialawi [51] na waje kutoa kiapo cha utii kwa Imamu Ridha na alindika amri ya hilo na kutuma katika maeneo mbalimbali [52].
Baada ya hapo khutba katika mimbari zilitolewa kwa jina la Imamu na dinari na dirhamu zikatengenezwa kwa jina lake. [53] Maamun alimwoza binti yake Ummu Habib kwa Imam Reza. [54] Pia, kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, Maamun alipewa lakabu ya Ridha (Al-Ridha min aal-Muhammad) yaani alimpa mtu ambaye ameridhiwa kutoka katika familia ya Muhammad. [55] Hata hivyo kwa mujibu wa riwaya nyingine kutoka kwa Imamu Jawad (as), baba yake alipewa lakabu ya “Ridha” na Mwenyezi Mungu.[56]
Maamun aliwakusanya maafisa wa serikali, makamanda wa jeshi, mahakimu na watu katika hafla na sherehe ya ili watoe baia na kiapo cha utii kwa Imam Ridha. [57] Imamu aliweka mikono yake mbele ya uso wake kwa namna ya kula kiapo cha utii kwa Mtume, kwa namna ambayo aliweka migongo ya mikono yake juu ya uso wake na viganja vya mikono yake kuwaelekea watu. [58] Wazungumzaji na washairi walitoa hotuba na kusoma mashairi kwa ajili ya sherehe hiyo. Mmoja wa washairi hao alikuwa ni Di’bil al-Khuza’i, ambaye alipata zawadi kutoka kwa Imam kwa kusoma shairi lake.[59]
Maamun alimwomba Imamu awatolee khutba watu. Imam pia alitoa khutba fupi sana kwa watu. [60] Amri na hukumu ya urithi wa kiti cha uongozi iliandikwa kwa hati ya Maamun, na Imam pia aliandika baadhi ya mambo nyuma ya hati hiyo. [61] Ali bin Isa Irbili, mwandishi wa kitabu Kashfu al-Ghumma anasema kuwa, mwaka 670 Hijria aliona hati hiyo katika mwandiko wa Maamun na Imamu na akasajili hilo katika kitabu chake cha Kashf al-Ghumma. [62]
Wapinzani wa urithi wa kiti cha uongozi wa Imamu Ridha (as)
Kwa mujibu wa riwaya ya Ya’qubi ni kuwa, Ismail bin Jafar bin Sulaiman, ambaye alifanywa kuwa mtawala wa Basra na Maamun, alikataa kutoa kiapo cha utii kwa Imam Ridha (a.s.) na Maamun akamtuma kwake Isa bin Yazid Jaludi naye akakimbia kutoka Basra. [63] Ya’qubi ameandika kwamba, Isa bin Yazid Jaludi alipewa kazi na Maamun kufikisha amri ya kutoa kiapo cha utii huko Makka. [64] Aliingia Makka akiwa na vitambaa vya kijani na akachukua baia na kiapo cha utii kutoka kwa watu kwa ajili ya Imamu Ridha (as). [65] Sheikh Sadouq ameripoti kwamba, Issa Jaludi baadaye alikuja kuwa miongoni mwa wapinzani wakubwa wa urithi wa kiti cha uongozi wa Imamru Ridha (as) na aliadhibiwa kwa kutofanya hivyo ambapo Maamun alimtia gerezani. [66] Ali bin Abi Imran na Abu Yunus wametajwa kuwa wapinzani wengine wa cheo cha urithi wa kiti cha uongozi alichopewa Imamu Ridha (as) na Maamun. [67]
Matukio
Baadhi ya matukio ya urithi wa kiti cha uongozi wa Imamu Ridha (as) yamebainishwa kuwa ni:
- Uasi wa watu wa Baghdad: Watu wa Baghdad, ambao waliogopa kwamba ushawishi wao katika serikali utadhoofika, hawakukubali hatua ya Maamun ya kumfanya Imamu Ridha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi, na wakamtimua kutoka Baghdad mtawala aliyekuwa amewekwa na Maamun na kisha wakampa kiapo cha utii Ibrahim bin Mahdi. [68]
- Baia na kiapo cha utii cha baadhi ya Maalawi kwa Maamun: Ingawa urithi wa kiti cha uongozi wa Imamu Ridha haukuwakurubisha Mashia wote na Maamun, lakini baadhi ya Mashia waliridhika na Maamun na wakatoa kiapo cha utii kwake. [69]
- Kunufaika Imamu Ridha na cheo cha urithi wa kiti cha uongozi: Ijapokuwa Imamu Ridha alikubali cheo hicho bila kupenda, lakini aliweza kutumia nafasi hii kueleza hadharani mafundisho mengi ambayo yalikuwa yakiambiwa tu maswahaba zake na Mashia. Aliyasema hayo hadharani na kwa uwazi na kuyabainisha kwa wote na kufanya mjadala na wanazuoni wa madhehebu mbalimbali. [70]
- Kuandaa uwanja wa Ushia nchini Iran: Kwa mujibu wa Seyyed Ali Akbar Qurashi, mwandishi wa Tafsir Ahsan al-Hadith, urithi wa kiti cha uongozi wa Imam Ridha ulifungua njia kwa Wairani kuwa Mashia; kwa sababu kuweko Iran Imamu Ridha, kuliwafanya masharifu wa Kialawi kuja Iran na kueneza mafundisho ya madhehebu ya Ushia. [71]
Monografia
Kumeandikwa vitabu vingi vya kujitegenea kuhusiana na maudhui ya urithi wa kiti cha uongozi wa Imamu Ridha (as). Baadhi ya athari hizo ni:
- Imam Reza (as), Maamun va mauzu velayati ahadi; mwandishi Sayyid Ghani Iftikhari. Kitabu hiki mbali na kubainisha hali ya kisiasa katika kipindi cha Imamu Ridha kuwa mrithi wa kiti cha uongozi, kinaelezea hali ya kisiasa na kijamii ya kipindi cha utawala wa Bani Abbas (kabla ya Maamun). [72]. Kitabu hiki kina kurasa 152. [73].
- Velayat Ahadi Emam Reza (as), mwandishi Muhammad Murtadha: Katika kitabu hiki mwandishi anabainisha malengo ya siri ya Maaamun kwa urithi wa kiti cha uongozi wa Imamu Ridha (as) na radiamali ya Imamu katika kukabiliana na tukio hili akitumia nyaraka za kihistoria. [74] Kitabu hiki kina kurasa 127 na chapa ya pili ilichapishwa mwaka 1386 Hijria Shamsia. [75]
- Negah be zendegi va velayat ahadi Emam Reza, mwandishi Muhammad Amini. Kitabu hiki kina kurasa 130 katika milango mitatu. [76] Kitabu hiki kilichapishwa kwa mara ya kwanza mwaka [77].