Nenda kwa yaliyomo

Mkopo:Nahju al-Balaghah

Kutoka wikishia
Nahj al-Balagha
Taarifa za kitabu
Tarehe ya kuandikwa400 H (Hijria)
MadaMkusanyiko wa misemo na maandishi ya Imamu Ali (a.s)
MtindoHadithi
LughaKiarabu
Kwa juhudi zaSayyid Radhi
Iliyohakikiwa naWatu mbalimbali
Idadi ya juzuu1


Nahju al-Balagha ni kitabu kinachojumuisha hotuba, barua, na semi fupi za Imamu Ali (a.s) ambazo Sayyid Radhi alizikusanya na kuzipanga kupitia juhudi zake binafsi. Wataalamu na watafiti wanakichukulia kitabu hichi kama ensaiklopidia ya utamaduni wa Kiislamu na moja kati ya vyanzo muhimu zaidi kwa ajili ya kuuelewa Uislamu pamoja na maadili ya kidini. Kitabu cha Nahju al-Balagha kina sifa ya kuwa na kiwango kikubwa cha ufasaha na uandishi makini. Jambo hili linasimama kama siri kuu ya mvuto na kudumu kwa maandiko haya katika historia yote.

Ujumuishi wa mada mbalimbali na upana wa maudhui za kitabu hichi vinasimama kama moja ya sifa na fadhila kubwa za Nahju al-Balagha. Maudhui ya kitabu hichi yanafuata mlolongo maalumu katika sehemu tatu kuu ambazo ni hotuba, barua, na semi fupi za hekima. Katika sehemu ya hotuba na semi fupi, unakutana na mada mbalimbali kama uelewa wa kumjua Mwenyezi Mungu, masuala ya kimaadili, kuuelewa ulimwengu, asili ya uumbaji, maumbile ya mwanadamu, pamoja na mifumo ya umma na serikali zilizofanya uadilifu au dhuluma mbalimbali. Kwa upande mwingine, sehemu ya barua za kitabu hichi imejikita zaidi katika uchambuzi wa masuala ya uongozi wa serikali, utawala bora, pamoja na namna ya viongozi na maafisa wa serikali wanavyopaswa kutangamana na kuamiliana na wananchi wao.

Wataalamu wa lugha wamekitafsiri kitabu cha Nahju al-Balagha katika lugha mbalimbali duniani zikiwemo lugha ya Kifarsi, Kiingereza, Kifaransa, Kihindi, Kiitaliano, Kituruki cha Istanbul, Kitajiki, na Kiurdu. Wasomi na wanazuoni wamekiandikia kitabu hichi vitabu kadhaa vya sherehe (tafsiri chambuzi). Miongoni mwazo ni kitabu Sharhu Nahju al-Balagha kilichotungwa na Ibnu Abi al Hadid pamoja na Sharhu Nahju al-Balagha kilichoandikwa na Ibnu Maitham al Bahrani. Vitabu viwili hivi vinasimama kama sherehe muhimu zaidi za lugha ya Kiarabu kuhusiana na kitabu cha Nahju al-Balagha.

Baadhi ya watafiti wamefanya juhudi kubwa za kukusanya semi na maneno mengine ya Imamu Ali (a.s) kutoka katika vitabu vyengine mbalimbali vya kihistoria ambayo Sayyid Radhi hakuyajumuisha katika matini asili ya Nahju al-Balagha. Wasomi hao wamechapisha maneno na semi hizo chini ya anwani ya Mustadraku Nahju al-Balagha. Miongoni mwa jitihada hizo za kitaaluma ni kitabu maarufu kiitwacho Nahju al-Saadah fi Mustadrak Nahju al-Balagha kilichotungwa na mwanachuoni maarufu aitwaye Muhammad Baqir al-Mahmoudi.

Miongoni mwa vyanzo vikuu alivyovitumia Sayyid Radhi katika kukusanya na kuandaa kitabu cha Nahju al-Balagha, ni vitabu vilivyoandikwa na wanazuoni wa Ahlu Sunna. Baadhi ya vyanzo hivyo ni kitabu cha Al-Bayan wa al-Tabyin kilichoandikwa na Al-Jahidh, kitabu cha Al-Maghazi kilichotungwa na Sa'id bin Yahya al-Umawi, kitabu cha Al-Jamal kilichoandikwa na Al-Waqidi, pamoja na Tarikh al-Tabari. Baadhi ya watafiti wanaamini kuwa hatua ya Sayyid Radhi ya kutosheka na vyanzo vya Ahlu Sunna, pamoja na kutoashiria isnadi za maneno ya Imamu Ali (a.s) ndani ya kitabu cha Nahju al-Balagha, kulileta ukosoaji na mapungufu kadhaa ya kitaalamu. Sababu hiyo ndiyo iliyowafanya wanachuoni na watafiti wengi kuchukua juhudi kubwa za kukusanya isnadi za Hadithi za kitabu hichi kutoka katika vyanzo vya kale vya kihistoria ya kuziweka katika mfumo wa nyaraka za isnadi, ili iwe ni thibitisho la kuthibitisha usahihi na ukweli wa maandiko yake.

Baadhi ya wanazuoni wa Kisunni wanatilia shaka utambulisho wa mkusanyaji wa athari hii, pamoja na kutilia shaka usahihi wa kunasibishwa kwa mapokezi ya kitabu hicho na Imamu Ali (a.s). Watafiti wanaounga mkono usahihi wa mapokezi hayo, wamebainisha wakisema kuwa, shaka hiyo inayohusiana na utambulisho wa mkusanyaji inadhihirisha ukosefu wa mapitio ya matini asili ya kitabu chenyewe, kwa sababu jina la mkusanyaji ambalo ni Sayyid Radhi linaonekana mara nyingi ndani ya matini ya kitabu hicho. Hali kadhalika, Ibnu Abi al-Hadid ambaye ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Ahlu Sunna, anaeleza kuwa kutilia shaka juu ya kunasibishwa kwa maudhui za Nahju al-Balagha na Imamu Ali (a.s) ni matokeo ya kufuata matamanio ya nafsi pamoja na ushabiki na taasubi pofu.

Umuhimu wa Nahju al-Balagha

(بئس الزاد إلی المعاد العدوان علی العباد) Tafsiri: Akiba mbaya zaidi kwa ajili ya Akhera ni kuwafanyia dhuluma waja wa Mwenyezi Mungu.

 Nahju al-Balagha, uhakiki wa Subhi Salih, 1414 H, Hikma ya 221, uk. 507.

Nahju al-Balagha ni kitabu kinachojumuisha hotuba, barua, na semi fupi zilizotokana na Imamu Ali (a.s) katika zama za ukhalifa wake.[1] Watafiti wanakitambua kitabu hichi kama ensaiklopidia ya utamaduni wa Kiislamu, na wanakitaja kuwa ni chanzo muhimu zaidi kwa ajili ya kuuelewa Uislamu na maadili ya kidini, kinachoshika nafasi ya tatu baada ya Qur'ani Tukufu na Hadithi.[2] Hali kadhalika, wanazuoni wamekieleza kitabu cha Nahju al-Balagha kuwa ni miongoni mwa vitabu vinavyopewa kipaumbele kikubwa cha kukihifadhi baada ya Qur'ani Tukufu, mtazamo ambao unapatikana ndani ya madhehebu ya Kishia bila ya kushirikiana na madhehebu mengine katika fikra hiyo.[3] Reza Ostadi amerekodi majina ya vitabu 370 katika tasnifu yake iitwayo Kitabnameye Nahju al-Balagha, vilivyoandikwa kuhusiana na Nahju al-Balagha hadi kufikia mwaka 1980 M.[4]

Sayyid Muhsin al-Amin katika kitabu cha A'yan al-Shiah, amekitambulisha kitabu cha Nahju al-Balagha kama moja ya fahari kubwa zaidi za ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.[5] Tafiti za kihistoria zinaonesha kuwa kitabu hichi kinashika nafasi ya pili baada ya Qur'ani Tukufu kwa kuwa na idadi kubwa ya nakala za maandishi ya mkono, sherehe, na tafsiri ndani ya utamaduni mzima wa Kiislamu. Fasihi nyingi za lugha ya Kifarsi na Kiarabu, zinaonesha kuwa Nahju al-Balagha inachukuwa nafasi ya pili baada ya Qur'ani Tukufu katika kuziathiri lugha mbili hizo.[6] Hali kadhalika, Muhaddith al- Nuri katika kitabu cha Mustadrak al-Wasa'il anasema kuwa, idadi kubwa ya wanazuoni wa zama za kale walikuwa wakikitaja kitabu hichi kwa jina la Akhu al-Qur’an (Kaka wa Qur'ani) pale walipotaka kuwakabidhi wanafunzi wao idhini (ijaza) rasmi ya kupokea na kunakili Nahju al-Balagha.[7]

Mkusanyaji

Makala asili: Sayyid Radhi

Mnamo mwaka wa 400 Hijria (sawa na mwaka 1010 M.), Sayyid Radhi alikusanya na kukipanga kitabu cha Nahju al-Balagha katika mfumo wa kitabu kamili.[8] Mwanazuoni huyu anatokana na ukoo wa Aalu Abi Talib.[9] Naye alikuwa ni mfasiri mzuri wa Qur'ani Tukufu na gwiji wa fasihi ya Kiarabu katika madhehebu ya Kishia, na alikuwa ni mwanatheolojia shupavu katika ulimwengu wa Kiislamu.[10]

Uteuzi wa Jina

Sayyid Radhi amebainisha akisema kuwa, nia kuu ya kukusanya kitabu cha Nahju al-Balagha ilikuwa ni kuitikia wito wa maombi ya marafiki zake waliomwomba akusanye semi zenye ufasaha mkubwa zaidi kutoka kwa Imamu Ali (a.s).[11] Mwandishi huyu alidhibiti na kukusanya sehemu maalumu tu ya semi zilizofikia kiwango cha juu zaidi cha ufasaha na balagha.[12] Hiyo ndiyo sababu iliyomfanya kukiita kitabu hichi Nahju al-Balagha, jina lenye maana ya Njia ya Balagha[13] ambayo Muhammad Abdu, aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Ahlu Sunna, alilieleza kama sifa sahihi zaidi kwa ajili kitabu hichi.[14]

Thamani ya Kifasihi

Ufasaha wa balagha ya Nahju al-Balagha unazingatiwa kama sababu kuu zinazokipa kitabu hichi mvuto mkubwa na sifa ya kudumu katika uwanja wa historia.[15] Wanazuoni wameziweka semi za Nahju al-Balagha katika daraja iliyo chini ya maneno ya Muumba, huku ikiwa juu ya maneno ya viumbe.[16] Wataalamu wa lugha ya Kiarabu wanatoa maelezo yanayothibitisha thamani kubwa ya kifasihi ya kitabu hichi. Miongoni mwa maelezo ya waalamu hao ni kama ifuatavyo:[17]

Kwanza, Ibnu Abi al-Hadid, mwanazuoni wa Ahlu Sunna na mshereheshaji wa karne ya saba, yeye anaona mstari mmoja tu wa kitabu hichi kuwa ni bora kuliko mistari 1,000 ya semi za Ibnu Nabatah.[18]

Pili, George Jordac, mwandishi wa Kikristo, yeye anaamini kuwa kitabu cha Nahju al-Balagha kinashika nafasi ya juu kabisa ya ufasaha baada ya Qur'ani Tukufu.[19]

Tatu, Sheikh Nasif al-Yaziji, mwanafasihi na mshairi wa Lebanon, yeye anaamini kuwa uhifadhi wa Qur'ani Tukufu na Nahju al-Balagha ndiyo nguzo kuu za kuwa nguli katika ufasaha na balagha ya lugha ya Kiarabu.[20]

Nne, Muhyi al-Din Abdul Hamid, mtaalamu wa lugha ya Kiarabu, huyu yeye amekitaja kitabu hichi kama chemchemi inayobubujika balagha na ufasaha, huku akiamini kuwa, maneno ya Nahju al-Balagha ndiyo maneno fasaha zaidi baada ya maneno ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w).[21]

Baadhi ya washereheshaji vya kitabu hichi wanamchukulia Imamu Ali (a.s) kuwa ndiye mwasisi wa fani ya utungaji wa tamthiliya yenye mafunzo.[22] Wataalamu hawa wanaamini kuwa Imamu Ali (a.s) ametumia fani hii chini ya hekima namba 289 ya Nahju al-Balagha akielezea wasifu wa mtu mwema ambaye kiuhalisia hayupo, akitengeneza mhusika wa kufikirika (kidhahania) kwa ajili ya kutoa kigezo bora kwa jamii mbalimbali.[23]

Mvuto kwa Wasio Waislamu

Kitabu cha Nahju al-Balagha kina mvuto mkubwa si tu kwa Mashia, bali hata kwa wasio Mashia and wasio Waislamu, hii ni kutokana na kiwango chake kikubwa vya ufasaha wa maneno yake.[24] George Sam'ani Jordac alitunga kitabu maalumu kiitwacho Rawa'iu Nahju al-Balagha, kwa ajili ya kutoa uchambuzi wa kifasihi na kuchunguza hekima zilizomo ndani ya Nahju al-Balagha.[25] Hali kadhalika, kuna idadi kadhaa ya wasio Waislamu waliosilimu baada ya kukisoma kitabu hichi.[26] Mwanafalsafa wa Kimarekani Muhammad Legenhausen alisilimu na kufuata madhehebu ya Kishia mara tu baada ya kusoma na kutafakari matini za kitabu cha Nahju al-Balagha.[27]

Maudhui ya Nahju al-Balagha

Muhammad Abduh, mmoja wa wanazuoni magwiji Ahlu Sunna akitoa wasifu wa kitabu hiki anasema: Unaposoma kurasa la kitabu hiki, nyakati fulani unajikuta ukipaa katika kipeo cha juu cha lulu za maana na misamiati teule aliyoisuka kwa ufasaha wa juu kabisa, huku nyakati nyingine ukijiona katikati ya vumbi na dhoruba za uwanja wa vita. Na mara nyengine unashuhudia akili iliyotukuka inayodhihiri kupitia nuru maneno, ikifanya kila juhudi kukuokoa wewe kutoka kwenye kiza nene ili ikupandishe hadi kileleni mbingu na kukupa maskani salama katika ulimwengu mtakatifu. Aidha wakati mwingine unajiona upo bega kwa bega na viongozi wa dola, ambapo Imamu Ali anawaongoza na kuwatadibisha katika sanaa ya siasa, busara ya uongozi, na njia za hekima.

 Abduh, Sharh Nahju al-Balagha, uk. 10.

Nakala ya hati ya mkono ya Sherehe (tafsiri chambuzi) ya Nahju al-Balagha ya Ibn Abi al-Hadid, iliyoandikwa katika karne ya 7 Hijria. Hati hii ya kale imehifadhiwa katika Makumbusho ya Malik mjini Tehran.[28]

Nasir Makarim Shirazi anaona kuwa ujumuishi wa mada mbalimbali pamoja na upana wa maudhui za kitabu hichi ni sifa ya kipekee kabisa kuhusiana na Nahju al-Balagha. Mwanazuoni huyu akikisifu kitabu hichi anasema kuwa, kimesheheni hotuba tamu na zenye maana ya kina juu ya mada tofauti, na wakati mwingine zenye sura ya kupingana zenyewe kwa zenyewe.[29] Ibnu Abi al-Hadid anaeleza kuwa, wakati mwingine Imamu Ali (a.s) anazungumza kama mpiganaji shupavu, na anadhihiri kama Bastam bin Qais na Utba bin Harith (wapambanaji wawili mashuhuri wa Kiarabu), na wakati mwingine kama mtawa anayetoa mawaidha na nasaha mbalimbali kwa umma wake kama alivyo Isa bin Mariam (a.s).[30] Abbas Mahmoud al-Aqqad amekitaja kitabu hichi kama chemchemi inayobubujika hekima za Kiungu.[31]

Wasomi wanaeleza kuwa, uchambuzi na usomaji wa kitabu hichi unamfanya msomaji kuwa na uelewa mpana juu ya mtazamo wa Imamu Ali (a.s) kuhusiana na Mwenyezi Mungu, mwanadamu, ulimwengu, asili ya uumbaji, na Siku ya Kiyama.[32] Kitabu hichi kinabainisha wazi sifa za kimaadili zinazohitajika katika kujenga shakhsia ya Insanu Kamil (mwanadamu aliyekamilika).[33] Pia kinatou maelezo ya kutosha kuhusiana na utume wa manabii, Uimamu, uongozi na utawala wa serikali, haki za mtu binafsi na jamii, asili ya maumbile, tabia za wanafiki na makafiri, pamoja na kutambulisha makundi katika uwanja wa kihistoria kama vile; Nakithina, Mariqina, na Qasitina.[34] Abdullah Jawadi Amuli anaamini kuwa, Sayyid Radhi aliteua maudhui za Nahju al-Balagha kwa ustadi mkubwa ili kuzuia mifarakano kati ya Shia na Sunni, jambo lililosaidia kuandikwa sherehe makini na madhubuti kupitia wanazuoni wa madhehebu ya Ahlu Sunna.[35]

Muundo wa Maudhui

Maudhui za kitabu cha Nahju al-Balagha zimepangwa kwa mlolongo maalumu katika sehemu tatu kuu ambazo ni hotuba, barua, na semi za hekima.

Hotuba

وَ إِنَّمَا يَنْبَغِي لِأَهْلِ الْعِصْمَةِ وَ الْمَصْنُوعِ إِلَيْهِمْ فِي السَّلَامَةِ أَنْ يَرْحَمُوا أَهْلَ الذُّنُوبِ وَ الْمَعْصِيَةِ وَ يَكُونَ الشُّكْرُ هُوَ الْغَالِبَ عَلَيْهِمْ وَ الْحَاجِزَ لَهُمْ عَنْهُم‏) Tafsiri: Inawapasa wale wasio na dhambi na waliosalimika katika dini yao, kuwahurumia wenye dhambi na waasi, na kushukuru kwa neema hii, na shukrani hizo ziwashughulishe kwa kiwango ambacho zigeuke kuwa ni ngao ya kuwazuia wasitaje aibu za watu.

 Nahju al-Balagha, uhakiki wa Subhi Salih, 1414 H, Hotuba ya 140, uk. 197.

Sehemu ya kwanza inajumuisha hotuba teule za Imamu Ali (a.s) yenye jumla ya hotuba 241.[36] Sayyid Ja'afar Shahidi anaichukulia sehemu hii kama ensaiklopidia ya utamaduni wa Kiislamu iliyosheheni mada mbalimbali, kama vile uelewa wa kumjua Mwenyezi Mungu, kuuelewa ulimwengu, asili ya uumbaji, maumbile ya mwanadamu, na mifumo ya serikali.[37] Mwanazuoni huyu anaamini kuwa, lengo la Imamu Ali (a.s) katika kubainisha masuala haya lilikuwa ni kutoa elimu ya kumjua Mwenyezi Mungu.[38] Sayyid Radhi aliteua hotuba nne miongoni mwa hotuba zote na kuzipa majina maalumu, ambayo ni Shiqshiqiyyah, Gharraa, Ash-bahu, na Qasi'ah.[39]

Hotuba ya Shiqshiqiyyah

Hotuba ya Shiqshiqiyyah ni miongoni mwa hotuba zinazoibua udadisi mwingi ndani ya kitabu cha Nahju al-Balagha.[40] Imamu Ali (a.s) amebainisha masuala yote yanayofungamana na ukhalifa na Uimamu ndani ya hotuba hii, huku akikosoa vikali utendaji kazi wa Makhalifa waliomtangulia, huku akiweka wazi makosa ya utawala wao, pamoja na kuonesha uharamu wa utawala wao.[41] Hali kadhalika, anaelezea lile tukio la kufurika kwa watu waliomiminika kwa ajili ya kula kiapo cha utiifu kwake, pamoja na kubainisha sababu zilizomfanya akubali kubeba majukumu ya uongozi wa serikali baada ya Othman bin Affan.[42]

Hotuba ya Gharra

Imamu Ali (a.s) amehimiza mno suala la ucha Mungu ndani ya Hotuba ya Gharra, huku akikumbusha neema za Mwenyezi Mungu, uhalisia wa dunia kama mahali pa mitihani, matukio ya Siku ya Kiyama, pamoja na mauti.[43] Sayyid Radhi anaeleza kuwa hotuba hii ilitetemesha miili ya wasikilizaji wake na kuwafnaya watokwe na machozi mara tu baada ya kuisikia maneno mazito ya hotuba hiyo.[44] Hotuba hii ilipewa jina la Gharra kutokana na kusheheni kwake fani za lugha na miondoko mizito ya kifasihi kama vile jinasi (mfanano wa lafudhi) na saj'i (vibwagizo).[45]

Hotuba ya Muttaqina

Hotuba ya Muttaqina (Wacha Mungu) ni miongoni mwa hotuba za kiroho na kimalezi zenye uzito mkubwa ndani ya kitabu hichi.[46] Imamu Ali (a.s) alitoa hotuba hii kwa ajili ya kuelezea sifa za wacha Mungu, kufuatia maombi ya mmoja wa wafuasi wake aitwaye Hammam.[47] Kiongozi huyu amezichambua kwa kina sifa mia moja za wacha Mungu na wenye kujiepusha na maovu katika hotuba yake.[48] Hammam al zidiwa na hisia za kiroho jambo lililopelekea kufariki dunia kutokana na mguso mzito wa mawaidha ya hotuba hii.[49]

Barua

Imamu Ali (a.s):

وَ إِنَّمَا يَنْبَغِي لِأَهْلِ الْعِصْمَةِ وَ الْمَصْنُوعِ إِلَيْهِمْ فِي السَّلَامَةِ أَنْ يَرْحَمُوا أَهْلَ الذُّنُوبِ وَ الْمَعْصِيَةِ وَ يَكُونَ الشُّكْرُ هُوَ الْغَالِبَ عَلَيْهِمْ وَ الْحَاجِزَ لَهُمْ عَنْهُم‏) Tafsiri: Na wala usikihatarishe kitu chochote kwa matumaini ya kupata kilicho zaidi ya hicho (yaani usijihatarishe kwa tamaa ya kupata ziada).

 Nahju al-Balagha, uhakiki wa Subhi Salih, 1414 H, Barua ya 31, uk. 403.

Sehemu ya barua za Nahju al-Balagha inajumuisha jumla ya vifungu 79 vyenye barua 63, maandiko 12 ya wasia yanayohusiana na maagizo ya kiserikali, na maandiko mengine ya mikataba mbalimbali.[50] Maudhui ya barua hizi, ambazo walengwa wake wakuu walikuwa ni, magavana, makamanda wa kijeshi, na wakusanyaji wa kodi, yamejikita katika uchambuzi wa masuala ya uongozi wa nchi, utawala bora, na namna maafisa wa kiserikali wanavyopaswa kuamiliana na wananchi wao.[51] Imamu Ali (a.s) anaweka wazi sifa za uongozi thabiti wa kisiasa.[52] Sayyid Ja'afar Shahidi anaamini kuwa, ingawa barua hizi zilitoka kwa mtawala mkuu kwenda kwa magavana wake, ila lugha ya mwandishi wake haikuwa ya kimabavu, bali inasomeka kama barua ya baba mwenye upendo anamuandikia mwanawe.[53] Barua ya Imamu Ali (a.s) kwenda kwa Imamu Hassan (a.s), agizo kwa Malik al-Ashtar kwa ajili ya uongozi wa Misri, na barua kwa Othman bin Hunaif na Ash'ath, zinasimama kama barua mashuhuri zaidi kati ya barua mbalimbali za Imamu Ali (a.s).

Semi Fupi

Imamu Ali (a.s):

إِذَا أَرْذَلَ اللَّهُ عَبْداً حَظَرَ عَلَيْهِ الْعِلْم‏‏‏ Tafsiri: Mwenyezi Mungu anapomdhalilisha mja Wake, humzuia kupata elimu (humnyima elimu).

 Nahju al-Balagha, uhakiki wa Subhi Salih, 1414 H, Hekima ya 288, uk. 526.

Sehemu ya tatu inajumuisha idadi ya semi fupi za busara 480, ambazo ima ni mawaidha, au majibu ya maswali mbalimbali.[54] Sayyid Radhi alitenga fungu maalumu alilolipa anwani ya Faslun fi Ghara'ibi Kalaamihi (Fungu linalohusu semi za kushangaza za Imamu Ali). Fungu ambalo limekusanya semi ngumu maalumu zinazohitaji ufafanuzi wa kina.[55] Fungu hili lina jumla ya Hadithi 9, ambapo Hadithi ya kwanza kabisa inazungumzia dhana ya kudhihiri kwa Imamu wa Zama (Imamu Mahdi).[56]

Pia angalia: Orodha ya maneno mafupi ya Nahju al-Balagha

Vyanzo vya Nahju al-Balagha

Sayyid Radhi alitaja vyanzo kahdaa alivyovitegemea katika kukusanya semi za Imamu Ali (a.s), vikiwemo kitabu cha Al-Bayan wa al-Tabyin cha Al-Jahidh, Al-Muqtadhab cha Al-Mubarrad, Al-Maghazi cha Sa'id bin Yahya al Umawi, Al-Jamal cha Al-Waqidi, Al-Maqamat cha Abu Ja'afar al-Iskafi, pamoja na Tarikh al-Tabari.[57] Tafiti zinasema kuwa kuna idadi ya vyanzo kumi na saba vilivyotajwa moja kwa moja ndani ya kitabu hichi.[58] Sayyid Radhi aliweza kufaidika na maktaba mbili kubwa zilizokuwepo Baghdad kwa ajili ya kazi hiyo, moja ikiwa ya kaka yake Sayyid Murtadha yenye vitabu 80,000 na nyingine ikiwa ni Maktaba ya Baitul-Hikma yenye vitabu 10,000.[59]

Ingawa baadhi ya wanazuoni waliisifu kazi kubwa ya Sayyid Radhi, ila pia hawakuacha kuwasilisha ukosoaji wao na kutaja mapungufu kadhaa ya mwandishi huyu shupavu.[60] Muhammad Taqi al-Shushtari katika tasnifu yake Bahju al-Sabbaghah fi Sharh Nahju al-Balagha amebainisha akisema kuwa, kwa sababu ya kutegemea kwake vitabu vya Ahlu Sunna peke yake, hiyo ilipelekea kupatikana kwa changamoto zifuatazo:

  • Kwanza, kunasibishwa kwa baadhi ya semi na Imamu Ali (a.s) huku semi hizo zikiwa zimetengenezwa na maadui zake.
  • Pili, kukatwa kwa baadhi ya sentensi kwa namna inayoharibu maana halisi iliyokusudiwa.
  • Tatu, kunasibishwa kwa baadhi ya semi ambazo mapokezi ya Shia yanazikanusha.
  • Nne, kunasibishwa kwa baadhi ya Hadithi za Maimamu wengine na Imamu Ali (a.s).
  • Tano, kunakiliwa kwa semi zilizosikiwa kupitia ndoto tu.
  • Sita, kunakiliwa kusiko sahihi kwa matukio ya kihistoria yaliyofungamana na hotuba husika za Imamu Ali (a.s).[61]

Isnadi za Hotuba, Barua na Hekima

Kitabu Nahju al-Saadah fi Mustadrak Nahju al-Balagha kilichoandikwa na Muhammad Baqir Mahmudi, ambamo ndani yake zimekusanywa sanad za khutba, barua na hekima za Nahju al-Balagha.

Kutoashiria isnadi za semi za Imamu Ali (a.s) ndani ya kitabu hichi kunatajwa kama changamoto kubwa dhidi ya kazi hii maridadi, jambo lililopelekea baadhi ya wanazuoni kuzichukulia Hadithi za kitabu hichi kama mapokezi yaliyokatika isnadi zake, na kutoweza zitumia kama ushahidi thabiti katika masuala ya kifiqhi.[62] Katika ketetela mbinu ya Sayyid Radhi, watafiti wanasema kuwa, vyanzo vya semi hizi vilikuwa ni mashuhuri mno katika zama zake, na hakukuwa na umuhimu wa kuvitaja katika kunukuu kwake.[63] Pamoja na hayo, wanalugha wengi walichukua juhudi kubwa za kukusanya isnadi kutoka katika vyanzo vya kale vya kihistoria na kuziweka katika mfumo wa nyaraka thibitishi za isnadi za Nahju al-Balagha, ili kuthibitisha usahihi wa kunasibishwa kwake na Imamu Ali (a.s).[64] Zifuatazo ni baadhi ya tasnifu za kitaalamu kuhusiana na vyanzo hivyo:

Tafsiri

Nahju al-Balagha, tafsiri ya Sayyid Jafar Shahidi.

Wataalamu wa lugha wamekitafsiri kitabu hichi katika lugha mbalimbali ulimwenguni zikiwemo lugha ya Kifarsi, Kiingereza, Kifaransa, Kihindi, Kiitaliano, Kituruki cha Istanbul, Kiurdu, Kimalayu, Kialbania, Kibosnia, Kigujarati, Kiashuri, Kiarmenia, Kiswahili, Kihausa, Kijapani, Kichina, Kirusi, Kihispania, pamoja na Kitajiki.[73] Tafiti za kibibliografia zinabainisha kuwa kuna zaidi ya aina 100 za matoleo ya tafsiri za kitabu hichi,[74] ambapo kuna karibu aina 40 za tafsiri kwa lugha ya Kifarsi,[75] takriban tafsiri 10 za Kiingereza, na tafsiri 13 za lugha ya Kiurdu.[76]

Ja'far Subhani anaamini kuwa, ididadi kubwa ya tafsiri za Kifarsi si sahihi na wala hazikubaliki kitaalamu, hii ni kwa sababu watafsiri wake hawakutou (au hawakuwa na) uzito unaostahichi katika elimu ya leksikolojia, fasihi, na sarufi ya lugha ya Kiarabu. Mwanazuoni huyu anasisitiza kuwa, tafsiri ya Mohammad Saleh Barghani pamoja na tafsiri ya Sayyid Ja'afar Shahidi, ndizo kazi zinazoaminika na zenye ufasaha mkubwa kuliko nyengine zote.[77] Wasomi wametaja kazi nyengine kadhaa za watafsiri wengine wa lugha ya Kifarsi ikiwemo kazi ya Ali Naqi Faidhu al-Islam,[78] Abdul Mohammad Ayati,[79] Mohammad Taqi Ja'fari,[80] Mohammad Dashti,[81] Mohammad Mehdi Fooladvand,[82] pamoja na Hossein Ansarian.[83]

Tafsiri ya Nahju al-Balagha ya Ali-Asghar Faqihi.

Moja ya matoleo muhimu ya lugha ya Kipashto ni lile lenye jina la Goftare Mughaddas, lililotolewa mnamo mwaka 1962 M. Toleo hili lilitolewa likiwa na maelezo ya pembizoni yaliyoandikwa na mshairi aitwaye Amir Hamza Khan Shinwari yaliyotokana na tafsiri ya Kiurdu ya Rais Ahmad Ja'afari.[84]

Watafiti wa Kimagharibi wanaitaja tafsiri ya lugha ya Kiingereza iliyoandikwa na mwanamke aitwaye Tahireh Saffarzadeh kama moja ya kazi mahiri na mashuhuri zaidi za lugha ya Kiingereza.[85]

Sherehe

Uandishi wa sherehe za Nahju al-Balagha ulianza miaka michache tu baada ya kukamilika kwa utunzi wake, amali ambayo bado inaendelea hadi leo.[86] Katika historia nzima ya Uislamu, hakuna kitabu chochote kile kilichofafanuliwa na kushereheshwa kwa kiwango kikubwa baada ya Qur'ani Tukufu kama ilivyo kuhusu Nahju al-Balagha.[87] Kuwepo kwa idadi kubwa ya sherehe za Nahju al-Balagha, kunaleta ugumu wa kupata idadi kamili na sahihi ya vitabu vyote vinavyohusiana na Nahju al-Balagha. Na hii ndiyo sababu iliyopelekea kuandikwa kwa makala maalumu kwa ajili ya kutafiti orodha kamili ya vitabu hivyo.[88] Baadhi ya vitabu katika orodha ya sherehe hizi ni kama ifuatavyo:

Sherehe za Kiarabu:

  1. Sharhu Nahju al-Balagha: kazi ya Ibnu Abi al-Hadid, mshairi wa madhehebu ya Muutazila,[89] ambaye sherehe yake ilileta mapinduzi makubwa katika mifumo ya uandishi wa sherehe za Nahju al-Balagha.[90]
  2. Sharhu Nahju al-Balagha: Kazi iliyofanywa na Ibnu Maitham al-Bahrani.[91]
  3. Minhaaju al-Baraa’a fi Sharh Nahju al-Balagha: kilichoandikwa na Habibullahi al-Khui.[92]
  4. Minhaaju al-Baraa’a fi Sharh Nahju al-Balagha: Kazi ya Qutb al-Rawandi.[93]
  5. Hada'iqu al-Haqa'iqi fi Sharh Nahju al-Balagha: kilichotungwa na Qutbuddin al-Kaidari mnamo mwaka 576 Hijria.[94]

Mustadrak za Kitabu

Kuna idadi kubwa ya wanazuoni waliofanya juhudi za kukusanya semi mbalimbali za Imamu Ali kutoka katika vitabu vya kihistoria ambazo hazikujumuishwa katika matini asili ya Nahju al-Balagha. Kazi za wanazuoni hawa zilichapishwa chini ya anwani ya Mustadrak.[95] Hata Sayyid Radhi mwenyewe pia naye aliacha baadhi ya kurasa za kitabu chake cha Nahju al-Balagha zikiwa tupu, wakati wa kukitunga kitabu hichi. Alifanya hivyo kwa lengo la kupata nafasi ya kuongeza semi mpya pindi atakapozipata hapo mbeleni.[96] Baadhi ya vitabu vya wanazuoni hao mbalimbali ni kama ifuatavyo:

  • Al-Tadhyilu ala Nahju al-Balagha: Kazi ya Abdullah bin Ismail al-Halabi, iliyoandikwa mnamo karne ya tano ya Hijria.[97]
  • Mulhaqu Nahju al-Balagha: Kazi iliyofanywa na Ahmad bin Yahya bin Naqah mnamo mwaka 729 Hijria.[98]
  • Mustadraku Nahju al-Balagha: Kitabu kilichoandikwa na Hadi Kashifu al-Ghitaa, kilichochapishwa mnamo mwaka 1354 Hijria.[99]
  • Tamamu Nahju al-Balagha: Tasnifu iliyotungwa na Sayyid Sadiq al-Musawi.[100]
  • Nahju al-Saadah fi Mustadrak Nahju al-Balagha: Kazi iliyoandikwa kupitia kalamu ya mwanazuoni Muhammad Baqir al-Mahmoudi.[101]

Shaka na Majibu Yake

Nakala ya kale ya Nahju al-Balagha kutoka karne ya 6 Hijria.

Baadhi ya wanazuoni wa Kisunni wamewasilisha shaka mbili kuu kuhusiana na kitabu cha Nahju al-Balagha: kwanza, haiko wazi kama maandiko haya yalikusanywa by Sayyid Radhi au yalikusanywa na kaka yake aitwaye Sayyid Murtadha; pili, kuna uwezo kuwa semi hizi si za Imamu Ali (a.s), bali zilitengenezwa kwa uongo na Sayyid Murtadha au Sayyid Radhi.[102] Ibnu Hajar al-Asqalani anaamini kuwa kitabu hichi ni tasnifu ya Sayyid Murtadha, huku akiyahisabu maneno yaliyomo ndani ya kitabu hichi kuwa ni uongo na uzushi usio na mashiko yoyote.[103]

Mkabala na hayo, wanazuoni wa Kishia pamoja na wataalamu wengi wa Ahlu Sunna wanashikilia msimamo thabiti, kuwa mkusanyaji halisi wa Nahju al-Balagha ni Sayyid Radhi, na kwamba yeye aliyakusanya maandiko haya kutoka katika kauli za Imamu Ali (a.s).[104] Watafiti wamesema kuwa, shaka hiyo inayohusu utambulisho wa mkusanyaji, inadhihirisha ukosefu wa mapitio ya matini asili ya kitabu chenyewe, kwa sababu pale mwandishi anapofafanua maneno magumu ya Imamu Ali (a.s), hutumia kauli isemayo: Qala al-Radhi (Sayyid Radhi anasema), jambo linalothibitisha kuwa mkusanyaji wa kazi hii alikuwa ni Sayyid Radhi.[105] Wachambuzi wa vitabu wanasema kuwa, idhini rasmi ambazo wanazuoni wa zama hizo walikuwa wakizitoa kwa ajili ya kunakili au kupokea yalimo katika kitabu hichi, ambazo minyororo ya mapokezi yake inafika moja kwa moja kwa Sayyid Radhi, zimefikia kiwango cha thibitisho la mfululizo la mutawatir, ukweli unoondoa shaka ya aina yoyote ile dhidi yake.[106] Najashi, nguli wa elumu ya rijal aliyeishi zama moja na Sayyid Radhi, amekinasibisha kitabu hichi kwa Sayyid Radhi kwa njia sahihi kabisa.[107]

Ibnu Abi al-Hadid akielezea jambo hili anasema kuwa, kutilia shaka juu ya kunasibishwa kwa maudhui za Nahju al-Balagha na Imamu Ali (a.s) ni matokeo ya kufuata matamanio ya nafsi pamoja na ushabiki na taasubi pofu.[108] Hoja thabiti inayobainisha ukweli huu inajengeka juu ya msingi usemao kuwa, sehemu fulani ya Nahju al-Balagha ni sehemu ya semi za Imamu Ali (a.s), kwa sababu usahihi wake umethibitika kupitia mapokezi ya mfululizo ya mutawatir, na kila mtu mwenye akili anahukumu kuwa matini yote iko katika mtiririko wenye mtindo mmoja unaolingana na unaoshikamana kisawasawa.[109] Ibnu Taymiyyah naye pia alikuwa akiichukulia Nahju al-Balagha kuwa ni maneno na semi za Imamu Ali (a.s), hii ni kwa mujibu wa yale aliyoyanakili mwanafunzi wake aitwaye Salahuddin al-Safadi.[110] Kadhalika, Allamah Bahr al-Ulum amebainisha ukweli huo akisema kuwa, ile kauli inayodai kuwa kitabu hichi kimetengenezwa kwa njia ya uongo ni miongoni mwa tuhuma kubwa katika uwanja wa historia.[111]

Ukusanyaji wa Kale

Katika harakati za kupinga madai ya uzushi, Sayyid Hibatuddin al-Shahrastani anaamini kuwa Sayyid Radhi si mwandishi wa kwanza kabisa kukusanya hotuba na semi za Imamu Ali (a.s), bali kulikuwa na watu wengi kabla yake waliokuwa wakihifadhi hotuba na maneno ya Imamu huyu muadhamu (a.s).[112] Yaaqubi ambaye ni mtaalamu wa fani ya historia, amebainisha wazi katika kitabu chake cha historia, uwepo wa hotuba mia nne zilizorithiwa kutoka kwa Imamu Ali (a.s).[113] Hali kadhalika, Al-Mas'udi ambaye ni mwandishi wa kitabu cha Muruju al-Dhahab anaeleza kuwa, kulikuwa na watu kadhaa waliohifadhi zaidi ya hotuba 480 zilizotolewa na Imamu Ali (a.s).[114] Ibnu Shu'uba al-Harrani mwandishi wa kitabu Tuhafu al-Uquul, naye pia anaamini kuwa, kama hotuba za Imamu Ali (a.s) zinazohusu tauhidi pekee zingekusanywa pamoja, basi ukubwa wa maandiko hayo ungekuwa sawa na ukubwa wa kitabu cha Tuhafu al-Uquul.[115]

Zaid bin Wahb ndiye mtu wa kwanza kabisa kuandika hotuba za Imamu Ali (a.s) na kuzifuma katika mfumo wa kitabu, naye alikuwa ni mmoja wa wafuasi wa Imamu Ali (a.s). Kitabu chake hicho kilichokuwa kikiitwa Kitabu al-Khutab kilichoendelea kuwepo hadi karne ya tano Hijria.[116] Vitabu kama vile Khutabu Amirul-Mu’minina kilichotungwa na Mas'ada bin Sadaqa, Khutabu Ali kilichoandikwa na Ibrahim bin Hakam al-Fazari, Khutabu Amirul-Muuminina kilichotungwa na Abdul Adhim al-Hassani, pamoja na kitabu cha Khutabu Aliyyin wa Kutubihi ila Ummaalihi kilichoandikwa na Ali bin Muhammad al-Madaini, vyote vinasomeka kama miongoni mwa maandiko ya mwanzo kabisa kabla ya zama za Sayyid Radhi.[117]

Rejea

  1. ↑ Mostafavi, «معرفی نهج البلاغه», uk. 23.
  2. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 11.
  3. ↑ Mostafavi, Uhusiano kati ya Nahjul Balagha na Qur'ani, uk. 32.
  4. ↑ Ostadi, Kitabnameh ye Nahju al-Balagha, uk. 5.
  5. ↑ Amin, A’yan al Shiah, Juz. 9, uk. 218.
  6. ↑ Rafiei, «اصالت علوی نهج البلاغه», uk. 131.
  7. ↑ Nuri, Mustadrak al Wasa'il, Juz. 21, uk. 204.
  8. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, uk. 559.
  9. ↑ Jafari, Sayyid Radhi, uk. 22.
  10. ↑ Amin, A’yan al Shiah, Juz. 9, uk. 218.
  11. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, Utangulizi, uk. 34.
  12. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, Utangulizi, uk. 35.
  13. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, Utangulizi, uk. 36.
  14. ↑ Abduh, Sharh Nahju al-Balagha, uk. 10.
  15. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 32.
  16. ↑ Ibn Abi al Hadid, Sharh Nahju al-Balagha, Juz. 1, uk. 24.
  17. ↑ Angalia: Al Husseini, Masadir Nahjul-Balagha wa Asanidihi, Juz. 1, uk. 105.
  18. ↑ Ibn Abi al Hadid, Sharh Nahju al-Balagha, Juz. 7, uk. 214.
  19. ↑ Jordac, Sauti ya Uadilifu wa Kibinadamu, uk. 282.
  20. ↑ Al Husseini, Masaadir Nahju al-Balagha, Juz. 1, uk. 108.
  21. ↑ Muhyi al Din, «Utangulizi», katika Sharh Nahju al-Balagha, uk. 2.
  22. ↑ Khoei, Minhaaj al Bara’ah, Juz. 21, uk. 379.
  23. ↑ Ibn Abi al Hadid, Sharh Nahju al-Balagha, Juz. 19, uk. 184; Khoei, Minhaaj al Bara’ah, Juz. 21, uk. 379; Makarim, Payame Imame Amir al Mu'minin, Juz. 14, uk. 395.
  24. ↑ Jordac, Sauti ya Uadilifu wa Kibinadamu, uk. 282; «نهج البلاغه از نگاه آنتوان بارا نویسنده مسیحی» (Nahju al-Balagha kwa mtazamo wa Antoine Bara, mwandishi Mkristo), Ahlolbait.
  25. ↑ Jordac, Rawa’i’ Nahju al-Balagha, uk. 4.
  26. ↑ «ماجرای مسلمان‌شدن یک آمریکایی به برکت نهج البلاغه» (Kisa cha kusilimu kwa Mmarekani kwa baraka ya Nahju al-Balagha), Hawzah News Agency; «اظهارات خواندنی جوان اروپایی که شیعه شد» (Kauli za kuvutia za kijana wa Ulaya aliyekuwa Shia), Estebsar; «مسلمان‌شدن ۸۰ سرخپوست با نهج البلاغه» (Wahindi Wekundu 80 walisilimu kupitia Nahju al-Balagha), Saheb News; «پدر و مادرم از طریق نهج البلاغه مسلمان شدند» (Wazazi wangu walisilimu kupitia Nahju al-Balagha), ISNA; «آشنایی با آموزه‌های متعالی نهج البلاغه زمینه‌ساز تشرف یک جوان اهل کوزوو به تشیع بود» (Ufahamu wa mafunzo matukufu ya Nahju al-Balagha ulimvutia kijana wa Kosovo kuwa Shia), Iqna News.
  27. ↑ «مسلمان‌شدن پروفسور لگنهاوزن با مطالعه نهج البلاغه» (Profesa Muhammad Legenhausen alisilimu kwa kusoma Nahju al-Balagha), Aparat; «پروفسور محمد لگنهاوزن چگونه مسلمان و شیعه شد؟» (Profesa Muhammad Legenhausen alisilimu na kuwa Shia vipi?), YouTube.
  28. ↑ «بندی از شرح نهج البلاغه ابن ابی‌الحدید» (Sehemu kutoka Sharhu Nahju al-Balagha ya Ibn Abi al-Hadid), Maktaba na Makumbusho ya Kitaifa ya Malek.
  29. ↑ Makarim, Payame Imame Amir al Mu'minin, Juz. 1, uk. 39.
  30. ↑ Ibn Abi al Hadid, Sharh Nahju al-Balagha, Juz. 11, uk. 153.
  31. ↑ Aqqad, Abqariyyat al Imam Ali, uk. 127.
  32. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 44.
  33. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 45.
  34. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 44.
  35. ↑ Jawadi Amoli, «تفسیر سوره جمعه جلسه ۱۰» (Tafsiri ya Sura ya Ijumaa, kipindi cha 10), Tovuti ya Esra.
  36. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, uk. 39.
  37. ↑ Shahidi, «Utangulizi», katika Nahju al-Balagha, uk. 14.
  38. ↑ Shahidi, «Utangulizi», katika Nahju al-Balagha, uk. 14.
  39. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 19.
  40. ↑ Ibn Maitham, Sharh Nahju al-Balagha, Juz. 1, uk. 251.
  41. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, uk. 48.
  42. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, uk. 49.
  43. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, uk. 107.
  44. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, uk. 114.
  45. ↑ Khoei, Minhaaj al Bara’ah, Juz. 6, uk. 70.
  46. ↑ Hushyar, «Sura ya Mwanadamu Mkamilifu», uk. 20.
  47. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, uk. 303.
  48. ↑ Mutahhari, Majmu'ah Athar, Juz. 16, uk. 360.
  49. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, uk. 306.
  50. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 19.
  51. ↑ Shahidi, «Utangulizi», katika Nahju al-Balagha, uk. 15.
  52. ↑ Beheshti, «Maadili ya Kisiasa», uk. 12.
  53. ↑ Shahidi, «Utangulizi», katika Nahju al-Balagha, uk. 15.
  54. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, uk. 469.
  55. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, uk. 515.
  56. ↑ Sayyid Radhi, Nahju al-Balagha, uk. 517.
  57. ↑ Ibrahim, «Utangulizi», katika Sharh Nahju al-Balagha, Juz. 1, uk. 7.
  58. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 24-25.
  59. ↑ Mostafavi, «Kutambulisha Nahju al-Balagha», uk. 35-36.
  60. ↑ Shushtari, Bahj al-Sabbaghah, Juz. 1, uk. 20.
  61. ↑ Shushtari, Bahj al-Sabbaghah, Juz. 1, uk. 20-22.
  62. ↑ Mehrizi, Ufahamu wa Matini, uk. 159.
  63. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 22.
  64. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 25.
  65. ↑ Mahmoudi, Nahj al-Sa'adah, Juz. 1, uk. 5.
  66. ↑ Kashif al-Ghita, Mustadrak Nahj al-Balagha, uk. 193.
  67. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 26.
  68. ↑ Nimah, Masadir Nahj al-Balagha, uk. 5.
  69. ↑ Dashti, Asnad wa Madarik-e Nahju al-Balagha, uk. 5.
  70. ↑ Dashti, Asnad wa Madarik-e Nahju al-Balagha, uk. 5.
  71. ↑ Ostadi, Kitabnameh-ye Nahju al-Balagha, uk. 8.
  72. ↑ Al Husseini, Masaadiru Nahju al-Balagha, Juz. 1, uk. 6.
  73. ↑ Dinparvar, «Nahju al-Balagha», uk. 60.
  74. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 77.
  75. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 78.
  76. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 77.
  77. ↑ Subhani, «Kupitia Nahju al-Balagha», uk. 45.
  78. ↑ Faidh al-Islam, Sharh Nahju al-Balagha, Juz. 1, uk. 10.
  79. ↑ Ayati, Nahju al-Balagha, uk. 5.
  80. ↑ Jafari, Nahju al-Balagha, uk. 5.
  81. ↑ Dashti, Nahju al-Balagha, uk. 5.
  82. ↑ Fooladvand, Nahju al-Balagha, uk. 5.
  83. ↑ Ansarian, Nahju al-Balagha, uk. 5.
  84. ↑ Irna, «آشنایی با مشاهیر و نخبگان فرهنگی پاکستان», uk. 2.
  85. ↑ «صفارزاده نهج البلاغه را به سه زبان ترجمه کرد», Tovuti ya Hawzah.
  86. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 73.
  87. ↑ Boroujerdi, «Sherehe za Nahju al-Balagha», uk. 119.
  88. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 73.
  89. ↑ Ibn Abi al Hadid, Sharh Nahju al-Balagha, Juz. 1, uk. 500.
  90. ↑ Boroujerdi, «Sherehe za Nahju al-Balagha», uk. 124.
  91. ↑ Ibn Maitham, Sharh Nahju al-Balagha, Juz. 1, uk. 400.
  92. ↑ Khoei, Minhaaj al Bara’ah, Juz. 1, uk. 300.
  93. ↑ Rawandi, Minhaaju al-Bara’ah, Juz. 1, uk. 250.
  94. ↑ Kaidari, Hada'iqu al-Haqa'iqi, Juz. 1, uk. 300.
  95. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 28.
  96. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 28.
  97. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 28.
  98. ↑ Hafezyan, «نهج البلاغه», uk. 28.
  99. ↑ Kashif al-Ghita, Mustadraku Nahju al-Balagha, J.1, uk.16.
  100. ↑ Mousavi, Tamamu Nahju al-Balagha, Juz. 1, uk. 500.
  101. ↑ Mahmoudi, Nahj al-Sa'adah, Juz. 1, uk. 500.
  102. ↑ Ibn Khallikan, Wafayat al-A'yan, Juz. 3, uk. 313; Yafei, Mira'at al-Jinan, Juz. 3, uk. 43.
  103. ↑ Ibn Hajar, Lisan al-Mizan, Juz. 4, uk. 223.
  104. ↑ Davani, «Mwandishi wa Nahju al-Balagha», uk. 117.
  105. ↑ Atardi, Sharh Nahju al-Balagha, Juz. 1, uk. 14.
  106. ↑ Shahrestani, «Ma huwa Nahju al-Balagha», uk. 13.
  107. ↑ Najashi, Rijal al-Najashi, uk. 398.
  108. ↑ Ibn Abi al Hadid, Sharh Nahju al-Balagha, Juz. 10, uk. 127.
  109. ↑ Ibn Abi al Hadid, Sharh Nahju al-Balagha, Juz. 10, uk. 128.
  110. ↑ Safadi, Al-Wafi bil-Wafayat, Juz. 2, uk. 277.
  111. ↑ Bahr al-Ulum, Al-Fawa'id al-Rijaliyah, Juz. 3, uk. 118.
  112. ↑ Shahrestani, «Ma huwa Nahju al-Balagha», uk. 21.
  113. ↑ Yaqubi, «Mwenendo wa Watu», uk. 15.
  114. ↑ Masudi, Muruju al-Dhahabi, Juz. 2, uk. 419.
  115. ↑ Harrani, Tuhafu al_Uquli, uk. 61.
  116. ↑ Mostafavi, «Kutambulisha Nahju al-Balagha», uk. 33.
  117. ↑ Mostafavi, «Kutambulisha Nahju al-Balagha», uk. 33-35.

Vyanzo

  • Abduh, Muhammad. Sharhu Nahju al-Balagha. Cairo: Matba'at al-Istiqamah, b.t.
  • Al-Husayni al-Khatib, Sayyid Abd al-Zahra. Masadiru Nahju al-Balagha wa Asaniduhu. Beirut: Dar al-Zahra, 1409 H.
  • Amin, Muhsin. A‘yanu al-Shi‘ah. Beirut: Dar al-Ta‘aruf li al-Matbu‘at, 1406 H.
  • Aqqad, Abbas Mahmud. Abqariyyatu al-Imamu Ali. Beirut: Al-Maktabah al-Asriyah, 1431 H.
  • Atardi, Azizullah. «Muqaddimah». Katika Sharhu Nahju al-Balagha ya mwanazuoni wa karne ya nane. Qum: Atarod, 1996 M.
  • Ayati, Abd al-Muhammad. Nahju al-Balagha. Tehran: Daftar-e Nashr-e Farhang-e Islami, 1999 M.
  • Bahr al-Ulum, Muhammad Mahdi ibn Murtadha. Al-Fawa’id al-Rijaliyyah. Tehran: Maktabat al-Sadiq, 1984 M.
  • Beheshti, Ahmad; Sadriyeh, Payam. «اخلاق سیاسی در نامه‌های نهج البلاغه» (Maadili ya kisiasa katika barua za Nahju al-Balagha). Pazhouhesh-haye Nahju al-Balagha, Na. 30 (2010 M), uk. 12–35.
  • Boroujerdi, Mustafa; Sadra'i Khoei, Ali. «شرح‌های نهج البلاغه» (Sherehe za Nahju al-Balagha). Katika Daneshnameh-ye Imamu Ali (a), Juz. 12. Tehran: Mu'assasah-ye Farhangi wa Andisheh-ye Islami, 2001 M.
  • Dashti, Muhammad. Asnad wa Madarik-e Nahju al-Balagha. Qum: Mu'assasah-ye Farhangi wa Tahqiqati-ye Amir al-Mu'minin (a), 1999 M.
  • Dashti, Muhammad. Ruwat wa Muhaddithan-e Nahju al-Balagha. Qum: Mu'assasah-ye Farhangi wa Tahqiqati-ye Amir al-Mu'minin (a), 1999 M..
  • Davani, Ali. «سید رضی گردآورنده نهج البلاغه» (Sayyid Radhi, mkusanyaji wa Nahju al-Balagha). Katika Maqalat darbareh-ye Nahju al-Balagha wa Gardavarandeh-ye An. Tehran: Bonyad-e Nahju al-Balagha, 1994 M.
  • Dinparvar, Sayyid Jamal al-Din. «نهج البلاغه؛ سندی ماندگار» (Nahju al-Balagha; hati ya kudumu). Pazhouhesh-haye Nahju al-Balagha, Na. 2–3 (2001 M), uk. 60–75.
  • Hafezyan Baboli, Abulfazl. «نهج البلاغه» (Nahju al-Balagha). Katika Daneshnameh-ye Imamu Ali (a), Juz. 12. Tehran: Mu'assasah-ye Farhangi wa Andisheh-ye Islami, 2001 M.
  • Harrani, Ibn Shu'bah. Tuhaf al-'Uqul 'an Al al-Rasul. Qum: Daftar-e Intisharat-e Islami, 1404 H.
  • Hushyar, Yaser; Tajalil, Jalil. «بررسی تطبیقی سیمای انسان کامل در خطبه متقین نهج البلاغه و آثار عزیزالدین نسفی» (Uchambuzi wa kulinganisha sura ya mwanadamu mkamilifu katika Hotuba ya Muttaqin ya Nahju al-Balagha na kazi za Aziz al-Din Nasafi). Pazhouhesh-haye Nahju al-Balagha, Na. 46 (2015 M), uk. 20–35.
  • Ibn Hajar al-Asqalani, Ahmad ibn Ali. Lisan al-Mizan. Beirut: Mu'assasat al-A'lami li al-Matbu'at, 1390 H.
  • Ibn Khallikan, Ahmad ibn Muhammad. Wafayat al-A'yan wa Anba' Abna' al-Zaman. Beirut: Dar Sadir, 1900 M.
  • Kaidari, Qutb al-Din. Hada'iq al-Haqa'iq fi Sharh Nahju al-Balagha. Qum: Bonyad-e Nahju al-Balagha, 1416 H.
  • Kashif al-Ghita, Hadi. Mustadrak Nahju al-Balagha. Beirut: Maktabat al-Andalus, b.t.
  • Lahiji, Mirza Muhammad Baqir. Sharh Nahju al-Balagha. Tehran: Markaz-e Pazhouhesh-e Miras-e Maktub, 2000 M.
  • Mahmoudi, Muhammad Baqir. Nahju al-Sa'adah fi Mustadrak Nahju al-Balagha. Tehran: Wizarat-e Farhang wa Irshad-e Islami, 1418 H.
  • Mas'udi, Ali ibn al-Hussein. Muruj al-Dhahab. Qum: Dar al-Hijrah, 1409 H.
  • Mehrizi, Mehdi. Shenakht-e Mutun-e Hadith wa Nahju al-Balagha. Qum: Markaz-e Jahani-ye Ulum-e Islami, 1998 M.
  • Moayedi, Abul Hassan. «راهنمای پژوهش‌های نهج البلاغه» (Mwongozo wa utafiti wa Nahju al-Balagha). Motale'at-e Tafsir, Na. 1 (2010 M), uk. 1–15.
  • Mostafavi, Sayyid Javad. Rabiteh-ye Nahju al-Balagha wa Qur'an. Tehran: Bonyad-e Nahju al-Balagha, 2007 M.
  • Mostafavi, Sayyid Javad. «معرفی نهج البلاغه» (Utambulisho wa Nahju al-Balagha). Meshkat, Na. 1 (1982 M), uk. 23–35.
  • Musawi, Sayyid Sadiq. Tamam Nahju al-Balagha. Beirut: Mu'assasat al-A'lami li al-Matbu'at, 1426 H.
  • Mutahhari, Murtadha. Majmu'ah Athar. Tehran: Sadra, 1993 M.
  • Najashi, Ahmad ibn Ali. Rijal al-Najashi. Qum: Daftar-e Intisharat-e Islami, 1365 Sh.
  • Ni'imah, Abdullah. Masadir Nahju al-Balagha. Najaf: Maktabat al-Rawdah al-Haydariyyah, 1392 H.
  • Nuri, Mirza Hussein. Mustadrak al-Wasa'il wa Mustanbat al-Masa'il. Beirut: Mu'assasat Al al-Bayt li-Ihya' al-Turath, 1408 H.
  • Qifti, Ali ibn Yusuf. Inbah al-Ruwat 'ala Anbah al-Nuhat. Beirut: Al-Maktabah al-Asriyyah, 1424 H.
  • Rafiei, Behrouz. «اصالت علوی نهج البلاغه» (Uhalisia wa Kialawi wa Nahju al-Balagha). Roshanshenasi-ye Olum-e Ensani, Na. 26 (2001 M), uk. 131–150.
  • Rah-avard-e Noor. «سی دی دانشنامه نهج البلاغه» (CD ya Ensaiklopidia ya Nahju al-Balagha). Rah-avard-e Noor, Na. 13 (2000 M), uk. 164–170.
  • Rawandi, Qutb al-Din. Minhaj al-Bara'ah fi Sharh Nahju al-Balagha. Qum: Maktabat Ayatullah Mar'ashi Najafi, 1406 H.
  • Safadi, Salah al-Din. Al-Wafi bi al-Wafayat. Beirut: Dar Ihya' al-Turath al-Arabi, 1420 H.
  • Sayyid Radhi, Muhammad ibn Hussein. Nahju al-Balagha. Qum: Hijrat, 1414 H.
  • Sayyid Radhi, Muhammad ibn Hussein. Nahju al-Balagha. Tafsiri ya Abd al-Muhammad Ayati. Tehran: Daftar-e Nashr-e Farhang-e Islami, 1999 M.
  • Sayyid Radhi, Muhammad ibn Hussein. Nahju al-Balagha. Tafsiri ya Hussein Ansarian. Tehran: Payam-e Azadi, 2009 M.
  • Sayyid Radhi, Muhammad ibn Hussein. Nahju al-Balagha. Tafsiri ya Muhammad Dashti. Qum: Mashhur, 2000 M.
  • Sayyid Radhi, Muhammad ibn Hussein. Nahju al-Balagha. Tafsiri ya Muhammad Mahdi Fuladvand. Tehran: Saeb, 2001 M.
  • Sayyid Radhi, Muhammad ibn Hussein. Nahju al-Balagha. Tafsiri ya Muhammad Taqi Ja'fari. Mashhad: Bonyad-e Pazhouheshhaye Islami, 2001 M.
  • Shahidi, Sayyid Ja'far. «مقدمه» (Utangulizi). Katika Nahju al-Balagha. Tehran: Sherkat-e Entesharat-e Elmi wa Farhangi, 1999 M.
  • Shahristani, Sayyid Hibat al-Din. Ma Huwa Nahju al-Balagha. Beirut: Dar al-Thaqafah, 1961 M.
  • Shushtari, Muhammad Taqi. Bahj al-Sabbaghah fi Sharh Nahju al-Balagha. Tehran: Amirkabir, 1997 M.
  • Taasisi ya Tebyan. Tembr-haye Iran. Qum: Mu'assasah-ye Farhangi wa Ettela'rasani-ye Tebyan, 2008 M.
  • Tabataba'i, Sayyid Abd al-Aziz. «بازمانده‌های نسخه‌های خطی نهج البلاغه تا پایان قرن هشتم هجری» (Nakala zilizosalia za maandishi ya mkono ya Nahju al-Balagha hadi mwisho wa karne ya nane Hijria). Turathuna, Na. 5 (1406 H), uk. 5–25.
  • Tabataba'i, Sayyid Abd al-Aziz. «در قلمرو نهج البلاغه» (Katika uga wa Nahju al-Balagha). Turathuna, Na. 29 (1412 H), uk. 24–50.
  • Tabataba'i, Sayyid Abd-al-Aziz. «بازمانده‌های نسخه‌های خطی نهج البلاغه» (Nakala zilizosalia za maandishi ya mkono za Nahju al-Balagha). Turathuna, Na. 7–8 (1406 H), uk. 15–35.
  • Wataalamu. Pazhouheshi dar Nahju al-Balagha. Tehran: Bonyad-e Nahju al-Balagha, 2022 M.
  • Yafei, Abdullah ibn As'ad. Mira'at al-Jinan wa Ibrat al-Yaqzan. Beirut: Dar al-Kutub al-Ilmiyyah, 1417 H.
  • Yaqubi, Ahmad ibn Ishaq. Mushakalat al-Nas li-Zamanihim. Beirut: Dar al-Kitab al-Jadid, 1980 M.
  • «بندی از شرح نهج البلاغه ابن ابی‌الحدید» (Sehemu kutoka Sharhu Nahju al-Balagha ya Ibn Abi al-Hadid). Maktaba na Makumbusho ya Kitaifa ya Malek. Tarehe ya kuchapishwa: 10 Aprili 2021. Tarehe ya kutembelewa: 25 Agosti 2026.
  • «نهج البلاغه از نگاه آنتوان بارا نویسنده مسیحی» (Nahju al-Balagha kwa mtazamo wa Antoine Bara, mwandishi Mkristo). Ahlolbait. Tarehe ya kuchapishwa: 10 Desemba 2017. Tarehe ya kutembelewa: 25 Agosti 2026.
  • «اظهارات خواندنی جوان اروپایی که شیعه شد» (Kauli za kuvutia za kijana wa Ulaya aliyekuwa Shia). Estebsar. Tarehe ya kutembelewa: 25 Agosti 2026.
  • «صفارزاده نهج البلاغه را به سه زبان ترجمه کرد» (Saffarzadeh alitafsiri Nahju al-Balagha katika lugha tatu). Hawzah. Tarehe ya kuchapishwa: 27 Agosti 2008. Tarehe ya kutembelewa: 25 Agosti 2026.
  • «تفسیر سوره جمعه جلسه ۱۰» (Tafsiri ya Sura ya Ijumaa, kipindi cha 10). Tovuti Rasmi ya Ayatullah Jawadi Amuli. Tarehe ya kuchapishwa: 16 Aprili 2018. Tarehe ya kutembelewa: 25 Agosti 2026.
  • «سایت پژوهشنامه نهج البلاغه» (Tovuti ya Jarida la Utafiti la Nahju al-Balagha). Chuo Kikuu cha Bu-Ali Sina. Tarehe ya kutembelewa: 25 Agosti 2026.
  • «مسلمان‌شدن ۸۰ سرخپوست با نهج البلاغه» (Wahindi Wekundu 80 walisilimu kupitia Nahju al-Balagha). Saheb News. Tarehe ya kuchapishwa: 8 Septemba 2014. Tarehe ya kutembelewa: 25 Agosti 2026.
  • «مسلمان‌شدن پروفسور لگنهاوزن با مطالعه نهج البلاغه» (Profesa Muhammad Legenhausen alisilimu kwa kusoma Nahju al-Balagha). Aparat. Tarehe ya kutembelewa: 25 Agosti 2026.
  • «ماجرای مسلمان‌شدن یک آمریکایی به برکت نهج البلاغه» (Kisa cha kusilimu kwa Mmarekani kwa baraka ya Nahju al-Balagha). Hawzah News Agency. Tarehe ya kuchapishwa: 8 Aprili 2012. Tarehe ya kutembelewa: 25 Agosti 2026.
  • «آشنایی با مشاهیر و نخبگان فرهنگی پاکستان» (Utambulisho wa watu mashuhuri na wasomi wa utamaduni wa Pakistan). IRNA. Tarehe ya kuchapishwa: 10 Februari 2010. Tarehe ya kutembelewa: 25 Agosti 2026.
  • «پدر و مادرم از طریق نهج البلاغه مسلمان شدند» (Wazazi wangu walisilimu kupitia Nahju al-Balagha). ISNA. Tarehe ya kuchapishwa: 20 Oktoba 2014. Tarehe ya kutembelewa: 25 Agosti 2026.
  • «پروفسور محمد لگنهاوزن چگونه مسلمان و شیعه شد؟» (Profesa Muhammad Legenhausen alisilimu na kuwa Shia vipi?). YouTube. Tarehe ya kutembelewa: 25 Agosti 2026.