Bibi Zainab (s.a)
| Jukumu | Mfikisha ujumbe wa Tukio la Karbala na Msimamizi wa Mateka wa Karbala |
|---|---|
| Kunia | Umm Kulthum na Umm al-Hassan |
| Tarehe ya kuzaliwa | 5 Jumada al-Awwal, Mwaka 5 Hijria au 6 Hijria |
| Mahali pa kuzaliwa | Madina |
| Kufariki | 15 Rajab, Mwaka 62 Hijria |
| Mahali pa kuzikwa | Damascus / Cairo (Kuna hitilafu) |
| Makazi | Madina |
| Lakabu | Zainab al-Kubra, Aqilatu Bani Hashim, Aalimatu Ghairu Muallima, Ummu al-Masaib, Kamila, Fadhila n.k. |
| Baba | Imamu Ali (a.s) |
| Mama | Bibi Fatima al-Zahra (s.a) |
| Mume | Abdullah bin Jafar |
| Watoto | Awn, Muhammad, Ali, Abbas, Umm Kulthum |
| Umri | Miaka 57 (kwa mujibu wa kauli mashuhuri) |
| Wazawa wa Imamu Mashuhuri | |
| Abbas bin Ali • Zainab Kubra • Fatima Masuma • Sayyid Muhammad • Ahmad bin Musa • Sayyida Nafisa Wazawa wengine wa Imamu | |
Bibi Zainab (a.s) (5 au 6 H – 62 H): ni binti wa Imamu Ali (a.s) na Bibi Fatima al-Zahra (a.s), ni shujaa na mbeba bendera ya harakati za Karbala baada ya kuuawa shahidi kaka yake, Imamu Hussein (a.s), na ndiye aliyekuwa kiongozi na msimamizi mkuu wa Mateka wa Karbala. Tukio la Karbala linahesabiwa kuwa ndio wasifu mkuu na tukio zito zaidi katika maisha ya Bibi Zainab (a.s). Baada ya mapambano ya Siku ya Ashura, yeye pamoja na watu wengine wa nyumba ya Mtume walichukuliwa mateka hadi katika mji wa Kufa na kisha kupelekwa Sham (Damascus). Usimamizi wa mateka waliosalia, kumlinda na kumhifadhi Imamu Sajjad (a.s), na kufikisha ujumbe wa Mashahidi wa Karbala kwa ulimwengu ndizo nguzo kuu tatu za risala ya Bibi Zainab baada ya Ashura. Hutuba yake mjini Kufa na Hutuba yake katika baraza la Yazid huko Sham, sambamba na kubainisha adhama na kudhulumiwa kwa Ahlul-Bayt (a.s), zilifichua ukatili na maovu ya watawala wa Bani Umayya kama vile Ubaidullahi bin Ziad na Yazid bin Muawia, jambo lililomlazimisha Yazid kuomba radhi kwa fedheha iliyomkuta yeye na wafuasi wake. Watoto wawili wa kiume wa Bibi Zainab, Awn na Muhammad, waliuawa shahidi katika medani ya Karbala.
Bibi Zainab (a.s) alipewa lakabu ya Ummu al-Masaa'ib (Mama wa Misiba) kutokana na majonzi mazito na machungu mazito aliyoyashuhudia maishani mwake. Aqiilatu Bani Hashim na Aalimatu Ghairu Muallamah ni miongoni mwa lakabu nyengine mashuhuri za bibi Zainab. Wanazuoni wa Kishia wanamsifu bibi huyu kwa sifa na fadhila mbalimbali tukufu; ikiwa ni pamoja na elimu na ufaqihi (welewa) mpana, ushujaa, ufasaha unaofanana na wa Imamu Ali (a.s), msimamo thabiti katika Ibada unaofanana na wa mama yake Bibi Fatima (a.s), pamoja na kusifika kwake kwa sifa ya kuwa yeye ndiye mfano halisi wa Sabrun Jamiil (subira njema). Baadhi ya wanazuoni wa Kishia, kwa kuzingatia daraja yake ya kiroho, wanaamini kuwa bibi huyu ni mwenye daraja ya utakaso na kinga dhidi ya madhambi (Isma).
Kwa mujibu wa rai mashuhuri, Bibi Zainab (a.s) alifariki dunia mnamo tarehe 15 Rajabu mwaka 62 H. Ila kuna maoni tofauti kuhusiana na mahali alipozikwa. Mtazamo maarufu zaidi ni ule unaoeleza kuwa kaburi lake lipo katika Haramu ya Bibi Zainab iliyopo mjini Dameski, huku wengine wakiitaja Makamu ya Bibi Zainab mjini Kairo na wengine wakiamini kuwa kaburi lake lipo kwenye Mava ya Baqii iliyopo mjini Madina.
Bibi Zainab (a.s) ana nafasi na hadhi tukufu katika utamaduni na fasihi ya Kishia. Waislamu wa Shia huadhimisha kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa na kufariki kwake, huwapa binti zao jina lake na huandaa makongamano mbalimbali kwa ajili ya kumuenzi. Nchini Iran, siku ya kuzaliwa kwake imetangazwa kuwa Siku ya Wauguzi. Kadhalika, vitabu vingi vimechapishwa katika lugha mbalimbali vikielezea maisha, shakhsia na fadhila za Bibi Zainab. Zaidi ya vitabu 334 vimetambulishwa katika lugha kama vile Kiarabu, Kiajemi, Kiurdu na Kiingereza vinavyomhusu Bibi Zainab, miongoni mwavyo vikiwa ni kitabu cha al-Khasa'is al-Zaynabiyyah kilichoandikwa na Sayyid Nuruddin al-Jaza'iri.
Kuzaliwa, Jina, Lakabu na Kunia
Bibi Zainab ni binti mkubwa wa Imamu Ali (a.s) na Bibi Fatima al-Zahra (a.s),[1] naye ni dada wa Imamu Hassan (a.s), Imamu Hussein (a.s),[2] na Ummu Kulthum.[3] Kuna hitilafu za mapokezi kuhusu tarehe halisi ya kuzaliwa kwa bibi huyu. Baadhi ya vyanzo vinaitaja tarehe 5 Jamadu al-Ula[4] ya mwaka wa 5 H,[5] na vingine vikiutaja mwaka wa 6 H.[6] Ila hakuna khitilafu kwamba yeye alizaliwa katika mji wa Madina. Baadhi ya mapokezi yameeleza kuwa alizaliwa miaka mitano kabla ya kufariki kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w).[7] Pia miongoni mwa miaka inayohusishwa na tukio hili ni mwaka wa 4 au 9 Hijiria, habari ambazo zinapatikana katika baadhi ya marejeo machache tu.[8] Imeelezwa kwamba, hakuna hata moja kati ya tarehe hizi zilizotajwa zenye ithibati madhubuti katika vyanzo vya historia.[9]
Jina la Bibi Zainab liliteuliwa moja kwa moja na bwana Mtume (s.a.w.w). Imeelezwa kuwa Malaika Jibril alimteremshia Mtume (s.a.w.w) jina hilo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.[10] Katika kitabu cha al-Khasa'isu al-Zainabiyyah imeelezwa kuwa, Mtume (s.a.w.w) alimbusu mjukuu wake huyo na kusema: "Wale waliohudhuria katika watu wa umma wangu na kulishuhudia tukio hili, basi wawajulishe juu ya utukufu wa binti huyu Zainab, wale ambao hawakuhudhuria katika tukio hili; kwani hakika yeye anafanana kabisa na bibi yake Khadija al-Kubra."[11] Kiusanifu wa lugha, neno "Zainab" lina maana ya "mti wenye muonekano mzuri na harufu ya kupendeza"[12] na pia lina maana ya "pambo la baba yake".[13]
Miongoni mwa kunia za Bibi Zainab (a.s) zilizotajwa katika vitabu mbalimbali ni pamoja na: Ummu Kulthum na Ummu al-Hassan.[14] Aidha alipewa lakabu ya "Zainab al-Kubra" Ili kumtofautisha na dada zake wenye jina kama hilo. Pia aliitwa "Siddiqatu al-Sughra" kwa ajili ya kutofautisha cheo chake na cha mama yake (Fatima) aliyepewa cheo cha "Siddiqatu al-Kubra".[15] Kuna lakabu nyingi zilizoripotiwa katika kumsifu bibi huyu.[16] Baadhi ya waandishi wameorodhesha zaidi ya lakabu sitini,[17] miongoni mwazo ni: Aqiilatu Bani Hashim, Aalimatu Ghairu Muallamah, Fahiimatu Ghayru Mufahhamah, [Maelezo 1] al-Arifah, al-Muwaththaqah, al-Faadhilah, al-Kaamilah, Aabidatu Aali Ali, Siddiqatu al-Sughra, Maasumatu al-Sughra, Aminatullah, Naa'ibatu al-Zahra, Naa'ibat al-Hussein, Aqiilat al-Nisa, Sharikatu al-Shuhada, al-Balighatu, al-Fasihatu, Sharikatu al-Hussein, na Mahbubatu al-Mustafa.[18]
Bibi Zainab alipewa lakabu ya Ummu al-Masa'ib kutokana na misiba mizito aliyoshuhudia tangu utotoni mwake. Miongoni mwa misiba iliyomkabili bibi huyu ni pamoja na: kufariki kwa babu yake Mtume (s.a.w.w), maradhi na kuuawa shahidi mama yake Bibi Fatima (a.s), kuuawa shahidi baba yake Amirul-Mu'minina (a.s), kuuawa shahidi kwa sumu kaka yake Imamu Hassan (a.s), na kilele cha misiba hii ni lile Tukio la Karbala na kupelekwa mateka katika miji ya Kufa na Sham.[19]
Mume na Watoto
Kulingana na vyanzo vya kihistoria, licha ya bibi Zainab (a.s) kuposwa na watu kadhaa mashuhuri, hatimaye alikubali kuolewa na mtoto wa ami yake, Abdullah bin Jafar.[21] Hakuna habari kamili kuhusiana na ndoa yao,[22] na wala hakuna kitabu cha historia kilichotoa habari au kufafanua tukio hilo.[23] Asma binti Umais, ambaye ni mama wa Abdullah, aliolewa na Imamu Ali (a.s), tukio lililojiri baada ya kifo cha Jafar, na hivyo Abdullah akawa ni rabiba (mwana wa kambo) aliyelelewa nyumbani kwa Imamu Ali (a.s).[24] Katika baadhi ya mapokeo imeelezwa kuwa, miongoni mwa masharti ya Bibi Zainab katika ndoa yake, ni kwamba kila mara ambapo Imamu Hussein (a.s) atasafiri, basi yeye naye awe huru kuandamana naye, na wala Abdullahi asiwe na haki ya kumzuia katika maamuzi hayo.[25]
Kuna idadi ya watoto wanne wa kiume walioitajwa kuwa ni wana wa bibi Zainab, nao ni; Ali, Awn al-Akbar, Abbas, Muhammad. Ama kwa upande wa watoto wa kike, Ummu Kulthum ndiye aliyetajwa kuwa ni watoto wa Bibi Zainab na Abdullah.[26] Fadhl bin Hassan Tabarsi ametaja watoto watatu wa kiume na binti mmoja, katika kitabu chake kiitwacho I'ilam al-Wara bi A'alam al-Huda, naye hakuashiria wala kutaja jina la mtoto yeyote yule aitwaye Abbas kitabuni humo.[27] Watoto wawili wa Bibi Zainab, ambao ni Awn[28] na Muhammad[29] waliuawa shahidi katika Tukio la Karbala. Sibtu ibn al-Jawzi katika kitabu chake cha Tadhkirat al-Khawass, amemhesabu Awn al-Asghar kuwa ni miongoni mwa Mashahidi wa Karbala. Aidha alimtaja Jumana binti al-Musayyab, akisema kuwa bibi huyu ndiye mama halisi wa mhanga huyu.[30] Katika Maqatil al-Talibiyyin, Khausaa binti Hafsa ametajwa kama ndiye mama hasa wa Muhammad.[31] Baadhi ya vyanzo vinasema kwamba, Awn ndiye mtoto pekee wa bibi Zainab aliyekufa shahidi pamoja na Mashahidi wa Karbala.[32]
Muawia bin Abi Sufian alitaka kumposa Ummu Kulthum, binti wa Bibi Zainab, kwa ajili ya mwanawe Yazid, ila Imamu Hussein (a.s) aliamua kumuoza mtoto wa ami yake aitwaye Qasim bin Muhammad bin Jafar bin Abi Talib.[33] Tawi la vizazi vya mwana wa Ali limepewa jina la "al-Zainabiyyun".[34]
Sifa na Fadhila
Kuna sifa na fadhila nyingi zilizotajwa kumhusu Bibi Zainab (a.s): Abdullah Mamaqani katika kitabu cha Tanqih al-Maqal ameandika kwa mfumo wa mshangao akisema: "Ni nani Zainab? Na nini kitakachokujulisha nani Zainab? Yeye ndiye Aqiilatu Bani Hashim." Kwa mtazamo wake, baada ya mama yake Bibi Fatima al-Zahra (a.s), hakuna mwanamke mwengine yeyote yule aliyefikia ukamilifu wa tabia njema kama yeye.[35] Wanazuoni kama vile Baqir Sharif Qurashi[36] na Sayyid Nuruddin Jaza'iri[37] wamebainisha wakisema kuwa, Bibi Zainab alikusanya sifa zote njema na ukamilifu, kiasi ya kwamba maneno hushindwa kumwelezea kikamilifu bibi huyu muadhamu.[38] Miongoni mwa sifa za mtukufu huyu ni kama ifuatavyo:
Elimu na Ufaqihi
Hutuba na maneno ya Bibi Zainab (a.s) mjini Kufa na mbele ya baraza la Yazid yaliyotegemea hoja thabiti kutoka kwenye Aya za Qur'ani ni moja kati ya hoja muhimu zinazothibitisha elimu yake ya kina.[39] Katika kitabu cha Mausu'atu Tabaqaat al-Fuqahaa, Bibi Zainab amehesabiwa kuwa ni miongoni mwa mafaqihi wakubwa wa karne ya kwanza Hijiria.[40] Yeye ni miongoni mwa wasimulizi na wapokezi wa Hadithi, aliyekuwa akinukuu kutoka kwa baba yake (Imamu Ali (a.s)) na mama yake Bibi Fatima (a.s).[41] Kwa mujibu wa maelezo ya kitabu cha Maqatil al-Talibiyyin, sahaba maarufu Abdullah bin Abbas alipokuwa akinukuu Hutuba ya Bibi Fatima kuhusu Fadak, aliyoipokea kutoka kwa Bibi Zainab alisema: "Ametusimulia mwena hekima wetu, Zainab binti Ali (a.s)."[42] Kadhalika Imamu Sajjad (a.s), na wanahadithi wengine akiwemo Jabir bin Abdullah al-Ansari,[43] Muhammad bin Amr, Ataa bin Saa'ib, na Fatima binti Imamu Hussein[44] walikuwa ni miongoni mwa wapokezi waliopokea Hadithi kutoka kwake.
Wakati wa uwepo wa Imam Ali (a.s.) mjini Kufa, Bibi Zaynab aliendesha darsa za tafsiri ya Qur'ani mahususi kwa ajili ya wanawake wa mji huo.[46] Kadhalika, imepokewa kwamba alikuwa kimbilio na tegemeo kuu la watu katika kubainisha masuala ya halali na haramu.[47] Na baadhi ya wanazuoni wanamthibitisha kuwa alikuwa mwenye elimu ya laduni.[48]
Fasaha ya Usemi (Hutuba)
Uwezo wa kusema wa Bibi Zainab ulifananishwa na wa Imamu Ali (a.s), kiasi kwamba wakati akihutubia ilionekana kana kwamba Amirul-Mu'minina mwenyewe ndiye aliyekuwa akizungumza katika hutuba ile.[49] Tabarsi katika kitabu cha al-Ihtijaj anasimulia kwamba siku msafara wa mateka ulipoingia Kufa, Imamu Sajjad (a.s) akiwa mgonjwa alikuwa akiwaasa watu waliokuwa wakilia, kisha Bibi Zainab akawaashiria watu wanyamaze. Msimulizi anasema pumzi zilizuiwa vifuani na hata sauti za kengele za wanyama zilikata. Kisha akaanza kuhutubia kwa maneno yaliyotikisa mji mzima.[50]
Ibada
Bibi Zainab alifananishwa na mama yake Bibi Fatima (a.s) katika ibada.[51] Imeelezwa kuwa ilikuwa ni kawaida yake kukesha kwa ajili ya kusali na kusoma Qur'ani maishani mwake mwote bila kuacha; hata katika usiku wa kumi na moja wa mwezi wa Muharram (usiku wa baada ya tukio la Ashura), pamoja na machungu yote yaliyomkuta, ila bado hakuacha kusali sala zake za usiku.[52] Fatima binti wa Imamu Hussein (a.s) anasema: "Shangazi yangu Zainab usiku kucha wa kuamkia Ashura alisimama kwenye mihrabu yake akimwomba na kumlilia Mola wake Mlezi."[53] Pia Imamu Sajjad (a.s) ameeleza akisema kuwa, licha ya ugumu wa safari ya mateka kuelekea Sham, sala ya usiku ya Bibi Zainab haikuachwa kusaliwa hata mara moja.[54] Imepokewa kuwa pale Imamu Hussein (a.s) alipokuwa akiagana naye kwa mara ya mwisho katika Siku ya Ashura, alimwambia: "Dada yangu, usinisahau katika sala yako ya usiku."[55] Kutokana na wingi wa ibada zake, alipewa lakabu ya "al-Abidah" (Mwenye Kufanya Ibada Nyingi).[56]
Hijabu na Staha
Kuhusu heshima ya hijabu na staha ya Bibi Zainab, Abdullah Mamaqani anasema kuwa, kabla ya tukio la Karbala hakukuwa na mwanamume hata mmoja aliyewahi kuuona mwili wala kivuli chake.[57] Imepokewa kutoka kwa Yahya al-Mazani, mmoja wa masahaba wa Imamu Hussein (a.s), akisema kuwa, ingawa yeye alikuwa ni jirani wa nyumba ya Imamu Ali (a.s) mjini Madina kwa muda mrefu, lakini kamwe hakuwahi kumwona Bibi Zainab, wala hata kuisikia sauti yake. Na pale alipokuwa akitoka usiku kwenda kuzuru kaburi la babu yake Mtume (s.a.w.w), Imamu Ali pamoja na Hassani na Husseini walikuwa wakitembea pembeni yake, ili asionekane na mtu yeyote asiyestahiki kumuona.[58]
Subira na Uvumilivu
Bibi Zainab anatambuliwa kama nguzo na kielelezo kikuu cha subira njema (Sabrun Jamil)[59] [Maelezo 2].[60] Kusimama kidete katika kulinda misingi ya dini, kujizuia wakati wa majaribio, kutodhihirisha udhaifu mbele ya adui, na kutotoa malalamiko mbele ya watu ndizo sifa kuu za uvumilivu wake.[61] Siku ya Ashura, pale aliposimama mbele ya mwili wa kaka yake uliojaa damu, alisema: "Ee Mola wetu Mlezi! Pokea dhabihu hii kutoka kwetu (Watu wa Nyumba ya Mtume)."[62] Kadhalika alipojibu dhihaka ya Ibn Ziad aliyemuuliza ameonaje kile Mungu alichowafanyia watu wa nyumba yake, alisema: «مَا رَأَیْتُ إلّا جَمِیلاً» (Sikuona chochote isipokuwa uzuri mtupu).[63]
Isma (Kinga ya Madhambi)
Baadhi ya wanazuoni kama vile Abdullahi Mamaqani[64] na Jafar al-Naqdi[65] kwa kuzingatia fadhila na hadhi yake kubwa ya kiroho, wanaamini kuwa bibi huyu ni mwenye daraja ya Isma (kinga dhidi ya madhambi). Sayyid Nuruddin Jaza'iri ameeleza akisema kuwa, bibi huyu alikuwa na daraja ya Isma Ndogo (al-Ismah al-Sughra).[66]
Kuandamana na Imamu Hussein (a.s) katika Tukio la Karbala na Uelimishaji Baada Yake
Tukio la Karbala ndilo tukio kubwa zaidi katika maisha ya Bibi Zainab (a.s).[67] Bibi Zainab alisimama na kaka yake (Imamu Hussein (a.s)) hadi wakati wa kuuawa kwake shahidi, na baada ya hapo aliwaongoza mateka kuelekea Kufa na hatimaye wakafika Sham.[68] Imeelezwa kwamba haijulikani wazi iwapo Bibi Zainab alifuatana na kaka yake tangu Madina au alijiunga naye baadaye. Kadhalika, namna Bibi Zainab alivyoondoka Madina kuelekea Makka haikutajwa katika vyanzo vya historia.[69] Ni wazi kwamba pale Imamu Hussein alipotoka Makka kuelekea Iraq, Bibi Zainab alikuwa pamoja naye.[70]
Kutokana na msimamo wake dhabiti mbele ya maadui, kufichua jinai za watawala na kutangaza hali ya kudhulumiwa kwa haki ya Ahlu al-Bait (a.s), Bibi Zainab anatambuliwa kama mbeba bendera ya mapinduzi ya Karbala.[71] Hutuba na miongozo yake ndiyo siri iliyobakiza ujumbe wa Ashura kuwa hai na kuamsha fahamu za umma.[72] Majukumu makuu matatu ya Bibi Zainab baada ya Ashura yameelezwa kuwa ni: Usimamizi wa mateka, ulinzi wa maisha ya Imamu Sajjad (a.s), na kufikisha ujumbe wa mashahidi wa Karbala kwa umma mzima.[73]
Huko Karbala
Sheikh al-Mufidu ananukuu kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s) kwamba usiku wa kuamkia Ashura, Bibi Zainab alikuwa akimuuguza wakati Imamu Hussein (a.s) alipokwenda hemani kwake na kusoma beti za kueleza kutokuwa na uaminifu kwa dunia. Imamu Sajjad anasema shangazi yake aliposikia maneno hayo alipatwa na huzuni nzito, lakini Imamu Hussein alimpa mawaidha ya subira na kumwambia: "Dada yangu, fahamu kwamba viumbe wote wa mbinguni na ardhini watakufa na hakuna kitakachobaki isipokuwa Mwenyezi Mungu pekee... Baba yangu, mama yangu na kaka yangu walikuwa bora kuliko mimi [na wote wameondoka duniani]..." Kisha alimtaka kuwa mtulivu na asifanye mambo yasiyofaa kisheria baada ya kufariki kwake.[75]
Alasiri ya Ashura, wakati jeshi la adui lilipomzingira Imamu Hussein (a.s), Bibi Zainab alitoka hemani na kumwambia Umar bin Sa'd: "Ewe mwana wa Sa'd! Je, Aba Abdillah (Imamu Hussein) anauawa nawe unatazama tu?!» Ibn Sa'd hakujibu chochote. Kisha Bibi Zainab akapaza sauti: "Je, hakuna Mwislamu hata mmoja miongoni mwenu?!» Lakini hakuna aliyemjibu.[76] Kulingana na vyanzo vingine, baada ya kuuawa shahidi Imamu Hussein, Bibi Zainab alisimama kando ya mwili wake na kusema: "Ee Mwenyezi Mungu, takabali dhabihu hii kutoka kwetu."[77] Kadhalika aligeukia upande wa Madina na kumlilia Mtume (s.a.w.w) akieleza masahibu ya familia yake, jambo lililowafanya marafiki na maadui wote kulia kwa pamoja.[78]
Watoto wawili wa kiume wa Bibi Zainab waliuawa shahidi Siku ya Ashura.[79] Sayyid Muhammad Kazim Qazwini anaeleza kuwa katika vitabu vya maombolezo hakuna masimulizi yanayoonyesha Bibi Zainab akilalamika au kupiga kelele kwa ajili ya watoto wake; kwani huzuni yake yote ilikuwa imemwelekea kaka yake Imamu Hussein (a.s).[80]
Huko Kufa
Baada ya mapambano, mateka walipelekwa Kufa.[81] Uongozi wa msafara ulikuwa mikononi mwa Bibi Zainab (a.s).[82] Wakati wa kuingia Kufa, alitoa Hutuba iliyowashangaza na kuwatia unyonge wote waliosikiliza.[83] Hidhyam bin Sharik al-Asadi anasema: "Wallahi sikuwahi kumwona mwanamke mfasaha wa maneno kama yeye; ilikuwa kana kwamba anazungumza kupitia ulimi wa Amirul-Mu'minina Ali (a.s). Alipowapigia kelele watu wawe kimya, halaiki yote ilinyamaza kimya kiasi kwamba hata milio ya kengele za ngamia haikusikika tena."[84] Mwishoni mwa Hutuba hiyo, kutokana na hofu ya wananchi kuasi dhidi ya utawala, kamanda wa kijeshi aliwapeleka mateka katika jumba la utawala (Dar al-Imarah) la Ubaidullahi bin Ziad.[85]
Kwa mujibu wa Sheikh al-Mufidu, Ibn Ziad aliweka kichwa cha Imamu Hussein mbele yake na kukipiga kwa kijiti. Bibi Zainab aliingia akiwa amejifunika na akasimama kishujaa kujadiliana na Ibn Ziad na kuzuia nia ya kumwua Imamu Sajjad (a.s) kwa kumwambia Ibn Ziad kuwa ikiwa anataka kumwua basi amwue yeye kwanza pamoja naye.[86]
Huko Sham
Baada ya hapo, Yazid bin Muawia alimtaka Ibn Ziad apeleke mateka pamoja na vichwa vya mashahidi huko Sham.[88] Kutokana na propaganda chafu za Bani Umayya dhidi ya kizazi cha Imamu Ali (a.s) huko Sham na kwa ajili ya kuimarisha utawala wa Yazid, wakati mateka walipoingia Sham, wananchi walivalia nguo mpya, wakapamba mji na kuanza kusherehekea kwa furaha;[89] Hata hivyo, Hutuba za Bibi Zainab na Imamu Sajjad (a.s) zilibadilisha kabisa mazingira ya Sham; chuki ya wananchi kwa Ahlul-Bayt iligeuka kuwa upendo, na hasira kali ikaelekezwa dhidi ya Yazid, jambo lililomfanya aone kuwa mauaji hayo yalizitingisha nguzo za utawala wake.[90]
Katika baraza lililohudhuriwa na wakuu wa serikali,[91] mbele ya watu wa familia ya Imamu Hussein waliokuwa wamesimama mbele yake kama mateka, Yazid alisoma mashairi ya kukufuru na yenye matusi, akazungumza maneno kuhusu ushindi wake na kuzifasiri aya za Qur'ani kwa manufaa yake mwenyewe,[92] na akaonyesha utovu wa adabu dhidi ya kichwa kitukufu cha Imamu Hussein (a.s).[93] Hapo ndipo Bibi Zainab aliposimama na kutoa Hutuba maarufu[94] iliyomfedhehesha na kumuumbua Yazid mbele ya viongozi hao.[95] Katika hutuba hiyo, alimdhalilisha, akamkemea na kumuumbua Yazid mbele ya wakuu na viongozi wa Sham, akalaani jinai zake, na hivyo akaweka mazingira ya kuamsha fahamu za wananchi na kutikisa nguzo za utawala wa Yazid.[96]
Kutokana na msimamo huu thabiti, furaha ya ushindi ya Bani Umayya ilitoweka,[97] na Yazid akalazimika kuomba radhi na kutupa lawama kwa Ibn Ziad.[98] Kisha Yazid akakubali ombi la Bibi Zainab na mateka la kufanya vikao vya maombolezo mjini Sham.[99]
Kufariki na Mahali pa Mazishi
Inaelezwa kwamba kuhusu wakati, mahali na namna ya kufariki kwa Bibi Zainab (a.s), hakuna taarifa za kina katika vyanzo vya kihistoria hadi kufikia karne ya nane Hijiria, na taarifa zilizopo zinaishia tu pale msafara wa mateka ulipowasili mjini Madina.[100] Pamoja na hayo, kufariki kwa Bibi Zainab (a.s) usiku wa Jumapili, tarehe 15 Rajabu mwaka 62 H ndio mtazamo mashuhuri zaidi.[101] Tarehe ya 14 Rajabu[102] na mwaka 65 H[103] pia zimetajwa.
Kuhusu eneo la kaburi lake kuna maoni makuu:
- Sham: Huu ndio mtazamo maarufu zaidi.[104] Eneo la haramu yake liko kusini mwa Dameski na panajulikana kama "Mji wa al-Sayyidah Zainab".[105]
- Misri: Baadhi ya wanahistoria wametaja kaburi lake kuwa lipo nchini Misri.[106] Eneo hili linajulikana kama Makamu ya Bibi Zainab mjini Kairo.[107] Sayyid Muhammad Kazim Qazwini katika kitabu cha Zainab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd, ameitaja rai hii kuwa ndiyo yenye uwezekano mkubwa zaidi.[108]
- Madina: Sayyid Muhsin al-Amin ameonelea kuwa alizikwa katika makaburi ya Baqi' mjini Madina.[109]
- Katika mji wa Sinjar kaskazini mwa Iraq kuna eneo linalonasibishwa naye na wananchi wa hapo.[110] Bila shaka, watafiti wanaona kuwa kuzikwa kwa Bibi Zainab katika eneo hili hakuna uthibitisho wowote wa kihistoria.[111]
Muhammad Jawad Mughniyyah katika kitabu chake cha al-Husayn wa Batalatu Karbala, kwa kupinga rai ya tatu, ameeleza kuwa kwa vile wanazuoni wanaoaminika kama vile al-Kulayni, Sheikh al-Saduq, Sheikh al-Mufid na Sheikh al-Tusi hawakubainisha mahali alipozikwa Bibi Zainab, basi haiwezekani kupendelea rai yoyote kati ya hizo tatu juu ya nyengine. Kadhalika, umaarufu wa Sham na Misri unapingana wenyewe kwa wenyewe, na kwa mtazamo huo hakuna mtazamo wenye nguvu zaidi ya mwingine. Kwa hivyo, haiwezekani kuthibitisha kwa uhakika mahali pa kaburi lake; lakini bila shaka yoyote, kuzuru maeneo hayo matakatifu yaliyopo Sham na Misri ni jambo linalofaa na kupendeza kwa ajili ya kuwatukuza Ahlul-Bayt.[112] Katika kitabu cha Maqtal-e Jame'-e Sayyid al-Shuhada, mitazamo yote mitatu imechambuliwa na kukosolewa, na hakuna mtazamo uliopewa uzito juu ya mwingine. Miongoni mwa hoja za ukosoaji huo ni kwamba ingawa Bibi Zainab alikuwa miongoni mwa shakhsia wakubwa na muhimu katika Uislamu, katika vitabu vya zamani vinavyotegemewa hakuna mtajo wowote wa mahali alipozikwa Bibi Zainab huko Sham, Misri wala Madina. Kwa hiyo, hakuna hata eneo moja kati ya haya matatu linaloweza kutajwa kwa yakini kuwa ndio mahali pa kaburi la Bibi Zainab (a.s).[113]
Kuhusu haramu maarufu iliyopo Dameski, imeelezwa pia kwamba jina la mwenye kaburi hilo lilirekodiwa kama Ummu Kulthum hadi kufikia karne ya nane Hijiria; lakini baada ya kipindi hicho, polepole eneo hilo lilianza kunasibishwa na Bibi Zainab al-Kubra.[114]
Eneo la Tal al-Zainabiyyah lililopo karibu na Haramu ya Imamu Hussein (a.s) mjini Karbala ni mahali aliposimama Bibi Zainab Siku ya Ashura kushuhudia medani ya mapambano.[115]
-
Picha ya zamani ya Makamu na msikiti wa Bibi Zainab nchini Misri ya mwaka 1884 M.
-
Haramu ya Bibi Zainab (a.s) kusini mwa Dameski, Syria.
-
Tal al-Zainabiyyah karibu na Haramu ya Imamu Hussein (a.s) huko Karbala.
Mashambulizi ya Makundi ya Kitakfiri Dhidi ya Haramu ya Bibi Zainab mjini Dameski
Kuanzia mwaka 2012 hadi 2015 M, kufuatia mashambulizi ya Makundi ya Kitakfiri kama vile Daesh nchini Syria, kulijiri mashambulizi kadhaa yalifanywa dhidi ya Haramu ya Bibi Zainab (a.s) ambayo yalipelekea uharibifu wa baadhi ya kumbi, kuba na minara, pamoja na kusababisha vifo vya baadhi ya wakazi (watumishi) na wafanya ziara;[116] lakini maeneo yote yaliyoharibiwa yalifanyiwa ukarabati wa kutosha na kurejeshwa katika hali yake ya zamani.[117]
Katika Utamaduni na Fasihi ya Kishia
Bibi Zainab anashikilia hadhi tukufu katika utamaduni na fasihi ya Kishia. Kila mwaka, katika siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa na kufariki kwake (15 Rajabu), mikusanyiko na vikao vya maombolezo hufanyika katika nchi mbalimbali kama vile Syria, Iraq, Uturuki, Misri na Iran.
Kuzaliwa: Waislamu katika mataifa mbalimbali husherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwake.[118] Katika nchi ya Iran, siku ya kuzaliwa kwake imetangazwa kuwa Siku ya Wauguzi kutokana na jinsi alivyomhudumia Imamu Sajjad (a.s) na wagonjwa wengine wakati wa msafara wa mateka.[119]
Kufariki: Waislamu huadhimisha siku ya kufariki kwake tarehe 15 Rajabu kwa kufanya vikao vya Maombolezo katika haramu yake huko Dameski na katika maeneo mengine ya ibada duniani.[120]
Kupewa Majina Watoto: Jina "Zainab" ni miongoni mwa majina yanayopendwa na kutumiwa zaidi na jamii za Kiislamu duniani kote.[121] Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Takwimu ya Uturuki, jina la Zainab limekuwa likiongoza katika orodha ya majina ya watoto wa kike nchini Uturuki tangu mwaka 2000 M.[122] Kadhalika, kwa mujibu wa ripoti za mashirika ya habari kutoka Shirika la Usajili wa Kiraia la Iran, jina la Zainab limekuwa jina la sita kwa umaarufu zaidi nchini Iran katika karne ya kumi na nne ya kalenda ya Hijria ya Shamsia.[123]
Makongamano: Makongamano mengi ya kitaifa na kimataifa yamefanyika kwa lengo la kubainisha nyanja mbalimbali za maisha na uongozi wa Bibi Zainab (a.s).[124] Kwa mfano, mnamo mwaka 1391 Sh, Kongamano la Kitaifa la Bibi Zainab (a.s) lilifanyika katika mji wa Qum,[125] na katika miaka ya 1402 na 1403 Sh Kongamano la Kimataifa la Bibi Zainab lilifanyika katika Chuo Kikuu cha Imam Hossein mjini Tehran.[126]
Ushairi na Fasihi: Washairi wengi wametunga mashairi kumhusu Bibi Zainab (a.s) katika lugha mbalimbali.[128] Baadhi ya mashairi haya yamejikita katika maudhui mbalimbali kama vile sifa, tenzi za maombolezo (marthiya), na uwepo wa Bibi Zainab huko Karbala. Vitabu kama vile Ayeneh-ye Sabr; dar Madayeh va Marasi-ye Hazrat-e Zainab kilichoandaliwa na Mahmoud Shahrokhi na Moshfeq Kashani, na kitabu cha Banou-ye Sabr; Bargozideh-ye She'r-e Mo'aser-e Mazhabi dar Setayesh-e Hazrat-e Zainab (s.a) kilichoandaliwa na Amir Mas'oud Taherian vimekusanya mashairi mbalimbali ya washairi kuhusu Bibi Zainab. Kadhalika, kitabu cha Aftab dar Hejab kilichoandikwa na Sayyid Mehdi Shoja'i,[129] na vitabu vya Banou-ye Qesseh-ye Man na Khoda-Hafez Derakhtan-e Sarv: Dastan-e Zendegi-ye Banu Zainab (s.a) vyote vikiwa ni kazi ya Mojgan Sheykhi[130] ni miongoni mwa kazi za kifasihi za masimulizi na riwaya zinazomhusu Bibi Zainab.
Rejea
- ↑ Ibn al-Athir, Usdu al-Ghaba, Jz. 6, uk. 132; Naqdi, Hayatu al-Sayyidah Zainab, uk. 22.
- ↑ Qurashi, al-Sayyidah Zainab, uk. 29–33.
- ↑ Dakhil, A'alamu al-Nisa, uk. 269.
- ↑ Dakhil, A'alamu al-Nisa, uk. 269; Qazwini, Zainab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd, uk. 31.
- ↑ Dakhil, A'lam al-Nisa, uk. 269; Naqdi, Hayatu al-Sayyidah Zainab, uk. 22; Mughniyyah, al-Hussein wa Batalatu Karbala, uk. 285.
- ↑ Sharaf al-Din, Aqiilatu al-Wahy, uk. 41; Qazwini, Zainab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd, uk. 31.
- ↑ Kahhalah, A'alam al-Nisa, Jz. 2, uk. 91; Hassun, A'alam al-Nisa al-Muuminat, uk. 436.
- ↑ Naqdi, Hayatu al-Sayyidah Zainab, uk. 22.
- ↑ Mahallati, Rayahinu al-Shari'ah, Jz. 3, uk. 33.
- ↑ Naqdi, Hayatu al-Sayyidah Zainab, uk. 21; Qurashi, al-Sayyidah Zainab, uk. 39.
- ↑ Jaza'iri, al-Khasa'isu al-Zainabiyyah, uk. 44.
- ↑ Ibn Mandhur, Lisan al-Arab, Jz. 1, uk. 453, chini ya neno «زنب»; Feiruzabadi, al-Qamus al-Muhit, uk. 95.
- ↑ Feiruzabadi, al-Qamus al-Muhit, uk. 95; Husseini Zabidi, Taju al-Arus, Jz. 2, uk. 60.
- ↑ Qurashi, al-Sayyidah Zainab, uk. 39; Qazwini, Zainab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd, uk. 38.
- ↑ Naqdi, Hayatu al-Sayyidah Zainab, uk. 21.
- ↑ Kwa mfano tazama: Jaza'iri, al-Khasa'isu al-Zainabiyyah, uk. 52–53; Rabbani Khalkhali, Chehreye Derakhshane Aqileye Bani Hashim Zainabe Kubra, uk. 16–19.
- ↑ Tazama: Rabbani Khalkhali, Derakhshane Aqileye Bani Hashim Zainabe Kubra, uk. 16–19.
- ↑ Jaza'iri, al-Khasa'isu al-Zainabiyyah, uk. 52–53; Rabbani Khalkhali, Chehreye Derakhshane Aqileye Bani Hashim Zainabe Kobra, uk. 16–19.
- ↑ Amin, Aayanu al-Shia, Jz. 7, uk. 137.
- ↑ Yaqub Hassan Dhahir, al-Masiratu al-Imam al-Sayyid Musa al-Sadr, Daru Bilal, Jz. 11, uk. 277.
- ↑ Ibn Sa'd, al-Tabaqatu al-Kubra, Jz. 8, uk. 340; Ibn al-Athir, Usdu al-Ghaba, Jz. 6, uk. 133; Tabarsi, I'ilam al-Wara, Jz. 1, uk. 396.
- ↑ Parto na Khamehyar, "Zainab bint Ali bin Abi Talib", uk. 150.
- ↑ Kwa mfano tazama: Ibn Saad, al-Tabaqat al-Kubra, Jz. 8, uk. 340; Ibn al-Athir, Usdu al-Ghaba, Jz. 6, uk. 133; Qurashi, al-Sayyidatu Zainab, uk. 44; Qazwini, Zainab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd, uk. 75–76; Ashur, Mawsuat Zainab al-Kubra, Jz. 1, uk. 34–35.
- ↑ Saffar, al-Mar'atu al-Azhimah, uk. 90.
- ↑ Kwa mfano tazama: Ashur, Mawsuatu Zainab al-Kubra, Jz. 1, uk. 34–35.
- ↑ Kwa mfano tazama: Ibn Saad, al-Tabaqatu al-Kubra, Jz. 8, uk. 340; Ibn al-Athir, Usdu al-Ghaba, Jz. 6, uk. 133; Kahhalah, A'lam al-Nisa, Jz. 2, uk. 92; Dakhil, A'lam al-Nisa, uk. 270; Qurashi, al-Sayyidah Zainab, uk. 48.
- ↑ Tabarsi, I'ilam al-Wara, Jz. 1, uk. 396.
- ↑ Sheikh al-Mufid, al-Irshad, Jz. 2, uk. 125; Abu al-Faraj al-Isfahani, Maqatil al-Talibiyyin, uk. 95; Tabari, Kamil-e Baha'i, uk. 647.
- ↑ Sheikh al-Mufid, al-Irshad, Jz. 2, uk. 125; Tabari, Kamil-e Baha'i, uk. 647.
- ↑ Sibt ibn al-Jawzi, Tadhkirat al-Khawass, uk. 192.
- ↑ Abu al-Faraj al-Isfahani, Maqatil al-Talibiyyin, uk. 95.
- ↑ Qurashi, al-Sayyidah Zainab, uk. 48.
- ↑ Amin, A'yan al-Shi'ah, Jz. 7, uk. 137; Qurashi, al-Sayyidah Zainab, uk. 49–50.
- ↑ Murtadha Zabidi, Taj al-Arus, Jz. 2, uk. 60; Kahhalah, Mu'jam Qaba'il al-Arab, Jz. 2, uk. 493.
- ↑ Mamaqani, Tanqih al-Maqal, Jz. 3, sehemu ya 2, uk. 79.
- ↑ Qurashi, al-Sayyidah Zainab, uk. 51.
- ↑ Jaza'iri, al-Khasa'is al-Zainabiyyah, uk. 51.
- ↑ Jaza'iri, al-Khasa'is al-Zainabiyyah, uk. 51.
- ↑ Tazama: Kahhalah, A'lam al-Nisa, Jz. 2, uk. 92–97.
- ↑ al-Lajnah al-Ilmiyyah fi Mu'assasat al-Imam al-Sadiq, Mawsu'at Tabaqat al-Fuqaha, Jz. 1, uk. 361.
- ↑ Kahhalah, A'lam al-Nisa, Jz. 2, uk. 91; al-Lajnah al-Ilmiyyah fi Mu'assasat al-Imam al-Sadiq, Mawsu'at Tabaqat al-Fuqaha, Jz. 1, uk. 362.
- ↑ Abu al-Faraj al-Isfahani, Maqatil al-Talibiyyin, uk. 95.
- ↑ al-Lajnah al-Ilmiyyah fi Mu'assasat al-Imam al-Sadiq, Mawsu'at Tabaqat al-Fuqaha, Jz. 1, uk. 362.
- ↑ Kahhalah, A'lam al-Nisa, Jz. 2, uk. 92.
- ↑ «بیانات در دیدار پنجاه هزار فرمانده بسیج سراسر کشور». Ofisi ya Kuhifadhi na Kuchapisha Kazi za Ayatollah Sayyid Ali Khamenei.
- ↑ Mahallati, Rayahin al-Shari'ah, 1349 Sh, Jz. 3, uk. 57.
- ↑ al-Lajnah al-Ilmiyyah fi Mu'assasat al-Imam al-Sadiq, Mawsu'at Tabaqat al-Fuqaha, 1418 H, Jz. 1, uk. 362.
- ↑ Jaza'iri, al-Khasa'is al-Zainabiyyah, 1425 H, uk. 67–68.
- ↑ Tabarsi, al-Ihtijaj, 1403 H, Jz. 2, uk. 304; Mamaqani, Tanqih al-Maqal, Jz. 3, sehemu ya 2, uk. 79; Jaza'iri, al-Khasa'is al-Zainabiyyah, 1425 H, uk. 96, 98.
- ↑ Tabarsi, al-Ihtijaj, Jz. 2, uk. 304.
- ↑ Naqdi, Hayat al-Sayyidah Zainab, uk. 74–75.
- ↑ Naqdi, Hayatu al-Sayyida Zainab, uk. 75.
- ↑ Mahallati, Rayahinu al-Shari'ah, Jz. 3, uk. 62.
- ↑ Naqdi, Hayatu al-Sayyidah Zainab, uk. 75; Jaza'iri, al-Khasa'isu al-Zainabiyyah, uk. 105.
- ↑ Jaza'iri, al-Khasa'isu al-Zainabiyyah, uk. 105; Naqdi, Hayat al-Sayyidah Zainab, uk. 75; Mahallati, Rayahinu al-Shari'ah, Jz. 3, uk. 62.
- ↑ Jaza'iri, al-Khasa'isu al-Zainabiyyah, uk. 104–105.
- ↑ Mamaqani, Tanqihu al-Maqal, Jz. 3, sehemu ya 2, uk. 79.
- ↑ Tazama: Naqdi, Hayat al-Sayyidah Zainab, uk. 28.
- ↑ Tazama: Mehdizadeh, «صبر و پایداری حضرت زینب(س)», Tovuti ya Hawzah; «حضرت زینب(س)، نماد صبر جمیل», Shirika la Habari la Hawzah.
- ↑ Muhaddithi, Farhange Ashura, uk. 216.
- ↑ «حضرت زینب(س)، نماد صبر جمیل», Shirika la Habari la Hawzah.
- ↑ Faidhu al-Islam, Khatune Do Sara, uk. 185.
- ↑ Sayyid Ibn Tawus, al-Luhuf, uk. 94; Kharazmi, Maqtal al-Hussein, uk. 47.
- ↑ Mamaqani, Tanqihu al-Maqal, Jz. 3, sehemu ya 2, uk. 79.
- ↑ Naqdi, Hayatu al-Sayyidah Zainab, uk. 75–76.
- ↑ Jaza'iri, al-Khasa'isu al-Zainabiyyah, uk. 57.
- ↑ Qazwini, Zainab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd, uk. 130.
- ↑ Mamaqani, Tanqihu al-Maqal, Jz. 3, sehemu ya 2, uk. 79.
- ↑ Qazwini, Zainab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd, 1424 H, uk. 137–138.
- ↑ Qazwini, Zainab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd, uk. 138.
- ↑ al-Lajnah al-Ilmiyyah fi Mu'assasat al-Imam al-Sadiq, Mawsuatu Tabaqati al-Fuqaha, Jz. 1, uk. 363.
- ↑ Muhaddithi, Farhange Ashura, uk. 216.
- ↑ Muhammadi Ishtehardi, "Zainab Payam-Avare Ashura", uk. 24.
- ↑ Khwarazmi, Maqtal al-Hussein, Jz. 2, uk. 47.
- ↑ Sheikh al-Mufid, al-Irshad, Jz. 2, uk. 93–94.
- ↑ Sheikh al-Mufid, al-Irshad, Jz. 2, uk. 112.
- ↑ Mughniyyah, al-Hussein wa Batalatu Karbala, uk. 433; Faydh al-Islam, Khatun-e Do Sara, uk. 185.
- ↑ Abu Mikhnaf, Waq'at al-Taff, uk. 295; Tabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, Jz. 5, uk. 348–349; Majlisi, Bihar al-Anwar, Jz. 45, uk. 59.
- ↑ Sheikh al-Mufid, al-Irshad, Jz. 2, uk. 125; Tabari, Kamil-e Baha'i, uk. 647.
- ↑ Qazwini, Zainab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd, uk. 201.
- ↑ Tabarsi, al-Ihtijaj, Jz. 2, uk. 109.
- ↑ Parto na Khamehyar, "Zainab bint Ali bin Abi Talib", uk. 152.
- ↑ Tabarsi, al-Ihtijaj, Jz. 2, uk. 109–113.
- ↑ Tabarsi, al-Ihtijaj, Jz. 2, uk. 109–110.
- ↑ Sadeqi Ardestani, Zainab Qahraman Dokhtar-e Ali, uk. 246.
- ↑ Sheikh al-Mufid, al-Irshad, Jz. 2, uk. 115–116.
- ↑ Majlisi, Bihar al-Anwar, Jz. 45, uk. 135.
- ↑ Hashiminejad, Darsi keh Hussein beh Insanha Amukht, uk. 211.
- ↑ Muhammadi Ishtehardi, Hazrat-e Zainab Forugh-e Taban-e Kowsar, 1379 Sh, uk. 327–328; Hashiminejad, Darsi keh Hussein beh Insanha Amukht, 1382 Sh, uk. 211.
- ↑ Hashiminejad, Darsi keh Hussein beh Insanha Amukht, uk. 213.
- ↑ Hashiminejad, Darsi keh Hussein beh Insanha Amukht, uk. 213.
- ↑ Muhammadi Ishtehardi, Hazrat-e Zainab Forugh-e Taban-e Kowsar, 1379 Sh, uk. 248.
- ↑ Tabarsi, al-Ihtijaj, Jz. 2, uk. 307.
- ↑ Majlisi, Bihar al-Anwar, Jz. 45, uk. 133–135.
- ↑ Hashiminejad, Darsi keh Hussein beh Insanha Amukht, uk. 215–216.
- ↑ Hashiminejad, Darsi keh Hussein beh Insanha Amukht, 1382 Sh, uk. 220–222.
- ↑ al-Lajnah al-Ilmiyyah fi Mu'assasat al-Imam al-Sadiq, Mawsu'at Tabaqat al-Fuqaha, Jz. 1, uk. 364.
- ↑ Rasuli Mahallati, Zainab Aqilat Bani Hashim, uk. 107–108.
- ↑ Tabari, Kamil-e Baha'i, uk. 644; Rasuli Mahallati, Zainab Aqilat Bani Hashim, uk. 108.
- ↑ Parto, «Zainab bint Ali bin Abi Talib», uk. 153.
- ↑ Qazwini, Zainab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd, uk. 591; Rasuli Mahallati, Zainab Aqilat Bani Hashim, uk. 112.
- ↑ Qurashi, al-Sayyidah Zainab, uk. 298; Qazwini, Zainab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd, uk. 591.
- ↑ Dakhil, A'lam al-Nisa, uk. 270.
- ↑ Qurashi, al-Sayyidah Zainab, uk. 299.
- ↑ Qurashi, al-Sayyidah Zainab, uk. 299.
- ↑ Shablanji, Nur al-Absar, uk. 377; Qurashi, al-Sayyidah Zainab, uk. 299.
- ↑ Kahhalah, A'lam al-Nisa, Jz. 2, uk. 99.
- ↑ Rezaei Tehrani, Sad Nokteh az Hezaran, 1392 Sh, uk. 259.
- ↑ Amin, A'yan al-Shi'ah, Jz. 7, uk. 140–141.
- ↑ Saffar, al-Mar'ah al-Azhimah, uk. 283.
- ↑ Saffar, al-Mar'ah al-Azhimah, 2000 M, uk. 285.
- ↑ Mughniyyah, al-Husayn wa Batalatu Karbala, 1426 H, uk. 395–397.
- ↑ Kikundi cha Wanahistoria, Tarikh-e Qiyam va Maqtal-e Jame'-e Sayyid al-Shuhada, 1391 Sh, Jz. 2, uk. 596–603.
- ↑ Kikundi cha Wanahistoria, Tarikh-e Qiyam va Maqtal-e Jame'-e Sayyid al-Shuhada, 1391 Sh, Jz. 2, uk. 601–602.
- ↑ Parto na Khamehyar, "Zainab bint Ali bin Abi Talib", uk. 159.
- ↑ «حمله تروریستی به حرم حضرت زینب در سوریه», Shirika la Habari la IRINN; «حمله به حرم حضرت زینب(س)», Tovuti ya Tabnak.
- ↑ «سوریه - تشریح عملیات مرمت و بازسازی آسیبهای وارده به حرم حضرت زینب سلام الله علیها», Tovuti Rasmi ya Ukarabati wa Maeneo Matakatifu.
- ↑ Tazama: «جهان غرق شادی از میلاد حضرت زینب(س)، پرستار کربلا», Shirika la Habari la IMNA; «برگزاری مراسم ولادت حضرت زینب(س) در زنجان», Tovuti ya Moje Rasa.
- ↑ Pouya, Zist-e Ma'sumaneh, uk. 336; «علت نامگذاری روز میلاد حضرت زینب(س) به روز پرستار», Tovuti ya Hawzah.
- ↑ Tazama: «عکس/ زائران کشورهای مختلف در مرقد حضرت زینب(س)», Mashregh News Agency; «امروز مراسم عزاداری حضرت زینب(س) در سوئد و هلند برگزار میشود», Shirika la Habari la Hawzah; «عزاداری سالروز وفات حضرت زینب(س) در کربلا», Tovuti ya Kimataifa ya Atabe News.
- ↑ Tazama: «معنی اسم زینب و نامهای هم آوا با آن + میزان فراوانی در ثبت احوال», Tovuti ya Rasekhoon.
- ↑ «زینب محبوبترین نام دختران ترکیه», Tovuti ya Entekhab.
- ↑ Tazama: «فهرست ۵۰ نام پرطرفدار در میان دختران ایران در یک قرن اخیر», Tovuti ya Shoar-e Sal; «فهرست ۵۰ نام پرطرفدار در میان دختران ایران در یک قرن اخیر», Shirika la Habari la ANA.
- ↑ Tazama: «همایش حضرت زینب(س) در حرم امام حسین(ع) برگزار شد», Shirika la Habari la Hawzah; «همایش رهروان حضرت زینب(س) در اردبیل», Shirika la Habari la IRIB; «همایش حضرت زینب الگوی ایستادگی در بوشهر برگزار شد», Shirika la Habari la Defa Press; «کنگره ملی حضرت زینب(س) در قم به کار خود پایان داد», Shirika la Habari la Jamhuri ya Kiislamu (IRNA).
- ↑ «کنگره ملی حضرت زینب(س) در قم به کار خود پایان داد», Shirika la Habari la Jamhuri ya Kiislamu (IRNA).
- ↑ «دومین همایش بینالمللی حضرت زینب (س) با مشارکت پرشور برگزار شد», Tovuti ya Andishgah-e Tajrobeh-Negari.
- ↑ Muhammadzadeh, Danikshnameh-ye She'r-e Ashura'i, 1386 Sh, Jz. 2, uk. 1287.
- ↑ Tazama: Amin Muqaddasi, «Uchambuzi wa Mashairi ya Ashura katika Fasihi ya Kifarsi na Kiarabu», uk. 79; «مجموعه اشعار خطبههای آتشین حضرت زینب(س)», Tovuti ya Hawzah.
- ↑ «آفتاب در حجاب، روایت رنج و استقامت», Tovuti ya Bustani ya Vitabu ya Tehran.
- ↑ «بانوی قصه من رمانی متفاوت با محوریت حضرت زینب(س)», Tovuti Maalumu ya Karbobala.
Maelezo
- ↑ Imamu Sajjad (a.s) baada ya hotuba ya Bibi Zainab mjini Kufa alimwambia bibi Zainab akiseme: «أَنْتِ بِحَمْدِ اللَّهِ عَالِمَةٌ غَیْرُ مُعَلَّمَةٍ فَهِمَةٌ غَیْرُ مُفَهَّمَةٍ» (Al-hamdulillahi, wewe ni mwanachuoni aliyeelimika bila ya kufundishwa na mtu, na mwelewa asiyehitaji kufahamishwa (Tabarsi, al-Ihtijaj, 1403 H, Jz. 2, uk. 305)).
- ↑ Kwa mujibu wa Hadithi kutoka kwa Imamu Baqir (a.s), subira njema ni ile ambayo mja hushikamana na subira bila ya kulalamika kwa watu kutokana na misiba inayomfika (Kulayni, al-Kafi, 1407 H, Jz. 2, uk. 93).
Marejeleo
- Abu al-Faraj al-Isfahani, Ali bin al-Hussein. Maqatil al-Talibiyyin. Qum: Sharif al-Radhi, 1416 H.
- Abu Mikhnaf, Lut bin Yahya. Waq'at al-Taff. Uhakiki: Muhammad Hadi al-Yusufi al-Gharawi. Qum: Majma' al-Alami li Ahl al-Bayt, Chapa ya 2, 1427 H.
- «آفتاب در حجاب، روایت رنج و استقامت» (Jua Ndani ya Hijabu: Simulizi ya Machungu na Subira). Tovuti ya Bustani ya Vitabu ya Tehran, Tarehe ya kuchapishwa: 6 Februari 2023 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Ahmad, Asghar. Ketabshenasi-ye Imamzadeh-ha va Beqa'-e Mobarrakeh. Qum: Sobh-e Sadeq, Chapa ya 1, 1384 Sh.
- Amin, Sayyid Muhsin. A'yan al-Shi'ah. Uhakiki: Hassan al-Amin. Beirut: Dar al-Ta'aruf, 1406 H / 1986 M.
- Amin Muqaddasi, Abu al-Hassan na Zahra Beheshti. «بررسی شعر عاشورایی در دو ادب فارسی و عربی با تکیه بر شهریار و جواهری» (Uchambuzi wa Mashairi ya Ashura katika Fasihi ya Kifarsi na Kiarabu). Jarida la Adabiyyat-e Paydari, Nambari 7 (1391 Sh).
- Ansari Qumi, Nasir al-Din. «کتابشناسی حضرت زینب علیها سلام» (Biblia ya Vitabu vya Bibi Zainab). Jarida la Waqf Mirath-e Javidan, Nambari 105 (1398 Sh).
- Ashur, Ali. Mawsu'at Zainab al-Kubra bint Amir al-Mu'minin Ali bin Abi Talib. Beirut: Dar Nadhir Abbud, 1429 H.
- «از موسوعة عقلیه الوحی رونمایی شد» (Mawsu'at Aqilat al-Wahy Yazinduliwa Rasmi). Shirika la Habari la ISNA, Tarehe ya kuchapishwa: 7 Juni 2012 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «بانوی قصه من رمانی متفاوت با محوریت حضرت زینب(س)» (Bibi wa Hadithi Yangu: Riwaya Maalumu Kuhusu Bibi Zainab). Tovuti Maalumu ya Karbobala, Tarehe ya kuchapishwa: 8 Novemba 2020 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «بیانات در دیدار پنجاه هزار فرمانده بسیج سراسر کشور» (Hotuba Mbele ya Makamanda wa Basiji). Tovuti ya Ofisi ya Kuhifadhi na Kuchapisha Kazi za Ayatullah Khamenei, Tarehe ya kuchapishwa: 20 Novemba 2013 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «برگزاری مراسم ولادت حضرت زینب(س) در زنجان» (Sherehe za Mazazi ya Bibi Zainab mjini Zanjan). Tovuti ya Moje Rasa, Tarehe ya kuchapishwa: 5 Novemba 2024 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Dakhil, Ali Muhammad Ali. A'lam al-Nisa. Beirut: al-Dar al-Islamiyyah, 1412 H / 1992 M.
- «دومین همایش بینالمللی حضرت زینب (س) با مشارکت پرشور برگزار شد» (Kongamano la Pili la Kimataifa la Bibi Zainab Lafanyika). Tovuti ya Andishgah-e Tajrobeh-Negari, Tarehe ya kuchapishwa: 9 Novemba 2024 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Faydh al-Islam, Sayyid Ali Naqi. Khatun-e Do Sara Sayyidatuna Zainab al-Kubra. Tehran: Nashr-e Athar-e Faydh al-Islam, Chapa ya 2, 1366 Sh.
- Fayruzabadi, Majd al-Din Muhammad bin Ya'qub. al-Qamus al-Muhit. Beirut: Mu'assasat al-Risalah, 1426 H / 2005 M.
- «فهرست ۵۰ نام پرطرفدار در میان دختران ایران در یک قرن اخیر» (Orodha ya Majina 50 Yanayoongoza kwa Wasichana). Tovuti ya Shoar-e Sal, Tarehe ya kuchapishwa: 11 Oktoba 2018 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «فهرست ۵۰ نام پرطرفدار در میان دختران ایران در یک قرن اخیر» (Majina Maarufu Zaidi ya Wasichana). Shirika la Habari la ANA, Tarehe ya kuchapishwa: 3 Oktoba 2018 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Hassun, Muhammad. A'lam al-Nisa al-Mu'minat. Qum: Uswah, Chapa ya 2, 1421 H.
- Hashiminejad, Sayyid Abd al-Karim. Darsi keh Hussein beh Insanha Amukht. Mashhad: Astan-e Quds-e Razavi, 1382 Sh.
- «حضرت زینب(س)، نماد صبر جمیل» (Bibi Zainab (a.s), Kielelezo cha Subira Njema). Shirika la Habari la Hawzah, Tarehe ya kuchapishwa: 30 Agosti 2020 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «حمله به حرم حضرت زینب(س)» (Shambulio Dhidi ya Haramu ya Bibi Zainab). Tovuti ya Tabnak, Tarehe ya kuchapishwa: 19 Julai 2012 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «حمله تروریستی به حرم حضرت زینب در سوریه» (Shambulio la Kigaidi Dhidi ya Haramu ya Bibi Zainab nchini Syria). Mtandao wa IRINN, Tarehe ya kuchapishwa: 19 Julai 2012 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Husseini Zabidi, Muhammad bin Muhammad. Taj al-Arus min Jawahir al-Qamus. Beirut: Dar al-Fikr, 1414 H / 1994 M.
- Ibn al-Athir al-Jazari, Ali bin Muhammad. Usdu al-Ghaba fi Ma'rifat al-Sahabah. Beirut: Dar al-Fikr, 1409 H / 1989 M.
- Ibn Manzhur, Muhammad bin Mukarram. Lisan al-Arab. Beirut: Dar Sadir, Chapa ya 3, 1414 H.
- Ibn Sa'd, Muhammad. al-Tabaqat al-Kubra. Beirut: Dar al-Kutub al-Ilmiyyah, 1410 H / 1990 M.
- «امروز مراسم عزاداری حضرت زینب(س) در سوئد و هلند برگزار میشود» (Shughuli za Maombolezo ya Bibi Zainab Kufanyika Sweden na Uholanzi). Shirika la Habari la Hawzah, Tarehe ya kuchapishwa: 13 Aprili 2017 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Jaza'iri, Sayyid Nuruddin. al-Khasa'is al-Zainabiyyah. Qum: al-Maktabah al-Haydariyyah, 1425 H.
- «جهان غرق شادی از میلاد حضرت زینب(س)، پرستار کربلا» (Ulimwengu Wafurika Furaha kwa Mazazi ya Bibi Zainab). Shirika la Habari la IMNA, Tarehe ya kuchapishwa: 7 Novemba 2024 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Kahhalah, Umar Ridha. A'lam al-Nisa fi Alamay al-Arab wa al-Islam. Beirut: Mu'assasat al-Risalah, 2008 M.
- Kahhalah, Umar Ridha. Mu'jam Qaba'il al-Arab. Beirut: Mu'assasat al-Risalah, 1414 H.
- Khwarazmi, Muwaffaq bin Ahmad. Maqtal al-Hussein. Uhakiki: Muhammad Samawi. Qum: Anwar al-Huda, Chapa ya 2, 1423 H.
- Kulayni, Muhammad bin Ya'qub. al-Kafi. Tehran: Dar al-Kutub al-Islamiyyah, 1407 H.
- al-Lajnah al-Ilmiyyah fi Mu'assasat al-Imam al-Sadiq. Mawsu'at Tabaqat al-Fuqaha. Chini ya usimamizi wa Jafar Subhani. Qum: Mu'assasat al-Imam al-Sadiq, 1418 H.
- «کتابشناسی حضرت زینب(س)» (Biblia ya Vitabu vya Bibi Zainab). Jarida la Ayeneh-ye Pazhoohesh, Nambari 115 (1388 Sh).
- «کنگره ملی حضرت زینب(س) در قم به کار خود پایان داد» (Kongamano la Kitaifa la Bibi Zainab Lamalizika mjini Qum). Shirika la Habari la IRNA, Tarehe ya kuchapishwa: 8 Juni 2012 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Mahallati, Dhabihullah. Rayahin al-Shari'ah. Tehran: Dar al-Kutub al-Islamiyyah, 1349 Sh.
- Majlisi, Muhammad Baqir. Bihar al-Anwar al-Jami'ah li Durar Akhbar al-A'immat al-Athar. Beirut: Dar Ihya al-Turath al-Arabi, Chapa ya 2, 1403 H.
- Mamaqani, Abdullah. Tanqih al-Maqal fi Ilm al-Rijal. Najaf: Bila mchapishaji, Bila tarehe.
- «مجموعه اشعار خطبههای آتشین حضرت زینب(س)» (Mkusanyiko wa Mashairi Kuhusu Hotuba za Bibi Zainab). Tovuti ya Hawzah, Tarehe ya kuchapishwa: 21 Aprili 2022 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «معنی اسم زینب و نامهای هم آوا با آن + میزان فراوانی در ثبت احوال» (Maana ya Jina Zainab na Umaarufu Wake). Tovuti ya Rasekhoon, Tarehe ya kuchapishwa: 9 Julai 2024 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Mehdizadeh, Zahra. «صبر و پایداری حضرت زینب(س)» (Subira na Uvumilivu wa Bibi Zainab). Tovuti ya Hawzah, Tarehe ya kuchapishwa: 2 Oktoba 2017 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Mughniyyah, Muhammad Jawad. al-Hussein wa Batalatu Karbala. Beirut: Dar al-Kutub al-Islami, 1426 H / 2005 M.
- Muhammadi Ishtehardi, Muhammad. Hazrat-e Zainab Forugh-e Taban-e Kowsar. Tehran: Borhan, Chapa ya 3, 1379 Sh.
- Muhammadi Ishtehardi, Muhammad. «زینب(س) پیامبر عاشورا» (Zainab (a.s) Mbeba Ujumbe wa Ashura). Jarida la Pasdar-e Islam, Nambari 198 (1377 Sh).
- Muhammadzadeh, Marziyeh. Danikshnameh-ye She'r-e Ashura'i. Tehran: Wizara ya Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu, 1386 Sh.
- Mohammadi Reyshahri, Mohammad. Danikshnameh-ye Imam Hussein (a.s). Qum: Dar al-Hadith, 1388 Sh.
- Murtadha Zabidi, Muhammad bin Muhammad. Taj al-Arus min Jawahir al-Qamus. Beirut: Dar al-Fikr, 1414 H.
- Naqdi, Jafar. Hayat al-Sayyidah Zainab bint al-Imam Amir al-Mu'minin Ali bin Abi Talib (a.s). Beirut: Mu'assasat al-A'lami, Chapa ya 1, 1419 H / 1998 M.
- Parto, Maryam na Ahmad Khamehyar. «زینب بنت علی بن ابیطالب» (Zainab bint Ali bin Abi Talib). Katika Danikshnameh-ye Jahan-e Islam (Jz. 22). Tehran: Bunyad-e Da'irat al-Ma'arif-e Islami, 1396 Sh.
- Pouya, Hassan. Zist-e Ma'sumaneh. Tehran: Nashr-e Orouj, 1403 Sh.
- Qazwini, Sayyid Muhammad Kazim. Zainab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd. Qum: Dar al-Ghadir, Chapa ya 2, 1424 H / 2003 M.
- Qurashi, Baqir Sharif. al-Sayyidah Zainab Batalat al-Tarikh wa Ra'idat al-Jihad fi al-Islam. Beirut: Dar al-Mahajjah al-Baydha, Chapa ya 1, 1422 H / 2001 M.
- Rabbani Khalkhali, Ali. Chehreh-ye Derakhshan-e Aqileh-ye Bani Hashim Zainab-e Kobra. Qum: Maktab al-Hussein, 1387 Sh.
- Rajabi Davani, Hossein. «چرا همسر حضرت زینب(س) ایشان را در کربلا همراهی نکرد؟» (Kwa Nini Mume wa Bibi Zainab Hakufuatana Naye Karbala?). Shirika la Habari la YJC, Tarehe ya kuchapishwa: 14 Februari 2016 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Rasuli Mahallati, Sayyid Hashim. Zainab Aqilat Bani Hashim. Tehran: Nashr-e Mash'ar, Bila tarehe.
- Saffar, Hassan. al-Mar'ah al-Azhimah. Dameski: Dar al-Ta'akhi, 2000 M.
- Sayyid Ibn Tawus, Ali bin Musa. al-Luhuf fi Qatla al-Tufuf. Qum: Anwar al-Huda, Bila tarehe.
- Shablanji, Mu'min bin Hassan. Nur al-Absar fi Manaqib Al Bayt al-Nabi al-Mukhtar. Qum: al-Sharif al-Radhi, Bila tarehe.
- Sharaf al-Din, Sayyid Abd al-Hussein. Aqilat al-Wahy. Uhakiki: Muhammad Rida Mamaqani. Bila mahali: Bila mchapishaji, Bila tarehe.
- Sheikh al-Mufid, Muhammad bin Nu'man. al-Irshad fi Ma'rifat Hujaj Allah ala al-Ibad. Qum: Kongresi ya Sheikh al-Mufid, Chapa ya 1, 1413 H.
- Sadeqi Ardestani, Ahmad. Zainab Qahraman Dokhtar-e Ali. Tehran: Motahhar, 1372 Sh.
- «سوریه - تشریح عملیات مرمت و بازسازی آسیبهای وارده به حرم حضرت زینب سلام الله علیها» (Syria: Ufafanuzi wa Kazi ya Ukarabati wa Haramu ya Bibi Zainab). Tovuti ya Ukarabati wa Maeneo Matakatifu, Tarehe ya kuchapishwa: 11 Juni 2014 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Sibt ibn al-Jawzi, Yusuf bin Qizughli. Tadhkirat al-Khawass. Tehran: Maktabat Naynawa al-Hadithah, Bila tarehe.
- Tabari, Imad al-Din Hassan bin Ali. Kamil-e Baha'i. Uhakiki: Akbar Safdari Qazwini. Tehran: Murtadhawi, Chapa ya 1, 1383 Sh.
- Tabari, Muhammad bin Jarir. Tarikh al-Umam wa al-Muluk. Kairo: Matba'at al-Istiqamah, 1358 H.
- Tabarsi, Ahmad bin Ali. al-Ihtijaj ala Ahl al-Lijaj. Uhakiki: Muhammad Baqir Khirsan. Mashhad: Nashr-e Murtadhawi, Chapa ya 1, 1403 H.
- Tabarsi, Fadhl bin Hassan. I'lam al-Wara bi A'lam al-Huda. Qum: Al al-Bayt, Chapa ya 1, 1417 H.
- «علت نامگذاری روز میلاد حضرت زینب(س) به روز پرستار» (Sababu ya Kutangaza Mazazi ya Bibi Zainab Kuwa Siku ya Wauguzi). Tovuti ya Hawzah, Tarehe ya kuchapishwa: 6 Novemba 2010 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «عزاداری سالروز وفات حضرت زینب(س) در کربلا» (Maombolezo ya Siku ya Kufariki Bibi Zainab huko Karbala). Tovuti ya Atabe News, Tarehe ya kuchapishwa: 18 Januari 2025 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «عکس/ زائران کشورهای مختلف در مرقد حضرت زینب(س)» (Picha: Wafanya Ziara kutoka Mataifa Mbalimbali Katika Haramu ya Bibi Zainab). Mashregh News Agency, Tarehe ya kuchapishwa: 5 Mei 2015 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «همایش حضرت زینب الگوی ایستادگی در بوشهر برگزار شد» (Kongamano la Bibi Zainab Kielelezo cha Subira mjini Bushehr). Shirika la Habari la Defa Press, Tarehe ya kuchapishwa: 25 Aprili 2016 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «همایش حضرت زینب(س) در حرم امام حسین(ع) برگزار شد» (Kongamano la Bibi Zainab Katika Haramu ya Imamu Hussein). Shirika la Habari la Hawzah, Tarehe ya kuchapishwa: 25 Oktoba 2017 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «همایش رهروان حضرت زینب(س) در اردبیل» (Kongamano la Wafuasi wa Bibi Zainab mjini Ardabil). Shirika la Habari la IRIB, Tarehe ya kuchapishwa: 3 Oktoba 2017 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- «زینب محبوبترین نام دختران ترکیه» (Zainab Jina Linaloongoza kwa Wasichana nchini Uturuki). Tovuti ya Entekhab, Tarehe ya kuchapishwa: 28 Februari 2017 M, Tarehe ya kutembelewa: 16 Agosti 2026 M.
- Ya'qub Hassan Dhahir. al-Masirah al-Imam al-Sayyid Musa al-Sadr. Beirut: Dar Bilal.
Viungo vya Nje
- «مدخل زینب بنت علی (ع)، در دانشنامه جهان اسلام» (Makala ya Zainab binti Ali (a.s), katika Danikshnameh-ye Jahan-e Islam).
- پیرامون مزار حضرت زینب(س) » (Utafiti Kuhusu Mahali pa Kaburi la Bibi Zainab (s.a)).
- Articles with hatnote templates targeting a nonexistent page
- Bibi Zainab
- Watoto wa Imamu Ali
- Mateka wa Tukio la Karbala
- Wapashaji Habari wa Tukio la Karbala
- Wana wa Maimamu Waliozikwa Damascus
- Watoto wa Bibi Fatima
- Masahaba wa Kike
- Wanawake wa Bani Hashim
- Wasimuliaji Hadithi kutoka kwa Imamu Ali
- Waombolezaji wa Maombolezo ya Ashura wa Karne ya 1 (Hijiria)