Ruqayyah binti ya Imamu Ali (as)

Kutoka wikishia
Ruqayyah binti Ali (a.s)
Ili kujua matumizi mengine angalia Ruqayyah (kwa ajili ya kuondoa utata)

Ruqayyah bint Ali (a.s) (alikuwa hai mpaka 61 Hijria), ni mke wa Muslim bin Aqil na mmoja wa mateka wa Karbala. Ruqayyah alikuweko katika tukio la Karbala. Alipata habari ya kuuawa shahidi mumewe Muslim bin Aqil wakati akiwa njiani kutoka Makka kuelekea Karbala.

Katika siku ya Ashura (mwezi kumi Muharram) pia watoto wake Abdallah na Muhammad kwa mujibu wa baadhi ya kauli waliuawa shahidi na yeye akachukuliwa mateka na Jeshi la Omar bin Sa’d. Kuna kaburi lililoko Cairo, Misri linalojulikana kwa jina lake. Kuna kaburi jingine katika mji wa Lahore Pakistan linalojulikana kwa jina la Bibi Mtakasifu ambalo linanasibishwa na kutajwa kuwa ni la Ruqayya bint Ali (a.s).

Nasaba

Ruqayya ni binti ya Imamu Ali (a.s) na mama yake ni Sahba' bint Rabi'a al-Taghlibiyya aliyekuwa kanizi wa Imamu Ali (a.s).[1] Dhabihullah Mahalati amemtambua Sahba' kuwa mama yake Ruqayyah na Omar bin Ali.[2]

Katika baadhi ya vyanzo, Ruqayya ametajwa kama Ummu Kulthum.[3] Sayyid Muhsin Amin ametambua kunia ya mabinti watatu wa Imamu Ali (a.s) kuwa ni Ruqayyah. Yeye amemuita Ruqayya kuwa ni Ummu Kulthum Wustaa na amemtambua kuwa huyu sio Ummu Kulthuum Kubra wala Ummu Kulthum Sughra (mke wa mmoja wa wajukuu wa Aqil).[4]

Ndoa na Watoto

Ruqayyah aliolewa na binamu yake yaani Muslim bin Aqil.[5] Kwa mujibu wa mwandishi wa Rayahin al-Shari'ah, Ruqayya alizaa na Muslim bin Aqil watoto wawili wa kiume wanaojulikana kwa majina ya Abdallah na Muhammad na binti mmoja.[6] Jina la binti yake halijatajwa katika kitabu hiki.[7] Dhabihullah Mahalati, mwandishi wa kitabu hiki amemtambua Abdallah kuwa ni mume wa Sakinah binti ya Imamu Hussein (a.s).[8]

Kuweko Katika Tukio la Karbala

Ruqayyah alikuweko katuika tukio la Ashura na alikwenda Karbala akiwa pamoja na Imamu Hussein (a.s).[9] Dhabihullah Mahalatii anasema, Ruqayyah alikuwa ameongozana na watoto wake watatu katika safari ya kuelekea Karbala.[10] Alipata habari ya kuuawa shahidi mumewe (Muslim bin Aqil) akiwa njani. Kwa mujibu wa waandishi wa historia, Abdallah bin Muslim aliuawa shahidi katika tukio la Karbala.[11] Mahalati mwandishi wa kitabu cha Rayahin al-Shari'ah amezungumzia kuuawa shahidi watoto wawili wa kiume wa Ruqayyah katika tukio la Karbala na yeye mama mtu kuchukuliwa mateka.[12]

Kaburi

Kaburi la Ruqayyah binti wa Imamu Ali (a.s)

Kwa mujibu wa Mu'jam al-Buldan ni kwamba, Ruqayyah amezikwa Cairo katika nchi ya Misri.[13] Mwaka 1416 Hijria kundi la Dawoodi Bohra la India lilifanyia mabadiliko dharih (eneo la nje linalozunguka kaburi lake).[14]

Haram ya Bibi Mtakasifu

Makala kuu: Bibi Mtakasifu

Katika mji wa Lahore, Pakistan kuna Haram inayotambuliwa kwa jina la Bibi mtakasifu[15] ambapo watu wanaamini kwamba, ndani yake amezikwa Ruqayyah binti ya Imamu Ali (a.s) na wanawake wengine watano.[16] Eneo hilo lina historia ya mamia ya miaka na ni miongoni mwa athari na turathi kongwe na za kufanya ziara katika mji wa Lahore.[17] Hata hivyo wahakiki wamepinga imani hii kwamba, Ruqayya binti ya Imamu Ali (a.s) amezikwa katika eneo hilo.[18]

Makala Zinazo Husiana

Rejea

Vyanzo