Nenda kwa yaliyomo

Mubahala ‌‌Baina ya Mtume na Wakristo wa Najrani

Kutoka wikishia

Mubahala / Maapizano (Kiarabu: المباهلة) kati ya Mtume (s.a.w.w) na Wakristo wa Najran ni moja ya matukio yaliyotokea mwanzoni mwa Uislamu ambayo yanatambuliwa kuwa ni ishara ya kuwa ni wa haki mwito na ulingaliaji wa Mtume (sa.w.w). Kadhalika tukio hili linaonyesha fadhila za Mtume (s.a.w.w) pamoja na watu aliofuatana nao kwa ajili ya kwenda kufanya mubahala (maapizano) na Wakristo yaani Imam Ali (a.s), Fatma (a.s), na Maimamu Hassan na Hussein (a.s).

Aya ya 61 ya Surat al-Imran imebainisha tukio hili na imeondokea kuwa mashuhuri kwa Aya ya Mubahala. Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaamini kwamba, katika Aya ya Mubahala Imam Ali (a.s) ni nafsi ya Mtume na kwa muktadha huo wanaitambua Aya hii kwamba, ni katika Aya zinazooonyesha fadhila za Imam Ali (a.s). Tukio hili limenukuliwa katika vyanzo na vitabu vya Shia na Suni.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ni kwamba, ujumbe wa Kikristo kutoka Najran ulifika kwa Mtume kujadili kuhusiana na madai yake ya Utume. Mtume sambamba na kujitambulisha yeye kwamba, ni Mtume wa Allah alimtaja Nabii Issa (a.s) kwamba, ni mja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu. lakini Wakristo walikataa na wakapendekeza kufanyika maapizano.

Asubuhi ya Siku ya Mubahala, Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) pamoja na binti yake Bibi Fatima Zahra (a.s), mkwe wake Imam Ali (a.s) na wajukuu zake Imam Hassan (a.s) na Imam Hussein (a.s) waliondoka Madina. Abu Haritha, mmoja wa wajumbe waandamizi wa ule ujumbe wa Kikristo, alipowaona wale waliokuwa wakifuatana na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wakakataa kufanya maapizano. Kuhusiana na siku na mwaka wa kutokea tukio hili, kuna mitazamo na rai tofauti. Hata hivyo wanahistoria mashuhuri zaidi wanaamini kwamba, tukio hili lilitokea katika mwaka wa 10 Hijiria. Kadhalika katika vitabu vya dua, kumetajwa amali na mambo ya kufanya tarehe 24 Mfunguo Tatu Dhul-Hija kwa anuani ya siku ya Mubahala. Kuna vitabu vilivyoandikwa na kutengenezwa athari za kisanaa kuhusiana na tukio la Mubahala.


Nafasi na umuhimu wake

Mubahala (maapizano) baina ya Mtume (s.a.w.w.) na Wakristo wa Najran ni miongoni mwa matukio yanayotumiwa kuthibitisha kwamba, mwito na da’awa ya Mtume ilikuwa ya haki. [1] Tukio hili limezungumziwa katika Surat al-Imran. [2] Kadhalika tukio hili linahesabiwa kuwa, linaonyesha fadhila kubwa walizonazo watu watano; (Mtume (s.a.w.w), Imam Ali (a.s), Fatma (a.s), Hassan (a.s) na Hussein (a.s)). [3] Tukio hilo limezungumziwa pia katika vyanzo vya tafsiri ya Qur’ani {4] na vya kihistoria [5].

Ufafanuzi wa tukio

Mtume (s.a.w.w) sambamba na kuwaandikia barua viongozi wa watawala mbalimbali duniani, alimuandikia pia barua askofu wa Najran, ambamo aliwataka watu wa Najran kuukubali Uislamu. Wakristo waliamua kutuma ujumbe kwenda Madina kuzungumza na Mtume (s.a.w.w) na wakakaa katika msikiti wa Madina na kufanya mazungumzo na Mtume. Mtume aliwajulisha kuwa: Hakika mfano wa Issa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam, aliumbwa kwa udongo kisha akamwambia: Kuwa naye akawa.

Kwa kuwa Nabii Isa alizaliwa bila baba, Wakristo wamedhani kuwa baba yake ni Mwenyezi Mungu. Aya hii inaondoa dhana hiyo ambayo inapingana na utukufu wa Mwenyezi Mungu, na inawapigia mfano wa ajabu zaidi katika kuumbwa Adam bila ya baba wala mama. Aliumbwa kwa udongo kisha akaambiwa: kuwa naye akawa, na kwa neno hilo hilo Nabii Isa (a.s) ndivyo alivyoumbwa. Wakristo wao walisisitiza kwamba, kuzaliwa Nabii Issa bila baba ni hoja na dalili ya kuwa kwake Mungu. [6] Ujumbe huo ulipokuwa haukukubaliana na hoja ya Mtume na wakati huo huo, kung’ang’ania msimamo wao, ikaamuliwa kufanyike mubahala na maapizano. Hivyo pande mbili zikaafikiana kwamba, kesho yake, wakatunae nje ya mji wa Madina katika jangwa na kufanya maapizano [6]. Muda ulipowadia Mtume alitoka akiwa pamoja na Ali, Fatma, Hassan na Hussein (a.s). Wakristo walipomuna Mtume amekuja kwa ajili ya Mubahala akiwa amefuatana na vipenzi vyake, mmoja wa wajumbe waandamizi wa ule ujumbe wa Kikristo, alipowaona wale waliokuwa wakifuatana na Mtukufu Mtume (s.a.w.w), alisema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba amekaa kama Manabii walivyokuwa wakiketi kwa ajili ya Mubahala”, na akarejea. Akaongeza: “Kama Muhammad (s.a.w.w) hakuwa kwenye haki, asingethubutu kuja kwa ajili ya Mubahala namna hii, na kama Muhammad (s.a.w.w) atakutana nasi katika Mubahala, basi hata Mkristo mmoja hatabaki hai kabla ya mwaka huu kuisha." Kwa muktadha huo, wakristo hao wakaomba suluhu na mapatano. Mtume akakubali ombi lao hilo kwa sharti la kulipa kodi. Baada ya manasara kurejea Najran, shakhsia wawili waliokuwa katika ujumbe ule walirejea tena kwa Mtume (s.a.w.w) wakiwa na zawadi na wakasilimu. [7] Fakhrurazi, mmoja wa wafasiri wa Qur’ani tukufu wa Ahlu-Sunna (aliyefariki 606 Hijria) amesema kuwa, wafasiri na wapokezi wa hadithi wameafikiana kuhusiana na tukio hili. [8]

Aya ya Mubahala

Aya ya Mubahala: (فَمَنْ حَاجَّكَ فِیهِ مِن بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ أَبْنَاءَنَا وَأَبْنَاءَكُمْ وَنِسَاءَنَا وَنِسَاءَكُمْ وَأَنفُسَنَا وَأَنفُسَكُمْ ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَل‌لَّعْنَتَ اللَّـهِ عَلَی الْكَاذِبِینَ)

Makala asili: Mubahala


فَمَنْ حَاجَّكَ فِيهِ مِن بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ أَبْنَاءَنَا وَأَبْنَاءَكُمْ وَنِسَاءنَا وَنِسَاءكُمْ وَأَنفُسَنَا وأَنفُسَكُمْ ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَل لَّعْنَةَ اللَّهِ عَلَى الْكَاذِبِينَ

Watakao kuhoji katika haya baada ya kukufikilia ilimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na wake zenu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.
(Quran: 3: 61)


Sayyid Nurullah Shushtari, anasema kuwa, wafasiri wana mtazamo mmoja kwamba, “watoto wetu” katika Aya ya Mubahala inaashiria Hassan na Hussein, “wake zetu” ni ishara ya Fatma na “ nafsi zetu au sisi wenyewe” anaashiriwa Imam Ali (as). [9] Kadhalika Allama Majlisi amezitambua hadithi zinazotoa dalili kwamba, Aya ya Mubahala imeshuka kwa watu wa Kishamia (Ahlul-Kisaa) ni mutawatir. [10] Katika kitabu cha Ihqaq al-Haqq (kilichoandikwa 1014 Hijria), kumeorodheshwa takribani vyanzo 60 vya Ahlu-Sunna ambavyo vinabainisha wazi kuhusiana na Aya hii kwamba, imeshuka kuwahusu watano hawa. [11] Maimamu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia [12] na baadhi ya masahaba wa Mtume [13] wakiwa na lengo la kuthibitisha fadhila za Imam Ali (a.s) waliitumia Aya hii.

Zama na Sehemu

Kwa mujibu wa vyanzo vya historia, tukio la Mubahala lilitokea baada ya Hijra ya Mtume ya kutoka Makka na kwenda Madina; [14] hata hivyo kuna rai na mitazamo tofauti kuhusiana na mwaka na siku yenyewe. Sheikh Mufid (aliga dunia 413 Hijiria) amesema kuwa, tukio la Mubahala lilitokea baada ya Fat’h Makka (mwaka wa 8 Hijria). [15] Katika kitabu cha Tarikh Tabari (kilichoandikwa 303 Hijiria), tukio hili limetajwa kuwa lilitokea mwaka wa 10 Hijiria. [16] Muhammad Reyshahri (aliyefariki 2022) ameandika katika kitabu cha Farhangnameh Mubahalah kwamba, waandishi mashuhuri wa historia wamesema kuwa, tukio hili linahusiana na mwaka wa 10 Hijiria na baadhi yao wameliheasabu kuwa lilitokea mwaka wa 9 Hijiria. [17]

Kuhusiana na siku lilipotokea tukio la Mubahala pia kuna rai na mitazamo tofauti; kama vile 21, [18] 24 [19] na 25 Dhul-Hija (Mfunguo Tatu). [20]. Sheikh Ansari anasema, tarehe 24 Dhul-Hija ndio mtazamo mashuhuri zaidi kwamba, tukio la Mubahala lilitokea katika siku hiyo. [21] Kadhalika katika vitabu vya dua, kumetajwa amali na mambo ya kufanya tarehe 24 Mfunguo Tatu Dhul-Hija kwa anuani ya siku ya Mubahala. [22] Sheikh Abbas Qomi, ametaja baadhi ya amali katika kitabu cha Mafatihul-Jinan kama vile dua, ghusli (josho) na kufunga Swaumu. [23]

Sehemu

Tukio la Mubahala lilitokea katika mji wa Madina; hata hivyo haifahamiki eneo hasa lilipotokea tukio hilo. Jirani na Baqi’i kuna msikiti unaofahamika kwa jina la Mubahala na Masjid al-Ijabah [24] ambapo wafanyaziara wa msikiti huo hulizuru eneo hilo kwa anuani ya sehemu lilipotokea tukio la Mubahala; [25] hata hivyo inaelezwa kuwa, hakukutajwa katika vyanzo vya historia msikiti unaojulikana kwa jina hili. [26] Muhammad Sadiq Najmi (aliyefariki 2011), mwandishi wa Kishia, yeye anaamini kwamba, msikiti huu hauna uhusiano na tukio la Mubahala na kosa hili limetokana na kushabihiana mafuhumu na maana ya ijabah na mubaha na vilevile maneno ya Ibn Mash’hadi ambaye aligizia kuswali katika msikiti wa Mubahala. [27] Ibn Mash’hadi (aliaga dunia 610 Hijiria) ametaja msikiti wa Mubahala katika kitabu chake cha al-Mazar na kukokoteza suala la kuswaliwa katika msikiti huo. [28] Muhammad Sadiq Najmi anasema: Sababu ya kutojengwa msikiti katika eneo lililopotokea tukio la Mubahala ni kwamba, Mtume hakuswali katika eneo hilo, na Waislamu walikuwa wakijenga msikiti katika maeneo ambayo kulikuwa na uhakika kwamba, Mtume aliswali hapo. [29]

Vitabu na athari za kisanaa

Mchoro wa tukio la Mubahala katika nakala ya Athar al-Baqiyah iliyoandikwa na Abu Rihan Biruni (tarehe ya kuchapishwa kwa nakala: 707 AH)

Kumeandikwa vitabu mbalimbali kuhusiana na kadhia ya Mubahala. Baadhi ya vitabu hivyo ni:

  • Manba’ shenasi vagheeye mubahala, mwandishi: Muhammad Ali Askari na Muhammad Ali Najafi. [30]
  • Mubahala dar Madineh, (La Mubahala de Médine) mwandishi: Louis Massignon. [32]
  • Mubahala Sadiqin, mwandishi: Sayyid Muhammad Alawi

Athari za kisanaa

Kuhusiana na tukio la Mubahala kuna athari mbambali zilizotengenezwa na kuzalishwa katika uga wa sanaa kama vile michoro, katuni hai (animation) n.k. Mojawapo ya athari na kazi kongwe kabisa ni mchoro ambao umewekwa katika nakala ya kitabu cha Aathar al-Baqiyah cha Abu Reihan Biruni. Nakala ya kitabu hiki inahifadhiwa nchini Ufaransa. [33] Rasul Ja’afariyan, mtafiti wa masuala ya historia anasema kuwa, kuna uwezekano mchoro huu uliongezwa na mwandikaji kwenye kitabu hicho. [34]