Al-Kafi (kitabu)
Kitabu cha al-Kafi (Kiarabu: الكافي) ni miongoni mwa vyanzo vya hadithi za Shia na chanzo muhimu na cha kutegemewa miongoni mwa Kutub al-Arba’ (vitabu vinne vya hadithi vya Waislamu wa Kishia). Kitabu hiki kimeandikwa na Muhammad bin Yaqub bin Is'haq, anayejulikana kama Thiqat al-Islam Kulayni, ambaye alikikusanya na kukiandika kitabu hiki kwa muda wa miaka 20. Kitabu cha Al-Kafi, ambacho kimeandikwa katika sehemu tatu, Usul, Furuu’ na Rawdha, ni mahali pa marejeo kwa wanachuoni wa Shia. Usul Kafi ndio inayohesabiwa kuwa sehemu maarufu zaidi ya kitabu hiki cha al-Kafi. Sheikh Kulayni alikusudia kukusanya hadithi za al-Kafi kwa msingi wa kutopingana na Qur'ani na kukubaliana na ijmaa (maafikiano).
Kutokana na uhusiano wake na masahaba wa Maimamu na upatikanaji wa misingi mia minne (Usul al-Arbaa Mia), Sheikh Kulayni amenukuu riwaya za kitabu hiki kwa kupitia kwa watu wachache sana wasiokuwa masahaba wa Maimamu. Kwa maana kwamba, hadithi zake nyingi alinukuu moja kwa moja kutoka kwa masahaba wa Maimamu. Kundi miongoni mwa wanazuoni wa Kishia linaamini juu ya usahihi wa hadithi zake zote, na kwa upande mwingine, kuna kundi la wanazuoni wa Kishia ambalo linakubali juu ya kuwepo kwa hadithi dhaifu katika al-Kafi. Inasemekana kwamba kupatiwa jina la kitabu hiki kumenasibishwa kwa Imamu wa Zama (a.t.f.s), hata hivyo wanazuoni wengi wamepinga madai haya.
Mwandishi
- Makala Kuu: Kulayni
Abu Ja'far Muhammad bin Ya'qub bin Is'haq al-Kulayni al-Razi mashuhuri kwa Thiqat al-Islam al-Kulayni na Sheikh wa Masheikh, ni mmoja wa wasomi na wanazuoni wakubwa wa elimu ya hadithi aliyeishi katika zama za Ghaiba Ndogo ya Imamu Mahdi (a.t.f.s) na alikutana na baadhi ya wapokezi wa hadithi waliosikia hadithi moja kwa moja kutoka kwa Imamu Hassan al-Askary (a.s) au Imamu Hadi (a.s). Sheikh Kulayni alikuwa akihesabiwa kuwa mmoja wa wasomi na wanazuoni wakubwa wa elimu ya hadithi wa Kishia katika nusu ya pili ya karne ya tatu na nusu ya kwanza ya karne ya nne Hijria. Kwa mujibu wa kile kilichobainishwa na kuelezwa katika tafsiri na vitabu vya historia kuhusu hali za binafsi za watu na historia, watu wote wapinzani na waungaji mkono wake wamezungumzia fadhila na adhama kubwa aliyokuwa nayo Sheikh Kulayni. [1]
Msukumo wa Kuandika Kitabu Hiki na Sababu ya Kukipa Jina Hili
Kama alivyoandika Sheikh Kulayni mwenyewe katika utangulizi wa kitabu hiki, ni kwamba, alialifu kitabu hiki cha al-Kafi kujibu ombi la mtu anayemwita ndugu wa kidini.
Ama kuhusiana na sababu ya kuitwa kitabu hiki kwa jina hili kumebainishwa nukta mbili.
- Maneno ya Shekhe Kulayni mwenyewe katika hotuba ya tohara ambapo anasema: Kitabu hiki ni Kafi (yaani kinatosha) kwa ajili ya taaluma zote za dini. [3]
- Jina la kitabu limechukuliwa kutoka katika maneno yanayonasibishwa na Imamu Mahdi (a.t.f.s) ambapo amesema: Kitabu hiki ni Kafi (kinatosha) kwa ajili ya Mashia wetu. Maneno haya aliyatoa baada ya kuonyeshwa kitabu hiki na akawa amekisifia [4] (hata hivyo haya ni madai tu kwani hakuna hadithi kama hii).
Nafasi ya Kitabu cha al-Kafi kwa Maulamaa wa Kishia
Sheikh Mufidu anasema: Kitabu hiki ni cha juu kabisa miongoni mwa vitabu vya Kishia ambacho kina faida nyingi mno. [5] Shahidi al-Awwal [6] na Muhaqqiq Karaki [7] wamekitambua kitabu hiki katika uwanja wa hadithi kwamba, hakina mithili miongoni mwa Shia Imamiyyah.
Shahid al-Thani anasema: «Hakuna kitabu mfano wa hiki duniani kwa upande wa ukusanyaji hadithi na dhuku nzuri katika upangiliaji wa milango yake». [8]
Muhammad Taqi Majlisi ameandika:
- Kitabu cha al-Kafi kina nguvu zaidi, jumuishi zaidi, bora zaidi na kikubwa zaidi kuliko vitabu vyote vya Usul vilivyoandikwa na kualifiwa na kundi ongofu (Shia Imamiyyah) [9].
Agha Bozorg Tehran anasema: Hakuna kitabu kilichoandikwa mithili ya al-Kafi katika uga wa kunukuu hadithi za Ahlul-Bayt (a.s). [10]
Al-Astrabadi ananukuu kutoka kwa wanazuoni na walimu wake ya kwamba, hakuna kilichoandikwa katika Uislamu ambacho kinalingana au kukaribia kitabu cha al-Kafi. [11]
Ayatullah Khui amenukuu kutoka kwa mwalimu wake Mirza Muhammad Hussein Naini kwamba hakuwa na uwezo wa kufanya mjadala na mdahalo katika sanadi (mapokezi) ya hadithi za al-Kafi. [12]
Kama ilivyoelezwa katika utangulizi wa kitabu hiki, Sheikh Kulayni amekusanya hadithi hizo kwa kuzingatia kigezo cha kutopingana na Qur'ani na kukubaliana na maafikiano (ijmaa), na pale ambapo hakuona sifa inayostahiki ya kuchukua hadithi moja mbele ya hadithi nyingine zilizokuwa na hali ya kugongana, basi aliichukua ile ambayo kwa mujibu wa maoni yake ilikuwa karibu na ukweli na uhalisia. [13]
Sifa Maalumu ya Kitabu Hiki
Wakati wa kuandika kitabu hiki akitumia misingi mia nne (vitabu 400 vya hadithi vilivyaondikwa na masahaba wa Maimamu) na kukutana ana kwa ana na masahaba wa Maimamu watoharifu (a.s) au watu ambao waliwaona masahaba, alinukuu katika kitabu chake hicho hadithi nyingi bila ya kupitia kwa watu wengine. Kwa maana kwamba, hadithi zake nyingi alinukuu moja kwa moja kutoka kwa masahaba wa Maimamu. Kuishi katika zama moja na Manaibu Wanne wa Imamu Mahdi kulimuandalia uwanja na mazingira mazuri ya kufanya uhakiki kuhusiana na kuwa na kutokuwa sahihi hadithi. [14] Hata hivyo kuhusiana na ibara hiyo ya mwisho inapasa kusema kwamba: Kuonyeshwa na kuwasilishwa kitabu Maimamu haikuwa ada iliyokuwa imeenea na kiwango cha vitabu vilivyopatiwa na kuonyeshwa Maimamu ni ndogo ikilinganishwa na vile ambavyo hawakupatiwa na kuonyeshwa. Fauka ya hayo, Shikhe Kulayni hakuwa na mawasiliano na maingiliano maalumu na Manaibu Wanne wa Imamu Mahdi (a.t.f.s). [15]
Nidhamu, mpangilio na kuwa jumuishi kitabu ni sifa nyingine maalumu ya kitabu cha al-Kafi. Kwa upande wa mpangilio, nidhamu na utaratibu katika kugawa hadithi, idadi ya hadithi na mlolongo wote wa sanadi na mapokezi ya hadithi na kutokana na kuwa jumushi na kuwa na ukamilifu katika uteuzi wa maudhui mbalimbali kama ya kiitikadi, kifiq’h, akhlaq, kijamii na kadhalika ni mambo ambayo kwa hakika ni ya kipekee kwa kitabu hiki. Kuhusiana na hili, Shekhe Kulayni alifanya idili na hima kubwa kuhakikisha kwamba, mwanzoni mwa kitabu analeta hadithi zenye upana na maelezo zaidi, zilizo wazi zaidi na ambazo ni sahihi zaidi na kisha baadaye kuorodhesha hadithi ambazo zina hali jumla, utata na kutoeleweka vyema. [16]
Kuidhinishwa kitabu na Imamu wa Zama (a.t.f.s)
Baadhi wamesema kuhusu kitabu cha al-Kafi kwamba kiliwasilishwa kwa Imamu Mahdi (a.t.f.s) na akasema:
«الکافی کاف لشیعتنا» Al-Kafi kinawatosha kabisa Mashia wetu, [17].Hata hivyo hili halina ukweli: Mirza Hussein Nuri anasema: Huu uvumi unaosemwa kwamba, kitabu cha al-Kafi kiliwasilishwa kwa Imamu Mahdi na akasema, al-Kafi kinatosha kwa Mashia wetu, maneno haya hayana asili na hayapo katika athari za uandishi za watu wetu. Ananukuu kutoka kwa al-Astarabadi msomi wa elimu ya hadithi ya kwamba, hakuna hadithi kama hii. [20]
Muundo na yaliyomo ]
Kitabu cha al-Kafi kinaundwa na sehemu tatu za Usul, Furu’ na Rawdha: Usul al-Kafi inajihusisha hadithi za kiitikadi, Furu' inazungumzia hadithi za kifiq'h na Rawdha inajihusisha na masuala ya historia.
Milango ya al-Kafi
Mwandishi wa kitabu cha al-Kafi amezigawa hadithi zake katika sehemu tatu jumla.
Usul al-Kafi
- Makala Kuu: Usul al-Kafi
Usul al-Kafi kinaundwa na sehemu kuu nane jumla ambapo Shekhe al-Kulayni ametambulisha kila sehemu miongoni mwa sehemu hizi kwa anuani ya kitabu. Anuani hizo jumla ni:
- Kitab al-Aql Wal-Jahl.
- Kitab Fadh al-Ilm
- Kitab al-Tawhid.
- Kitab al-Hujjah.
- Kitab al-Iman Wal-Kufr.
- Kitab al-Duaa.
- Kitab Fadhl al-Qur’an.
- Kitab al-Ish’rah.
Furu' al-Kafi
Furu' al-Kafi inajumuisha hadithi zinazohusiana na masuala ya fiqh na kuna jumla ya sehemu 26 ambazo ni:
- Kitab al-Tahara (Kitabu cha Tohara).
- Kitab al-Haydh (Kitabu cha Hedhi).
- Kitab al-Jana'iz (Kitabu cha Maiti).
- Kitab al-Salat (Kitabu cha Sala).
- Kitab al-Zakat wa l-Sadaqah (Kitabu cha Zaka na Sadaka).
- Kitab al-siyam (Kitabu cha Swaumu).
- Kitab al-Hajj (Kitabu cha Hija).
- Kitab al-Jihad (Kitabu cha Jihadi).
- Kitab al-Ma'isha (Kitabu cha Maisha).
- Kitab al-Nikah (Kitabu cha Nikaha).
- Kitab al-'aqiqa (Kitabu cha Akika).
- Kitab al-Talaq (Kitabu cha Talaka).
- Kitab al-'itq wa l-tadbir wa l-mukataba (Kitabu cha ukombozi, usimamizi na uandishi).
- Kitab al-Sweyd (Kitabu cha Uwindaji).
- Kitab al-Dhaba'ih (Kitabu cha Kuchinja).
- Kitab al-at'ima (Kitabu cha Vyakula).
- Kitab al-ashriba (Kitabu cha Vinywaji).
- Kitab al-zey wa l-tajammul wa l-muruwwa (Kitabu cha mavazi, mapambo na muruwa).
- Kitab al-Dawajin (Kitabu cha Wanyama).
- Kitab al-Wasaya (Kitabu cha Wasia).
- Kitab al-Mawarith (Kitabu cha Urithi).
- Kitab al-Hudud (Kitabu cha Adhabu).
- Kitab al-Diyat (Kitabu cha Dia).
- Kitab al-hahadat (Kitabu cha Ushahidi).
- Kitab al-Qadha' wa l-Ahkam (Kitabu cha Hukumu na Sheria).
- Kitab al-Ayman wa l-nudhur wa l-kaffarat (Kitabu cha Viapo, Nadhiri na Kafara).
Rawdhat al-Kafi
- Rawdhat al-Kafi sehemu hii ina hadithi mbalimbali bila kuzingatia utaratibu maalumu. Sehemu hii ya kitabu inajuhusisha na maudhui tofauti. Licha ya kuwa baadhi hawaitambui Rawdhat al-Kafi kuwa ni sehemu ya kitabu cha al-Kafi [20] lakini Najjashi na Sheikh Tusi wamesema bayana na kwa uwazi kabisa kwamba, Rawdha ni sehemu ya mwisho ya kitabu cha al-Kafi. [21] [22]
- Kufanya taawili na kufasiri baadhi ya Aya za Qur’an.
- Nasaha na Ahlul-bayt (a.s).
- Ndoto na aina zake.
- Maumivu na tiba.
- Namna ya kuumbwa ulimwengu na baadhi ya matukio yake.
- Historia ya baadhi ya Mitume wa Allah.
- Fadhiza za Shia na majukumu yake.
- Baadhi ya masuala ya kihistoria ya mwanzoni mwa Uislamu na kipindi cha Ukhalifa wa Amirul-Muuminina (a.s).
- Imamu Mahdi (a.t.f.s) na sifa zake na vilevile masahaba na zama za uwepo wake.
- Historia ya maisha ya baadhi ya masahaba na watu wengine
Maudhui ya kwanza ya kitabu cha Rawdha ni barua ambayo Imamu Sadiq (a.s) aliwaandikia Mashia na masahaba zake kama maelekezo kwao ili kwa kusoma na kkuchunguza kwa makini dhamira zake na kujifunza na kuitumia, waweze kuwa na mdakhala na maingiliano ya kijamii na kushirikiana na watu wengine (wapinzani na ambao wana itikadi tofauti na wao), waamiliane nao kwa mujibu wa kanuni za maadili na imani na wasiandae mazingira ya tuhuma na mtazamo mbaya dhidi yao wenyewe. Barua hii inamalizika kwa kuwataka kuchunga utulivu, unyenyekevu, haya, soni na kushirikiana kwa wema na watu wa batili na kumtii Mwenyezi Mungu sambamba na kuwafuata Ahlul-Bayt (a.s). [24]
Hadithi ya mwisho ya kitabu hiki imepokewa kutoka kwa Imamu Baqir (a.s) akimjibu mtu mmoja aliyemwambia Mtume: “Nyinyi ni familia ya rehema ambayo Mwenyezi Mungu amekufanyeni kuwa ni wa kipekee, ambapo Imamuu akasema: Sisi tuko hivi, na tunamshukuru Mungu. Hatumpotoshi yeyote na hatumuondoi yeyote kutoka kwenye njia iliyo sawa. Hakika dunia haitokwisha mpaka Mwenyezi Mungu amlete mtu katika familia yetu, Ahlul-Bayt, ambaye anafuata Kitabu cha Mwenyezi Mungu, wala haoni kitendo kiovu miongoni mwenu isipokuwa akikanushe (akabiliane nacho). [25]
Idadi ya Hadithi za al-Kafi
Idadi ya hadithi katika kitabu cha al-Kafi imetajwa kwa takwimu tofauti. Yusuf Bahrani katika Lu’lu al-Bahrain ametaja idadi ya hadithi hizo kuwa ni 16,199, Dk. Hossein Ali Mahfouz katika utangulizi wa al-Kafi amezitaja kuwa ni 15,176, Allama Majlisi 16,121, na baadhi ya watu wa zama hizi kama Sheikh Abdul Rasuol al-Ghafar wamehesabu hadithi hizo kuwa ni 15,503. Tofauti hii ya takwimu inasababishwa na njia ya kuhesabu hadithi. Kwa maana kwamba, baadhi wameichukulia riwaya iliyotajwa kwa sanadi na mapokezi mawili kuwa ni riwaya mbili, na wengine wameichukulia kuwa ni riwaya moja. Baadhi ya hadithi za Mursala pia zimehesabiwa kuwa ni hadithi moja, na baadhi hakuzileta hizo katika hesabu. Hata hivyo katika baadhi ya mambo nadra inawezekana hitilafu hiyo ikawa imetokana na kutokuwepo kwa baadhi ya hadith katika baadhi ya matoleo. [26]
Itibari ya Hadithi za Kitabu Hiki
Kuhusiana na itibari ya hadithi za al-Kafi kuna mitazamo miwili:
Baadhi ya wanazuoni kama vile Muhaddith Nouri, wanaona hadithi zote za al-Kafi kuwa ni sahihi na hazihitaji kuhakikiwa kwa mujibu wa elimu ya Rijaal na wanataja sababu kama vile nafasi nzuri ya kitabu cha al-Kafi na mwandishi wake mbele ya wanachuoni, na pia uwepo wake katika kipindi cha Ghaiba Ndogo na uwezekano wa kuchunguzwa hadithi zake na Manaibu na wawakilishi wa Imamu wa Zama. [27]
Mkabala na wao kuna kundi la wanazuoni wametia doa sababu hizi na wakasema kuwa, hakukuweko na mawasiliano baina ya Shekhe Kulayni na Manaibu wa Imamu na kwa hiyo hakunukuu hadithi kutoka kwao na kama kitabu hiki kiliwasilishwa basi jambo hilo lingeashiriwa katika utangulizi wa kitabu. Kwa upande mwingine, baadhi ya wapokezi na vyanzo vya Kafi vimechukuliwa kuwa dhaifu kwa mtazamo wa elimu ya Rijaal na, na kwa hiyo, riwaya za Kitabu cha Kafi haziwezi kuzingatiwa bila ya kuhitaji uhakiki wa elimu ya Rijaal. [28]
Sherhe (Ufafanuzi) za al-Kafi
Katika duru za mwanzo kitabu cha al-Kafi kilizingatiwa mno na Wanazuoni na watafiti wa elimu ya hadithi. Kwa muktadha huo kukafanyika kazi nyingi kuhusiana na kitabu hiki. Agha Bozorg Tehran ameandika sherhe 27 katika kitabu chake cha al-Dhariah na akatambulisha sehemu ya Usul al-Kafi au kitabu chote na kuandika ufafanuzi ambao idadi yake inafikia 10. [28]
- Ufafanuzi wa Mulla Sadra, aliaga dunia 1050 Hijria.
- Kitabu cha al-Wafi cha Faydh al-Kashani aliyeaga dunia 1091 Hijria.
- Kitabu cha Mir'at al-'uqul cha Al-Allama al-Majlisi, aliyeaga dunia 1110 Hijria.
- Sherhe ya al-Kafi ya Mulla Salih Mazandarani, aliyeaga dunia 1110 Hijria.
- Sherhe ya al-Kafi ya Mulla Khalil Qazwini kwa lugha ya Kifarsi inayojulikana kwa jina la “Swafi” na sherhe ya lugha ya Kiarabu inayojulikana kwa jina la “Shafi”.
- Al-Rawashih al-samawiyyah fi sharh al-Kafi kilincoandikwa na Seyyid Muhammad Baqir Mirdamad
- Shehr ya Amir Isma'il Khatunabadi.
- Manhaj al-Yaqin kilichoandikwa na Alaauddin Muhammad Golstaneh. [29]
Rejea
Vyanzo