Amr bin Abd Wudd

Kutoka wikishia

Amr bin Abd Wudd au Amr bin Abd Wadd (Kiarabu: عمرو بن عبد وُدّ) (aliuawa mwaka wa 5 Hijiria) anatambulika kuwa mpiganaji shujaa wa Makureshi ambaye aliuawa na Imamu Ali (a.s) katika Vita vya Khandaq. Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi Mtume (s.a.w.w) amesema: Pigo la Ali bin Abi Talib (a.s) siku ya Khandaq ni bora zaidi kuliko ibada ya binadamu wote na majini wote. Ibn Taymiyyah, mwanazuoni wa Ahlu Sunna na muasisi wa Usalafi amekana juu ya uwepo wa Amr bin Abd Wudd. Baadhi ya wahakiki wanasema kuwa, sababu ya Ibn Taymiyyah kufanya hivyo ni kukana fadhila za Imamu Ali (a.s).

Kwa mujibu wa riwaya kutoka katika kitabu Manaqib Aal Abi Talib, kilichoandikwa na Ibn Shahrashub, Imam Ali (a.s) alipokuwa akipigana na Amr bin Abd Wudd, baada ya Amr kumtemea mate usoni, aliacha kupigana kwa dakika chache ili hasira zake, zishuke na kisha akamuua Amr.

Kuuawa katika Vita vya Khandaq

Kuhusiana na kuzaliwa na maisha ya Amr bin Abd Wudd, hakuna habari katika vyanzo vya kihistoria na hadithi, ghairi ya kuwa alikuwa anatoka katika kabila la Bani Amer bin Lu’y tawi la Kureishi. [1] Imekuja katika vyanzo vya Kishia na Kisunni ya kwamba, katika Vita vya Ah’zab (Khandaq) katika mwaka wa tano wa Hijiria, akiwa pamoja na Ikrimah bin Abi Jahl, Hubayra bin Abi Wahab, Nufil bin Abdullah bin Mughirah na Dhirar bin Khattab, alifanikiwa kuvuka kwa shida Khandaq lililokuwa limechimbwa na Waislamu. [2] Amr bin Abd Wudd, ambaye alikuwa shujaa wa tatu wa Wakureshi, [3] na alihesabiwa kuwa sawa na wapiganaji elfu moja, [4] alijitokeza na kutamba mbele ya wapiganaji wa Kiislamu na akawadhalilisha na akasema: Nimechoka kupiga kelele kwa ajili ya wapiganaji miongoni mwenu. [5] Kwa mujibu wa vyanzo, Ali bin Abi Talib, baada ya kila mara kutamba Amr bin Abd Wudd, alikuwa akisimama na kutangaza kuwa tayari kupigana naye; lakini kwa ombi la Mtume, aliketi; mpaka Mtume alipomruhusu Imam Ali (a.s) kupigana na akamfunga kilemba chake kichwani na akampa upanga wake kwa ajili ya kupigana na Amr. [6]

Pigo la Imamu Ali (a.s)

Imam Ali (a.s) kwanza alimlingania Amr bin Abd Wudd juu ya kushuhudia kwamba, Mwenyezi Mungu ni mmoja (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) na risala ya Utume, na baada ya kukataa, alimtaka aondoke na kurejea kwa njia ile ile aliyokuja nayo, na alipokataa, alimwambia ashuke kwenye farasi wake ili wapigane, naye akakubali na hata kwa mujibu wa riwaya ya Ibn Abi al-Hadid alimfuatilia farasi wake [7] au kwamba alimpiga farasi wake usoni na farasi akakimbia [8]. Kwa mujibu wa riwaya ya Jabir bin Abdullah Ansari, ambaye alikuwa pamoja na Imam Ali (a.s), mapigano kati ya Ali bin Abi Talib na Amr bin Abd Wudd yalipamba moto, mpaka Imamu Ali alipotoa sauti ya takbira na Waislamu wakatambua kuwa, Amr bin Abd Wudd alikuwa ameuawa. [9] Jabir bin Abdullah, ambaye alishuhudia tukio hili, alifananisha kutoroka kwa washirikina wengine baada ya kifo cha Amr na kuuawa kwa Jalut na Daudi na kushindwa kwa jeshi la Jalut. [10]

Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria, mbali na Amr bin Abd Wudd, mwanawe Hisl pia aliuawa na Imam Ali (a.s). [11] Baadhi ya ripoti zinasema kwamba, baada ya kumuua Amr bin Abd Wudd, Imam Ali (a.s) aliweka kichwa chake mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ambapo katika hali hii Abu Bakr na Umar walisimama na kuubusu uso wa Ali (a.s) na Mtume (s.a.w.w) ambaye furaha yake ilikuwa dhahiri usoni mwake akasema: Huu ni ushindi (wa kweli) au akasema: Huu ni ushindi wa kwanza na haiba ya washirikina imesambaratika na kuanzia sasa hawatapigana nasi tena, bali sisi ndio tutakaopigana nao. [12]

Kwa mujibu wa yaliyotajwa katika kitabu Manaqib Aal Abi Talib, kilichoandikwa na Ibn Shahrashub Mazandarani (aliyefariki dunia 588 Hijiria) akinukuu kutoka kwa Imam Ali (a.s), Amr Ibn Abd Wudd alimtemea mate usoni Imamu Ali wakati wanapigana na Imam Ali (a.s), ili kuepusha kumuua Amr bin Abd Wudd kwa hasira na ghadhabu, alimwacha kwa dakika chache na baada ya hasira zake kushuka, akamuua Amr katika njia ya Mwenyezi Mungu. [13]

Katika vyanzo vya hadithi imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwamba, pigo la Ali (a.s) dhidi ya Amr bin Abd Wudd katika Vita vya Khandaq ni bora zaidi kuliko ibada ya majini na wanadamu. [16] Katika baadhi ya hadithi, katika vyanzo vya Ahlu Sunna imenukuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwamba, baada ya pigo la Imam Ali (a.s) kwa Amr, alimwambia: Ewe Ali, bishara njema ziwe juu yako, kwamba pigo lako la leo ni bora zaidi kuliko amali za Umma wangu. [17] Na katika riwaya nyingine ya Hakim Nishaburi, katika al-Mustadraa Ala al-Sahihein, amenukuu kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwamba, pigo la Ali (a.s) ni bora zaidi kuliko amali za umma wangu mpaka Siku ya Kiyama. [18] ] Imam Ali (a.s) baada ya kumuua Amr Ibn Abd Wudd hakuchukua chochote kutoka katika vitu vyake binafsi. Walipomuuliza kwa nini hukufanya hivyo na hukuchukua vazi lake la nyuma ambalo halikuwa na mfano Uarabuni, alisema: Nilikuwa na haya kufichua ubaya wa mwili wa binamu yangu. [19] Dada yake Amr pia baada ya kufahamu kuhusiana na hilo alisema: Sitajuta kamwe kwamba ndugu yangu aliuawa, kwa sababu aliuawa na mtu mtukufu na kama ingekuwa vinginevyo, ningelilia madhali ni hai. [20]

Kutilia shaka uwepo wa Amr

Ibn Taymiyyah, mwanachuoni wa Kisunni na mwanzilishi wa Usalafi, ametilia shaka kuwepo kwa Amr bin Abd Wudd; [21] kwa mujibu wake ni kuwa, hakuna alama yoyote ya jina la Amr bin Abd Wudd katika vita vya Badr na Uhud na vile vile katika vita vingine na kile ambacho kimenukuliwa kumhusu katika Vita vya Khandaq hakijaja katika chanzo chochote kile cha Sahihayen yaani katika Sahih Muslim na Sahih al-Bukhari. [22] Pamoja na hayo, kuwepo kwa Amr bin Abd Wudd katika vita vya Khandaq kumetajwa katika vyanzo vya kihistoria kama vile Tarikh al-Tabari [23] na Tarikh al-Islam Dhahabi [24] na Hakim Naishaburi, mmoja wa wanazuoni wa Kisunni, katika kitabu cha al-Mustadrak Ala al-Sahihein, amenukuu hadithi inayoonyesha kuwepo kwa Amr bin Abd Wudd katika Vita vya Badr na kujeruhiwa kwake. [25] Pia, katika vyanzo vya historia, kuna mashairi yaliyonukuliwa ya Hassan bin Thabit, sahaba wa Mtume, kuhusu kujivunia kuuawa kwa Amr na Imam Ali, [26] na pia kumenukuliwa mashairi katika maombolezo yake kutoka kwa Musafi’ bin Abd Manaf na[27] Hubayra bin Abi Wahab [28] waliofuatana na Amr bin Abd Wudd katika kuvuka handaki [29] na dada yake Amr [30].

Baadhi ya wahakiki wanasema kuwa, sababu ya Ibn Taymiyyah kufanya hivyo ni kukana fadhila za Imamu Ali (a.s). [31]

Vyanzo

  • ʿĀmilī, Jaʿfar Murtaḍā al-. Al-Ṣaḥīḥ min sīrat al-nabīyy. Qom: Dār al-Ḥadīth, 1426 AH.
  • Dhahabī, Muḥammad b. Aḥmad al-. Tārīkh al-Islām wa wafayāt al-mashāhīr wa l-aʿlām. Edited by ʿUmar ʿAbd al-Salām Tadmurī. Beirut: Dār al-Kitāb al-ʿArabī, 1410 AH.
  • Furūzānfar. Aḥādīth wa qiṣaṣ-i mathnawī. Translated to Farsi by Ḥusayn Dāwūdī, Tehran: Amīr Kabīr, 1387 Sh.
  • Ḥākim al-Niyshābūrī, Muḥammad b. ʿAbd Allah. Al-Mustadrak ʿalā l-ṣaḥīḥayn. Edited by Muṣṭafā ʿAbd al-Qādir ʿAṭāʾ. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1411 AH.
  • Ḥillī, Ḥasan b. Yūsuf al-. Nahj al-ḥaqq wa kashf al-ṣidq. Edited by Faraj Allāh Ḥasanī. Beirut: Dār al-Kutub al-Lubnānī, 1982.
  • Ibn Hishām, ʿAbd al-Malik. Sīrat al-nabīyy. Edited by Muḥammad Muḥyī l-Dīn ʿAbd al-Ḥamīd. Cairo: Maktab Muḥammad ʿAlī Ṣabīḥ, 1383 AH.
  • Ibn ʿAsākir, ʿAlī b. al-Ḥasan. Tārīkh madīnat Damascus. Beirut: Dār al-Fikr, 1415 AH.
  • Ibn Shahrāshūb, Muḥammad b. ʿAlī. Manāqib Āl Abī Ṭālib. Najaf: al-Maṭbaʿa al-Ḥaydarīyya, 1375 AH.
  • Ibn Taymīyya, Aḥmad b. ʿAbd al-Ḥalīm. Manhaj al-sunna al-nabawīyya. Edited by Muḥammad Rashād Sālim. Riyadh: Jāmiʿat al-Imām Muḥammad b. Suʿūd al-Islāmīyya, 1406 AH.
  • Group of Authors. Imām ʿAlī. Qom: Sāzmā-i Ḥajj wa Zīyārat, [n.d].
  • Mahdawī Dāmghānī, Maḥmūd. 1383 Sh. "Maʾkhadh-i khudū andākhtan-i khaṣm bar ḥaḍrat-i ʿAlī (a)." Faṣlnāma-yi Adabīyāt-i Farsī 1, 2:60-66.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Al-Irshād fī maʿrifat hujaj Allāh ʿalā l-ʿibād. Edited by Muʾassisat Āl al-Bayt li-Iḥyāʾ al-Turāth. Qom: al-Muʾtamar al-ʿĀlamī, 1413 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārīkh al-umam wa l-mulūk. Beirut: Dār al-Turāth, 1387 AH.