La Hukma Illa Lillah

Kutoka wikishia

La hukma Illa Lillah (Kiarabu: لا حكم إلا لله) (Hakuna hukumu isipokuwa hukumu ya Mwenyezi Mungu) hii ilikuwa kaulimbiu ya Makhawariji katika kupinga hukumu katika vita vya Siffin. Makhawariji wakitumia nara na kaulimbiu hii, katika hatua ya kwanza, walitangaza upinzani wao dhidi ya hukumu ya mwanadamu na hawakukubali usuluhishi na hukumu ya Abu Musa Ash'ari na Amr bi al-A’s, ambao waliteuliwa kuwa mahakimu na Imam Ali (a.s) na Mu'awiyah, na wakasema kwamba utoaji hukumu ni wa Mwenyezi Mungu pekee na hakuna mtu mwingine yeyote mwenye haki ya kutoa hukumu.

Imam Ali (a.s) aliichukulia kaulimbiu hii kuwa ni kauli ya kweli, lakini imekusudiwa maana batili ndani yake. Aliona kuwepo kwa mtawala, awe mzuri au mbaya, ni muhimu kwa ajili ya kusimamia jamii.

Kauli mbiu hii iliendelea kutumiwa na Makhawariji hata baada ya vita vya Nahrwan na ilitambuliwa kama moja ya misingi yao ya kidini na ilitumiwa katika harakati zao zilizofuata.

Baadhi ya watafiti wametambua kwamba, ufahamu potofu na usio sahihi, ubedui wa Makhawariji na kutodiriki na kutofahamu kwao kwa usahihi maana ya Uimamu na siasa, ni mambo yaliyokuwa na  taathira katika kuundika mtazamo na ufahamu potovu wa kaulimbiu ya “La Hukma Illa Lilllah”.

Utambuzi wa maana

“La Hukma Illa Lillah” ilikuwa kaulimbiu ya Makhawariji katika kumpinga na kukabiliana na Imam Ali (a.s) [1] ambapo kutokana na kutumia nara na kaulimbiu hii waliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Muhakkamah. [2] Maana ya Hukm katika kauli mbiu hii imetambuliwa kuwa ni “kutoa hukumu” kwa maana kwamba, hakuna awezaye kutoa hukumu isipokuwa Mwenyezi Mungu. [3] Nara na kaulimbiu hii imechukuliwa kutoka katika maneno ya Qur'an:

لا حکم الا لله
Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu

Kaulimbiu ambayo imerudiwa katika Aya kadhaa za Qur'an. [4] Baadaye makusudio ya ibara na maneno hayo ikawa ikitumiwa katika mazungumzo ya Makhawariji kukataa kila mamlaka na utawalishaji isipokuwa wa Mwenyezi Mungu. [5]

Matumizi ya awali

Matumizi ya kwanza ya kaulimbiu ya "La Hukma Illa Lillah" yalikuwa ni kwa wale waliopinga hukumu ya awali na usuluhishi katika Vita vya Siffin; wakati jeshi la Sham lilipokaribia kushindwa katika vita, kwa hila za Amr bin As, walitundika Qur'an juu ya mikuki na kutaka usuluhishi na hukumu ya Qur’an. [6] Imamu Ali (a.s) alikubali hilo kutokana na kung’ang’ania watu wake wa karibu ambapo alimuandikia barua Muawiyyah na kumueleza hilo. [7] Hatimaye, maafikiano yaliandikwa na masharti ya hukumu yakaanishwa.[8]

Wakati Ash'ath bin Qays Kindi alipokuwa akisoma waraka wa makubaliano ya awali kwa makabila mbalimbali, kuliibuka malalamiko katika mhimili wa “La Hukma Illa Lillah”; vijana wawili wa kabila la Anzah walijitokeza na kutoa nara ya “La Hukma Illa Lillah” na wakalishambulia jeshi la Muawiyah na wakauawa jirani na hema la Muawiyah. [9] Baadhi wanaamini kwamba vijana hawa wawili walikuwa wa kwanza kutumia kaulimbiu ya “La Hukma Illa Lilllah.” [10] Baada ya tukio hili, Ash’ath alienda karibu na kabila la Murad na kuwasomea pia waraka wa mapatano hayo. Saleh bin Shaqiq, mmoja wa wazee wa kabila hilo, alitumia kaulimbiu ya “La Hukma Illa Lillah” katika kujibu mapatano haya. [11] Tukio kama hilo lilitokea katika kabila la Bani Rasib [12].

Upinzani dhidi ya hukumu kwa kutumia neno “La Hukma Illa Lillah” haukuishia kwenye malalamiko na upinzani wa ulimi tu, kwani wakati Ash'ath alipofika kwa kabila la Bani Tamim, watu wa kabila hili walimshambulia kwa kauli mbiu ya “La Hukma Illa Lillah” na wakampiga farasi wa Ash’th. [13] Al-Baladhuri, mwandishi wa Ansab al-Ashraf, anaamini kwamba, kauli mbiu iliyotajwa ilisikika kwa mara ya kwanza kutoka kwa kabila hili; [14] lakini Yaqoubi, mwanahistoria wa karne ya tatu Hijria, anaamini kwamba, kwa mara ya kwanza kaulimbiu ilitolewa, kabla ya kukutana majaji wawili na mtu aliyejulikana kwa jina la Urwa bin Adiya Tamimi. [15]

Kubadilika na kuwa kaulimbiu ya Makhawariji

Baada ya kuandikwa barua ya utoaji hukumu katika vita vya Siffin mnamo tarehe 17 Safar mwaka wa 37 Hijiria, [16] jeshi la Imam lilirudi Kufa; lakini baadhi ya watu ambao baadaye walikuja kujulikana kama Makhawariji walijitenga na jeshi la Imam Ali kwa kaulimbiu ya "La Hukma Illa Lillah" na wakakaa Harura karibu na Kufa na wakakataa kurejea Kufa. [17] Na hata kutishia kwamba, kama Imamu hatakubali kubadilisha uamuzi wa kukubali usuluhishi na hukumu watamchukia na kupigana naye.[18]

Wakiegemea kauli mbiu ya “La Hukma Illa Lillah” walitoa mwito wa kuacha usuluhishi na hukumu ya watu binafsi katika masuala ya dini, [19] kuvunja agano na Mu’awiyah na kuendeleza vita naye. [20] Walidai kwamba walitubia dhambi ya kukubali hukumu na Imam Ali (a.s) na wakawahesabu Waislamu wengine kuwa ni watenda dhambi na makafiri na wakawataka watubie, vinginevyo wataingia vitani nao. [21] Hii ni katika hali ambayo, tangu awali Imamu Ali alikuwa akipinga kukubali hukumu hiyo na alikubali hilo kwa lazima na kwa vitisho vya masahaba zake wakiwemo watu ambao baadaye walijunga na Makhawariji na hakuwa tayari kuvunja agano baada ya kukubali usuluhishi na hukumu.[22] Ibn Kuwaa, mmoja wa viongozi wa Makhawariji, alikuwa akiunga mkono usuluhishi hapo mwanzoni na alikuwa mmoja wa watu waliopinga uwakilishi wa Abdullah bin Abbas kama kamanda wa jeshi la Kufa na akamtwisha Abu Musa Ash'ari kwa Imamu; [23] lakini baadaye akiwa pamoja na Shabath ibn Rabi’ Tamimi akawa miongoni mwa watu ambao walizungumzia suala la utawala na hukumu ya Mwenyezi Mungu kwa kaulimbiu ya “La Hukma Illa Lillah” (Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu). [24]

Mjadala na Imamu Ali (a.s)

Makhawariji walikuwa wakijadiliana na kubishana na Imamu Ali (a.s) katika matukio mbalimbali wakitegemea nara hii. Kwa mfano, Abu Musa al-Ash’ari alipochaguliwa kuwa hakimu, watu wawili kutoka kwa Makhawariji walioitwa Zareh bin Al-Barj Ta’i na Hurqus bin Zuhair Sa’di walikuja kwa Imam Ali (a.s) na kutoa nara na  kaulimbiu isemayo “Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu” na wakamtaka Imam atubie matendo yake na aende kupigana na Muawiya. Imam pia aliwakumbusha juu ya kutimiza ahadi na hakukubali ombi lao. [25]

Katika matukio mengine kadhaa, Makhawariji walimsumbua na kumuudhi Imamu Ali (a.s) kwa kauli mbiu hii; kiasi kwamba, wakati Imamu alipokuwa akielekea msikiti wa Kufa kutoa khutba, mtu mmoja karibu na msikiti huo alitamka kauli mbiu ya “La Hukma Illa Lilllah” na wengine kadhaa wakarudia sentensi hiyo hiyo. [26] Kadhalika wakati Imamu Ali (a.s) alipokuwa akitoa hotuba katika msikiti wa Kufa, Makhawariji walikatiza hotuba yake mara kadhaa kwa kaulimbiu hii. [27] Na suala hili lilikaririwa mara kadhaa baadaye [28].

Mabadiliko ya ufahamu wa kaulimbiu

Makhawariji ambao hapo mwanzo, kwa kaulimbiu ya La Hukma Illa Lillah, waliichukulia hukumu na maamuzi kuwa ni ya Mwenyezi Mungu pekee, baada ya muda fulani walikusudia maana nyingine na wakaamini kwamba, serikali na utawala ni wa Mwenyezi Mungu tu na hakuna yeyote iwe ni Ali (a.s) au Mu'awiyah ambaye ana haki ya kutawala. Kwa hatua yao hii walikuwa wakitaka jamii isiyo na utawala. [29]

Ayatullah Sobhani, katika kitabu chake cha Al-Insaf fi Masail Dama fiha al-Khilaf anaamini kwamba, ulazima wa serikali hauhitaji kutoa ushahidi; kama ambavyo umuhimu wake umetajwa katika riwaya za Mtume (s.a.w.w) na Maimamu Maasumu [30]. Ili kuhifadhi tawhidi na utawala wa Mwenyezi Mungu, kwa ufahamu potofu na usio sahihi waliuona utawala wowote wa mwanadamu kuwa ni batili na wakatangaza kuwa utawala ni wa Mungu peke yake. [31] Baadhi ya watafiti wengine wanaamini kwamba, wengi wa Makhawaariji walitokana na Mabedui ambao hawakuwa na ufahamu wa kimsingi na sahihi wa Uimamu na siasa kama suala ambalo ni zaidi ya ukabila, na kwa hiyo walionyesha mielekeo yao katika mfumo wa tafsiri potovu ya kaulimbiu ya: "La Hukma Illa Lillahi". [32]

Msimamo wa Imamu Ali (a.s)

Katika kujibu madai yao kwamba, watu wametawala katika dini ya Mwenyezi Mungu, Imam Ali (a.s) alisema kuwa kuwaweka watu kutawala kwa misingi ya Qur’an haimaanishi kuwatawala watu katika dini ya Mwenyezi Mungu. [33] Vile vile alisema, kwamba hiki ni kitendo ambacho hakuna njia ya kukiepuka; kwa sababu Qur’an yenyewe haiwezi kusema. Mara moja katika mjadala na Makhawariji, alichukua Qur’an pamoja naye na akaiambia: “Ewe Quran, kuwa mwamuzi”. (toa hukumu) Makhawariji wakasema kuwa, Qur’an haisemi. Imamu akajibu, unatarajiaje Qur'ani itawale miongoni mwa watu bila ya uingiliaji wa mwanadamu? [34]

Imam Ali (a.s) alichukulia nara ya “Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu” kuwa ni  msemo wa kweli, ambao umekusudiwa batili. Alipinga rai ya Makhawariji kwamba utawala ni mahususi kwa Mwenyezi Mungu aliwapa changamoto kwa namna ambayo watu walilazimika kuwa na mtawala, awe ni mtu mwema au mhalifu. Aliona kuwepo kwa serikali kuwa ni jambo la lazima ili kuleta nidhamu na utulivu na kuwanufaisha waumini na hata makafiri, na kupanga mambo na usalama. [35] Radiamali na jibu la Imamu Ali (a.s) kwa nara na kaulimbiu ya “La Hukma Illa Lillah” imetajwa katika khutba ya 40 ya Nahj al-Balagha.[36]

Ingawa majadiliano ya Imam Ali (a.s) na Makhawariji [37] yalipelekea kurejea kwa watu elfu nne [38] au Makhawariji wote [39]; lakini baada ya kutokuwa na natija kisa cha utawala bado walikuwa wakisisitiza kwamba, Imamu Ali (a.s) anapaswa kuhesabiwa kuwa ametenda dhambi na ni kafiri na ni kwa sababu hii, ndio maana walikataa kuandamana na Imam Ali (a.s) na jeshi la Kufa kuendeleza vita na Muawiya. [40] Walikusanyika katika nyumba ya Abdallah bin Wahab al-Rasibi [41] na kujiandaa kwa ajili ya vita dhidi ya Imamu Ali na hatimaye walishindwa katika vita vya Nahrawan.[42]

Kutumiwa nara hii baada ya vita vya Nahrawan

Nara na kaulimbiu ya “La Hukma Illa Lillah” (Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu) iliendelea kubakia kama moja ya nembo muhimu za Makhawariji na baadaye Ibn Muljam al-Muradi alitumia ibara hii hii kama hoja wakati wa kumpiga upanga Imamu Ali (as). [43] Baada ya miaka mingi pia, kaulimbiu hii ilikuwa ikitambuliwa kama moja ya misingi yao ya kiitikadi [44] na ilikuwa ikitumiwa katika harakati zao. [45]