Nenda kwa yaliyomo

Salih al-Mu'minin

Kutoka wikishia

Swalih al-Mu'minin (Kiarabu: صَالِحُ الْمُؤْمِنِينَ) maana yake ni waumini bora au waumini wema. Swalih al-muminin ni neno la Qur’an lililochukuliwa kutoka katika aya ya nne ya Surat al-Tahrim. Katika aya hii, swalih al-mu'minin anatambulishwa kuwa ni mtu anayemuunga mkono Mwenyezi Mungu pamoja na Mtume wa uislamu(s.a.w.w), Jibril na Malaika wengine.

Baadhi ya wafasiri wamelichukulia neno hili kuwa ni la umoja na kielelezo chake kinarejelea mtu mmoja tu, huku wengine wamelichukulia kuwa ni neno la jumla na linajumuisha waislamu wote wachamungu. Katika mtazamo wa kwanza, wafasiri wa kishia wanamchukulia Imam Ali(a.s) kama kielelezo pekee cha neno hilo, na katika mtazamo wa pili wanachukulia waislamu wote wachamungu ndio kielelezo bora zaidi. Egemeo na ushahidi wa kundi hili ni riwaya ambazo zimesimuliwa katika vyanzo vya Shia na Sunni ambazo zimezingatia ya kuwa Imam Ali(a.s) ni kielelezo pekee cha waumini wema.

Utambuzi wa maana (conceptology)

Neno hili swalih al-muuminin lina maana ya waumini wema kabisa na waja bora na wastahiki. [1] Baadhi ya wafasiri wanaona kuwa, neno swalih lililokuja katika mpangilio tajwa ni jina lenye maana jumla. [2] na hivyo wakafikia natija hii kwamba, linajumuisha waumini wote wema wenye taqwa na imani kamili. [3] Mkabala na hao, baadhi wamepinga neno hilo kuwa jumuishi na badala yake wanaamini kuwa, neno hilo linamhusu mtu mmoja tu. [4] Allama Muhammad Hussein Tabatabai, mfasiri mkubwa wa Qur’an tukufu ni miongoni mwa wanazuoni ambao wanapinga kwamba, neno hilo lina maana jumuishi. Allama Tabatabi anasema: Swalih al-muuminina ni tofauti na al-swalih minal-muuminina(صالح المؤمنین) na kwamba, al-Swalih Minal-Muuminina(الصالح من المؤمنین) ina maana jumuishi lakini swalih al-muuminin haitoi maana jumuishi. [5]

Aya ya waumini wema

Neno swalih al-muuminin (Waumini wema na bora kabisa) limechukuliwa kutoka katika Aya hii: ﴾ إِنْ تَتُوبَا إِلَى اللَّهِ فَقَدْ صَغَتْ قُلُوبُكُمَا ۖ وَإِنْ تَظَاهَرَا عَلَيْهِ فَإِنَّ اللَّهَ هُوَ مَوْلاَهُ وَجِبْرِيلُ وَصَالِحُ الْمُؤْمِنِينَ ۖ وَالْمَلاَئِكَةُ بَعْدَ ذٰلِكَ ظَهِيرٌ ; Kama nyinyi wawili mtatubia kwa Mwenyezi Mungu, basi nyoyo zenu zimekwishaelekea kwenye haki, na mkisaidiana dhidi yake (Mtume), basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye kiongozi wake(mlinzi wake) na Jibrili na waumini wema na zaidi ya hayo Malaika pia watasaidia ﴿. [6] Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana aya hii inatambulika kwa aya ya swalih al-muuminin. [7]

Sababu ya kushuka kwake

Kuhusiana na sababu ya kushuka Aya hii ya Swalih al-Muuminin kuna hadithi zilizonukuliwa zinazoelezea kuudhiwa Bwana Mtume(s.a.w.w) na wake zake. [8] Kwa mujibu wa hadithi hizi Mtume alikwenda kwa mmoja wa wake zake akiwa amekula asali na harufu ya asali ikawa imebakia. Bibi Aisha akiwa pamoja na baadhi ya wake wengine wa Bwana Mtume walichukua uamuzi wa kuwa mbali (kujitenga) na Mtume(s.a.w.w) atakapokwenda kwao kwa kisingizio cha kuwa ana harufu mbaya ya asali aliyokula. Baada ya kuamiliana hivyo na Mtume, mbora huyo wa viumbe aliamua kujiharamishia asali. Imekuja katika baadhi ya hadithi kwamba, Mtume aliamua kujitenga na wake zake na alikata shauri kuwapa talaka. Baada ya muda zikashuka baadhi ya Aya katika Surat al-Tahrim zikimzuia Mtume kujiharamishia alicho kihalalisha Mwenyezi Mungu [9]

Aya hii inawataka wake za Mtume watubu kutokana na kumuudhi Mtume na kuwaonya kwamba, kama watang’ang’ania na uamuzi wao wa kumuudhi Mtume, basi watambue kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye kiongozi, mlinzi na msimamizi na katika kila hatari inayomkabili basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye kiongozi wake(mlinzi wake) na Jibrili na waumini wema na zaidi ya hayo Malaika pia watasaidia. [10]

Swalih al-muuminin( muumini mwema) ni nani?

Kuhusiana na kielelezo na mfano wa Swalih al-Muuminin kuna hitilafu za kimitazamo baina ya wafasiri wa Kishia na Kisuni. Baadhi ya vielelezo na mifano ya hilo inayoingia katika neno hili na ambayo imetajwa ni:

  • Imamu Ali bin Abi Twalib(a.s): Kwa mujibu wa Allama Muhammad Baqir Majlisi [11] Maulamaa wa kishia na kama alivyosema Allama Hilli [12] ni kwamba, wafasiri wana mtazamo mmoja kwamba, Swalih al-Muuminin ni Imamu Ali(a.s). Ushahidi wao ni hadithi zilizoko katika vitabu vya Kishia [13] na vya Kisuni [14] ambapo zinamtambulisha Imamu Ali(a.s) kama kielelezo na mfano pekee wa hilo. Kuhusiana na sababu ya hilo wanasema kuwa, Swalih al-Muuminin (mja mwema miongoni mwa waumini) lazima awe katika waumini wema na bora kabisa [15] na awe Maasumu (asiyetenda dhambi); kwa sababu hilo limekuja na kuambatanishwa na Jibril na Malaika wengine. [16] Allama Muhammad Hussein Tabatabai, mfasiri mkubwa wa Qur’an Tukufu wa kishia anasema kuwa, Imam Ali ni mfano na kielelzo pekee cha Swalih al-Muuminin. [17]
  • Waislamu wote wachamungu: Ayatullah Nassir Makarim Shirazi, mfasiri wa Qur’an wa kishia amemtambulisha Imamu Ali(a.s) kama kielelezo na mfano kamili kabisa wa hilo. [19] Aidha kama alivyosema al-Alusi, mfasiri wa Qur’an wa kisuni ni kwamba, Ali, Abubakar na Omar ni mifano ya wazi ya waumini wema; hata hivyo, hili haliwahusu wao tu. [20] Alusi mfasiri wa kisuni (alifariki 1270 H) anasema: Ibn Asakir amewatambua Abubakar na Omar kuwa ni vielelezo vya wazi ya waumini bora; [21] kwa sababu mabinti zao wawili yaani Aisha na Hafsa walikuwa ni katika wake za Mtume na walikuwa wakiwazuia wasimuudhi Mtume. [22] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi zilizonukuliwa katika vyanzo na vitabu vya waislamu wa madhehebu ya Suni ni kwamba, Abubakar au Omar wametambulishwa peke yake kwamba, ni vielelezo vya waumini wema na bora. [23] Hata hivyo mapokezi ya hadithi hii yametambuliwa kuwa ni dhaifu. [24]