Nenda kwa yaliyomo

Mkopo:Tabarri

Kutoka wikishia

Tabarri (التبرّي) ni kitendo cha kuchukia na kujitenga na maadui wa Allah na maadui wa vipenzi Vyake. Mizizi ya dhana hii inapatikana katika Qur'ani Tukufu, ambapo neno hili na minyambuliko yake limetumika katika Sura ishirini za Qur'ani.

Washia wanaamini kwamba Uimamu katika uhalisia wake ni wadhifa wa kimungu, ambapo Imamu huteuliwa moja kwa moja na Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sababu anawakilisha mwendelezo wa Ujumbe wa Mungu na ni dhamana ya kulindwa na kubaki kwa ujumbe huo. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikuwa amekwishaainisha utambulisho wa Maimamu wa Ahlu al-Bayt (a.s) watakaokuja baada yake. Kwa hiyo, kutokana na umuhimu wa nafasi ya Uimamu katika Uislamu na hadhi yake, Washia wanaamini kwamba wale waliowazuia Maimamu kutekeleza majukumu yao waliyopewa, au wale waliokuwa wakiwafanyia vitimbi na hila Maimamu wa Ahlu al-Bayt (a.s) kwa sababu ya chuki zao, ni maadui wa Mwenyezi Mungu, na hivyo ni wajibu kuwafanyia Tabarri (kujitenga na kujiepusha nao).


Katika suala hili la wadhifa wa Uimamu, wanachuoni wa Kishia wametegea baadhi ya Aya za Qur'ani ili kuthibitisha madai yao. Mimongoni mwa Aya zinazotumika kuthibisha jambo hilo, kama vile: Aya za 18 na 19 za Suratu Hud, Aya ya 25 ya Suratual-Anfal, na Aya ya 22 ya Suratu al-Mujadilah. Vilevile wametegea Hadithi nyingi zilizopokewa kwa mmiminiko mkubwa kutoka katika vitabu vikuu vya Hadithi vya Ahlu Sunna na Washia, ambazo zimekuja zikieleza daraja na hadhi ya Imam Ali (a.s). Hadithi hizi zimebainisha wazi kwamba mtu yeyote anayejikaribisha na kuwa mfuasi (Muwali) wa Amir al-Mu'minina, basi anakuwa mfuasi wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na anayemfanyia uadui yeye basi huyo anakuwa amemfanyia uadui Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Kwa msingi huu, wametoa ushahidi juu ya wajibu wa kufanya Tabarri (kujitenga) na maadui zake (a.s) na wajibu wa kufanya Tawalli (kuwa na urafiki na kuwafuata) marafiki na wafuasi wake.

Maana ya Tabarri

Neno "Bara'a" (برأ), ambalo ndilo asili ya maneno "Al-Bur'u" (البُرْءِ), "Al-Bara'" (البَرَاءِ), na "Al-Tabarri" (التبرّي), kimsingi linamaanisha: Kujitenga au kujiepusha na jambo lolote ambalo mtu anachukia na hapendi kuwa karibu nalo. Ndio maana husemwa: "Bara'atu minal maradh" (Nimepona/nimejitenga na ugonjwa), au "Bari'itu min fulan" (Nimejitenga na fulani), "Tabarra'atu", na "Abra'atuhu min kadha" (Nimemtoa hatiani/nimemtakasa na jambo fulani), "Barra'tuhu" (nimemuepusha), na mtu huitwa "Bari'un" (Asiye na hatia/aliyejitenga na kasoro), na kundi la watu huitwa "Bura'aau" au "Barii'una" (Waiso na makosa au waliojitenga). Hakika mizizi ya maneno "Bara'a" (برأ) na "Baraya" (برى) inakaribiana sana kimaana, na msingi mmoja unayoyaunganisha maneno haya ni: Kuwa mbali na mapungufu au kasoro, iwe ni katika hatua ya kuumbwa (takuwini) au baada yake.[1]

Na kwa namna hii ndivyo uliyotumika katika dhana ya uumbaji, yaani ukuaji na uumbaji kwa njia maalumu. Hakika uumbaji baada ya ukadiriaji, na kitendo baada ya kutoka katika hatua ya nguvu wezekano (kabla ya kuja katika umbile jengine), ni ukamilishaji wa kitu na ni uondoaji wa pande zote za mapungufu pamoja na udhaifu kutoka katika kitu hicho kilichoko katika hautua ya kiuwezekano. Kwa hiyo, uhalisia wa neno "al-bur'u" na "al-tabri'a" unarejea kwenye ukamilishaji na uondoaji wa athari mbaya za udhaifu; kama ilivyo katika Aya isemayo: "Hakika mimi niko mbali na yale mnayomshirikisha nayo (Mola wenu)" (إِنِّي بَرِي‏ءٌ مِمَّا تُشْرِكُونَ), yaani mimi niko safi na niko mbali kabisa na itikadi au amali hii.[2]


Dalili za kisheria za Tabarri

Tabarri katika Qur'ani Tukufu

Hakika istilahi na mafundisho ya Tabarri yanarejea kwenye mafunzo msingi ya Qur'ani; hii ni kutokana na kuwepo kwa Surah katika Qur'ani Tukufu inayozinduka kwa kutaja suala la kujitenga (Bara'ah) kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w) dhidi ya mshirikina, na Sura hii imepewa jina la "Suratu al-Baraa'ah". Mzizi wa neno Baraa'ah na mnyambuliko wake umetumika katika Sura ishirini tofauti za Qur'ani, na imekuja katika Aya 27 tofauti. Kwa ujumla msamiati huu na mnyambuliko wake umetumika mara thelathini ndani ya Qur'ani Tukufu.[3] Miongoni mwa matumizi hayo ni:

Kufanya Tabarri dhidi ya shirki,[4] na kadhalika kudhihirisha amali ya kujitenga kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w) dhidi ya wapinzani wake, na kujitenga kwa wapinzani wake dhidi yake (s.a.w.w).[5] Qur'ani Tukufu unautaja msamiati wa Baraa'ah na Tabarri katika maana yake ya kilugha kwa sura mbili zifuatazo:

  • Wa kwanza: Ni kujitenga na maadui wa Mwenyezi Mungu na kutoka katika baiah ya mshirikina na makafiri.
  • Wa pili: Ina maana ya kukata mahusiano na kujitenga kabisa na wafuasi wa mrengo wa batili.[6]


Tabarri ndani ya Hadithi

Mtume Mtukufu (s.a.w.w) alisisitiza mno katika Hadithi zake juu ya umuhimu wa Tabarri, na akafafanua kuwa Bara'ah (ambayo ni kuchukia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu) ni miongoni mwa vifungo thabiti zaidi vya Imani (mіn awthaqі urayu al-іman).[7] Vilevile, Imam al-Sadiq (a.s) alibainisha wazi kuhusu wajibu wa kufanya Tabarri dhidi ya wale wanaopingana na dini ya Mwenyezi Mungu, marafiki wa maadui wa Mwenyezi Mungu, na maadui wa marafiki wa Mwenyezi Mungu.[8]

Kadhalika, riwaya mbalimbali zimesisitiza juu ya kuambatana na kushikamana kwa pamoja kati ya dhana ya Tawalli na Tabarri.


Tabarri katika madhehebu ya Kiislamu

Sehemu kubwa ya makundi na madhehebu ya Kiislamu yalikuwa yakiamini suala la Tabarri kwa mujibu wa msisitizo mkubwa wa Qur'ani na hadithi za Mtume juu ya jambo hilo. Hapakuwa na ikhitilafu miongoni mwao kuhusu dhana ya jumla ya Qur'ani kuhusiana na Tabarri, pamoja na udharura na umuhimu wake; hata hivyo, zilitokea ikhitilafu miongoni mwao katika kuainisha mifano halisi ya kufanya uadui dhidi ya Mwenyezi Mungu na vigezo vya kutoka katika dini. Mitazamo ya makundi ya Kiislamu kuhusu nani anayeingia katika kundi la watu wa batili, na pia wanatofautiana kimawazo katika namna ya kukabiliana nao. Kutokana na hali hiyo, Kiislamu waligawanyika mbali mbali, ambapo baadhi yao walipindukia mipaka katika kutoa hukumu ya ukufuru (takfiri) na kupanua wigo wa upotevu, kiasi kwamba baadhi yao waliwachukulia Shia Imamiyyah na Zaidiyyah kuwa ni miongoni mwa makundi ya kikafiri, licha ya kuingia kwao waziwazi chini ya kivuli cha dini ya Kiislamu na kusimama katika safu ya Waislamu.[9] Jambo hili lilifuatiwa na upingamizi mkubwa kutoka kwa wanachuoni na wanateolojia wengi wa Kiislamu.[10]


Tabarri kwa mtazamo wa Shia

Maimamu wa Kishia walilizungumzia suala la Tabarri katika nyakati na matukio tofauti, na wakaichukulia Tabarri katika baadhi ya matukio kuwa ni miongoni mwa mambo ya lazima katika Uislamu na Imani, na miongoni mwa mambo ya wajibu katika sheria. Hii ndio sababu iliyowafanya Washia kuiweka Tabarri pamoja na Tawalli (Kutawalisha na kujenga urafiki na mapenzi) — ambayo ni dhana inayopingana na kutofautiana na dhana ya Tabarri — ndani ya Furuu za Dini na mambo ya wajibu. Maana inayokusudiwa hapa ni kuwa, na kuwa na uadui dhidi ya maadui wa Ahlu al-Bait wa Mtume (s.a.w.w) na kujitenga (kufanya Tabarri) na maadui hao.[11]

Katika historia yote ya Kiislamu, Tabarri imekuwa na mizizi madhubuti ndani ya jamii, ima katika masuala ya kilam (kiitikadi) na kiimani kama vile suala la Uimamu na ukhalifa wa Mtume (s.a.w.w), au katika malengo na migogoro ya kisiasa, na wakati mwingine katika masuala binafsi.[12] Hapa, msingi wa Tabarri ukienda sambamba na msingi wa Tawalli, unapata nafasi ya maalumu na uzito wa kipekee katika madhehebu ya Ushia. Msingi huu unahesabiwa kuwa ni miongoni mwa mafundisho makuu kwa wafuasi wa madhehebu haya.

Washia wanaamini kuwa imani ya Uimamu uliowekwa kwa nass (uteuzi wa kauli ya wazi) ni miongoni mwa Usulu za Dini (Misingi ya Dini), na wanaamini kwamba, Uimamu kwa sharti hili (sharti la kuteuliwa kwa Imam) ni mwendelezo wa Ujumbe wa Utume na ndio mdhamini wa kulinda na kubaki salama kwa Uislamu. Na Maimamu Kumi na Wawili baada ya Mtume (s.a.w.w) ni maasumu (waliohifadhiwa dhidi ya dhambi) na walioteuliwa kutoka upande wa Mwenyezi Mungu, ambapo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) aliwatambulisha, na kila Imam pia alimtambulisha Imam anayefuata. Maimamu (amani iwe juu yao) wanailinda dini dhidi ya upotoshaji wowote, mapungufu, au mabadiliko katika upande wa kiitikadi na hukumu za kifiqhi.[13] Kulingana na itikadi hii, maadui wa Maimamu — yaani wale wanaozuia kudhihirika kwa Uimamu na hivyo kuzuia kudhihirika kwa ura safi na ya kweli ya Uislamu, au wale waliokuwa wakiwachukia Ahlu al-Bayt wa Mtume (s.a.w.w) — basi hao ni maadui wa Mwenyezi Mungu na ni wajibu kujitenga (Tabarri) nao.[14]

Wanazuoni na wafasiri wa Kishia, wakitegemewa msaada wa Riwaya nyingi zinazoaminika kutoka katika vitabu vya Hadithi vya Kishia na Kisunni kuhusu Imam Ali (a.s),wamezichukulia baadhi ya Aya za Qur'ani, zikiwemo Aya za 18 na 19 za Suratu Hud, Aya ya 25 ya Suratu al-Anfal, na aya ya 22 ya Suratu al-Mujadilah, kuwa zinahesabu uadui dhidi ya Ali (a.s), kuwa ni sawa na uadui dhidi ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w), jambo linalolazimisha kujitenga (Bara'ah/Tabarri) na maadui zake (a.s).[15]


Wanaopaswa kufanyiwa Tabarri

Qur'ani Tukufu imeashiria katika Sura zaidi ya moja kuhusu suala la kujitenga na Washirikina waabudu masanamu, viongozi wa shirikina, na walinganiaji wa upotovu na mkengeuko, pamoja na kujitenga na vile wanavyoviabudu. Kuna Aya nyingi za Qur'ani zinazotamka wazi kujitenga na watu na amali kadhaa, miongoni mwao ni:

  • Kujitenga na Ushirikina.
  • Kujitenga na ibada ya masanamu.
  • Kujitenga na viongozi wa ushirikina, upotovu, na maabudiwa yao.

Miongoni mwa Aya hizo ni: Baadhi ya Aya za Suratu al-Mumtahanah zinazungumzia kujitenga kwa Nabii Ibrahimu na masahaba zake pale aliposema:

قَدْ كَانَتْ لَكُمْ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ فِي إِبْرَاهِيمَ وَالَّذِينَ مَعَهُ إِذْ قَالُوا لِقَوْمِهِمْ إِنَّا بُرَآءُ مِنكُمْ وَمِمَّا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ كَفَرْنَا بِكُمْ وَبَدَا بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةُ وَالْبَغْضَاءُ أَبَدًا حَتَّىٰ تُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ

"Nanyi mlipata mfano mwema (kutoka) kwa Ibrahimu na wale waliokuwa pamoja naye walipowaambia watu wao: Hakika sisi tumejitenga nanyi na vile mnavyoviabudu badala ya Allah. Tumekukataeni, na uadui na chuki baina yetu na nyinyi zimedhihiri (na zitabaki) milele mpaka mumwamini Allah."[16]

Pamoja na kuzingatia kwamba Mwenyezi Mungu amekataza vikali mwanzoni mwa Sura hii kuwafanya maadui wa Mwenyezi Mungu kuwa ni marafiki na walezi, pia amewaletea Waislamu kiigizo kinachoheshimika ambacho ni Nabii Ibrahimu (a.s) aliyewaambia watu wake ambao ni washirikina:

إِلَّا قَوْلَ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ لَأَسْتَغْفِرَنَّ لَكَ وَمَا أَمْلِكُ لَكَ مِنَ اللَّهِ مِن شَيْءٍ رَّبَّنَا عَلَيْكَ تَوَكَّلْنَا وَإِلَيْكَ أَنَبْنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ

"Isipokuwa (ile) kauli ya Ibrahimu kwa baba yake (isemayo): Hakika nitakuombea msamaha, lakini (pia tambua ya kwamba mimi binafsi) sina uwezo wa kukufanyia lolote mbele ya Allah. Ewe Mola wetu! Kwako Tumekutegemea Wewe, na tumerejea Kwako, na Kwako ndiko kwenye marejeo."[17]

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasisitiza katika Sura hiyo hiyo juu ya udharura wa kufuata nyayo za Ibrahimu na masahaba zake na kuwafanya kuwa mfano bora zaidi kwa Waislamu kwa kusema:

لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِيهِمْ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ ۚ وَمَن يَتَوَلَّ فَإِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ

"Hakika mmepata ndani yao mfano mwema kwa yule anayemtarajia Allah na Siku ya Mwisho. Na anayegeuka (na kumpa kisogo Mola wake), basi hakika Allah ni Mkwasi, Mhimidiwa."[18]

Pia kuna Hadithi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) zinazotubainishia wale ambao ni lazima kujitenge nao. Kwa mfano, katika Hadithi yake akimwambaia Imam Ali (a.s) amesema: "Mimi ni amani kwa yule aliyefanya amani nawe, na ni vita kwa yule aliyepigana nawe," au ile isemayo: "Maimamu baada yangu ni Maimamu kumi na mbili, na mwenye kuwapinga ni sawa na aliyenipinga mimi." Pia maneno ya Mtume (s.a.w.w) kuhusu Imam Ali (a.s), Bibi Fatima (a.s), Imam Hassan (a.s), na Imam Hussein (a.s), yanasema: "Mimi ni vita kwa yule anayepigana nanyi, na ni amani kwa yule anayefanya amani nanyi."[19]

Kadhalika, Maimamu wa Kishia (a.s) walikuwa wakibainisha uhalisia wa watu maalumu, hususa ambao hukumu ya Tabarri inawahusu, kama vile:

  • Wale waliodhulumu kizazi kitakatifu cha Mtume Mtukufu (s.a.w.w) na kuvunja heshima yao.
  • Wale waliobatilisha na kubadilisha sunna ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w) na wale waliowafukuza masahaba wateule wa Mtume (s.a.w.w).
  • Wale waliozigawa mali za mafukara miongoni mwa matajiri.
  • Wale waliopigana vita dhidi ya Maimamu wa Ahlu al-Bayt (a.s).
  • Wauaji wa Imam Ali (a.s) na wauaji wote wa Maimamu na kizazi cha Ahlu al-Bayt (a.s).[20]

Pamoja na kuzingatia kwamba, imani hii ni imani madhubuti kwa Mashia, ila si kila mtu ambaye si Mshia anastahiki kufanyiwa Tabarri, bali wajibu wa Tabarri unawahusu wale tu waliodhihirisha uadui (wakainua bendera ya uadui) dhidi ya Kizazi Kitakatifu cha Mtume (s.a.w.w) kwa mujibu wa ibara za Riwaya na vyanzo vya kifikihi huku wakijua nafsi yao, au wale walioathiriwa na Magulati (itikadi ya kupitiliza mipaka) na wanaoamini uungu wa Imam Ali (a.s) au uungu wa mwanadamu fulani, au mfano wa Mufawwidha[21] ambao walikuwa wakiamini kwamba jambo la uumbaji, utoaji riziki, kuhuisha na kufisha limekabidhiwa kwa Mtume (s.a.w.w) na Imam Ali (a.s).

Hali kadhalika kuna mifano ya watu wanaopaswa kujitengwa nao waliotajwa kupitia ndimi za Maimamu Maasumu (a.s) katika maeneo zaidi pamoja na kuashiria sifa za watu hao. Miongoni mwao ni: Mdhalimu wa kizazi cha Mtume (s.a.w.w) na wavunjaji wa heshima zao; wabadilishaji wa sunna za Mtume; na waliowadhalilisha masahaba wateule na kuwafukuza kutoka katika ardhi zao, na wale waliojimilikisha mali za mafukara na kuzifanya kuwa ni mzunguko miongoni mwa matajiri pekee. Na miongoni mwa wale ambao walotiliwa mkazo kujitenga nao ni: Nakithina (watu wa vita vya Jamal), Qasitina (Muawiya na jeshi lake), na Mariqina (Makhawariji), pamoja na maimamu wote wa ukafiri na upotovu, viongozi wa dhuluma na uonevu, wauaji wa Amirul Muuminin na wauaji wa Maimamu katika kizazi chake na Ahlu al-Bayt wake.[22]


Njia na mitindo ya kudhihirisha Tabarri

Mbinu ya kuonesha na kutangaza wazi Tabarri — iwe katika jamii ya Kishia au ya Kisunni — inaathiriwa na mambo mengi katika upana na ufinyu wake, ikiwa ni pamoja na mchango wa mamlaka na serikali ambazo huendesha mwelekeo wa Tabarri kulingana na maslahi yao; ambao wakitaka hupandisha kiwango cha Tabarri hadi kiwango cha juu kabisa, au kukishusha hadi kiwango cha chini kabisa. Na ni lazima tuelewe kwamba, mwendo na sira ya idadi kubwa ya wanazuoni wa Kishia — katika kudhihirisha Tabarri dhidi ya maadui, ilikuwa ni kwa kiwango maalumu. Hii ni kwa ajili ya cha kufuata nyayo za Imam Ali (a.s) katika kuchunga msingi wa kuimarisha umoja, kudumisha vifungo vya udugu wa Kiislamu, na jitihada za Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu na kuyaweka pamoja.

Kuna ushahidi mwingi juu ya hilo unaoonekana katika sira na wasifu wa maisha ya wanazuoni wakubwa, kama vile Sheikh al-Mufid, Sayyid al-Murtadha, Sheikh al-Tusi, Mirza Hassan al-Shirazi, Mirza Muhammad Hussein al-Naini, Ayatullah Hussein Borujerdi, na Imam Khomeini.

Pia, kuna riwaya kdhaa zinazohimiza kujiepusha na uchochezi wowote ule wa kihisia na kuepuka kuzusha mazingira ya kudhaniana vibaya. Riwaya ambazo zimesaidia sana katika kushikamana na sira hii.[23]

Pamoja na hayo, kuna ushahidi unaoonesha kudhihirishwa kwa Tabarri katika zama za utulivu wa baadhi ya Serikali za Kishia kama vile Aal-Buyah, Wafatimiyya, Wasafawi, Adil Shahi, utawala wa Shahini, na Qutb Shahi.[24]

Kwa upande mwingine, wafuasi wa baadhi ya madhehebu ya Kisunni ya Kisalafi (Uwahabi) walifanya vitendo vya aina yake vya Tabarri, kama vile kushambulia miji ya Kiislamu ya Najaf al-Ashraf na Karbala al-Mualla, kuvunja makaburi ya Maimamu wa Kishia, kuharibu makaburi ya Masahaba, viongozi wakuu wa madhehebu ya Kiislamu, na eneo alilozaliwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w) huko Makkatu al-Mukarramah.[25]

Falsafa ya Tabarri

Irada ya Kiungu imefanya hukumu na sheria za Mwenyezi Mungu ziendane na maumbile asilia ya mwanadamu (fitra). Mwanadamu, pamoja na uwezo wake wa kiutambuzi, ana mihemko, hisia na mwelekeo mbalimbali unaosogea kati ya kukubali na kukataa.

Katika hali ya kawaida, hisia hasi kama ghadhabu, majonzi, kilio na mfano wa hayo, zimeumbwa ndani ya mwanadamu kwa hikma na madhumuni maalumu. Kama zingekuwa hazina hikma yoyote, kuwepo kwake kungeashiria ubatili katika muundo wa kimaumbile wa mwanadamu. Kwa hiyo, kama ambavyo ndani ya mwanadamu kuna mapenzi, pia kuna chuki na uadui; kama fitra ya mwanadamu inavyomvuta kumpenda anayemfanyia wema, vivyo hivyo humfanya achukie na ajitenge na anayemfanyia uovu.

Na jambo la kuzingatia hapa ni kwamba, mwanadamu mwenye imani hatakikani kutumia maslahi yake binafsi, matamanio ya nafsi yake, au masuala ya kimada kama kipimo cha kuamua nani wa kumfanyia Tabarri na nani wa kumfanyia Tawalli. Badala yake, anapaswa kuifanya dini na maadili ya Kiungu kuwa mhimili unaoongoza mwelekeo wake katika pande zote; hii ni kwa sababu jambo hili lina athari kubwa na hatari kwa mustakabali wa mwanadamu na furaha yake ya duniani na Akhera. Uadui na uhasama katika masuala haya unamaanisha kuvutwa kwa mwanadamu kwenda kinyume kabisa na mwelekeo wa Ujumbe wa Kiungu, kama inavyofaidika kauli hiyo kutoka katika aya ya sita ya Surat Fatir:

إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا

"Hakika Shetani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa adui."[26]

Ikiwa kuwapenda vipenzi wa Mwenyezi Mungu ni jambo la lazima, basi vivyo hivyo kuwa na uadui na kujitenga na maadui wa Mwenyezi Mungu ni jambo lisiloepukika. Hili ni hitaji la kimaumbile la mwanadamu (fitra) na ni kichocheo cha kufikia ukamilifu na furaha ya kibinadamu. Iwapo hakutakuwa na "uadui" dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu, taratibu mwenendo wa mwanadamu kuelekea kwao utabadilika na kuwa wa kirafiki; na kutokana na mwingiliano huo, ataathiriwa na tabia zao, atakubali maneno yao na mitazamo yao, na hatimaye kugeuka na kuwa shetani kama wao.

Fuatilia kwamba msimamo wa kujihami dhidi ya maadui hujenga mfumo wa ulinzi ndani ya mwanadamu unaomkinga na hatari pamoja na madhara yanayomkabili. Kama vile mwili ulivyowekewa mifumo miwili ya kuvuta na kutoa — ambapo wa kwanza huvuta vitu vyenye manufaa na vinavyoendana na muundo wa viungo vya mwili, na wa pili hutoa nje vitu vyenye madhara kama vile vijidudu (bacteria) na sumu — vivyo hivyo katika sehemu ya pili ya muundo wa mwanadamu (roho) kuna mfumo wa kuvuta na kutoa. Mfumo huu unatumika kuvuta mambo yanayosaidia ukamilifu wa nafsi na kukurubia makundi yanayosaidia kufikia lengo hili ili kuwafanya kuwa rafiki, kunufaika na elimu yao, ukamilifu wao, kuongoka kwa uongofu wao, na maadili mema waliyonayo.

Kwa upande mwingine, mwanadamu anakuwa na msimamo wa kujiepusha na makundi ambayo yanaweza kumletea madhara. Hivyo, harakati yake inakuwa kati ya kuwapenda wema na mambo mema, na kuchukia pamoja na kuwa na uadui dhidi ya uovu na wale wanaouwakilisha. Hata hivyo, kujitenga huku hakumaanishi kujivua na kuacha jukumu kubwa lililo juu ya mabega ya waumini, ambalo ni kuamrisha mema na kukataza mabaya, kufikisha jumbe za Mwenyezi Mungu, kueneza maadili ya Kiungu miongoni mwa wanadamu, na kuwasaidia waliopotoka kuelekea katika kheri na furaha.

Rejea

  1. ↑ Al-Raghib al-Isfahani, Al-Mufradat fi Gharib al-Qur'an, Uk. 50; Ibn Manzur, Lisan al-Arab, Juzuu 1, Uk. 32.
  2. ↑ Mustafawi, Al-Tahqiq fi Kalimat al-Qur'an al-Karim, Juzuu 1, Uk. 240.
  3. ↑ Mustafawi, Al-Tahqiq fi Kalimat al-Qur'an, Juzuu 1, Uk. 239.
  4. ↑ Suratu al-An'am: 19, 78.
  5. ↑ Suratu Yunus: 41; Suratu al-Shu'ara: 216.
  6. ↑ Tabarsi, Majma' al-Bayan, Juzuu 5, Uk. 3-4.
  7. ↑ Al-Muttaqi al-Hindi, Kanzu al-Ummal, Juzuu 1, Uk. 257; Allamah Majlisi, Bihar al-Anwar, Juzuu 66, Uk. 242.
  8. ↑ Sheikh Saduq, Al-I'tiqadat, Uk. 111.
  9. ↑ Al-Baghdadi, Al-Farqu baina al-Firaq, Uk. 16, 278, 281.
  10. ↑ Kwa mfano tazama: Adhud al-Din al-Iji, Uk. 394-395.
  11. ↑ Sheikh Saduq, Al-I'tiqadat, Uk. 78-81; Lahiji, Sarmaye ye Iman, Uk. 154-155.
  12. ↑ Ibn Abi al-Hadid, Sharh Nahj al-Balagha, Jz. 4, Uk. 54, 56-58.
  13. ↑ Ili kujua zaidi kuhusu nafasi na majukumu ya Uimamu katika hadithi, rejea: Al-Kulayni, Al-Kafi, Jz. 1, Uk. 198-203, Hadithi kutoka kwa Imam al-Ridha (a.s).
  14. ↑ Sheikh Saduq, Al-I'tiqadat, Uk. 81; Lahiji, Sarmayeye Iman, Uk. 154-155.
  15. ↑ Sheikh Saduq, Al-I'tiqadat, Uk. 77-78; Al-Haskani, Shawahid al-Tanzil, Jz. 2, Uk. 329.
  16. ↑ Suratu al-Mumtahanah: 4.
  17. ↑ Suratu al-Mumtahanah: 4.
  18. ↑ Suratu al-Mumtahanah: 6.
  19. ↑ Sheikh Saduq, Al-I'tiqadat, Uk. 78-81 na 125; Al-Hurr al-Amili, Wasa'il al-Shia, Jz. 16, Uk. 177-183.
  20. ↑ Sheikh Saduq, Al-Khisal, Jz. 2, Uk. 607-608; Al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Jz. 10, Uk. 358, Jz. 65, Uk. 263.
  21. ↑ Tafwidh ina maana ya kuamini kuwa Mwenyezi Mungu amekabidhi mambo yote kwa Mtume (s.a.w.w) na Maimamu (a.s) jambo linalopelekea kuondosha nafasi ya Mwenyezi Mungu na ...
  22. ↑ Sheikh Saduq, Al-I'tiqadat, Uk. 71-76; Al-Tabataba'i al-Yazdi, Al-Urwa al-Wuthqa, Jz. 1, Uk. 67-68; Al-Naraqi, Mustanad al-Shia, Jz. 1, Uk. 204.
  23. ↑ Sheikh Saduq, Al-I'tiqadat, Uk. 82.
  24. ↑ Al-Maqdisi, Takmilatu Tarikh al-Tabari, Jz. 1, Uk. 183-187; Ibn al-Jawzi, Al-Muntadham fi Tarikh al-Umam wa al-Muluk, Jz. 14, Uk. 150-151; Ibn Khallikan, Wafayat al-A'yan, Jz. 1, Uk. 407.
  25. ↑ Al-Mahbuba, Madhi al-Najaf wa Haadhiruhaa, Jz. 1, Uk. 324-326; Sayyid Muhsin al-Amin, Kashf al-Irtiyab, Uk. 13-14 na 22-23; Al-Karkukli, Duhat al-Wuzara, Uk. 212.
  26. ↑ Surat Fatir: 6.

Vyanzo

  • Qur'ani Tukufu.
  • Ibn Abi Al-Hadid, Abdul Hamid bin Hibatullah, Sharh Nahj al-Balagha, tahqiq: Muhammad Abu Al-Fadl Ibrahim, Beirut, Dar Ihya al-Kutub al-Arabiyyah, 1378 H.
  • Ibn Al-Jawzi, Abdul Rahman bin Ali, Al-Muntazam fi Tarikh al-Muluk wal-Umam, tahqiq: Muhammad Abdul Qadir Ata na Mustafa Abdul Qadir Ata, Beirut, Dar al-Kutub al-Ilmiyyah, chapa ya 1, 1412 H/1992 M.
  • Ibn Khallikan, Ahmad bin Muhammad, Wafayat al-A'yan wa Anba' Abna' az-Zaman, tahqiq: Ihsan Abbas, Beirut, Dar Sader, 1968–1977 M.
  • Al Mahbubah, Sheikh Jaafar Baqir, Madhi an-Najaf wa Hadiruhu, Beirut, Dar al-Adhwa, chapa ya 2, 1406 H/1986 M.
  • Al-Amin, Muhsin, Kashf al-Irtiyaab fi Atba' Muhammad bin Abd al-Wahhab, Tehran, bila mchapishaji, bila tarehe.
  • Al-Baghdadi, Abdul Qahir bin Tahir, Al-Farq baina al-Firaq, Beirut, Dar al-Kutub al-Ilmiyyah, bila tarehe.
  • Al-Hurr Al-Amili, Muhammad bin Al-Hasan, Wasa'il ash-Shi'ah, Qum, Mu'assasat Aal al-Bait li-Ihya at-Turath, 1410 H.
  • Al-Haskani, Ubaidullah bin Abdullah, Shawahid at-Tanzil li-Qawa'id at-Tafdil, tahqiq: Muhammad Baqir Al-Mahmudi, Tehran, 1411 H/1990 M.
  • Ar-Raghib Al-Isfahani, Al-Husain bin Muhammad, Al-Mufradat fi Gharib al-Qur'an, Beirut, Dar Ihya at-Turath al-Arabi, chapa ya 1, 1428 H/2008 M.
  • As-Saduq, Muhammad bin Ali, Al-I'tiqadat, Qum, Al-Mu'tamar al-Alami li-Alfiyyat ash-Sheikh al-Mufid, bila tarehe.
  • As-Saduq, Muhammad bin Ali, Al-Khisal, Qum, Mu'assasat an-Nashr al-Islami, bila tarehe.
  • Muhammad Kazim At-Tabatabai Al-Yazdi, Al-Urwah al-Wuthqa, Qum, Mu'assasat an-Nashr al-Islami, 1421 H.
  • At-Tabrisi, Al-Fadl bin Al-Hasan, Majma' al-Bayan fi Tafsir al-Qur'an, Qum, Dar al-Ma'rifah, chapa ya 1, 1406 H.
  • Al-Karkukli, Rasul, Dawhat al-Wuzara fi Tarikh Waqa'i Baghdad az-Zawra, Qum, bila mchapishaji, 1372 Sh.
  • Al-Kulaini, Muhammad bin Yaqub, Al-Kafi, tahqiq: Ali Akbar Al-Ghaffari, Tehran, Dar al-Kutub al-Islamiyyah, chapa ya 3, 1388 H.
  • Al-Muttaqi Al-Hindi, Ali bin Husam ad-Din, Kanz al-Ummal fi Sunan al-Aqwal wal-Af'al, Hyderabad, 1384 H/1975 M.
  • Al-Majlisi, Muhammad Baqir, Bihar al-Anwar, Beirut, Dar Ihya at-Turath al-Arabi, 1403 H/1983 M.
  • Al-Majlisi, Muhammad Baqir, Bihar al-Anwar, tahqiq: As-Sayyid Ibrahim Al-Miyanji, Beirut, Dar Ihya at-Turath al-Arabi, chapa ya 3, 1403 H/1983 M.
  • Al-Maqdisi, Muhammad bin Abdul Malik, Takmilat Tarikh at-Tabari, Beirut, 1961 M.
  • An-Naraqi, Ahmad bin Muhammad, Mustanad ash-Shi'ah, Qum, Mu'assasat Aal al-Bait li-Ihya at-Turath, chapa ya 1, 1429 H.
  • Lahiji, Abdul Razzaq bin Ali, Sarmaya-yi Iman, Tehran, 1362 Sh.
  • Hassan Mustafawi, At-Tahqiq fi Kalimat al-Qur'an al-Karim, Tehran, Wizara ya Utamaduni na Uongozi wa Kiislamu, chapa ya 1, 1368 Sh.
  • Ibn Manzur, Muhammad bin Mukarram, Lisan al-Arab, Beirut, Dar Sader, 2003 M.