Nenda kwa yaliyomo

Karbala

Kutoka wikishia
Mji mtukufu wa Karbala katika nchi ya Iraq
Ramani ya mji wa Karbala

Karbala (Kiarabu: كربلاء) au Karbala-e-Mualla ni moja ya miji ya Mashia ya kufanya ziara na kijiografia mji huu upo nchini Iraq. Imam Hussein ibn Ali ibn Abi Twalib (a.s) pamoja na masahaba zake waliuawa kishahidi mwaka 61 Hijiria katika tukio la Karbala katika jangwa la Karbala huko Iraq. Kuuawa shahidi Imamu Hussein (a.s) na masahaba zake katika mji huo na kuweko Haram ya Imam Hussein (a.s) na Haram ya Abul-Fadhl al-Abbas (a.s) ni mambo ambayo yameufanya mji wa Karbala kuwa na umuhimu zaidi kwa waislamu wa madhehebu ya Shia.

Historia ya Karbala inarejea nyuma kabla ya Uislamu na katika zama za Babeli ya kale. Baada ya kukombolewa ardhi na maeneo mbalimbali na Waislamu, pembezoni na Karbala na jirani na mto Furati yalikuwa yakiishi makabila kadhaa tofauti. Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein na masahaba zake katika tukio la Ashura 10 Muharram 61 Hijiria na kuzikwa mwili wake mtukufu katika eneo la Karbala, Waislamu wa madhehebu ya Shia wakawa wakielekea Karbala kwa ajili ya kwenda kulizuru kaburi la mtukufu huyo. Hatua ya Mashia ya kulipa umuhimu suala la kumzuru Imam Hussein na mashahidi wengine wa Karbala, ni jambo ambalo kwa hakika liliandaa mazingira ya kuufanya mji wa Karbala kuwa makazi ya waislamu wa kishia. Kuanzia karne ya pili na ya tatu Hijiria kwa mara ya kwanza misingi ya ujenzi na maendeleo iliwekwa katika mji huo, na kuanza kuonekana ishara za ustawi na maendeleo. Katika kipindi cha utawala wa ukoo wa Buwaih, kulifanyika mambo na kuchukuliwa hatua nyingi kwa ajili ya ujenzi wa mji wa Karbala; hata hivyo mambo mengine ya kuleta ustawi na maendeleo sambamba na kuupanua mji huo yalifanyika zaidi katika kipindi cha tawala za koo za Safavi na Qajar.

Sambamba na hatua za ustawi wa mji wa Karbala, katika karne ya 3 Hijiria, kuliasisiwa shule za kidini katika mji huo. Ustawi wa kielimu katika Hawza ya kielimu (Chuo Kikuu cha Kidini) ya Karbala ulikuwa na hali ya panda shuka katika kipindi chote cha historia. Kwa maana kwamba, kuna wakati kilinawiri ma kipindi fulani kilififia na kudorora. Sambamba na ustawi na kunawiri elimu katika Hawza za Karbala, familia mbalimbali zilielekea Karbala kwa ajili ya kuufanya mji huo kuwa makazi yao lengo ingawa lengo hasa lilikuwa kwenda kusoma na kutafuuta elimu: Miongoni mwa familia hizo ni Aal-Twaama, Aal-Naqib, Bahbahani, Sharistani na Shirazi.

Katika kipindi cha karne mbili za karibuni mji wa Karbala ulishuhudia matukio mbalimbali. Shambulio la kundi la Mawahabi dhidi ya Karbala, shambulio la Najib Pasha liwali na mtawala wa Othmania dhidi ya mji huo, mapinduzi ya 1920 na Intifadha ya Shaabaniyah ni baadhi ya matukio hayo ya karne hizi mbili. Mji wa Karbala katika karne ya 20 baada ya kuanguka utawala wa Ufalme wa Othmania (Ottoman Empire) ulidhibitiwa na kukaliwa kwa mabavu na waingereza. Katika kipindi hiki mji huo ulishuhudia kuanzishwa vyama na vikundi vya kisiasa, kijamii na kiutamaduni na kuongezeka kwake baada ya Iraq kupata uhuru. Miongoni mwa vyama hivyo muhimu vya Mashia vinavyotambuliwa katika mji wa Karbala ni The Committee of Union and Progress, the National Islamic Society, Islamic Da'wa Party in Karbala na tawi la Islamic Supreme Council of Iraq.

Katika minasaba mbalimbali Mashia kutoka maeneo mbalimbali ya dunia hufunga safari na kuelekea katika mji wa Karbala kwa ajili ya kufanya ziara. Kilele cha safari hizi na mahudhurio haya huko Karbala ni katika maombolezo ya mwezi Muharram na Safar (Mfunguo Nne na Mfunguo Tano) hususan katika matembezi ya Arubaini ya Imamu Hussein (a.s). Idadi ya wafanyaziara katika Arubaini ya Imamu Hussein (a.s) iliripotiwa kuwa milioni 20 mwaka 2015 na 2016. Katika kipindi chote cha historia Karbala ilijulikana na kuitwa kwa majina tofauti. Al-Ghadhiriyya, Nainawa, Aqar, Taff, al-Ha'ir, na Nawawis ni miongoni mwa majina hayo.

Utambulisho

Picha mpya ya muonekano wa juu wa Karbala; Baada ya kuanguka kwa utawala wa Baath mwaka 2003, ikiangaza majengo ya mji.

Karbala ni katika miji ya kiziara (ya kufanya ziara) na mitukufu ya Mashia huko Iraq.[1] Mji huu kijiografia uko katikati ya Iraq yapata kilomita 100 kusini magharibi mwa mji mkuu Baghdad.[2] Kuuawa shahidi Imam Hussein (a.s) na masahaba zake katika tukio la Karbala, kuweko Haram ya Imam Hussein na Haram ya Abul Fadhl al-Abbas (a.s) na maeneo mengine ya kufanya ziara, ni mambo ambayo yameufanya mji wa Karbala kuwa mji unaotembelewa zaidi miongoni mwa miji ya ziara ya Mashia hususan katika masiku ya maombolezo ya Muharram na kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein (a.s).[3]

Baada ya utawala wa Othmania kuanguka mwaka 1914 na baada ya kuanguka pia utawala wa dikteta Saddam mwaka 2003, mji wa Karbala ukaondokewa kupata nafasi maalumu ya kisiasa nchini Iraq. Fat’wa ya jihadi ya Ayatullah Muhammad Taqi Shirazi, Marjaa wa Mashia katika mji wa Karbala dhidi ya Uingereza na kuongoza kwake harakati ya 1920 ya wananchi wa Iraq ya kulalamikia kuendelea kuweko Uingereza katika nchi hiyo, ni jambo linalobainisha nafasi muhimu ya kisiasa ya Iraq katika historia ya leo ya Iraq.[4] Baada ya kuanguka utawala wa Saddam pia, misimamo ya Umarjaa wa kidini wa Kishia nchini Iraq kuhusiana na matukio ya kisiasa na kijamii ya nchi hiyo na ya ulimwengu wa Kiislamu hutangazwa katika Swala ya Ijumaa. Kutangazwa fat’wa dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh na Marjaa wa Kishia Ayatullah Sayyied Ali Sistani katika jukwaa na mimbari yya Swala ya Ijumaa Karbala ni miongoni mwa mifano ambayo tunaweza kuiashiria.[5]

Kwa mujibu wa sensa ya watu iliyofanyika mwaka 2015, idadi ya wakazi wa Karbala ilielezwa kuwa ni 700,000.[6] Katika kipindi chote cha historia Karbala ilijulikana na kuitwa kwa majina tofauti. Al-Ghadhiriyya, Nainawa, 'Aqar, Taff, al-Ha'ir, na Nawawis ni miongoni mwa majina hayo.[7]

Historia

Baadhi ya vyanzo vya kale vya historia, vimeitambua Karbala kwamba, inarejea katika zama za kabla ya Uislamu katika kipindi cha Babeli ya kale.[8] Kuna ripoti zilizotolewa ambazo zinaonyesha pia kwamba, kabla ya kuanza harakati ya waislamu kukomboa ardhi na maeneo mengine, Karbala lilikuwa eneo la makaburi ya wakristo na huku wengine wakilitambulisha eneo hilo kuwa, hekalu la moto la Wazartoshti.[9] Tangu kale maeneo ya pambizoni na Karbala hususan maeneo yaliyo jirani na mto Furat yalikuwa na vijiji vingi.[10] Mbali na hayo kuna ripoti mbalimbali zinazoonyesha juu ya kuweko Manabii au kwa uchache baadhi ya Manabii ambao ni watukufu watano kama Nabii Nuhu na Ibrahim (a.s) huko Karbala. Hili linaonekana katika maandiko ya riwaya na hadithi.[11]


Imekuja katika ripoti kwamba, Khalid ibn Walid katika mwaka wa 12 Hijiria wakati wa kujiri vita vya Hira (The Battle of Hira) na baada kudhibitiwa Hira (eneo ambalo hii leo lipo jirani na Najaf ya leo) aliweka kambi katika mji wa Karbala.[12] Baadhi ya nukuuu zinaonyesha kuwa, Imam Ali ibn Abi Twalib (a.s) alipita hapo wakati alipokuwa akirejea kutoka katika vita vya Siffin ambapo inaelezwa kuwa, Imam Ali (a.s) alisimama Karbala kwa ajili ya kuswali na kupumzika na alitoa habari ya tukio la Karbala na matukio ya baadaye yatakayomkumba mwanawe Hussein, masahaba zake na familia yake.[13]

Tukio muhimu kabisa ambalo limeifanya Karbala kuwa mashuhuri na kuwa muhimu kwa Mashia ni tukio la Ashura. Katika tukio hili, Imam Hussein ibn Ali ibn Abi Twalib (a.s) baada ya kukataa kumpa baia na kiapo cha utiifu Yazid alifunga safari ya kuelekea katika mji wa Kufa baada ya kumfikia barua mbalimbali[14] kutoka katika mji huo zikimtaka aende huko. Kwa muktadha huo akaondoka Makka na kuelekea huko.[15] Baada ya msafara wa Imam Hussein (a.s) kusimamishwa na Hurr bin Yazid al-Riyahi katika njia ya kuelekea Kufa na kwa amri ya Ubaydallah ibn Ziyad mtawala wa Kufa,[16] msafara huo ulilazimika kupiga kambi Karbala.[17] Baada ya siku kadhaa za msafara wa Imam Hussein (a.s) kusimama na kuweko Karbala, katika siku ya 10 Muharram mwaka 61 Hijiria, kukatokea vita baina ya jeshi la Imam Hussein (a.s) na jeshi la Umar ibn Sa'd,[18]. Imamu Hussein (a.s) aliuawa shahidi pamoja na masahaba wake wengi katika siku hii. Manusura na watu waliobakia katika msafara wa Imam Hussein ambao wengi wao walikuwa wanawake na watoto walichukuliwa mateka. Awali mateka hao walipelekwa Kufa na baadaye Damascus makao makuu ya utawala wa Yazid huko Sham wakati huo.[19]

Sisitizo la Maimamu wa waislamu wa madhehebu ya Shia juu ya kuzuru Haram ya Imam Hussein na Mashia kulizingatia mno hilo, ni jambo lilioandaa uwanja na mazingira ya kujengwa jengo katika kaburi la Imam Hussein, kupanuliwa kwake na kujenga nyumba za makazi kwa ajili ya wafanyaziara na watu wa karibu na kaburi la Imam Huussein huko Karbala katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah na Bani Abbas.[20] Kuibuka na kudhihiri harakati na mapinduzi ya Kishia baada ya tukio la Karbala, hilo nalo lilikuwa na nafasi katika suala la Mashia kuzingatia na kulipa umuhimu kaburi la Imam Hussein (a.s). Katika harakati yao kundi la Tawwabin baada ya kuondoka Nukhaila (kambi ya kijeshi jirani na Kufa) kwa ajili ya kuelekea Damascus, wakiwa njiani walizuru kaburi la Imam Hussein (a.s)[21] na wakatangaza kushikamana kwao na njia ya Imam Hussein.[22] Katika harakati ya Mukhtar al-Thaqafi pia, kulikuweko na hali ya kuzingatia na kuipa umuhimu Karbala na kuzuru kaburi la Imam Hussein (a.s). Mukhtar al-Thaqafi alikuwa mtu wa kwanza ambaye sambamba na kujenga jengo juu ya kaburi la Imam Hussein (a.s), alijenga pia msikiti, na kijiji kidogo[23] kilichokuwa na idadi ya nyumba kadhaa zilizokuwa zimejengwa kwa udongo. Kadhalika alipanda miti kadhaa ikiwemo mitende.[24]

Kuongezeka wafanyaziara huko Karbala na kuuishi baadhi ya Waislamu maeneo ya jirani na kaburi la Imam Hussein (a.s) kulisadifiana na kudhoofika utawala wa Bani Umayyah na kuanza kuundika serikali ya Bani Abbas. Ni katika kipindi hicho ambapo kujenga na kuboresha eneo la Karbala kulichukua mkondo wa dhati zaidi. Kukajengwa nyumba mpya katika maeneo ya jirani na kaburi la Imam Hussein (a.s). Nyumba hizo zilikuwa na matofali na kulitumika vifaa vya ujenzi mwafaka zaidi.[25]

Hatua hizi za Mashia zilikuwa zikionekana kuwa tisho kwa baadhi ya watawala wa Kiabbasi. Kwa msingi huo watawala na makhalifa kama Harun Rashid na Mutawakkil Abbasi katika zama za utawala wao walitoa amri ya kubomolewa Haram na majengo yaliyokuwa yameizunguka haram hiyo.[26] Pamoja na hayo, ilikuwa ikionekana kuwa, hatua za watawa hao hazijaweza kuzuia kubadilika mji wa Karbala na kuwa makazi ya baadhi ya Mashia. Baada ya Harun, katika kipindi cha utawala wa mwanawe Ma'mun Abbasi, Haramu ya Imam pamoja na majengo yake yaliyokuwa yamebomolewa, yalifanyiwa ukarabati na kwa namna fulani ustawi ukawa umepatikana Karbala.[27] Baada ya ubomoaji uliofanyika katika zama za Mutawakkil pia, ukarabati na ujenzi wa mji wa Karbala ukawa umerejea ambapo mbali na Haram hiyo kukarabatiwa na maeneo yake yaliyokuwa yamebomolewa, kukawa kumeasisiwa na kuanzishwa maeneo mapya likiwemo soko la Karbala.[28] Katika zama za watawa wa ukoo wa Bani Abbas kuliasisiwa pia vituo vya kielimu na masahaba wa Maimamu huko Karbala na hilo kutajwa kuwa duru ya kwanza ya Hawza ya Karbala (Chuo Kikkuu cha Kidini).[29] Mwenendo wa ujenzi na usanifu majengo huko Karbala ulichukua sura mpya katika zama za Aal Buwaih,[30] ambapo baadhi wanaitaja duru hiyo kama kipindi cha kustawi na kuchanua usanifu majengo huko Karbala.[31] Watawala wa ukoo wa Buwaih sambamba na kufanya ziara ya Imam Hussein, walichukua hatua ya kujadidisha jengo la Haram ya Imam Hussein (a.s) na kuupanua mji wa Karbala. Kujenga mzingo wa kwanza wa mji, kujenga maeneo ya makazi na masoko mapya, skuli za kidini kama Madrasa Udhdiya na Masjid Raas al-Hussein zilizojengwa kwa amri ya Adud al-Dawla al-Daylami mwaka 372 Hijiria ni hatua ambazo zinaonyesha kustawi na kupanuka mji wa Karbala.[32]

Kutokana na wafalme wa ukoo wa Safavi na Qajar kuyazingatia na kuyapa umuhimu maeneo matakatifu ya kidini, kuanzia karne ya 10 -13 Hijria, sambamba na Wairani wengi kuishi katika mji wa Karbala, mji huo uliingia katika hatua mpya ya usanifu majengo na kung'ara kimajengo na sanaa ya majengo. Katika kipindi hiki, mbali na majengo kujadidishwa na kupanuliwa, Haram ya Imam Hussein, Haram ya Abul Fadhl al-Abbas (a.s) na maeneo mengine ya kufanya ziara Karbala, Wairani waliokuwa wakiishi Karbala walikuwa na nafasi muhimu na mchango mkubwa katika kustawi masomo na biashara na kuanzishwa Husseiniya, vyuo vya kidini, maktaba na kujengwa misikiti katika duru hii. Watafiti na watambuzi wa masuala ya jiografia kama Carsten Niebuhr na John Asher baada ya kuutembelea mji wa Karbala walizungumzia katika kumbukumbu zao za safari suala la kustawi mji wa Karbala katika zama za ufalme wa Othmania.[33] Johh Peters, mtafiti na mwanaikolojia kutoka Marekani naye aliutembelea mji wa Karbala mwaka 1890 na kuandika: Sehemu mpya ya Karbala ambayo iko nje ya ngome na mzingo wa mji wa zamani ina barabara pana na zilizopangwa vizuri kama miji ya Ulaya.[34]

Maeneo ya Ziara

Muonekano wa Haram ya Imam Hussein (a.s.) na Hadhrat Abbas (a.s.).
Kilima cha Zainabiya

Kuweko Haram ya Imam Hussein (a.s) na Haram ya Abul-Fadhl al-Abbas (a.s) ni mambo ambayo yameufanya mji wa Karbala kuwa katika orodha ya miji muhimu kabisa ya kufanya ziara kwa waislamu wa madhehebu ya shia.[35] Haram ya Imam Hussein (a.s) ni mahali alipozikwa Imam Hussein (a.s), idadi kadhaa ya watu wa familia ya Bani Hashim na masahaba wa Imam Hussein waliouawa kishahidi katika tukio la Karbala.[36] Kufanya ziara katika Haram ya Imam Hussein (a.s) daima ni miongoni mwa amali ambazo zimekuwa zikizingatiwa na kupewa umuhimu na Waislamu wa madhehebu ya Shia. Kuusiwa kufanya ziara ya Imam Hussein (a.s) katika baadhi ya siku maalumu kama Ashura[37], Arubaini[38] na tarehe 15 Shaaban (nusu ya Shaaban)[39], ni mambo ambayo yamefanya katika siku hizi kushuhudiwa idadi kubwa ya wafanyaziara huko Karbala.[40] Katika fikihi ya Kishia Haram na turba ya Imam Hussein (a.s) vina hukumu zao maalumu.[41]

Haram ya Imam Hussein (a.s) mara kadhaa imebomolewa na wapinzani wa Ushia hususan makhalifa wa Bani Abbas na kundi la Mawahabi. Moja ya ubomoaji wa mwanzo uliofanywa dhidi ya Haram ya Imam Hussein (a.s) ilikuwa ni katika zama za Mutawakkil[42] na wa mwisho wake ulikuwa katika mwaka 1411 Hijiria uliofanywa na utawala wa Baath nchini Iraq ambao ulifanywa wakati wa kujiri Intifadha ya Shaabaniyah.[43]

Haram ya Abul-Fadhl al-Abbas (a.s) nayo ipo umbali wa mita 378 upande wa kaskazini mashariki mwa Haram ya Imam Hussein. Wafanyaziara wa Karbala mbali na kuzuru Haram ya Imam Hussein (a.s) hufanya ziara pia katika Haram ya Abul-Fadhl al-Abbas (a.s).[44] Waislamu wa madhehebu ya Shia hufanya maombolezo katika siku ya Tasua (9 Muharram) katika Haram ya Abul-Fadhl al-Abbas. Katika kalenda ya maombolezo ya Shia, siku ya Tasua (9 Muharram) inasibishwa na Abul Fadhl al-Abbas (a.s).[45]

Mji wa Karbala mbali na kuwa na Haram mbili za Imam Hussein na Abdul-Fadhl al-Abbas (a.s) una maeneo mengine ya kufanya ziara pia ambapo akthari yake yanahusiana na tukio la Karbala. Al-Mukhayyam, eneo alilouliwa Imam Hussein na kaburi la Hurr ibn Yazid al-Riyahi ni miongoni mwa maeneo hayo. Aidha jirani na Haram ya Imam Hussein (a.s) kuna mafikio na vituo viwili vya Imamu Swadiq (a.s) na Imam Mahdi (a.s) ambavyo katika utamaduni wa Mashia ni maeneo yanayoheshimiwa na waislamu wa kishia huyazuru na kuyatembelea maeneo hayo.[46]

Matukio ya Kisiasa na Kijamii ya Karne Mbili za Karibuni

Maqam ya Imam Mahdi (a.j.t.f) katika mji wa Karbala

Katika karne mbili za hivi karibuni, mji wa Karbala ulishuhudia matukio na mageuzi mbalimbali ya kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

Shambulio la Mawahabi

Tarehe 18 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1216 Hijria, Mawahabi wakiongozwa na Abdul-Aziz bin Saud kutoka Hijaz (Saudi Arabia) waliingia Iraq na kufanya hujuma na mashambulio dhidi ya mji wa Karbala. Waliingia katika mji huo kupitia eneo la al-Mukhayyam na kufanya mauaji, uporaji wa mali za watu na vitu vya thamani katika Haram ya Imam Hussein (a.s). Katika siku hiyo akthari ya wananchi wa mji huo kwa mujibu wa ada ya siku zote katika siku ya Eidul Ghadir walikuwa wameelekea katika mji wa Najaf kwa ajili ya kufanya ziara katika Haram ya Imam Ali ibn Abi Twalib (a.s). Kwa msingi huo mji wa Karbala ulikuwa mtupu na haukuwa na wanaume kwa ajili ya kusimama kidete na kukabiliana na hujuma na mashambulio hayo. Vyanzo vya historia vinasema kuwa, idadi ya watu waliouawa katika tukio hilo chungu ilikuwa baina ya 1000 mpaka 4000. Aidha katika tukio hilo Haram ya Imam Hussein (a.s) ilidhurika pakubwa.[47]

Shambulio la Necib Pasha

Baada ya wakazi wa Karbala kuupinga na kuukataa utawala wa Othamania mwaka 1285 Hijria, Mehmed Necib Pasha (Muhammad Najib Pasha) mtawala wa Kiothamnia huko Iraq aliwapatia wakazi wa mji wa Karbala muhula wa siku kadhaa wawe wameukubali utawala wa ufalme wa Othamnia na kujisalimisha. Najib Pash alitoa amri ya kushambuliwa mji wa Karbala baada ya kushindwa upatanishi wa Sayyied Kadhim Rashti, mmoja wa Maulamaa aliyekuwa mkazi wa Karbala na kiongozi nambari mbili wa Sheikhiyyah, upatanishi ambao ulikuwa na lengo la kuzuia hujuma na mashambulio ya jeshi la Othmania ndani ya mji na kutosalimu amri wakazi wa Karbala. Askari wa Othmania walikuwa na ruhusa ya kushambulia maeneo yote isipokuwa Haram ya Imam Hussein (a.s), Haram ya Abul-Fadhl al-Abbas (a.s) na nyumba ya Sayyied Kadhim Rashti. Baadhi ya wakazi wa mji wa Karbala wakiwa na lengo la kusalimisha maisha yao waliomba hifadhi katika Haram ya Abul-Fadhl (a.s). Pamoja na hayo eneo hili takatifu pia halikusalimika na hujuma na mashambulio ya askari wa ufalme wa Othmania. Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, watu wapatao 10,000 waliuawa katika tukio hili. Tukio hilo limeondokea kuwa mashuhuri kwa jina la tukio la Ghadir al-Dam.[48]

Mapambano Dhidi ya Ukoloni

Mji wa Karbala katika zama za kushindwa utawala wa Othmania na kuweko Uingereza nchini Iraq mwaka 1917, ulikuwa moja ya vituo muhimu vya mapambano dhidi ya Waingereza. Harakati ya 1920 Miladia ambayo baadaye ilikuja kufahamika kama Thawrat al-Ishirin (Mapinduzi ya Ishirini) iliibuka kwa uongozi wa Muhammad Taqi Shirazi, Marjaa wa Kishia huko Karbala. Harakati hii ilitokea baada ya Uingereza kutotekeleza ahadi yake ya kuondoka Iraq na uhuru wa nchi hiyo.[49]

Intifadha ya Shaabaniyyah

Uwepo mkubwa wa jeshi la Baath la Iraq kwenye mlango wa Haram ya Hazrat Abbas (a.s) huko Karbala baada ya kukandamizwa intifadha ya Shabaniyah.

Makala asili: Intifadha ya Shaabaniyyah

Wakati wa kujiri harakati na mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala wa Wabaath uliokuwa ukiongozwa na Saddam Hussein mwezi Shaaban 1411 Hijiria, mji wa Karbala ulikuwa moja ya vituo vikuu vya harakati hiyo. Mji huo na miji mingine 13 ya Iraq iliangukia mikononi mwa vikosi vya wananchi wakati wa Intifadha ya Shaabaniyyah [50], lakini baadaye harakati hii ya wananchi ilisambaratishwa na kukandamizwa na vikosi vilivyokuwa chini ya uongozi wa Saddam. Wakati wa kusambaratishwa na kukandamizwa harakati hii ya wananchi, Haram ya Imam Hussein (a.s) ilidhuriwa na mashambulio ya jeshi la Baath. Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo, watu baina ya 300 hadi 500 waliuliwa katika maeneo mbalimbali ya Iraq kufuatia ukandamizaji wa jeshi dhidi ya harakati hiyo huku wengine wapatao milioni 2 wakilazimika kuwa wakimbizi.[51]

Mapigano na Jeshi la Iraq Baada ya Kuanguka Utawala wa Saddam

Kuwepo kwa majeshi ya muungano wa Marekani huko Karbala baada ya uvamizi wa Iraq mwaka 2003; Katika picha hii, mwanajeshi wa Kimarekani amesimama karibu na gari la kujitoa mhanga kwenye barabara inayoelekea kwenye haram ya Hazrat Abbas(a.s).

Wakati wa mashambulio ya jeshi la Marekani dhidi ya Iraq mwaka 2003, mji wa Karbala ulishuhudia mapigano ya hapa na pale baina ya wakazi wa mji huo na vikosi vya Marekani katika barabara zinazoishia Haram ya Imam Hussein(a.s) na Haram ya Abul-Fadhl al-Abbas(a.s). Kadhalika mwaka 2004 kuliibuka mapigano ya kijeshi baina ya kundi la Mashia lenye mfungamano na Harakati ya Sadr maarufu kama Jaysh al-Mahdi na Wamarekani katika miji wa Najaf, Basra na kitongoji cha Sadr Baghdad. Wamarekani wakiwa na lengo la kukabiliana na shambulio tarajiwa la wafuasi wa Sadr huko Karbala waliingia katika mji huo wakiwa na silaha na zana za kisasa kama magari ya deraya, ambapo sambamba na kushambulia ofisi ya Harakati ya Sadr walifunga pia njia za kando kando ya Haram. Sababu kuu ya mapigano hayo ilielezwa kuwa ni kupinga Iraq kukaliwa kwa mabavu na jeshi la Marekani. [52] Mashia ambao ni wafuasi wa Jaysh al-Mahdi huko Karbala mwaka 2007 walikabiliana kivita na Wamarekani kwa tofauti hii kwamba, upande wa pili hasimu wa mapigano na jeshi la Mahdi walikuwa polisi wa Iraq na Wamarekani waliingia katika medani ya mapigano kama kusaidia na kutoa himaya kwa polisi ya Iraq.[53]

Mashambulio ya Kigaidi Karbala

Baada ya kuondolewa madarakani utawala wa chama cha Baath cha Saddam nchini Iraq, makundi ya kigaidi na kukufurisha yenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh yakishirikiana na kundi la maafisa wa zamani wenye mfungamano na chama cha Baath yalifanya hujuma, mashambulio na operesheni tofautii tofauti za kigaidi katika mji wa Karbala. [54] Mashambulio haya ya kigaidi ambayo yalikuwa yakifanywa pia katika miji mingine ya Iraq yalisababisha hasara kubwa ya roho na mali. Katika mji wa Karbala hujuma za kigaidi zilikuwa zikitekelezwa zaidi katika siku za maombolezo ya Imam Hussein(a.s) na katika matembezi ya kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein(a.s). [55]

Vyama na Vikundi vya Kisiasa na Kijamii

Katika karne mbili za hivi karibuni, mji wa Karbala kutokana na kuwa makazi ya Marajii Taqlidi wa Kishia na kuwa na ustawi wa vyuo vya kidini uliondokea kuwa na nafasi muhimu katika matukio ya kisiasa na kijamii ya Iraq. Harakati za vikundi vya kisiasa na kijamii huko Karbala wakati mwingine zilikwenda sambamba na matukio ya Iran. Radiamali ya Maulamaa waliokuwa wakiishi Najaf na Karbala mkabala na Harakati ya Mapinduzi ya Katiba ya Iran ni miongoni mwa matukio hayo. Kama ambavyo kadhia ya Mapinduzi ya katiba iliwatikisa Maulamaa na Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf, ilikuwa na taathira pia kwa Karabala isipokuwa kwa tofauti hii kwamba, watu wa Kabla walikuwa na msimamo hasi kuhusiana na mapinduzi hayo ya katiba nchini Iran. [56]

Katika karne ya 20 Karbala na hususan katika kipindi cha kukaliwa kwa mabavu na Uingereza, ilishuhudia pia kuundwa na kuibuka harakati na mirengo mbalimbali au kuasisiwa matawii ya vyama vilivyokuwa na harakati amilifu nchini Iraq. Uongozi wa Marja' wa Kidini katika mji wa Karbala na Chuo Kikuu cha Kidini cha mji huo ulikuwa na ushirikiano wa kisiasa, kifikra na kiutamaduni na baadhi ya harakati amilifu katika mji wa Karbala. Kujikomboa Iraq na kuondoka Uingereza katika nchi hiyo yalikuwa moja ya malengo makuu ya harakati za Iraq katika nusu ya kwanza ya karne ya 20. The Committee of Union and Progress na National Islamic Society vilikuwa miongoni mwa vyama na harakati zilizokuwa amilifu katika mji wa Karbala. [57] Chama cha National Islamic Society kilianzishwa na Muhammad Ridha Shirazi mtoto wa Muhammad Taqi Shirazi, Uongozi wa Marja' wa Kidini Karbala na idadi kadhaa ya wanazuoni wa Kishia katika mji huo huko Karbala na lengo lilikuwa ni kupambana na kukabiliana na uwepo wa Uingereza. Chama hicho kiliasisiwa mwaka 1917. Kikundi hiki kilikuwa na nafasi muihimu katika kutokea mapinduzi ya Iraq ya 1920 baada ya fat'wa ya jihadi ya Mirza Shirazi. [58]

Sambamba na kuundwa makundi mbalimbali ya kikomunisti katika kivuli cha kupigania uhuru wa Iraq, kulianzishwa tawi la vyama vya kikomunisti kama Iraqi Communist Party katika miji ya Karbala na Najaf na kuwa na harakati muhimu na pana ya kuwavutia vijana upande wake. [59] Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) na uongozi wa Marja' Karbala na Najaf wakiwa na lengo la kukabiliana na vitisho vyenye wigo mpana vya Ukomunisti dhidi ya Uislamu, walifikiria kuanzisha vyama. [60] Hatimaye mwaka 1956 kuliundwa chama kilichojulikana kwa jina la Hizb al-Daw'at al-Islamiya ( Islamic Dawa Party). Moja ya vikao na mikutano ya awali ya chama hiki kilifanyika katika mji wa Karabala. [61] Idadi kadhaa ya viongozi wa kisiasa wa chama hiki kama Ibrahim al-Jaafari na Nouri al-Maliki walikuwa watu wa Karbala. [62] Baada ya Hizb al-Daw'ah, mwaka 1962 kukaasisiwa Islamic Action Organization katika mji wa Karbala kilichokuwa na mfungamano na familia ya Shirazi. [63]

Katika kipindi cha utawala wa chama cha Baath kwa uongozi Saddam Hussein pia baadhi ya Maulamaa na viongozi wa kidini wa Kishia wa Kiiraqi waliasisisi Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq (Islamic Supreme Council of Iraq). [64] Baada ya kuangushwa utawala wa Saddam kuliundwa harakati na makundi mbalimbali ya kisiasa nchini Iraq ambapo mengi yake yalianzisha matawi yao katika mji wa Karabala na kuendesha harakati za kisiasa na kiutamaduni. Miongoni mwa makundi hayo ni Jumuiya ya Badr ya Iraq na Harakati ya Sadr.

Tamaduni

Mapinduzi ya Imam al-Hussein (a.s) na tukio la Karbala yaliacha athari ya kudumu ya kitamaduni kwa jamii ya kishia. Mji wa Karbala ulikuwa ndio chimbuko la shughuli nyingi za kitamaduni za Shia zilizotokana na Ashura. Baadhi ya vitendo hivyo ni pamoja na sherehe za maombolezo ya Tuwairij, Ziyarah ya Arubaini na maandamano yake, ujenzi wa husseiniyyat na vituo vya kidini, utengenezaji wa turbah na tasbih kwa kutumia udongo wa Karbala na maombolezo yanayoashiria matukio ya Karbala.

Ziara ya Arubaini

Moja ya hafla za kidini za Waislamu wa madhehebu ya Kishia ni ziara ya kumbukumbu ya Arubaini huko Karbala. Kuanzia karne za mwanzo, Mashia walikuwa wakizingatia na kulipa umuhimu suala la ziara ya Arubaini. Walifanya hivyo wakitekeleza maagizo ya Maimamu Maasumina(a.s). Mashia wengi nchini Iraq, wa Iran na wa maeneo mengine ya dunia wakiwa na lengo la kufika Karbala kwa ajili ya kumbukumbu ya Arubaini, hutembea kwa miguu kutoka Najaf hadi Karbala. Marasimu haya ni mashuhuri kwa jina la matembezi ya Arubaini. Siku ya kumbukumbu ya Arubaini mjumiko mkubwa wa waombolezaji kutoka miji mbalimbali ya karibu na ya mbali ya Iraq na maeneo mengine ya dunia hukusanyika katika mji wa Karabala. [65]

Turba ya Karbala

Turba ya Karbala au Turba ya Imam Hussein (a.s) ambao ni udongo au vumbi linalochukuliwa kutoka kando kando ya kaburi la Imam Hussein (a.s) ambayo ina fadhila kubwa kwa mujibu wa nukuu zilizokuja katika riwaya na hadithi mbalimbali, inaheshimiwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia. [67] Mashia hutumia udongo huu kutengeneza kipande cha udongo cha kusujudia na tasbihi. [68] Katika vitabu viya fikihi inaelezwa kuwa, ni mustahabu wakati wa kuswali kusujudu juu ya udongo wa Karbala. [69].

Kuasisiwa Husseiniya

Jengo linalohusishwa na Husseiniyya ya zamani ya watu wa Isfahan (Iran) iliyopo mtaa wa al-Qibla huko Karbala; kando ya jengo hilo kuna wanawake waliovalia chador za kiiran. Picha hii ilipigwa mnamo 1956.

Kuanzisha Husseiniya kwa ajili ya kuwapokea na kuwaweka hapo wafanyaziara ni miongoni mwa hatua ambazo zilifanywa katika karne zilizopita. Historia ya kujengwa Husseiniya ya kwanza huko Karbala inarejea katika karne ya 11 Hijiria. Sambamba na kufanyiwa ukarabati sehemu ya maeneo matakafu ya Iraq katika kipindi cha utawala wa Qajar, liwali wa Kiothmania huko Iraq mwaka 1127 alijenga Husseiniya kwa ajili ya kutoa huduma ya makazi kwa wafanyaziara. [70] Baadaye katika mwaka 1368 kundi la wafanyabiashara ambao walikuwa ni Wairani walinunua eneo hilo kutoka kwa Shirika la Waqf la Iraq ambapo wakishirikiana na kundi la wafanyabiashara wa Iraq na Kuwait waliifanyia ukarabati Husseiniya hiyo. Baada ya kukarabatiwa, Husseiniya hiyo ikaondokea kufahamika kwa jina la Husseiniya wa Watehran. Na baadaye ilibadilishwa jina na kufahamika kwa jina la Husseiniya ya Haidariyah. [71] Kabla ya kipindi hiki, hakuna ripoti zozote zinazoonyesha juu ya kuweko kwa maeneo yaliyojulikana kwa jina la Husseiniya. Baada ya kipindi, Husseiniya nyingi mashuhuri katika mji wa Karbala zilijengwa baada ya muongo wa kwanza na wa pili wa karne ya 14 Hijiria. [72] Idadi kadhaa ya Husseiniya hizi za kihistoria zimejengwa na Maulamaa, wafanyabishara wa Kiirani na baadhi yazo zimejengwa na Mashia wa India. [73] Baada ya kuanguka utawala wa Baath nchini Iraq, uanzishaji na ujenzi wa Husseiniya na makazi ya wafanyaziara ulichukua wigo mpana na hata ujenzi wa hoteli haujaweza kupunguza mwenendo wa ujenzi wa Husseiniya. [74]

Vyuo Vikuu vya Kidini na Vituo vya Kielimu

Makala Asili: Chuo Kikuu cha kidini cha Karbala (Hawza)

Historia ya elimu za kidini za Kiislamu Karbala inarejea katika karne za mwanzo za Hijiria kwa kuweko baadhi ya Maimamu Maasumu (a.s) na wapokezi wa hadithi wa Kishia. Katika zama hizo, shakhsia hao walijishughulisha na kufundisha, kulea na kuandaa wanafunzi huko Karbala. Abdallah ibn Ja’far Himyari mmoja wa watu wa karibu wa Imam Hadi (a.s) na Imam Hassan Askary (a.s) alifanikiwa kulea wanafunzi mbalimbali katika mji huo. [75] Baada ya kipindi cha Ghaiba, mafakihi kama Najashi, Sayyied ibn Tawus, Shahid al-Awwal na Ibn Fahd Hilli walisoma katika mji huo. [76]

Katika karne ya 9 Hijiria, Chuo cha kidini katika mji wa Karbala kilianza kazi zake ambapo shakhsia wa kwanza wakubwa wa shule hiyo ni Sayyied Izzuddin Hussein ibn Mus'aid Hairi na Faidhullah Barmaki Baghdadi. [77] Katika shule hiyo kulikuweko na maktaba mbili za kifikra za Akhbari na Usuli. Hata hivyo maktaba ya Akhbari haikuwa na wafuasi wengi. [78] Kudhihiri utawala wa Safavi, kulipelekea maktaba ya Akhbari kuhuishwa na Muhammad Amin Astrabadi. Baada ya kuanguka utawala wa Safavi, kulianza vitendo vya maudhi vya Waafghani Masuni sambamba na mashinikizo ya Nadir Shah, jambo lililowalazimisha Maulamaa Kiirani kuhajiri na kuelekea Iraq hususan Karbala. Katika zama hizi, maktaba ya Akhbari ilifikia kilele chake katika mji wa Karbala na Maulamaa wengi wa Kiirani walikuwa na fikra na itikadi za Kiakhbari. Pamoja na hayo yote, kutokana na sababu mbalimbali maktaba ya Akhbari ikaelekea upande wa kuanguka na kusambaratika. [79]

Katika karne ya 13 Hijiria, chuo cha kidini cha Karbala hakikuwa na ustawi na hali yake ya kunawili ya huko nyuma. Hiyo ilitokana na kuhajiri Maulamaa wa Kiirani kuelekea Najaf au kurejea Iran. Hali ilibadilika baada ya Muhammad Taqi Shirazi kuhama kutoka Samarra na kuelekea Kadhimein na baadaye Karbala. Uongozi wake kwa mapambano dhidi ya uvamizi wa Uingeza huko Iraq na kushiriki baadhi ya wanazuoni na wanafunzi wa masomo ya dini wa Chuo Kikuu cha Kidini cha Karbala katika harakati jumuishi dhidi ya Uingereza, ni jambo ambalo lilikipa uhai mpya chuo cha Karbala. [80]

Katika karne mbalimbali kulianzishwa na kuasisiwa shule tofauti katika mji wa Karbala. Idadi kubwa ya shule hizi zilijengwa na Maulamaa wa Kiislamu waliokuwa wakiishi Iraq. Shule ya Sayyied Mujahid, Sadr A’dham Nouri na shule ya Khui ni miongoni mwa skuli hizo. [81] Mbali na shule hizo za kidini, kulijengwa pia maktaba mbalimbali katika mji wa Karbala ambapo baadhi ya maktaba hizo zina nafasi maalumu na zinazingatiwa na wahakiki wa Kishia kutokana na kuwa na nakala za hati ya mkono. [82] Baadhi ya wanahistoria wameorodhesha jumla ya maktaba 78 katika mji wa Karbala ambapo baadhi ya maktaba hizo zilianzishwa na Maulamaa waliokuwa wakiishi katika mji huo. [83] Mbali na vyuo vya kielimu Chuo Kikuu cha Karbala, Chuo Kikuu cha Ahlul-Bayt na vituo vya utafiti wa kielimu vyenye mfungamana na Haram ya Imam Hussein na Haram ya Abul –fadhl al-Abbas (a.s) navyo baada ya kuanguka utawala wa Baath vilifanya harakati mbalimbali za kielimu na kiutafiti katika uga wa madhehebu ya Kishia. [84]

Familia na Shakhsia

Tangu katika karne za awali za kuasisiwa Karbala mpaka katika zama hizi, mji huo ulikuwa na umekuwa na historia ya kuwa na familia na koo mbalimbali. Baadhi ya familia hizo zilianza kuishi Karbala katika karne za awali. Familia na ukoo wa Aal Tu’mah na Aal-Naqib ni miongoni mwa familia hizo. Ukoo wa Aal-Tu’mah ambapo kizazi chake kinarejea na kuishia kwa Ibrahim Mujab, sharifu (sayyied) wa kwanza kuishi Karbala, inahesabiwa kuwa familia kongwe zaidi ya kisharifu ambayo iliishi katika karne ya tatu Hijiria katika mji wa Karbala. [85] Ukoo wa Aal-Naqib kwa upande wake, unanasibishwa na Imam Kadhim (a.s) na uliishi katika mji wa Karbala kuanzia karne ya tano Hijiria. [86] Umashuhuri mkubwa zaidi ni maalumu kwa familia za kielimu ambazo zilikuwa zikitoka katika maeneo mbalimbali ya Iraq, Iran, katika mataifa ya Kiarabu na India na kuelekea katika mji huo kwa minajili ya kutafuta elimu. Baadhi ya familia za wanazuoni wa kidini baada ya kupata daraja ya Ijtihadi au kukamilisha masomo ya msingi ya vyuo vya kidini zilikuwa zikirejea katika mataifa yao. [87] Familia za Bahbahani, Sadr, Shirazi, Shahristani, Kashmiri, Rashti na Mar’ashi ni baadhi tu ya familia mashuhuri zinazotambuliwa huko Karbala. [88] Katika zama hizi, baadhi ya shakhsia wa kisiasa wa Kishia nchini Iraq na Iran walikuwa watu wa Karbala. Ibrahim al-Ja’fari na Nouri al-Malik wanasiasa wa Kishia nchini Iraq na Ali Akbar Salehi mwanasiasa wa Iran wamezaliwa katika mji wa Karbala.

Rejea

  1. Rahnemaye Safar be Karbala Mu'alla.
  2. [1]
  3. [2]
  4. Alu Taa'mah, Mirathu Karbala, uk. 84-186.
  5. I'lam Jihad Ulamaye Shia wa Sunni., Khabarghozari Tasnim.
  6. «Major Cities».
  7. Alu Taa'mah, Mirathu Karbala, uk. 31-36.
  8. Alu Taa'mah, Mirathu Karbala, uk. 31.
  9. Alu Taa'mah, Mirathu Karbala, uk. 36.
  10. Alu Taa'mah, Mirathu Karbala, uk. 20-21.
  11. Allamah Majlisi, Bihar al-Anwar, 1403 H, juz. 44, uk. 301.
  12. Khalili, Mausu'at al-'Atabat al-Muqaddasah, 1407 H, juz. 8, uk. 197.
  13. Dinawari, Akhbar al-Tiwal, uk. 298.
  14. Baladzuri, Ansab al-Ashraf, juz. 3, uk. 157-158; Sheikh Mufid, al-Irshad, 1399 H, juz. 2, uk. 36-37.
  15. Tabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, juz. 5, uk. 381.
  16. Tabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, juz. 5, uk. 401.
  17. Maqram, Maqtal al-Hussein (a.s), 1426 H, uk. 192.
  18. Tabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, 1967 juz. 5, uk. 417; Sheikh Mufid, al-Irsyad, 1399 H, juz. 2, uk. 91.
  19. Sheikh Mufid, 1388, Al-Irshad, uk. 509-523.
  20. Alu Taa'mah, Mirathu Karbala, uk. 31 na 32.
  21. Ibn Athir, Al-Kamil fi al-Tarikh, juz. 4, uk. 178.
  22. Tabari, Tarikh Tabari, 1493 H, juz. 4, uk. 456-457.
  23. Al-Sadr, Nuzhat Ahlul-Haramain fi Imarat al-Mashhadin, uk. 21, 23, 26.
  24. Al-Anshari, Imarat Karbala, 2005, uk. 95.
  25. Kelidar, Tarikh Karbala al-Mu'alla, uk. 19 ; Al-Ansari, Imarat Karbala, 2005, uk. 96.
  26. Alu Taa'mah, Mirathu Karbala, 1373, uk. 32 na 33.
  27. Jam'i az Newisandegan, Negahi Nu be Jaryane Ashura, uk. 420-421.
  28. Al-Ansari, Imarat Karbala, 2005, uk. 96 na 97.
  29. Sayyid Kibari, Hauzehaye Ilmiyeh Shiah dar Gostare Jahan, uk. 256.
  30. Amin, Dairat al-Ma'arif al-Islamiyyah al-Shi'iyah, juz. 11, uk. 356.
  31. Al-Ansari, Imarat Karbala, 2005, uk. 96 na 99.
  32. Musawi Zanjani, Jaulat fi Amakin al-Muqaddasah, uk. 83.
  33. Al-Ansari, Imarat Karbala, 2005, uk. 61 na 70.
  34. John punnett: Nippuar or Explorations and Avcentures on the Euphrates 1880 - 1890, page: 331, Volume II - second compaign 1897.peters
  35. Ashlani, Shahr-hae Muqaddas Shia, Markaz Mutalaat wa Paskhuguwi Be Shubuhat.
  36. Isfahani, Maqatil al-Talibin, Dar al-Ma'rifah, uk. 118.
  37. Ibnu Qqulawayah, Kamil al-Ziyarat, 1356 S, uk. 173.
  38. Sheikh Mufid, Kitab al-Mazār, uk. 53.
  39. Ibnu Qqulawayah, Kamil al-Ziyarat, 1356 S, uk. 181.
  40. «Bertepatan dengan Asyura Husaini, 3 juta peziarah di Karbala al-Mualla».؛«Be Munasabat Ashura Husseini; 3 Milion Zaira Dar Karbala Muali.», Khabarighozari Mehr.
  41. Rejea: Falah-Zadeh, Ahkāme Fiqhi Safar Ziarati Atabāt, Markaz Tahqiq Hajj, uk. 14, 17, 18, na 36.
  42. Aalu Taa'mah, Karbala wa Haramhaye Mutahhar, 1388 H, uk. 94 na 95.
  43. «Rewayati Az Ruzehaye Jesarate Saddam Be Karbala», Akhabarighozari Tasnim.
  44. «Karbala biduni Haram wa Ziarat Hazrate Abal Fadhl; Karbala Nemishavad». Abul Fadhl Abbas/ «Ziarat Haram Hazrate Abbas (a.s)», Paygahe Internet Asr Shieh.
  45. «Haram Abul-Fadhl Abbas (a.s) Dar Ruze Tasu'a.», Khabarighozari Iysna.
  46. Qummi, Amākin Ziyārati Siyahati dar Iraq, uk. 45-54.
  47. Aalu Taa'mah, Mirathu Karbala, 1435 H, uk. 116-121.
  48. Aalu Taa'mah, Mirathu Karbala, 1435 H, uk. 125-132; «Gozaresh Yeki Keshtar; Riwayati Mustanad Az Qatl Amu 19 Hizar Nafari Shiiyan Dar Hamle Be Karbala.», Khabarghozari Tasnim.
  49. Zamizam, Karbala wa al-Harakah al-Wataniyyah fi al-Qarn al-Ishrin, uk. 63-95.
  50. Tabraiyan, Intifadhah Shaabaniyah, uk. 230.
  51. «Majira Intifadhah Shaabaiyah Chist?»
  52. «Hudhur Tankihaye Amerikayi Dar Karbala.»,, Paygah Khabari Fardah.
  53. «Dargiri Niruhaye Amerikayi Ba Shabenidhamiyan Artesh Mahdi Dar Karbala.»,, Khabarighozari Iysna.
  54. «Amerika Chegune Al-Qaedaha Ra Takfiri Kard?/ Afsar Itilaat Rezhim Baath Chegune Daish Ra Beujud Ovard?», Paygah Khabari Mashrik.
  55. «Yaddoshtehaye Yek Irani Az Ashuraa Khunin Dar Karbala.»., Paygah Internet Shabake BBC.

Vyanzo

  • Abu l-Faraj al-Isfahani, ʿAli b. al-Ḥussein. Maqatil al-talibiyyin. Mhariri: Aḥmad Ṣaqar. Beirut: Dar al-Maʿrifa, [n.d].
  • Abu Zayd al-'Amili, Aḥmad ʿAbd Allah. Muḥammad Baqir al-Ṣadr: al-Sira wa l-masira fi haqa'iq wa l-watha'iq. Beirut: Mu'assisat al-'Arif li-l-Matbu'at, 1428 AH.
  • Al Tu'ma, Salman Hadi. Karbala wa ḥaramha-yi muṭahhar. Tehran: Mash'ar, 1388 Sh.
  • Al Tu'ma, Salman Hadi. Mirath karbala'. Mfasiri: Muḥammad Riḍa Ansari. Tehran: Markaz-i Chap wa Nashr-i Sazmān-i Tablighat, 1373 Sh.
  • Al Tu'ma, Salman Hadi. Turath Karbala'. Tehran: Nashr-i Mash'ar, 1435 AH.
  • Amin, Ḥusayn al-. Dāʾirat al-maʿārif al-Islāmīyya al-Shīʿa. Chapa ya pili. Beirut: Dāʾirat al-Taʿārif li-l-Maṭbūʿāt, 1413 AH.
  • Anṣārī, Raʾūf Muḥammad Jamīl al-. ʿImārat Karbalāʾ dirāsat ʿumrānīyya wa takhṭīṭīyya. Damascus: Muʾassisat al-Ṣāliḥānī, 2005.
  • Balādhurī, Aḥmad b. Yaḥyā al-. Ansāb al-ashrāf. Mhariri: Muḥammad Bāqir Maḥmūdī. Beirut: Dār al-Taʿāruf, 1977.
  • Dīnawarī, Aḥmad b. Dāwūd al-. Al-Akhbār al-ṭiwāl. Mfasiri: Mahdawī Dāmghānī. Tehran: Nashr-i Niyy, 1371 Sh.
  • Fallāḥzāda, Muḥammad Ḥussein. Aḥkām-i fiqhī-yi safar-i zīyāratī-yi ʿatabāt. Tehran: Markaz-i Taḥqīqāt-i Ḥajj, 1386 Sh.
  • Ibn Athīr, ʿAlī b. Abī l-Karam. Al-Kāmil fī l-Tārīkh. Beirut: Dār al-Ṣādir, 1386 AH.
  • Ibn Qūlawayh, Jaʿfar b. Muḥammad. Kāmil al-zīyārāt. Mhariri: Abd al-Ḥusayn Amīnī. Najaf: Dār al-Murtaḍawīyya, 1356 Sh.
  • Khalīlī, Jaʿfar. Mawsūʿat al-ʿatabāt al-muqaddasa. Chapa ya pili. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1407 AH.
  • Kilīdār, Sayyid ʿAbd al-Ḥussein. Tārīkh Karbalāʾ. Najaf: al-Maṭbaʿa al-ʿAlawīyya, 1349 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Chapa ya pili. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Al-Irshād fī maʿrifat ḥujaj Allāh ʿAlā l-ʿIbād. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1399 AH.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Al-Mazār. Qom: Kungira-yi Jahānī-yi Ḥizāra-yi Sheikh al-Mufīd, 1413 AH.
  • Muʾmin, ʿAlī. Sanawāt al-jamr. Beirut: [n.p], 2004.
  • Muqarram, ʿAbd al-Razzāq al-Mūsawī al-. Maqtal al-Ḥussein. Beirut: Muʾassisat Kharsān li-l-Maṭbūʿāt, 1426 Ah.
  • Mūsawī Zanjānī, Ibrāhīm. Jawlat fī al-amākin al-muqaddasa. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1405 AH.
  • Kundi la wandishi. Nigāhīno bi jaryān-i ʿĀshūrā. Chapa ya sita. Qom: Būstān-i Kitāb, 1387 Sh.
  • Nuwiynī, Muḥammad al-. Aḍwāʾ ʿalā maʿālim muḥāfiẓat Karbala. Najaf: Maṭbaʿat al-Qaḍāʾ, 1391 AH.
  • Qummī, Muḥammad Riḍā. Amākin-i zīyāratī sīyāḥatī-yi Iraq. Chapa ya pili. Tehran: Nashr-i Mashʿar, 1380 Sh.
  • Ṣadr, Sayyid Ḥussein al-. Nuzhat ahl al-ḥaramayn fī ʿimārat al-mashhadayn. Chapa ya pili. Karbala: Maṭbaʿat Ahl al-Bayt, 1384 AH.
  • Sayyid Kubārī, Sayyid ʿAlī Riḍā. Ḥawzahā-yi ʿilmīyya-yi Shīʿa. Tehran: Amīr Kabīr, 1378 Sh.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārīkh al-umam wa l-mulūk. Edited by Muḥammad Abū l-Faḍl Ibrāhīm. Beirut: Dār al-Turāth, 1976.
  • Tabarrāʾīyān, Ṣafāʾ al-Dīn. Intifāḍa-yi shaʿbānīyya. Tehran: Markaz-i Asnād-i Inqilāb-i Islāmī, 1391 Sh.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥassan al-. Tahdhīb al-aḥkām. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Zamayzim, Saʿīd Rashīd al-. Karbala wa l-ḥarkat al-waṭanīyya. Karbala: Markaz Karbala li-l-Dirāsāt wa l-Buḥūth, 1436 AH.