Nenda kwa yaliyomo

Jihadi

Kutoka wikishia

Jihadi: Maana ya Jihadi ni jitihada ya kupambana ndani ya njia ya Mwenye Ezi Mungu kwa kuitoa muhanga nafsi pamo na mali. Dhana hii inahusiana na jitihada za kupigana vita dhidi ya washrikina pamoja na waasi wavunjao amani na kusimama dhidi ya Uislamu. Shabaha yake kuu ni kuupa hadhi Uislamu na kudumisha nembo zake. Katika akida ya Kiislamu, Jihadi huhesabiwa kama ni moja ya Furu'u Ad-Din (matawi ya dini). Wanasheria wa Kiislamu wamechambua na kufafanua hukumu za Jihadi kupitia vitabu vyao mbali mbali vinavyojadili hukuza za kifiqhi, chini ya mlango maalumu unaohusiana na Jihadi. Wafasiri wengi wa Qur'ani wanashikilia isemayo kuwa; sheria ya Jihadi ilianzishwa miezi saba takriban baada ya tukio la Hijra ya bwana Mtume (s.a.w.w) ya kutoka Makka kuelekea Madina.

Maandiko matakatifu, yakiwemo ya Qur'ani na Hadithi, yamebainishwa sifa na fadhila kadhaa adhimu kuhusiana na dhana ya Jihadi katika njia ya Mwenye Ezi Mungu. Aidha kuna masuala mengine mengi yaliotajwa ndani ya maandiko hayo kuhusiana na faida za Jihadi, kama vile; kulinda na kuwapa himaya wanaokandamizwa na wasiojiweza, kuzuia udhalimu na uvamizi, kupambana na ushirikina na ibada ya masanamu, pamoja na kuimarisha na kudumisha kwa dini.

Kwa mtazamo wa mafaqihi (wanazuoni wa Fiqhi), dhana ya Jihadi hugawika katika aina mbili kuu: Jihadi Anzishi (Ibtidai) na Jihadi ya Kujihami (Difai). Jihadi Anzishi ni mapambano ya vita dhidi ya washirikina na wasioamini yale ylioletwa na bwana Mtume (s.a.w.w), kwa lengo la kuwaita kwenye Uislamu na Tauhidi (ibada ya Mungu MMoja). Ama Jihadi ya Kujihami, ina maana ya kuhami na kuzitetea ardhi za Kiislamu mbele ya mashambulizi ya wavamizi fulani.

Dhana ya Jihadi Katika zama za sasa (karne ya kumi na tano Hijria), inaonekana kupotoshwa na kutumiwa isivyostahiki kupitia makundi ya Kiislamu yenye itikadi kali kama vile Al-Qaeda na Daesh. Mwenendo wa kikatili wa makundi haya umesababisha kupotoka na kubadilika maana ya Jihadi kutoka kwenye malengo yake msingi na hatimae kuleta madhara makubwa ndani ya Uislamu na ulimwengu kwa jumla. Makundi haya yamepelekea kuzua chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia), na hatimaye, kutoa kisingizio cha kushambulia kwa dhana ya Jihadi na kupata maana mpya kabisa kinyume na ile maana yake halisi.


Uchambuzi wa Dhana ya Jihadi na Nafasi Yake

Jihadi ni istilahi maalumu ilioko katika sheria za Kiislamu (fiqh), ikimaanisha mapambano ndani ya njia ya Mwenye Ezi Mungu kwa kutumia nafsi pamoja na mali. Mapambano haya huwa ni mapambano ya kivita dhidi ya washirikina na wanaoasi mamlaka halali. Madhumuni ya mapambano haya ni kuendeleza Uislamu pamoja na kusimamisha nembo zake. [1] Jihadi ni moja ya sehemu za Matawi ya Dini (Furu al-Din). [2] Wanazuoni wa sheria (fuqaha), wamechambua kwa kina hukumu zake za kisheria kuhusiana na Jihadi, kwenye sura (mlango) maalumu vitabuni mwao kwa jina la "Jihadi". [3] Kuna idadi ya maneno 35 ndani ya Qur’ani kuhusiana na Jihadi pamoja na maneno mengine yanayofungamana nalo. [4] Aidha, kuna Hadithi nyingi kuhusiana na kanuni na fadhila zake, zilizonukuliwa katika vyanzo mbali mbali vya Hadithi, Hadithi ambazo huwa ndiyo rejeo linalotumiwa na wanazuoni wa sheria katika mchakato wao wa kutoa hukumu za kisheria kuhusiana na Jihadi. [5]

Ukiachilia mbali ile maana mahsusi ya kifiqhi kuhusiana na dhana ya Jihadi. Matini mbali mbali za kidini, zimeonekana kutaja dhana hii huku ikirejela ile maana yake ya kilugha na ya kiujumla. [6] Yaani kwa maana ya 'kujitaabisha' au kufanya 'jitihada' kwa ajili ya kufikia lengo fulani. [7] Tukirejea katika baadhi ya Hadithi, tutakuta baadhi ya amali fulani zimepewa hadhi na sifa ya Jihadi, jambo linaloashiria uzito na umuhimu wa amali hizo. [8] Kwa mfano, katika Riwaya fulani, umeelezwa kwamba; 'Jihad al-Akbar' (Jihadi Kuu) ni ile jitihada ya nafsi katika kupambana na Ibilisi pamoja na matamanio haramu. [9] Aidha, vitendo kama vile; kuamrisha mema na kukataza mabaya, kutekeleza ibada ya Hija, kunena kauli adilifu mbele ya sultani (kiongozi) dhalimu, kujitahidi kuhuisha amali (nyenendo) njema katika jamii, muamala mwema wa mke kwa mumewe, jitihada za mwanamume za kuchuma riziki halali kwa ajili ya familia yake, pamoja na kufunga saumu katika hali ya joto kali, vyote hivyo vimezingatiwa kuwa ni Jihadi katika njia ya Mwenye Ezi Mungu. [10]


Tafsiri Mpana ya Jihadi Kulingana na Mwongozo wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei

Kwa mujibu wa mtazamo na muongozo wa Kiongozi Mkuu wa pili wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ni kwamba; Dhana ya Jihadi haiwezi kubanwa katika mabano ya medani za kivita tu. Bali, inajumuisha nyanja zote za maisha ya umma, ikiwemo siasa, utamaduni, fikra, uchumi na ulinganizi (tabligh). [11] Kwa maoni yake, jitihada yoyote ile inayofanywa kwa nia ya kuzima shari za adui, huhisabiwa kuwa ni Jihadi. Kwa mfano, katika moja ya hotuba zake kwa kundi la wazalishaji na wahamasishaji wa uchumi wa Iran, alibainisha akisema kwamba; Suala la uzalishaji na kujitahidi katika njia hiyo ni moja ya Jihadi zilizo wazi kabisa, hii kwa sababu maadui wa Iran wamekusudia kuidhoofisha nchi hiyo. [12]


Nafasi ya Jihadi Ndani ya Uislamu

Kuna Aya Qur'ani na Hadithi kadhaa zilizokuja kubainisha sifa mbali mbali adhimu kuhusiana na umuhimu wa Jihadi. [13] Aya za 20 na 21 za Sura At-Tawba, ndio Aya zilizokuja zikielezea hadhi ya juu mno waliyonayo mbele ya Mungu, wale wanaopambana katika njia ya Mwenye Ezi Mungu kwa nafsi zao pamoja na mali zao. Watu hawa wanatambuliwa kama ni miongoni mwa watu waliofanikiwa, nao wamepewa ahadi ya kupata rehema za Mwenye Ezi Mungu, kupata maridhawa ya Mwenye Ezi Mungu, pamoja na bustani za milele. [14]

Kwa mujibu wa Aya ya 95 ya Suratu An-Nisa, Mwenye Ezi Mungu amewainua na kuwapa hadhi ya juu kabisa, wale wja wake wanaoshiriki jihadi hadi, ikilinganishwa na Waislamu wengine ambao hawakushiriki vita vya kupigana Jihadi. [15] Katika baadhi ya Riwaya, Jihadi imefafanuliwa kama ni moja ya milango ya Jannah, ambayo Mwenye Ezi Mungu ameifungua kwa ajili ya wapenzi wake na waja wake maalumu. [16] Katika moja ya Riwaya zinazozungumzia umuhimu wa Jihadi, amali hii imetajwa kama ni tendo lenye uzito na hadhi kubwa zaidi baada ya kutimiza faradhi (msingi), na katika riwaya nyingine, imeelezwa kama kitendo bora zaidi baada ya kusilimu. [17] Aidha, katika Riwaya nyengine, Jihadi huchukuliwa kama ni kilele cha juu cha Uislamu, pia Riwaya nyengine zinahisabu amali hii kama ni moja ya misingi ya imani. [19]

Kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa wataalamu wa fiqhi ya Kishia anayeitwa Muhammad Fadhil Lankarani ni kwamba: Kuna umuhimu na malipo makukubwa katika kupigana Jihadi na kufa muhanga kwa ajili ya Mwenye Ezi Mungu na kuhuisha dini Yake. Hivyo basi, suala la Jihadi haliwezi kuingia kwenye mabano ya ile sheria au hukumu ya kiakili iitwayo (Daf’u Al-dharar Al-muhtamal), nayo ni ile hukumu inayomtaka mtu kujiepusha jambo linaloweza kumsababishia madhara. Ila kwa kwakuwa Jihadi ina malipo na manufaa makubwa, haiwezi kuingia ndani ya sheria hiyo ya kuepuka hatari inayotarajiwa. [20]


Imamu Ali (a.s) Anasema:

Baada ya mtu kuamua kuwa Muislamu, Jihadi ndilo tendo lenye hadhi ya juu kabisa, na ni ndiyo uti wa mgongo unaosimamisha dini. Jihadi hujenga heshima isiyo kifani na ni amale yenye malipo makubwa mno. Jihadi ni amali ngumu lakini thawabu ni nyingi, na malipo yake baada ya shahada, ni bishara ya uhakika wa kupata Pepo (kufa shahidi ni tiketi ya moja kwa moja ya kwenda Peponi).

Sheikh Hurr Amili, Wasa’il al-Shi’ah, juz. 15, uk. 94, Chapa ya Mwaka 1416 Shamsia.


Malengo na Matunda ya Kijihadi

·       Kutokomeza fitina. [21]

·       Kuwahami wanaodhulumiwa na waliodhoofishwa (wanaokandsamizwa). [22]

·       Kupigana dhidi ya ushirikina na ibada za kuabudu masanamu. [23]

·       Kujilinda dhidi ya dhuluma na uvamizi. [24]

·       Kuimarisha misingi na ustawi wa dini. [25]

·       Kuhifadhi na kulinda maeneo ya ibada. [26]


Maoni Tofauti Kuhusiana na Chanzo cha Amri ya Jihadi Katika Uislamu

Kuna hali ya kutofautiana kimawazo miongoni mwa wataalamu (wanazuoni) wa fani ya tafsiri ya Qur'ani, kuhusu ni Aya gani iliyotoa amri ya kwanza ya Jihadi, na ni katika muktadha upi au ni katika mazingira gani iliteremshwa Aya hiyo. [27] Miongoni mwa wanazuoni hawa, akiwemo Fakhru al-Razi na Tabrisi wanaamini kwamba; Aya ya 39 ya Suratu Al-Hajj, ndiyo Aya kwanza kabisa iliyotoa idhini ya kupigana jihadi, ambayo ilikuja kuwaidhinisha Waislamu kupambana na wapagani wa Makka. [28] Kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu hawa, wapagani wa Makka walikuwa wakiwapiga, kuwatesa na kuwaadhibu Waislamu wa wakati huo. Waislamu hao walikuwa wakimwendea bwana Mtume (s.a.w.w), hali wakiwa na majeraha na vichwa vilivyopasuliwa kufuatia mateso hayo, huku wakilalamika na kuomba ruhusa ya kupigana na mahasimu hao. Hata hivyo, kila mara bwana Mtume (s.a.w.w), alikuwa akiwahimiza kuwa na subira, akisema kwamba; bado amri ya kupigana Jihadi haijaamuriwa na Mwenye Ezi Mungu. Hali hii iliendelea hadi kumalizika kipindi cha uhamaji (Hijra), Waislamu wakahama kutoka Makka kwenda Madina, na miezi saba baadaye, [29] Aya ya idhini ya Jihadi iliteremshwa na hivyo ikawa ndiyo amri ya kwanza kutolewa kwa ajili ya kupigana Jihadi. [30]

Kwa upande wa pili kuna baadhi ya wanazuoni wanaoamini kwamba; Aya ya 190 ya Suratu al-Baqarah isemayo: (وَ قَاتِلُوا فِی سَبِیلِ اللَّهِ الَّذِینَ یُقَاتِلُونَکُمْ) (Na pambaneni katika njia ya Mwenye Ezi Mungu na wale wanaokushambulieni), ndiyo Aya ya kwanza iliyowaamuru Waislamu kupigana Jihadi dhidi ya wapinzani wao. Pia kuna wengine wanaosema kwamba; Aya ya kwanza kuhusiana na suala hili, ni ile Aya ya 111 Sura ya At-Tawba. [31] [Maelezo 1: Mwenye Ezi Mungu amenunua kutoka kwa Waumini nafsi zao pamoja na mali zao kwa thamani ya kuwapa Pepo. Wao wanapigana katika Njia ya Mwenye Ezi Mungu, hivyo wanaua na kuuawa. Hii ni ahadi ya haki aliyoitoa juu Yake, ahadi ambayo imetajwa katika Taurati, Injili na Qur'ani. Na ni nani basi mtekelezaji zaidi wa ahadi zake kuliko Mwenye Ezi Mungu? Hivyo, furahieni mkataba wenu mlioufunga Naye. Na huu ndio ukombozi na ushindi adhimu. Chanzo: Qur'ani, 9:111; tafsiri ya Qur’ani ya Makarem Shirazi]

Kulingana na maoni na maelezo ya mwanazuoni na mfasiri wa Qur’ani anayeitwa Makarem Shirazi ni kwamba; Aya ya 39 ya Suratu Al-Hajj, iliyotumia neno ‘ruhusa’ (kwa Kiarabu ‘idhin’), indiyo Aya inayoonekana kuwa wazi zaidi katika kutoa amri ya Jihadi. Hivyo Aya hii ndiyo Aya yenye haki zaidi ya kuhisabiwa kuwa ndiyo ya kwanza kuidhinisha Jihadi. [32]

Baadhi ya wafasiri wa Qur’ani, wakutumia Aya ya 111 ya Suratu Tawba kama msingi wa hoja zao, wanasisitiza wakisema kwamba; dhana ya Jihadi si uvumbuzi wa kipekee uliovumbuliwa na Uislamu, bali ni mwendelezo wa kanuni ya ziliyokuwepo katika mifumo yote ya sharia zilizotangulia. [33]

Aina za Jihadi

Kwa mtazamo wa mafaqhi wa Kiislamu, Jihadi imegawanywa katika aina mbili: Jihadi ya Kuanzisha vita (Jihadi Anzishi) na Jihadi ya Kujihami. [34]

Jihadi Anzishi

Makala kuu: Jihadi Anzishi au Ibtidai

Jihadi Anzishi ni Jihadi ya kuanzisha vita dhidi ya washirikina na wasioamini kwa lengo la kuwaita kwenye Uislamu na kuwaleta kwenye imani ya kuamini Mungu mmoja. [35] Katika aina hii ya Jihadi, Waislamu ndio wanaoanzisha vita dhidi ya wengine. [36] Kwa makubaliano ya wanasheria wote wa Kiislamu, ni kwamba; Ni Wajibu Kifai (wajibu wa kijamii) kupigana Jihadi kwa ajili ya kueneza Uislamu. Hii ina maana ya kwamba; wajibu huu unamkabili kila Muislamu aliye baleghe, aliye huru, mwanamume, ambaye hana tatizo la kukabiliwa na ugonjwa au uzee. Wajibu huu ni mapambano dhidi ya wasioamini ambao hawako chini ya ulinzi wa Waislamu na ambao ni waasi. [37] Kwa mtazamo wa wanasheria wa Kishia (Shia Imamiyya), ni kwamba; Jihadi Anzishi haiwezi kukubalika bila ya kuwepo Imamu Maasumu, na haiwezi kujiri bila ya kupata ruhusa yake, au ya mwakilishi wake maalum. [38] Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni wameiruhusu Jihadi hii hata katika kipindi cha kutowepo kwa Imamu Maasumu. [39]

Masharti mengine yaliyowekwa na mafaqihi kwa ajili ya Jihadi Anzishi (kuanza vita visivyo vya kujitetea), ni pamoja na; Waislamu kuwa na nguvu za kutosha katika kuanzisha vita, kuwalingania na kuwaita kwenye Uislamu wale wasioamini, pamoja na kuwapa hoja za kutosha kabla ya kuanza vita hivyo dhidi yao. [40]

Jihadi ya Kujihami

Jihadi ya kujihami ni vita vya mapambano yanayofanywa kwa lengo la kuulinda Uislamu pamoja na nchi za Kiislamu dhidi ya mvamizi fulani aliyevamia nchi hizo. Hii ni pale adui anapokusudia kuzitawala nchi hizo, kufuta heshima yake, kupora mali za Waislamu, au kuua idadi fulani kati ya Waislamu wa nchi hizo. [41] Kulingana na maoni ya wataalamu wa sheria za Kiislamu (mafaqihi wenye dajara ya ijitihadi), ni kwamba; mapambano haya ya kujilinda yana hukumu ya wajibu wa pamoja (Wajibu Kifaya), kwa kila mtu mwenye uwezo wa kupigana, wakiwemo wanaume, wanawake, wazee, vijana, watumwa na walio huru. [42]

Aina hii ya jihadi haihitaji kuwepo kwa Imamu Maasumu na kupata ruhusa yake, au ruhusa maalumu itokayo kwa mwakilishi wake. [43] Baadhi ya vita vilivyopigwa wakati wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), ambavyo vinahesabiwa kuwa ni vita vya kujihami, ni kama vile; vita vya Ahzab, Uhud, Mu'tah, Tabuk na Hunain. [44]

Aidha, mwanazuoni Mohammad Javad Fazel Lankarani, ametaja aina nyingine ya jihadi aliyoiita "Jihad Dhibbiyy". [45] Aina hii ya Jihadi amechopoa ndani ya dhahiri ya maandishi wa wanazuoni mbali mbali. Jihadi hii inalenga kuulinda Uislamu kama Uislamu. Kwa mantiki hiyo, ikiwa kuna tishio la kuangamizwa kwa Uislamu kutoka kwa mtawala yeypte yule dhalimu duniani, hapo inakuwa ni wajibu kwa kila Muislamu binafsi kuulinda Uislamu. [46]


Adabu na Sheria (Hukumu) za Jihadi

Wanasheria wa Kiislamu, wakitegemea Aya za Qur'ani pamoja na Hadithi, wamebainisha adabu na kanuni kadhaa kuhusiana na Jihadi, ambazo baadhi yake ni kama ifuatavyo:

·       Marufuku ya vita ndani ya miezi mitukufu: Wanasheria, wakirejelea baadhi ya Aya kama vile Aya ya 217 Suratu Al-Baqara na Aya ya 36 ya Suratu Al-Tawba, wanasema kwamba; ni haramu kwa Waislamu kupigana Jihadi ndani ya miezi mitukufu, ambayo ni; Rajab, Dhul-Qa'dah, Dhul-Hijjah, na Muharram). [47] [48] Hata hivyo, baadhi ya wanasheria (mafaqihi) wa Kisunni wanaamini kwamba; Sheria hii ilifutwa, na hivyo Waislamu wanaruhusiwa kupigana Jihadi wakati wowote na mahali popote. [49]

·       Wakati wa kuanza vita: Inapendekezwa kuanza vita baada ya jua kupinduka (baada ya adhuhuri) na baada ya kusaliwa kwa sala ya Adhuhuri na Alasiri. Pia, haipendelewi kushambulia wakati wa usiku isipokuwa kwa dharura tu. [50]

·       Hukumu ya Muislamu Anayeuawa Vitani: Kuna makubaliano kamili kutoka kwa wanasheria wa Kishia, ya kwamba; yeyote yeyote yule anayeuawa katika uwanja wa vita, anahisabiwa kuwa ni shahidi na huwa na hukumu maalum za kishahidi. [51]

·       Matumizi ya silaha: Inaruhusiwa kupigana na adui kwa kutumia aina yoyote ile ya silaha na kwa njia yoyote ile itakayopelekea ushindi. [52] Hata hivyo, haipendelewi kukata miti, kurusha moto, au kuelekeza maji kwa adui ili kuwazamisha, isipokuwa kwa dharura tu. [53]

·       Kulinda wasio wapiganaji: Ni haramu kuwaua wanawake, watoto, wasio na akili timamu, na wasikuwa na uwezo kujihami, kama wazee, vipofu, na vilema, mradi tu wasiwe ni kwa kutoa ushauri wa kimapigano vitani humo. Hata hivyo, sheria hii haitumiki katika hali ya dharura; kwa mfano, adui akiwatumia watu hao kama ni ngao, au ikiwa ushindi dhidi ya maadui hao, utegemea kuwalenga watu hao mbao ni marufuku kuuawa. [54]

·       Hila vitani: Yaruhusiwa kutumia hila vitani, isipokuwa tu kama maadui hao walipewa ahadi ya amani kutoka kwa Waislamu. [55]

·       Kuomba msaada kwa wasio Waislamu: Inaruhusiwa kuomba msaada wa kijeshi kutoka kwa wasio Waislamu, ikiwa kufanya hivyo kutakuwa na maslahi na hakutakuwa na hatari ya usaliti. [56]

·       Kumtii kiongozi: Ni lazima kwa wapiganaji wote kumtii kamanda wao. [57]


Ukwepaji na Utoro wa Kukimbia Mapambano ya Jihadi

Makala ya Kuu: Utoro wa Kukimbia Vitani

Kwa mujibu wa sheria, ni haramu mtu kutoroka na kukimbia katika medani za vita. Kwa mujibu wa kauli za baadhi ya mafaqihi (wanazuoni wa sheria za Kiislamu) pamoja na baadhi ya wafasiri wa Qur'ani, ni kwamba; Suala la kutoroka vita linatambulikana kama mojawapo ya madhambi makuu (mina al-kabaa’ir). [58] Isipokuwa, iwapo idadi ya wapiganaji wa Kiislamu itapungua na kuwa chini ya nusu ya vikosi vya adui; mazingira ambayo, hufuta wajibu wa kupambana na maadui hao. [59]

Kadhalika ni kwa Muislamu kukhalifu amri inayomtaka kushiriki Jihadi. [60] Baadhi ya Aya za Qur'ani Tukufu zimebainisha wazi chimbuko la ukiukaji huu. Miongoni mwa sabubu zilizotajwa na Qur’ani, ni pamoja na; khofu, [61] mwelekeo wa kupenda anasa za dunia, [62] udhaifu wa imani, unafiki, [63] maradhi ya nafsi pamoja na uasi. [64] Kuna madhara kadhaa yaliotajwa ndani ya Qur'ani kuhusiana na ukiukaji wa jihadi, miongoni mwa madhara hayo ni kama vile: maangamizi, [65] adhabu za kidunia pamoja na Akhera, [66] kunyimwa neema na baraka duniani pamoja na Akera, [67] kuchipuka kwa fitina na ufisadi ndani ya jamii. [68]


Uchambuzi wa Fatwa Maarufu za Mafaqihi wa Kishia Kuhusu Jihadi

Makala Kuu: Hukumu za Jihadi

Ufuatao ni muhtasari wa baadhi ya fatwa muhimu zilizotolewa na mafaqihi (wanasheria wa Kiislamu) na Maraji’i Al-Taqlid (viongozi wakuu wa kidini wenye hadhi na idhini ya kutoa fatwa) wa madhehebu ya Shia katika vipindi mbalimbali vya historia kuhusiana na uwajibu wa Jihadi:

1.     Kufuatia mashambulizi ya Urusi katika ardhi ya Waislamu nchini Iran kati ya miaka 1241-1243 H, na kunyakua sehemu ya ardhi hiyo, baadhi ya Ulamaa wacha Mungu kama vile Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghita, Sayyid Ali Tabataba'i, Mirzai Qommi, Mulla Ahmad Naraqi, na Sayyid Muhammad Mujahid, walisimama na kutoa fatwa ya kupigana Jihadi. Walifanya hivyo ili kutekeleza faradhi ya kuunusuru Umma wa Kiislamu na kuunga mkono Dola ya Qajar katika kuwalinda Waislamu dhidi ya maadui wa dini ya Mwenye Ezi Mungu. [69] Fatwa hizi tukufu, pamoja na risala za fiqhi kuhusiana na Jihadi, zilikusanywa katika kitabu kiitwacho Ahkam al-Jihad wa Asbab al-Rashad kwa amri ya kiongozi Abbas Mirza, ambaye alikuwa ni mrithi wa kiti cha ufalme wa wakati huo. [70]

2.   Fatwa ya jihadi iliyotolewa na Muhammad Taqi Shirazi mnamo mwezi 20 Rabiul Awwal 1337 Hijiria, ni mfano mwingine wa fatwa yenye athari kubwa uwanja wa kisiasa. Fatwa hii Iliandaliwa kama jibu dhidi ya ukoloni na udhibiti wa Uingereza nchini Iraq. [71] fatwa hiyo ilitoka ikisema: "Ni wajibu kwa Wairaqi kudai haki zao za kimsingi, na ni sharti katika harakati zao hizo kuzingatia kanuni za amani na utulivu. Hata hivyo, endapo utawala wa Uingereza utagoma kutimiza matakwa yao halali, inaruhusiwa kwao kisheria kutumia nguvu ya kujilinda (kupigana Jihadi)." [72]

3.      Katika historia ya hivi karibuni, ya mwaka 2014, kufuatia udhibiti wa kundi la kigaidi la Daesh katika maeneo makubwa ya magharibi na kaskazini mwa Iraq, Ayatullah Sayyid Ali Sistani alionekana kusimama kidete na kutoa fatwa ya Jihadi dhidi ya kundi hilo. [73] Fatwa hii ililenga kukabiliana na tishio la Daesh katika kuismbaratisha jamii pamoja na kupoteza malengo ya dini. Kisheria ilikuja kubainisha kuwa; ni Wajibu Kifaya (wajibu wa kijumuiya) kwa raia wote wa Iraq wenye uwezo wa kimwili na kijeshi kupambana na magaidi. Na kwamba kila mmoja mwenye uwezo huo, anatakiwa kujitokeza na kulinda nchi, umma na maene matakatifu yao kwa kujiunga na majeshi ya ulinzi na usalama wa nchi hiyo. [74]


Dhana Chachu na Shupavu Kuhusiana na Falsafa ya Jihadi


Mnamo karne ya kumi na nne na kumi na tano Hijria, dhana ya jihadi imegeuka kuwa ndiyo kiini cha mijadala kwa baadhi ya Waislamu wenye mirengo ya Kisalafi, likiwemo kundi la Al-Qaeda na ISIS. [75] Makundi ya kiJihadi Salafi, yanaonekana kuitukuza zaidi jihadi kuliko Furu' al-Din zote (matawi ya dini). Wao huitukuza amali hii na kuipa kipau mbele zaidi kuliko misingi mengine yote ya kiutenda ndani ya Uislamu, kama vile sala, saumu na hija. Masalafi hawa wanaamini kuwa Muislamu yeyote asiyetekeleza jihadi, anaonekana kuwa ameshindwa kuielewa misingi halisi ya Uislamu. [76]

Imeelezwa kuwa baadhi ya makundi haya yenye itikadi kali, yalioathiriwa na fikra za Sayyid Qutb, [77] yanashikilia mtazamo usemao kuwa; Kiasli Ardhi zilizomo ulimwnguni humu, ima ni Dar al-Islam (eneo la utawala wa Kiislamu) au ni Dar al-Harb (ardhi ya ujahili), ambalo ni eneo la vita. Dar al-Islam ni lile eneo linalotawaliwa na Uislamu, ambalo sharia za Kiislamu zinatekelezwa ndani yake, na hukumu zake zinasimama ipaswavyo. Hivyo basi, jamii yoyote ile isiyo na sifa hizi, inajulikana kama ni Dar al-Harb, ambapo Waislamu wana wajibu wa kupambana nayo au kuwa katika suluhu nayo huku wakiitoza jizya (ushuru maalumu) jamii ya wakazi wake. [78]

Kwa kupotosha maana ya jihadi na kupanua wigo na vigezo vya dhana ya ukafiri, [79] makundi haya ya Jihadi ya Kisalafi, yamemeonekana kutekeleza vitendo kadhaa vya kigaidi na kusababisha ghasia ndani ya mataifa mabli mbali ulimwenguni, hususan maeneo ya Waislamu, na hivyo kuwasilisha taswira hasi na ya kikatili juu ya Uislamu duniani. [80]

Kinyume na mtazamo huu, mafaqihi (wanazuoni wa sheria) wa upande wa madhehebu ya Kishia wana ijma (makubaliano kamili) ya kwamba hakuna jihadi Anzishi katika zama za Ghaiba ya Imamu Maasumu (kutowepo kwa Imamu maasumu), ispokuwa Jihadi ya Kujihami (defensive Jihad), ambayo ni Jihadi ya kujitetea dhidi ya wavamizi. Jiahi hii haimaanishi matumizi ya nguvu na ghasia, bali ni haki ya msingi ya kila taifa kujilinda dhidi ya uvamizi. [81] Kulingana na Ni’imatullah Salihi Najafabadi, faqihi wa Kishia, ni kwamba; Jihadi ilioko katika Uislamu sio chombo cha kulazimisha imani kwa njia ya Jihadi Anzishi (offensive Jihad) dhidi ya jamii zisizoamini Uislamu, ambazo hazioneshi uadui dhidi ya Waislamu. [82] Akirejelea Aya ya 90 ya Surah An-Nisaa, Najafabadi anaharamisha vita vya kuanzisha dhidi ya makafiri wasio na madhara kwa Uislamu, [83] na anashikilia nadharia isemayo kuwa; Vita vyote vya bwana Mtume (s.a.w.w), vilikuwa ni vita vya kujitetea dhidi ya uchokozi wa maadui, ambavyo vililenga kuwakomboa wale waliokuwa wakikandamizwa. [84]