Imani

Kutoka wikishia

Imani (Kiarabu: الإيمان) ni kuwa na itikadi ya moyoni juu ya Mwenyezi Mungu na upweke Wake, (ya kwamba Mungu ni mmoja) Utume, mafundisho ya Mtume (s.a.w.w) na Maimamu Maasumina kumi na wawili (a.s). Mafakihi wa Shia wanaichukulia imani kuwa ni miongoni mwa masharti ya lazima Marjaa Taqlidi, Imamu wa Sala ya Jamaa, kadhi na mpokeaji wa Zaka. Kulingana na wanazuoni wengi wa Kishia, imani sio jambo la kufuata na kuiga (sio katika mambo ya kukalidi).

Wanateolojia wa madhehebu ya Shia wamezingatia ulazima wa imani sambamba na imani ya tawhidi, Utume wa Mtume (s.a.w.w), uadilifu wa Mwenyezi Mungu na ufufuo, imani juu ya Uimamu wa Maimamu maasumina baada ya Mtume. Kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'ani Tukufu, imani ni tofauti na Uislamu na iko katika kiwango cha juu zaidi yake; pia, imani ina uwezo wa kuongezeka na kupungua, na hakuna mtu anayeweza kulazimishwa kuamini.

Wanazuoni wengi wa Kishia wanaamini kwamba, Uislamu ni imani tu, na kwa msingi huu, kila muumini anahesabiwa kuwa Mwislamu; lakini sio kila mwislamu ni muumini. Baadhi ya wanazuoni wa Kishia, kama vile Khwaja Nasiruddin Tusi na Shahid Thani, wanaamini kwamba, imani na Uislamu wa kweli ni kitu kimoja; lakini Uislamu wa dhahiri uko katika kiwango cha chini kuliko imani.

Utambuzi wa Maana

Katika hadithi na kazi za fiqhi za wanazuoni wa Kishia, imani inatumika katika maana mbili za Aam (jumla) na Khaas (maalumu). Maana ya jumla ni kuamini kwa moyo mafundisho yote ya Mtume wa Uislamu, na maana maalumu, sambamba na maana ya kwanza, inaambatana na kuamini Uimamu na Wilayah (uongozi) wa Maimamu kumi na wawili. [1] Kwa mujibu wa maana maalumu na makhsusi ya imani, Mashia wote Imamiyah (Mashia wa Maimamu Kumi na Wawili) wanahesabiwa kuwa ni waumini. [2]

Imani kwa maana maalumu imetumika katika vipengele vingi vya fikihi, kama vile ijtihadi, taqlid, tohara, Sala, Zaka, Khumsi, Saumu, itikafu, Hija, wakfu, nadhiri, utoajii hukumu na ushuhuda, na inachukuliwa kuwa ni sharti kwa ajili ya kusihi na kukubalika kwa ibada zote. [3] Imani ni sharti kwa Marjas Taqlid, Imamu wa Sala ya Jamaa, anayestahiki Zaka na Khumsi, kadhi, shahidi na mgawaji wa mali aliyeteuliwa na Hakim Shar’i (mtawala wa kisheria). [4] Imeelezwa kuwa, mafakihi wengi wameweka sharti la imani kwa muadhini na anayefanya Hija ya niaba. [5]

Sheikh Mufid, mmoja wa wanavyuoni wa Shia Imamiyyah, anaichukulia imani kuwa ni kusadikisha kwa moyo na kukiri kwa ulimi na kitendo cha utiifu; [6] Shafi’i mmoja wa Maulamaa wa Ahlu-Sunna pia ana mtazamo huu huu. [7] Baadhi ya wanazuoni wa Shia Imamiyyah akiwemo, Sayyid Murtadha, Sheikh Tusi, Ibn Maytham Bahrani, Fadhil Miqdad na Abdul-Razzaq Lahiji wanaamini kwamba, imani ni kitendo cha moyo na kazi ya moyo, na kwa msingi huo, imani ndio ile itikadi ya moyo kwa Mwenyezi Mungu, Mtume na wahyi, na Muumini ni mtu anayeamini kwa moyo wake na wala haitaji kukiri kwa ulimi. [8]

Vielelezo

Katika Qur'ani Tukufu, kuna vielelezo na mifano ya imani ambayo imebainishwa; miongoni mwayo ni imani juu ya Mwenyezi Mungu, [9] imani kwa Manabii wote, [10] imani katika yale ambayo Mwenyezi Mungu aliwateremshia Manabii; kama vitabu vya mbinguni, [11] kuamini Siku ya Kiyama, [12] kuamini Malaika, [13] na imani kuhusu ghaibu. [14]

Wanateolojia wa Kishia wanaona imani inalazimiana na kuamini tawhidi, uadilifu wa Mwenyezi Mungu, ufufuo, Manabii na imani ya Uimamu wa Maimamu Maasumu baada ya Mtume na kwamba, ni muhimu kwa ajili ya imani. [15] Kwa upande mwingine, Muutazilah wanaamini kwamba, imani maana yake ni kuamini tawhidi, uadilifu, kuukubali Utume wa Mtume, bishara na habari mbaya (tishio la adhabu) na kusimama kidete kuamrisha mema na kukataza maovu. [16] Ashairah wanaamini kuwa sharti la imani ni kusadikisha kila alicholeta Mtume; kama vile kumpwekesha Mwenyezi Mungu na wajibu wa Sala. [17]

Athari na Sifa Maalumu

Aya nyingi za Qur’ani kuhusiana na imani zinaelezea athari na sifa maalumu za imani. Imani ina tofauti na Uislamu na ipo katika daraja ya juu zaidi. [18] Imani ni uhakika na ukweli ambao unaambatana na mapenzi makubwa na shadidi juu ya Mwenyezi Mungu. [19] Mwenyezi Mungu anawatoa waumini kutoka katika giza na kuwaleta katika ulimwengu wa nuru. [20]

Kwa mujibu wa Qur’ani tukufu, imani ina uwezo wa kupungua na kuongezeka [21] na kupitia kwayo nyoyo za waumini hufikia utulivu na uthabiti. [22] Kadhalika imekuja katika Qur’ani ya kwamba, haiwezekani kumfanya mtu aamini kwa kumlazimisha na hivyo kumfanya awe muumini. [23]

Katika Aya za Qur'ani Tukufu kumebainishwa makosa, mapungufu na dhambi za waumini na wametakiwa kujirekebisha. [24]

Imani ya Kufuata (Kukalidi)

Ni mashuhuri baina ya wanazuoni wa Shia Imamiyah ya kwamba, katika imani suala la kufuata (kukalidi) halitoshi. [25] Mu’utazilah na Ashairah walio wengi wanaafikiana na Mashia katika mtazamo huu. [26] Mkabala na mafakihi wa Ahlu-Sunna, [27] Hashawiyah na Taalimiyah wanatambua kwamba, imani kwa njia ya kukalidi na kufuata pia ni sahihi. [28]

Uhusiano wa Uislamu na Imani

Wanazuoni wengi wa Kishia wanaamini kwamba, Uislamu na imani ni maneno mawili yenye mafuhumu na maana tofauti. Kwa msingi huo, wanaona kuwa, neno Uislamu lina maana jumla ikilinganishwa na maana ya imani; kwa maana kwamba, kila Muumini ni Muislamu, lakini sio kila Mwislamu ni Muumini. [29] Walio wengi katika Ashairah wana imani hii pia. [30]

Pamoja na hayo, Mu’tazilah [31] na walio wengi katika Makhawariji, Zaydiyyah, [32] Abu Hanifa na wafuasi wake [33] na Sheikh Tusi, [34] hawajakubaliana na suala la kuweko tofauti baina ya Uislamu na imani. Amin al-Islam Tabarsi amedai katika tafsiri yake ya Maj’maa al-Bayan chini ya Aya ya 35 ya Surat al-A'hzab kwamba: Imani na Uislamu ni jambo moja miongoni mwa wafasiri wengi wa Qur’ani na kukaririwa kwake ni kukariri kwa lafudhi tu. [35]

Khaaje Nasiru al-Din al-Tusi mwanateolojia wa karne ya 7 Hijria, [36] Shahid Thani fakihi wa Kishia wa karne ya 10 Hijria, [37] na Taftazani, mwanateolojia wa karne ya 8 Hijria, [38] wanaamini kwamba, imani na Uislamu wa kweli ni kitu kimoja; lakini Uislamu wa dhahiri unatofauti na imani na uko katika sura jumla; kwa msingi huu, watu ambao wana Uislamu wa dhahiri, hakuna ulazima kuwa wawe ni waumini lakini waumini wote ni Waislamu.

Allama Tabatabai (1281-1360 Hijria Shamsia), mwanafalsafa na mfasiri wa Qur’ani anasema kuwa, Uislamu na imani vina daraja na ili kufikia katika kila daraja la Uislamu, sharti la kufikia daraja inayofuata ni imani; kiasi kwamba, daraja ya kwanza ya Uislamu ni kukubali kidhahiri amri na makatazo ya Mwenyezi Mungu na baada ya hapo, no hatua ya kwanza ya imani, yaani kuamini kwa moyo na kuwa na imani na madhumuni na makusudio ya shahada mbili hatua ambayo hupelekea kufanyia kazi hukumu na sheria za Uislamu. [39]

Rejea

Vyanzo