Nabii Ibrahimu

Kutoka wikishia

Nabii Ibrahimu (Kiarabu: النبي إبراهيم (ع)), ambaye pia anajulikana kwa jina la Ibrahimu Khalilu (إبراهيم الخليل): Ni nabii wa pili miongoni mwa manabii wa Ulu al-Azmi. Ibrahimu aliteuliwa kuwa nabii kati ya watu wa Mesopotamia (baina ya mto Euphrates Tigris), kwa ajili ya kumlingania mtawala wa wakati huo (Namrud), pamoja na watu waliokuwa wakiishi eneo hilo kwenye imani ya Mungu mmoja. Ni watu wachache tu miongoni mwao walikubali mwaliko wake, hivyo alipokata tamaa katika kuwalingania watu hao alihama kwenda Palestina.

Kulingana na Qur’ani, watu wa Ibrahimu waliokuwa wakiabudu sanamu, walimtia mikononi na kumtupa kwenye moto baada Ibrahimu kuangamiza masanamu yao, lakini kwa amri ya Mwenye Ezi Mungu, moto huo ukawa baridi na salama kwa Ibrahimu.

Ismaili (Ishmaeli) na Ishaqa (Isaka) ni wana wawili na warithi wa nabii Ibrahimu. Ukoo wa Bani Israili, ambao ni asili ya manabii wengi, ikiwa ni pamoja na bibi Mariamu, mama wa Nabii Issa (Yesu), unatokana na kizazi cha Ibrahimu kupitia Nabii Ishaq. Mtume wa Uislamu pia anatokana na ukoo wa Ibrahimu kupitia kwa Ismaili, mwana mwingine wa Ibrahimu.

Qur’ani inahusisha ujenzi wa Kaaba na mwaliko wa kuwaita watu kwenye ibada ya Hajj kwa Nabii Ibrahimu, na kumtambulisha kama ni Khalilullah (rafiki wa Mungu). Kulingana na Aya za Qura’ni, baada ya kutahiniwa na kujaribiwa kwa mitihani mbalimbali, ikiwa ni pamoja na amri ya kuchinja mwanawe (Ismaili), Ibrahimu alipata hadhi ya uimamu mbali na cheo chake cha mwanzo cha unabii.

Wasifu wake

Kuzaliwa hadi kufariki

Watafiti wengi wamezingatia karne ya 20 kabla ya Kristo (Issa) kama ndio tarehe ya kuzaliwa kwa nabii Ibrahimu (a.s), huku wengine wakidai kwamba; tarehe sahihi zaidi ni 1996 kabla ya Kristo (Issa). [1] Katika kitabu cha Hawaadithu al-Ayyami, siku ya kuzaliwa kwake imetajwa kuwa ni mwezi kumi Muharram. [2] Baadhi ya wanahistoria wanadhani kuwa yeye alizaliwa mwezi mosi Dhul-Hijja. [3]

kaburi la Nabii Ibrahim katika mji wa Hebroni huko Palestina

Katika vyanzo vya Kiislamu, miji kadhaa imetajwa kuwa ni mahali pa kuzaliwa kwa Ibrahim (a.s). Kulingana na chanzo cha kihistoria cha Tabari, baadhi ya wanazuoni wameutaja mji wa Baabul au Kutha, ambao ni mji liokuwa ukitawaliwa na Namrudh wakati huo, ulioko maeneo ya Mesopotamia ya Iraq, kuwa ndio mahali alipo zaliwa nabii Ibrahimu. Pia kuna wengine walio utaja mji wa Al-Warqa au Harran, kuwa ndio mahali pa kuzaliwa kwake, na kusema kuwa baadaye baba yake alimpeleka Baabul au Kutha. [4] Katika moja ya Hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s), mji wa "Kutha" umetajwa kuwa ndio mahali pa kuzaliwa kwake na ndio makao makuu ya Namrudh. [5] Ibn Batuta, mtalii wa kihistoria wa karne ya sita Hijria, ametaja eneo liitwalo Bursi lililopo kati ya Halabu na Baghdad nchini Iraq, yeye amedai kwamba; eneo hilo ndilo linalodaiwa kuwa ni mahali pa kuzaliwa kwa Ibrahim. [6]

Ibrahim (a.s) aliishi miaka 179 au 200 na kufariki dunia huko Hebroni, Palestina, eneo ambalo leo hii linajulikana kwa jina la Al-Khalil. [7]

Baba yake

Kuna tofauti ya maoni kuhusiana jina hasa la baba yake Ibrahimu. Katika maandiko ya Agano la Kale, baba yake ametambuliwa kwa jina la "Terah" [8], ambalo limetajwa katika vyanzo vya historia ya Kiislamu kama ni Taarukh [9] au "Taraakh". [10] Katika Qur’ani, kuna ibara isemayo: ((وَ إِذْ قالَ إِبْراهِیمُ لِأَبِیهِ آزَرَ ; Na [taja] pale Ibrahimu alipomwambia baba yake Aazar)). [11] Kulingana na Aya hii, baadhi ya wafasiri wa Kisunni wanamchukulia “Aazar” kuwa ni baba wa Nabii Ibrahimu, [12] lakini wafasiri wa Kishia hawachukulii neno "abu" (baba) lililoko katika Aya hii kuwa na maana ya baba halisi. [13] Kulingana nao; neno "ab" katika Kiarabu si tu hutumiwa kwa maana ya baba, bali pia kwa maana ya mjomba, babu, mlezi, n.k. Allamah Tabatabai katika kitabu chake kiitwacho Al-Mizan anasema: "Bila shaka, 'Azar' aliyezungumziwa katika Aya hii si baba halisi wa nabii Ibrahimu, lakini kutokana na baadhi ya sifa maalumu alizo kuwa nazo, alijulikana kama ndiye baba yake, kwani neno “abu” linaweza kuwa na maana ya mjomba wa Ibrahimu, na kulingana na matumizi ya lugha ya Kiarabu, neno 'ab' pia hutumiwa kwa maana ya babu, ami na hata baba wa kambo. [14] Ibrahimu alikataa uhusiano na “Azar”, ambaye alimwita baba, ila hakuwa baba yake halisi. [15]

Kulingana na ripoti za vyanzo vya kihistoria, katika mwaka ambao nabii Ibrahimu (a.s) alizaliwa, kwa amri ya Namrudh, kila mtoto aliyezaliwa aliuawa. Hii ni kwa sababu utabiri wa wachawi walikuwa wametabiri kwamba; mwaka huo atazaliwa mtoto ambaye atagejenga msingi wa kupinga dini ya Namrudh na wafuasi wake na kuyavunja masanamu yao. Kwa sababu hiyo, mama wa Ibrahimu alikhofu watu wa Namrudh kumdhuru Ibrahimu, hivyo alimweka ndani ya pango karibu na nyumba yake, na baada ya miezi kumi na tano, alikwenda pangoni humo usiku na kumtoa nje ya pango hilo. [16]

Ndoa na watoto

Sarah alikuwa ndiye mke wa kwanza wa nabii Ibrahimu (a.s), na kulingana na Torati, mke huyo alimwoa huko Ur ndani ya mji wa Wakaldayo (Chaldeans). [17] Kulingana na kamusi ya Dehkhoda, kitongoji cha Ur au Aur kilichotajwa Torati kilikuwa mji na eneo la zamani la Sumer kusini mwa Babylonia. Mji huu, uliopo karibu na reli ya sasa kati ya Basra na Baghdad kusini mwa Iraq, ulikuwa ni kitovu muhimu cha utamaduni wa Sumeri, na kulingana na Torati, mji huo ndio mahali alipozaliwa nabii Ibrahimu (a.s). Jina la mji huu mkubwa, ulioanzishwa katika nyakati za zamani, lilipotea katika historia katika karne ya 4 Kabla ya Kristo, ambapo mji huo ilibaki chini ya kifusi miaka kadhaa, na kupatikana upya katika karne ya 19. [18] Kulingana na Torati, Sarah alikuwa ndugu wa kambo wa Ibrahimu, [19] lakini kulingana na Hadithi za Kishia, Sarah alikuwa ni binti wa khaloo yake Ibrahimu (a.s), na ni dada wa nabii Lutu (a.s). [20] Kulingana na mojawapo ya Hadithi hizi, Ibrahimu alimwoa binti huyu huko Kutha, ambaye alikuwa tajiri wa mali zikiwemo ardhi na mifugo. Baada ya Saraha kuaana na nabii Ibrahimu (a.s), mali zake ziingia ndani milki ya nabii Ibrahimu, naye akaiboresha na kuikuza zaidi mali hiyo. Kwa kweli, katika eneo lao, hapakuwa na mtu mwingine aliyekuwa na utajiri na mali kama yeye. [21]

Nabii Ibrahim hakubahatika kuwa na watoto kupitia Sarah, kwa hiyo Sarah aliamua kumpa mjakazi wake aliye julikana kwa jina la Hajar ambapo nabii Ibrahimu alipata mtoto aitwaye Ismail kupitia mjakazi huyo. [22] Pia Nabii Ibrahim baada ya miaka kadhaa, alibahatika kupata mtoto aliyeitwa Is'haq kupitia kwa bibi Sarah. Tukio la kuzaliwa kwa Is'haq, ima linafikiriwa kutokea miaka 5 au 13 baada ya Ismail. [23] Kulingana na ripoti fulani, wakati wa kuzaliwa kwa Is'haq, nabii Ibrahim alikuwa na zaidi ya miaka 100 huku bibi Sarah akiwa na miaka 90. [24] Kulingana na ripoti nyingine, Is'haq alizaliwa miaka 30 baada ya Ismail ambapo kwa wakati huo, nabii Ibrahimu alikuwa tayari amesha fikisha umri wa miaka 120. [25]

Imesemekana kwamba baada ya bibi Sara kufariki dunia, Ibrahim (a.s) alioa wanawake wengine wawili, ambapo mmoja alizaa naye watoto wanne na mwingine akazaa naye watoto saba, na jumla ya watoto wake wote ikawa ni watoto 13. [26] Ma’adhi, Zimran, Sarhaj, na Sabq ni watoto wake kupitia mke aliyeitwa "Kinturaa", na Naafis, Madyan, Kishan, Shuruukh, Umaym, Lut, na Yaqshan kutoka kwa mkewe aliyeitwa "Hajuni". [27]

Ibrahim ndani ya Qur’ani

Ibrahim ametajwa mara 69 katika Qur'ani. [28] Kuna Sura kamili ndani ya Qur’ani iliyopewa jila Ibrahim, Sura ambayo inahusiana na maisha ya nabii Ibrahim. [29] Qur'ani inaelezea mambo mengi kuhussiana na nabii Ibrahim, ikiwa ni pamoja na unabii wake na wito wake wa kuwaita watu kwenye tawhidi, uimamu wake, nia ya kumchinja mwanae (Ismail), miujiza ya kufufuka kwa ndege wanne baada ya kifo chao, na kupoza kwa moto kwa ajili yake.

Utume, Uimamu na Cheo cha Ukhalili (Kipenzi cha Mungu)

Katika Aya kadhaa za Qur'ani, tunapata kuzungumziwa kwa unabii wa nabii Ibrahim na wito wake wa kuwalingania watu tawhid. [30] Vile vile ametajwa tena katika Aya ya 35 ya Surat Al-Ahqaf, Aya ambayo inazungumzia mitume wa Ulu al-Azmi, ambapo Ibrahim ni mmoja wao, naye ni mtume wa pili wa Ulu al-Azmi baada ya nabii Nuhu (a.s). [31] Kulingana na Aya ya 124 ya Surat Al-Baqarah, Mwenye Ezi Mungu alimteua nabii Ibrahim (a.s) kama ni Imamu baada ya kumpima kwa vipimo kadhaa. Kwa mujibu wa mfasiri maarufu aitwaye Tabatabai ni kwamba; mamlaka ya Uimamu katika Aya hii inamaanisha uongofu wa kiroho; mamlaka ambayo hupatikana baada ya kufikia ukamilifu wa kiakili na kiimani, na ni cheo maalum cha kiroho kinachopatikana baada ya jitihada nyingi. [32]

Kulingana na Aya za Qur'ani, Mwenye Ezi Mungu alimchagua Ibrahim (a.s) kuwa ni Khalil (rafiki au kipenzi). Hiyo ndiyo sababu ya yeye kupewa jina la "Khalilullah" (rafiki wa Mwenye Ezi Mungu). [33] Kulingana na Hadithi zilizosimuliwa katika kitabu cha "Ilal Al-sharaii", kusujudu kwa wingi, kuto puuza maombi ya watu, kuto taka msaada kutoka kwa asiyekuwa Mwenye Ezi Mungu, kuwalisha watu, na ibada ya usiku ni miongoni mwa sababu zilizomfanya yeye apewe cheo cha Khalilullah na Mwenye Ezi Mungu. [34]

Ibrahim ni Baba wa Mitume

Kulingana na Qur'ani, Ibrahim ni babu wa idadi kadhaa ya mitume waliofuata baada yake. [35] Mtoto wake (Is-haq) ni babu wa Waisraili, na mitume kama Yakubu, Yusufu, Daudi, Suleimani, Ayubu, Mussa, Haruni, na mitume wengine wa Waisraili walizaliwa kupitia katika kizazi chake. [36]

Pia nasaba ya Nabii Issa kupitia kwa mama yake, Maryamu (a.s), inafikia hadi kwa Nabii Yakubu, mwana wa Is-haq. [37] Kulingana na Hadithi za Kiislamu, nasaba ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) inamfikia nabii Ibrahim kwa njia ya Isma'il, mwana mwingine wa Ibrahim. [38] Hiyo ndiyo sababu, yeye kupewa jina la "Abu al-Anbiya" (baba wa manabii). [39]

Miujiza

Kulingana na aya za Qur'an, kupoza kwa moto na kuwafufua ndege wanne ni miongoni mwa miujiza ya Nabii Ibrahim:

  • Kupoza kwa moto: Kulingana na Aya 57 hadi 70 ya Surat Anbiyaa, Ibrahim baada ya kuona watu wake hwataki kuacha kuabudu masanamu, aliamua kuyavunja masanamu hayo, kisha kulihusisha sanamu na kitendo hicho, akisema kuwaambai waabudio madanamu hayo; kama masanamu yana uwezo kuongea, basi yaulizeni ili yakupeni khabari. Washirikina walishindwa kutoa hoja, lakini bado waliamua kumuadhibu na kumtupa katika moto kwa sababu ya kuvunja masanamu yao. Hata hivyo, pale Ibrahimu alipofika motoni humo, kwa amri ya Mwenye Ezi Mungu, moto huo ukawa ni baridi usio na madhara kwake. [40]
  • Kuwafufua ndege wanne: Kulingana na Aya 260 ya Surat al-Baqarah, Mwenye Ezi Mungu alimtaka Nabii Ibrahim kuchinja ndege wanne na kuchanganya nyama zao, kisha kuziweka katika milima kadhaa. Ibrahim alitekeleza agizo hilo na kisha akawaita ndege hao. Ghafla ndege hao walifufuka na kumkaribia.

Hijra

Katika Aya ya 71 ya Surat al-Anbiya, imeelezwa kuhusiana na Ibrahim (a.s) ya kwamba: "Sisi tumempeleka (Ibrahim) pamoja na Lut katika nchi ambayo tumeibariki kwa ajili ya walimwengu." [41] Baadhi ya vitabu vya tafsiri vimefungamanisha nchi iliyozungumziwa katika Aya hii na ardhi ya Sham [42] au Palestina au Bayt al-Maqdis. [43] Katika moja ya Riwaya ya Imamu Swadiq (a.s), Bayt al-Maqdis pia imeashiriwa kama ni moja ya ardhi za marudio ya hijra ya Ibrahim (a.s). [44]

Ujenzi wa Ka'aba

Katika Aya ya 127 ya Surat al-Baqarah, imeelezwa kuwa; Ibrahim alisaidiana na mwanaeIsmail katika kujenga Kaaba [45] na kwa amri ya Mwenye Ezi Mungu aliwaita watu kushiriki ibada ya Hijja. [46] Kulingana na baadhi ya Riwaya, kwa mara ya kwanza kabisa Ka'aba ilijengwa na Nabii Adam (a.s) na kurekebisha tena na nabii Ibrahim. [47]

Kuchinja mwanawe

Makala asili: Dhabihullah

Moja ya majaribio ya Mwenyezi Mungu kwa Ibrahim ilikuwa amri ya kumchinja mwanawe. Kulingana na ripoti ya Qur'an, Ibrahim aliota ndotoni kwake kuwa anamchinja mwanae. Naye akaliweka suala hilo mbele ya mwanae, na mwanae alimtii baba yake na kumtaka atii amri ya Mwenye Ezi Mungu. Lakini wakati Ibrahim alipomlaza mwanawe kwa ajili ya kuchinja akiwa katika eneo la kuchinja, sauti ikasema: "Ewe Ibrahim, kwa hakika umetimiza agizo la ndoto yako. Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wafanyao mema. [Yaani tunaikubali nia yao safi na tukufu bila ya wao kutekeleza tendo lao]. Hakika jaribio hili lilikuwa ni la wazi na tumemwokoa mwanao kutoka kwenye uhanga mkubwa". [48]

Qur'an haikutaja jina la mwana wa Ibrahim ambaye alipaswa kuchinjwa. Hivyo basi kuna tofauti za maoni kati ya Washia na Masunni juu ya suala hili. Baadhi wanasema alikuwa ni Ismail na wengine wanasema alikuwa ni Is-haq [49]. Sheikh Tusi anaamini kuwa; kwa mujibu wa Riwaya za Shia, yaonekena kwamba; yeye alikuwa ni Ismail. [50] Mulla Sadra Mazandarani katika ufafanuzi wa kitabu Furu’u al-Kafi anafikiria maoni haya kuwa ni mtazamo mashuhuri kati ya wanazuoni wa Shia. [51] Katika Ziyara Ghufaila (ziara maalum ya Imamu Hussein (a.s) ya katikati ya Rajab), kuna ibara isemayo: ... Salamu iwe juu yako, Ewe mrithi wa Ismail, kichinjwa cha Mwenye Ezi Mungu! [52]"

Ibrahim katika Maagano Mawili

Katika Agano la Kale, Ibrahimu anatajwa kwanza kwa jina la Abramu; [53] lakini katika sura ya 17, Mungu anamwambia: "Na hii ni ahadi kati yangu na wewe, na wewe utakuwa ni baba wa mataifa mengi; na jina lako baada ya hapa halitakuwa Abramu, bali litakuwa ni Ibrahimu, kwa maana nimekufanya kuwa baba wa mataifa mengi."[54]

Kulingana na riwaya za Agano la Kale, Ibrahimu anatokana na kabila za Aramu (Aramaic), kutoka Bara Arabu lililohamia kando ya Mesopotamia (mto furati) katika Syria ya kaskazini. [55] Kulingana na Mwanzo Aya ya 11, ni kwamba; Terahi, (ambaye ni baba wa Ibrahim) akiwa pamoja na Ibrahim, Sarah, na Lutu, walianza safari kutoka Harani (Ur) kuelekea Kanaani, ila walifika Harani, Terahi alibaki eneo hilo ambako alifariki dunia. [56] Baadhi ya watafiti kutokana na maelezo ya Aya hii, wameibuka na natija ya kwamba; Ibrahimu alizaliwa huko Ur, lakini katika Mwanzo, Sura ya 12, ni kwamba; Harani (Ur) inatajwa kuwa ndipo mahali pa kuzaliwa kwa Ibrahimu. [57]

Kulingana na Taurati, Ibrahimu aliishi Harani hadi umri wa miaka 75, kisha akaenda Kanaani kwa amri ya Mungu. Alifanya safari hiyo akifuatana na mkewe (Sarah), pamoja na mtoto wa kaka yake (Lutu), na baadhi ya watu wa Harani. Walifika Kanaani, wakaweka hema upande wa mashariki wa Betheli, na kujenga madhabahu. [58] Baadaye, kutokana na njaa, walihamia Misri, [59] lakini baada ya muda mfupi, walirudi tena Betheli, [60] na baadaye wakahamia Hebroni (Al-khaliil), ambako walifanya makazi yao. [61]

Katika Taurati inasemekana kwamba; Ibrahimu alipoingia Misri, alimtambulisha Sarah (mkewe) kama ni dada yake, alifanya hivyo ili kujilinda na hatari za Wamisri juu ya zao za kumpokonya mkewe, endapo wangelijua kuwa yeye alikuwa ni mkewe. Farao wa Misri, aliyevutiwa na uzuri wa Sara, alimchukua kama ni mkewe, na kumtendea hisani Ibrahimu kama ni tunzo yake. Ila muda si mrefu, Mungu alimletea Farao na watu wake mapigo kutokana na tendo hilo ovu dhidi ya Ibrahim. [62] Ayatullah Tabatabai anaamini kwamba sehemu hii ya Hadithi ya Ibrahimu ilioko katika Taurati, inaonyesha kwamba Hadithi hiyo ni hadithi potofu, kwani mwelekeo wake hauendani sifa za mitume na utukufu wao, pia hadithi hii haioani, na hadithi zilizoko katika matoleo mengine ya Taurati. [63]

Agano la Kale linamtaja Isaka (Is-haqa) kama ni dhabihu (mchinjwa) wa Ibrahimu. [64] Katika baadhi ya matukio, Isaka anatajwa kuwa ndiye mtoto pekee wa Ibrahimu. [65] Pia katika Taurati, inasemekana kwamba; Mungu alimpa Ibrahimu ahadi ya kwamba; ardhi yote kuanzia Nile hadi Euphrates itawapa na kuwathithisha watoto wake wa baadaye, ambao watatokana na Isaka. [66]

Katika Agano Jipya, Ibrahimu anatajwa mara 72, na nasaba ya Yesu Kristo anatokana na Ibrahimu kupitia kwa Isaka, kupitia mababu 39 (Mathayo 1:1-7) au kupitia mababu 54 (Luka 3:24-25). Imani ya Ibrahimu katika Agano Jipya inaelezwa kuwa ni ya juu zaidi. Ibrahimu aliishi kama mgeni katika Palestina, ambayo haikuwa nchi yake mwenyewe, na alitii amri ya Mungu kwa kumtoa mwanawe kama ni dhabihu. [67]

Ibrahimu kwa mtazamo wa Irfani ya Uislamu

Kutoka kwa mtazamo wa wanafalsafa (wanairfani) wengi wa Kiislamu, ni kwamba; Ibrahimu (a.s) alikuwa msafiri wa kiroho ambaye alipata ukamilifu wa juu kabisa kupitia ngazi mbali mbali za kimaadili katika safari yake ya maadili ya kiroho. Abdulkarim al-Qushayri, mwanafalsafa (mwanairfani) na mfasiri wa karne ya nne na tano, anaamini kwamba; Ibrahimu (a.s) aliuona ulimwengu wa kiroho kabla ya kuanza safari yake, na kwamba hilo ilimfanya apendezwe na safari hiyo ya kiroho. Hata hivyo, Rashid al-Din Maybudi anaamini kwamba; mvuto huu ulimfanya awe na hamu ya kuvutika na kila maonesho na sura za madhihiriko (maakisiko) ya Kiungu, lakini alipogundua kutokuwa imara kwa maakisiko hayo, alielewa kwamba; maakisiko na madhihiriko hayo katu hayawezi kuwa na uhusiano na upendo wa dhati na halisi. [69]

Kulingana na maoni ya wanairfani ni kwamba; maelezo na riwaya juu ya kisa cha nabii Ibrahim zilizokuja katika Qura’n, kama vile kupoza kwa moto, nia ya kumchinja Ismail, kuepuka na ibada za kuabudu sayari za angani, kumuomba Mungu amuoneshe namna ya kufufuka kwa wafu, na kuchinja ndege, zimejaa ishara za kiroho yenye mkondo wa tafsiri za ndani kabisa. [70] Kwa mfano, katika kisa cha Ibrahim cha kuepukana na nyota, mwezi, na jua, na badala yake kuelekea kwa Mwenye Ezi Mungu, bwana Qushairi, aliifasiri nyota kama ni mwanga mdogo wa akili, mwezi kama ni elimu inayo husiana na matawi ya elimu ya amri za kiungu (elimu fafanuzi ya sharia za Mungu), na jua kama mysticism (elimu ya kumjua Mungu). [71] Abdurazzaq Kashani aliona matatu haya, kama ni maelezo na fafanuzi za viwango na daraja tatu za; kinafsi, kimoyo, na kiroho, ambapo Nabii hufikia kituo cha umoja (upweke wa Mungu) kwa kupita kwenye ngazi za viwango hivi vitatu. [72]

Kulingana na tafsiri ya Ibn Arabi ni kwamba; maana iliyokusudiwa katika nyota, mwezi, na jua ambayo Ibrahimu anakanusha uungu wao, si kwamba yeye alikusudia maumbile ya vitu hivyo, bali ni nuru na uwezo wa kiroho uliopo ndani ya vitu hivyo. [74]

Bibliografia (Seti ya Orodha ya Vitabu)

Kitabu Qahremane Tawhid (Bingwa wa Tawhidi) kilichoandikwa na Naser Makarem Shirazi, kilichochapishwa na Shule ya Imam Ali ibn Abi Talib (a.s), nacho ni kitabu kinachotoa maelezo na tafsiri ya Aya zinazohusiana na Nabii Ibrahim (a.s), kitabu hichi ni kitabu chenye kutoa picha kamili juu ya maisha, fikra na nyenendo za Nabii Ibrahim, chenye idadi ya kurasa 224. [75]

Maudhui yanayo fungamana

Vyanzo

  • The Holy Qurʾān.
  • The Bible. New Revised Standard Version.
  • Abu l-Futūḥ Rāzī, Ḥusayn b. ʿAlī. Rawḍ al-Jinān wa Rawḥ al-Janān. Mashhad: 1408 AH.
  • Azraqī, ʿAbd Allāh b. Aḥmad. Akhbār Makka. Mecca: Dār al-Thiqāfa, 1403 AH.
  • ʿAyyāshī, Muḥammad b. Masʿūd. Tafsīr ʿayyāshī. Tehran: Islāmiyya, 1380 AH.
  • Fakhr Rāzī, Abu Abd Allāh Muḥammad b. Umar. Mafātīh al-ghayb. Third Edition. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1420 AH.
  • Fīrūzmihr, Muḥammad Mahdī. Muqāyisa qiṣṣa Ibrāhīm dar Qurʾān wa Tawrāt. Mīqāt Hajj, [n.d].
  • Fayḍ Kāshānī, Mullā Muḥsin. Tafsīr al-Ṣāfī. Tehran: Intishārāt al-Ṣadr, 1415 AH.
  • Ibn al-Athīr. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Beirut: Dār Ṣādir, 1385 AH.
  • Ibn Saʿd, Muḥammad b. Manīʿ al-Baṣrī. Al-Ṭabaqāt al-kubrā. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1410 AH-1990.
  • Ibn ʿAbd Rabbih, Aḥmad Muḥammad. Al-ʿIqd al-farīd. Beirut: 1402 AH-1982.
  • Ibn Kathīr. Al-Bidāya wa al-nahāya. Beirut: Dār al-Fikr, 1407 AH-1986.
  • Ibn Hishām, ʿAbd al-Malik. Al-Sīra al-nabawīyya. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].
  • Kāshānī, Mullā Fatḥ Allāh. Tafsīr Manhaj al-Ṣādiqīn. 3rd Edition. Tehrān: Kitābfurūshī Muḥammad Ḥasan Ilmī, 1336 Sh.
  • Masʿūdī, ʿAlī b. Ḥusayn. Ithbāt al-waṣīyya li-l Imām ʿAlī b. Abī Tālib. Qom: Anṣārīyān, 1384 Sh.
  • Mughniya, Muḥammad Jawād. Tafsīr al-kāshif. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1424 AH.
  • Māzandarānī, Muḥammad Hādī b. Muḥammad Ṣāliḥ. Sharḥ furūʿ al-kāfī. Edited by Muhammad Jawād Maḥmudī and Muḥammad Ḥusayn Dirāyatī. 1st Edition. Qom: Dār al-Hadīth li-Tibāʿat wa al-Nashr, 1429 AH.
  • Makārim Shirāzī, Nāṣir. Tafsīr-i Nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1374 Sh.
  • Maḥallī, Jalāl al‑Dīn and Jalāl al‑Dīn, al-Siyūṭī. Tafsīr al-Jalālayn. Beirut: Muʾassisat al-Nur li l-Matbuʿāt, 1416 AH.
  • Nishābūrī, Nizām al-Dīn. Tafsīr gharāʾib al-Qurʾān. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1420 AH.
  • Sajjādī. Ibrāhīm khalīl (a). Dāʾirat al-Maʿārif Islāmī.
  • Sayyid Quṭb. Fī ẓilāl al-Qurʾān. Beirut: Dār al-Shurūq. Edition 35. 1425 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. ʿIlal al-shārāyiʿ. Qom: Kitābfurūshī dāwarī. 1385 Sh.
  • Ṭāhirī, Muḥammad Ḥusayn. Ibrāhīm wa khāndānash dar Tawrāt wa Qurʾān. Dar Faslnāma Maʿrifat Adyān. 1388 Sh.
  • Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾan. Qom: Intishārāt Islamī Jamiʿa Mudarrisīn Ḥawza ʿIlmiyya, 1417 AH.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Tehrān: Intishārāt Nāsir Khusrow, 1372 Sh.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārīkh al-umam wa al-mulūk. Beirut: Dār al-Turāth, 1967.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. Ḥasan. Al-Tibyān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār Iḥyāʿ al-Turāth al-Arabī, [n.d].