Aya ya al-Ikmal

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Ayat al-Ikmal)

Ayat ya al-Ikmal (Kiarabu: آية الإكمال) (Aya ya kukamilika dini) ni sehemu ya Aya ya 3 katika Surat al-Maidah ambapo Mwenyezi Mungu anazungumzia kukata tamaa makafiri, kukamilika dini, kutimia neema za Mwenyezi Mungu na kukubaliwa dini ya Uislamu kwamba, ndio mafundisho ya mwisho kwa ajili ya wanadamu. Waislamu wa madhehebu ya Shia wakitegemea hadithi mbalimbali zilizopokewa kutoka kwa Ahlul-Bayt (as) wanaamini kuwa, Aya hii ilishuka katika tukio la Ghadir na makusudio ya kukamilika dini na kutimia neema za Allah ni kutangazwa Wilaya na uongozi wa Imamu Ali na kwamba, yeye ni mrithi wa Mtume (s.a.w.w.) na kiongozi wa Waislamu baada yake. Mkabala na nadharia hii, Waislamu wa madhehebu ya Ahlu- Sunna wanasema kuwa, Aya hii ilishuka katika siku ya Arafa na wanaamini kuwa, makusudio ya kukamilika dini ni kubainishwa hukumu na sheria zote za Uislamu.

Wafasiri wa Ahlu Sunna

Kutokana na kuwa mwanzo na mwisho wa Aya hii kumezungumziwa hukumu mbalimbali za kisheria, wafasiri wa Ahlu-Sunna wanasema kuwa, makusudio ya kukamilika dini ni kukamilika hukumu na sheria zote za Kiislamu; lakini Waislamu wa madhehebu ya Shia wao wanasema kuwa, kwa kuzingatia kwamba, Aya inazungumzia kukata tamaa makafiri, hukumu na sheria za Kiislamu pekee haziwezi kuwa sababu ya kukataa tamaa makafiri na Uislamu; kwani kukata tamaa kikamilifu makafiri hutokea pale Mwenyezi Mungu anapomteua na kumuainisha mtu ambaye ni mrithi na kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume kwa minajili ya kuwa msimamizi wa masuala ya dini na ambaye ataiendeleza dini. Shekhe Murtadha Mutahhari, msomi mahiri wa Kiislamu amezungumzia tofauti ya “Ikmal” na It’mam” kwa kusema: “Itmam” inasemwa pale inapokuwa kwamba, kitu kilikuwa na mapungufu hapo kabla; lakini katika “Ikmal” yumkini dhahiri yake yake ikawa sahihi na iliyokamilika, lakini kwa kuwa haina athari tarajiwa, itakuwa haijakamilika. Katika Aya ya al-Ikmal, suala la kuteuliwa Imamu Ali kuwa Imamu, hilo ni sehemu ya dini na wakati huo huo ni kamilisho la dini kama ambavyo pia ni sababu ya kukamilika viungo na vipengee vingine vya dini; hii ni kutokana na kuwa, roho ya dini ni Wilaya (uongozi) na Uimamu.

Nafasi

Ayat al-Ikmal ni sehemu ya Aya ya tatu ya Surat al-Maidah. [1] Aya hii ni miongoni mwa hoja zinazotumiwa na Waislamu wa madhebu ya Shia kwa ajili ya kuthibitisha Uimamu wa Imamu Ali (as), [2] katika Aya hii kuna mambo manne yamezungumziwa ambayo ni: Kukata tamaa makafiri, kukamilika dini, kutimia neema za Mwenyezi Mungu na kukubaliwa dini ya Uislamu kwamba, ndio mafundisho ya mwisho kwa ajili ya wanadamu. [3] Waislamu wa madhehebu ya Shia wakitegemea hadithi mbalimbali zilizopokewa kutoka kwa Ahlul-Bayt (as) wanaamini kuwa, mambo haya manne yalitimia kwa kutangazwa Imamu Ali (as) kuwa mrithi na kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume (s.a.w.w). [4]

Andiko na Tarjumi ya Aya

… الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الإِسْلامَ دِينًا ….

Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini.

Sababu ya kushuka kwake

Kadhalika angalia: Tukio la Ghadir

Vyanzo vya Waislamu wa madhehebu ya Shia vinatambua sababu ya kushuka Aya ya Ikmal kwamba, ni tukio la Ghadir na Wilaya (uongozi) wa Imamu Ali (as) kwa Waislamu. [5] Mashia wanaamini kwamba, baada ya Mtume (s.a.w.w) kumaliza kutekeleza Hija yake ya mwisho, akiwa nijani wakati wa kurejea aliwakusanya Waislamu katika eneo linalojulikana kwa jina la Ghadir na akawahutubia Waislamu ambapo katika hotuba yake hiyo alimtangaza rasmi Imamu Ali (as) kuwa Walii na kiongozi wa Waislamu baada yake. Baada ya hotuba hiyo, Waislamu walimpa baina na kiapo cha utii Imam (as) sambamba na kumpongeza ambapo miongoni mwa walikuwemo masahaba mashuhuri. [6] Kisha ikashuka Aya ya al-Ikmal na kutoa habari ya kukamilika dini. Allama Amini katika kitabu chake cha al-Ghadir na Mir Hamid Hussein katika kitabu chake cha Abaqat al-Anwar wameorodhesha ushahidi mwingi kutoka katika vyanzo vya Ahlu-Sunna unaothibitisha na kuunga mkono kushuka Aya hii kuhusiana na Imamu (as) na tukio la Ghadir. [7]

Wakati wa kushuka kwake

Waislamu wameafikiana kuhusiana na kwamba, Ayat al-Ikmal ilishuka katika Hjjat al-Wida’ (Hija ya kuaga). Hata hivyo wana mitazamo tofauti kuhusiana na siku ya kushuka kwake. [8] Akthari ya hadithi [9] za Ahlu-Sunna na Ij’maa ya wanazuoni wa Kishia ni kwamba, Aya hii ilishuka katika siku ya Ghadir au muda mchache baada yake. [10] Baadhi ya ya Maulamaa wa Ahlu-Sunna pia sambamba na kubainisha hadithi za kushuka Aya hii katika siku ya Ghadir wamezitambua hadithi hizo kuwa ni dhaifu. [11] Allama Amini sanjari na kubainisha sanadi (mapokezi) na itibari ya hadithi za Ahlul-Sunna anaamini kwamba, hadithi hizo ni za kuaminika na kutegemewa kwa mujibu wa vigezo vya Ahlu-Sunna. [12] Kwa mujibu wa baadhi ya vitabu na vyanzo vya Ahlu-Sunna vikiwemo vitabu viwili vya tafsiri na histioria vya Ibn Kathir al-Dimashqi ni kwamba, Aya hii ilishuka siku ya Arafa (9 Dhul-Hija). [13] Seyyid Ja’far Murtadha al-Amili mtafiti wa masuala ya historia wa Kishia anaamini kwamba, Aya ya Ikmal ilishuka mara mbili: Mara ya kwanza ilishuka katika siku ya Arafa ambapo kutokana na sababu fulani Mtume alikuwa na wasiwasi wa kulitangaza hilo. Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana kukashuka Aya ya al-Tabligh ambapo ndani yake Mwenyezi Mungu alimdhaminia Bwana Mtume kwamba, hakutatokea tatizo. Kisha Aya hiyo ikashushwa tena katika siku ya Ghadir. [14]

Makusudio ya kukamilika dini

Wafasiri wa Kishia na Kisuni wana mitazamo tofauti [15] kuhusiana na sehemu ya Aya hii inayosema:

أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ

nimekukamiliishieni Dini yenu

Kutokana na kuwa mwanzo na mwisho wa Aya hii kumezungumziwa hukumu mbalimbali za kisheria, wafasiri wa Ahlu-Sunna wanasema kuwa, makusudio ya kukamilika dini ni kukamilika hukumu na sheria zote za Kiislamu. [16] Lakini Waislamu wa madhehebu ya Shia wao wanasema kuwa, kwa kuzingatia kwamba, Aya inazungumzia kukata tamaa makafiri, hukumu na sheria za Kiislamu pekee haziwezi kuwa sababu ya kukataa tamaa makafiri na Uislamu; kwani kukata tamaa kikamilifu makafiri hutokea pale Mwenyezi Mungu anapomteua na kumuainisha mtu ambaye ni mrithi na kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume kwa minajili ya kuwa msimamizi wa masuala ya dini na hivyo kuifanya dini iendelee kuweko. Katika natija ni kuwa, Aya ya kukamilika dini inahusiana na tukio la Ghadir Khum (tarehe 18 Dhul-Hija mwaka 10 Hijria) na kutangazwa Wilaya na uongozi wa Ali (as). [17] Kadhalika kwa kutangazwa hukumu za kisheria zilizokuja katika Aya hii, hukumu za Kiislamu hazikukamilika; kwani baada ya Aya hiyo kulishuka Aya zingine zilizokuwa zikibainisha hukumu na sheria za Kiislamu. [18] Waislamu wa madhehebu ya Kishia wakitegemea hadithi za Ahlu-Sunna, wanasema kuwa, makusudia ya kukamilika dini na kutimia neema za Allah ni kutangazwa Wilaya (uongozi) na Ukhalifa wa Imamu Ali kwa Waislamu baada ya Mtume (s.a.w.w). [19]

Tofauti ya Ikmal na It’mam

Shekhe Murtadha Mutahhari, mwanazuoni na mwanafikra mahiri wa Kishia amezungumzia tofauti ya “Ikmal” na It’mam” kwa kusema: “Itmam” inasemwa pale inapokuwa kwamba, kitu kilikuwa na mapungufu hapo kabla; kama jengo ambalo linajulikana kuwa halijakamilika kutokana na kutokamilika mambo yake yote yanayohusiana na ujenzi wake. Lakini katika “Ikmal” yumkini dhahiri yake ikawa sahihi na iliyokamilika, lakini kwa kuwa haina athari tarajiwa, itakuwa haijakamilika. Kwa maana kwamba, yumkini mwili wake ukawa uko sahihi na uliokamilika, lakini kutokana na kuwa hauna roho na zile athari tarajiwa, huelezwa kuwa sio kamili. Katika Aya ya al-Ikmal, amri hii (ya kuteuliwa Imamu Ali kuwa Imamu) kwa kuzingatia kwamba, ni amri katika amri za dini na kipengee miongoni mwa vipengee vyake, hilo linapelekea kukamilika dini. Kwa hivyo hili hili agizo kwa kuzingatia kwamba, kama lisingekuweko, maagizo na maamrisho mengine yote yangekuwa na mapungufu; hii ni kutokana na kuwa, roho ya dini ni Wilaya (uongozi) na Uimamu na kama mtu hana Wilaya (uongozi) na Uimamu, amali zake ni mithili ya mwili ambao hauna roho. [20]

Rejea

Vyanzo