Nenda kwa yaliyomo

Di'bil bin Ali al-Khuza'i

Kutoka wikishia
Kaburi linalohusishwa na Di'bil bin Ali al-Khuza'i katika mji wa Shush

Di'bil bin Ali al-Khuza'i (Kiarabu:دعبل بن علي الخزاعي) (148-245 H) alikuwa mmoja wa washairi na masahaba wa Imamu Kadhim (a.s) na Imamu Ridha (a.s). Anasifika kwa kutunga shairi la Tai’yya. Kwa mara ya kwanza alimsomea Imamu Ridha (a.s) shairi hilo huko Marv ambapo lilipokelewa vyema na Imamu na Mashia. Di’bil amepokea hadithi pia kutoka kwa Maimamu (as) ambapo miongoni mwa tunayoweza kuashiria ni Khutba ya Shaqshaqiya. Katika mashairi yake, Di'bil alikuwa akiwakejeli maadui wa Ahlul-Bayt (a.s). Aliuawa mwaka wa 245 Hijiria kwa kumdhihaki mmoja wa watawala wa Bani Abbas na akazikwa Shush.

Utambulisho na Nafasi

Di'bil bin Ali al-Khuzai alikuwa mmoja wa washairi na wapokezi wa Hadithi wa Ahlul-Bayt (a.s) katika karne ya pili na ya tatu ya Hijria. [1] Shairi la Ta’iyya ambalo ni mashuhuri kuhusiana na dhulma zilizowapata Ahul-Bayt (a.s) lilitungwa na yeye. Kwa mara ya kwanza alimsomea Imamu Ridha (a.s) shairi hilo huko Marv ambapo lilipokelewa vyema na Imamu huyo na Mashia kwa ujumla. [2]

Di’bil alitunga mashairi mengi ya kuwasifu na kuwaomboleza Ahlul-Bayt (a.s.) [3] Aliposikia habari za kuuawa shahidi Imamu Ridha (a.s), alitunga majimui ya beti za mashairi alizozipa jina la Raiya kwa ajili ya kumuomboleza. [4] Kwa mujibu wa baadhi ya watafiti Di’bil alikuwa na nafasi maalumu katika ushairi. [5] «Tabaqata al-Shuaraa» na Diwani la mashairi yake ni miongoni mwa kazi za Di’bil. [6]Kwa mujibu wa Sayyid Mohsin Amin, mwandishi wa kitabu cha A’yan al-Shiah, diwani ya mashairi ya Di’bil ilikuweko mpaka kufikia karne ya 13 Hijria; lakini baada ya hapo, ikatoweka. [7] Baadhi ya waandishi wamefanya juhudi za kukusanya mashairi yake yaliyonukuliwa katika vitabu mbalimbali. [8]

Jina la Di’bil limetambulika kuwa ni Hassan, Abdul-Rahman au Muhammad; lakini aliondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu ya Di’bil. [9] Kuniya yake ni Abu Ali, [10] au Abu Ja’far [11]. Di’bil alizaliwa mwaka wa 148 Hijria. [12] Di’bil alikuwa mwenyeji wa Kufa na alikuwa akifanya safari katika miji mbalimbali. [13] Nasaba ya Di’bil inafika kwa kabila la Khuzai, moja ya makabila ya Yemen. [14] Budayl bin Warqa’ na mwanawe Abdallah bin Budayl ni mababu wawili wa Di’bil ambao walikuwa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.). [15] Abdallah bin Budayl alikuwa pia mmoja wa masahaba wa Imamu Ali (a.s) ambaye akiwa na kabila la Khuzai alipigana katika vita vya Siffin dhidi ya Muawiya bin Abi Sufiyan na kuuawa shahidi. [16] Hata hivyo katika baadhi ya vyanzo vingine, nasaba yake imesajiliwa kivingine. [17]

Kunukuu Hadithi

Sehemu ya maandishi ya Rayeh, yaliyowekwa kwenye kaburi la Imam Reza (a.s.), ambayo yanasomeka:قَبْرَانِ فِي طُوسَ خَيْرُ النَّاسِ كُلِّهِمْ وَ قَبْرُ شَرِّهِمْ هَذَا مِنَ الْعِبَرِ مَا يَنْفَعُ الرِّجْسُ مِنْ قُرْبِ الزَّكِيِّ وَ لَا عَلَى الزَّكِيِّ بِقُرْبِ الرِّجْسِ مِنْ ضَرَر.

Di’bil alikuwa ni mmoja wa masahaba wa Imamu Kadhim (a.s) na Imam Ridha (a.s). [18] Pia alimdiriki Imamu Jawad (a.s). [19] Yeye ni miongoni mwa waliopokea na kunukuu khutba ya Shaqshaqiyya. [20] Aidha amezingatiwa kuwa na cheo kikubwa miongoni mwa masahaba wa Maimamu wa Kishia. (21] Di’bil amenukuu hadithi pia kutoka kwa watu kama Sufiyan Thawri, Malik bin Anas (kiongozi wa madhehebu ya Malik), Said bin Sufiyan na Muhammad bin Ismail. [22] Kadhalika Ali bin Ali bin Zarin (kaka wa Di’bil), Mussa bin Hammad Yazidi, Abasalat Hirawi na Ali bin Hakim ni miongoni mwa watu waliopokea na kunukuu hadithi kutoka kwa Di’bil. [23]

Kifo

Kaburi linalohusishwa na Di'bil bin Ali al-Khuza'i katika mji wa Shush

Di’bil aliuawa mwaka wa 245 Hijria [24] kutokana na kumkejeli mmoja wa watawala wa Bani Abbas. [26] Pia, imeelezwa kwamba Di’bil alikuwa na lugha kali na hakuna khalifa au waziri ambaye alisalimika na dhihaka na kejeli zake na akthari ya watu walikuwa wakiogopa dhihaka zake. [26] Kadhalika inanukuliwa kwamba, Di’bil alikuwa na ghera na mapenzi makubwa na Ahlul-Bayt (a.s) [27] na alikuwa akiwadhihaki tu maadui wa Ahlul-Bayt (a.s.). [28] Kutokana na kejeli na utani aliokuwa akiwafanyia makhalifa daima alikuwa ni mwenye kukimbia na kujificha. [29].

Baadhi ya watafiti wamesema, kuna uwezekano kwamba Di’bil aliuawa kwa sababu ya kumkejeli Mutawakkil Abbasi, kwa sababu baada ya kuharibiwa kwa kaburi la Imamu Hussein (a.s.) kwa amri ya Mutawakkil, Di’bil; alimfanyia kejeli Mutawakkil katika shairi na kumuomboleza Imamu Hussein (a.s). [30] Katika baadhi ya vyanzo imetajwa sehemu na tarehe nyingine ya kuaga kwake dunia. [31] Kwa mujibu wa ripoti ya Abul-Futuh Razi, mwandishi wa tafsiri ya Ruh al-Jinan ni kwamba, katika lahadha za mwisho za umri wake. Di’bil alitunga beti za maishairi katika kukiri kuhusu Tawhidi, Utume na Wilaya ya Imamu Ali (a.s) [32] na mashairi hayo yakaandikwa katika kaburi lake. [33] Di’bil aliusia kwamba, mashairi ya Tai’yya yawekwe kaburini kwake. [34] Kaburi la Di’bil linapatikana Shush. [35]

Rejea

Vyanzo