Hadith Tayr al-Mashwi

Kutoka wikishia

Hadithi ya Tayr al-Mashwi (Kiarabu: حديث الطائر المشوي) (ndege/kuku wa kuchoma) inahusiana na sifa na fadhila za Ali bin Abi Talib (a.s). Kwa mujibu wa maudhui ya riwaya hii, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikusudia kula nyama ya ndege (kuku) aliyechomwa, na akamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t) amshirikishe katika kula) chakula (hicho na yule mtu ambaye ni) kipenzi (chake s.w.t) zaidi kuliko wanadamu wote. Haukupita muda mrefu, Imam Ali (a.s.) akaja (na kuingia) kwa Mtume (s.a.w.w) na akashiriki pamoja naye kula chakula hicho (kwa maana: Wakala pamoja ndege huyo / kuku huyo wa kuchoma). Hadithi hii ni riwaya sahihi na inapatikana katika vyanzo vya Shia na Sunni. Imesemekana kuwa wapokezi tisini waliisimulia Hadithi hii kutoka kwa Anas bin Malik. Baadhi ya wanateolojia wa Shia, kwa kugemea katika riwaya (hadithi) hii, wamemchukulia Imam Ali bin Abi Tali (a.s) kuwa ni mtu anayependwa zaidi na Mwenyezi Mungu(s.w.t), - moja ya dalili zao katika kulithibitisha hilo ni riwaya hii - na wamehitimisha hoja yao wakisema kwamba yeye ndiye aliyestahiki kumrithi (kwa maana: Kuwa Khalifa wa) Bwana Mtume (s.a.w.w).

Andiko la Hadithi

"إنَّ النَّبِی (ص) کانَ عِندَهُ طائِرٌ، فَقالَ: اللَّهُمَ ائتِني بِأَحَبِّ خَلقِک إلَيک؛ يأکلُ مَعي مِن هذَا الطَّيرِ. فَجاءَ أبو بَکرٍ، فَرَدَّهُ، ثُمَّ جاءَ عُمَرُ، فَرَدَّهُ، ثُمَّ جاءَ عَلِي، فَأَذِنَ لَهُ".

“Mtume (s.a.w.w) aliletewa (Ndege) Kuku (wa kuchomwa, akiwa tayari kwa ajili ya kuliwa). Mtume (s.a.w.w) akasema: Ewe Mola wangu! Naomba unitumie (uniletee) kiumbe wako umpendaye zaidi ashiriki katika kula kuku huyu pamoja naye. Baada ya hapo, Abubakar alikuja, lakini Mtume (s.a.w.w) hakumkubali. Kisha Umar akaja, Mtume (s.a.w.w) hakumkubali pia. Kisha Ali (a.s) akaja, Mtume (s.a.w.w) akampa ruhusa (ya kuingia na kula pamoja naye kuku huyo wa kuchomwa) [1]. Hadithi hii imesimuliwa katika vyanzo vya Shia kwa (kuwepo na) utofauti kidogo [2].

Maudhui

Kwa mujibu wa hadithi ya Tayr al-Mashwi, Imam Ali (a.s) ndiye kipenzi zaidi cha watu kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) [3]. Katika riwaya (hadithi) hii, imeelezwa kwamba Mtume (s.a.w.w) alikusudia kula nyama ya ndege (kuku) aliyechomwa, na akamuomba Mwenyezi Mungu(s.w.t) amletee mtu wa kula pamoja naye kuku huyo ambaye ndiye kipenzi chake (s.w.t) zaidi kuliko wanadamu wote, na akaja Imam Ali (a.s) na Mtume (s.a.w.w) akala pamoja naye [4].

Kabla ya Imam Ali (a.s), walikuja Abubakar na Umar kwa Mtume (s.a.w.w), lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) aliwarudisha [5]. Katika baadhi ya nukuu za hadithi hii, imeelezwa kwamba baada ya Dua ya Mtume (s.a.w.w), Aisha na Hafsa kila mmoja kwa upande wake aliomba dua kwamba Baba yake ndio aje (atokeze ili kuja) kula pamoja na Mtume [6]. Anas bin Malik, pia amenukuliwa akisema: “Nilitaka (nilitamani sana) mtu huyu (wa kujitokeza ili aje kula pamoja na Mtume -s.a.w.w-) awe ni Sa'd bin Ubadah. Kwa hiyo, Hadhrat Ali (a.s.) alipokuja kwenye mlango wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w), nilimkatalia (kuingia ndani, akarudi), lakini haikuchukua muda mrefu Hadhrat Ali (a.s) akaja tena na kula chakula kile pamoja na Mtume (s.a.w.w) [7]”. Umaalumu wa kuku huyu wa kuchomwa na kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya riwaya, ni huu kwamba: Baada ya dua ile ya Mtume (s.a.w.w), Malaika Jibrail (a.s) aliteremka kutoka mbinguni na kuja kwa Mtume (s.a.w.w) akiwa na ndege (kuku) yule.

- وسألتُ الله القریب المجیب، فهبط علي حبیبی جبرئیل و معه هذا الطیر

Na (umaalumu mwingine wa kuku yule, unadhihirika pale kwenye) Dua ya Mtume (s.a.w.w) na msisitizo wake kwamba ni Imam Ali (a.s) tu atakaye kula pamoja naye

- فرفعت یدى الى السماء فقلت : اللهم یَسّر عبداً یُحبّک و یُحبنى یاکل معى هذا الطائر[8]

Basi nikainua mikono yangu mbinguni na kuomba kwa kusema: Ee Mwenyezi Mungu!, mfanyie wepesi mja anayekupenda Wewe na kunipenda mimi aje kula pamoja nami ndege (kuku) huyu. Hii inaonyesha nafasi maalum aliyokuwa nayo Imam Ali (a.s) kwa Mtume (s.a.w.w).

Itibari

Wanachuoni wa Kishia wameichukulia Hadithi ya Tayr al-Mashwi kuwa ni Mutawatir (kwa maana: Ni hadithi yenye kutegemewa na iliyopokelewa na wapokezi wengi). [9]. Kundi la Wanazuoni wa Hadithi wa Kisunni pia wamethibitisha usahihi na kutegemewa kwake [10] . Hadithi ya ndege (kuku) ya kuchoma, imesimuliwa na kunukuliwa na Masahaba kadhaa nukuu zao zikiwa na madhumuni zinazofanana au kukaribiana; ikiwa ni pamoja na Safina, mtumishi wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) [11]. al-Sadi al-Kabir ananukuu na kusimulia (hadithi hii) kutoka kwa Anas bin Malik [12], Yahya bin Kathir kutoka kwa Anas bin Malik [13], Uthman bin Tawil kutoka kwa Anas bin Malik [14], Abdullah bin Anas bin Malik kutoka kwa baba yake [15], na Ali bin Abdullah bin Abbas kutoka kwa baba yake [16].

Kulingana na Ibn Kathir al-Dimashqiy na ambaye ni mwanachuoni wa Kisunni, watu tisini waliisimulia hadithi hii kupitia njia ya Anas bin Malik pekee [17]. Hata hivyo, Ibn Kathir anasema: “Moyo wangu hauikubali hadithi hii, ingawa wapokezi wake ni wengi mno”[18]. Allamah Amini, katika kumjibu Ibn Kathir anasema: “Moyo wake umepigwa muhuri na Mwenyezi Mungu (s.w.t), na akasema: Kukanusha Hadithi ya Tayr licha ya ushahidi wote uliotajwa (kuhusiana na hadithi hiyo), hakuna maana yoyote” [19].

Kwa mujibu wa riwaya ya Ibn Shahr Ashub, Sayyid Ismail Himyari, mshairi wa karne ya pili ya mwandamo wa Hijiria (aliyefariki Mwaka 179 Hijiria), ameandaa shairi kuhusiana na tukio la hadithi ya ndege (kuku wa kuchoma), shairi hilo linaanza namna hii:

نُبِّئتُ اَنَّ اَبانا كان عن اَنَس يَروی حديثاً عجيباً مُعجِباً عَجَباً

فی طائرٍ جاء مَشويّاً بِه بَشَرٌ يوماً و كان رسولُ الله مُحتَجِباً

ادناه منه فلما ان رآه دعا ربا قریبا لاهل الخیر منتجبا

ادخل الی احبّ الخلق کلهم طرا الیک فاعطاه الذی طلبا


Maana ya shairi hili

Habari zilinifikia (niliambiwa) kwamba baba yetu alikuwa anasimua Hadithi ya ajabu na yenye kushangaza mno kutoka kwa Anas, kuhusu kuku wa kuchoma ambaye siku moja aliletwa na mtu (mbele ya Mtume - s.a.w.w-, na Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa nyumbani kwake mbali na macho ya watu, kuku huyo akapelekwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, na macho yake (s.a.w.w) yalipotua juu yake (alipomuona kuku yule), aliinua mikono yake na kumuomba Mola wake kuhusiana na mtu wa karibu yake zaidi na mwema zaidi kuliko watu watu, kwa kusema: Niletee mtu anayependwa zaidi mbele yako. Mwenyezi Mungu akampa kile alichokiomba.

Matumizi ya Teolojia

Hadithi ya Tayr al-Mashwi imechukuliwa kuwa ni miongoni mwa fadhila za Imam Ali (a.s). [20] Wanateolojia wa Kishia wametumia hadithi hii kuthibitisha kipaumbele cha Imam Ali (a.s) kwa Uimamu na Ukhalifa [21]. Sheikh Mufid, akitegemea (hadithi) riwaya ya Tayr katika kuashiria kwamba Imam Ali (a.s) ndiye kiumbe anayependwa zaidi na Mwenyezi Mungu (s.w.t), anaona kuwa lazimu ya hilo ni Imam Ali (a.s) kuwa bora zaidi; kwa sababu kwa mujibu wa imani (na itikadi yake), chanzo cha mapenzi ya Mwenyezi Mungu (kwake) kiko katika msingi wa haki, na wala si kwa sababu ya upendeleo. Kwa hiyo, Ali (a.s) kuwa kwake kipenzi zaidi kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t), na kiumbe bora wa kwa Mwenyezi Mungu, hilo linathibitisha kwamba yeye ndiye Imam (na Khalifa); kwa sababu hairuhusiwi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kumtanguliza aliye bora mbele ya yule aliyekuwa bora zaidi katika masiala ya utume na ukhalifa wa umma [22]. Sayyid Murtadha katika Al-Fusul Al-Mukhtara, akinukuu maneno ya Sheikh Mufid, amesisitiza kuwa kiumbe anayependwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu(s.w.t), ana thawabu nyingi zaidi kuliko watu wote, na mtu wa aina hiyo hakuna shaka kwamba, ana ubora zaidi katika matendo na ibada kuliko viumbe vingine vyote. Huu ni ushahidi na dalili ya fadhila za Imam Ali (a.s) juu ya watu wote isipokuwa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) [23].

Kazi (athari) zinazohusiana na hili

Kwa mujibu wa Ibn Kathir al-Dimashqi, Mwanachuoni wa Kisunni, vimeandikwa vitabu vingi vyenye kukusanya lafudhi mbalimbali za Hadithi ya Tayr: Abubakar bin Mardowaih, Muhammad bin Ahmed bin Hamdan na Muhammad bin Jarir Tabari wana athari (na kazi kubwa) juu ya jambo hili. Mwanateolojia wa Kisunni Abu Bakar Baghilani pia aliandika kitabu dhidi ya jambo hilo [24]. Pia, Mirhamid Hussein ameiweka wakfu juzuu ya 13 (kitabu cha nne cha njia ya pili) ya Abaqat al-Anwar kwa hadithi hii (yaani: Juzuu hiyo ya 13 ameifanya kuwa ni mahsusi kwa ajili ya hadithi hii), na ametaja ushahidi wake kupitia wapokezi wa Kisunni kwa kutaja majina ya wapokezi na kukosoa kila hadithi kwa undani zaidi [25]. Sehemu hii ya kitabu chake, chenye kurasa 736 na ambacho kwa ujumla ni juzuu mbili, kilichapishwa katika mji wa Lucknow India), mwaka 1306 AH [26].

Rejea

Vyanzo