Aya ya Khair al-Bariyya

Kutoka wikishia
Aya ya Khair al-Bariyya

Aya ya Khair al-Bariyya (Kiarabu: آية خير البرية) ni Aya ya 7 ya Surat al-Bayyinah, ambayo ni miongoni mwa Aya ambazo zimeshuka kuhusiana na Imamu Ali bin Abi Talib (a.s). Kwa mujibu wa hadithi ambazo zimenukuliwa katika vyanzo vya Kishia na Kisunni kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ni kwamba, makusudio ya Khair al-Bariyyah yenye maana ya viumbe bora ni Imamu Ali (a.s) na wafuasi wake.

Baadhi ya wafasiri kupitia Aya hii wamefikia natija hii kwamba, waja wema na waumini wana ubora hata kwa Malaika; kwani neno Bariyya linajumuisha viumbe vyote.

Andiko na Tarjumi

Aya ya 7 katika Surat al-Bayyinah ni mashuhuri kwa jina la Aya ya Khair al-Bariyya. [1]


إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُوْلَئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ

Hakika walio amini na wakatenda mema, hao ndio viumbe bora..
(Quran: 98: 7)

Nafasi na Umuhimu

Aya ya Khair al-Bariyya inahesabiwa kuwa miongoni mwa Aya zinazoonyesha fadhila na ubora wa Imamu Ali ibn Abi Twalib (a.s). [2] Imenukuliwa kutoka kwa Ibn Abbas ya kwaba, Aya hii ilishuka kuhusiana na Imamu Ali (a.s). [3] Kwa mujibu wa wanazuoni wa Kishia ni kuwa, Imamu Ali (a.s) alitumia Aya hii na sababu ya kushuka kwake ili kuthibitisha haki yake katika Baraza la watu Sita (baraza hili liliteuliwa na Omar bin al-Khattab kabla ya kifo chake kwa ajili ya kuainisha na kuchagua khalifa atakayeongoza Waislamu baada yake). [4]

Ayatullah Nasser Makarim Shirazi (alizaliwa: 1305 Hijria Shamsia), mmoja wa wafasiri wa Kishia akitumia kama hoja hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) zinazozungumzia sababu ya kushuka Aya hii na ndani yake wametajwa Ali (a.s) na wafiasi wake [5] anasema kuwa: Neno Shia lilikuweko tangu zama za Bwana Mtume (s.a.w.w) na makusudio ya Shia katika hadithi hizi ni wafuasi maalumu wa Imamu Ali (a.s). [6]

Makusudio ya Khair al-Bariyya

Katika vitabu vya hadithi vya Waislamu wa Kishia na Kisunni, kuna hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (saww) ambazo ndani yake "Khair al-Bariyya" (viumbe bora) imefasiriwa kuwa ni Imamu Ali (a.s) na Mashia. [7] Hakim Khaskani (aliaga dunia: 490 AH) mmoja wa Maulamaa wa Kisuni amenukuu katika kitabu chake cha Shawahid al-Tanzil zaidi ya hadithi 20 kuhusiana na maudhui hii kwa mapokezi tofauti. [8] Miongoni mwa hadithi hizo ni iile iliyopokewa na Ibn Abbas ambapo anasema, wakati Aya hii iliposhuka, Mtume (s.a.w.w) alimhutubu Imamu Ali (a.s) kwa kumwambia: Khair al-Bariyya "Huyo ni kiumbe bora" na ni wewe na Mashia wako (wafuasi wako). Siku ya Kiyama Wewe na Mashia wako, mtakuja hali ya mmemridhia Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu atakuwa radhi nanyi (atafurahi na nyinyi). [9]

Nukta za kitafsiri

Moja ya nukta za kitakfsiri ambayo imeelezwa na wafasiri kutoka katika Aya hii ni kuwa, waja wema na waumini wana ubora kwa Malaika; kwani neno "Bariyya" linajumuisha viumbe vyote. [10]

Kushuka Aya katika mji wa Makka

Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, Aya ya Khair al-Bariyya ilishuka katika hali ambayo, Mtume (s.a.w.w) alikuwa Makka katika Masjid al-Haram (katika msikiti wa Makka). [11] Kwa mujibu wa Tafsir Nemooneh (Tafsir al-Amthal) jambo hili halikinzani na Aya hii kuwa ni Madani (iliyoshuka Madina); kwani yumkini Sura ikawa ni Madani (iliyoshuka Madina) na Aya hii ikawa imeshuka katika safari za Mtume kutoka Madina kwenda Makka. [12]

Vyanzo

  • Ḥākim al-Ḥaskānī, ʿUbayd Allāh b. ʿAbd Allāh al-. Shawāhid al-tanzīl li-qawāʿid al-tafḍīl. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1393 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūnah. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1374 Sh.
  • Suyūṭī, ʿAbd al-Raḥmān b. Abī Bakr al-. Al-Durr al-manthūr fī tafsīr al-maʾthūr. Qom: Maktabaṭ Āyat Allāh al-Marʿashī, 1404 AH.
  • Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Intishārāt-i Islāmī (Jāmiʿat al-Mudarrisīn), 1417 AH.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Tehran: Naṣir Khusraw, 1372 Sh.