Nenda kwa yaliyomo

Laylat al-Mabit

Kutoka wikishia
Makala hii inazungumzia tukio la Laylat al-Mabit. Ili kujua kuhusiana na Aya yenye jina kama hili, basi unashauriwa kuangalia makala ya Aya ya Laylat al-Mabit.

Laylat al-Mabit (Kiarabu: ليلة المبيت) ni usiku ambao Imamu Ali (a.s) alilala katika kitanda cha Mtume (s.a.w.w) ili kuokoa maisha ya mbora huyo wa viumbe. Katika usiku huu washirikina wakiwa kikundi walikusudia kuivamia nyumba ya Mtume (s.a.w.w) ili wamuue. Kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kwa takwa la Mtume (s.a.w.w), Imamu Ali alilala sehemu ya Mtume na matokeo yake washirikina walipovamia nyumba ya Mtume hawakumpata mjumbe huyo wa Allah na badala yake walikuta Imamu Ali (a.s) ndiye aliyelala sehemu ya Mtume (s.a.w.w). Kwa hila hiyo, Mtume akawa ameondoka usiku huo na kuhajiri kuelekea Madina. Akthari ya wafasiri wa Qur’an tukufu wanasema kuwa, sababu ya kushuka Aya ya Shiraa au Aya ya Laylat al-Mabit ni kujitolea huku kwa Imamu Ali (a.s) katika Laylat al-Mabit. Vitabu vya historia vinaeleza kuwa, tukio hili lilitokea katika usiku wa kwanza wa mwezi Mfunguo Sita (Rabiul-Awwal).

Nafasi na umuhimu

Laylat al-Mabit inaelezwa kuwa ni tukio ambalo Imam Ali (a.s) alilala kwenye kitanda cha Mtume ili kuokoa maisha ya Mtume. Tukio hili linachukuliwa kuwa ni miongoni mwa fadhila za Imamu Ali (a.s), na Imam Ali (a.s.) alilitumia hili kama hoja katika baraza la watu sita (lililoteuliwa kumchagua khalifa na kiongozi baada ya Omar) ili kuthibitisha haki yake. [1] Wafasiri wa Qur’an wanalitambulia tukio hili kuwa sababu ya kushuka Aya ya Shiraa au Aya ya Laylat al-Mabit kuhusiana na Imam Ali (a.s). [2]

Kwa mujibu wa riwaya ya Sayyid Ibn Tawus, Mtume (s.a.w.w) alilitaja tukio hili katika khutba ya Ghadir na akalitambua kuwa ni jukumu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Imam Ali (a.s). [3] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi mbalimbali, wakati Imamu Ali (a.s) alipokuwa amelala katika sehemu ya Mtume (s.a.w.w), Jibril akaja juu ya kichwa chake na Mikail akaja chini ya miguu yake. Jibril akasema: "Wamebarikiwa walio kama wewe, ewe mwana wa Abu Talib, kwamba Mwenyezi Mungu atajifakhirisha kwako mbele ya Malaika".[4]

Kujitolea Imamu Ali ni zaidi ya kusalimu amri Ismail

Sayyid Ibn Tawus amelinganisha kulala Imam Ali juu ya kitanda cha Mtume (s.a.w.w) na kujisalimisha kwa Ismail, mtoto wa Nabii Ibrahim, katika tukio la amri ya kuchinjwa. Kwa maoni yake ni kuwa kujitoa mhanga Imam Ali ni bora kuliko utii wa Ismail; kwa sababu Ismail alikuwa tayari kuchinjwa na baba yake; lakini Imam Ali (a.s) alikuwa amejitayarisha kuuawa na maadui zake. [5]

Njama ya kumuua Mtume (s.a.w.w)

Kwa mujibu wa vyanzo vya historia ni kwamba, washirikina wa Makka walikusanyika katika Dar al-Nadwa kwa ajili ya kuchukua uamuzi kuhusiana na namna ya kukabiliana na Mtume (s.a.w.w) ambapo kila mmoja alitoa pendekezo lake. Abu Jahl alitoa pendekezo lake kwa kusema: Tumuue Mtume, lakini mauaji yake yanapaswa kuyashirikisha makabila yote, ili Bani Hashim wasiweze kupigana vita na makabila yote kwa ajili ya kulipiza kisasi na hivyo kulazimika kukubali dia. [6]

Hatimaye pendekezo lake hilo lilikubaliwa na kwa msingi huo wakakubaliana kutekeleza mpango wao usiku na kila kabila litoe mtu mmoja. Kufuatia uamuzi huo, Jibril alimshukia Mtume (s.a.w.w) na kumjulisha mipango ya washirikina. [7] Kwa hiyo, Mtume (s.a.w.w) aliamua kuondoka nyumbani kwake kwenda Madina kabla ya washirikina kufika. [8]

Kulala Imamu Ali (a.s) katika kitanda cha Mtume (s.a.w.w)

Kwa mujibu wa riwaya ya Majlisi, Mtume alimwambia Ali (a.s): "Washirikina wanataka kuniua usiku huu, je, utalala kitandani mwangu?" Imam Ali (a.s) akasema: “Je, katika hali hii, utasalimika? Mtume (s.a.w.w) akasema: Ndio. Imam Ali (a.s) alitabasamu, akasujudu sijida ya kushukuru, na aliponyanyua kichwa chake kutoka kwenye sijda, alisema: "Fanya kile ulichotakiwa ambapo macho, masikio na moyo wangu viwe fidia kwako". [9] Mtume (s.a.w.w), akamkumbatia Ali na wote wawili wakalia na kisha wakatengana. [10]

Washirikina walikuwa wameizunguka nyumba ya Mtume (s.a.w.w) tangu mwanzo wa usiku. Walitakiwa kushambulia usiku wa manane; lakini Abu Lahab alisema kwamba wakati huu, wanawake na watoto wamo ndani ya nyumba hiyo, na baadaye Waarabu watasema kuhusu sisi kwamba hatukulinda heshima ya watoto wa ami yao. [11] Walimpiga Ali (a.s) kwa jiwe ambaye alikuwa amelala kitandani ili kuhakikisha kwamba kuna mtu amelala na hawakuwa na shaka kuwa aliyelala pale ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. [12] Ilipofika asubuhi walivamia nyumba ya Mtume na walipomuona Ali (a.s) kwenye kitanda cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), wakasema, "Yuko wapi Muhammad (s.a.w.w)?" Ali (a.s) akajibu: “kwani mlimkabidhi kwangu hata mnamtaka kutoka kwangu?! Alifanya jambo ambalo liliwafanya walazimike kuondoka hapo." Wakati huu, walimshambulia Ali (a.s) na kumsumbua, na kisha wakamtoa nje ya nyumba na kumpiga. Walimfunga ndani ya Masjid al-Haram kwa muda wa saa kadhaa kisha wakamwachilia huru. [13]

Katika riwaya nyingine, imeelezwa kwamba Ali (a.s) alipowaona wakichomoa panga zao na wakimjia, aliuchukua upanga wa Khalid bin Walid, ambaye alikuwa mbele ya kila mtu, kwa hila na akawafukuza kutoka kwake. Walisema hatuna kazi yoyote na wewe; Lakini tuambie, yuko wapi Muhammad (s.a.w.w)? Ali akajibu, sijui habari zake. Kisha Maquraishi wakaanza kumtafuta Mtume (s.a.w.w). [14]

Sheikh Tusi katika Misbah al-Muttahajid aliripoti kwamba, wakati wa kutokea tukio hili ulikuwa katika usiku wa kwanza wa Rabi'ul Awwal katika mwaka wa kwanza wa hijra ya Mtume (s.a.w.w). [15]

Kushuka Aya ya Shiraa kumhusu Imamu Ali (a.s)

Makala asili: Aya ya Laylat al-Mabit

Maulamaa wa Kishia [16] na kundi miongoni mwa Maulamaa wa Kisunni [17] wanaamini kwamba, Aya ya Laylat al-Mabit au Aya ya Shiraa (Aya ya 207 katika Surat al-Baqarah) ilishuka kuhusiana na tukio la kujitokea muhanga Imamu Ali katika Laylat al-Mabit ambapo alilala katika kitanda cha Mtume (s.a.w.w) na kuokoa maisha ya mbora huyo wa viumbe.

Kwa mujibu wa kauli ya Ibnu Abi Al-Hadid, mwanachuoni wa madhehebu ya Ahlul-Sunna katika maelezo yake ya tafsiri ya Nahju Al-Balagha, ananukuu kutoka kwa mwalimu wake Abu Jafar ya kwamba, imethibiti kwa sura ya tawatur (mapokezi mengi) ya kwamba Aya hii iliteremshwa kuhusiana na Imam Ali (a.s) katika tukio la Laylatul-Mabit na kila mwenye kukana hili ima atakuwa mwendawazimu au hana uhusiano wowote na Waislamu. [18]

Katika Aya ya Shiraa Mwenyezi Mungu anawasifu watu ambao wako tayari kujitolea muhanga roho na maisha yao kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu. [19]

Kazi za sanaa

Mashairi

Kumetungwa mashairi mengi kuhusiana na tukio la Laylat al-Mabit. Hassan bin Ali Habal ambaye ni mashuhuri kwa lakabu ya Amir al-Shuaraa Yemen (Kiongozi wa Washairi wa Yemen) mwaka 1076 alitoa mjumuiko wa mashairi yanayozungumzia tukio hili. [21]

Filamu ya matukio ya kweli ya Laylat al-Mabit

Hii ni filamu ya matukio ya kweli (documentary) inayotoa wasifu wa Imamu Ali (a.s) pamoja na kujitolea kwake muhanga katika usiku wa tukio la Laylatul-Mabit. Filamu hii imewahi kuonyeshwa katika Televisheni ya Iran. [22]

Rejea

Vyanzo

  • ʿAyyāshī, Muḥammad b. Masʿūd al-. Tafsīr al-ʿAyyāshī. Edited by Sayyid Hāshim Rasūlī. Tehran: Maktabat al-ʿIlmīyya al-Islāmīyya, 1363 Sh.
  • Ḥākim al-Niyshābūrī, Muḥammad b. ʿAbd Allāh al-. Al-Mustadrak ʿalā l-ṣaḥīḥayn. Edited by Muṣṭafā ʿAbd al-Qādir ʿAṭā. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, [n.d].
  • Ḥalabī, ʿAlī b. Ibrāhīm al-. Al-Sīra al-Ḥalabīyya. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].
  • Ibn Hishām, ʿAbd al-Malik. Al-Sīra al-nabawīyya. Edited by Muḥammad Muḥyī l-Dīn ʿAbd al-Ḥamīd. Cairo: Maktabat Muḥammad ʿAlī Ṣabīḥ, [n.d].
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Dār al-Wafāʾ, 1403 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Amālī. Qom: Muʾassisat al-Biʿtha, 1417 AH.
  • Subḥānī, Jaʿfar. Furūgh-i abadīyyat. Qom: Būstān-i Kitāb, 1386 Sh.
  • Ṭabāṭabāyī, Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Third edition. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1973 AH.
  • Tabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Iʿlām al-warā bi aʿlām al-hudā. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt li-Iḥyāʾ al-Turāth, 1417 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Amālī. Qom: Dār al-Thirqāfa, 1414 AH.