Kuvunjwa masanamu

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na mkasa wa kuvunjwa masanamu. Ili kuangalia kitabu chenye jina hili hili angalia makala ya Kasr Asnam al-Jahiliya (kitabu).

Kuvunjwa masanamu (Kiarabu: واقعة كسر الأصنام) kunaashiria tukio kuvunjwa masanamu katika paa la Kaaba kitendo ambacho kilifanywa na Imamu Ali bin Abi Talib (a.s). Katika tukio hili, Imam Ali (a.s) alikanyaga juu ya mabega ya Mtume (s.a.w.w) na akaenda hadi juu ya Al-Kaaba na kuyatupa chini masanamu kama vile Hubal. Tukio hili limesimuliwa katika vyanzo vya Shia na Sunni. Tukio hili lilitokea siku ya Laylat al-Mabit (usiku ambao Mtume aliondoka Makka, na kisha Ali (a.s) akalala kwenye kitanda chake ili kuwahadaa maadui zake) au lilitokea wakati wa Fat'h Makka (kukombolewa Makka).

Tukio la kuvunjwa masanamu limetajwa kuwa sababu ya kushuka Aya isemayo:«وَ قُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَ زَهَقَ الْبَاطِلُ...»Na sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka.Au Aya isemayo:«وَ رَفَعْناهُ مَكاناً عَلِيًّا»Na tulimuinua daraja ya juu. Baada ya tukio hili, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimtambulisha Nabii Ibrahim (a.s) kama mvunja masanamu wa kwanza na Imam Ali (a.s) kama mvunja masanamu wa mwisho. Katika baadhi ya riwaya, Ali (a.s) ametajwa kama Kassir al-Asnam (mvunjaji masanamu).

Tukio la kuvunjwa masanamu linachukuliwa kuwa ni miongoni mwa fadhila za Imam Ali (a.s). Imam Ali (a.s) aliitaja fadhila hii kwenye baraza la watu sita ambalo liliundwa kumteua khalifa baada ya Omar bin al-Khattab. Katika baadhi ya vyanzo vya Sunni, tukio hili limetajwa kuwa ni uthibitisho wa ulazima wa kuharibu na kubomoa suhula na nyeno za kutenda dhambi.

Ufafanuzi wa Tukio

Tukio la Kasr al-Isnam au Hadith ya Kasr al-Isnam [1] (kuvunja masanamu) inahusu kisa cha Imam Ali (a.s) kubebwa mabegani na Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) ili aweze kuvunja masanamu juu ya paa la Kaaba. [2] Katika tukio hili, kumebainishwa kuhusu kuvunjwa baadhi ya masanamu muhimu (kwa washirikina) kama vile Sanamu la Hubal. [3] Bila shaka, kuna tofauti kuhusu maelezo ya tukio hili kwa undani. Kwa kuzingatia baadhi ya riwaya, kwanza Ali (a.s) aliomba kumweka Mtume (s.a.w.w) mabegani mwake; lakini hakuweza. Kwa hiyo, Ali (a.s) alipanda juu ya mabega ya Mtume (s.a.w.w) [4] na kuyatupa masanamu hayo kutoka juu ya Al-Kaaba hadi chini. Katika riwaya nyingine, imetajwa kuhusu pendekezo la mwanzo la Imam Ali (a.s) kwa Mtume (s.a.w.w) kupanda juu ya mabega yake, ambalo Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimkumbusha Ali (a.s) kwamba hakuna mtu anayeweza kufanya jambo kama hilo. [5] Kwa mujibu wa Jabir bin Abdullah, suala hili lilitokana na uzito wa mzigo wa Utume. [6] Kuna sababu zingine zimetajwa kuhusiana na jambo hili. [7] Kwa mujibu wa nukuu nyingine, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alimuamuru Ali (a.s) tangu mwanzo kupanda juu ya mabega yake [8].

Kuna riwaya tofauti kuhusu jinsi Imam Ali (a.s) alivyoshuka kutoka kwenye paa la Al-Kaaba. Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, Imam Ali (a.s) alijirusha kutoka kwenye paa la Al-Kaaba, ambalo ukuta wake ulikuwa dhiraa arobaini [9] wakati huo, lakini hakudhurika. [10] Kwa mujibu wa hadithi Mtume (s.a.w.w) amesema: Jibril alikuteremsha kutoka juu ya Al-Kaaba. [11] Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Omar bin al-Khattab, baada ya Imam Ali (a.s) kuyatupa masanamu hayo, Mtume (s.a.w.w) alimwambia ashuke na Ali alishuka kama ndege ambaye alikuwa ana mbawa mbili, na Umar alikuwa akitamani kupata nafasi kama hii na alikuwa akisema kwamba Mungu ambaye Ali alikuwa anamuabudu hakumuacha Ali aanguke chini. [12]

Kwa mujibu wa hadithi mbalimbali, kuhusiana na tukio hilo, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akisoma Aya hi:[14] [13] «وَ قُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَ زَهَقَ الْبَاطِلُ إِنَّ الْبَاطِلَ کاَنَ زَهُوقًا ; Na sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka. Hakika uwongo lazima utoweke!» Ni kwa msingio huo ndio maana tukio la kuvunjwa masanamu limetambuliwa kuwa sababu ya kushuka Aya hii. [15] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa na Ibn Shahrashub ni kwamba, Aya ya: [16] «وَ رَفَعْناهُ مَكاناً عَلِيًّا ; Na tulimuinua daraja ya juu».Ilishukka kuhusiana na tukio hilo. [17]

Tukio la kuvunjwa masanamu limenukuliwa katika vitabu vya Shia [18] na Sunni [19]. Abdullah bin Abbas, [20] Jabir bin Abdullah Ansari [21] na Abu Mariam [22] wamesimulia tukio hili. Allama Amini amekusanya orodha ya wanazuoni wa Kisunni ambao wameripoti tukio hili katika kitabu chake cha al-Ghadir. [23]

Fadhila Zake

Mchoro wa Kasr Asnam, ambao ulifanywa katika karne ya 11 kwa amri ya Sultan Murad III, mtawala wa Ottoman, umechorwa na Sayyid Suleiman Kasim Pasha.

Kubebwa Ali (a.s) mabegani na Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) kumetambuliwa kuwa ni miongoni mwa fadhila za kipekee za Ali (a.s). [24] Tukkio hili limetajwa pia katika vitabu vya kuandika fadhila [25] na katika beti za mashairi za washairi. [26] Baada ya tukio hili, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimtambulisha Nabii Ibrahim (a.s) kama mvunja masanamu wa kwanza na Imam Ali (a.s) kama mvunja masanamu wa mwisho. [27] Katika baadhi ya hadithi Ali (a.s) ametajwa kama "Kasir al-Asnam" (mvunja masanamu). [28] Pia, Ibn Jawzi, mwanachuoni wa Kisunni (aliyefariki mwaka 654 Hijiria) katika kitabu chake Tadhkirat Al-Khawas, alipokuwa akinukuu maneno mbalimbali kuhusu kumtaja Imam Ali (a.s), alinukuu kauli ambayo kwa mujibu wake jina ambalo mama yake Imam Ali (a.s) alimpa ni Haidar, kutokana na kuwa, atapanda katika mabega ya Mtume (s.a.w.w) ili kuyavunja masanamu, na hivyo aliitwa Ali (daraja ya juu). Hata hivyo, Ibn Jawzi ana maoni kwamba mama yake alimpa jina Ali (a.s) wakati wa kuzaliwa.[29]

Kutumia tukio la kuvunja masanamu kama hoja katika baraza la watu sita

Imam Ali (a.s) alijifaharisha na kisa cha kuvunja masanamu [30] na alikuwa akisema: Mimi ndiye niliyekanyaga kwa mguu muhuri wa Utume (alama iliyochongwa baina ya mabega mawili ya Mtume na inaashiria Utume. [31] Katika baraza la watu sita, ambalo lilifanyika kumteua khalifa baada ya Omar bin al-Khattab, alichukua kauli ya kukiri kutoka kwa wale waliokuwepo kwamba hakuna mtu mwingine aliyekuwa na fadhila hiyo isipokuwa yeye tu. [32] Pia inasemekana kwamba Omar bin al-Khattab alitamani sana lau angepata yeye fadhila hiyo. [33]

Wakati wa Kutokea Kwake

Katika vyanzo vingi hakujatajwa zama na kipindi lilipotokea tukio la kuvunjwa masanamu bali vyanzo hivyo vimetosheka tu na kutaja kwamba, tukio hilo lilitokea usiku [34] na kwa siri. [35] Pamoja na hayo baadhi ya vyanzo vinasema kuwa, tukio hilo lilitokea siku ya Laylat al-Mabit (36] (usiku ambao Mtume aliondoka Makka na Ali (a.s) akalala kwenye kitanda chake ili kuwahadaa maadui zake) au lilitokea wakati wa Fat'h Makka (kukombolewa Makka). [37] Allama Majlisi amenukuu katika kitabu chake cha Bihar al-Anwar hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) ambayo inaeleza kuwa tukio hili lilitokea katika siku ya Nairuzi. [38]

Katika kitabu cha Ensaiklopidia ya Amirul-Muuminina baada ya kuchambuliwa na kuchunguzwa hadithi mbalimbali, imetambuliwa kwamba, uwezekano wa kwamba, tukio hili lilitokea katika siku ya Laylatul-Mabit ni mkubwa zaidi. [39] Kadhalika Allama Majlisi amezungumzia uwezekano huu kwamba, kuvunjwa masanamu kulifanytika mara nyingi. [40]

Natija

Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, kuvunjwa kwa masanamu kwa mikono ya Imamu Ali (a.s) kuliwafanya washirikina baada ya hapo wasiyaweke masanamu katika nyumba ya Mwenyezi Mungu. [41] Katika baadhi ya vyanzo vya Sunni, tukio hili linazingatiwa kuwa ni uthibitisho wa ulazima wa kuangamiza nyenzo na suhula za kutendea dhambi [42].

Katika Mashairi

Tukio la Imamu Ali (a.s) kuvunja masanamu limeakisiwa mno katika mashairi ya Kiarabu na Kifarsi ya washairi wa Kishia na Kisunni.