Aya ya Mubahala
- Makala hii inahusiana na Aya ya Mubahala (maapizano). Kama unataka kujua kuhusiana na tukio la Mubahala, angalia makala ya Mubahala (maapizano) kati ya ya Mtume (s.a.w.w) na Wakristo wa Najran.
Jina la Aya | Aya ya Maapizano |
---|---|
Sura Husika | Surat al-Imran |
Namba ya Aya | 61 |
Juzuu | 3 |
Sababu ya Kushuka | Mjadala kati ya Wakristo wa Najran na Mtume (s.a.w.w) |
Mahali pa Kushuka | Madina |
Maudhui | Itikadi |
Mada Yake | Mubahala Baina ya Mtume na Wakristo wa Najrani |
Mengineyo | Fadhila za As'hab al-Kisaa |
Aya ya Mubahala (Kiarabu: آية المباهلة) (Surat al-Imran Aya ya 61) inaashiria tukio la maapizano baina ya Mtume (s.a.w.w) na Wakristo wa Najran ambalo lilitokea baada ya kuibuka hitilafu kuhusiana na kadhia ya Nabii Issa Masih (a.s). Wafasiri wa Kishia na akthari ya Ahlu-Sunna wanasema kuwa, Aya hii ni ishara ya kuwa haki mwito na ulingaliaji wa Mtume (s.a.w.w) na inaonyesha fadhila za Ahlul-Bait (a.s). Kadhalika wanasema kuwa, makusudio ya “watoto wetu” katika Aya ya Mubahala ni Hassan na Hussein(a.s), makusudio ya “wake zetu” ni Fatma (a.s) na madhumuni ya “nafsi zetu au sisi wenyewe” katika Aya hiyo ni Imamu Ali (a.s).
Maimamu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia na baadhi ya masahaba wa Mtume wakiwa na lengo la kuthibitisha fadhila za Imam Ali (a.s) waliitumia Aya hii. Kadhalika Aya hii inatumiwa kuhalalisha ushiriki wa wanawake katika harakati za kisiasa na kijamii.
Andiko la Aya na Tarjuma yake
فَمَنْ حَاجَّكَ فِيهِ مِن بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ أَبْنَاءَنَا وَأَبْنَاءَكُمْ وَنِسَاءنَا وَنِسَاءكُمْ وَأَنفُسَنَا وأَنفُسَكُمْ ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَل لَّعْنَةَ اللَّهِ عَلَى الْكَاذِبِينَ
Watakao kuhoji katika haya baada ya kukufikilia ilimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na wake zenu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.
(Qur'ani: 3: 61)
Nafasi
Aya ya Mubahala ni katika Aya zinazotumiwa kuonyesha fadhila za Ahlul-Kisaa (Watu wa Kishamia) ambao ni Ali (a.s), Fatma (a.s), Hassan (a.s) na Hussein (a.s). [1] Abdallah bin Baydhawi, mmoja wa wafasiri wa Qur’an wa Ahlu-Sunna ameitaja Aya hii kama hoja ya kuthibitisha Utume wa Nabii Muhammad pamoja na fadhila kubwa walionayo watu alioambatana nao katika tukio la Mubahala. [2] Kadhalika Jarullah Zamakhshari (aliyeaga dunia 538 Hijiria) ambaye pia ni miongoni mwa wafasiri mashuhuri wa Qur’ani wa Kisuni naye pia amesema kuwa, Aya hii ni katika hoja kubwa kabisa ya kuthibitisha fadhila za Ahlul-Kisaa (Kishamia). [3] Fadhl bin Hassan Tabrasi (alifariki dunia 469 Hijiria) mfasiri wa Kishia naye amesema, Aya hii inaonyesha na kuthibitisha ubora wa Bibi Fatma (a.s) kwa wanawake wote duniani. [4]
Sababu ya Kushuka
- Makala Asili: Mubahala Baina ya Mtume na Wakristo wa Najran.
Aya ya Mubahala ilishuka kutoa jibu kwa Wakristo wa Najran. [5] Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ni kwamba, ujumbe wa Kikristo kutoka Najran ulifika kwa Mtume kujadili kuhusiana na madai yake ya Utume. Mtume sambamba na kujitambulisha yeye kwamba, ni Mtume alimtaja Nabii Issa (a.s) kwamba, ni mja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo Wakristo wao walisisitiza kwamba, kuzaliwa Nabii Issa bila baba ni hoja na dalili ya kuwa kwake ni Mungu. [6] Wakristo wa Najran walikataa hoja walizopatiwa na kung’ang’ania msimamo wao na hivyo Mtume akawaita kufanya maapizano na wao wakaafiki pendekezo hilo. Muda ulipowadia Mtume alitoka akiwa pamoja na Ali, Fatma, Hassan na Hussein (a.s). Wakristo walipomuna Mtume amekuja kwa ajili ya Mubahala akiwa amefuatana na vipenzi vyake, mmoja wa wajumbe waandamizi wa ule ujumbe wa Kikristo, alipowaona wale waliokuwa wakifuatana na Mtukufu Mtume (s.a.w.w), alisema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba amekaa kama Manabii walivyokuwa wakiketi kwa ajili ya Mubahala”, na akarejea. Akaongeza: “Kama Muhammad (s.a.w.w) hakuwa kwenye haki, asingethubutu kuja kwa Mubahala namna hii, na kama Muhammad (s.a.w.w) atakutana nasi katika Mubahala, basi hata Mkristo mmoja hatabaki hai kabla ya mwaka huu kuisha." Kwa muktadha huo, Wakristo hao wakaomba suluhu na mapatano na wakamtaka Mtume awakubalie walipe kodi na kubakia katika dini yao. Mtume akawakubalia ombi lao. [7]
Tafsiri
Sayyid Nurullah Husseini Shushtari, anasema kuwa, wafasiri wana mtazamo mmoja kwamba, “watoto wetu” katika Aya ya Mubahala inaashiria Hassan na Hussein, “wake zetu” ni ishara ya Fatma na “nafsi zetu au sisi wenyewe” anaashiriwa Imam Ali (a.s). [8] Kadhalika Allama Majlisi amezitambua hadithi zinazotoa dalili kwamba, Aya ya Mubahala imeshuka kwa watu wa Kishamia (Ahlul-Kisaa) ni mutawatir. [9] Katika kitabu cha Ihqaq al-Haqq (kilichoandikwa 1014 Hijria), kumeorodheshwa takribani vyanzo 60 vya Ahlu-Sunna ambavyo vinabainisha wazi kuhusiana na kwamba, Aya hii imeshuka kuwahusu watano hawa; [10] miongoni mwavyo ni kitabu cha al-Kashshaaf cha Zamakhshari, [11] Tafsir al-Kabir ya Fakhrurazi, [12] na Anwar al-Tanzil wa asrar al-Ta’wil kilichoandikwa na Abdullah bin Omar Baydhawi. [13]
Hoja za Kihistoria
Kwa mujibu wa hadithi mbalimbali Maimamu wa Kishia na baadhi wa masahaba walitumia Aya ya Mubahala kwa ajili ya kuthibitisha ubora na fadhila za Imam Ali (as). Baadhi yao ni:
Sa’d bin Abi Waqqas
Amar bin Sa’d bin Abi Waqqas amenukuu kutoka kwa baba yake Sa’d bin Abi Waqqas kwamba, Muawiyya alimuuliza Sa’d kwa kumwambia, kwa nini humtukani Ali? Sa’d akasema: Madhali mambo matatu ningali nayakumbuka, katu siwezi kumtuka yeye; ambapo kama moja kati ya mambo hayo matatu lingekuwa linanihusu mimi basi ningelipenda kuliko hawa ngamia wangu wenye manyoya mekundu; miongoni mwayo ni wakati Aya ya Mubahala iliposhuka, Mtume (s.a.w.w) aliwaita Ali, Fatma, Hassan na Hussein na kusema: (اَللهُمَّ هؤلاءِ اَهلُ بَیتی ; Ewe Mola mlezi! Hawa ni watu wangu wa nyumbani (Ahlu-Baiti wangu)). [18]
Imam Kadhim (a.s)
Harun mtawala wa Bani Abbas alimwambia Imam Kadhim (a.s): Vipi wewe unasema kwamba, "sisi ni katika kizazi cha Mtume" katika hali ambayo Mtume hana kizazi kwani kikawaida kizazi cha mtu huendelea kupitia mtoto wa kiume, na sio binti, na nyinyi sio katika watoto wa binti ya Mtume? Katika jibu lake, Imam Kadhim alisoma sehemu ya Aya ya Mubahala na kisha akasema: Hakuna mtu aliyesema kwamba, wakati wa kufanya Mubahala na manaswara, ghairi ya Ali bin Abi Talib, Fatma, Hassan na Hussein, Mtume alikuja na mtu mwingine. Hivyo basi makusudio ya “watoto wetu” katika Aya ya Mubahala ni Hassan na Hussein na makusudio ya “wake zetu” ni Fatma na makusudio ya “na sisi wenyewe” ni Ali bin Abi Talib. [19]
Imamu Ridha (a.s)
Kwa mujibu wa nukuu ya Sheikh Mufid ni kwamba, Ma’amun mtawala wa Bani Abbas alimtaka Imam Ridha (a.s) ataje fadhila kubwa kabisa ya Imam Ali (a.s) ambayo imeashiria katika Qur'ani Tukufu. Katika kujibu hilo, Imam Ridha alisoma Aya ya Mubahala. [16] Ma’mun akasema: Katika Aya hii Mwenyezi Mungu ameleta lafudhi ya wingi katika maneno ya watoto na wanawake, katika hali ambayo, Mtume alikuja na watoto wawili wa kiume na binti yake pekee katika tukio hilo la Mubahala. Hivyo basi hata kuita nafsi (yake)_pia, kiuhakika ni Mtume peke yake. Katika hali hii, hakutakuwa na fadhila zozote kwa ajili ya Imam Ali. Imamu Ridha (a.s) akajibu kwa kusema:
- Kile ulichokisema siyo sahihi; kwani mlinganiaji na muitaji, anamuita mtu asiyekuwa yeye (hajiiti mwenyewe); kama ambavyo muamrishaji anamuamrisha mtu asiyekuwa yeye; na siyo sahihi ajiite na kujilingania yeye mwenyewe; kama ambavyo mtu hawezi kujipa amri na maagizo yeye mwenyewe. Mtume wa Mwenyezi Mungu katika Aya ya Mubahala, hakumuita mtu mwingine ghairi ya Imam Ali. Hivyo basi inathibiti kwamba, yeye ni nafsi iliyokusudiwa na Mwenyezi Mungu katika kitabu chake na hukumu yake ameiweka katika Qur’ani.
Ufahamu wa kifiq’h
Baadhi ya watafiti na wafasiri wa Qur’an wa zama hizi, wamedondoa nukta na kuja na welewa wa kifiq’h kuhusiana na Aya ya Mubahala na miongoni mwa nukta hizo ni:
- Kuhalalisha ushiriki wa wanawake katika masuala ya kisiasa na kijamii; nukta hii imetolewa katika neno “na wake zetu” katika Aya ya Mubahala na kuhudhuria Bibi Fatma (a.s) katika tukio hilo la maapizano. [22] Sayyid Abd al-Ala al-Sabziwari, mfasiri wa Kishia (aliaga dunia 1414 Hijria) anasema kuwa, pamoja na kuwa, msingi wa Qur'ani ni kinaya na kuhifadhi heshima ya wanawake, kutumiwa neno “nisaa” katika Aya ya Mubahala ina makusudio na ishara na moja ya ishara hizi ni kushiriki wanawake katika masuala yanayohusiana na dini. [23] Rashid Ridha anasema, katika Aya ya Mubahala ushiriki wa wanawake na wanaume katika mapambano ya kikaumu na kidini umetolewa hukumu, na hukumu hii inahusiana na kuweko usawa baina ya wanawake na wanaume katika kazi za umma na za kawaida, isipokuwa kama kutakuwa kumeondolewa na kufumbiwa macho katika baadhi ya masuala kama vita. [24].
- Uhalali wa Mubahala: Mwandishi wa makala ya “Usomaji Mpya wa Kifiq’h; wa Aya ya Mubahala” ameitumia Aya ya Mubahala kuhalalisha kufanya maapizano katika Uislamu. [25] Akiwa na lengo la kuthibitisha madai yake ametoa mifano ya maagizo ya kufanya maapizano au mafunzo ya namna ya kufanya maapizano yaliyotolewa na Maimamu Maasumina (a.s). Imekuja pia katika tafsiri ya Nemooneh kwamba, licha ya kuwa mhutubiwa wa kufanya Mubahala katika Aya ya Mubahala ni Mtume mwenyewe na hilo ni makhsusi kwake, lakini wito wa kufanya maapizano ni jambo la halali na lina hukumu jumla. [28]
- Uhalali wa kutetea Uislamu kwa kujitolea kwa hali na mali: [29] Abd al-A’la al-Sabziwari anasema katika Tafsiri ya Mawahib al-Rahman kwamba, moja ya nukta zinazofahamika katika Aya ya Mubahala ni kwamba, lengo la kila mwanadamu linapaswa kuwa ni kuhakikisha haki inapatikana na kuitetea na awe na utayari wa kujitolea katika njia hii kwa roho na mali. [30]
Rejea
Vyanzo