Maimamu wa Kishia

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Maimamu watakatifu)

Maimamu wa Kishia (Kiarabu: أئمة أهل البيت) au Maimamu kutoka familia ya Mtume (s.a.w.w) ni viongozi kumi na mbili, ambao ni watu wa nyumba ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambao kwa mujibu wa Hadithi, wao ndio warithi wa bwana Mtume (s.a.w.w.) na ni Maimamu wa jamii ya Kiislamu baada yake. Imamu wa kwanza wa Mashia ni Imam Ali (a.s) na maimamu wengine wanaofuatia baada yake, ni watoto wake na wajukuu wa bibi Zahra (a.s). Kwa mujibu wa madhehebu ya Shia Imamiyyah, Maimamu (a.s) wameteuliwa kuwa Maimamu na Mwenyezi Mungu nao viongozi wenye sifa kadhaa, miongoni mwazo ni kama vile; umaasumu, ubora, wana ujuzi uliofungamana na elimu ghaibu na wana haki ya kuombea waja wa Mungu shufaa. Maimamu (a.s) wana majukumu yote ya Mtume (s.a.w.w) isipokuwa kupokea ufunuo na kuleta Sheria tu.

Masunni hawakubali Uimamu wa Maimamu wa Kishia, lakini wanaonyesha upendo juu yao na kukubaliana na mamlaka yao ya kidini na kielimu. Majina ya Maimamu 12 hayajatajwa katika Qur'an, lakini kuna baadhi ya Hadithi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kama vile Hadithi ya hotuba ya Ghadir, Hadithi iliyo nukuliwa na Jabir na Hadithi ya Makhalifa Kumi na mbili (a.s). Kwa mujibu wa Hadithi hizi, Maimamu na warithi wa Mtume (s.a.w.w) ni watu kumi na mbili, wote ni kutoka kwa Maquraishi na familia ya Mtume (s.a.w.w).

Kwa mujibu wa maoni ya madhehebu ya Mashia Ithnaashariyyah, Imam Ali (a.s) aliteuliwa na kupewa cheo cha Uimamu kupitia vielelezo vya wazi kabisa kutoka Mtume (s.a.w.w). Yaani yeye aliteuliwa moja kwa moja na Mtume (s.a.w.w). Tangu wakati huo, kila imamu amemtambulisha Imamu atakaye fuata baada yake kwa vielelezo vya wazi na kwa maandishi. Kwa hiyo, warithi 12 baada ya Mtume (s.a.w.w), ni hawa wafuatao: Ali bin Abi Talib, Hassan bin Ali, Hussein bin Ali, Ali bin Hussein, Muhammad bin Ali, Ja’afar bin Muhammad, Mussa bin Jafa’ar, Ali bin Mussa. Muhammad bin Ali, Ali bin Muhammad, Hassan bin Ali na Mahdi (amani iwe juu yao). Kwa mujibu wa mtazamo mashuhuri wa Kishia, Maimamu kumi na mmoja waliuawa kishahidi na wa mwisho ambaye ni Mahdi aliyeahidiwa kudhuhiri, yuko katika ghaibu.

Kuna vitabu vingi vilivyo andikwa na kuhusiana na wasifu wa Maimamu wa Kishia na sifa zao, Kitabu maarufu kwa wanazuoni wa madhehebu ya Shia ni al-Irshadu na Dal'il al-Imama, na kutoka upande wa Sunni ni Yanaabiu al-Muwadda na Tadhkratu al-Khawas.

Sifa na wasifu makhususi wa Imamu

Imani ya uimamu wa maimamu kumi na wawili ni miongoni mwa itikadi za madhehebu ya Shia Ithnaashariyya. [1] Kwa mtazamo wa Mashia, Maimamu wameteuliwa na Mwenyezi Mungu na hutangazwa kupitia Mtume Muhammad (s.a.w.w). [2]

Mashia wanaamini kwamba ijapokuwa majina ya Maimamu hayakutajwa ndani ya Qur’an, lakini Uimamu wa wao umetajwa katika Aya kadhaa. Miongoni mwa Aya zinazo zungumzia Uimamu, kama vile; Aya ya Ulul-Amr, Aya ya Tat-hir, Aya ya Wilayah, Aya ya al-Ikmal, Aya ya Tabligh na Aya ya Saadiqina. [3] Bila shaka majina na idadi ya Maimamu hao (a.s) yametajwa katika Hadith. [4]

Kwa mujibu nadharia na itikadi ya Shia, Maimamu wana majukumu yote aliyo nayo Mtume (s.a.w.w), kama vile kueleza aya za Qur'an, kufafanua sheria za kidini, kulea na kuelimisha watu katika jamii, kujibu maswali ya kidini, kusimamisha haki na uadilifu katika jamii, na kulinda mipaka ya Uislamu, tofauti yao na Mtume (s.a.w.w) ni katika suala la kupokea ufunuo na kuleta Sheria. [5]

Sifa na wasifu makhususi

Kwa mtazamo wa madhehebu ya Mashia wa Imamiyya, baadhi ya sifa za Maimamu kumi na mbili ni kama zifuatazo: [Maelezo 1]

  • Umaasumu: Kama vile Mtume (s.a.w.w) alivyo Maasumu, Maimamu ni Maasumu, yaani hawatendi dhambi na hawana aina yoyote ile ya mitelezo ya upotofu. [6]
  • Ubora: Kupitia mtazamo wa wanachuoni wa Kishia, Maimamu ni watu bora kabisa, nao ni bora kuliko viumbe wote, malaika na watu wengine wote, isipokuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w). Kuna Hadithi kadhaa kuhusiana na ubora wa Maimamu (a.s), Hadithi ambazo ni mustafidhu (zinazokaribia daraja ya “mutawatir”). [8]
  • Elimu ya ghaibu: Maimamu wana elimu ya ghaibu kutoka kwa Mwenyezi Mungu [9]
  • Wilayatu takwiiniyyah na wilayatu tashri’iyyah: Maana yake ni; Mamlaka ya uendeshaji ulimwengu wa kimaada na Kisheria. Wanachuoni wengi wa Kishia wanakubaliana uthibitisho unao ashiria mamlaka hayo ya Maimamu (a.s). Hakuna tofauti wa khitilafu baina wanazuoni kuhusiana na mamlaka ya Maimamu juu ya nafsi pamoja na mali zao [11] Kwa kuzingatia Hadithi zinazo elezea kukabidhiwa Mtume pamoja na Maimamu mamalaka ya mambo mbali mbali, [12] Hadithi hizo pia zinathibisha mamlaka juu ya kutunga sheria. [13]

Pia angalia neno tafwidh (uwakala hurui)

  • Daraja ya uombezi: Maimamu wote wana nafasi ya uombezi kama alivyo Mtume (s.a.w.w). [14]
  • Mamlaka ya kidini na kielimu: Kwa kuzingatia matini kadhaa za Hadithi, kama vile Hadithi ya Thaqalaini [15] na Hadith ya Safina [16], Maimamu wana mamlaka ya kielimu na kidini na ni wajibu watu katika mambo ya kidini kuwarejea wao. Hivyo basi Maimamu ndio suluhisho na mamabo yote ya kieleimu na kidini. [17]
  • Mamlaka ya uongozi wa jamii: Maimamu (a.s) wana jukumu la uongozi na utawala wa jamii ya Kiislamu baada ya Mtume (s.a.w.w.). [18]
  • Wajibu wa kutiiwa: Kwa mujibu wa Aya ya Ulul-Amr, Maimamu (a.s) wanachukuliwa kuwa ni Mufttaridh al-Ta'ah (ni wajibu kutiiwa). Kwa hiyo ni wajibu kuwatii bila ya mipaka, yaani kama ilivyo kuwa ni wajibu kumtii Allah na Mtume wake (s.a.w.w.) bila ya mipaka, basi pia nao wanatakiwa kutiiwa bila ya mipaka. [19]

Kwa mujibu wa wanazuoni wengi wa Kishia, Maimamu wote wa Kishia wamekufa au watakufa kifo cha kishahidi. [20] Hoja yao katika madai hayo ni baadhi ya vielelezo vya Hadithi, [21] ikiwa ni pamoja na Hadithi kutoka kwa Imam al-Rida (a.s) iliyo nukuliwa na Abasalt, ambayo inasema: “وَ اللهِ مَا مِنَّا إِلَّا مَقْتُولٌ شَهِيد” ; "Wa Allahi hakuna yeyote miongoni mwetu isipokuwa atuawa Shahid". [22] Kulingana maelezo ya Hadithi hii, maimamu wote watakufa kwa kifo cha kishahidi. [23]

Uongozi wa Maimamu kulingana na kalenda ya Hijiria Qamaria

Imamu Ali Imamu Hassan Imamu Hussein Imamu Sajjad Imamu Baqir Imamu Swadiq Imamu Kadhim Imamu Ridha Imamu Jawad Imamu Hadi Imamu Hassan Askari Imamu Mahdi
11.H 40.H 50.H 61.H 94.H 115.H 148.H 183.H 203.H 220.H 254.H 260.H

Uimamu wa Maimamu

Makala Asili: Uimamu wa Maimamu wa Kishia

Ili kuthibitisha Uimamu wa Maimamu kumi na wawili, wanavyuoni wa Shia wamewasilisha hoja mbali mbali za kimantiki (kiakili) pia hoja za maandiko. Hoza za kimantiki zilizo simamishwa na wanazuoni hao ni kama vile; Umaasumu na ubora wa Maimamu (a.s). Kwa upande wa hoja za maandiko, wao wametoa vielelezo vya baadhi ya Hadithi kama vile; Hadithi ya Jabir, Hadithi ya Lauh, na Hadithi ya Makhalifa 12. [24]

Hadithi ya Jabir

Makala Asili: Hadithi ya Jabir

Baada ya kuteremshwa Aya isemayo; «يا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللهَ وَ أَطِيعُوا الرَّسُولَ وَ أُولِي الْأَمْرِ مِنْكُمْ» Jabir bin Abdullah Ansari alimuuliza Mtume kuhusu maana ya ‘Ulul-amri’ (viongozi wenye mamlaka), na Mtume (s.a.w.w) akajibu kwa kusema: “Hao ni makhalifa (warithi) wangu na Maimamu wa Waislamu baada yangu. Wa kwanza wao ni Ali bin Abi Talib, na baada yake; ni Hassan, Hussein, Ali bin Hussein, Muhammad bin Ali, Ja’afar bin Muhammad, Mussa bin Ja’afar, Ali bin Mussa, Muhammad bin Ali, Ali bin Muhammad, Hassan bin Ali, na baada yake yeye ni mtoto wake ambaye jina la kunia yake ni sawa na kunia yangu...”. [26]

Hadithi ya Makhalifa 12

Makala asili: Hadithi ya Makhalifa kumi na mbili

Kuna baadhi ya Hadithi zilizo simuliwa na Wasunni ambapo idadi ya makhalifa wa Mtume (s.a.w.w.) na baadhi ya sifa zao, kama vile sifa ya Uquraishi, zimetajwa ndani yake. Mtume (s.a.w.w.) katika Hadithi iliyo nukuliwa na Jabir bin Samra kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) amesema: “Dini hii itaendelea kuwa salama madhali (endapo) mtatawaliwa na Makhalifa 12, ambao wote wanatokana na ukoo wa Kikuraishi” "Katika Hadithi iliyonukuliwa na Ibn Massoud, idadi ya Warithi watakao shika nafasi ya uongozi baada ya Mtume (s.a.w.w.) ni 12, ambayo ni sawa na idadi ya viongozi wa Israeli. Kwa mujibu wa maelezo ya Sulaiman bin Ibrahim Qanduzi, ambaye ni mwanazuoni wa Kisunni, makhalifa kumi na mbili walio kusudiwa katika Hadithi ya bwana Mtume (sa.w.w) ni Maimamu kumi na mbili wa Kishia, kwa sababu Hadithi hii haiwezi kuingiza wengine wasiokuwa hao. [30]

Uarifisho wa Maimamu

Shia wa Imamiyya (Ithnaashariyya) wakitegemea misingi ya hoja za kiakili [31] na maandiko kama vile Hadithi maarufu ya Ghadir na Hadithi ya Manzila, wanaamini kwamba Khalifa mwadilifu na asiye na kifani wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), ni Ali bin Abi Talib (a.s). [32] Baada ya Imam Ali (a.s), wanao fuatia kwa mpangilio baada yake ni; Imam Hassan (a.s), Imamu Hussein (a.s), Imamu Sajjad (a.s.), Imam Baqir (a.s), Imamu Sadiq (a.s), Imamu Musa Kadhim (a.s), Imamu Ridha (a.s), Imamu Jawad (a.s), Imamu Hadi (a.s), Imamu Hasan Askari (a.s.), na Imamu Mahdi (a.s). Hao ndio wanaosimamia Uimamu na uongozi wa jamii ya Kiislamu baada ya Mtume (s.aw.w.). [33]

Maelezo ya Ufafanuzi

  • Hoja za kiakili ni pamoja na ushahidi kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuwa na lengo la kumteua mrithi wake, na kwamba Ali bin Abi Talib (a.s) alikuwa mtu pekee anayekidhi vigezo vyote vya mrithi huyo.
  • Hadithi maarufu ya Ghadir inaeleza kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimteua Ali bin Abi Talib (a.s) kuwa mrithi wake mbele ya waumini wote huko Ghadir Khum, mji ulioko Saudi Arabia.
  • Imamu wa kwanza wa Shia Imamia ni Ali bin Abi Talib (a.s), ambaye alikufa mwaka wa 40 Hijiria. Imamu wa mwisho wa Mashia ni Imamu Mahdi (a.s), ambaye anaaminika kuwa amejificha na atarudi siku moja kurejesha haki duniani.
Jina Lakabu Kunia Tarehe ya kuzaliwa Mwaka wa kuzaliwa Mahala alipozaliwa Siku ya kifo cha kishahidi Mwaka wa shahada Mahala alipopatia shahada Uimamu Kipindi cha Uimamu Jina la mama
Ali bin Abi Talib Amirul Muuminina Abu al-Hassan 13 Rajabu/10 October 30 Mwaka wa Tembo /599M Kaa'ba 21 Ramadhani/28 January 40H/661M Kufa 11H/632-40/661M Miaka 29 Fatima bint Asad
Hassan bin Ali Al-Mujtaba Abu Muhammad 15 Ramadani/1 March 3H/625M Madina 28 Safar/27 March 50H/670M Madina 40H/661-50/670M Miaka 10 Bibi Fatma Zahraa(a.s)
Hussein bin Ali Sayyidu al-Shuhadaa Abu Abdillahi 3 Sha'ban/8 January 4H/626M Madina 10 Muharram/10 October 61H/680M Karbala 50H/670-61/680M Miaka 10 Bibi Fatma Zahraa(a.s)
Ali bin Hussein Sajjad, Zainul-'abidin Abu al-Hassan 5 Sha'ban/6 January 38H/658M Madina 25 Muharram/19 October 95H/713M Madina 61H/680-95/713M Miaka 35 Shahrbanu
Muhammad bin Ali Baqiru al-'Ulum Abu Ja'far 1 Rajabu/10 May 57H/677M Madina 7 Dhul-Hijja/28 January 114H/733M Madina 95H/713-114/733M Miaka 19 Fatima bint al-Imam al-Hassan
Ja'far bin Muhammad Swadiq Abu Abdillah 17 Rabiu al-awwal/20 April 83H/704M Madina 25 Shawwal/14 December 148H/765M Madina 114H/733-148/765M Miaka 34 Ummu Farwa bint al-Qasim
Mussa bin Ja'afar Kadhim Abu al-Hassan 7 Safar/8 November 128H/745M Madina 25 Rajab/1 September 183H/799M Kadhimiyya 148H/765-183/799M Miaka 35 Hamida al-Barbariyya
Ali bin Mussa Ridha Abu al-Hassan 11 Dhul-Qa'da/29 December 148H/765M Madina Mwisho wa Safar/5 September 203H/818M Mash-had 183H/799-203/818M Miaka 20 Najma Khatun
Muhammad bin Ali Taqii, Jawad Abu Ja'far 10 Rajab/8 April 195H/811M Madina Mwisho wa Dhul-Qa'da/25 November 220H/835M Kadhimiyya 203H/818-220/835M Miaka 17 Sabika
Ali bin Muhammad Hadi, Naqii Abu al-Hassan 15 Dhul-Hijja/6 March 212H/828M Madina 3 Rajab/28 June 254H/868M Samarra 220H/835-254/868M Miaka 34 Samana al-Maghribiyya
Hassan bin Muhammad Zakiyyun, Askari Abu Muhammad 10 Rabiu Thani/4 December 232H/846M Madina 8 RabiU Thani/1 January 260H/874M Samarra 254H/868-260/874M Miaka 6 Hudayth
Hujjatu bin Hassan Qaim Abu al-Qasim 15 Sha'ban/29 July 255H/289M Samarra - - - 260H/874M Kuanzia 260H/874M Mpaka (1445H) Narjis

Imam Ali (a.s)

Makala asili: Imam Ali (a.s)

Ali bin Abi Talib, maarufu kama Imam Ali (a.s) na akiitwa Amirul Mu'minin (a.s), ni Imamu wa kwanza wa Shia, mtoto wa Abu Talib na Fatima bint Asad, alizaliwa tarehe 13 Rajab mwaka wa 30 Hijiri katika Kaaba. [34] Alikuwa ni mtu wa kwanza kumuamini Mtume (s.a.w.w), [35] na alikuwa karibu sana na bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) amabaye alioa binti yake, Fatima (s.a). [36]

Ingawa Mtume Muhammad (s.a.w.w) mara kadhaa alimtambulisha Ali (a.s) kama mrithi wake, [37] -ikiwemo tukio la Ghadir Khum- ila Abu Bakar alichaguliwa kuwa Khalifa wa kwanza wa Waislamu baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w). [38] Baada ya kipindi cha miaka 25 ya subira na kujiepusha na mapinduzi, na kwa nia ya kuhifadhi amani na kulinda umoja wa jamii ya Kiislamu katika zama za Makhalifa watatu, Ali (a.s) alichaguliwa kuwa Khalifa wa Waislamu mnamo mwaka wa 35 Hijiria. [39] Katika ukhalifa wake wa miaka minne na miezi tisa, vilitokea vita vitatu vya ndani vya Waislamu wenyewe kwa wenyewe, amabavyo ni: Vita vya Jamal, vita vya Siffiin, na vita vya Nahrawani.

Ali (a.s) alipigwa upanga na Ibn Muljim Muradi akiwa ndani ya mihrabu ya Msikiti wa Kufa wakati wa sala ya asubuhi ya tarehe 19 Ramadhani, mwaka wa 40 Hijiria, na akafa tarehe 21 Ramadhani na kuzikwa huko mjini Najaf nchini Iraq. [41] Ali (a.s) alikuwa na wasifu wa sifa nyingi mno, ikiwa ni pamoja na ujasiri, uchamungu, na hekima. [42] Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba; zaidi ya Aya 300 zimeteremshwa kumsifu Ali (a.s). [43] Pia imepokelewa kutoka kwake kwamba Mungu hakuteremsha aya yoyote ambayo ndani yake mna ibara isemayo «یا أیها الذین آمنوا» "Enyi mlioamini", isipokuwa Ali (a.s) yuko mbele ya Waumini hao na ndiye Amiri wao. [44]

Imamu Hassan (a.s)

Makala asili: Imamu Hassan (a.s)

Hassan bin Ali (a.s), anayejulikana kama Imamu Hassan (a.s) au Imamu Hassan al-Mujtaba, ni mwana wa Imam Ali bin Abi Talib (a.s) na bibi Fatima (a.s), alizaliwa tarehe 15 Ramadhani mwaka wa 3 Hijiri huko Madina. [45]

Baada ya kuuawa kwa baba yake, kupitia amri ya Mungu na wasia wa marehemu baba yake, Imamu Hassan (a.s) alichukua nafasi ya baba yake kama ni Imamu wa kwanza wa Mashia. Alitawala kama Khalifa wa Waislamu kwa takriban miezi sita. [46] Katika kipindi hichi, Muawiya bin Abi Sufiyan, aliivamia Iraq, ambayo ilikuwa makao makuu ya utawala wa Imamu Hassan (a.s). Aliweza kuwadanganya na kuwachochea makamanda wa jeshi la Imamu Hassan (a.s) dhidi yake, na hatimaye Imamu Hassan (a.s) alilazimika kukubali suluhusho la amani baina yake na Muawiya. Katika amani hii, Imam Hassan (a.s.) alikubaliana kukabidhi utawala dhahiri (usio kuwa na idhini ya Mungu) kwa Muawiya, kwa masharti ya kwamba baada ya kifo cha Muawiya, utawala utarudishwa kwa Imamu Hassan (a.s) na familia yake na wafuasi wake watakuwa salama. [47] Imamu Hassan (a.s) aliongoza kama Imamu kwa miaka 10, na akafa kwa sumu mnamo mwezi 28 Safar mwaka wa 50 Hijiria, kwa uchochezi wa Muawiya, kupitia mkono wa mkewe, Ja'ada. Baada Imamu Hassan kufariki alizikwa katika makaburi ya Baqi'. [49]

Imamu Hassan (a.s) alikuwa mmoja wa wale waliokuwa katika tukio la kufunikwa shuka la Hadithi ya Kisaa, [50] na alikuwa ni mmoja wa wale waliokuwapo katika tukio la Mtihani wa Mubahala, [51] na ni mmoja wa Ahlul-Bayt (a.s) ambao Aya ya Utakaso imeshuka juu yao. [52]

Imam Hussein (a.s)

Makala asili: Imamu Hussein (a.s)

Imamu Hussein (a.s), anayejulikana pia kama Abu Abdillahi na Sayyid al-Shuhada, ni Imamu wa tatu wa Shia, na mwana wa Imamu Ali bin Abi Talib na Fatima Zahra. Alizaliwa mwezi 3 Shaaban mwaka wa nne wa Hijiria huko Madina. [53] Imamu Hussein (a.s) alichukua nafasi ya Uimamu kupitia amri ya Mtume, wasia wa baba yake na msisitizo ya kaka yake, baada ya kuuawa kwa kaka yake (Imamu Hassan (a.s)) kishahidi. [54]

Imamu Hussein (a.s) alitawala kwa kipindi cha miaka kumi, [55] ambapo miezi sita ya mwisho ya utawala wake iliambatana na ukhalifa wa Mu'awiyah. [56] Mnamo mwaka wa 60 Hijiria Muawiyah aliaga dunia, na nafasi yake ya ukhalifa ilikaliwa na Yazid ibn Mu'awiyah. [57] Yazid alitaka Imamu Hussein (a.s) ampe kiapo cha utiifu juu yake cha kumuidhinisha kushika nafasi ya ukhalifa, kwa hivyo alimtuma gavana wake huko Madina amtake Hussein (a.s) amwapie kiapo cha utiifu, na akikataa kufanya hivyo, basi amkate kichwa na akitume kichwa hicho nchi Syria (kwenye mamlaka ya Yazid bin Muawiyah). Gavana wa Yazid aliyoko huko Madina, alimfikishia Imamu Hussein (a.s) salamu za Yazid, Imam Hussein (a.s) alikataa kumwapia Yazid, na akaamua kuondoka Madina -wakati wa usiku- yeye na familia yake pamoja na baadhi ya masahaba wake na kuelekea Makka. [58]

Baada ya muda Imamu Hussein alielekea mjini Kufa akiwa pamoja na familia yake watu na baadhi ya Masahaba wake, alifanya hivyo kutokana na barua za watu wa Kufa walizomwandikia wakimwalika Imamu Hussein (a.s) kuenda jijini mwao. [59] Imam Hussein (a.s) alifika Karbala, mahala ambapo alikabiliwa na kuzingirwa na wanajeshi wa Yazid ibn Mu'awiyah, mnamo mwezi 10 Muharram, yeye pamoja na Masahaba zake walipambana na jeshi hilo -lililo ongozwa na Omar bin Sa’ad- kwa ushujaa mkubwa kabisa. Hatimae katika vita hivyo vya siku ya Ashura, yeye yeye pamoja na masahaba zake waliuawa shahidi, na wanawake na watoto walibakia mateka mikononi mwa maadui, miongoni mwao akiwemo Imamu Sajjad (a.s) ambaye alikuwa ni mgonjwa katika wakati wa vita hivyo. [60]

Imamu Hussein (a.s) ni mmoja wa walifunikwa shuka waliotajwa katika Hadithi ya Kisaa. [61] Pia yeye ni mmoja wa waliohudhuria tukio la changamoto ya Mubahala, [62] na ni mmoja wa Ahlul-Bayt (a.s) walio shukiwa na Aya ya utakaso. [63]

Imamu Sajjad (a.s)

Makala asili: Imamu Sajjad (a.s)

Ali bin Hussein (a.s), anayejulikana pia kama Sajjad na Zainal Abidin, ni Imamu wa nne wa Shia, mwana wa Imam Hussein (a.s), yeye aliyezaliwa na Shahrbanu binti Yazdegerd wa Tatu (mfalme wa Iran), mwaka wa 38 Hijiria huko Madina. [64]

Imam Sajjad (a.s) alitekwa nyara katika tukio la Karbala na kupelekwa pamoja na mateka wa Karbala kwenda katika mji wa Kufa [65] na Sham (Syria). [66] Akiwa mjini Sham, alitoa hotuba ya kujitambulisha yeye pamoja na baba zake ambayo iliwagusa mno watu wa Sham. [67] Aliporejeshwa Madina baada ya kumalizika kwa kipindi cha umateka, alibaki Madina akijishughulisha na ibada, na hakufungamana na yeyote isipokuwa waumini makhususi wa madhehebu ya Shia, kama Abu Hamza Thumali na Abu Khalid Kaabuli. Waumini hao pia walieneza maarifa waliyojifunza kutoka kwake miongoni mwa Shia. [68]

Imamu wa nne baada ya miaka 34 ya ukaimu wake katika nafasi ya Uimamu, [69] akiwa na umri wa miaka 57, mwaka wa 95 Hijiria, [70] aliuawa kwa sumu kwa mkono wa Walid ibnu Abdu al-lmalik [71] na akazikwa katika makaburi ya Baqi'i karibu na mjomba wake Imamu Hassan (a.s). [72]

Mkusanyiko wa maombi na dua za Imam Sajjad (a.s), ambazo zinajumuisha maarifa mengi ya kidini ndani, yamekusanywa katika kitabu kiitwacho Sahifa Sajjadiya. [73]

Imamu Muhammad Baqir (a.s)

Makala asili: Imamu Muhammad al-Baqir (a.s)

Imamu Muhammad bin Ali, maarufu kama Imamu Muhammad al-Baqir (a.s), ni Imamu wa tano wa Shia. Yeye ni mtoto wa Imamu Sajjad (a.s) na mama yake ni Fatima binti wa Imamu Hassan (a.s) [74], naye alizaliwa huko Madina mwaka wa 57 Hijiria. [75] Baada ya baba yake, alitawazwa kuwa Imamu kupitia amri ya Mungu, Mtume (s.a.w.w), pamoja na wasia wa Maimamu waliotangulia kabla yake. Mnamo mwaka wa 114 Hijiria, [77] aliuawa kwa sumu kupitia mkono wa Ibrahim bin Walid bin Ablulmalik, [78] ambaye ni ndugu wa Hisham khalifa wa Amawiy. Baada kifo chake, Imamu Muhammad al-Baqir alizikwa karibu na kaburi la baba yake katika makaburi ya Baqi'i. Yeye pia alikuwa na miongoni mwa walio hudhuria katika tukio la vita vya Karbala, ambapo wakati huo alikuwa na umri wa miaka minne. [80]

Katika kipindi cha Imamu wa tano, ambacho kilidumu kwa miaka 18 au 19, [81] kulikuwa na harakati za kimapinduzi na vita vya kila siku kutokana na dhuluma za Bani Umayyah. Harakati hizo ziliufanya utawala wa kikhalifa uwe katika hali ya fazaa za kila siku, jambo ambalo lilileta afuani kwa upande wa Mashia, ambapo serikali hiyo ilikuwa haina wakati wa kuwahijumu na kuwadhuru Ahlul-Bayt (a.s). [82] Kwa upande mwingine, tukio la Karbala na unyonge wa Ahlul Bait uliamsha hisia za Waislamu na kuwafanya wawe karibu naye Zaidi. Jambo hili liliunda fursa mpya kwake ya kusambaza ukweli wa Kiislamu na maarifa sahihi ya dini kwa mtazamo halisi wa Ahlul-Bayt (a.s), fursa ambayo haijawezekana katika vya Maimamu waliopita kabla yake. Katika kipindi cha Imamu Muhammad al-Baqir (a.s) kilichoambatana na fursa hiyo muhimu, kulionekana kiwango kikubwa mno cha Hadithi kilicho nukuliwa kutoka kwake (a.s). [83] Kulingana na maelezo ya Sheikh Mufid ni kwamba, Hadithi zilizo nukuliwa kutoka kwa Muhammad al-Baqir (a.s) kuhusiana na maarifa ya kidini ni nyingi mno, kiasi ya kwamba hakuna hata mtoto mmoja wa Imamu Hassan na Hussein (a.s) aliyeacha kiwango kama hicho cha urithi wa Hadithi. [84]

Imamu Swadiq (a.s)

Makala asili: Imam Swadiq (a.s)

Ja'far bin Muhammad, anayejulikana pia kama Imamu Swadiq (a.s), Imamu wa sita wa Shia, alikuwa mwana wa Imamu al-Baqir (a.s) na Ummu Farwa, binti ya Qasim bin Muhammad bin Abi Bakr. Alizaliwa tarehe 17 Rabi'u al-Awwal mwaka 83 Hijiria huko Madina. [85] Aliuawa shahidi na Mansur, Khalifa wa ukoo wa Banu Abbas, mwaka 148 Hijiria kupitia sumu [87] na akazikwa katika mava ya Baqi'i. [88]

Imamu Ja'far as-Sadiq, katika kipindi cha miaka 34 ya uimamu wake, [89] alipata fursa nzuri ya kueneza mafundisho ya Kiislamu kutokana na udhaifu wa utawala wa Bani Umayyah. Yeye alitumia udhaifu katika kueneza mafunzo ya dini kwa kadri ya uwezo wake. Imamu Ja'far as-Sadiq alikuwa ni mwanazuoni (Imamu) na mwalimu mashuhuri katika zama hizo, wanafunzi wake walijumuisha wanafunzi wengi wa Sunni na Shia. Juhudi zake ziliweza kutoa matunda ya wanafunzi wengi walibobea katika fani mbali mbali za elimu. [90] Inasemekana kwamba alikuwa na wanafunzi na wapokezi wa Hadithi wanao fikia zaidi ya watu 4,000. [91] Mingoni mwa wanafunzi walio orodheshwa ndani ya vyanzo mbali mbali kama vile; Zurara, Muhammad bin Muslim, Muuminu Taq, Hisham bin al-Hakam, Abaan bin Taghlib, Hisham bin Salim, Jabir bin Hayyan kwa upande wa Mashia. [92] Kutoka upande wa pili wa Ahlu-Sunna, kuna watu kama vile; Sufian al-Thauri, Abu Hanifa (mkuu wa madhehebu ya Hanafi), na Malik ibn Anas, kiongozi wa madhehebu ya Maliki. [93]

Sheikh Mufid alisema kwamba; Imamu Ja'afar al-Sadiq ndiye chanzo cha Hadithi nyingi zaidi miongoni mwa Maimamu kutoka ukoo wa Ahlu al-Bait (a). [94] Hii ndiyo sababu hasa ya wakati mwingine madhehebu ya Shia kujulikana kwa jina la madhehebu ya Ja'afariyyun. [95]

Imamu Musa Kadhim (a.s)

Makala Asili: Imamu Musa al-Kadhim (a.s)

Musa bin Ja’afar, anaye julikana kwa umaarufu lakabu ya al-Kadhim au wakati mwingine kwa lakabu ya la Babu al-Hawaiji, alikuwa ni Imamu wa saba wa Shia Imamiyyah, naye ni mtoto wa Imamu Ja’afar aliyempata kupitia ndoa yake na bibi Hamida. Musa bin Ja’afar alizaliwa mnamo mwaka wa 128 Hijiria huko Abua, eneo lililopo kati ya mji wa Makka na Madina. [96]

Imamu al-Kadhim (a.s) alichukua nafasi ya uongozi wa jamii baada ya baba yake, kupitia wasia wa wazi kutoka kwa Imamu Jaafar (a.s.). [97] Kipindi cha Uimamu wa Imamu wa saba kilicho chukuwa muda wa miaka 35, [98] kiliambatana na uongozi wa makhalifa watatu wa utawala wa Bani Abbas, nao ni; Mansoor, Hadi, Mahdi na Haruna. [99] Kipindi hichi kwa upande wa ukhalifa wa Banu Abbasi kilikuwa ndio kipindi cha upeo wa nguvu katika ukhalifa wao na ni kipindi kigumu kwa Imamu Kadhim (a.s.) pamoja na Mashia wake. Katika kipindi hichi Imamu alilazimika kufanya taqiyya mbele ya serikali na pia aliwaagiza Mashia kufanya hivyo kwa ajili ya usalama wao. [100] Mnamo mwezi 20 Shawwal mwaka 179 Hijiria, wakati Haruna alipokwenda Madina akiwemo katika safari ya Hija, aliamuru Imamu Kadhim (a.s) afungwe huko Madina. Baada ya hapo Imamu akahamishwa kutoka jela ya Madina hadi Basra na kutoka Basra hadi Baghdad. [101] Mnamo mwaka 183 Hijiria Imamu Kadhim (a.s) alikiwa katika gereza la Baghdad, aliuawa kwa sumu kupitia mkono wa Sindi bin Shahik na kuzikwa katika mava inayo julikana kwa jina la “Maqabiru Quraishi” (Makaburi ya Mquraish) [102] ambalo kwa hivi sasa liko katika eneo lijulikanalo kwa jina la Kadhimeini nchini Iraq. [103]

Imamu Ali al-Ridha (a.s)

Makala Asili: Imamu Ali al-Ridha (a.s)

Ali bin Musa bin Ja'afar, anayejulikana kama Imam Ridha (a.s) na Imamu wa nane wa kwa upande wa madhehebu ya Shia, na ni mtoto wa Imamu Musa al-Kadhim (a.s) kupitia mkewe ajulikanaye kwa jina la Najmah Khatun. Alizaliwa mnamo mwaka wa 148 Hijiria huko Madina na akafa kishahidi mnamo mwaka 203 Hijiria akiwa na umri wa miaka 55 huko Tusi (Mash-had) nchini Iran. [104]

Imamu Ridha (a.s) alichukua madaraka baada ya kufariki baba yake, kwa amri ya Mungu na kwa wasia ulio usiwa na Imamu Musa al-Kadhim (a.s) juu ya Uimamu wake. [105] Kipindi cha ukhalifa (Uimamu) wa Imamu kilichukuwa muda miaka 20 (183-203 Hijiria), [106] ambayo iliambatana na utawala wa Haruna al-Rashid na wanawe wawili Aminu na Maamuni. [107]

Baada ya kufariki Haruna al-Rashid, Maamuni alishika nafasi ya ukhalifa wa baba yake. [108] Maamuni aliamua kumfanya Imamu wa nane kuwa ni mrithi wake ili aweze kuhalalisha ukhalifa wake, kudhibiti shughuli za Imam Ridha (a.s) na kupunguza cheo na hadhi ya Uimamu wake mbele ya jamii. [109] Nia yake hiyo ndiyo sababu iliyomfanya yeye mnamo mwaka 211 Hijiria [110], amtake Imamu aondoke Madina na aende Marwu (mji uliopo Turkmenistan). [111] Maamuni kwanza alimpendekeza Imamu (a.s) kushika nafasi ya ukhalifa, kisha akampendekeza awe mshauri wa wake mkuu, ambapo pendekezo hilo likataliwa kata kata na Imamu Ridha (a.s). Maamuni hakusita katika sisitizo la matakwa yake, na hatimae akamlazimisha Imamu kukubali cheo cha nafasi ya Ushauri mkuu. Imamu alikubali kushika kushika nafasi hiyo urithi wa ukhalifa kwa masharti kwamba; yeye atashika nafasi hiyo ila hatoingilia mambo ya uteuzi au utenguzi wa viongozi wa serikali. [112] Baada ya muda, Maamun, alipo ona maendeleo ya haraka ya Mashia na kwa ajili ya kuhifadhi ukhalifa wake, aliamua kumtilia sumu Imamu Ridha (a.s) na kumwondoa duniani haraka iwezekanavyo, na hatimae kufa shahidi. [113]

Kuna Hadithi madhubuti na maarufu (Hadithi silsilat al-dhahab) iliyo nukuliwa kutoka kwa Imamu al-Ridha (a.s), [114] inayoelezea tukio lililotokea wakati Imamu alipokuwa njia kutoka Nishapur akielekea Marwu. Hadithi hiyo inasema kwamba; Imam Ridha (a.s) alipokuwa huko Marwu, Maamuni alipanga mikutano kadhaa ya majadiliano kati ya Imamu na viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali, ambayo ilisababisha kudhihiri kwa upeo wa Imamu katika sekta ya elimu na maarifa. [115]

Imamu Jawad (a.s)

Makala Asili: Imamu Jawadi (a.s)

Muhammad bin Ali maarufu kama Imamu Jawad na Imamu Muhammad Taqi (a.s) ni Imamu wa tisa wa madhehebu ya Shia Ithnaashariyya. Yeye ni mwana wa Imamu Ali Ridha (a.s) na mama yake mzazi ni bibi Sabīqa Nuubiyya. Imamu Imamu Jawad (a.s) alizaliwa mnamo mwezi wa Ramadhani mwaka wa 195 Hijiria huko Madina. [116] na akafa mwaka wa 220 Hijiria huko Baghdad. [117] Baada kifo chake alizikwa karibu na babu yake ambaye ni Imamu wa Saba, katika “Makaburi ya Mquraish” huko Kadhimeini nchini Iraq. [118]

Imam Jawad (a.s) alichukua nafasi ya imamu akiwa na umri wa miaka minane [119] kupitia wasia wa baba yake. [120] Suala utoto wake (udogo wake kiumri) ulisababisha baadhi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kuwa na shaka juu ya Uimamu wake; baadhi yao waliamua kushikamana na kaka wa Imamu Ridha (a.s), aliye julikana kwa jina la Abdullah bin Musa, wakidhani kuwa yeye ndiye imamu. Wengine miongoni mwao walijiunga na kundi la Waaqifiyyah واقفیه”, lakini wengi wao walikubaliana na uimamu Imam Jawad (a.s). Walifanya hivyo baada ya kumjaribu na kumtahini kieleimu, pia kwa kuzingatia amri na wasia wa Imamu Ali Ridha (a.s) juu ya. [121] Kipindi cha Uimamu wake kilicho dumu kwa muda wa miaka kumi na saba, [122] kiliambatana na ukhalifa wa Maamuni na Mu'utasim. [123]

Maamun mnamo mwaka 204 Hijiria alimwita Imamu Jawad kwenda mjini Baghdad, mji ambao kwa wakati huo ulikuwa ndio mji mkuu wa ukhalifa. Alifanya hivyo kwa dhamira kumweka chini ya uangalizi wake, na kwa nia ya kumuoza binti yake aitwaye Ummul-Fadhli. [124] Baada ya muda Iamu Jawad (a.s) alirudi Madina na akaishi Madina hadi mwisho wa ukhalifa wa Maamuni. Baada ya kifo cha Maamuni, Mu'utasim alichukua mamlaka ya ukhalifa na mnamo 200 Hijiria akamwita Imamu kwenda Baghdad, na akamweka chini ya uangalizi wake. Hatimae kupitia uchochezi wa Mu’utasim Imamu Jawad (a.s) akatiliwa sumu na kuawa kupitia mkono wa mkewe. [125]

Imamu Hadi (a.s)

Makala kuu: Imamu Hadi (a.s)

Ali bin Muhammad maarufu kama Imamu Hadi au Imam Ali al-Naqi (a.s), ni Imamu wa kumi wa Mashia, Naye ni mtoto wa Imam Jawad kupitia mkewe aitwaye Samanah Maghribiyyah. Imamu Hadi (a.s) alizaliwa mnamo mwaka 212 Hijiria katika eneo linaloitwa Swaryaa karibu na mji wa Madina, [126] na aalifariki mnamo mwaka 254 Hijiria huko Samarraa [127] kupitia sumu aliyopewa na al-Mu'utazzu Billahi, Khalifa wa Banu Abbasi. [128]

Imam Hadi (a.s) alishika nafasi ya Uimamu wa Shia kwa muda wa miaka 33 (220-254 Hijiria). [129] Kipindi cha Uimamu wake kilikwenda sambamba na utawala wa Makhalifa sita wa Bani Abbasi, ambao ni; al-Mu'utasim, al-Wa'thiq, al-Mutawakkil, al-Mansur, al-Musta'inu na al-Mu'utazzu. [130]

Al-Mutawakkil alimwita Imam Hadi (a.s.) kutoka Madina kwenda Samarraa mnamo mwaka 233 Hijiria, [131] kwa nia ya kumweka chini ya uangalizi wake, [132] naye akabaki huko hadi mwisho wa maisha yake. [133] Baada ya kifo cha al-Mutawakkil; al-Mansur, al-Musta'inu na al-Mu'utazzu walichukua madaraka na Imam Hadi (a.s) aliuliwa kwa sumu katika kipindi cha ukhalifa wa al-Muu'tazzu. [134]

Imam Hadi (a.s) alitumia njia ya dua na ziara mbali mbali (sala na salamu) ili kuwafundisha na kuwafahamisha Mashia wake mafunzo mbali mbali ya dini ya Kiislamu. [135] Ziaratu al-Jamiah al-Kabirah, ni mojawapo ya dua muhimu za Mashia, zilizo pokewa kutoka kwake (a.s). [136]

Imamu Hassan Askari (a.s)

Makala asili: Imamu Askari (a.s)

Hassan bin Ali (a.s) anayejulikana kwa jina la Imamu Hassan Askari (a.s), ni Imamu wa 11 wa Mashia wanao amini Maimamu Kumi na mbili, yeye ni mtoto wa Imamu Hadi (a.s) kupitia mkewe aitwaye bibi Hadithu. Hassan bin Ali (a.s) ni mzaliwa wa Madina, aliye zaliwa mwaka wa 232 Hijiria. [138] Mwaka wa 260 Hijiria [139], Imamu Hassan Askari alipewa sumu na kuuawa kishahidi kupitia njama za ukhalifa wa Bani Abbasi. [140] Baada kifo chake alizikwa nyumbani kwake huko Samarra, karibu na kaburi la baba yake. [141]

Imamu wa 11, kwa mujibu wa maelekezo na wasia wa baba yake, alishika nafasi ya Uimamu baada ya kifo cha baba yake. Katika Uimamu wake ulio chukuwa kipindi cha miaka sita, [142] aliishi sambamba na zama za al-Muu'tazu, Muhtadi na Mu’utamidu Abbasi. [143] Imamu aliishi chini ya usimamizi na uangalizi wa makhalifa wa Banu Abbasi huko Samarraa na alifungwa mara kadhaa kwa amri yao. [144] Kulingana na usemi wa wanazuoni wengine ni kwamba; kubaki kwake mjini Samarra kwa muda mrefu kiasi hicho ilikuwa ni aina Fulani ya kuwekwa kizuizini na kuwekwa chini ya uangalizi wa khalifa wa wakati huo. Jambo hili lilimfanya aishi na makhalifa kwa mfumo wa “taqiyya” maishani mwake. 146] Kama walivyo wafanya Maimamu kadhaa wa kabla yake, naye pia alikuwa akiwasiliana na Mashia wake kupitia mtandao maalumu wa mawakala. [147] Inasemekana kwamba; shinikizo la ukali wa makhalifa wa wakati huo, kwa upande mmoja, lilitokana na ongezeko la idadi ya mashia pamoja na ongozeko la nguvu za Mashia. Kwa upande mwingine, pia uwepo wa dalili zinazo ashiria kuwepo kwa mtoto wa kiume wa Imamu wa 11, ambaye alihesabiwa kuwa ndiye Mahdi aliyeahidiwa kuja kusimamisha uadilifu, lilipelekea khofu kwa makhalifa hao na kuwafanya wawe na tahadhari zaidi. [148]

Neno Askari linatokana na neno la Kiarabu “عسکری” lenye maana ya kambi ya kijeshi. Na kwa kuwa Imamu Hassan na baba yake (Imamu Hadi) walikuwa kifungoni katika kambi ya kijeshi, hii ilipelekea Maimamu hawa kuitwa Askaraini “عسکرین” kwa maana ya wanakambi wawili, au kwa lungha nyingine ni wafungwa wawili wa kambini. [149]

Imam Mahdi (a.s)

Makala asili: Imam Mahdi (a.t.f.s)

Muhammad bin Hassan, anayejulikana kwa jina la Imam Mahdi na Imam Zaman (a.s), ni Imamu wa kumi na mbili na wa mwisho wa madhehebu ya Shia Ithna Ashari, naye ni mwana wa Imamu Askari (a.s) na mama yake ni bibi Narjis Khaatun, kwa jinsi ya vielelezo vya kihistoria, yeye alizaliwa mwezi 15 Shaban mwaka 255 Hijiria katika mji wa Sammaraa. [150]

Imamu Mahdi alichukua uongozi akiwa na umri wa miaka mitano. [151] Mtume (s.a.w.w) pamoja na Maimamu (a.s), wote kwa pamoja walithibitisha Uimamu wake. [152] Alikuwa amefichwa kutoka mbele ya macho watu hadi alipouawa baba yake mnamo mwaka 260 Hijiria. Katika kipindi chote hicho, hakuna aliyeweza kukutana naye isipokuwa baadhi tu ya watukufu wa Kishia. [153] Baada ya kuuawa kwa baba yake -kwa amri ya Mungu- alitoweka kutoka machoni mwa watu wote. Aliishi katika “Ghaiba ndogo” kwa karibu na miaka sabini. Katika kipindi hichi alikuwa akiwasiliana na Mashia kupitia manaibu wake wanne maalumu. Kwa kuanza kwa “Ghaiba kubwa” iliyo anza mnamo mwaka 329 Hijria, mawasiliano ya Shia na Imamu kupitia manaibu maalum yalimalizika. [154]

Kwa mujibu wa maelezo ya Hadithi; wakati wote wa kutokuwepo Imamu Zamani (Imamu Mahdi) (a.t.f.s), Mashia wanahimizwa na kupewa sisitizo la kusubiri zama za kudhihiri kwa Imamu wa Zama (Imamu Mahdi) (a.t.f.s). Jambo hili la kusubiri linachukuliwa kuwa ni mojawapo ya matendo bora zaidi ya amali za mwanadamu. [155] Mashia kwa kuzingatia maelezo ya Hadithi zinazo husiana na kudhiri kwake, wanaamini kwamba; [156] baada ya kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s), jamii ya Kiislamu itajawa na haki na uadilifu, na neema itaenea kila mahala. [157] Kuna Hadithi nyingi mno katika vyanzo mbali mbali, zinazo elelezea ishara na dalili za kudhiri kwa Imamu Mahdi (a.s). [158]

Hadhi na nafasi ya Maimamu wa Shia mbele Sunni

Waislamu wa madhehebu ya Sunni hawakubaliani na nadharia ya Uimamu wa Maimamu wa madhehebu ya Shia Ithna Ashari; ya kwamba wao ndiwo warithi wa bwana Mtume (s.a.w.w), [159] ila wana mahaba maalumu juu yao. [160] Kulingana na Hadithi itokayo kwa bwana Mtume (s.a.w.w), iliyosimuliwa katika vyanzo vyao, ni kwamba; watu wa Mtume walio faradhishwa kuwapenda kulingana na amri ya Aya ya Mawaddah (Aya ya mapenzi), [161] ni: Ali (a.s), Fatima (a.s), pamoja na kizazi chao. [162] Fakhru al-Din al-Razi, mfasiri na mwanafalsafa wa madhehebu ya Sunni wa karne ya sita Hijiria, ameona kuwa; Kwa mujibu wa Aya Aya ya Mawaddah, Hadithi, sala na salamu za Mtume na Aali zake katika tahiyatu ya kila sala pamoja na nyenendo (sira) za bwana Mtume (s.a.w.w), hayo yote yana ashiria ulazima wa kuwapenda kina Ali (a.s), Fatima (a.s), na kizazi chao kwa jumla. [163]

Baadhi ya wanazuoni wa madhehebu ya Sunni walikuwa na kawaida ya kuzuru makaburi ya Muimamu wa Kishia na kuomba dua pamoja na shufaa kwa jaha ya Maimamu hao. Miongoni mwa walio kuwa kawaida hiyo ni Abu Ali Khallal, mwanazuoni wa madhehebu ya Sunni wa karne ya tatu Hijiria, ambaye kwa kauli yake alisema kwamba; kila wakati alipokuwa na shida, alikwenda kutembelea kaburi la Mussa bin Ja’afar (a.s) na kumwomba msaada, na hatimae matilaba yake yalikamilika. [164] Imepokewa kutoka kwa Abu Bakar Muhammad ibnu Khuzaimah, mwanafaqihi, mpokezi Hadithi, na mfasiri wa madhehemu ya Sunni wa karne ya tatu na ya nne Hijiria kwamba; mara nyingi alikwenda kumtembelea kaburi la Imam Ridha (a.s) na heshima unyenyekevu wake kwenye kaburi hilo, liliwafanya wengine kumstaajabia. [165] Ibn Hibban, mpokezi Hadithi wa madhehebu ya Sunni wa karne ya tatu na ya nne, alisema kwamba; wakati alipokuwa mjini Tusi, kila wakati alipokuwa na shida, alikwenda kumtembelea Ali bin Musa al-Ridha (a.s) (kaburini kwake) na kuomba shida zake, na bila matilaba yake yalikubaliwa na shida zake zilitatuka. [166]

Kulingana na kauli ya bwana Ja'afar Subhani, ni kwamba; wengi wa wanazuoni wa Kisunni wamekubali mamlaka ya kidini na kitaaluma ya Maimamu wa Shia (a.s). [167] Kwa mfano, imepokewa kutoka kwa Abu Hanifa, mwanzilishi wa madhehebu ya Hanafi, akisema kwamba; sikuona mtu yeyote mwenye elimu ya sheria ya kumpindukia na kumpiku Ja'afar bin Muhammad (a.s). [168] Kauli kama hii pia imepokewa kutoka kwa Muhammad bin Muslim bin Shihab al-Zuhri, mmoja wa Taabiina (wafuasi wa Masahaba), mwanafiqhi, na mpokezi wa Hadithi wa madhehebu ya Sunni wa karne ya kwanza na ya pili ya Hijiria, kuhusiana na Imamu Sajjad (a.s). [169] Abdullah bin 'Ataa Makkiy, mmoja wa wapokezi wa Hadithi wa madhehebu ya Sunni na sahaba wa Imamu Baqir (a.s), alisema: "Sijawahi kuona wanazuoni wameporomoka mabega na kudumaa mbele ya mtu yeyote yule, kama nilivyo waona mbele ya Muhammad bin Ali (a.s). Nilimwona Hakim bin Utaiba -mmoja wa wanazuoni wakubwa wa mji wa Kufa- amekaa (amekunyaa) mbele yake kama mwanafunzi tu asiyekwa na upeo wa elimu." [170]

Bibliografia (Orodha au seti ya Vyanzo Msingi)

Makala asili: Orodha ya vitabu msingi kuhusu Maimamu wa Shia

Kuna vitabu vingi vilivyo andikwa na wafuasi wa madhehebu ya Sunni pamoja na Shia, kuuhusiana na wasifu wa Maimamu wa Shia na sifa zao mahususi. Seti ya vitabu vya Shia Miongoni mwa vitabu vya wanazuoni wa Shia kuhusu wasifu wa Maimamu na sifa zao, ifuatavyo:

  1. Dalaailu al-Imama, kitabu kilicho andikwa kwa lugha ya Kiarabu na Muhammad bin Jariri al-Tabari (aliyezaliwa mwaka 224 na kufariki 310 Hijiria), kitabu hichi ni kuhusu maisha, miujiza na wasifu za bibi Fatima pamoja na Maimamu (a.s).
  2. Al-Irshadu fi Ma'arifati Hujaji Allah 'Ala al-'Ibadi, kitabu cha kitheolojia na kihistoria kilichoandikwa kwa lugha ya Kiarabu na Sheikh Mufidu (aliyezaliwa mwaka 336 na kufariki 413 Hijiria) faqihi na mwanafalsafa wa madhehebu ya Shia. Kitabu hichi, kinahusiana historia ya maisha na wasifu za Imamu (a.s), kwa kutegemea muktadha Hadithi. Muhammad Baqir Saidi al-Khurasani alikitafsiri kitabu hiki kwa Kiajemi.
  3. Manaqibu Aali Abi Talib, kitabu cha Kiarabu kuhusu wasifu wa Maimamu kumi na nne watakatifu (a.s), kilichoandikwa na Ibnu Shahri Aashuub al-Mazaandarani (aliyezaliwa mwaka 488 na kufariki 588 Hijiria).
  4. I’lamu al-Waraa bi-A'alami al-Huda, kitabu cha lugha ya Kiarabu, kilichoandikwa na Fadhlu bin Hassan al-Tabarsi (aliyezaliwa mwaka 548 na kufariki 548 Hijiria) kuhusu maisha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (a.s) na Maimamu watakatifu (a.s).
  5. Kashfu al-Ghummah fi Ma'arifati al-Aimmah (a.s), ni kazi ya Kiarabu katika wasifu, hadhi na miujiza ya Maimamu kumi na nne watakatifu (a.s) iliyoandikwa na Ali bin Isa al-Arbily (aliyezaliwa 692 na kufariki 692 Hjiria).
  6. Rawdhatu al-Wa'idhina wa-Basiratu al-Mutta’idhina, kilichoandikwa na Fataali Nishaaburi (aliyezaliwa mwaka 508 na kufariki 508 Hijiria) kuhusu historia ya maisha ya Mtume Mtukufu (a.s) na Ahl al-Bait (a.s). Kitabu hichi kimetafsiriwa kwa Kiajemi na Mahmoud Mahdawi Daamghani.
  7. Jalaau al-‘Uyuni, kitabu cha Kifarsi (Kiajemi) kilichoandikwa na Muhammad Baqir Majlisi (aliye zaliwa mwaka 1037 na kufariki 1110 Hijiria) ambacho kimeandikwa katika sura kumi na nne kuhusu historia ya maisha ya Maimamu kumi na nne watakatifu (a.s).
  8. Muntaha al-Amaali fi Taarikhi al-Nabi wa al-Aali, kazi ya Sheikh Abbas Qomi (aliye zaliwa mwaka 1294 na kufariki 1359 Hijiri) inayozungumza kwa kina juu ya maisha ya Maimamu kumi na nne watukufu (a.s).

Vitabu vya Wasunni kuhusu maisha na sifa za Maimamu 12

Baadhi ya vitabu vya Wasunni kuhusu maisha na sifa za Maimamu 12 ni kama ifuatavyo:

  1. Mataalibu al-Sauul fi Manaqibi Aali al-Rasuuli ni kitabu cha Kiarabu kilichoandikwa na Muhammad bin Talhah Shafi'i (aliye zaliwa mwaka 582 na kufariki 652 Hijiria) ambacho kinaangazia maisha ya Maimamu 12 katika sura 12. [171]
  2. Tadhkiratu al-Khawas mina al-Aimma fi Dhikri Khasaaisi al-Aimma, kazi ya Yusuf bin Qazaoghuli anayejulikana kama Subtu bin Jawzi, mwanahistoria na mwanazuoni wa Sunni wa madhehebu ya Hanafi (aliye fariki mwaka 654 Hijiria) ameandia kitabu hichi katika sura 12 kuhusiana maisha ya Maimamu 12 na sifa zao (a.s). [172]
  3. Alfusulu al-Muhimma fi Ma’arifati al-Aimma kilichoandikwa na Ibn Sabbagh Maliki (aliye fariki mwaka 855 Hijiria), naye ni mwandishi wa madhehebu ya Sunni wa karne ya 9, ambaye amefafanua kitabuni mwake maisha na sifa za Maimamu 12. [173] Wanazuozi wengi wa Shia na Sunni wamenukuu khabari zao kutoka kitabu hiki. [174]
  4. Aimmatu Ithnaa Ashara au kwa jina jingine Sadharatu al-Dhahabiyya, kiliyoandikwa na Ibn Tuulun, mwanazuoni wa madhehebu ya Hanafi wa Damascus (aliye fariki mwaka 953 Hijiria). [175]
  5. Al-Ittihafu Bihubbi al-Asharafi, kazi ya Jamal al-Din Shabarawi (aliye zaliwa (aliye zaliwa mwaka1092 na kufariki 1172 Hijiria), ni mmoja wa wanazuoni wa Sunni mashehebu ya Shafi'i wa kutoka nchini Misri. Kitabu hichi kinazungumzia maisha ya familia ya Mtume na Maimamu 12 (a.s). [176]
  6. Nuru al-Absari fi Manaaqibi Aali Baiti al-Nabiyyi al-Mukhtari, kilichoandikwa na Muumin Shablanji, mmoja wa wanazuoni wa madhehebu ya Sunni wa karne ya 13 Hijiria, aliye andika juu ya maisha ya Mtume (s.a.w.w), Maimamu wa Shia, na Makhalifa wa Kisunni.
  7. Yanaabi’u al-Mawadda Lidhawi al-Qurbaa, ni kitabu kuhusu maisha, wasifu, na hadhi maalum za Ahl al-Bait wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), [177] kilicho andikwa na Suleiman bin Ibrahim Qanduzi (aliye fariki mwaka 1294 Hijiria) ambaye ni mwanazuoni wa ya Hanafi. [178]

Mada zinazohusiana

Vyanzo

  • Abu Dawud. Sunan. Cairo: Dar Ihya al-Sunna al-Nabawiyya
  • Ahmad b. Hanbal. Al-Musnad Ahmad. Cairo: 1313AH
  • Bukhari, Muhammad b. Isma'il al-. Sahih al-Bukhari. 1315AH
  • Hakim al-Niyshaburi, Muhammad b. 'Abd Allah al-. Al-Mustadrak 'ala al-Sahihayn. Hyderabad, 1334 AH
  • Al-Hilli, al-Hasan b. Yusuf al-. Kashf al-murad fi tajrid al-i'tiqad. Qom: Maktabat al-Mustafawi
  • Ibn Tulun, Shams al-Din Muhammad. Al-A'imma al-ithna 'ashar. ed. Munjid, Salah al-din. Beirut, 1985
  • Jawhari, Ahmad b. 'Ayyash al-. Muqtadab al-athar. Qom, 1379
  • Khazzaz al-Qumi, 'Ali b. Muhammad al-. Kifayat al-athar. Qom, 1401AH
  • Makarim Shirazi, Nasir. Payam-i Qur'an.
  • Muslim b. al-Hajjaj. Sahih Muslim. ed. Muhammad Fu'ad 'Abd al-Baqi. Cairo, 1955.
  • Najashi, Ahmad b. 'Ali al-. Rijal. ed. Musa Shubayri Zanjani. Qom, 1407AH
  • Nu'mani, Muhammad b. Ibrahim al-. Al-Ghayba. Beirut, 1983
  • Sharif al-Murtada al-. Al-Dhakhira fi 'ilm al-kalam. ed. Ahmad Husayni. Qom, 1411AH
  • Saduq, Muhammad b. 'Ali b. Babawayh al-. Al-Khisal. ed. 'Ali Akbar Ghaffari. Qom 1403 AH.
  • Tusi, Muhammad b. al-Hasan al-. Al-Tibyan fi tafsir al-Qur'an.
  • Sibt bin al-Jawzi, Yusuf. Tadhkirat al-khawas. Najaf, 1964.
  • Sulaym bin Qays al-Hilali. Kitab Sulaym bin Qays al-Hilali. ed. 'Alawi Hasani Najafi. Beirut, 1980.
  • Tabataba'i, Shi'a dar Islam. Qom: Daftar Intisharat Islami, 1383 SH.