Mwezi wa Ramadhani

Kutoka wikishia
Ramadhan Mubarak

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani (Kiarabu: شهر رمضان المبارك) ni mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiislamu ya Hijiria ambapo ndani yake Waislamu wamefaradhishiwa funga ya swaumu. Katika hadithi zimeelezwa fadhila mbalimbali za mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mwezi huu umetajwa kuwa ni mwezi wa kualikwa (kuwa katika ugeni) na Mwenyezi Mungu, mwezi wa rehema, maghufira, baraka na machipuo ya Qur’an. Kwa mujibu wa hadithi, katika mwezi huu milango ya mbinguni na ya peponi hufunguliwa huku milango ya motoni ikifungwa. Usiku wa cheo kitukufu (Laylatul-Qadr) ambapo Qur’an ilishushwa ndani ya usiku huo, unapatikana katika mwezi huu. Baadhi ya vitabu vingine vya mbinguni kama Taurati na Injili pia vilishushwa ndani ya mwezi huu mtukufu. Ramadhani ndio mwezi pekee ambao jina lake limetajwa ndani ya Qur’an. Mwezi huu unaheshimiwa sana na Waislamu na una nafasi maalumu kwa wafuasi wa dini hii. Katika mwezi huu Waislamu huzingatia zaidi masuala ya ibada, dua na kuomba maghufira. Katika vitabu vya dua kumenukuliwa na kuelezwa amali na ibada mbalimbali zinazopaswa kufanywa katika mwezi huu.

Miongoni mwa amali muhimu zaidi ndani ya mwezi wa Ramadhani ni kusoma Qur’an, kuhuisha nyusiku za Qadr, Dua, Sala, Kuomba toba na maghufira, Kufuturisha na kuwasaidia wasio na uwezo.

Miongoni mwa matukio muhimu yaliyotokea katika mwezi huu ni kushushwa Qur’ani katika usiku wa cheo kitukufu (Laylatul-Qadr) ambao ni bora kuliko miezi elfu moja, kuuawa shahidi Imam Ali ibn Abi Twalib (a.s), Imam wa Kwanza wa Waislamu wa madhehebu ya Shia tukio ambalo lilitokea mwezi wa 21 wa Ramadhani. Imamu Hassan Mujtaba (a.s) pia alizaliwa tarehe 15 ya mwezi huu.

Kufanya ibada na kufunga Swaumu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ni sehemu ya utambulisho wa Waislamu. Katika jamii za Kiislamu kuna ada, tamaduni na desturi mbalimbali kama vile kualikana, kufanya marasimu kwa pamoja, kusafisha misikiti na maeneo ya kidini, hafla za upatanishi, kupika vyakula mbalimbali vya futari katika mwezi wa Ramadhani na kadhalika.

Nafasi Yake

Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiislamu ya Hijiria[1] ambapo ni wajibu kwa Waislamu kufunga Swaumu ndani yake.[2] Qur’an tukufu.[3] na baadhi ya vitabu vya mbinguni kama kitabu cha Ibrahim, Injili, Taurati na Zaburi vilishushwa kwa Mitume katika mwezi huu wa Ramadhani.[4] Neno Ramadhani limetajwa mara moja katika Qur’an[5] na ndio mwezi pekee uliotajwa ndani ya Qur’an tukufu.[6]

Kadhalika usiku wa cheo kitukufu (Laylatul-Qadri) ambamo ndani yake ilishushwa Qur’an[7] kwa mujibu wa hadithi[8] na tafsiri[9] unapatikana ndani ya mwezi huu.[10]

Kilugha neno Ramadhani ambalo linatokana na ramadha ina maana ya joto kali la jua linalounguza.[11] Imenukuliwa kwamba, sababu ya kuitwa Ramadhani ni kuwa, Ramadhani inaunguza dhambi.[12] Aidha katika vyanzo vya hadithi Ramadhani imetajwa kuwa ni miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu.[13]

Sifa Maalumu

Katika hotuba yake ya Shabani (ya kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani) Bwana Mtume (s.a.w.w) ametaja fadhila za mwezi mtukufu wa Ramadhani ambapo baadhi ya fadhila hizo ni:

  • Katika mwezi huu watu wanaalikwa katika ugeni wa Mwenyezi Mungu.
  • Usiku wa cheo kitukufu ambao ni bora kuliko miezi elfu moja unapatikana ndani ya mwezi huu.
  • Kuhuisha na kuswali katika kila moja ya nyusiku zake ni sawa na kuswali swala za nyusiku 70 za miezi mingine.
  • Mwezi huu ni mwezi wa subira na malipo ya subira ni Pepo.
  • Mwezi wa kuliwazana.
  • Ni mwezi ambao riziki za waja zinaongezwa.

Kwa mujibu wa hadithi kutoka kwa Mtume, huu ni mwezi ambao kama thamani yake itatambuliwa, basi mtu atatamani mwaka mzima uwe Ramadhani.[14] Kwa mujibu wa hadithi mbalimbali zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w), mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kufungwa milango ya Motoni na kufunguliwa milango ya Peponi na ni mwezi ambao mashetani wamefungwa minyororo.[15]

  • Katika zama za Bwana Mtume, mwezi wa Ramadhani ulikuwa ukiitwa kwa jina la Marzuq (mruzukiwa).[16]

Vilevile katika hadithi zilizopokewa kutoka kwa Maasumina (a.s), mwezi wa Ramadhani umetajwa kuwa ni mwezi wa Mwenyezi Mungu,[17] mwezi wa rehma na msamaha wa Mwenyezi Mungu.[18] mwezi wa baraka na kuongezewa maradufu mambo mema na kufutwa Madhambi[19] na ni mwezi ambao kama mja hatasamehewa ndani yake hakuna matumaini ya kusamehewa kwake katika miezi mingine. [20]

Amali

Makala Asili: Amali za Mwezi wa Ramadhani

Mwezi wa Ramadhani una hukumu na amali makhsusi ambapo baadhi zinashirikiana na baadhi ya nyingine ni kwa ajili ya siku maalumu.

Kufaradhishwa Swaumu

Makala Asili: Swaumu

Waislamu wamefaradhishiwa funga ya Saumu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.[21] Swaumu ni kujiepusha na kufanya baadhi ya mambo kama kula na kunywa kuanzia adhana ya alfajiri mpaka adhana ya Magharibi.[22] Amri ya kufunga swaumu katika mwezi wa Ramadhani na sehemu ya hukumu zinazohusiana nayo zimekuja katika Qur’an[23] na katika vitabu vya fikihi vya Waislamu. Kwa mujibu wa fatuwa ya wanazuoni wa fikihi ni kwamba, kama mtu amesamehewa kufunga kutokana na udhuru wa kisheria aliona (kama kuwa mgonjwa au mwanamke kuwa katika ada yake ya mwezi) basi hapaswi kula mbele ya watu na kujidhihirisha.[24]

Kusoma Dua

Makala ya Asili: Dua za Masiku ya Mwezi wa Ramadhani

Kusoma dua ya daku kama dua ya al-Baha na dua ya Abu Hamza Thumali,[25] na vilevile ya dua ya Iftitah wakati wa usiku,[26] dua ya: «یا عَلِی یا عَظیمُ»، «اَللّهُمَّ اَدْخِلْ عَلی اَهْلِ الْقُبُورِ السُّرُورَ» na «اَللّهُمَّ ارْزُقْنی حَجَّ بَیتِک الْحَرامِ» Baada ya swala za wajibu[27] ni miongoni mwa amali za pamoja ndani ya mwezi huu.

Kusoma Qur’an

Makala ya Asili: Kusoma Qur’an

Katika baadhi ya hadhiti mwezi wa Ramadhani umetambulishwa kuwa ni machipuo ya Qur’an.[28] Kadhalika thawabu za kusoma Aya moja ya Qur’an katika mwezi huu ni sawa na kuhitimisha Qur’an katika miezi mingine.[29] katika baadhi ya nchi za Kiislamu kuanzia mwanzo wa mwezi huu, Waislamu husoma juzuu moja ya Qur’an kila siku na hadi kumalizika mwezi wa Ramadhani huwa wamekamilisha kusoma Qur’an yote (msahafu mzima). Uhitimishaji huu wa Qur’an hufanyika zaidi katika misikiti na maeneo mengine ya kidini na hufanyika kwa sura ya mjumuiko (kwa pamoja). Vile vile nchini Iran usomaji wa juzuu moja ya Qur’an hurushwa hewani kupitia Radio na Televisheni.

Kukesha Katika Usiku wa Cheo Kitukufu

Makala ya Asili: Laylatul Qadr

Kwa mujibu wa hadithi mbalimbali, Laylatul-Qadr inapatikana katika usiku wa tarehe 19, 21 na 23 katika Ramadhani.[30] Katika baadhi ya hadithi usiku wa kuamkia Ramadhani 23 umetajwa kuwa ndimo mnamopatikana Laylatul-Qadr.[31] Sheikh Swaduq amesema: Walimu wetu wamekubaliana kwa kauli moja kwamba, Laylatul-Qadr ni usiku wa kuamkia Ramadhani 23.[32] Allama Taabatabai anasema: Kauli mashuhuri baina ya Waislamu wa Ahlu-sunna ni kwamba, usiku Laylatul-Qadr ni katika usiku wa kuamkia Ramadhani 27.[33] Waislamu wa madhehebu ya Shia wao huhuisha na kukesha katika usiku 19, 21 na 23 za Ramadhani kila mwaka, na hubakia katika nyusiku hizi wakifanya ibada, kusoma Qur’an na kuomba dua mpaka wakati wa kula daku. Hujikusanya katika maeneo ya kidini au majumbani mwao na kukesha kwa ibada.[34] Kusoma dua ya Jawshan Kabir na kuweka msahabu kichwani ni miongoni mwa amali muhimu zinazofanyika katika nyusiku hizi tatu.[35]

Swala za Mustahabu

Makala ya Asili: Swala za Mwezi wa Ramadhani

Swala za mustahabu ni katika amali na ibada za mwezi mtukufu wa Ramadhani; baadhi ya Swala hizi zinashirikiana na zinatekelezwa na katika nyusiku zote za mwezi wa Ramadhani na baadhi yake zinatekelezwa katika siku makhsusi na maalumu.[36] Miongoni mwa Swala hizo za Sunna ni kuswali rakaa 1,000 katika nyusiku na mwezi wa Ramadhani ambapo hili limeusiwa.[37] Kuswali Swala hizo kumetambuliwa zaidi namna hii: Kuanzia usiku wa kwanza hadi wa 20 katika kila usiku rakaa 20 na kuanzia usiku wa 20 Ramadhani hadi mwisho kunaswaliwa rakaa 30 kila usiku na katika nyusiku ambazo kuna uwezekano wa kuweko Laylatul-Qadr (usiku wenye cheo kitukufu) mbali na rakaa hizo tajwa kunaswaliwa pia rakaa nyingine 100.[38] Waislamu wa madhehebu ya Kisuni wao huswali Sala za mustahabu rakaa 20 kila usiku wa mwezi wa Ramadhani ambayo inajulikana kwa jina la Sala ya tarawehe. Masuni huswali kwa jamaa Swala hii wakimfuata Khalifa wa Pili Omar ibn Al-Khattab. Waislamu wa madhehebu ya Shia wao wanasema kuwa, kuswali Swala hiyo kwa jamaa ni bidaa na uzushi.[39]

Kukaa Itikafu Katika Kumi la Mwisho

Makala ya Asili: Itikafu

Kukaa itikafu katika kumi la mwisho la Ramadhani ni mustahabu na hili ni jambo ambalo lina fadhila kubwa.[40] Kumi na mwishoni ni muda bora kabisa wa Itikafu na kufanya hivyo kumetambuliwa kuwa thawabu zake ni mithili ya Hija mbili na Umra mbili.[41] Mtume (s.a.w.w) awali alichagua kumi la mwanzo, kisha kumi na pili na hatimaye kumi la mwsho la mwezi huu wa Ramadhani kwa ajili ya Itikafu na baada ya hapo alikuwa akifanya itikafu katika kumi la mwisho la Ramadhani mpaka mwishoni mwa umri wake.[42]

Ada na Tamaduni

Katika jamii za Kiislamu kuna ada na tamaduni nyingi za mwezi wa Ramadhani.

Vitanga vya Chakula vya Futari

Makala ya Asili: Futari

Waislamu wa mataifa mbalimbali hutandika vitanga vya futari katika maeneo ya kidini na kadhalika. Waislamu hualikana majumbani mwao kwa ajili ya futari na katika maeneo ya kidini wakati wa kufuturu hugawanywa chakula cha nadhiri. Kwa mujibu wa hadithi zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume, malipo ya mtu ambaye katika mwezi wa Ramadhani atamualika muumini kwa ajili ya furati hata kama litakuwa ni fumba la maji au tende moja ni mithili ya kumuachilia huru mtumwa.

Kuamsha Watu Kula Daku

Tangazo la kuwadia wakati wa Swala na kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku ni mambo ambayo yamekuwa yakifanyika tangu kale kwa mbinu mbalimbali kama vile waadhini kuzunguka katika mitaa, kuwasha taa za chemli na kuzitundika sehemu, kugonga milango ya nyumba na kadhalika. Katika jamii mbalimbali kuna ada tofauti za kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku hasa maeneo ya vijijini. Katika maeneo ya Afrika Mashariki vikundi mbalimbali hutumia dufu na kuimba kaswida kwa ajili ya kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku. Ada na utamaduni huu wa kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku, ni mkongwe sio Afrika Mashariki tu, bali hata katika mataifa mengine ya dunia. Baadhi ya maeneo hutumia upigaji ngoma na kadhalika kwa ajili ya kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku. Kadhalika nchini Iran kabla ya adhana husomwa dua ya daku (Dua al-Baha) na kabla ya adhana husomwa minong'ono ya Rabbana ambayo hurushwa hewani na Shirika la Radio na Utangazaji la Iran na kupitia vipaza sauti vya misikitini.

Maandamano ya Siku ya Quds

Makala ya Asili: Siku ya kimataifa ya Quds

Siku ya Quds au siku ya kimataifa ya Quds ni Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Imam Ruhullah Khomeini muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tarehe 7 Agosti 1979 alitangaza rasmi Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kila mwaka kuwa, Siku ya Kimataifa ya Quds[43] na siku ya kufanya maandamano kutangaza himaya na uungaji mkono kwa wananchi madhulumu wa Palestina na ukombozi wa msikiti wa al-Aqswa[44]. Katika ujumbe wake wa kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa "Siku ya Kimataifa ya Quds", Imam Khomeini aliwataka Waislamu na wapenda haki kote ulimwenguni kujitokeza kila mwaka katika siku hii kwa ajili ya kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina na kuungana kwa ajili ya kukata mikono ya utawala haramu wa Israel unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina huku ukitenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi hao madhulumu.

Kuainisha Mwanzo na Mwisho wa Mwezi wa Ramadhani

Makala za Asili: Kuangalia Mwezi Mwandamo na Kuonekana Mwezi

Mwanzo na mwisho wa mwezi wa Ramadhani huthibitika kupitia moja ya njia zifuatazo:

  1. Kuonekana mwezi: Mtu mwenyewe auone mwezi mwandamo wa mwanzo na mwisho wa mwezi.
  2. Apate yakini kutokana na taarifa za watu.
  3. Ushahidi wa wanaume wawili waadilifu ambapo maneno ya mmoja yasikinzane na ya mwenzake.
  4. Kukamilika siku 30 za mwezi uliopita wa Hijiria.
  5. Hukumu ya mtawala wa kisheria (fakihi aliyetimiza masharti).

Baadhi ya hadithi zinasema mwezi wa Ramadhani una siku thelathini huku kundi la Maulamaa wa Kishia lilikuwa likiamini hilo; lakini mkabala na hilo, baadhi ya hadithi zinasema kuwa, mwezi wa Ramadhani kama ilivyo miezi mingine ya Hijria unaweza kuwa na siku 29 au 30. Wanazuoni mashuhuri wa fikihi wana mtazamo huu. Mwezi wa Ramadhani hufikia tamati kwa kuanza mwezi Shawwal (Mfunguo Mosi) na kutangazwa Eidul Fitr). Miongoni mwa amali za siku ya Eidul Fitr ni kutoa Zakat al-Fitr na Kuswali Swala ya Eid.

Matukio Muhimu

Makala ya asili: Matukio katika mwezi wa Ramadhani

Vitabu

Kuna vitabu vingi na tofauti tofauti vilivyoandikwa vikizungumzia mwezi wa Ramadhani. Baadhi ya vitabu hivyo ni:

  • Shahrullah fil Kitab Wasunna kilichoandikwa na Muhammad Muhammadi Reyshahri. Kitabu hiki kinatoa ripoti jumla kuhusiana na sifa maalumu, fadhila na adabu za mwezi wa Ramadhani kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'an na hadithi za Ahlul-Beiti (a.s). Kitabu hiki kimerajumiwa kwa lugha ya Kifarsi kikiwa na anuani ya Pezhuheshi Jamee Dar Baroye Mahe Mobarak Ramezan az Negahe Qur'ani va Hadis. Aidha dondoo za kitabu hiki zimechapishwa kwa anuani ya Moraghebat Mahe Ramezan.[49]
  • Dar Mahzare Mahe Mobarak Ramezan: Kitabu hiki kinazungumzia fadhila, amali, hukumu za kisheria za mwezi wa Ramadhani pamoja na minasaba katika mwezi huu. Kimeandikwa na Abul-Fadhl Sheikhi.
  • Ahamiyat Mahe Mobarak Ramezan Az Didgahe Qur'an Va Revayat" ambacho kimeandikwa na Akbar Akbarzadeh.
  • Ramezan Dar Farhang Mardom, kimeandikwa na Sayyid Ahmad Vakiliyan. Kitabu hiki ni dondoo za adabu, ada na imani ya watu wa Iran kuhusiana na mwezi wa Ramadhani.[50]

Rejea

  1. Qarasi, Qamus Qur'an, juz. 3, uk. 123, 1412 H
  2. Bastani, Farhangi Abjadi, uk. 443, 1375 S
  3. Surat Al-Baqarah: 185
  4. Kulaini, al-Kafi, juz. 2, uk. 629, 1407 H
  5. Surat Al-Baqarah: 185
  6. Qiraati, Tafsir Nur, juz. 1, uk. 285, 1388 S
  7. Surat al-qadr, aya ya 1
  8. Tazama:Kulaini, al-Kafi, 1407 H, juz. 4, uk. 66, 157 na 158
  9. Tazama: Tabrasi, Majma' al-Bayan, juz. 10, uk. 786, 1372 S
  10. Tabatabai, al-Mizan, juz. 20, uk. 334, 1390 H
  11. Raib, Mufradat al-fadhul-Quran, 1412 H, uk. 366
  12. Majilisi, Biharul-anuar,1403 H, juz. 55, uk. 341
  13. Mazandaran, Sherhul-Kafii, 1382 S, juz. 5, uk. 110
  14. Majilisi, Biharul-anuar, 1403 H, juz. 93,uk. 347
  15. Majilisi, Biharul-anuar, 1403 H, juz. 93,uk. 347
  16. Swaduq, Man la yahdhuruhu al-faqih, 1413 H, juz. 2, uk. 160
  17. Swaduq, Al-amali, 1376 S, uk. 19,
  18. Majilisi, Biharul-anuar, 1403 H, juz. 93,uk. 342
  19. Majilisi, Biharul-anuar, 1403 H, juz. 93,uk. 340
  20. Kulaini, al-Kafi,1407 H, juz. 4, uk. 66
  21. Tabatabai Yazdi, Al-urwatul-uthqa(mahsha), 1419 H, juz. 3, uk. 521
  22. Allamah Hilli, Tadzkirah al-Ulama, 1414 H, juz. 6, uk. 120
  23. surat al-Baqara, aya ya 183-185 na 187
  24. Tazama: Gulpaygan, Majmau al-masail, 1409 H, juz. 3, uk. 215
  25. Sayyied bin Twaus, Iqbal bil-amali al-hasanat, 1376 S, juz. 1, uk. 156-185
  26. Sayyied bin Twaus, Iqbal bil-amali al-hasanat, 1376 S, juz. 1, uk. 138
  27. Sayyied bin Twaus, Iqbal bil-amali al-hasanat, 1376 S, juz. 1, uk. 79-80
  28. Kulaini, al-Kafi,1407 H, juz. 2, uk. 630,
  29. Majilisi, Biharul-anuar, 1403 H, juz. 93, uk. 341
  30. Tazama: Kulaini, al-Kafi, 1407 H, juz. 4, uk. 156-160
  31. Tazama: Kulaini, al-Kafi, 1407 H, juz. 4, uk. 158
  32. Swaduq, al-khiswal, 1362 S, juz.2, uk. 519
  33. Tabatabai, Al-mizan, 1390 H, juz. 20, uk. 334
  34. Majidi Khomenei,((shabehaye qadr dar Iran)), uk. 21
  35. Majidi Khomenei,((shabehaye qadr dar Iran)), uk. 22
  36. Tazama: Qumi, Mafatihul-jinan, Nashr us'we, uk. 183, 238 na 239
  37. Qumi, Mafatihul-jinan, Nashr us'we, uk. 183 na 184
  38. Najafii, Jawahir al-kalam, Daru ihiyai turath al-arabi, juz. 12, uk. 187-189
  39. Swaqiqi, Daeshname haji wa haramein sharifein
  40. Qumi, Mafatihul=jinan, Nashr us'we, uk.234
  41. Qumi, Mafatihul=jinan, Nashr us'we, uk.234
  42. Kulaini, al-Kafi,1407 H, juz. 4, uk. 175,
  43. Swaduq, Uyun akhbar al-ridha(a.s), 1378 H, juz.1, uk. 295-297
  44. Tazama: Rahimi, ((Ramadhan))
  45. Imam Khomein, Swahife imam, 1389 S, juz.9, uk.267
  46. Imam Khomeini, Taudhihul-masail(mahsh), 1424 H, juz. 1
  47. Huru Amuli, Wasailu-shia, 1409 H, juz.10, uk. 267-274
  48. Sayyied Ibn Twaus, Al-iqbal, 1376 S, juz. 1, uk. 33-35
  49. Huru Amuli, Wasailu-shia, 1409 H, juz.10, uk. 261-268
  50. Tazama: Bahrani, Al-hadaiq al-nadhirah, 1405 H, juz. 13, uk. 270-271; Amuli, Misbahul-huda, 1380 H, juz. 8, uk. 384

Vyanzo

  • Qur'an
  • Allamah Majlisi, Muhammad Baqir, Bihār al-Anwār, Dar al-Kitab Islamiyah
  • Amuli, Mirza Muhammad Taqi, Misbāh al-Hudā fi Sharh Urwah al-Wuthqā.
  • Bahrani, Sheikh Yusuf, Al-Hadāiq al-Nadhirah, Da al-Kitab al-Islamiyah.
  • Kulaini, Muhammad bin Ya'qub, Kāfi, Dar al-Kitab al-Islamiyyah, 1407 H.
  • Mas'udi, Ali bin al-Hussein, Muruj al-Dzahab wa Ma'adin al-Jauhar, Mhakiki: Daghir As'ad, Qom: Dar al-Hijrah, Chapa ya pili, 1409 H.
  • Muhammad Rey Shahri, Shahrullāh fi al-Kitāb wa al-Sunah (Terjemah Persia: Shahr Khuda), Intisharat Dar al-Hadith.
  • Muhammad Rey Shahri, Mizān al-Hikmah, Intisharat Dar al-Hadis.
  • Najafi, Muhammad Hassan, Jawāhir al-Kalām, Intisharat Dairah al-Ma'arif Fiqh Islami.
  • Sayyied Ibnu Tawus, Iqbāl bi A'mal al-Hasanah, Intisharat Daftar Tablighat Islami.
  • Sheikh Hurr Amili, Muhammad bin Hassan, Wasāil al-Shiah, Qom: Muasasah Ali al-Bayt (a.s), 1405 H.
  • Sheikh Saduq, Muhammad bin Ali, Amāli, Nashar Saduq, 1367 H.