Sala

Kutoka wikishia
Sala ni nguzo ya dini


Sala (Kiarabu: الصلاة) ni amali muhimu zaidi ya kiibada kwa Waislamu, ambayo inajumuisha dhikri, matendo na harakati maalumu. Katika hadith mbalimbali Sala imetajwa kuwa ni “Nguzo ya Dini” na “sharti la kutakabaliwa amali zingine”. Sala ina hukumu na taratibu maalumu; miongoni mwazo ni: Inapaswa kusaliwa mtu akiwa na udhu na kwa kuelekea kibla. Pia inasaliwa kwa namna mbili, furada (kwa mtu mmoja mmoja) na kwa jamaa, na inapendekezwa isaliwe kwa jamaa.

Sala zimegawanyika katika wajibu na mustahabu:

Katika hadithi, kumeelezwa matokeo mabaya ya kuacha na kupuuza Sala ambapo, mojawapo ni kunyimwa uombezi wa Ahlul-Bayt. Kuchelewesha Sala na kutosali mwanzo wa wakati na kuswali bila ya khushui na kunyenyekea ni mifano ya kutoipa umuhimu Sala na kuichukulia kirahisi. Pia kumkumbuka Mwenyezi Mungu, kupambana na shirki na kuabudu masanamu, kuzuia ufisadi ni miongoni mwa hekima zake za wajibu.

Ibada ya Sala ipo pia katika dini zingine; hata hivyo, namna yake ya kuisali na kuitekeleza ni tofauti kulingana na sharia.

Nafasi na umuhimu

Sala ni ibada ya Waislamu, ambayo imetajwa mara 98 katika Qur'an. [1] [2] Kulingana na Aya za Qur'an, Sala ni kizuizi na kinga ya kutenda dhambi, [3] njia ya wokovu, [4] ] msaidizi katika matatizo [5] Na ni moja ya amri muhimu za Mungu kwa Manabii [6] na daghadagha na wasiwasi wa Manabii hasa kuhusu familia zao [7].

Sala ni miongoni mwa mambo muhimu ya dini ya Kiislamu [8] na pia ni ibada ambayo kwa mujibu wa fat'wa ya mafaqihi haitakiwi kuachwa kwa hali yoyote ile, [9] na kuiacha inachukuliwa kuwa ni miongoni mwa madhambi makubwa, [10] na ishara kufuru na nifaki. [11]. Katika vitabu vya Wasail al-Shia na Mustadrak, kumenukuliwa zaidi ya hadithi 11,600 kuhusu maudhui ya Sala. [12] Pia kuna sehemu katika vitabu vya fiqhi yenye anuani ya Kitab al-Salaat, ambayo ni maalumu kwa ajili ya kujadili hukumu na adabu za Sala. [13]

Kumeandiwa na kuchapishwa athari za kujitegemea kuhusiana na maudhui ya Sala ambapo, takwimu zake hadi kufikia mwaka 1376 Hijiria Shamsia takriban zilikuwa vitabu elfu mbili na mamia ya mashairi. [14] Kufikia mwaka wa 2019, kulikuwa na takriban misikiti 3,600,000 iliyokuwa imejengwa ulimwenguni. [15] Pia, katika sehemu za umma na barabara, kuna mahali palipowekwa wakfu kwa ajili ya kusali, panapoitwa chumba cha kusalia.

Kwa mujibu wa Muhammadi Rayshahri (aliyefariki 1401 Hijria Shamsia), mwanazuoni na mtafiti wa elimu ya hadithi wa Kishia, Sala ilifaradhishwa na kuwa wajibu mwanzoni mwa Utume huko Makka. [16] Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa katika kitabu cha Bihar al-Anwar, siku moja tu baada ya kupewa Utume, Mtume (s.a.w.w) alisali Sala akiwa pamoja na Imamu Ali (a.s), Mtukufu Bibi Khadija na wengine. [17]


Ibara zilizotumika katika hadithi kuhusiana na Sala

  • Nguzo ya dini; [18]
  • Wajibu wa kwanza wa Mwenyezi Mungu; [19]
  • Amali ya kwanza itakayohesabiwa; [20]
  • Wenzo wa kumkweza Muumini; [21]
  • Ishara ya imani; [22]
  • Wenzo bora kabisa wa Kujikurubisha Kwa Mwenyezi Mungu; [23]
  • Funguo ya pepo; [24]
  • Kitu cha kuwatambua Mashia wakweli; [25]
  • Wenzo wa kutakabaliwa dua; [26]
  • Wenzo wa kutoharisha roho; [27]
  • Ngome mkabala na shetani; [28]
  • Kafara ya madhambi; [29]
  • Wenzo wa kumfukuzia shetani; [30]
  • Idhinisho la kupita katika daraja la sirati. [31]

Namna ya kusali

Rakaa ya kwanza

Hali ya mwili ukiwa kwenye rukuu

Kwanza tunatia udhu, Kisha tunasimama tukiwa tumeelekea kibla na kutia nia. Kisha tunatamka takbirat al-Ihram (Takbira ya kuhirimia); yaani tunanyoosha mikono usawa wa masikio na kusema: “Allah Akbar”. Baada ya kusoma Surat al-Fatiha tunasoma sura nyingine yoyote. Baada ya hapo tunarukuu na kutaja dhikri ya rukuu na kisha tunanyanyua kichwa na kusimama wima na kisha tunasujudu. Katika sijida tunataja dhikri ya sijida na kisha tunakaa na kisha tunasujudu tena na kusoma dhikri ya sijida. [32] Dhikri inayosomwa wakati wa kurukuu ni: «سُبحانَ رَبّیَ العظیمِ و بِحَمدِه» Na Dhikri inayosomwa wakati wa kusujudu ni: «سُبحانَ رَبّیَ الاَعلیٰ وَ بِحَمدِه» au kusema: «سبحانَ‌الله». Mara tatu katika kila kipengee yaani katika rukuuu na katika sijda inatosheleza. [33]

Rakaa ya pili

Hali ya mwili ukiwa kwenye sujud

Baada ya sijida ya pili tunasimama na kufanya kama tulivyofanya katika rakaa ya kwanza, tunasoma Surat al-Fatiha na sura nyingine yeyote. Kisha tunasoam dua ya kunuti. Katika kunuti, tunanyoosha mikono yetu juu huku matumbo ya viganja vyetu vya mikono yakiwa yameelekea mbinguni na kisha kusoma dua ya kunuti. Baada ya kunuti, tunarukuu na kusoma dhikri ya kunuti. Baada ya rukuu tunasimama na kama ilivyokuwa katika rakaa ya kwanza, tunaleta sijida mbili. [34] Katika kunuti inasomwa dua hii: «رَبَّنا آتِنا فِی الدُّنْیا حَسَنَةً وَ فِی الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَ قِنا عَذابَ النَّار» au dua nyingine yeyote.

Tashahudi

Hali ya mwili ukiwa kwenye tashahud na kuelekea katika utoaji wa salamu

Baada ya sijida ya pili tunakaa na kusoma tashahudi ambayo ni: «اَشْهَدُ اَنْ لااِلهَ اِلاَّ الله وَحْدَهُ لاشَرِیكَ لَهُ، وَاَشْهَدُ اَنَّ مُحَمَداً عَبْدُهُ وَ رَسُولُه، اَلّلهُمَّ صَلِّ عَلی مُحَمَّد وَ آلِ مُحَمَّد [35]»

Salamu ya Sala

Katika Sala ya rakaa mbili baada ya tashahudi kinachofuata ni Salamu ya Sala ambayo ni: «اَلسَّلامُ عَلَیْكَ اَیُّهَا النَّبِیُّ وَ رَحْمَةُ الله وَ بَرَکاتُهُ، اَلسَّلامُ عَلَیْنا وَ عَلی عِبادِ الله الصّالِحینَ، اَلسَّلامُ عَلَیكُمْ وَ رَحْمَةُ الله وَ بَرَکاتُهُ». Na kwa salamu hiyo Sala inakuwa imemalizika. [36]

Rakaa za tatu na nne

Baada ya kusoma tashahudi tunasimama na kusoma tasbihat al-Ar’baa (tasbihi nne) ambazo ni:(سُبْحانَ الله وَ الْحَمْدُ لِله وَ لا اِلهَ اِلّا الله وَ الله أكْبَر). Na baada ya hapo tunarukuu na kisha tunasujudu. Katika Sala ya rakaa tatu, baada ya sijida ya pili ya rakaa ya tatu, tutasoma tashahudi na kisha salamu ya Sala. Katika Sala ya rakaa nne, baada ya sijida ya rakaa ya tatu, tunasimama tena na baada ya kukamisha kusoma tasbihi nne, tutarukuu na kutekeleza sijida mbili, kisha tashahudi na salamu ya Sala. [37]

Hukumu na adabu za Sala

Mambo ya wajibu katika Salama

Makala asili: Mambo ya wajibu katika Sala

Mambo ya wajibu katika Sala ni vipengee vikuu na asili vya Sala ambavyo kwa mujibu wa nadharia mashuhuri ya mafakihi ni: nia, Takriba ya Kuhirimia (Takbirat al-Iḥrām, qiyam (kusimama), kurukuu, sijida, kusoma al-Hamd na sura moja, dhikra (kama dhikr za kurukuuu na kusujudu), tashahudi, salamu, utaratibu na mfuatanisho. [38] Mambo ya wajibu katika Sala yamegawanyika mara mbili, wajibu ambazo ni nguzo na wajibu ambazo sio nguzo: Mambo ya wajibu (matano) ya Sala ambayo ni nguzo kama yataachwa kwa makusudi au kwa kukosea, yakaongezwa au kupunguzwa, Sala inabatilika. Lakini mambo sita ya wajibu ambayo sio nguzo endapo anayesali ataongeza au kupunguza kwa makusudi tu ndipo Sala yake inapobatilika. [39]

Vibatilishi vya Sala

Sala inabatilika kwa moja kati ya mambo yafuatayo:

  • Hadath kubwa (Kila kinachosababisha ghusl-kuoga-) au hadath ndogo (kitu kinachotengua udhu).
  • Kugeuka sana kutoka kwa muelekeo wa Kibla.
  • Kuzungumza kwa makusudi;
  • Kucheka kwa makusudi na kwa sauti;
  • Kufunga mikono, nako ni kuuweka mkono mmoja juu ya mwingine wakati wa hali ya kisimamo kwenye Sala;
  • Kulia kwa makusudi kwa ajili ya jambo la kidunia; [40]
  • Kusema: Aaamin’ baada ya kumaliza kusoma Surat al-Fatiha.
  • Kufanya mambo ambayo yanavuruga Sala; kama vile kurukaruka na kupiga makofi;
  • Kula na kunywa;
  • Kutilia shaka katika idadi ya rakaa za mbili au rakaa tatu au rakaa mbili za mwanzo katika Sala yenye rakaa nne.
  • Kuongeza au kupunguza nguzo miongoni mwa nguzo za Sala kwa makusudi au kwa kusahau au kuongeza au kupunguza kwa makusudi wajibu ambao si nguzo katika Sala. [41]

Hukumu zingine

  • Tohara: Ni wajibu kutia udhu kwa ajili ya sala za wajibu. [42] Katika baadhi ya wakati, badala ya udhu inapaswa kufanya tayamamu; kama inapotokea maji yamekosekana, maji kuwa na madhara kwa mtu (akitia udhu kwa maji ataumwa) na muda kuwa finyu. [43]
  • Mahali pa kusalia: Kumebainishwa masharti kadhaa kuhusiana na mahali pa kusalia na miongoni mwayo ni: Pasiwe pa kughusubu (pasiwe pametikana kwa kunyanganya), iwe sehemu iliyotulia (isiwe na mtikisiko), pasiwe na najisi, sehemu ya kuweka paji la uso (kwa ajili ya kusujudu) isiwe juu au chini zaidi ya sehemu ya kuweka magoti kwa kiwango cha zaidi ya vidole vinne. [44]
  • Nguo ya mwenye kusali: Nguo ya mwanaume mwenye kusali inapasa kusitiri tupu mbili (ya mbele na ya nyuma) na nguo ya mwanamke mwenye kusali inapasa kufunika mwili wake wote; hata hivyo sio lazima kwa mwanamke wakati wa kusali kufunika mduara wa uso wake, mikono na miguu mpaka kwenye viganja. [45]
  • Sala inapasa kusaliwa ilihali mtu ameelekea kibla (Kaaba). [46]
  • Sala ya kupunguza: Mtu aliyeko safarini anapaswa kupunguza rakaa za Sala za rakaa nne na kusali rakaa mbili badala ya rakaa nne. [47] Kuna masharti ambayo yanapasa kutimia ili kuhesabika safari yake ya kisheria; miongoni mwayo ni: Majimui ya masafa ya kwenda na kurudi kwa akali yawe farsakh nane kisheria (baina ya kilomita 40 hadi 45). [48]

Adabu za Sala

Kuna adabu na mambo ya mustahabu ya Sala ambayo yamebainishwa na baadhi ya hayo ni: Kuswali mwanzo wa wakati, kujipamba wakati wa Sala, kuswali msikitini na kwa jamaa, kuomba dua mwanzoni mwa Sala, kuwa na mahudhurio ya moyo na kuwa na unyenyekevu.[49] Baada ya Sala pia kuna amali na matendo ya kufanya ambayo yamebainishwa ambayo yanafahamika kama taaqibat (yanayofuata); kama vile, kusoma Ayat al-Kursi, kukariri tasbihat Zahra (as) na kusujudu sijida ya shukr (kushukuru).[50] Baadhi ya vitendo hivi pia vimetajwa katika kitabu cha Mafatih al-Jinan. [51]

Sala za wajibu na mustahabu

Makala asili: Sala za wajibu

Sala aza wajibu ni Sala ambazo ni wajibu kuzisali na kama hazitasaliwa kwa muda wake maalumu, huwa wajibu kulipa kadhaa. Sala hizo ni:

  1. Sala za kila siku: Rakaa 17 na katika nyakati tano (alfajiri, adhuhuri, alasiri, magharibi na Isha) na Sala hizo zinafahamika kwa majina hayo;
  2. Sala ya Majanga: Hii ni Sala ambayo huwa wajibu kuisali wakati kunapotokea baadhi ya matukio ya kimaumbile kama vile tetemeko la ardhi, kupatwa kwa jua (kusuf) na kupatwa kwa mwezi (khusuf);
  3. Sala ya maiti: Hii ni Sala ambayo husaliwa jeneza la Mwislamu kabla ya kuzikwa kwake, na haijuzu kuzika maiti ya Mwislamu pasi na kuisalia;
  4. Sala ya Tawafu: Sala hii husaliwa baada ya kumaliza kutufu Kaaba(kuzunguka);
  5. Sala ya kuwalipia deni wazazi wawili (qadhaa) ambayo ni wajibu kwa mtoto mkubwa wa kiume;
  6. Sala ambayo imekuwa wajibu kwa sababu ya nadhiri, kiapo na kadhalika. [52]

Sala za mustahabu

Makala asili: Sala za mustahabu

Sala za mustahabu au nafila, ni Sala ambazo sio wajibu kuzisali; pamoja na hayo imekokotezwa na kupendekezwa kuzisali; kama Sala za nafila za kila siku na Sala ya usiku. [53] Sala zote za mustahabu zina rakaa mbili isipokuwa Sala ya Witiri. [54]

Matokeo ya kutoipa umuhimu Sala

  • Kukosa uombezi wa wa Ahlul-Bayt (a.s): [55] Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa na Abi Basir ni kwamba, Imam Swadiq (a.s) alipokaribia kuaga dunia, aliwakusanya watu wake wa karibu na kusema: Hatopata uombezi wetu mtu ambaye anaipuuza Sala. [56]
  • Kukumbwa na mambo 15: Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Mtume (saww) akimhutubu bintiye Fatima Zahra (a.s) ni kwamba, mtu ambaye anaichukulia wepesi Sala na haipi umuhimu, Mwenyezi atamfanya akumbwe na mambo 15. [57]
  1. Umri wake kutokuwa na baraka;
  2. Kutokuwa na baraka mali yake;
  3. Kutokuwa na ujira amali;
  4. Usowa wake kukosa nuru;
  5. Kutojibiwa dua zake;
  6. Kifo cha madhila;
  7. Kutonufaika na dua za wengine;
  8. Kufa na njaa;
  9. Kufa na kiu kwa namna ambayo kadiri anavyokuja maji kiu chake hakikatiki;
  10. Kuteswa na Malaika kaburini;
  11. Giza kaburini;
  12. Kubanwa na kaburi;
  13. Siku ya Kiyama, Malaika atamvuta usoni na viumbe vitatazama;
  14. Hesabu kali siku ya Kiyama;
  15. Mwenyezi Mungu hatamtazama kwa jicho la rehma (huruma) na atakuwa na adhabu ya kuumiza. [58]

Kuchelewesha Sala na kutoisali mwanzo wa wakati bila ya udhuru [59] na kusali bila ya khushui (unyenyekevu) ni miongoni mwa mambo ambayo yametajwa kuwa mifano ya wazi ya kuipuuza Sala na kutoipa umuhimu. [60] Kwa ajili ya taarifa na maelezo zaidi, angalia hapa pia: Tarik al-Salah (asiyesali).

Hekima na wajibu wa Sala

Katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Ridha (a.s) imeelezwa kuwa, falsafa ya kuwajibishwa Sala ni kukiri juu ya Umola wa Mwenyezi Mungu, kupamabana na shirk, na kuabudu masanamu, kuonyesha udhalili mja mbele ya adhama ya Mwenyezi Mungu, kupambana na mghafala, kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu, kuzuia ufisadi, kutenda dhambi, kutotii amri na kadhalika. [78] Katika tafsiri ya Nemooneh pia imeelezwa kwamba, kuimarisha moyo wa nidhamu, kulingania usafi na utakasifu, kulea fadhila za kimaadili, kuzipa thamani amali zingine na kusamehewa madhambi kuwa ni katika hekima za kuwa wajibu Sala.

Kadhalika katika Aya:((وَأَقِمِ الصَّلَاةَ لِذِكْرِي ; na ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi)) [80] Imeeleza na kubainisha lengo la Sala kwamba, kumkumbuka na kumtaja Mwenyezi Mungu. [81] Imenukuliwa kutoka kwa Bibi Fatima Zahra (a.s) ya kwamba: Mwenyezi Mungu amewajibisha Sala ili waja wawe mbali na kiburi (takaburi). [82] Katika Nahaj al-Balagha imekuja pia kwamba, Sala inabomoa na kusambaratisha kiburi na hali ya kujiona. [83]

Bibliografia

Kumeandikwa na kutarjumiwa athari na vitabu mbalimbali na kwa lugha tofauti kuhusiana na maudhui ya Sala. [87] Baadhi ya athari hizo ni:

  • Adab Namaz, mwandishi: Imam Khomeini: Kitabu hiki kinabainisha adabu za kinyoyo na siri za kimaanawi za Sala na kina utangulizi wa kwanza na wa pili ambapo mwandishi ameandika akiwahubu watoto wake.
  • Asrar al-Salah, mwandishi Mirza Jawad Malaki Tabrizi: Kitabu hiki kinahusiana na malezi, mahudhurio ya moyo na utambuzi wa Sala.
  • Asrar Namaz, mwandishi Imamu Khomeini: Tafsiri ya Kiirfani ya Sala, kuanzia adhana mpaka tashuhudi na kutoa salamu ya kumaliza Sala.
  • Al-Salat fil al-Kitab wal-Sunnah, mwandishi Muhammad Muhammadi Rayshahri: Kitabu hiki kinajumuisha na kuzungumzia Aya za Qur’an, hadithi zilizopokewa na Mashia na Masuni kuhusiana na ulazima wa Sala, hekima yake, Sala kabla ya Uislamu, ubora wa Sala, sifa zake maalumu, nyakati za Sala, adabu zake na kadhalika.
  • Raazihaye Namaz, mwandishi Abdallah Jawad Amoli: Kitabu hiki ni mtazamo wa Kifalsafa kuhusiana na Sala na hukumu zake.

Vyanzo

  • Abū l-Futūḥ al-Rāzī, Ḥusayn b. ʿAlī. Al-Tafsīr al-kabīr. Mashhad: Āstān-i Quds-i Raḍawī, 1408 AH.
  • Āmadī, ʿAbd al-Wāḥid Muḥammad al-. Ghurar al-Ḥikam. Tehran: Dānshgāh-i Tehran, [n.d].
  • Amīn, Muḥsin al-. Aʿyān al-Shīʿa. Beirut: Dār al-Taʿāruf, 1403 AH.
  • Ḥarrānī, Ḥasan b. ʿAlī al-. Tuḥaf al-ʿuqūl. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1363 Sh.
  • Ḥurr al-ʿĀmilī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Wasāʾil al-Shīʿa. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1409 AH.
  • Imām Khomeinī. Tawḍīh al-masāʾil. Edition 8. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1424 AH.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1362 Sh.
  • Mughnīya, Muḥammad Jawād al-. Al-Fiqh ʿalā al-madhāhib al-khamsa. Beirut: Dār al-Jawād, 1421 AH.
  • Muḥammadī Reyshahrī, Muḥammad. Al-Ṣalāt fī al-Kitāb wa al-sunna. Translated to Farsi by ʿAbd al-Hādī Masʿūdī. First edition Qom: Dār al-Ḥadīth, 1377 Sh.
  • Muḥammadī Riyshahrī, Muḥammad. Mīzān al-ḥikma. Qom: Dār al-Ḥadīth, [n.d].
  • Muttaqī al-Hindī, ʿAlī al-. Kanz al-ʿummāl. Hyderabad: Dāʾirat al-Maʿārif al-ʿUthmānīyya, 1364 AH.
  • Nūrī, Mīrzā Ḥusayn al-. Mustadrak al-wasāʾil. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1407 AH.
  • Nurūzī, Muḥammad Masʿūd. Muqaddamaʾī bar falsafa-yi namāz. Tehran: Intishārāt Bayn al-Milalī-yi Yādāwarān, [n.p].
  • Pāyanda, Abū l-Qāsim. Nahj al-faṣāḥa. [n.p]: Dār al-ʿilm, 1387 Sh.
  • Rāwandī, Saʿīd b. Hibat Allāh. Shihāb al-akhbār. Qom: Dār al-Ḥadīth, 1388 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Khiṣāl. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1362 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Man lā yaḥḍuruh al-faqīh. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1367 Sh.