Mutawakkil Abbasi

Kutoka wikishia

Mutawakkil Abbasi (207-247 Hijria) alikuwa khalifa wa 10 wa utawala wa ukoo wa Bani Abbas ambaye aliingia madarakani 232 Hijria na katika kipindi chote cha utawala wake kilisadifiana na Uimamu wa Imam Hadi (as). Mutawakkil Abbasi alikuwa adui wa Ahlul-Beiti (as) na alikuwa akiwafanyia uadui, dhihaki na masihara. Mwaka 236, kaburi la Imam Hussein (as) lilibomolewa kwa amri ya Mutawakkil na sehemu yake ikafanywa shamba. Hatua hiyo ilikabiliwa na malalamiko ya wananchi. Mwaka 233 Hijria, Imam Hadi (as) aliitwa Samarra baada ya watu kuelekea kwake na kuwasema vibaya watu waliokuwa wakiteuliwa na Mutawakkil na kubakia huko hadi mwishoni mwa umri wake. Watafiti wa masuala ya kihistoria wanasema kuwa, kidhahiri Mutawakkil alikuwa akimheshimu; lakini daima alikuwa akimdunisha na na kufanya njama dhidi yake. Kwa mujibu wa mtazamo wa watafiti ni kwamba, katika kipindi cha utawala wa Mutawakkil, Waislamu wa Kishia walikumbana na masaibu mengi. Wengi miongoni mwao waliuliwa au walifungwa jela. Kadhalika kwa amri ya Mutawakkil, Alawiyun (watu kutoka katika kizazii cha Imam Ali as) walikabiliwa na mashinikizo mengi ya kiuchumi. Mwakak 234 Hiijria, kwa amri ya Mutawakkil, madhehebu ya kiteolojia ya Ahlul-Hadith ikawa madhehebu rasmi ya utawala na itikadi zao kama uwezekano wa kumuona Mwenyezi Mungu na kwamba, Qur'ani haijaumbwa zikaenea. Mutawakkil kinyume na Ma'mun na Mu'tasim Abbasi alifanya juhudi za kukabiliana na kundi la Mu'tazilah na akaweka kanuni na sheria kali kwa Ahlu-Dhimma (Ahlul-Kitab wanaoishi katika nchi za Kiislamu ambao wanapaswa kulipa kodi). Mutawakkil aliingia madarakani akisaidiwa na Waturuki na kwa mujibu wa wahakiki, baada ya kushika kwake hatamu za uongozi, zama za upenyaji na kuwa na ushawishi Waturuki katika utawala wa Kiislamu zikaanza. Awali Mutawakkil alikuwa na uhusiano mzuri na Waturuki; lakini baada ya kuona nguvu yao inaongezeka siku baada ya siku akahisi hatari na hivyo akaamua kukabiliana nao. Kushadidi na kushika kasi hasama na uadui baina ya Waturuki na Mutawakkil, kila upande ukafanya njama dhidi ya upande mwingine. Hatimaye Mutawakkil aliuawa na mwanawe Muntasir Abbasi kwa msaada wa Waturuki. Kuuawa kwake kukawa mwanzo wa kuporomoka nguvu za utawala wa Bani Abbas na kuanguka. Historia inaonyesha kuwa, Mutawakkil alikuwa na mapenzi makubwa na suala la kujenga makasri na majengo ya kifahari na alikuwa akitumia gharama kubwa katika ujenzi huo. Msikiti wa Jamia wa Samarra (Masjid Jami'u Samarra) ni katika mabaki ya majengo yake katika zama hizo.

Utambulisho jumla

Ja'far bin Mu'tasim mashuhuri kwa jina la Mutawakkil Abbasi ni mtoto wa Mu'tasim Abbasi (utawala wake: 218-227 Hijria) na ni mjukuu wa Harun al-Rashid (alitawala:170-193 Hijria). Huyu ni khalifa wa 10 katika mlolongo wa makhalifa kutoka katika ukoo wa Bani Abbas. [1] Alizaliwa 207 Hijria. [2] Mwaka 227 Hijria aliteuliwa na kaka yake Wathiq, mtawala wa Kiabbasi kuwa Amirul-Haj (kiongozi na msimamizi wa Mahujaji). [3] Baada ya kuaga dunia Wathiq mwaka 232 Hijria, Ja'far biin Mu'tasim akiwa na umri wa miaka 36 aliteuliwa na makamanda wa Kituruki na shakhsia wakubwa katika utawala wa Kiabbasi kuwa Khalifa na kisha akaitwa kwa jina la al-Mutawakkil ʿalā Allāh kufuatia pendekezo lililokuwa limetolewa na Ahmad bin Abi Dawud. [4] Inaelezwa kuwa, hii ilikuwa mara ya kwanza katika historia ya Uislamu kwa Waturuki kuingilia suala la kuchagua Khalifa na walifanikiwa kumuweka madarakani mtu waliyemkusudia. [5] Ni kutokana na hilo ndio maana baadhi ya waandishii wanakitambua kipindi cha kuanza uongozi na ukhalifa wa Mutawakkil kwa zama za kuanza upenyaji na ushawishi wa Waturuki; [6] zama ambazo zilianza sambamba na ukhalifa wa Mutawakkil ziliendelea mpaka mwaka 334 Hijria. [7] Mutawakkil anatambulishwa kuwa khalifa mmwagaji damu, dhalimu na alikuwa mstari wa mbele katika kunywa pombe na kushiriki katika vikao vya ufuska na dhambi. [8] Kwa mujibu wa utabiri wa Imam Ali ibn Abi Twalib (as), khalifa wa 10 wa Bani Abbasi yaani Mutawakkil ni kafiri zaidi miongoni mwao. [9]

Uadui dhidi ya Ahlul-Bayt (as)

Mutawakkil Abbasi alikuwa na chuki na uadui sana dhidi ya Ahlul-Bayt (as) hususan Imam Ali ibn Abi Twalib (as). [10] Abul-Faraj Isfahani anasema, Mutawakkil alikuwa mstari wa mbele zaidi katika kuamiliana vibaya na watu wa kizazi cha Imam Ali (as) kuliko makhalifa wote wa Bani Abbasi; kiasi kwamba, alifikia hatua ya kubomoa kaburi la Imam Hussein (as) [11] Mutawakkil alikuwa akimuua kiila mtu aliyemdhania kuwa ni mfuasi na mwenye kumpenda Ali na kizazi cha Ali na alikuwa akipora mali zake. [12] Dhahabi mmoja wa waandishi wa historia wa karne ya 8 Hijria anasema, Mutawakkil alikuwa Naswibi (mtu mwenye kumfanyia uadui Imam Ali (as) au mmoja wa Ahlul-Bayt a.s) na hakuna tofauti yoyote ya kimtazamo kuhusiana na hili. [13] Mutawakkil alikuwa akikaa pamoja na maadui wengine wa Ahlul-Bayt (as) kama Ali ibn Jaham, Omar ibn Faraj na ibn Utrujah [14] ambao walikuwa wakisema maneno mabaya mno dhidi ya Imam Ali (as). [15] Mutawakkil Abbasi alikuwa na mfanyakazi ambaye alikuwa akimshabihisha na Imam Ali (as) na kisha huanza kumfanyia dhihaki na masihara. [16] Kwa mujibu wa nukuu ya Khatib Baghdadi, mwanahistoria wa karne ya 5 Hijria, Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Nasr bin Ali alinukuu hadithi kuhusu fadhila za Imam Hassan na Hussein (as) mbele ya Mutawakkil na Mutawakkil akadhani kwamba, bwana huyo ni Mshia, hivyo akatoa amri atandikwe viboko 1000. [17] Nasr bin Ali alitandikwa viboko mtawalia mpaka kukapatikana ushahidi wa kuthibitisha kwamba ni Suni, ndipo Mutawakkil alipotoa amri ya Bwana yule kuachwa kutandikwa viboko. [18]

Kubomoa Haram ya Imam Hussein (as)

Makala asili: Kubomolewa Haram ya Imam Hussein (as)

Mwaka 236 Hijria Mutawakkil Abbasi alitoa amri ya kubomolewa kaburi la Imam Hussein ibn Ali (as). [19] kwa muktadha huo, athari zote zilizokuwako kando kando ya kaburi hilo zikatokomezwa; lakini hakuna mtu aliyechukua hatua ya kubomoa kaburi la Imam Hussein mpaka Mayahudi walipopewa jukumu la kubomoa kaburi hilo. [20] Baada ya kubomoa makaburi wakachimba ardhi hiyo na kisha kuifanya mashamba [21] na wafanyaziara wakawa wakifuatiliwa. [22] Inaelezwa kuwa, Mutawakkil alichukua hatua mara mbili ya kubomoa kaburi la Imam Hussein (as); mara ya kwanza mwaka 233 Hijria na mara nyingine mwaka 236 Hijria. Katika kipindi hiki jengo la Haram lilikuwa limefanyiwa ukarabati. Ubomoaji wa mara ya pili ulikuwa mkubwa zaidi. [23] Kubomolewa Haram ya Imam Hussein (as) kuliwakasirisha mno Waislamu; kiasi kwamba, wakazi wa Baghdad waliandika nara dhidi ya Mutawakkil katika kuta za misikiti na washairi wakawa wakitunga beti zx mashairi za kumkejeli na kumdhalilisha. [24]


Kuitwa Samarra Imam Hadi (as)

Mwaka 233 Hijria, Mutawakkil Abbasi alimlazimisha Imam Hadi (as) atoke Madina na kwenda Samarra. [25] Sheikh Mufid mmoja wa mafakihi na mwanateolojia wa Shia Imamiya amesema kuwa, tukio hilo lilitokea mwaka 243 Hijria; [26] hata hivyo Rasul Ja’fariyan, mtafiti wa masuala ya historia ya Kiislamu anaitambua tarehe hiyo kwamba, si sahihi. [27] Inaelezwa kuwa, sababu ya kitendo hicho cha Mutawakkil ni hatua ya gavana na mtawala wa Madina Abdallah ibn Muhammad [28] na Buraihah Abbas Imam wa Swala ya Jamaa wa Haram mbili aliyeteuliwa na Khalifa cha kutoa maneno mabaya dhidi ya Imam Hadi (as) [29] na kadhalika ripoti mbalimbali zilizokuwea zikionyesha kuelekea watu kwa Imam Hadi (as). [30] Katika barua yake kwa Mutawakkil, Imam Hadi alikataa kuweko maneno mabaya dhidi yake; [31], hata hivyo katika jibu la barua yake kwa Imam Hadi, Mutawakkil alimtaka kwa heshima Imam Hadi (as) afunge safari na kuelekea katika mji wa Samarra. [32] Maandiko ya barua ya Mutawakkil yametajwa katika vitabu vya al-Kafi na al-Irshad. [33] Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana Yahya bin Harthama akapewa jukumu na Mutawakkil Abbasi la kumhamshia Imam Hadi (as) katika mji wa Samarra. [34] Imenukuliwa kutoka kwa Yahya ibn Harthama ya kwamba, wananchi wa Madina baada ya kusikia amri hiyo ya Mutawakkil, walifadhaika sana, wakaomboleza na kupiga mayowe ambapo kabla ya hapo, mji wa Madina haukuwahi kushuhudia hali kama hii. [35] Imam Hadi (as) akiwa katika mji wa Samarra kidhahiri alikuwa akiheshimiwa na Mutawakkil, lakini kimsingi Mutawakkil alikuwa akifanya njama dhidi ya Imam huyo [36] ili adhama na heshima ya watu kwa Imam huyo ipungue. [37] Daima Mutawakkil alikuwa akimdunisha na kumdhalilisha Imam Hadi (as). [38] Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa na Sayyid Ibn Tawus katika kitabu cha Muhaj al-Da’wat ni kwamba: Wakati wa kutokea moja ya udunishaji na udhalilishaji huu, Imam Hadi (as) alisoma dua ya madhulumu dhidi ya dhalimu na baada ya siku tatu Mutawakkil akauawa. [39]

Hali ya Mashia

Mutawakkil alikuwa akiwafanyia uadui Mashia kidhahiri kabisa na bila kificho na alikuwa akiwapatia zawadi watuiwaliokuwa wakiwasema vibaya Mashia. [40] Kutokana na chuki kubwa aliyokuwa nayo dhidi ya Mashia, alikuwa akiwasema vibaya makhalifa waliuotangulia ambao walikuwa wapole kwa Mashia. [41] Ardhi ya Fadak ambayo walirejeshewa watu wa familia ya Ali bin Abi Twalib katika zama za khalifa Ma’um, ilichukuliwa tena katika zama za utawala wa Mutawakkil. [42] Mutawakkil alikuwa akiwakamata na kuwatia jela wafuasi wa madhehebu ya Shia na alilifanya hilo kwa wigo mpana sana na aliwaua wengi miongoni mwao. [43] Mutawakkil alitoa amri ya kutiwa mbaroni Yahya bin Omar mmoja wa wajukuu wa Zayd bin Ali na akapigwa na kuadhibiwa. [44] Kadhalika Hassan bin Zayd, mashuhuri kama mhubiri na mlinganiaji mkubwa katika zama za Mutawakkil aliomba hifadhi ya ukimbizi Tabarestan na Deylam. [45] Aidha watu wa ukoo wa Abi Twalib walifukuzwa Misri kwa amri ya Mutawakkil. [46] Kwa mujibu wa ripoti ya Abul Faraj Isfahani, watu wa familia na ukoo wa Abi Twalib walitawanyika na kuishi katika maeneo tofauti katika zama za utawala wa Mutawakkil na walikuwa wakiishi maisha ya kujificha [47] ambapo miongoni mwao ni Ahmad bin Issa bin Zayd ambaye aliaga dunia katika kipindi hicho. [48] Waislamu wa madhehebu ya Shia walikabiliwa na hali mbaya katika zama za utawala wa Mutawakkil Abbasi katika hali ambayo, katika zama za makhalifa watatu wa kabla yake yaani Ma’mun, Mu’tasim na Wathiq Abbasi walikuwa na uhuru wa kiwango fulani. [49] Licha ya uadui mkubwa wa Mutawakkil Abbasi dhidi ya Mashia, lakini baadhi ya Mashia walifanikiwa kupenya na kuingia ndani ya utawala wake. Miongoni mwao ni Ibn Sikkit ambaye alikuwa ndani ya utawala wa Mutawakkil [50] ambapo alikuwa na jukumu la kuwalea watoto wa Mutawakkil. [51]

Hatua zilizochukuliwa na Mutawakkil

Yaqut al-Hamawi mwanajiografia wa karne ya 7 Hijria anasema kuwa, Mutawakkil alikuwa na mapenzi makubwa ya kujenga makasri na majengo ya kifahari kwa namna ambayo hakuna Khalifa aliyejenga majengo na makasri kama yeye. [52] Katika kitabu cha Maathar al Kubaraa fi Tarikh Samarra kumetajwa orodha ya majina ya makasri zaidi ya 30 ambayo Mutawakkil alijenga huko Samarra kwa ajili yake (ukiacha makasri aliyowajengea watu wake wa karibu). [53] Inaelezwa kuwa, Mutawakkil alitumia karibu dirihamu milioni 300 kwa ajili ya kujenga majengo na makasri hayo. [54] Alitoa amri ya kujengwa msikiti wa Jamia (msikiti mkuu) huko Samarra. [55] Ibn Jawzi mwandishi wa historia wa karne ya 6 Hijria anasema kuwa, ujenzi wa msikiti huo ulianza mwaka 234 Hijria na kukamilika baada ya miaka mitatu yaani mwaka 237 Hijria na kwamba, uligharimu kiasi cha zaidi ya dinari 380,000. [56]. Msikiti huu unatambuliwa pia kwa jina la Jami’u al-Mutawakkil, kama ambavyo umeondokea pia kuwa mashuhuri kwa jina la Jami’u Malawiyah. [57] Hii leo mabaki ya msikiti huu yanaonekana umbali wa kilomita moja kutoka katika mji wa Samarra. [58].

Kuwapendelea Ahlul-Hadith

Mwaka 234 Mutawakkil Abbasi alitoa amri ya kuenezwa madhehebu ya Ahlul-Hadithi [59] kama ambavyo alitoa agizo la madhehebu hiyo kuwa ndio madhehedbu rasmi ya utawala. [60] Kinyume na makhalifa wa kabla yake [61], Mutawakkil alikuwa akikabiliana na kundi la Mu’tazilah na alitoa amri kwa wanateolojia kuzungumzia suala la uwezekano wa kumuona Mwenyezi Mungu. [62] Mutawakkil alipiga marufuku itikadi ya kwamba, Qur’ani imeumbwa [63] na na aliwachilia huru watu wote waliokuwa wamefungwa jela na mtawala wa kabla yake yaani Wathiq Abbasi kwa kosa la kutoamiani kwamba, Qur’ani imeumbwa [64] ambapo miongoni mwao alikuwemo Ahmad bin Hanbal. [65]

Mashinikizo dhidi ya Ahl al-dhimma (wasiokuwa Waislamu)

Mwaka 235 Hijria, mtawala Mutawakkil aliweka sheria kali dhidi ya ahl al-dhimma (wasiokuwa Waislamu). [66] Kupiga marufuku kuvaa mavazi ya Waislamu, ulazima wa kuvaa mavazi kama ya wakulima, kushona kitambaa ambacho kinatofautiana na kilemba, kupiga marufuku kupanda farasi, kupiga marufuku kuwaajiri ahl al-dhimma katika kazi za serikali na utawala, kuchukua kodi kutoka kwao, kubomoa makanisa mapya na kusawazisha makaburi yao na ardhi ni miongoni mwa maagizo yaliyotolewa na Mutawakkil. [67] Jurji Zaydan, mwandishi wa kitabu cha Tarikh al-Tamaddun al-Islami anasema: Muamala huu wa Mutawakkil na Ahl al-Dhimma ulitokana na kuwa pamoja Wakristo wa Homs na Waislamu katika uasi dhidi ya gavana wa mji wa Homs. [68] Licha ya kuweko mashinikizo yasiyo na kifani ya Mutawakkil dhidi ya Ahl al-Dhimma, lakini baadhi ya wasomi na wanazuoni wa Kikristo akiwemo Hunayn bin Is’haq (tabibu na mnajimu) alikuwa akihudumu katika vyombo vya utawala wa khalifa Mutawakkil. [69]

Makabiliano na Waturuki

Mutawakkil ambaye aliingia madarakani kwa msaada wa Waturuki, awali alifanya mambo ya kuwaridhisha Waturuki na akawapa nguvu ya kufanya mambo ya kisiasa; lakini baada ya muda aliweka kando mbinu hiyo na akafanya hima ya kubana nguvu na mamlaka ya Waturuki. [70] Mutawakkil alichukua hatua ya kuwatangaza watoto wake watatu, Muhammad, Abu Abdallah na Ibrahim kuwa warithi wa kiti cha utawala; Muhammad akawa mrithi wa khalifa wa Kiabbasi kwa lakabu ya Muntasir, Abu Abdallah akiwa na lakabu ya Mu’tazz akawa mrithi wa kiti cha utawala cha Muntasir na Ibrahim akiwa na lakabu ya Muayyid akawa mrithi wa kiti cha utawala cha Mu’tazz. [71] Utawala wa Afrika na Magharibi akapatiwa Muntasir, Khorasan na Rey akapewa Mu’tazz huku utawala wa Sham na Palestina ukikabidhiwa kwa Muayyid. [72] Muhammad Suhail Thaqqush, mwandishi wa kitabu cha Tarikh al-Dawlah al-Abbasiyah anasema, hatua hii ya Mutawakkil ilifanyika katika fremu ya kudhoofisha nguvu, mamlaka na upenyaji wa Waturuki ambao katika zama za ukhalifa wa Mu’tasim na Wathiq Abbasi walikuwa wakidhibiti maeneo ya ardhi zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Bani Abbas. [73] Thaqqush anaamini kuwa, Waturuki ambao walikuwa na habari kuhusiana na uamuzi wa Mutawakkil wa kupunguza nguvu na ushawishi wao, walifanya njama nyingi na ni kwa sababu hiyo Mutawakkil akiwa na lengo la kuepukana na njama zao hizo alichukua uamuzi wa kuhamisha makao makuu ya utawala. [74] Mwaka 244 Hijria, Mutawakkil alielekea Damascus ili akaufanye mji huo kuwa makao makuu ya utawala wake. Hata hivyo aliona kwamba, hali ya hewa na mazingira ya huko hayafai kwa maisha. Kwa msingi huo, aliondoka katika mji huo baada ya kukaa kwa muda wa miezi miwili na kurejea Samarra. [75] Kwa mujibu wa Thaqqush, baada ya kurejea Samarra, uadui wa Waturuki na khalifa ulifikia hatua ya kutowezekana tena kurejea nyuma na kila mmoja alikuwa akitaka kumuondoa mwenzake katika ulingo wa siasa na utawala. [76]

Kuaga dunia

Mutawakkil Abbasi aliaga dunia 247 Hijria baada ya kutawala kwa muda wa miaka 14 na miezi miwili. Mutawakkil aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 40 baada ya kuuawa na mwanawe Muntasir [77] na kuzikwa katika kasri lake katika mji wa Mahuzeh. [78] Pamoja na kuwa Mutawakkil alimfanya mwanawe Muntasir kuwa khalifa wake, lakini hakuwa na uhusiano mzuri naye, na alikuwa akimfanyia masihara na dhihaki katika matukio mengi na wakati mwingine akimsema vibaya na alikuwa akimtishia kumuua. [79] Inaelezwa katika ripoti nyingine ya Tabari, mwandishi wa historia wa karne ya 4 Hijria ambapo ananukuu kwa kusema, Mutawakkil alikuwa amechukua uamuzi wa kumuua Muntasir na makamanda kadhaa wa Kituruki. [80] Kadhalika, Ibn Khaldun, mwandishi wa historia wa karne ya 8 anaamini kwamba, wakati Mutawakkil alimpomvunjia heshima Ali bin Abi Twalib, Muntasir alisimama na kumzuia hilo baba yake. Mutawakkil alimvua ukhalifa Muntasir na kutishia kumuua. [81] Muntasir ambaye alikuwa amekasirishwa mno na mienendo hiyo ya baba yake dhidi yake, alishirikiana na makamanda wa Kituruki na kumuua Mutawakkil aliyekuwa katika hali ya ulevi. [82] Katika baadhi ya ripoti tukio hili limetajwa kuwa, lilitokea wakati Mutawakkil alipokuwa akimtusi na kumvunjia heshima mtukufu bibi Fatma Zahra (as). [83] Muhammad Jawad Mughniya, mwandishi wa kitabu cha al-Shiah wal-Hakimun ameandika: Siku moja Muntasir alimsikia baba yake akimsema vibaya bibi Fatma Zahra (as) na ni kwa sababu hiyo akaondoka na kwenda kwa mmoja wa mafakihi na kuulizia hukumu ya kitendo hiki cha baba yake. [84] Fakihi akasema, ni halali kumwagwa damu ya baba yake; lakini akabainisha kwamba, mtu ambaye atamuua baba yake, umri wake unakuwa mfupi na hivyo akamtahadharisha na hatua ya kumuua baba yake. [85] Pamoja na hayo, Muntasir alimuua baba yake na baada ya kupita miezi saba tu naye akauawa. [86] Baada ya kuuawa Mutawakkil, Waturuki wakapata nguvu na ushawishi mkubwa zaidi katika utawala [87] na nguvu na heshima ya makhalifa wa Bani Abbasi ikaelekea kupungua na kuporomoka; kiasi kwamba, katika kipindi cha karne moja baada ya Mutawakkil, makhalifa 11 waliongia madarakani wote walikuwa vibaraka wa Waturuki ambapo baadaye waliuawa au kuondolewa madarakani. [88].