Amirul Muuminina (Lakabu)
Amirul-Muuminina (Kiarabu: أمير المؤمنين (لقب)) ni jina(lakabu) ambalo kwa mujibu wa imani ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ni makhsusi kwa Ali bin Abi Twalib(a.s), na wafuasi wa madhehebu haya hawalitumii jina na lakabu hii kwa Maimamu wa kishia (a.s) wengine. Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaamini kwamba, lakabu hii ilitumika kwa mara ya kwanza katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w) kwa Ali bin Abi Twalib na ni maalumu kwake tu. Sheikh Mufid ambaye ni mmoja wa Maulamaa na wanazuoni wakubwa na mtajika wa Waislamu wa Kishia katika karne ya 5 Hijiria amesema katika kitabu chake cha Al-Irshad: Mtume (s.a.w.w) alimtangaza Mrithi na kiongozi wa Waislamu baada yake katika tukio la Ghadir khum na kumuarifisha kuwa ni msimamizi wa mambo ya Waislamu wote na kisha akawataka Maswahaba wamsalimie kwa lakabu ya Amirul-Muuminina (as). Kuhusiana na hilo, kuna riwaya zilizonukuliwa kutoka kwa Ummu Salamah na Anas bin Malik zinazoonyesha kuwa, lakabu ya Amirul-Muuminin ilikuwa ikitumika hata katika zama za uhai wa Bwana Mtume (s.a.w.w).
Utambuzi wa Maana
Amirul-Muuminina ina maana ya Amir, kamanda na kiongozi wa Waislamu[1]. Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaamini kwamba, sifa hii ni kwa ajili ya Imam Ali pekee na haijuzu au haifai kuitumia kwa Maimamu wengine kwa mujibu wa riwaya zilizo pokelewa kutoka kwao(a.s).[2] Pia kwa mujibu wa kile kilichokuja katika kitabu cha Mafatihu Al-Jinan ni kuwa, Waislamu wa Kishia wamekokotezwa kwamba, katika siku ya Eidul Ghadirpindi wanapokutana wataje neno ambalo ndani yake kuna kiashirio cha kuonyesha kushikamana na Wilaya (Uongozi) ya Amirul-Muuminin.
Kutumiwa kwa mara ya kwanza
Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaamini kuwa, lakabu ya Amirul-Muuminina ilitumiwa kwa mara ya kwanza na Bwana Mtume (s.a.w.w) mwenyewe na alimhutubu Imam Ali bin Abi Twalib na alilitamka hilo kwa kinywa chake mwenyewe; lakini kutokana na kuwekwa kando Imam Ali katika suala la ukhalifa na uongozi, neno hili likawa limetumika kwa wigo mpana zaidi kwa Khalifa wa pili na wa tatu yaani Omar bin al-Khattab na Othman bin Affan[3]. Katika hoja yao Mashia wamekuwa wakitumia riwaya na hadithi zilizopokewa na kunukuliwa na Masuni na Mashia ili kuthibitisha madai yao hayo. Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Ummu Salamah na Anas bin Malik, Mtume (s.a.w.w) ambayo inasema, Mtume alimtaja Imam Ali kwa lakabu ya Amirul-Muuminina wakati alipokuwa akizungumza na wake zake wawili. Aidha kwa mujibu wa hadithi kadhaa zilizonukuliwa kutoka kwa Mardawiya Isfahani, mmoja wa wanazuoni wa Ahlu-Sunnah ambaye ameziweka katika kitabu chake cha Manaqib ya kwamba, Mtume (s.a.w.w) alimuita mara chungu nzima Ali bin Abi Twalib kwa lakabu ya Amirul-Muuminina. Imekuja katika moja ya hadithi hizo kwamba, Malaika Jibril alimsifu na kumuita Ali bin Abi Twalib kwa lakabu ya Amirul-Muuminin mbele ya Bwana Mtume (s.a.w.w).
Kadhalika imekuja katika hadithi na riwaya zilipokewa na waislamu wa madhehebu ya Shia kwamba, wakati wa tukio la Ghadir pia Bwana Mtume (s.a.w.w) alimtangaza Ali kuwa ni mrithi na kiongozi wa Waislamu baada yake na kwamba, ni kiongozi na msimamizi wa mambo ya waislamu wote na kisha akataka Maswahaba wamsalimie Ali kwa lakabu ya Amirul-Muuminina kwa msingi huo, waislamu wakiwa na lengo la kutekeleza takwa hili la Bwana Mtume (s.a.w.w) wakawa wakiingia makundi kwa makundi katika hema la Ali (as) na kumsalimia kwa mtindo uleule aliotaka Mtume asalimiwe kwao. Kwa mujibu wa hadithi nyingine ni kuwa, Bwana Mtume (s.a.w.w) aliwataka maswahaba wengine saba akiwemo Abubakar, Omar, Talha na Zubeir wamsalimie Ali bin Abi Twalib kwa salamu hii na wao walijibu takwa hilo la Bwana Mtume (s.a.w.w). Waislamu wa madhehebu ya shia wakiwa na lengo la kuthibitisha kwamba, lakabu ya Amirul-Muuminina ni kwa ajili ya Imam Ali tu, wametumia pia maneno ya Omar bin al-Khattab ambapo kwa mujibu wake alimtaja na kumpongeza Imam Ali siku ya Ghadir Khum kuwa ni kiongozi na msimamizi wa mambo ya waumini wote wanaume na wanawake[4]. Na kwa mujibu wa baadhi ya watafiti ni kuwa, kutumiwa neno muumini katika maneno haya ya Omar bin Al-Khattab, kuna maana ya kukubali umaalumu wa lakabu ya Amirul-Muuminin kwa Imam Ali bin Abi Twalib (as) pekee[5].
Matumizi ya Kisiasa
Ibn Khaldun mwanahistoria wa Kisuni amesema kuhusiana na kujitokeza lakabu ya Amirul-Muuminina katika zama za Khalifa wa pili na kutumiwa hilo kwa Omar bin al-Khattab: Maswahaba walimuita Abubakar kwa jina la Khalifa wa Mtume wa Allah, baada yake walimuita Omar bin al-Khattab Khalifa wa Mtume wa Allah, lakini kwa kuwa neno hili lilikuwa zito, mmoja wa maswahaba ambaye jina lake watu wametofautiana aliyejulikana kwa jina la Abdallah bin Jahash au Amr bin al-Aas, Mughira bin Shu'bah au Abu Mussa al-Sh'ari alimhutubuu na kumuita Omar kwa jina la Amiirul-Muuminina[6]. Maswahaba wakafurahishwa na hilo, hivyo wakapasisha uamuzi wa kumuita Omar kwa lakabu hiyo ya Amirul-Muuminina.
Yaaqubi mwanahistoria wa karne ya 3 Hijria anasema kuwa, tukio hili lilijiri mwaka wa 18 Hijria. Kwa mujibu wa ripoti ya Ibn Khaldun ni kwamba, katika zama hizo makamanda wa jeshi walikuwa wakiitwa kwa jina au lakabu ya Amirul-Muuminina, maswahaba nao walikuwa wakimuita kwa lakabu ya Amirul-Muumnina Saad bin Abi Waqas aliyekuwa kamanda wa jeshi la waislamu katika vita vya Qadisiyyah mwaka wa 14 Hijria. Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, Khalifa wa pili mwenyewe alikuwa na mchango na nafasi katika kutajwa jina hili. Katika kipindi chote cha historia ya tawala za Kiislamu baada ya Mtume (s.a.w.w), lakabu ya Amirul-Muuminina ilipata matumizi ya kisiasa na kidini na ili kuashiria tu ni kwamba, ukimuondoa Abubakar katika Khulafau Rashidin, jina hili la Amirul-Muuminina daima lilikuwa likitumiwa kwa makhalifa na watawala wa Bani Umayyah na Bani Abbas[7].
Monografia
Sayyied Ibn Tawus, mpokezi wa hadithi wa Kishia katika karne ya 7 Hijria, amesema katika kitabu chake cha Alyaqin Bi-Ikhtisas Maulana Ali Bi-Imrat Amirul-Muuminina akitegemea hadithi 220 kutoka katika vyanzo vya Ahlu Sunna kwamba, lakabu ya Amirul-Muumina ni makhsusi kwa Imamu Ali[8]. Ibn Tawus anaamini kwamba, Amirul-Muuminina ni lakabu ambayo Bwana Mtume (s.a.w.w) alifanya kuwa maalumu na makhsusi kwa ajili ya Ali bin Abi Twalib(a.s)[9].
Rejea
- ↑ Dairatu al- Maarif tashayuu, juzuu ya 2, kurasa ya 522
- ↑ Al-Majlisy, Biharu al-Anuwar, juzuu ya 37, kurasa ya 334; Al-Huru Al-Amili, wasailu-shia, juzuu ya 14, kurasa ya 600.
- ↑ Al-Mufiid, Al-Irshad, juzuu ya 1, kurasa ya 48; Ibnu Aqida Al-kuufi, Fadhwail Amirul-muuminiin, kurasa ya 13, Ibnu Asakir, Tarekh madinatu damashk, juzuu ya 42, kurasa ya 303 na 386
- ↑ Al-Mufiid, Al-Irshad, juzuu ya 1, kurasa ya 177
- ↑ Muntadhar muqadam«بررسی کاربردهای لقب امیرالمؤمنین در بستر تاریخ اسلام»,kurasa ya 136
- ↑ Al-Yakubi, Tarekh Al-Yakubii, juzuu ya 2, kurasa ya 147-150; Ibnu Khaldun, Muqadimatu Ibnu Khaldun, juzuu ya 1, kurasa ya 435-436.
- ↑ Ibnu Khaldun, Muqadimatu Ibnu Khaldun, juzuu ya 1, kurasa ya 436-438
- ↑ Taqadamii ma'asumii, Nurul-Amiir fii tathibiti khutbatu al-Ghadir, kurasa ya 97.
- ↑ Ibnu Tawus, Al-Yaqiin bi-khitisas maulana Ali(a.s) bi-Imaratul-muuminiin.
Vyanzo
- Omadim Abdul-Wahid bin Muhammad, Ghurar al-Hikam Wadurar al-Kalim, Qum, Dar al-Kitab al-Islami, 1410, Hijria/1990 Miladia.
- Ibn Khaldun, Abdul-Rahman bin Muhammad, Divan al-Mubtada Wal-Khabar Fi Tarikh al-Arab Wal-Barbar Waman Asarahum Min Dhawi Shaan al-Akbar, Uhakiki: Khalid Shahadah, Beirut, Darul-Fikr, 1408 Hijria/1988 Miladia.
- Ibn Asakir, Tarikh Madinat Dameshq, Uhakiki: Ali Shiri, Beirut, Darul Fikr, 1425 Hijria.
- Ibn, Aqdat Kufi, Fadhail Amirul-Muuminina, mkusanyaji: Abdul-Razaq Muhammad Hussein Hirzuddin, Qum, Intisharat Dalil, 1397 Hijria Shamsia.
- Ibn Mardawiya, Ahmad bin Mussa, Manaqib Ali bin Abi Twalib, Qum, Darul Hadith, 1382 Hijria Shamsia.
- Abuu Naim al-Isfahani, Ahmad bin Abdallah, Hilyat al-Auliiyaa Watabaqat al-Asfiyaa, Beirut, Darul Kutub al-Arabiy, 1407 Hijria.
- Abdus Muhammad Taqi na Muhammad Muhammadi Isht-hardou, Bistopanj Asl az Usul Akhlaq Imaman, Qum, Kituo cha Usambazaji, Ofisi ya Tablighat Islami, 1477 Hijria Shamsia.
- Hurr al-Amili, Muhammad bin Hassan, Wasail al-Shia, mhakiki: Muhammadreza Husseini Jalali, Qum, Taasisi ya Aal Beit Li-Ihyaa al-Turath, 1416 Hijria.
- Taqadumi Maasumi, Amir, Nurul Amir (as) Fi Tathbit Khutbat al-Ghadir: Muayyidat Hadithiya min Kutub Ahl Sunna Likhutbat al-Nabi al-A'dham al-Ghadiriyah, Qum, Maulud Kaabeh, 1379 Hijria Shamsia.
- Dairat al-Maarif Tashayuy, chini ya usimamizi wa Sadr al-Haj Sayyid Jawadi na Kamranifani pamoja na Bahauddin Khorramshahi, Jz 2, Tehran, Taasisi ya Uchapishaji ya Hekmat, 1368.
- Sheikh Mufid, Muhammad bin Muhammad, al-Irshad Fi Maarifat Hujajullah Alaa Ibadi, Mhakiki: Taasisi ya Aal Beit Li-Ihyaa al-Turath, Qum, al-Muutamar al-Alami Li-Al-Fiyah Sheikh Mufid, 1413 Hijria,
- Tabari, Muhammad bin Jarir, Tarikh al-Umam Wal-Muluk (Tarikh Tabari), Muhammad Abul-Fadhl Ibrahim, Beirut, Rawai'u al-Turath al-Arabi, Bita.
- Qumi, Sheikh Abbas, MNafatihul Jinan, Mtarjumi: Musavi Damghhani, Mash'had, Taasisi ya Uchapishaji ya Astane Quds Razavi, Chapa ya 11.
- Majlisi, Muhammad Baqir, Biharul al-Anwar, Beirut, Taasisi ya al-Wafaa, 1403 Hijria.
- Muntaziri Muqaddam, Hamid ((Baresii Karbordihaye Laghabe Amirul-Muuminina Dar Bastar Tarikh Islam)), Dar Majaleh Tarikh Islam Dar Ayineh Pezhuhesh, Qum, Taasisi ya Imam Khomeini, 1387 Hijria Shamsia.
- Yaaqubi, Ahmad bin Wadhih, Tarikh al-Yaaqubi, Beirut, Dar Saadir, Bita.