Kaaba

Kutoka wikishia
Al-Kaaba Tukufu

Kaaba (Kiarabu: الكعبة) ni kibla cha Waislamu na ni eneo takatifu zaidi kwa Waislamu katika mgongo wa ardhi. Wanazuoni na wasomi wa Kiislamu wanahesabu Kaaba kuwa eneo la kwanza kwa ajili ya kufanya ibada kwa wote na alama ya mwanadamu ya kuelekea kwa (upande wa) Mwenyezi Mungu.

Jengo hili linapatikana katika msikiti wa Makka (Masjdul Haraam) katika mji wa Makka. Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, Waislamu lazima wasali Sala zao wakiwa wameelekea upande wa Kaaba, na mahujaji lazima waizunguke Kaaba wakati wa kutekeleza ibada ya tawafu kama ambavyo pia wakati wa kuchinja ni lazima kukielekeza kichinjwa hicho upande wa Kaaba yaani kibla. Katika eneo takatifu la Al-Kaaba, hakuna mtu mwenye haki ya kushambulia wanadamu au wanyama. Imam Ali (a.s) alizaliwa ndani ya Kaaba.

Kwa mujibu wa rai na mtazamo mashuhuri miongoni mwa wanazuoni wa Kishia, kwa kuzingatia hadithi, Kaaba ilijengwa kabla ya Nabii Ibrahim (a.s), katika kipindi cha Adam (a.s), na hata kwa mujibu wa baadhi, ilijengwa kabla hata ya kuumbwa Adam (a.s). Hata hivyo, kuna kundi la wasomi na wanahistoria linalopinga nadharia hii na wanahusisha jengo la asili (la kwanza) la Kaaba na Ibrahim (a.s).

Miaka mitano kabla ya kubaathiwa na kupewa Utume Mtume wa Uislamu, Kaaba ilibomolewa na kuharibiwa kwa sababu ya mafuriko yaliyotokea. Makureshi wakaikarabati upya kabisa na kwa mara ya kwanza, wakaijengea paa na mifereji ya maji. Katika miaka ya 64 na 1040 Hijiria, Kaaba nzima ilikarabatiwa. Katika zama hizi, Kaaba imejengwa kwa marumaru na paa na nguzo zake zimekarabatiwa.

Ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu (Kaaba), kuna chumba kidogo chenye ngazi za kwenda kwenye paa ya Kaaba. Chumba hiki kidogo kina mlango mdogo unaoitwa Bab al-Tawba. Kaaba ina nguzo nne. Rukn Hajar al-Aswad ni maarufu zaidi kwa sababu ya kuweko hapo Hajar al-Aswad (jiwe jeusi) na Tawafu inaanzia hapo kama ambavyo inamalizikia hapo pia.

Umuhimu na nafasi yake

Waislamu wanaichukulia Kaaba kuwa ni sehemu takatifu zaidi katika mgongo wa ardhi, [3] nyumba ya kwanza ya tauhidi [4] na alama ya tauhidi. [5] Qur’ani tukufu imeiita Kaaba kwamba, ni nyumba iliyobarikiwa na sababu yake ni kuwa, Kaaba ni wenzo wa uongofu, mshikamano na ukaribu na kuwa na ukuruba na Mwenyezi Mungu. [6]

Kwa kuzingatia hadithi mbalimbali, Imamu Ali (a.s) aliitambulisha Kaaba kuwa ni bendera ya Uislamu. [7] Imamu Swadiq (a.s) alichukulia kuitazama Kaaba kuwa ni ibada [8] na akasema kwamba, maadamu Kaaba imesimama (ingalipo), dini hiyo (Uislamu) itabakia na kudumu pia. [9]

Baada ya kupita zama Kaaba iliondoka kutoka katika eneo la kumuabudu Mungu mmoja na kuwa kituo cha masanamu; [10] lakini baada ya Fat’h Makka (kukombolewa Makka) Mtume wa Uislamu aliharibu masanamu yaliyokuwako katika Kaaba. [11]

Majina ya Kaaba

"Kaaba" ndilo jina linalotumika sana miongoni mwa majina ya nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu na kwa hiyo inajulikana kwa jina hili, [29] na pia jina hili limetumika katika Qur’an. [30] Qur'an pia inaitaja Kaaba kwa jina "Bayt" (nyumba) [31] (katika michanganyiko tofauti) imetajwa kuwa mashuhuri zaidi kwa “Baytullah” (nyumba ya Mwenyezi Mungu). [32] Majina mengine ni: Al-Bayt, [33] Al-Bayt al-Haram, [34] Al-Bayt al-Atiq, [35] "Al-Bayt al-Ma'mur" [36] na "Al-Bayt al-Muharram" [37]

Katika zama za kale mno, Kaaba pia ilikuwa ikiitwa kwa majina mengine kama vile Qaadis, Naadhir na Al-Qariyah al-Qadimah. [38]

Sababu ya kuitwa kwa jina la Kaaba

Kuhusiana na sababu ya eneo hilo takatifu ambalo ni kibla cha Waislamu kuitwa kwa jina la Kaaba, kumetajwa sababu mbili:

  • Nyumba ya Mwenyezi Mungu iko katika umbo la mraba na Waarabu wanaita jina hili kwa nyumba ambayo ina kona nne.
  • Kaaba kilugha ina maana ya urefu. Jengo la Kaaba linaitwa kwa jina hili kwa sababu ya urefu wake kutoka ardhini. [40]

Kibla na Hija

Makala asili: Kibla na Hija

Kibla cha kwanza cha Waislamu kilikuwa Baytul-Muqaddas (Bayt al-Maqdis) mpaka ikateremshwa Aya huko Madina na ikatolewa amri ya kubadili Qibla kuelekea Kaaba na kuanzia wakati huo Kaaba ikawa ni Kibla cha Waislamu. [41] Ni lazima na wajibu kwa kila Muislamu kuielekea Kaaba wakati wa kusali. [42]

Wakati wa kutekeleza amali na matendo ya Hija, mahujaji wanapaswa kuizunguka Al-Kaaba. [43] Kwa maneno mengine ni kuwa, miongoni mwa amali za Hija ni kufanya tawafu (kuizunguka Kaaba mara saba).

Umaanawi wa Kaaba

Wameichukulia na kuihesabu Al-Kaaba kuwa ni kibla na ni alama ya kuelekeza uwepo mzima wa mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu. [44] Thamani ya Kaaba imetambuliwa kutokana na hili kwamba, imejengwa kwa jina la Tawhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) na ni thamani kubwa ya kiitikadi iliyo juu ya ubinadamu na hiyo ni kwa kuwa imejengwa kwa kwa fikra: Tawhidi imejengwa kwa mkono wa mwanadamu na yeye ndiye mwanzilishi wa Tawhid.” [45]

Iqbal Lahori, mwanafikra wa Kiislamu ameashiria pia asili ya Tawhidi kuhusiana na Kaaba katika moja ya beti zake za mashairi. [46] Aidha Muhammad Hussein Gharawi Isfahani, mmoja wa mafakihi wa Kishia naye ana beti za mashairi zinazoashiria umaanawi wa Kaaba. [47] Vile vile Henry Corbin, mtaalamu wa mambo ya nchi za mashariki (Orientalist) ameashiria katika maandiko yake kuhusu siri ya kimaanawi ya Kaaba kwa mtazamo wa Waislamu na anatambua kuwa, miili ya ulimwengu huu ni ishara na ramani iliyochukuliwa kutoka katika sura nzuri katika ulimwengu mwingine. [48] Yeye anaona kuwa, uhalisia wa ulimwengu huu uko katika hukumu ya kioo ambacho kinaakisi sura za nuru. [49] Kadhalika anasema kuwa, Hija na matendo pamoja na amali zake zinazofanyika katika Kaaba, zinaonyesha sura ya mwili wa nuru wa hujaji ambapo mwili wake una taathira katika ulimwengu wa malakuti. [50]

Kuhusu Kaaba walisema, mwenye nyumba hiyo ni Mwenyezi Mungu na watu ni ndio wenye kuishi ndani ya nyumba hiyo. Kwa ajili hiyo, ndio maana mwenye kuhiji anaswali Sala zake kwa ukamilifu (bila kupunguza kama msafiri) bila kujali ametoka wapi na amekata masafa kiasi gani. Kwa sababu yeye si msafiri [51] Sana'i, mshairi wa Kiislamu na arif wa karne ya 6 Hijiria, anamlingania mwanadamu na kumtaka aachane na mahusiano ya kimaada na anaamini kwamba, maadamu mwanadamu yuko pamoja na nafsi yake na anajifikiria mwenyewe, hatakuwa katika Kaaba. [52]

Hassanzadeh Amoli anasema: "Ewe Mola wangu! Kuna faida gani ya kuwa na mwili wa kuelekea Kaaba ikiwa moyo hauelekei kwa Mwenyezi Mungu wa Kaaba?" [53]

Historia ya Kaaba

Imeelezwa katika hadithi nyingi kwamba, Kaaba ilijengwa kabla ya Nabii Ibrahim (a.s) na kwa mikono ya Nabii Adam (a.s). [54] Hata hivyo katika baadhi ya hadithi, kujengwa kwa Kaaba kunanasibishwa kabla ya kuumbwa kwa Adam (a.s). [55] Pamoja na hayo mtazamo maarufu miongoni mwa wanachuoni wa Kishia ni kwamba, ujenzi wa Kaaba unahusiana na kipindi cha kabla ya Ibrahim. [56] Kwa msingi huo, inasemekana kwamba jengo hili liliharibiwa na kutokomezwa na tufani (gharika) iliyotokea katika zama za Nabii Nuhu. [57] Kisha Nabii Ibrahim, pamoja na mwanawe Ismail, walikuja kuijenga upya Kaaba kwa msingi ule ule. [58]

Kinyume na nadharia hii, Allama Tabatabai amehusisha ujenzi wa Kaaba na Ibrahim (a.s). [59] Muhammad Jawad Mughniya, mmoja wa wafasiri wa Kishia, pia alizingatia hadithi zinaoeleza kwamba, Kaaba iliyojengwa kabla ya Adam kuwa ni khabar wahed (hadithi ambayo haijathibiti uhakika wake kuwa, ni kutoka kwa Maasumu) na hivyo akazikataa. [60]

Ukarabati wa Kaaba

Miaka mitano kabla ya kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad (s.a.w.w), kulitokea mafuriko huko Makka na Kaaba ikaharibiwa na kubomolewa. [62] Kwa mujibu wa baadhi ya nukuu, Kaaba ilishika moto na kuteketezwa. [63] Kabla ya hapo Kaaba haikuwa na paa. [64] Baada ya mafuriko na kubomolewa Kaaba, Makureshi walifanya hima ya kuijenga upya [65] na wakaijengea paa na mifereji ya maji. [66] Ukuta ambao Ibrahim aliujenga kwa ajili ya Kaaba ulielezwa kuwa na urefu wa takribani mita 4.5 na inaelezwa kuwa, urefu wa ukuta wa Kaaba, wakati wa ujenzi wa Makureshi ulifikia kama mita tisa. [67]

Kubomolewa na kukarabatiwa na Abdullah bin Zubayr na Hajjaj bin Yusuf

Katika mwaka wa 64 Hijiria, Mazubayr walipigana na Bani Umayya, na katika vita hivi, Kaaba iliharibiwa vibaya sana. [68] Abdullah bin Zubeyr, licha ya upinzani wa baadhi ya masahaba, aliuondoa ukuta uliobaki wa Kaaba kutoka kwenye msingi wake na akaijenga kwa mara nyingine tena. [69] Katika kuijenga upya Kaaba aliuongeza urefu wa Al-Kaaba hadi kufikia mita 13.5 [70] Alijenga mlango wa Al-Kaaba kuanzia ardhi, mlango ambao ulikuwa umeinuliwa karibu mita mbili kutoka ardhini na Makureshi. [71] Kisha akaweka mapaa mawili kwa ajili ya Kaaba. [72] Ibn Zubayr pia aliweka milango miwili kwa ajili ya Al-Kaaba: Mmoja wa kuingia na mwingine wa kutokea. [73] Baada ya kuuawa Ibn Zubeyr, Hajjaj bin Yusuf alibadilisha marekebisho mengi yaliyokuwa yamefanywa na Ibn Zubayr na kuyarejesha katika hali yake ya awali. [74]

Ukarabati wa mwaka 1040 Hijiria

Mnamo 1039 Hijria, mafuriko makubwa yalitokea huko Makka. Maji yaliingia Masjid al-Haram na kuharibu kuta za Kaaba. Hatimaye kuta ziliziobakia zikaboloewa na nyumba ya Mwenyezi Mungu ikajengwa upya. Ripoti ya mafuriko haya na kujengwa upya Kaaba imeandikwa na Mulla Zaynu al-Abidin Kashani mmoja wa Maulamaa wa Kishia katika zama hizo katika risala ndogo inayoitwa " “Mufarrahat al-Anam fi taasisi Baytillah al-Haram”[76] ambapo yeye mwenye alikuwa miongoni mwa vibarua walioshiriki kujenga Kaaba wakati huo.

Ukarabati wa zama hizi

Baada ya kujengwa upya kwa Kaaba mnamo mwaka wa 1040 Hijria, kilichofanyika ni matengenezo na kuweka marumaru juu yake tu. [77] Matengenezo muhimu zaidi kati ya hayo yalikuwa ni kuziwekea marumaru kuta za nje za Al-Kaaba, ambao ulianza mwaka 1414 Hijiria na kumalizika mwaka 1415 Hijiria. [78] Mpango wa kuweka marumaru ndani ya Kaaba pia ulitekelezwa mnamo tarehe 10 Muharram mwaka 1417 Hijiria. [79] Katika mpango huu, pamoja kuweka marumaru sehemu mbalimbali ndani ya Kaaba, nguzo na paa za Kaaba ziliondolewa kabisa na kujengwa upya. [80]

Sehemu za nje ya Kaaba

Hajar al-As’wad

Hajar al-Aswad ni jiwe takatifu lililowekwa juu ya ukuta wa Kaaba ambapo tawafu (kuzunguka Kaaba) huanzia na kuishia hapo. [107]

Mustajar na Multazam

Mustajar ni sehemu ya ukuta wa magharibi wa Kaaba ambayo ipo katika ukuta wa nyuma wa Kaaba. [108] Mustajar iko jirani na Rukn Yamani (109) na mkabala na nyumba ya Mwenyezi Mungu. [110] Ukuta wa Kaaba ambao ulipasuka na kuachia njia kwa ajili ya Fatima binti Assad, mama wa Imamu Ali (as) na akaingia hapo kwa ajili ya kwenda kujifunga Ali, unatambulika kwa jina la Mustajar. [111]

Multazam katika maana moja, imetambuliwa kuwa ni sehemu ya ukuta wa Kaaba baina ya Hajar al-Aswad na mlango wa Kaaba. [112] na katika maana nyingine, imetumiwa kama yenye maana moja na Mustajar. [113]

Mlango wa Kaaba

Mlango wa Kaaba upo katika ukuta wa mashariki wa Kaaba [114] na katika hadithi zilizopokewa na Waislamu wa madhehebu ya Shia, imeusiwa kusoma dua wakati wa kufika katika sehemu hiyo. [115]

Shadharwan

Shadharwan ni muinuko mfupi unaozunguka ukuta wa Al-Kaaba kuelekea upande wa chini [116], ambao upo katika pande nyingine tatu za Al-Kaaba isipokuwa katika sehemu ya Hijr Ismail. [117] Mafakihi mashuhuri wa Kishia wanmeutambua mtokezo huu kuwa ni sehemu katika Kaaba ambayo mwenye kufanya Tawaf afanye Tawaf nje yake. [118]

Mifereji ya dhahabu

Mifereji ya maji iliyotengenezwa kwa dhahabu ipo juu ya ukuta wa kaskazini wa Kaaba ambapo maji yanamwagikia katika paa na kumiminikia katika Hijr Ismail. [119] Inausiwa na kuupendekezwa kusoma dua chini ya miefereji hii na kutambuliwa kama ni mustahabu kufanya hivyo. [120]

Pazia la Kaaba

Kufunika Kaaba ni katika sunna na ada za kale na jambo lenye umuhimu mkubwa na katika zama za ujahilia moja ya iliyokuwa kazi muhimu ni kubadilisha pazia ya Kaaba (kiswa). [121 Kufunika Kaaba kulikuwa kukifanyika kwa vitambaa vya rangi tofauti tofauti; wakati mwingine pazia hili lilikuwa la rangi nyeupe, [122] kijani na wakati mwingine rangi ya njano. Katika zama za Al-Nasir Abbasi rangi ya pazia hilo ikawa ni nyeusi na kisha kuanzia wakati huo na kuendelea rangi hiyo ikabakia na kutobadilishwa. [123] Pazia la Kaaba aghalab lilikuwa likiandaliwa huko Misri na Sham na ilikuwa mara chache sana kuandaliwa katika maeneo mengine ya dunia kama Iran. [124] Hii leo pazia hili linaandaliwa na kushonwa katika viwandwa vya Saudi Arabia. [125]

Ndani ya Kaaba

Mlango wa Tauba, ndani ya al-kaaba

Mwanzoni Kaaba haikuwa na paa na miaka mitano kabla ya kutumwa Mtume Muhammad (saww), paa lake lilijengwa wakati Makureshi waliokarabati Kaaba hiyo ambalo lilikuwa na nguzo sita za mstari miwili ambapo kila mstari ulikuwa na nguzo tatu. Wakati Kaaba ilipokuja kufanyiwa ukarabati na Ibn Zubayr, nguzo sita zilibadilishwa na kuwa tatu na hadi leo nguzo hizo tatu za paa la Kaaba zimebakia. [126] Ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu (Kaaba), kuna chumba kidogo chenye ngazi za kwenda kwenye paa la Al-Kaaba. [127] Chumba hiki kidogo kina mlango mdogo unaoitwa Bab al-Tawba. [128] Mlango huu umejengwa kwa kutumia dhahabu. [129]

Kuanzia zama za kale, makabila, kaumu na wafalme walikuwa wakituma zawadi huko Makka zitundikwe ndani ya Kaaba. [130] Kadhakika kuna kisima ndani ya Kaaba ambacho ndani yake mlikuwa mkiwekwa zawadi. Kisima kicho kilitokomezwa katika kipindi ambacho Makureshi walifanyia ukarabati Kaaba. [131]

Arkan (nguzo) za Kaaba

Arkan ni wingi wa Rukn ambayo ina maana ya nguzo na msingi. [132] Kwa kuwa katika pembe nne ndani ya Kaaba kuna nguzo nne ambazo zinashikilia paa ya Kaaba, kila moja kati ya pembe hiyo ya Kaaba ambayo ina nguzo inajulikana kwa jina la rukn. [133] Kaaba ina rukn (nguzo) nne:

  • Rukn Sharqi: (Rukn Hajar al-Ass'wad): Nguzo hii takribani ipo upande wa mashariki na kisima cha zamzam na hapo inapatikana Hajar al-Aswad (jiwe jeusi). [134] Kila tawafu huanza mkabala wa Hajar al-As'wad kama ambavyo pia humalizikia hapo. [135]
  • Rukn Shimali au Iraqi: Ni moja ya engo za Kaaba ambayo takribani iko upande wa kaskazini mwa Saudi Arabia yaani upande wa nchi ya Iraq [136] na anayefanya tawafu baada ya engo hiyo huwa anafika katika Hijr Ismail. [137]
  • Rukn Gharbi au Shami: Nguzo hii ya Magharibi ni moja ya engo za Kaaba ambayo iko upande wa Magharibi [138] na anayefanya tawafu huifikia nguzo hiyo baada ya kupita Hijr Ismail. [139]
  • Rukn Junubi au Rukn Yamani: Hii ni nguzo ambayo iko kando ya Mustajar [140]. Nguzo hii ni moja ya engo za Kaaba ambayo takribani ipo upande wa kusini na upande wa nchi ya Yemen na mahujaji katika tawafu baada ya hapo hufika katika Hajar al-As'wad. [141]

Matukio muhimu

Makala asili: Mzaliwa wa Kaaba

Imamu Ali bin Abi Twalib (a.s) alizaliwa katika Kaaba. [142] baadhi ya vyanzo vya Ahlu-Sunna pia vimesajili na kunukuu tukio hili. [143]

Kuwekwa Hajar al-As'wad na Mtume Muhammad

Kadhalika angalia: Hajar al-Aswad

Ilikuwa miaka mitano kabla ya kubaathiwa Bwana Mtume na kupewa Utume ambapo kulitokea mafuriko makubwa katika mji wa Makka na Kaaba ikabomolewa. [144] Baada ya mafuriko hayo, Makureshi wakafanya hima ya kuikarabati al-Kaaba. [145] Katika tukio la kukarabatiwa al-Ka'aba ambapo kila kabila miongoni mwa makabila lilitaka lenyewe ndio lipachike na kubandika Hajar al-Aswad. Hitilafu zikaongezeka na kushadidi kuhusiana na jambo hilo na hatimaye kwa pendekezo la Muhammad (s.a.w.w) jiwe hili likawekwa katika kitambaa na kila upande wa kitambaa hicho wakashikilia viongozi na wakuu wa makabila na baada ya kufika sehemu ya kuweka jiwe hilo, Mtume mwenyewe akalichukua na kulibandika sehemu yake mahususi, [146] na kwa hekima na busara hiyo akawa ameepusha kuibuka mzozo mkubwa na hata pengine mapigano baina ya makabila hayo.

Matukio Mengine

Makala asili: Watu wa tembo, mwaka wa tembo na Abraha

Abraha kiongozi wa Yemen mwaka 571 Miladia, akiwa na jeshi lake alishambulia Makka akiwa na nia kuibomoa Kaaba. Alipofika alikutana na muujiza wa Mwenyezi Mungu ambapo ndege ndege makundi kwa makundi walijiitokeza na kuuwatupia mawe ya udongo wa Motoni wanajeshi wa Abraha walikuwa wakidondosha mvua ya vijiwe na jeshi la Abraha likaangamia baada ya kufanywa kama majani yaliyo liwa! [147]

Baada ya Abdallah ibn Zubeyr kukataa kumpa baia na kipao cha utii Yazid, jeshi lililokuwa likiongozwa na Kamanda Husayn ibn Numary lilifunga safari na kuelekea Makka kwa ajili ya kukabiliana naye. Jeshi hilo liliwasili Makka mwezi Muharram mwaka 64 Hijiria na mwezi Rabiul Awwal mwaka huo huo likafanya mashambulio dhidi ya jeshi la ibn Zubayr kwa mtambo wa kutupia mawe katika vita. Katika shambulio hilo, Kaaba iliharibiwa. [148]

Mwezi Dhul-Hija mwaka 317 Hijiria, kundi la Qarmatian lilishambulia Makka. Wapiganaji wake waling'oa Hajar al-Aswad (jiwe jeusi) na kuondoka nalo na mwaka 339 Hijiria Qarmatian wakakubali kurejesha Hajar al-Aswad lakini kwa kupatiwa kiwango kikubwa cha fedha. [149]