Ziara

Kutoka wikishia

Ziara ((Kiarabu: الزيارة)) Neno Ziara katika tamaduni za Kishia humaanisha kutembelea au kuzuru makaburi. Moja ya amali zinazosisitizwa mno kwenye madhehebu ya shia, ni kutembelea au kuzuru makaburi ya Manabii, Maimamu, makaburi ya watu wa kizazi cha Maimamu pamoja na waumini mbali mbali. Kuzuru makaburi ni moja wapo ya matendo yanayohimidiwa na Uislamu, ambayo yamerithiwa na kutunzwa kutoka katika historia ya Waislamu waliotangulia.

Ibnu Taymiyyah na wafuasi wa madhehebu ya Kiwahabi, kinyume na madhehebu mengine ya Waislamu, wanachukulia suala la waumini kuzuru makaburi ya manabii na viongozi wa kidini kwa nia ya kupamata uombezi mbele ya Mwenye Ezi Mungu au kwa nia ya kujibiwa kwa dua zao, kuwa ni uzushi na ushirikina. Hata hivyo, wanazuoni wa Kishia pamoja na wanazuoni kadhaa wa upande wa Ahlu-sunna hawakubaliani na maoni haya. Badala yake wanaliona tendo hili kuwa ni halali na lenye kheri ndani yake. Fatwa za wanazuoni hawa zimtegemea vyanzo kadhaa vya Kiislamu, zikiwemo Sunna za bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja na maimamu watakatifu (a.s), nyenendo za masahaba na matabiina (wafuasi wa masahab), makubaliano ya wanazuoni (ijma’u), pamoja nyenendo na tabia za Waislamu katika zama mbali mbali.

Kuna kazi kadhaa andishi zilizo andikwa na wanazuoni mbali mbali wa Kiislamu kuhusiana na: uhalali wa kufanya ziara (kuzuru makaburi), faida zake, kupendekezwa kwake katika Uislamu pamoja na kujibu pingamizi za Ibn Taymiyyah kuhusiana na amali hii ya kuzuru makaburi. Miongoni mwa vitabu vilivyo andikwa na wanazuoni mbali mbali ni; Kitabu Shifaa-u al-Siqaam fi Ziyarat Khayri al-Anami kilichoandikwa na Taqi al-Din al-Subki na Tuhfatu al-Zuwwar ila Qabri al-Nabi al-Mukhtari, kilichoandikwa na Ibn Hajar al-Haitami. Miongoni mwa vitabu muhimu kuhusiana na faida za kuzuru makaburi ni al-Mazar fi Kaifiyyati Ziarati al-Nabi wa al-A-immati al-At-hari, kilichoandikwa na Shahid al-Awwal. Kitabu hichi kinazungumzia faida pamoja na mapendekezo ya kuzuru kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja na Maimamu wa Kishia (a.s), ambacho pia ndani yake kimechambua adabu za ziara hizo.

Nafasi ya Kuzuru Makaburi katika Utamaduni wa Kiislamu

Neno Ziara (kuzuru) ni neno la Kiarabu lenye maana ya kutembelea, ambalo kiistilahi ya kidini humaanisha kuhudhuria kwenye eneo la karibu ya, waumini, wachamungu, na hasa makaburi ya Manabii, Maimamu pamoja na watoto wa maimamu. Tendo hili la kuzuru makaburi hufanyika kwa kufuata taratibu zenye kufungamana na amali maalum ndani yake. [1] Kwa mujibu wa maelezo ya Ja'afar Subhani, ni kwamba; Tendo la ziara ya kuzuru kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w), Ahlul-Bait wake (a.s) pamoja na makaburi ya waumini, ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Kiislamu. [2]

Miongoni mwa wanazuoni wa Ahlus-Sunnah waliothamini mno ziara ya kuzuru kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w), na kuamini ya kwamba tendo hilo ni lenye faida kumbwa mno ni; Ibnu Dhiyaa al-Makki (aliyefariki dunia mwaka 854 Hijiria), Shawkani, Shams al-Din al-Dhahabi (aliyefariki mwaka 748 Hijiria), na Abdulrahman al-Jaziri. [3] Pia wanazuoni hawa wameripoti ya kwamba; Ilikuwa ni ada kwa mahujaji kuzuru kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w) baada ya kumaliza ibada zao za Hija. [4]

Nafasi Maalumu ya Ziara kwa Wafuasi wa Shia

Ziara inachukuliwa kuwa ni moja ya nembo na alama kuu inayo watambulisho Shia. Nembo hii ni moja ya mbolea na sababu zilizohuisha madhehebu ya Shia na kuwapa utambulisho maalumu mbele ya Jamii na watu mbali mbali. Wafuasi wa Shia, wakishikamana na Hadithi kutoka kwa Maimamu watakatifu (a.s), ambazo zinazoelezea dhawabu na kutoa mosha juu ya amali hii, wamekuwa mbele katika amali hii. [5] Mashia hufunga safari kutoka miji ya mbali kwa ajili ya ziara za kutembelea makaburi. Kila mwaka, Mashia kadhaa hufunga safari kutoka miji mbali mbali duniani kwa ajili ya kutembelea makaburi ya Maimamu na baadhi ya watoto wa maimamu (a.s). Kwa mfano, mnamo Agosti 2018 mkuu wa Haramu ya Imamu Ridha (a.s) aliripoti akisema kwamba; Kuna idadi ya watu milioni 28 kutoka miji mbali mbali ya Iran pia kutoka baadhi ya nchi nyingine, wanao safiri kila mwaka kuelekea mji wa Mashhad kwa ajili ya kutembelea kaburi la Imam Ridha (a.s). [6] Pia, kwa mujibu wa kituo cha takwimu cha Haramu ya Abbas (Shrine of Hadhrat Abbas (a.s)) ni kwamba; Kuna kiasi cha Idadi ya watu milioni 22 waliohudhuria katika matembezi ya Arubaini ya mwaka 1402. [7]

Ziarat-nameh

Makala Asili: Ziarat-nameh

Ni neno la Kiajemi (Kifarsi) linalo maandishi kitabu chenye sala na salamu zisomwazo wakati wa kutembelea makaburi ya maimamu wa Shia (a.s). Ndani ya kitabu hicho huwa mno sala na salamu za heshima kwa ajili ya aliyezikwa kaburini humo. [8] Ingawa kila mtenda ziara anaweza kusoma dua azitakazo au kutawasali mbele ya makaburi hayo kwa kutumia lugha yake mwenyewe, ila inapendekezwa kusoma sala na salamu maalumu zilizomo ndani ya vitabu vya ziara, ambazo zimeandikwa na Maimamu maasumi (a.s), ambazo kiistilahi huitwa Ziaratu al-Ma-athuarah. [9] Miongoni mwa matini zilizomo ndani ya vitabu hivyo, ni pamoja na baadhi ya masuala ya kidini kama vile; tawhidi, utume na sifa za Mwenye Ezi Mungu. Pia muktadha wa mada zake imegusia masuala mengine kadhaa, kama vile; kuwajua Maimamu maasumina, sifa zao, mamlaka yao, Tawalli na Tabarri, shufaa na kutawasali. [10]

Ziara ya Ifanywayo Mbali na Eneo la Kaburi

Ziara ya mbali inahisabiwa kuwa ni miongoni mwa ziara zilizo pendekezwa katika Hadith za Shia, nayo ni aina ya ziara ifanywayo na wale wasio na uwezo wa kutembelea makaburi hayo ana kwa ana. [11] Kwa mfano, katika Hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s), imeelezwa ya kwamba; mtu asiyeweza kuzuru kaburi kwa karibu, basi asimame mahali penye muinuko kisha asali rakaa mbili, akimaliza kusali ayaelekee makaburi yetu na kuwatolea salimu wahusika wa makaburi hayo, bila shaka sala na salamu zake zitatufikia tu. [12] Katika Riwaya nyingine iliopokewa kutoka kwake imeeleza kwamba; Iwapo mtu atasimama sehemu iliyo wazi na kuangalia kulia na kushoto, kisha akanyanyua kichwa chake kuelekea mbinguni na kujenga taswira ya kaburi la Imamu Husein (a.s) na kusema: (السَّلامُ عَلَیْکَ یا اباعَبْدِاللَّهِ، السَّلامُ عَلَیْکَ وَ رَحْمَةُاللَّهِ وَ بَرَکاتُهُ ; Amani ya Mwenye Ezi MUngu na baraza zake ziwe juu yako ewe Abaa ‘Abdillahi), bila shaka mtu huyo atalipwa malipo ya kumzuru Imamu Hussein (a.s). [13]

Ziara za Makaburi ya Maimamu wa Kishia Kulingana na Wafuasi wa Madhehebu ya Kisunni

Wanahistoria wameripoti matukio kadhaa yaoneshayo baadhi ya wanazuoni wa Kisunni pia walikuwa wakitembelea makaburi ya baadhi ya Maimamu wa Kishia. [14] Kwa mfano, Ibnu Hibban, mwanazuoni wa Hadithi wa Kisunni wa karne ya tatu na ya nne Hijria, anaeleza akisema: Mara nyingi nilikuwa nikienda kutembelea kaburi la Imamu Ridha (a.s) huko Mashhad na kumuomba msaada, ambapo matatizo yangu yalitatuliwa kupitia dua zangu hizo nizilizo muomba Mungu kupitia baraka zake yeye. [15] Pia, Ibnu Hajar Asqalani alisimulia kuwa Abu Bakar Muhammad bin Khuzaima, faqih, mfasiri na mwanazuoni wa Hadithi wa Kisunni katika karne ya tatu na ya nne Hijria, na Abu Ali Thaqafi, mwanazuoni kutoka Nishabur, wakifuatana na watu wengine kadhaa kutoka kwa wafuasi wa Kisunni walikwenda kutembelea kaburi la Imamu Ridha (a.s). [16] Sam-‘ani, ambaye ni mwanahistoria, mwanazuoni wa Hadithi na faqih wa Kishafi'i wa karne ya sita Hijria, alikwenda kutembelea kaburi la Imamu Kadhim (a.s)) na kumuomba msaada (kutawasali) kaburini hapo. [17] Imeripotiwa pia kutoka kwa Shafi'i, ambaye ni mmoja wa mafakihi wanne wa Kisunni, kwamba alilisifu na kulielezea kaburi la Imamu Kadhim (a.s) kama ni "dawa ya uponyaji." [18]

Misingi ya Uhalali wa Ziara ya Kuzuru Makaburi

Wanazuoni wa Kiislamu wametoa hoja zifuatazo kuthibitisha uhalali wa kuzuru makaburi:

Sunna za Bwana Mtume (s.a.w.w)

Ziara za kuzuru makaburi zilikuwa ni jambo halali na la kawaida tokea mwanzoni mwa Uislamu. Kulingana na Ibnu Shabba katika kitabu chake Tarekhu al-Madina al-Munawwara, ni kwamba; Pale Bwana Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akirudi Madina baada ya ushindi wa ukombozi wa Makka, alikwenda kutembelea kaburi la mama yake Amina na akasema: "Hili ni kaburi la mama yangu, niliomba ruhusa ya kutembelea kaburi hili kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu, Naye akaniruhusu. [19] Pia imesimuliwa kuwa alitembelea makaburi ya mashahidi wa vita vya Uhud [20] na makaburi ya waumini wengine kwenye mava ya Baqi. [21] Katika baadhi ya vyanzo vya Hadithi za Kisunni, kuna Hadithi za Mtume (s.a.w.w) zinazohimiza na kuelezea faida ya kufanya kuzuru makaburi. [21] Kwa mfano, imesimuliwa kutoka kwake kwamba; (مَنْ زَارَ قَبْرِي وَجَبَتْ لَهُ شَفَاعَتِی ; Mtu yeyote atakayezuru kaburi langu, huyo atapata uombezi wangu Siku ya Kiyama).[22]

Hadithi na Sira za Maimamu Maasumina (Watakatifu) (a.s)

Kuna Hadithi nyingi katika vyanzo vya Hadithi za Kishia, zinazozungumzia faida na upendekezwaji wa kutembelea kaburi la Mtume (s.a.w.w), makaburi ya Maimamu wa Kishia (a.s), pamoja na makaburi ya waumini wa kawaida. Kulaini katika kitabu chake kiitwacho Al-Kafi ametenga mlango maalumu wenye jina la بَابُ فَضْلِ الزِّيَارَاتِ وَ ثَوَابِهَا ; (Mlango wa Faida za Ziara na Thawabu Zake), ambao ndani yake umekusanya Hadithi kadhaa zinazohusiana na mada hii. [23] Hurru al-Amili naye ametenga mlango maalumu kwa ajili ya amali ya kuzuru makaburi, kwa jina la «Abwabu al-Mazaari wa Maa Yunasibuhu» [24] katika kitabu chake kiitwacho Wasa'il al-Shi'a, ambamo ndani yake amekusanya Hadithi maalumu zinazohusiana na faida na thawabu za kutembelea kaburi ya Mtume (s.a.w), makaburi ya Maimamu wa Kishia (a.s), Manabii wa Mwenyezi Mungu, makaburi ya watoto wa Maimamu kama vile Bibi Maasuma (s.a) na Bwana Abdul Adhim al-Hassani (a.s), kutembelea makaburi ya mashahidi na waumini, kudaukia na kumtembelea ndugu wa Kiislamu akiwa mzima au mgonjwa, na masuala mengine kadhaa juu ya mada hizo. Mlango huo ulioko kitabuni humo umegawika katika sura tofauti, zilizobeba idadi ya sura 106 ndani yake. [25]

Pia, Katika vyanzo vya kihistoria, yameripotiwa matukio kadhaa yanayo akisi nyenendo za Maimamu wa Kishia kuhusiana na suala la kuzuru makaburi. Hakim al-Nishaburi katika kitabu chake «Al-Mustadrak 'Ala al-Sahihain» amesimulia fulani isemayo kuwa; Kila Ijumaa Bibi Fatima (s.a) alikuwa na kwaida ya kutembelea kaburi la Hamza bin Abdul-Muttalib, ambapo pia alionekana akisali na kulia kaburini hapo. [26] Pia katika moja ya Hadithi iliyo simuliwa kutoka kwa Imamu Baqir (a.s), ni kwamba; Kila usiku wa Ijumaa, Imamu Hussein (a.s) alikuwa akienda kutembelea kaburi la Imamu Hassan (a.s). [27] Katika kitabu kiitwacho Kamilu al-Ziyarat kuna Hadithi iliyosimuliwa kutoka kwa Imamu Ridha (a.s), isemayo kwamba; Imamu Sajjad (a.s) alikuwa na kawaida ya kutembelea kaburi la Imamu Ali (a.s), akisalia karibu na kaburi hilo, akilia pamoja na kutoa salamu kaburini hapo. [28]

Matendo ya Masahaba, Mataabi’ina Pamoja na Ijmaa ya Wanazuoni

Subki, ambaye ni mwanazuoni wa Kisunni wa karne ya nane Hijria, amerejelea Hadithi kadhaa kutoka vyanzo mbalimbali vya Hadithi za Kisunni katika kitabu chake kiitwacho Shifa’u al-Siqam, [29] Hadithi ambazo zinaonesha wazi ya kwamba; baadhi ya Masahaba na Mataabiin walikuwa na kawaida ya kuzuru kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja na makaburi yawaumini wengine, na walikuwa na kawaida ya kutoa salamu kwa waliolala makaburini humo. [30]

Ibnu Taymiyyah na Wafuasi wa Madhehebu ya Kiwahhabi, ni Wapinzani wa Amali ya Kuzuru Makaburi

Kwa mujibu wa nukuu za Muhammad Abdu al-Hayyi Lucknawi (aliyefariki mwaka 1304 Hijria), ambaye ni mwanafiqih na mwanazuoni wa Hadithi wa Kihanafi kutoka India, ni kwamba; hakuna hata mmoja wa mafakihi wanne wa Kisunni na wanazuoni wa Kiislamu aliyekataza ziara za kuzuru makaburi ya waumini, hususan kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w), wala kusafiri kwa ajili ya kufanya ziara hiyo. [31] Kwa mujibu wa maelezo ya Lucknawi, Ibn Taymiyyah (aliye ishi kati ya 661 na 728 Hijria), alikuwa mtu wa kwanza kabisa kupinga ijmaa hii, na ndiye wa kwanza kutilia shaka uhalali wa ziara za makaburi. [32] Pia kwa maoni yake ni kwamba; Ni halali kutoa salamu na kuomba dua kwa ajili ya waliolala makaburini humo, ila miongoni mwa vitendo visivyo halali; ni kuomba haja zako kutoka kwao, kuwaweka kama ni wasuluhishi kati ya Mungu waja wake, pamoja na kuwapia wao kwa ajili ya kuomba haja zako. [33] Yeye anaihisabu aina kama hii ya ziara, kuwa ni miongoni mwa matendo ya bid'a (uzushi) na ushirikina. [34]

Karne kadhaa baada ya Ibn Taymiyyah, ambayo ni karne ya kumi na mbili, upinzani dhidi ya uhalali wa ziara ulirudishwa uwanjani na wafuasi wa madhehebu ya Kiwahabi, na hadi leo (karne ya kumi na tano Hijria), wao wanakihisabu kitendo hiki kuwa ni kitendo cha haramu, na pia wanawazuia Waislamu kufanya ziara hizo. [35]

Ukosoaji wa Maoni ya Ibnu Taymiyyah na Maoni ya Kiwahhabi kutoka kwa Wanazuoni wa Kiislamu

Wanazuoni wengi wa Kisunni kama vile Nawawi, [36] Ibnu Hajar Asqalani, [37] Ghazali, [38] Mulla Ali Qari Hanafi, [39] Shams al-Din Dhahabi, [40] Jassas, [41] Ibnu Abidin faqih wa Kihanafi, [42] Zarqani faqih wa Kimaliki, [43] Ibn Qudamah Hanbali [44] pamoja na wengine kadhaa, wanaamini kwamba; Hadithi ya Shadd al-Rihal ambayo Ibn Taymiyyah aliitumia na kuitegemea katika kuthibitisha makatazo ya ziara za kuzuru makaburi, [45] haikatazi kuzuru makaburi, hususan kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w). Badala yake, Hadithi hiyo inaelezea faida za misikiti mitatu mikuu ambayo ni: Msikiti wa Makka, Msikiti wa Mtume na Msikiti wa Al-Aqsa.

Ja'afar Subhani ambaye ni faqihi wa Kishia amesema kuwa; kutembelea makaburi na kuomba msaada kutoka kwa waliozikwa makaburini humo, hakumaanishi kuwa wao ndiwo wanao timiza haja za wanao zuru au wanao omba msaada bila ya kutegemea idhini na rehema kutoka kwa Mungu, bali wao huwa ni kiungo baina ya waja na Mola wao, na kama si hivyo basi jambo hili lingekuwa ni shirki. Bali kutokana na hadhi walizo nazo mbele ya Mwenye Ezi Mungu, watu huwatumia maiti hao kama ni wawakilishi wa maombi yao mbele ya Mola wao, ili kurahisisha upatikanaji wa matilaba yao. [46]

Adabu za Kuzuru Makaburi

Sheikh Abbas Qummi katika kitabu cha Mafatih al-Jinan, akirejelea Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Maimamu wa Kishia (a.s), ameeleza adabu kadhaa za kufanya ziara ambazo baadhi yake ni kama ifuatavyo:

  • Kukoga josho la ziara.
  • Kuvaa nguo safi zenye tohara.
  • Kuushughulisha ulimi wako katika kumtaja Mwenye Ezi Mungu.
  • Kuwa na udhu na tohara kamili ya mwili.
  • Kusali Sala ya ziara.
  • Kusoma Qur’ani karibu na makaburi.
  • Kutubu na kuomba msamaha kutokana na madhambi.
  • Kuacha maneno yasiyo na maana.
  • Kutopaza sauti wakati wa kufanya ziara. [47]

Bibliografia (Vitabu Vilivyoandikwa Kuhusu Ziara na Faida Zake)

  • Kitabu cha Kamil al-Ziyarat: Kazi ya Kihadithi ya Ibn Qulawayh ambayo inakusanya hadithi kutoka kwa Maimamu Maasumina (a.s) kuhusu faida na thawabu za ziara, jinsi ya kufanya ziara na adabu za kutembelea makaburi yao. [48]
  • Kitabu cha al-Mazaru fi Kayfiyyati Ziyarati al-Nabi wa al-A-immati al-At’hari, Maarufu kama "Kitabu al-Mazar", kilichoandikwa na Shahid al-Awwal: Kitabu hichi kina sehemu mbili, [49] ambapo sehemu ya kwanza inahusiana na ziara ambayo inajumuisha sura nane na hitimisho moja kuhusiana na adabu pamoja na faida za kutembelea makaburi ya Maimamu Maasumina (a.s). [50]
  • Tuhfatu al-Zuwwari ilaa Qabri al-Nabi al-Mukhtari, kilichoandikwa na Ibn Hajar Haytami, ambaye ni mwanazuoni wa Kisunni (aliye ishi kati ya mwaka 909 na 974 Hijria): Kitabu hichi kinazungumzia ziara ya kaburi la bwana Mtume (s.a.w.w), adabu za ziara na matendo baada ya kumaliza ziara, ambacho kinajumuisha ndani yake utangulizi mmoja na sura nne. [51]
  • Kitabu cha Aadabu Ziaarat az Diidgaahe Maasuumiina (a.s) (Adabu za Ziara kwa Mtazamo wa Maasumu (a.s)): Kitbabu ni Tafsiri ya mlango uitwao "Babu al-Mazar" kutoka kitabu cha Wasa'il al-Shi'a ambayo ni kazi ya Mohsin Dimeh Kaarguraab na Abolfazl Kadhimi, ambao waliufasiri mlango huo kitoka katika lugha ya Kiarabu kwenda lugha ya Kiajemi. [51]

Rejea

Vyanzo